10 Feb 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-49

Asalam aleykum,

Wiki hii klabu ya soka ya Liverpool imejikuta ikiingia kwenye mkumbo wa timu za Uingereza ambazo zinamilikiwa na matajiri kutoka nje ya nchi hii.Nadhani wapenzi wa kabumbu huko nyumbani wanafahamu jinsi Waingereza walivyo “vichaa” kwa soka.Hawa watu wanaupenda mchezo huo kupita kiasi,japokuwa michezo kama rugby na kriketi nayo ina wapenzi wa kutosha pia.Kimsingi,mapenzi ya soka hapa hayazingatii ukubwa wa klabu kama ilivyo huko nyumbani ambako takriban kila mpenzi wa soka ni aidha mwana-Simba au Yanga, bila kujali kama yuko Ifakara,Tunduru,Mkomazi au Ujiji.Timu nyingi za hapa ziko kama wawakilishi wa miji flani,na ikitokea mji una timu mbili maarufu basi kunakuwa na takriban mgawanyo sawa wa wapenzi wa timu hizo.Na uzuri wa mapenzi ya soka hapa ni kwamba hata timu ikishuka daraja bado watu wanaendelea kuipenda.Labda tuseme kuwa hapa watu wana mapenzi ya dhati na timu zao,na wanaendelea kuzishabikia liwake jua au inyeshe mvua.

Kutokana na ukereketwa uliokithiri katika soka, Waingereza wamekuwa wakipendelea kuona timu zao zikiwa chini ya miliki yao wao wenyewe. Lakini katika miaka ya karibuni hali halisi imeanza kubadili jiographia ya umiliki wa vilabu vya soka vya nchi hii. Chelsea ilijikuta ikisalimu amri kwa mabilioni ya Mrusi Roman Abramovich, Manchester United nayo ikasalimu amri kwa familia ya Glazier ya Marekani, Aston Villa ikaangukia mikononi mwa Mmmarekani mwingine Randy Lerner, na wiki hii Liverpool nayo imejikuta ikidakwa na mabilionea wa Kimarekani George Gillett na Tom Hicks.Kwa upande wa Scotland, klabu ya Hearts nayo inamilikiwa na tajiri Mrusi mwenye uraia wa Lithuania Vladmir Romanov.Na usidhani kwamba matajiri hawa wamefanikiwa kuzimiliki klabu hizi kirahisi.La hasha,kilichowasaidia ni mabilioni ya fedha zao ambazo pamoja na upinzani kutoka kwa Waingereza wazawa zimefanikiwa kulainisha mioyo magumu.Hawakukosea waliosema penye udhia penyeza rupia,ila hapa kinachopenyezwa ni mamilioni ya pauni za Kiingereza.

Na hawa matajiri wanaleta mabadiliko ya kweli katika soka la nchi hii.Kinachoitwa “Mapinduzi ya Roman (Abramovich)” kimepelekea klabu hiyo ya London (Chelsea) kufanikiwa kuchukua makombe kadhaa ambayo kabla ya hapo ilikuwa ni kama ndoto za mchana.Kwa upande wa Skotland,Romanov amefanikiwa kuibadili Hearts hadi kufikia kutishia ubabe uliozoeleka wa wapinzani wakuu (Old Firm) Glasgow Rangers na Celtic.Klabu zinalazimika kukubali wamiliki kutoka nje kutokana na ukweli kwamba gharama za uendeshaji ziko juu sana,hasa linapokuja suala la kununua wachezaji wakali kimataifa.Ni hivi,timu inahitaji wachezaji wenye uwezo wa kuipeleka timu hiyo kwenye mashindano ya kimataifa ambayo licha ya kujenga heshima ya timu,huleta mamilioni ya fedha kwa njia ya udhamini na matangazo.Wachambuzi wa mambo ya soka la hapa wanatabiri kuendelea kwa ujio wa matajiri kutoka nje kuja kumiliki vilabu vya hapa hususan vile vyenye majina lakini vinasuasua kutokana na ukata.

Huko nyumbani klabu zetu “kuu” za Simba na Yanga ni vurugu tupu.Mara usikie timu iko chini ya Rais mara iko chini ya Mkurugenzi,basi alimradi ni vurugu mtindo mmoja.Nimesoma sehemu flani kuwa “Rais” wa Yanga anataka kuvunja uongozi na kuuweka mikononi mwa kamati itayojumuisha makundi ya Yanga-Kampuni,Yanga-Asili na Yanga-Academia.Timu moja makundi matatu!Ukijiuliza makundi hayo yanatokea wapi,utabaini kuwa sanasana ni matokeo ya songombingo za wanaojiita “wanachama.”Wanachama gani ambao hawataki kuona maendeleo ya klabu yao?Wengi wa hao wanaojiita wanachama ni wepesi wa kupiga kelele dhidi ya kocha wakati wao wenyewe hawajahi hata kucheza chandimu.Kibaya zaidi ni kwamba hao “wanachama” hawana mchango wowote wa kiuchumi kwa klabu,na ndio maana kila unapojiri msimu wa usajili inabidi klabu itembeze bakuli kwa wafadhili.

Hapo Msimbazi nako hakuna tofauti na watani wao.Nimesoma kwenye gazeti moja kwamba “picha haziivi” kati ya Mwenyekiti na Katibu wake mkuu.Inachekesha zaidi kusikia kuwa kiongozi mmoja mwandamizi wa klabu hiyo alitaka “kuanzisha vita” kwa vile tu alipewa fedha pungufu baada ya mechi.Tuwe wakweli,makundi ya wahuni ndani ya vilabu hayawezi kutoa viongozi bora.Na hapa nataka niwe mu-wazi zaidi:binafsi niliposikia baadhi ya wana-Taliban wamefanikiwa kuchukua uongozi ndani ya Simba nilijua dhahiri kuwa muda si mrefu zile chokochoko walizokuwa wakizifanya kutoka msituni zitahamia ndani ya uongozi.Hivi hao Taliban walikuwa wanapinga nini kabla hawajaingia madarakani?Na je baada ya kuingia madarakani wamebadili nini kwa mujibu wa yale yaliyowapeleka msituni?

Matatizo ya Simba na Yanga ni njaa.Na dawa pekee ya njaa ni chakula.Na chakula kinachohitajika katika klabu hizo ni fedha.Na fedha zinazohitajika sio za wafadhili bali watu wenye mamlaka kamili ya kuziendesha klabu hizo kibiashara.David Beckham amenunuliwa kwenda kucheza soka Marekani sio tu kwa vile ni mtaalam sana wa krosi na free kicks bali pia jina lake ni biashara tosha,kitu wanachokiita “Brand Beckham,” na Simba na Yanga zinastahili kabisa kuwa na “Brand Simba” au “Brand Yanga” Umaarufu unalipa,na laiti Simba na Yanga wangetambua kuwa wana utajiri mkubwa unaotokana na umaarufu wao basi pengine kusingekuwa na ubabaishaji unaendelea hivi sasa.Naamini kabisa kuwa wapo watu wenye uwezo wao ambao wangependa kuwekeza kwenye klabu hizo lakini wanahofia hao wanaojiita wanachama,ambao huwa mbogo pindi wakisikia uongozi unataka kuongeza ada ya uanachama kwa ajili ya maendeleo ya klabu.Naamini wapenzi wengi wa soka watakubaliana nami kwenye imani yangu kwamba adui namba moja wa maendeleo ya Simba na Yanga ni hawa jamaa wanaojiita wanachama.Inafahamika kuwa liinapokuja suala la uchaguzi kwenye vilabu,hawa jamaa huhangaika kuwapigia debe watu ambao wanaamini pindi wakiingia madarakani watawakumbuka kimaslahi.Na kiongozi atakayeamua kwadhibiti wababaishaji hawa anakuwa hana uhai mrefu kwenye uongozi kwa vile anaonekana hana manufaa kwa hao wenye njaa zao.

Nimesema Simba na Yanga zina utajiri mkubwa unaokaliwa.Kuna mamilioni ya wapenzi ambao miongoni mwao ni watu wenye uwezo mkubwa kiuchumi na kitaaluma.Hawa,na sio hao wababaishaji wachache wanaojiita wanachama,ndio wanaoweza kuleta mabadiliko kwenye vilabu hivi.Kama kweli hao wanachama wangekuwa wanataka maendeleo ya vilabu hivyo basi wasingepingana na mawazo ya kuzigeuza klabu hizo kujiendesha kibiashara.Wanachama hawataki kuziona klabu hizo zikigeuka kuwa makampuni kwa vile wanajua ikitokea hivyo basi migogoro itakwisha,na migogoro ikiisha inamaana kuna watu watabaki wanapiga miayo ya njaa kwa vile migogoro hiyo inawaletea ridhki.Yayumkinika kabisa kusema kwamba Simba na Yanga hazihitaji wanachama bali zinahitaji watu wenye mapenzi ya dhati ambao wataleta maendeleo ya kweli kwa klabu hizo.

Mwisho,kama kuna kundi ambalo limekuwa likitumia vibaya sana uhuru wa kwenda mahakamani basi ni hao wanaojiita wanachama.Utakuta kundi moja linafungua kesi,jingine linafungua kesi dhidi ya kundi la mwanzo,na jingine linafungua kesi ya uhalali wa kundi jingine,na kadhalika na kadhalika.Natambua kuwa kwenda mahakamani ni haki ya msingi ya kila raia lakini ni muhimu pia kufahamu kuwa uhuru ukitumiwa bila busara inakuwa kero.Katika hili ambalo lina mantiki za kisheria,waheshimiwa wabunge wanaweza kutusaidia kututengenezea mswada wa kuwabana wababaishaji kwenye medani ya soka na michezo mingineyo.

Alamsiki

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.