10 Nov 2010


Muungwana mmoja amenitumia comment ambayo kwa hakika imenigusa sana.Naomba niinukuu
Mbona umekatisha mijadala ya kuendeleza nchi ghafla mno. nilitegemea utakuwa na tasmini ya matokeo ya uchaguzi lakini umezimika ghafla. Vipi au jamani inakuwaje uchungu na nchi unakuwa kwa muda tu? Au wameshakutishia na wewe?
Naelewa kwanini mzalendo huyu anataka tufanye tathmini ya uchaguzi mkuu ambao wengi wetu tuliupa umuhimu wa kipekee kutokana na mwenendo wa mambo ulivyo huko nyumbani.Baada ya kushuhudia taifa likienda mrama kwa kugubikwa na ufisadi ilionekana ni lazima Watanzania wenye uchungu wa dhati kwa nchi yao wachukue hatua zinazostahili.Na hatua mwafaka ilionekana kuwa ni kuing'oa CCM madarakani.

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,Dkt Wilbroad Slaa,ameweka bayana msimamo wake kuwa uchaguzi huo ulichakachuliwa.Baadhi ya taasisi zilizotuhumiwa kufanya uchakachuaji huo zimejitokeza hadharani na kukanusha tuhuma hizo.Haihitaji hata cheti cha kozi ya siku 1 ya uchambuzi wa siasa kumaizi kuwa hakuna hata mmoja kati ya wanaotuhumiwa atakiri mchango wake katika kuirejesha CCM madarakani.Wakubali ili waadhibiwe?

Kadhalika,kuna dhana iliyojengeka kuwa katika uhalisia barani Afrika na katika baadhi ya nchi "za dunia ya tatu" sio rahisi kwa chama tawala kushindwa uchaguzi,na ikitokea kimeshindwa basi yayumkinika kuhitimisha kuwa hayo ni matokeo ya uzembe wa chama husika au migogoro ndani ya chama hicho.Hebu chukulia mfano mazingira ya uchaguzi wetu.Vyombo vya dola vilionyesha waziwazi kuipendelea CCM huku watendaji wa taasisi zinazopaswa kuwa huru wakijibidiisha kumlinda mgombea wa chama tawala.Ndio maana haikumtia hofu Mhariri wa Daily News,gazeti linaloendeshwa kwa kodi za walalahoi,kutamka bayana kuwa Dkt Slaa asingeweza kuwa rais hata baada ya miaka mitano.Kujiamini huko hakukutokana na uimara wa CCM bali ndoa ya kifisadi kati ya taasisi za umma na chama hicho tawala.

Tulisikia taarifa kadhaa kuhusu watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutowatendea haki wagombea wa vyama vya upinzani.Kadhalika,ilifika mahala Msajili wa Vyama vya Siasa akaamua kuweka wazi mahaba yake kwa CCM na kujipachika jukumubla kuitetea hata pale ilipokosea waziwazi.

Sasa unaweza kujiuliza,"kama tulishaona mwenendo wa aina hiyo ie wa kuitengenezea CCM mazingira ya ushindi,kwanini tulijipa matumaini kuwa Dkt Slaa angeibuka mshindi?".Jibu rahisi kwa mtizamo wangu ni kwamba kulikuwa na matumaini kuwa sauti kubwa ya umma ingeweza kukwaza jitihada zozote za uchakachuaji.Au hata kama jitihada hizo zingefanyika basi zingezidiwa nguvu na sauti hiyo ya umma.

Naomba kukiri hadharani kuwa hofu yangu kubwa haikuwa kwenye mikakati ya kundi dogo lakini lenye nguvu kubwa la mafisadi bali MTAJI MKUU WA CCM yaani umasikini wa Watanzania walio wengi.CCM inategemea sana masikini na hata matokeo "halali" yanathibitisha hilo ambapo maeneo yaliyogubikwa na umasikini ndio yaliyoipa CCM kura nyingi.Huu ni uhusiano ambao kitaaluma unaweza kuelezwa kama wa mnyanyasaji na mnyanywasaji (abuser-abused relationship).Mnyanyasaji anawekeza nguvu nyingi kumwaminisha mnyanyaswaji kuwa pasipo uwepo wake (mnyanyasaji) basi mnyanyaswaji hatakuwa na maisha.Ndio hadithi za amani na utulivu,umoja wa kitaifa,mshikamano,na madude mengine kama hayo.

Kitaaluma,mnyanyaswaji anaweza kufikia mahala akawa anaskia raha kunyanyaswa (punch drunk).Ni kama hali ya kuzowea makonde kwa bondia.Hakuna maelezo mengine mwafaka ya kuelezea namna watu wanaoamka wakiwa hawajui siku iyaisha vipi,wanaotembea maili kadhaa kusaka maji safi japo wafadhili wanamwaga fedha za miradi ya maji,wanaoshinda juani kutwa nzima na kulala vibambazani wakiuza peremende lakini bado wanaandamwa na jeshi la mgambo huku polisi wakiwawinda wawabambikizie kesi,wanaokwenda mahospitalini na kuambulia matibabu hewa kwa vile hakuna madawa,watu wenye watoto ambao makalio yanaota sugu kwa kukaa sakafuni mashuleni,watu ambao haki zao hazipatikani bila kutoa "kitu kidogo" kisha watu haohao wakipigie kura chama kinachostawisha mateso yao.

Na kwa waliodhani akina sie tuliokuwa tukipiga kelele za nguvu kutaka CCM iondoke tulikuwa na chuki binafsi basi matukio mawili yaliyojiri hata masaa 72 hayajapita baada ya CCM kurejea madarakani yanapaswa kuwafumbua macho.Tukio la kwanza ni la mtuhumiwa wa ufisadi wa rada,Mzee wa Vijisenti Andrew Chenge kuchukua fomu ya kugombea Uspika kisha kufanya press conference iliyojaa ngebe,nyodo na dharau kwa wote wanaokerwa na ufisadi.Binafsi,naamini kuwa Chenge katumwa na kundi flani linalotaka kuifakamia keki ya taifa kwa kasi ya marathon hasa kwa vile wanaelewa kuwa Awamu hii ya Tano inaweza kuwa ni lala salama.Chenge ameonyesha bayana kuwa anataka kuwa Spika ili kusafisha majina ya "waliosingiziwa kuwa mafisadi".

Lakini kubwa zaidi ni hisia zangu kuwa Chenge ana baraka kamili za uongozi wa juu wa CCM ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti Jakaya Kikwete.Si bado tunakumbuka jinsi Kikwete alivyokwenda jimboni kwa Chenge kumpigia debe na kisha akatetea uamuzi wake wa kuwapigia debe watuhumiwa wa ufisadi kwa kudai kuwa kinachowakabili ni tuhuma tu.Kama tuhuma si tatizo mbona Bashe aliondolewa kwenye mchakato wa mchujo wa kupata wagombea ubunge kwa tiketi ya CCM kwa tuhuma kuwa sio raia wa Tanzania?Kwahiyo tuhuma kwa Chenge,Mramba,nk zinapaswa kubaki tuhuma tu lakini kwa wengine tuhuma ni sawa na hukumu!

Na kwa wanaidhani Chenge anafanya utani mbaya ( a bad joke) basi labda hawaielewi CCM vizuri.Chenge anaweza kabisa kupitishwa katika mfumo wa "kidemokrasia" wa CCM.Yea,kama ameendelea kuongoza kamati ya maadili ya chama hicho na kupitishwa kugombea ubunge (na kushinda) iweje basi kuukwaa uspika liwe suala gumu?Nguvu anayo,sababu anazo,sapoti anayo na VIJISENTI anavyo.Kipi cha kumzuwia kumrithi Samuel Sitta?

Tukio la pili linahisiana na hilo la kwanza ambapo Taasisi ya Kuzuwia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekurupuka na kudai kuwa Chenge alishasafishwa katika tuhuma za ufisadi wa rada.Yaleyale ya kuisafisha Richmond japo angalau katika ishu ya Richmond serikali ya Kikwete ilikuwa na umri wa zaidi ya mwaka madarakani.Safari hii vimbwanga vimeanza hata kabla ya wiki kumalizika tangu iingie madarakani!Maumivu ya kichwa huanza polepole...

Na kwa kuthibitisha kuwa kura za kuirejesha CCM madarakani zilikuwa kura za kuubariki ufisadi,Ubalozi wa Uingereza umeishushua TAKUKURU kwa kutoa ufafanuzi kuhusu suala la ufisadi wa rada.Sijui nani ameipa TAKUKURU madaraka ya kusafisha watuhumiwa lakini hata sie tusio na uelewa mkubwa wa masuala ya sheria tunafahamu kuwa jukumu la kuhukumu ni la mahakama.Badala ya taasisi hiyo kumpeleka Chenge mahakamani ili kama kusafishwa asafishwe huku,yenyewe imekurupuka na utetezi wake wa kifisadi pasipo hoja za msingi.Hii yote ni katika kuandaa mazingira mazuri kwa Chenge kuwa Spika wa Bunge jipya.

Nitaendelea na tathmini yangu kadri siku zinavyosonga mbele.Najua kuna mengi tu ya kuyazungumzia hasa tukizingatia mazingaombwe yaliyotawala Awamu iliyopita hivyo ni suala la muda tu kabla hayajajiri mengine mengi ya kuwasuta wale wote waliotarajia miujiza kutoka kwa CCM.

1 comment:

  1. TUMEFIKIA HATUA YA KUJIULIZA HIVI KUNA WANAUME TANZANIA!? AU NAO WEZI? MAANA MAMBO TUNAYOFANYIWA NA VIONGOZI HAWA,INAKUFANYA UTOKE NA MWIKO, KIATU MCHONGOKO NA KUBAMIZA NACHO VIONGOZI MAFISADI WANAOJIGAMBA HADHARANI BILA AIBU!! JAMANI YANATOKEA NCHI NYINGINE, KALENGWA BUSH ITAKUWA FISADI ANAYESABABISHA MAISHA YAKO YAHANGAIKE KILA LEO? TUMEKUWAJE! MBONA NI UJINGA SANA? OOH NCHI YA AMANI! WELL WELL KUFA KWETU, MAHANGAIKO YA DOLA 1 KWA SIKU NDIO AMANI! THE END IS NEAR.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.