14 Jan 2011



Pichani ni Jeshi La Polisi Tanzania likiwa KAZINI.Hii ilikuwa huko Arusha ambapo WALIUA,na sasa WAMEUA TENA huko Mbeya.

Brandy Nelson, Mbeya na Ramadhan Semtawa

POLISI nchini wameendelea kutumia risasi za moto dhidi ya raia na jana wanadaiwa kuwauwa watu wawili kwa kuwapiga risasi katika vurugu zilizotokea katika wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Habari kutoka Mbarali zinasema polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za moto kuzima vurugu ambazo chanzo chake ni mabishano baina ya raia na polisi hao.

Vurugu hizo zilizotokea jana majira ya saa nane mchana zinadaiwa kusababishwa na baadhi ya wakazi wa kata ya Ubaruku kuzuia kuingia katika eneo lao lori lenye uzito wa zaidi ya tani kumi.

Baadhi ya walioshuhudia tukio hilo walisema hatua ya wananchi kuzuia kwa lori hilo inatokana na kuwepo kwa amri ya serikali wilayani Mbarali itayokataza magari yenye uzito mkubwa wa zaidi ya tani kumi kuingia katika kata ya Ubaruku.

Mmoja wa mashuhuda hao alisema lori hilo lilipokuwa likijaribu kuingie katika eneo hilo wananchi walianza kulizuia huku wakimhoji dereva wake sababu za kuvunja amri iliyopo.

“……walipokuwa wakiendelea kuhojiana na dereva, polisi walifika hapo na hapo wananchi wakaanza kuwauliza polisi sababu za kuruhusu gari kuingie katika eneo lao wakati serikali imeishakataza..,” alisema shuhuda huyo na kuongeza:

“ ni kama polisi na wananchi walishindwa kuelewana lugha hapo tukaanza kusikia mabomu ya machozi na risasi…”.

Alisema hatua ya polisi iliwafanya wananchi kutawanyika na wengine kuanza kuyavamia magari yaliyokuwa kwenye kituo cha mafuta likiwemo gari lililosababisha mvutano huo.

Katika tafrani hiyo magari mawili yaliyokuwa kwenye kituo cha mafuta yalichomwa moto. Magari hayo yanasadikiwa kuwa ni mali ya ndugu wa mwekezaji katika shamba la mpunga la Mbarali.

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Cosmas Kayombo alipohojiwa alikiri kupata taarifa hizo lakini akadai kwamba yuko mbali na tukio hilo na amedai kuwa amewasiliana na mbunge jimbo la Mbarali Dickson Kulufi afike eneo la Tukio.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi alipohojiwa alisema kuwa analifuatilia tukio na mpaka tunakwenda mitamboni tayari gari nne mbili zikiwa zimebeba askari wa kutuliza ghasia (FFU), moja ikiwa imebeba polisi waliovalia kiraia huku wakiongozwa na king`ora kikipiga kelele zikiwa zinaelekea eneo la tukio.

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.