31 May 2010


Ukisoma habari zifuatazo unaweza kukubaliana nami kuwa AKUTUKANAE HAKUCHAGULII TUSI.Katika habari ya kwanza tunashuhudia Waziri wetu wa Fedha akiongea vitu ambavyo vinaleta maana tu vikiangaliwa kwa maadnishi lakini sio mtaani.Na katika habari ya pili,tunashuhudia uzembe uliozoeleka wa kitokee kwanza kisha tufanye kitu flani.Yaani siku zote hizi mtu aliyekabidhiwa dhamana ya kuongoza Jeshi la Polisi alikuwa hafahamu kuwa kituo cha polisi kisicho na silaha hakina tofauti simba wa karatasi!
Hebu soma habari husika hapa chini
Mkulo: Uchumi unazidi kukua 

Saturday, 29 May 2010 09:22

Exuper Kachenje

SERIKALI imesema kuwa ukuaji wa pato la taifa katika unakadiriwa kuongezeka na kwamba pato halisi litakua kwa asilimia 7 katika mwaka 2010.

Akiwasilisha taarifa ya mwelekeo wa uchumi kwa mwaka 2009 na mwelekeo katika kipindi cha kuanzia 2010 hadi 2013 mbele ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo alisema kuna matarajio makubwa uchumi kuendelea kukua.

Huku akiwaomba radhi wabunge kwa kuchelewa kuwapa nakala ya taarifa hiyo, Mkulo alisema maelezo hayo yalipitishwa juzi asubuhi na Baraza la Mawaziri.

"Naomba radhi waheshimiwa kwa kuchelewa kuwapatia nakala ya taarifa hii kwa kuwa imepitishwa jana asubuhi (juzi) na Baraza la Mawaziri hivyo imechelewa kuchapwa," Mkulo alisema.

Mkulo alisema kuwa katika mwaka 2011, pato halisi la uchumi litakuwa kwa asilimia 7.1, mwaka 2012 asilimia 7.4 na hadi kufikia mwaka 2013 pato halisi la taifa litafikia asilimia 7.8.

“Kama ilivyotarajiwa athari za msukosuko wa uchumi zilikuwa za mpito, hivyo ukuaji wa pato la taifa unakadiriwa kuanza kuongezeka. Pato halisi litakua kwa asilimia 7.0 mwaka 2010, asilimia 7.1 mwaka 2011, asilimia 7.4 mwaka 2012 na kuendelea kuongezeka hadi asilimia 7.8 mwaka 2013,” alisema Mkulo.

Alifafanua kuwa malengo hayo yanatarajiwa kufikiwa kwa kutekeleza sera na misingi ya uchumi kwa kuzingatia mambo mbalimbali, ikiwemo mwenendo wa uchumi wa dunia na hitaji la kujenga uwezo kukabiliana na athari za msukosuko wa uchumi wa dunia.

Alitaja misingi mingine kuwa ni kuendelea kutengemaza vigezo muhimu vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii hasa mfumuko wa bei, kuweka msukumo katika utekelezaji Dira ya Maendeleo ya Taifa, Mkukuta awamu ya pili, Kilimo Kwanza na kuelekeza rasilimali kwenye maeneo chochezi ya uchumi kwa haraka zaidi.

Kwa mujibu wa Mkulo katika kipindi hicho miradi inayopewa kipaumbele katika mwongozo huo wa bajeti itakuwa ni pamoja na miundombinu, uendelezaji ardhi na makazi pamoja na vitambulisho vya taifa.

Vingine ni nishati, viwanda, sekta ya fedha na pia kutaja uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba mwaka huu kuwa ni kipaumbele cha kipekee kwa serikali katika mwaka huu kwa lengo la kuhakikisha unafanyika kama ilivyopangwa.
Waziri huyo alisema katika muda huo kasi ya upandaji wa bei inakisiwa kupungua hadi asilimia 8.0 kufikia mwezi Juni mwaka huu na kupungua zaidi hadi asilimia tano ifikapo Juni 2011.

Aidha, alisema katika kipindi hicho mapato ya ndani ya taifa yatafikia uwiano wa asilimia 17.3 kwa mwaka 2010/11; asilimia 17.4 mwaka 2011/2012 na asilimia 17.6 ifikapo mwaka 2012/2013.

Alisema serikali pia inalenga kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayokidhi uagizaji bidhaa kutoka nje na huduma kwa kipindi kisichopungua miezi mitano; kuwa na viwango imara vya ubadilishaji wa fedha; kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara na kuedeleza kilimo na kupunguza viwango vya riba.
Kuhusu biashara, Mkulo alisema Tanzania imeshuka katika vigezo vya urahisi wa kufanya biashara kutoka nafasi ya 126 kati ya nchi 183 na kuwa ya 131 mwaka 2009.

Kuhusu mapato ya ndani, Waziri Mkulo alisema yaliongezeka kwa asilimia 18.1 kufikia Sh4,293.1 bilioni mwaka 2008/09; kutoka Sh3,634.6 bilioni mwaka 2007/08 na kwamba kiasi hicho ni pungufu ya asilimia 10 kwa mwaka 2008/09.

Kwa kipindi cha Julai 2009 hadi Machi 2010, mapato ya ndani yalifikia Sh3,490.3 bilioni ikiwa chini ya asilimia 8.7 ya makisio ya Sh3,924.9 kwa kipindi hicho akieleza kuwa hali hiyo ilitokana na athari za kuyumba kwa uchumi wa dunia.

Mkulo alisema kwa kipindi cha Julai 2009 hadi Machi mwaka huu matumizi ya serikali yamefikia Sh6,143.9 bilioni kati ya makisio ya Sh6,718.7 kwa kipindi hicho, ikiwa ni upungufu wa asilimia tisa uliotokana na upungufu wa mapato.

Wakichangia maelezo hayo wabunge walitaka serikali ieleze itafanya nini kuwezesha wananchi kumiliki uchumi badala ya kumiliki asilimia 10 pekee kama ilivyo sasa.

CHANZO: Mwananchi

IGP Mwema afuta vituo

na Sitta Tumma na Ali Lityawi
SIKU tatu baada ya wananchi wa Kata ya Mbarika, wilayani Misungwi, mkoani Mwanza kuvamia kituo cha polisi na kuua majambazi watatu, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema ameanza kulikarabati upya jeshi hilo.
Tanzania Daima imethibitishiwa hilo; ukarabati wa jeshi hilo umelenga kuvipunguza kwa kuvifutilia mbali baadhi ya vituo vidogo visivyokuwa na silaha wala askari wa kutosha.

Wakati IGP Mwema akipanga kuvifumua vituo hivyo, jeshi la polisi mkoani Mwanza halijamkamata mtu hata mmoja kuhusiana na tukio la kuvamia na kuvunja kituo cha polisi Mbalika na kuua watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.

Akithibitisha yote hayo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanmza, Simon Sirro (RPC), alisema IGP Mwema yupo katika mikakati ya kupunguza utitiri wa vituo vidogo vidogo vya polisi, kwani vimeonekana havina faida kwa wananchi.

“Unajua vituo hivi vidogo visivyokuwa na silaha havina faida kwa maana hiyo mkuu wa polisi kwa sasa yuko katika mpango wa kuvipunguza.

“Mkakati huu madhumuni yake ni kuwa na kituo kimoja kila kata chenye silaha na askari wa kutosha,” alisema Kamanda Sirro.

Mei 27 mwaka huu majira ya saa 1:30 jioni, wananchi wa Mbalika, wilayani Misungwi mkoani hapa, walivamia na kuvunja kituo cha Mbalika kisha kuua watuhumiwa.

Moja ya sababu za wananchi hao kuvamia na kufanya mauaji katika kituo hicho, inaonekana ni kutokuwa na silaha pamoja na askari wa kutosha kituoni hapo na kumshtua IGP Mwema.

Kamanda Sirro, alipoulizwa mikakati ya kupunguza vituo hivyo, alisema hana jibu anayepaswa kulizungumzia ni IGP Mwema pekee.

Tanzania Daima, ilipomtafuta IGP Mwema kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi, simu yake ilipokelewa na msaidizi ambaye alidai yuko mkutanoni.

“Afande IGP yupo kikaoni huku Kilolo mkoani Iringa; atakuwa Dar es Salaam kesho (leo),” alisema msaidizi huyo.


4 comments:

  1. Kufuta vituo vya polisi inatuonesha kuwa bado jeshi letu la polisi linasafari ndefu sana kuingia kwenye dunia hii ya upolisi wa kisayansi na teknolojia...Ukweli ni kwamba jeshi letu ni maarufu sana kwa kutumia nguvu nyingi na akili kidogo. Kifupi jeshi la polisi halina maarifa ndiyo maana aliendani na wakati uliyopo sasa. Alichokifanya Afande mwema ni uthibitisho wa hiyo kauli yangu hapo awali.

    ReplyDelete
  2. Wanahangaika na vivuli vyao wao wenyewe walarushwa na wabadhirifu ndani na nje ya serikali ndiyo maswahiba wao. Hivyo madhara ya kuichekelea rushwahuendana na kuongeza uhalifu. Wasipobadilika katika kuwafikisha mafisadi katika ngazi husika za kisheria...hata kama nchi nzima watakuwa polisi basi bado uhalifu utakuwa pale pale...ndiyo sababu nikasema kwamaba wanahangaika na vivuli vyao wenyewe..

    ReplyDelete
  3. uchumi haukui wala nini unazidi kushuka ingekuwa nchi za watu mkulo saa hizi angetakiwa ajiuzulu kwa kudanganya umma leo asubuhi nimesikiliza kipindi cha watanzania tuzungumze magazeti radio free inasemekana serikali imezidisha matumizi hasa kwa safari za nje za viongozi na posho zisizokuwa na msingi jamani hivi tutafika kuwa na maendeleo kama wenzetu jibu ni hakuna ccm mpaka lini

    ReplyDelete
  4. Takwimu zote zimewakilishwa kwa asilimia na hiyo inaonesha ni usanii mtupu kwa Mkulo...Bunge la makabwela katika nchi ya uingereza iliwahi kumbana waziri wa ulinzi enzi hizo kutoka labour kuhusiana na idadi ya helicopta zilizopo huko afaghanstan baada ya kutumia takwimu za aslimia na baadae kumtambua kwamba ongezeko la vifaa vya kijeshi ilikuwa kuongoze ni vichache

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.