10 Apr 2011




Habari zilizopatikana kutoka Dodoma kwenye kikao cha CCM chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete zinaeleza kuwa baadhi ya viongozi waadamizi wa chama hicho wamevuliwa madaraka.Kwa mujibu wa vyanzo vya mtandaoni,waliokumbwa na panga la Kikwete ni pamoja na maswahiba wake wakuu kisiasa,Edward Lowassa na Rostam Aziz.Wengine wanaotajwa kwa mujibu wa habari hizo ni "Mzee wa Vijisenti" Andrew Chenge na "mgosi" Yusuph Makamba.

Ningependa kuichambua habari hii kwa kirefu lakini nasubiri kwanza tamko rasmi la CCM.Hata hivyo,tukiamini kuwa habari hizo ni sahihi,kuna uwezekano ya yafuatayo kutokea:

Kwanza,ni muhimu kufahamu watu kama Lowassa na Rostam wametoka wapi.Hawa walikuwa vioungo muhimu kwa ushindi wa Kikwete mwaka 2005.Wanaowajua vema wanawa-describe kwa mlolongo huu:Lowassa-mwanasiasa haswa (simaanishi kuwa ni mwanasiasa mwadilifu),Rostam-bwana fedha,na Kikwete-mtawala.Wajuzi wa siasa chafu wanaeleza kuwa ushirikiano huo wa watu hawa watatu ulitumia kila aina ya mbinu kuhakikisha Kikwete anaingia Ikulu hapo 2005.Na ikawa hivyo,baada ya viongozi hao wakuu wa "Mtandao" kufanikiwa kupenya takriban kila kundi la jamii;kutoka viongozi wa dini hadi wakuu wa taasisi za dola,kutoka wanahabari hadi wasanii.

Pasipo kuuma maneno,ushirika huu usio mtakatika wa Lowassa,Rostam na Kikwete ni mithili ya joka lenye vichwa vitatu.Sasa iwapo ni kweli kuwa Kikwete kaamua kubaki kichwa pekee kwenye joka hilo basi yayumkinika kubashiri kuwa uhai wa joka hilo nao uko matatani.

Pili,kwa kufuata mlolongo wa nilichoandika hapo juu,inaelezwa kuwa Lowassa ndiye aliyefanya kazi kubwa zaidi ya kutengeneza serikali ya Kikwete.Ikumbukwe kuwa japo wote wawili walishashika nyadhifa mbalimbali serikali kabla ya 2005,Lowassa alikuwa amejijenga zaidi kiuchumi na kisiasa ukilinganisha na Kikwete.Kadhalika-na hapa nafafanua kwanini niliandika hapo juu kuwa Lowassa ni mwanasiasa haswa(japo simaanishi ni mwanasiasa mwadilifu)-ni ukweli kuwa mwanasiasa huyo ana ushawishi wa kisiasa zaidi ya Kikwete.Japo wote wawili ni wapenda umaarufu (populists),wakati Kikwete amekuwa akitumia zaidi turufu ya "tabasamu la muda wote" na "kuwa karibu na watu",Lowassa amekwenda mbali zaidi na kujifanya anayafahamu matatizo ya wananchi na kuyatolea ufumbuzi mapema (ndio maana licha ya kulazimika kujiuzulu kutokana na ufisadi wa Richmond bado kuna wanaomwona kama mwajibikaji).Kwa kifupi,Lowassa ni mwepesi wa kuchukua maamuzi (hususan yale yatayopelekea yeye kuonekana kama "Sokoine flani hivi"),Kikwete ni mzito wa maamuzi (huku walio karibu naye wakidai tatizo sio uzito wa maamuzi bali hajui vipaumbele vyake).

Inaaminika kuwa Lowassa ana ufuasi mkubwa ndani ya CCM na serikalini kwa ujumla.Kwa mujibu wa wajuzi wa mambo,faida aliyonayo Lowassa ndani ya chama hicho ni uwezo wa kifedha,ambapo inaelezwa kwamba amewasaidia viongozi mbalimbali wa CCM kiuchumi na kuwawezesha kuwepo walipo leo.Kadhalika,akiutumia vema urafiki wake na Kikwete, na nafasi yake kama Waziri Mkuu kabla ya skandali ya Richmond,aliweza kutengeneza "mtandao ndani ya mtandao",kwa maana ya kuwaweka madarakani watu wenye utiifu kwake zaidi kuliko CCM au Kikwete.Inaelezwa wateuliwa wengi kwenye nafasi za kiserikali na kichama ngazi za mikoa na wilaya ni wafuasi wa Lowassa,kwa mfano ma-RC na ma-DC,na wenyeviti na makatibu wa CCM mikoani na wilayani.

Swali la muhimu ni je,kuondoka kwa Lowassa katika wadhifa mmoja kutazuwia nguvu na ushawishi wake kwa wafuasi wake,wengi wao wakiwa ni watu walio madarakani kutokana na fadhila za mwanasiasa huyo?

La tatu ni ukweli kuwa Lowassa anataka urais hapo 2015.Na hilo halikuanza jana au juzi bali wajuzi wa mambo wanaeleza kuwa kulikuwa na makubaliano rasmi kati ya Kikwete na Lowassa kuwa wangepokezana uongozi maara baada ya Kikwete kumaliza miaka yake 10.Japo suala la Richmond lilizua mfarakano wa aina flani kati ya wawili hao lakini ukweli unabaki kuwa "heshima" aliyotoa Kikwete kwa Lowassa kwa kutomtimua bali kusubiri ajiuzulu mwenyewe iliwaacha wawili hao wakiendelea na urafiki wao japo si kama ilivyokuwa mwanzoni.

Haifahamiki kama Kikwete bado anaheshimu "makubaliano" yake na Lowassa kuhusu "kupokezana kijiti cha urais hapo 2015" lakini hiyo haimzuwii Lowassa kuamini kuwa "piga au" lazima achukue nafasi hiyo.Of course,kuna majina kama Bernard Membe (mtu anayetajwa kuuweka uhusiano na Lowassa katika wakati mgumu kwa vile yeye na Lowassa "picha hazipandi" ilhali yeye na Kikwete ni "damu damu",na Kikwete na Lowassa ndio hivyo tena "hawakufahamiana mtaani" kama ilivyowahi kutamkwa hadharani ) lakini turufu ya Lowassa haitegemei sana baraka za Kikwete bali ushawishi na nguvu yake ndani ya CCM,sambamba na uwezo wake mkubwa wa kifedha (alizitoa wapi....waulize TAKUKURU).Na ana faida nyingine kubwa ambayo ni uswahiba wake na Rostam,mfanyabiashara mwenye asili ya kiasia anayetajwa kuwa na nguvu zaidi ya Kikwete-kutokana na utajiri wake unaoweza kumfanya kuwa mtu tajiri kuliko wote Tanzania.Kadhalika,inaelezwa kuwa Rostam ni mjuzi wa mbinu chafu hususan kwa kutumia fedha zake na "njaa" za wanaohitaji chochote kutoka kwake.

Jingine,ambalo linaweza kuwa si la msingi sana japo lina umuhimu wa aina flani ni ukweli kwamba Lowassa na Rostam wana siri muhimu kumhusu Kikwete na urais wake kwa ujumla.Njia pekee kuwadhibiti wawili hao kwa kutumia Idara ya Usalama wa Taifa.Katika siasa zetu za "ovyo ovyo" ni rahisi tu kwa rais kuiamuru taasisi hiyo imfanyie kazi zake binafsi badala ya zile za kikatiba.Hilo linawezekana zaidi kutokana na nafasi ya Rais kama consumer wa taarifa zote za kishushushu.

Nisingependa kutabiri matokeo kabla ya taarifa kamili ya CCM lakini tukiamini habari zilizopo na ikathibitika kuwa ni kweli basi nachobashiri ni mwanzo wa mwisho wa chama hicho tawala.Naomba unielewe vizuri: tatizo la msingi sio kutimuliwa kwa Lowassa na Rostam bali ukweli kuwa USHIRIKA WA WACHAWI HAUDUMU.Sambamba na hilo ni ukweli mwingine kuwa JOKA LENYE VICHWA VITATU HALIWEZI KUWA HAI MUDA MREFU PINDI VICHWA VIWILI VIKIKATWA.

Lakini la muhimu kuliko yote ni manufaa kwa Watanzania kutokana na mabadiliko hayo ndani ya CCM.Kwa kifupi,ukiacha vichwa vikubwa vya habari kwenye magazeti yetu,mabadiliko hayo hayana manufaa yoyote kwa masikini wasio na hakika ya mlo wao wa kesho,wanafunzi wanaokaa sakafuni kwa uhaba wa madawati,akina mama wanaoletewa bajaj za kuwawahisha hospitali wakiwa wajawazito japo wabunge wanapewa mashangingi ya uheshimiwa,nk nk nk.Wa kuondoka na CCM kama chama kilichopo madarakani.Wanapoondoana ndani kwa ndani haimsaidii Mtanzania wa kawaida.

1 comment:

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.