4 Jan 2010


Je mama Kikwete ameanza kampeni kwa ajili ya mumewe?

na Nkwazi Mhango

Siku hizi mke wa rais, Salma Kikwete, anaonekana kwenye kurasa za mbele za magazeti karibu kila siku akiwa mikoani akihamasisha hili na lile. Wengi wanahoji. Kwanini sasa na si tangu mwanzo mume wake alipoingia ikulu? Na kwanini asiseme wazi kuwa anampigia kampeni mumewe? Maana, inajulikana alivyo mwana CCM damu damu tena mjumbe wa vikao vyake?

Watetezi wake wanaweza kusema anafanya kazi ya shirika lake lisilo la kiserikali la WAMA. Haiwezekani mumewe akawa mkuu wa serikali naye akawa na shirika lisilo la kiserikali kusiwe na mgongano wa kimaslahi kisheria. Uzoefu tulioupata toka kwa Anna Mkapa ungetosha kumsaidia rais Jakaya Kikwete kuondokana na aina hii ya ufisadi sugu na unyemelezi kwa kutumia mgongo wa ikulu kama angekuwa ni mtu wa kujifunza na kudhamiria kutenda haki kwa taifa.

Ngo yake ni ya mashaka-kwanini ianzishwe baada ya mumewe kuwa rais? Kuanzisha NGO baada ya mume kuwa rais ni ishara tosha ya ufisadi na usasi wa ngawira. Mbona hatuoni wake wa viongozi wa vyama vingine wakiwa na NGOs? Hata wakiwa nazo nani atazichangia iwapo wanaochangia NGOs za wake wa marais wanatafuta kuwa karibu na ikulu ili waihujumu nchi kwa kupata upendeleo kama ilivyokuwa kwa EOTF ambayo ilitumiwa na watu wengi kuliibia taifa? Mke wa Kaisari hapaswi kutenda tendo lenye kuweza kutia shaka au doa utawala wa mumewe.

Tuliishi na kumuona baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere. Mkewe-mama Maria-hakuwahi kujihusisha na upuuzi mdogo mdogo wa kutafuta pesa kwa mgongo wa mumewe.

Niliwahi kuwaandikia barua EOTF na WAMA kuwaonya juu ya hatari ya kuitumia ikulu. Hawakuwahi kunijibu zaidi ya kufumba macho na kuendelea kutengeneza pesa kwa mgogo wa ikulu. Ila nafurahi. WAMA wamefanya jambo moja (la maana la kuondoa aibu)-kuondoa maneno yasemayo WAMA Foundation the office of the First Lady of the United Republic of Tanzania kwenye wavuti wao. Niliandika baruapepe ifuatayo kwa WAMA tarehe 3 Septemba 09:

Kama mzalendo, nimejaribu kukusanya baadhi ya maoni kuhusiana jinsi ufisadi unavyoingia ikulu kiasi cha kututatiza. Kwa sasa Anna Mkapa mke wa rais wa zamani na mumwe wako msambweni. Ukiangalia kinachofanywa na WAMA hakina tofauti na Fursa sawa kwa Wote (Wake za wakubwa).
Kuondoa aibu, nimejitolea kuwasiliana nanyi ili angalau mjue tunavyojihisi kwenye wimbi hili la ufisadi wa kutumia madaraka ya waume zenu. Mama Salma NGO yako ni ulaji mtupu kusema ukweli. Acha kuna kesho. Ni uamuzi wako kuamua. Kuna kesho wakati madaraka yatakuwa mikononi mwa wengine. Hasa nikizingatia kilichompata Regina Chiluba ambacho kinapaswa kumpata hata Anna Mkapa, nimeona bora niseme hata kama nitapuuziwa. Ila najua ujumbe utafika. Someni alama za nyakati na mjue kuwa madaraka yana mwisho na yanalevya. Kuna siku mtakumbuka mchango huu.
Kila la heri,

Bahati mbaya sana , hata wavuti wa Kurungenzi ya habari Ikulu unaonekana kutangaza biashara ya WAMA badala ya wizara za serikali! Ajabu hakuna anayestuka wala kupiga kelele!

Kama umma ukishupaa NGO hii inaweza kufutwa hata na mahakama kutokana na mgongano wa maslahi ukiachia mbali kuwa kichaka cha ufisadi kutokana na uwezekano wa kuchangiwa pesa chafu kutokana na kutokuwapo sheria makini ya kuchuja na kutangaza wafadhili wa WAMA.

Hata hivyo nimefarijika kuwa sauti yangu imesikika na fedheha imeondoka. Maana neno Jamhuri ya Muungano, kisheria, halipaswi kutumiwa na mtu au taasisi yoyote isipokuwa mihimili mitatu ya dola yaani Bunge, Mahakama na Utawala. Cheo cha Ofisi ya First lady hakimo katika katiba yetu.

Kwanini mapenzi kwa wanawake na watoto yaanze baada ya kuupata urais kama siyo gea ya kuitumia vibaya ikulu? Ina maana rais na washauri wake hawalioni hili au wameridhia kwa sababu NGO ya mke wa rais inaweza kutumika kama kivuli cha kuanza kampeni hata kabla ya tume kutanganza hivyo? Inabidi tustuke. Ajabu hata wapinzani hawajaliona hili!

Tanzania inaweza kuwa nchi pekee ambapo rais na mkewe wote ni marais. Kikwete ni rais wa jamhuri huku mkewe akiwa rais wa WAMA. Ukitaka kujua hili jikumbushe mapokezi anayopewa na coverage anayopata Salma kwenye vyombo vya habari. Ajabu ukitafuta uhalali wake kikatiba haupo!

Hata kama anajulikana kwa ubabe na upayukaji wake, bado mke wa rais wa Kenya Lucy Kibaki hana mamlaka kama aliyo nayo Salma ambaye anaweza kuingia mkoa wowote kwa kisingizio cha NGO yake na kufanya shughuli za kisiasa kama kulakiwa na viongozi wa mikoa na kukagua miradi ya maendeleo ukiachia mbali kutoa kauli mbiu zinazoonyesha wazi kumpigia debe mumewe.

Salma anchomzidi Lucy ni ile hali ya kufanya kitu waitacho waingereza one woman show. Kwani kila lilipo jina WAMA yupo yeye. Hii maana yake ni kwamba yeye ni dikteta na mpenda madaraka anayetaka kufanya kila kitu peke yake. Kwanini hatuoni makamu wake au hata wasaidizi wengine wakifanya shughuli za WAMA kama kweli ni ya umma kama anavyodai? Kuthitibitisha hili, tembelea tovuti ya WAMA uone ukweli huu. Hii haiwezi ikawa taasisi ya wanawake na watoto wa Tanzania .

Kuonyesha kuna namna ya kampeni na kutumia mamlaka ya mume wake, hivi karibuni, Mama Kikwete amewahi kutoa namba yake ya simu ya mkononi ambayo ni 0754-294450 kwa wanawake mkoani Singida ili waweze kumpigia au kumtumia ujumbe mfupi wa maneno pindi waume zao watakapowanyanyasa kutokana na kitendo cha wao kwenda kupima kwaajili ya kujua afya zao. Japo kwa juu hili linaweza kuonekana ni jambo bora, kwa mtu anayejua mipaka ya mamlaka yake na utaratibu wa utawala kisheria, angeshauri wahusika waelekeze madai yao kunakohusika-polisi, vituo vya kutetea haki za binadamu hata wizarani.
Licha ya kuwa ubabe, hii ni kampeni ya wazi kuonyesha wahusika wanawajali wananchi jambo ambalo si kweli. Kwanini hasira zake zisielekezwe kwenye kumshauri mumewe kupambana na ufisadi kama ana uchungu na nchi hii? Yaani hajui kuwa ujinga na umaskini ndivyo vyanzo vya haya yote? Sijui hata kwenye kupokea misaada anauliza usafi wa mtoaji.

Kwa nijuavyo upenzi wa sifa wa watawala wetu na watu wao, kama utafanyika uchunguzi huru juu ya matumizi ya MAWA, ushingae pesa inayotumiwa kwenye ziara ikawa kubwa kuliko hiyo inayowafikia walengwa. Bahati mbaya sijwahi kusoma popote taarifa ya mahesabu ya mwaka ya si WAMA wala EOTF.

Wengi wanaweza kuona kama tunamuandama mke wa rais au kutotambua umuhimu wa kupigania haki za akina mama. Kwanini mke wa rais wakati tuna wizara yenye watendaji wanaolipwa pesa ya kodi yetu? Kwanini misaada hiyo anayopokea isipelekwe wizarani au kwenye mashirika huru kama kweli ana uchungu na walengwa na si kujipatia umaarufu, pesa na kubwa zaidi kutumia ikulu kwa manufaa binafsi yawe yake au mumewe na marafiki zake?

Je Salma Kikwete ameanza kampeni kwa ajili ya mumewe hata kabla ya kipenga kupulizwa? Je akina mama wa Tanzania wataingia mkenge wake huku waume na kaka zao wakizidi kuteswa na sera za Kikwete za kuvumilia mafisadi? Je atawalainisha wasahau kuwa Kikwete hajatimiza ahadi hata moja? Je watahoji uhalali wa NGO yake na kumwambia ukweli kuwa ni ya mashaka na ulaji?

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.