26 Jun 2010

Sijui ni ukosefu wa mawasiliano au uzembe tu,au pengine ni mkakati wa makusudi wa kutoa kauli zinazotofautiana ili baadaye iwe rahisi "kuziruka kimanga",lakini ni dhahiri kuwa mmoja kati ya viongozi hawa anatudanganya.Wakati Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe akirejea ahadi kama ya mwaka 2005 (wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu) kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi,Makamu Mwenyekiti wa CCM Pius Msekwa anasema bayana kuwa suala hilo halipo (labda Waislamu wenyewe walishughulikie "kivyao").Hebu soma kwanza hapa chini

Kwa mujibu wa Gazeti la Tanzania Daima: SERIKALI imesema Mahakama ya Kadhi itaanza katika mwaka wa fedha 2010/11 baada ya jopo la wanazuoni wa Kiislamu wanaoziangalia na kuzihuisha sheria za Kiislamu kukamilisha kazi hiyo.

Jambo hilo lilibainishwa jana bungeni na Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe wakati akisoma hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2010/2011 ambapo ameliomba Bunge limuidhinishie kiasi cha sh bilioni 116.8

Alisema kuwa jopo hilo linaziangalia na kuzihuisha sheria za Kiislamu zinazohusiana na ndoa, mirathi na urithi kwa madhumini ya kuziorodhesha ili zitambuliwe chini ya sheria za dini ya Kiislamu (Islamic Law resstatment act).

Aliongeza kuwa jopo hilo lilianza kazi hiyo baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kukutana na Mufti, Sheikh Mkuu, Issa Bin Shaaban Simba, na kukubaliana kuwa waanzishe mchakato wa Mahakama ya Kadhi.

Lakini Gazeti la Majira linaripoti kwamba:

Katika hatua nyingine, Bw. Msekwa amefafanua sababu za ilani ya CCM mwaka huu kutohusisha kipengele cha uanzishwaji wa Mahakam ya Kadhi kama ilivyokuwa mwaka 2005.

Alisema kuwa ahadi hiyo iliyotolewa 2005 tayari utekelezaji wake umekamilika.

Katika ilani hiyo, kifungu namba 108(b) CCM iliahidi kulipatia ufumbuzi suala la kuanzishwa mahakama ya kadhi Tanzania bara, ambalo limekamilika kwa kukabidhi wenye dini yenyewe wahusike katika uanzishwaji wa mahakama hiyo, kwa kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siyo ya kidini.

"Serikali inaweza kukubali au kukataa, ndiyo maana ya kulipatia ufumbuzi lakini watu wanalitafsiri vibaya kuwa
serikali kupitia kifungu hicho imekubali kuanzishwa kwa mahakama hiyo wakati sivyo," alisema Bw. Msekwa.

Alibanisha kuwa serikali ilifanyia kazi kupitia Tume ya Kurekebisha sheria ambayo ilishauri kwamba haitakuwa sahihi kwa mahakama ya kadhi kuundwa na serikali kwa kuwa ni suala linalohusu taratibu za dini ya kiislamu.

Aliongeza kuwa baada ya serikali kupata ushauri huo ilifanya uamuzi kwamba haitaunda mahakama ya kadhi lakini kwa kuwa suala hilo linahusu taratibu za dini la kiislamu, waislamu wapo huru kuunda mahakama hiyo ndani ya taratibu za dini yao.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.