Tuhuma za kuuawa kwa Mwakyembe na wenzake kwa IGP na Mwandishi wetu FEBRUARI 8, mwaka huu, Dk. Mwakyembe alizungumza na baadhi ya viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam. 

Baada ya maelezo hayo, polisi walimtaka aweke madai yake kwenye maandishi na siku moja baadaye Dk. Mwakyembe aliwasilisha taarifa yake ya maandishi. 

Dk. Mwakyembe amesema kwenye barua hiyo, “Pamoja na kwamba taarifa hii ni mpya yenye matukio ya takriban mwezi moja tu, naamini kwa dhati kuwa msingi wake (kwa maana ya wahusika na maudhui) hautofautiani na ule wa matukio mengine ya awali ambayo baadhi yake yalisharipotiwa polisi na vyombo vingine vya usalama kwa lengo la kuchunguzwa. 

Maelezo ya Barua ya Mwakyembe “Bado nina imani kubwa na Jeshi letu la Polisi kwamba litaifanyia kazi taarifa hii bila kujali nguvu ya ukwasi na ya kisiasa ya watuhumiwa na kwa kuzingatia misingi ya haki na ukweli. 

“Msingi wa mimi kushtuka na kuamua kulivalia njuga suala hili kwa kuwataarifu watu mbalimbali wenye uelewa na kuvitaarifu vyombo vya dola, ni taarifa nilizozipata kutoka Songea Januari 22, 2011 kuhusu kundi la watu saba lililoingia mjini humo usiku wa Januari 21, 2011 kwa gari iliyodaiwa kuwa ya wizara yangu (Ujenzi) aina ya Land Cruiser yenye usajili nambari STK 68… (ambayo kipindi fulani katika safari hiyo ilibadilishwa namba yake kuwa STK 68…). 

Gari hiyo iliwateremsha “abiria” hao saba sehemu iitwayo Madaba na baadaye kuchukuliwa na gari nyingine (Hardtop Land Cruiser yenye namba za usajili T7…BDU) hadi Top Inn ya mjini Songea. “Majina ya baadhi ya watu hao saba ni Wasomali wawili Hafidh na Faraj; kijana wa Kichagga kwa jina Mustafa a.k.a “Master”; Mkusa, jamaa ambaye wenzake wanaamini kuwa yuko Usalama wa Taifa; na mtu mwingine (jina tunalo) kutoka Tanga anayedaiwa kuwa na utaalamu mkubwa wa kukaba watu. 

“Mwenyeji aliyewapokea Songea watu hao saba ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya (kaitaja) akiongozana na mtu aitwaye Manya. Kilichowafanya baadhi ya watu waanze kulidadisi kundi hili ni dhamira ya safari yao. Tetesi zilisema walikuwa wanaelekea Mbunde kwa mganga maarufu wa kienyeji kwa jina (linahifadhiwa). Hivyo, udadisi ukaongezeka kujua nani anakwenda “kulogwa” safari hii. 

Tetesi zikarejea na jina langu na msululu wa majina mengine: Dk. Slaa (Willibrod), Anne Kilango - Malecela, Reginald Mengi, Profesa Mwandosya na Benard Membe. “Pamoja na kwamba sina imani na ushirikina au nguvu za giza, kutajwa kwa jina langu na fursa ya pekee niliyokuwa nayo ya kujua kilichokuwa kinafanyika, kukanipa ari, nguvu na shauku ya aina yake kutaka kulielewa zaidi suala hili ili ikibidi, niwataarifu wenzangu nao waelewe. 

“Usiku wa Jumamosi Januari 22, 2011 kundi hilo lilielekea Mbunde, wilayani Namtumbo, (kwa gari aina ya Defender STK 26…, likiendeshwa na (jina tunalo) kukutana na ‘mganga’ …ambaye anaishi ndani ya Selous Game Reserve With Impunity. Defender hiyo iligeuza kurejea Songea siku mbili baadaye na kuwaacha ‘wageni’ hao kwa mganga ambako walikaa siku saba ‘wakitengenezwa’. Walirejea Songea Januari 29, 2011 na kesho yake Januari 30, 2011 wakaanza safari ya kurejea Dar es Salaam. 

“Kutoka Songea hadi Mafinga walitumia ile Hard Top iliyowatoa Madaba hadi Top Inn ya Songea (T7… BDU). Walifika Mafinga milango ya saa mbili usiku na kukuta gari mbili zikiwasubiri: Hilux Mayai ya (kampuni moja) na Defender iliyowaongoza hadi Morogoro. Walipokewa Morogoro na askari (jina tunalo). 

Hapo kundi likagawanyika: watu wanne wakiwemo wale Wasomali wawili wakaingia kwenye Nissan Patrol (T8… ADH) mali ya (kampuni jina tunalo) na wengine wakabaki Morogoro. “Kufuatana na ‘mganga’ mwenyewe, ambaye wapelelezi wako wanaweza kuongea naye kama walivyofanya walionipa taarifa hizi, aliwapa masharti ya kutotumia silaha za moto ila njia nyingine kumuua kwanza Mwakyembe, baadaye Slaa, n.k., n.k, n.k. kwa zamu; alitengeneza dawa ya kuwapooza wale wengine (wanaosubiri) kwenye orodha ya kuuawa (Dk. Slaa, Anne Kilango, Mengi, Mwandosya na Membe) wasitaharuki na kupiga kelele za nguvu hata kuamsha hasira za wananchi mauaji yakitokea; aliwazindika vilivyo wasiweze kudhuriwa na tendo la kuua na alitengeneza dawa ya kuwapumbaza “waliohukumiwa kifo” (wawe mfano wa mbwa mbele ya chatu). 

“Jijini Dar es Salaam ‘wahitimu’ hao walifikia Kiwalani karibu na kiwanda cha Mohamed Enterprises. Jirani na kiwanda hicho kuna jengo la ghorofa: Februari 5, 2011, wageni wawili zaidi waliwasili kwa ndege kutoka Uganda; mwanaume mmoja (aliyechanganya rangi) na mwanamke mmoja (mweusi vilivyo). Walipokewa na gari mbili: moja ya polisi (PT 02…) na ya pili yenye namba za kibalozi (aina ya RAV 4). 

Ushiriki wa Al Shabaab “Jioni wakawa na mazungumzo ya kina na Wasomali wawili niliowaelezea awali ambao inadaiwa ni wapiganaji wa Harakat al-Shabaab al- Mujahideen (kwa kifupi Al- Shabaab). “Niliweza kupata picha pana zaidi kwa nini wapiganaji wa kikundi hicho (kinachopambana na wanaodhaniwa kuwa maadui wa Uislamu) wameingizwa nchini. 

Nimeweza kukusanya taarifa zinazodai kuwa awali walifikiriwa kuletwa wapiganaji kutoka Rwanda, lakini wazo hili lilikataliwa na wafadhili wa mpango huu ambao walitaka ‘wanaharakati’ wa aina hiyo watoke Somalia. Ndipo kikundi hicho kikashawishiwa kwamba Tanzania kuna tatizo la udini la Uislamu kutishiwa. 

Mimi na wenzangu hao watano tumejengewa hoja kuwa maadui wa Uislamu tunaotumiwa na makanisa, hivyo hatuna budi kukatishwa maisha yetu. “Niliweza vilevile kupata picha kuwa wafadhili wa kundi hili, wana mahusiano ya karibu na Sheikh …(jina tunalo) ambaye baadhi ya utabiri wake unatokana na agenda za wafadhili hao. 

Inadaiwa kuwa utabiri wa sheikh … mwaka jana ulimlenga Dk. Slaa ambaye alidaiwa kubebwa na makanisa. “Utabiri” huo haukutimia kwa kuogopa kuiingiza nchi kwenye machafuko makubwa ya kisiasa/kidini ambayo yangewaweka pabaya hata wafadhili wa mpango huo. “Inadaiwa kuwa Sheikh … ameombwa tena kutoa utabiri wa mwanasiasa na kiongozi mmoja kupoteza maisha mwezi huu (Fabruari). 

Inadaiwa kuwa mwanasiasa huyo anayetembea na kifo ni mimi na tayari maandalizi ya ‘hukumu yangu’ yamefanywa: “(a) Kijana mmoja kwa jina la Hassan alitumwa kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma siku ya Jumamosi Februari 5, 2011 kwa “maandalizi” hayo (mahali pa kufikia kikosi hicho cha mauaji, utambuzi wa nyumba ya kuishi niliyopangiwa na kumtafuta mhudumu mmoja wa Bunge ili ile ‘portion’ ya mganga ya kunipumbaza kabla ya hukumu, iweze kunyunyizwa kwenye kiti changu Bungeni); “(b) Kesho yake (Jumapili) Februari 6, mnamo saa nne usiku, kikosi hicho cha mauaji kikiwa na watu watano kiliondoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kwa gari aina ya Land Cruiser nyeupe ya mkongo (T3… AKU) na kimejichimbia Dodoma mpaka leo (Februari 9). 

“Waliomo kwenye kikosi hicho ni Wasomali wale wawili, mgeni moja (wa kiume) kutoka Uganda, Mustafa a.k.a “Master” na kijana mmoja ambaye Januari 19, 2011 aliwabeba Wasomali hao kutoka Morogoro hadi Ununio kupitia Kibaha na Baobab kwa gari aina ya VX Land Cruiser (T6…APF). Kijana huyo ana shepu ya Kitutsi na anaongea Kifaransa. 

“Utabiri atakaoufanya Sheikh … (pengine aamue kuachana nao sasa baada ya kubaini kuwa tunaujua) utakuwa na lengo la kuwapumbaza wananchi waelekeze macho na masikio yao zaidi kwenye utabiri wake kuliko kwenye njama za kundi hilo za muda mrefu za mauaji. “Kila siku ya Mungu napata taarifa za ziada kutoka kwa raia wema kuhusu suala hili. 

Naziingiza kwenye taarifa hii ili ziwasaidie katika upelelezi: “Inadaiwa kuwa Wasomali hao waliingia nchini kutokea Kenya na wakaja kwa barabara hadi Dodoma. Walitumia gari aina ya RAV4 (new model – T8… AQS) Januari 8, 2011 na kusafirishwa hadi Morogoro ambako walipokewa na askari niliyemtaja awali… wa polisi Morogoro. “Mjini Morogoro, walikaa hoteli mbili tofauti: Hilux Hotel Morogoro na Top Life. 

Aliyewafanyia Wasomali hao booking hapo Top Life ni mmiliki wa hoteli ya….(jina la hoteli na mmiliki tunalo). “Magari waliyotumia wakiwa Morogoro ni RAV4 T8… AQS, VX Land Cruiser STK 1…, Mercedes Benz (Station Wagon) T8… BDT, Toyota Mark II GX100 nyeupe T2… BKR na wakiwa Dar es Salaam wametumia magari VX Land Cruiser T6… APF, Nissan Patrol T8… ADH.” 

“Naomba nihitimishe maelezo haya kuwa nimekuwa muwazi kwa asimilia 100 na hata vyanzo vyangu vya habari ni miongoni mwa watu hao niliowataja katika taarifa hii ambao naamini utachukua hatua ya kuwahoji kulipatia ufumbuzi suala hili. 

“Suala la msingi hapa, si uhai wangu, kwani iko siku lazima nitakufa kama ambavyo hao mafisadi wanaodhani wanaweza kufadhili vifo vya wenzao watakavyokufa hata wao hatimaye, watake wasitake, hakika ni suala la muda tu. Suala la msingi hapa ni mustakabali wa taifa letu, taifa aliloliasisi Mwalimu Nyerere na kulilea kwa misingi ya usawa, haki, umoja, amani na utulivu. 

“Nimejieleza awali kuwa nina imani kubwa na Jeshi letu la Polisi kwamba litaifanyia kazi taarifa hii bila kujali nguvu ya ukwasi na ya kisiasa ya watuhumiwa na kwa kuzingatia misingi ya haki na ukweli. 

“Hata hivyo nalazimika kusema nitasikitika sana ikiwa taswira ya ‘ukorofi’ niliyopewa kwenye kesi moja ya awali (2009) itapewa nafasi kwenye suala hili, hivyo kuninyima fursa ya kusikilizwa vizuri na ulinzi ninaostahili kama raia Kikatiba na kisheria. Niko tayari wakati wowote na mahali popote kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi litakaponihitaji.”