26 Feb 2011


Yayumkinika kuhisi kuwa laiti Baba wa Taifa angefufuka leo huenda angeishia kutoa machozi.Taifa alilohangaika na wenzie kulipigania uhuru limegeuka kituko.Upande mmoja tunamwona Rais wetu akijibidiisha kusaka amani Ivory Coast ilhali wakazi wa Gongo la Mboto wanaporwa amani na usalama wao na wazembe wa Jeshi la Wababaishaji Tanzania...ooops,I meant Jeshi la Walipua mabomu...oh,not again.Nilitaka kuandika Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).Kwa upande mwingine ni ziara ya haramia wa Dowans ambaye licha ya kukimbia ukombozi wa Wazanzibari baada ya Mapinduzi amemudu kututapeli,kabla ya kuja kutuhubiria namna ya kuzalisha umeme,na kukumbushia fidia anayopaswa kulipwa kwa kututapeli!

Huku baadhi yetu tukizidi kusononeshwa na namna ombwe la uongozi linavyozidi kufidiwa kwa vitendo vya ufisadi,tunashuhudia eneo jingine ambalo lilisaidia sana kuifanya Tanzania ya Nyerere iheshimike kwa msimamo wake thabiti.Hapa nazungumzia sera za nje za nchi yetu.

Baada ya Mwalimu kung'atuka na nafasi yake kurithiwa na watu ambao kama Urais ni somo basi kwao halikuwemo kwenye silabasi (maana angalau anayepata zero anakuwa amesoma lakini hakufaulu),nchi yetu imegeuka kichekesho linapokuja suala la msimamo wetu kama taifa huru.

Na ukidhani naandika haya kama uzushi basi soma habari hii inayoeleza kuwa Tanzania imeogopa kutoa msimamo wake kuhusu uanaharamu wa dikteta Muamar Ghaddafi dhidi ya wananchi wake wanaodai mabadiliko nchini Libya.


Kwa mujibu wa habari hiyo,Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa Bernard Membe amedai kuwa


Tanzania kama nchi haiwezi kujitokeza wazi wazi kuunga mkono ama kupinga kinachotokea nchini humo kwa sababu ina raia wake wanaoishi huko hivyo kitendo chochote cha kushabikia kwa kuunga mkono ama kupinga kinahatarisha maisha yao.




Katika habari hiyo,Membe amenukuliwa akisema:
Unajua tuna raia wetu kule sasa siyo vizuri kuonyesha utashi wetu inaweza kuhatarisha maisha ya wananchi wetu kwani hii ilitokea kule Misri kwa wale waliojitokeza kuunga mkono waliweza kushambuliwa na kuharibiwa biashara zao

Ungetegemea Membe angejaribu angalau kuficha ombwe katika sera yetu ya nje kwa angalau kudanganya kama mwanadiplomasia kwamba "tunafuatilia kwa karibu matukio ya nchini Libya na tuko katika mchakato wa kuweka bayana msimamo wetu".

Yaani Membe anataka kutuzuga kwamba laiti Tanzania ikilaani unyama wa Ghaddafi dhidi ya raia wake basi kiongozi huyo wa Libya atalipa kisasi kwa kuwadhuru Watanzania 26 (kwa mujibu wa takwimu zake) waliopo nchini humo?

Kichekesho ni kwamba serikali ya CCM ambayo Membe ni miongoni mwa Waziri wake ilimudu kulaani "vurugu zilizosababishwa na Chadema huko Arusha" (ilhali waliopaswa kulaaniwa ni polisi wanaoamini katika ubabe kama wa Ghaddafi) japokuwa kuna Watanzania waliouawa na kujeruhiwa ni Watanzania pia (pamoja na raia mmoja wa Kenya).

Labda nitoe mfano bora zaidi.Hivi wakati Nyerere alipoweka wazi msimamo wake dhidi ya Makaburu wa Afrika Kusini hakukuwa na maslahi yoyote ya Tanzania katika nchi hiyo?Au,je tulipoamua kukabiliana na nduli Idi Amini hakukuwa na Mtanzania huko Uganda?

Ukweli ulio bayana ni kwamba si Membe wala bosi wake Kikwete wenye uthubutu wa kulaani unyama unaofanywa na Ghaddafi.Na si ajabu wanaombea afanikiwe kuteketeza raia wake na kubaki madarakani kisha wajipendekeze kwa kupitisha bakuli huko.

Lakini kwa upande mwingine kumlaumu Membe katika hili ni sawa na kumtaka mwanafunzi wa chekechea aandike thesis kuhusu mada ngumu kama Quantum Physics.Hivi kwa watu wanaoshindwa japo kumkemea mwarabu Adawi anayeifanya nchi yetu kama darasa la majaribio ya kudalilisha uhuru wa taifa,na badala yake wanampa fursa ya mwaliko hapo Ikulu kukutana na Makamu wa Rais (bila kusahau dokezo lake kuwa asipigwe picha),wataweza vipi kumudu mambo mazito kama uhusiano wa kimataifa?

Unapoona kiongozi wa nchi anashindwa kuwawajibisha Waziri wa Ulinzi Dkt Hussein Mwinyi,Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange,na wazembe wote waliogeuza makazi ya raia yaliyo jirani na kabi za jeshi kuwa viwanja vya mazoezi ya kulipua mabomu,basi ni wazi kumtegemea aongoze vema nchi katika masuala ya kimataifa ni sawa na kutarajia damu kutoka kwenye jiwe.

Mwinyi,Mkapa na sasa Kikwete wamefanikiwa sana kuifuta Tanzania kutoka katika nafasi yake kama taifa lenye msimamo na uongozi dhidi ya tawala dhalimu,mfano wa kupigiwa mstari ukiwa nafasi ya Tanzania katika mapambano ya ukombozi Kusini mwa Afrika.

Katika stadi za siasa tunafundishwa kwamba sera imara ya mambo ya nje inategemea sana uimara katika sera za mbalimbali za ndani ya nchi.Sasa kwa mwenendo huu ambapo Taifa letu lipo katika hatari ya kugeuzwa koloni binafsi la mafisadi ambao wanarahisishiwa azma hiyo na uongozi dhaifu wa Kikwete (anayechelea kuwaudhi maswahiba zake wanaoliingiza mkenge taifa letu),itakuwa ni njozi za mchana za mtu mwenye njaa kutegemea nchi hii irejee zama za Mwalimu ambapo tulimudu kujitengenezea heshima kubwa kutokana na misimamo thabiti na isiyoendekeza kujikomba,uoga,unafiki au ubabaishaji.

Kwa mwenendo huu,nalazimika kuafikiana na kauli za Sheikh Yahya kuwa nchi yetu inaweza kukumbwa na mabalaa makubwa huko mbeleni (japo nawalaumu waandishi wa habari walioshindwa kumhoji mnajimu huyo kuhusu utabiri wake kwamba mtu yeyote ambaye angejitokeza kugombea dhidi ya Kikwete katika uchaguzi mkuu uliopita angekufa).


1 comment:

  1. Kaka umenena! Wasi wasi wangu ni Je, hawa jamaa au wapambe wao huwa wanafuatilia maandishi haya au wenyewe wanajikita kwenye blog zile za ulimbwende na masifa? I wish makala zako zingekuwa zinaandikwa kwenye Rai na magazeti yanayosomwa kila siku tena first page, hapo ndo watu wangeelewa jinsi unavyodigest maandiko yako kabla ya kuyatoa. Udumu na tutaendelea kujifunza toka kwako.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.