8 May 2009


Venance George, Kilombero

BAADHI ya wadau katika Wilaya ya Kilombero, wameitahadharisha serikali kuhusu uanzishwaji wa taasisi zenye mtazamo kama wa Deci ili kuwanusuru wananchi wasipoteze mali zao.

Tahadhari hiyo inafuatia kuanzishwa kwa PUFDIA, katika mji mdogo wa Ifakara ambayo watu wanaifananisha na Deci. Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wadau hao, Ibrahim Madon na Kenedy Haule waliishauri serikali kudhibiti uanzishwaji wa taasisi kama hizo. Walisema kama serikali haitakuwa makini, baadhi ya watu wachache wanaojali maslahi yao, watakuwa wanaanzisha taasisi hizo na kuendelea kuwakamua wananchi maskini.

Walitolea mfano wa Deci ambayo ilipigwa marufuku na serikali hivi karibuni, baada ya kuanzisha kwa mchezo wa upatu ambao baadaye ungesababisha hasara kubwa kwa wateja wengi wao wakiwa ni wananchi maskini. Taasisi ya PUFDIA imeingia wilayani humo hivi karibuni na kujinadi kwamba ni taasisi mpya inayotoa huduma za miradi mitano endelevu kwa ajili ya maendeleo ya watu wa nchi nzima.

Miradi inayoshughulika na taasisi hiyo ni pamoja na udhamini wa masomo ya sekondari hadi chuo kikuu kwa kwa mtoto wa mtu yeyote. Katika mchakato wake taasisi hiyo inaeleza kuwa chini ya mradi wa elimu, itatoa fedha za kulipia gharama zote za masomo na bajeti inayotolewa kwa kila mtoto ni Sh 570,000 kwa wale wanaosoma shule za msingi wakati wale wanaosoma shule za sekondari watapewa Sh980,000 na Sh 2.64 milioni kwa vyuo vikuu.Gharama hizo ni kwa kila muhula.

Mradi mwingine ni wa kujengewa nyumba za thamani ya Sh 6 milioni kama msaada kwa mwananchi yeyote mwenye shida ya nyumba wakati wanaotaka kujengewa shule wanatakiwa kwenda katika ofisi hiyo kujaza fomu yenye uwezo wa kujengewa shule yenye thamani ya Sh 46.2 milioni

Taasisi hiyo pia imesema itasaidia wananchi kwa kuwapa mikopo isiyo na riba yenye thamani ya Sh 2,470,000. Mwandishi wa habari hizi alikwenda katika ofisi za PUFDIA na kuwahoji maofisa wake ambao hata hivyo, hawakutaka kutaja majina yao. Maafisa hao walidai kuwa huduma wanazotoa ni halali na kwamba wanalipia kodi.

Kwa mujibu wa maelezo yao, taasisi hiyo inafadhiliwa na taasisi kubwa ya kidini iliyoko nje ya nchi. Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, alikiri kuwepo kwa taasisi hiyo na kwamba maafisa wake, walikwenda ofisini kwake kuomba kutoa huduma hiyo.

Alisema hata hivyo atalipitia upya jalada la taasisi hiyo na kuelezea mustakhabali wake.


CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.