19 Nov 2008


UONGOZI wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) umekifunga chuo hicho kwa muda usiojulikana kutokana na mgomo wa wanafunzi.

Uongozi wa chuo hicho umefikia uamuzi huo, baada ya wanafunzi katika chuo hicho kufanya mgomo kuishinikiza serikali kuwarudisha vyuoni wanafunzi waliofungiwa.

Kabla ya kufungwa kwa chuo hicho jana, bodi ya chuo hicho ilifanya kikao, ili kujua wachukue uamuzi gani.

Awali, akizungumza na Tanzania Daima jana chuoni hapo, Rais wa DIT, Cleophace Maharangata, alisema mgomo wao bado unaendelea lakini bodi ya chuo inafanya kikao kuamua kama chuo kifungwe ama la.

“Sisi tunasubiri tamko baada ya kikao…uamuzi wowote utakaotolewa sisi tupo tayari,” alisema.

Naye mwalimu wa chuo hicho ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini alisema mgomo huo upo kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza, huku wanafunzi wa astashahada (diploma) wakiendelea na masomo kama kawaida.

Awali Rais wa wanafunzi hao, alisema mgomo huo ulianza rasmi juzi baada ya wanafunzi kutoingia madarasani huku wakiwa wameshika mabango yaliyobeba ujumbe mbalimbali.

Kufungwa kwa chuo hicho kunafanya idadi ya vyuo vilivyofungwa kufikia saba. Vyuo vingine ambavyo vimeshafungwa ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Chuo Kikuu cha Elimu Mkwawa (MUCE), Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Moshi Ushirika.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.