29 May 2013


Tarehe kama hii, miaka mitano uliyopita,mama mpendwa Adelina Mapango, uliagana nasi. Nikisema 'uliagana nasi' inaweza kutafsiriwa kana kwamba ulipata nafasi ya kutuaga.Nilikuja huko nyumbani kukuuguza Februari 2008, lakini tangu nilipokuona pale Muhimbili hadi tarehe 29 Mei 2008 hukuwahi japo kuniambia neno moja la mwisho.Nakumbuka ulivyokuwa ukiniangalia kwa upendo wako mkubwa,nakumbuka pia tabasamu lako licha ya maumivu makubwa uliyokuwa nayo.Lakini kila nilipojaribu angalau kusikia neno lako moja tu,haikuwezekana hadi siku unafariki.

Mama mpendwa, kabla ya kifo chako sikuwahi kuelewa maana ya kufiwa na mzazi au mtu wa karibu.Sasa sio tu naelewa bali kila siku ya Mungu tangu siku ulipotutoka imekuwa kama ndoto mbaya ambayo natamani iishe ili hali irejee kuwa kama zamani.Kwa bahati mbaya, ndoto hiyo mbaya ni ukweli (hali halisi), na hadi sasa matarajio kuwa kuna siku nitaamka na kukuona au kukusikia ukiwa hai yanazidi kufifia.Kwa kifupi,mama mpendwa,hadi leo bado napata shida kuamini na kukubali kuwa haupo nasi.

Nyakati mbili ngumu zaidi kwangu ni wakati ninapofanya sala kabla ya kulala ambapo wakati wa uhai wako nilikuwa nikisali "Ee Bwana uijalie familia yangu yani Baba na Mama..." lakini sasa inabidi nimtaje Baba pekee.Pia wakati wa uhai wako,nilijenga utaratibu kwamba nikipiga simu naanza kuongea na Baba kisha anapitisha simu kwako tunaanza kutia stori mbalimbali.Sasa,mama,nikimaliza kuongea na Baba huwa najikuta nasahau kuwa haupo hapo nyumbani,na kumwambia Baba akupe simu...then nakumbuka haupo.Naishia kutoa machozi.

Nikiwa mbinafsi,nitaangalia tu jinsi ninavyopata shida kukabiliana na ukweli kuwa hauko nasi.Lakini kuna rafiki yako kipenzi Baba Mzee Chahali ambaye yeye amekuwa mtu tofauti kabisa tangu ulipoondoka.Kama unavyokumbuka,baba ni mtu mkimya,mwenye marafiki wachache, na rafiki yake mkuu ulikuwa wewe.Sasa tangu uondoke,baba amekuwa mnyonge kupita kiasi.Kibaya zaid, ameendelea kudai labda yeye ndio angestahili kutangulia mbele ya haki kwa vile alikuwa amekuzidi kiumri.Kwa hakika, baba ameendelea kuwa katika wakati mgumu sana licha ya sapoti kubwa tunayompatia.

Lakini pia kuna rafiki zako wapenda Kulwa na Doto (Peter na Paul). Pengine kwa vile wao ni last borns, walikuwa wakikuchukulia zaidi ya mzazi, ulikuwa kama bibi yao, shangazi yao, na kikubwa zaidi, rafiki yao.Kila ninapoongea na wadogo zangu hawa najiskia kutokwa na machozi.Kimsingi, sidhani kama waliwahi kuwaza kuwa na maisha bila ya uwepo wako mama.

Familia yote kwa ujumla inakukumbuka sana mama.Nina mkanda wa video niliowarekodi wewe na baba mlipokuwa mnaadhimisha miaka 50 ya ndoa yenu mwaka 2005,lakini kila nikijaribu kuuangalia najikuta nabubujikwa na machozi.Katika mkanda huo uliongea mambo mengi ya msingi kuhusu maisha.Kuna nyakati nataka kuuangalia ili nirejee wosia wako lakini nashindwa kwa sababu ya uchungu.

Mama nilikupenda sana,ninakupenda sana,na nitaendelea kukupenda milele.Kwangu, japo hupo nasi kimwili,lakini unaendelea kuishi nasi kiroho.Nitazidi kukukumbuka kwa sala kila siku,na ninaamini huko uliko unapata faraja kila ninapotenda mambo kwa kuzingatia mafundisho yako.

WE MISS YOU SO MUCH MAMA MPENDWA

PUMZIKO LA MILELE AKUPE EE BWANA NA MWANGA WA MILELE AKUANGAZIE UPUMZIKE KWA AMANI AMINA

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.