8 Sept 2010

Image and video hosting by TinyPic
Josephine Mushumbusi, amezungumza kupitia Mwanasheria Mkuu wa Chadema, ambaye pia ni wakili wa Dk Willibrod Slaa, Tundu Lissu, akaviambia vyombo vya habari kuhusu tuhuma zinazowakabili yeye na Dk. Slaa kuwa kwa mara nyingine, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimerejesha mfumo wa uchaguzi unaobadilishwa kuwa mfumo ya kijinga (a silly season). Akasema kwamba CCM wamekuwa wakikishambulia Chadema kuwa ni chama Wachagga; kwamba baadhi ya viongozi wake ndio walimuua Chacha Wangwe; na kwamba Dk Slaa ametumwa na kanisa Katoliki kugombea urais; lakini baada ya kuona hadithi hizo zimepuuzwa, sasa wameibuka na suala jipya na “ndoa za Dk. Slaa” wakidhani zitawasaidia kugeuza macho ya umma kutoka kwenye masuala muhimu ya wakati huu.

Akasema CCM hawataki Dk. Slaa na Chadema wajadili wizi, ubadhirifu wa fedha na mali za umma; hawataki wajadili wizi wa Sh. bilioni 772 zilizoibwa katika mwaka 2008/9 tu, kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali; hawataki Chadema itaje majina ya wezi wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT); hataki Chadema wajadili jinsi JK na rafiki zake, akina Edward Lowasaa, Nazir Karamagi, Andrew Chenge na Rostam Azizi walivyofilisi taifa hili; hawataki Chadema ijadili madai halali ya wafanyakazi wa Tanzania na ahadi za ‘maisha bora kwa kila Mtanzania.’ CCM hawataki Chadema kijadili sera mbadala ambazo zinalenga kuwakomboa Watanzania kutoka lindi la umaskini.

Wanataka kulielekeza taifa zima katika kujadili masuala ya ‘chumbani’ kwa Dk. Slaa; analala na nani, ana wake wangapi, kawapata wapi na kadhalika; ili kwa kufanya hivyo mgombea wao awarubuni wananchi kwa ziara mikoani na ahadi kemkem zisizotekelezeka.

Tundu Lissu amesisitiza kuwa kila wanapoona wamebanwa, CCM huwa wanabuni njama za kukomoa washindani wao, kama walivyofanya huko nyuma. Alitoa mifano ya kilichotokea miaka ya 1995 na 2005.

Mwaka 1995: Kwa kumwogopa Mrema aliyekuwa tishio kwa CCM, walimtumia mwanamke mmoja, aitwaye Angelina, wakidai ni kimada aliyezaa na Mrema; akawa analala getini kwa Mrema, Masaki, Dar es Salaam. Wakamdhalilisha. Baada ya uchaguzi, Mrema akashindwa, na suala la Angelina halikujadiliwa tena.

Mwaka 2005 tishio la CCM ilikuwa Chama cha Wananchi (CUF), hasa Zanzibar. CCM wakamtumia Inspekta Jenerali wa Polisi, Omar Mahita, siku chache kabla ya uchaguzi, kudai kuwa amekamata lori lenye mapanga, majambia, visu na silaha nyingine zenye nembo ya CUF. Wakakipaka chama matope. Baada ya uchaguzi, hatukuelezwa lolote kuhusu visu hivyo.

Mwaka huo huo, katika uchaguzi wa ndani ya chama, baada ya kundi la JK kuona limezidiwa mno, likaamua kumzushia Dk. Salim Ahmed Salim likidai ni Mwarabu, na muuaji wa Rais Abeid Amani Karume. Wakamhujumu, Na baada ya uchaguzi hawakuzungumzia tena uarabu wa Dk. Salim.

Mwaka 2010: Tishio la CCM ni Chadema na Dk. Slaa. Baada ya kuona upepo unawaendea vibaya, CCM wameamua kufanya siasa za mtaro wa maji taka; hizi wanazotumia watu kumwandama Dk Slaa.

Tundu Lissu alisema kuwa Chadema hawako tayari kufanya siasa za majitaka; na kwamba Watanzania hawako katika kujadili mambo hayo, kama hali ya afya za wagombea, ambao baadhi wanadaiwa kuwa na virusi vya ukimwi kiasi cha kubadili damu kila baada ya miezi, na kwamba kwa sababu ya unyonge huo, baadhi yao waanguka mara kadhaa jukwaani.

Akasema wao hawatazungumzia baadhi ya wagombea urais wana wake wangapi, mahawara wangapi, na wamewaweka katika ofisi gani za umma, wapi wamepewa mikataba minono ya fedha kwa upendeleo, na kadhalika. Akasisitiza kwamba Chadema haitajibu uchafu unaosambazwa na vyombo vya habari, lakini akasema, “sauti yetu itasikika iwapo wataenda mahakamani.”
Akasema Chadema itazungumzia umaskini wa Watanzania na namna ya kuupunguza au kuuondoa; jinsi Tanzania ilivyo nchi ya tatu katika Afrika lakini wanakijiji wanalazimishwa kujenga shule za kata huku serikali ikifuja mabilioni ya pesa (kama hizo bilioni 772/- zilizotafunwa ndani ya mwaka mmoja.

Akasema Chadema itajadili malipo ya anasa kwa mawaziri, maisha duni ya polisi, walimu, wauguzi na makundi mengine yanayonyonywa katika jamii. Akasema Chadema itajadili jinsi ya kuboresha afya za wananchi.

Akasema, “hatutaki siasa za chumbani, bali za hadharani.”

Kwanini wamshambulie Dk Slaa? Kwa sababu ni Dk. Slaa.

- Ana rekodi ya kuwashinda CCM mara tatu, kwa miaka 15 mfululizo
- Amekuwa sauti kuu ya wananchi Bungeni, inayotetea masilahi ya umma
- Kuliko kiongozi yeyote aliyewahi kuwapo Tanzania ndani ya miaka 50, ni Dk Slaa pekee aliyetaja hadharani mafisadi 11 bla woga wowote. Walioathirika kwa ujasiri wake ndio hao wanaomsakama sasa kwa mambo ya chumbani badala ya mambo ya hadharani.


4 comments:

  1. Hatari tupu hii. Ukianza kuchambua ya wenzako hakikisha yakwako yako safi. CCM wameanza sasa inakula kwao.

    ReplyDelete
  2. wakizdisha wanavuliwa uraia....maslah ya wakubwa hayo.....ila hili la ukimwi kama kweli vile

    ReplyDelete
  3. MWAKA HUU CCM LAZIMA ILE KWENU KUANZIA KIKWETE NA RAFIKI ZAKE HATA KAMA ATAINGIA MADARAKANI BAC NI KWA KURA CHACHE SANA. DR. SLAA ANAMTOA JASHO NDIO MANA ANAANGUKA HADHARANI

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.