9 May 2013


HUU ni mwendelezo wa makala ya iliyopita iliyojaribu kujadili mwelekeo wa mageuzi ya kisiasa huko nyumbani tangu yaruhusiwe takriban miaka 20 iliyopita.
Pamoja na mambo mengine, katika makala hiyo nilibainisha waziwazi kuwapo kwa wanasiasa watatu waandamizi wa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), ambao binafsi ninawaona kama kikwazo kwa ufanisi wa mageuzi hayo, sambamba na kuwa hatari kwa ustawi wa Taifa.
Niliwataja wanasiasa hao kuwa ni Stephen Wassira, Nape Nnauye na Mwigulu Nchemba. Kwa bahati nzuri, kati ya nilipoandika makala hiyo na sasa kumejitokeza majina mengine ya viongozi wa CCM wenye mtizamo na vitendo kama wa hao watatu, na hilo linalazimisha kupanua zaidi wigo wa mjadala huu.
Lakini kabla sijarukia majina hayo mapya ni vema nikiendeleza pale nilipoishia katika makala iliyopita, ambapo baada ya kuwajadili Wassira na Nape, inabidi kumwangalia Mwigulu Nchemba.
Ninapata shida kumwelewa mwanasiasa huyu. Wasifu wake unaonyesha kuwa ni mtu aliyeelimika lakini matendo yake yanakinzana kabisa na uelewa wa mtu wa kiwango cha aina yake ya elimu.
Kati ya vitendo vingi vinavyokera kama ni kweli amefanya yeye, ni kumvisha mbwa bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwenye mkutano wa hadhara. Sijui lengo lilikuwa kuwafananisha CHADEMA na mbwa au ni mwendelezo tu wa siasa mufilisi za wanasiasa wetu? Lililo wazi ni kuwa mtu mwenye uelewa tu wa kawaida hawezi kufanya kitendo cha aina hiyo.
Lakini pengine tukio litakalobaki vichwani mwa Watanzania wengi kuhusu Mwigulu na siasa zake za chuki (hususan dhidi ya CHADEMA) ni hili la ‘tuhuma za ugaidi dhidi ya Wilfred Lwakatare.’
Nisingependa kujadili kwa undani suala hili kwa vile tayari lipo mahakamani (japo majuzi baadhi ya wabunge wameamua kupuuza busara hiyo – hatuwezi kuwalaumu sana kwani yayumkinika kuhitimisha kuwa kuna uhaba mkubwa wa busara miongoni mwa wabunge wetu).
Kwa kufuatilia mtiririko wa suala la Lwakatare, ni rahisi kuhitimisha uhusika wa Mwigulu katika aidha kutengeneza mkakati fyongo wa kujenga picha kuwa CHADEMA ni chama cha kigaidi au kutumia mkakati huo kupigia mstari ajenda hiyo ya ugaidi.
Kwamba Mwigulu ameshaashiria mara kadhaa kuwa na uelewa wa uwepo wa ‘video ya Lwakatare’ hata kabla haijawekwa mtandaoni si jambo la kujadili tena. Labda tunachopaswa kujiuliza ni kama uhusika wa Mwigulu katika mkakati huo ni ajenda yake binafsi ya chuki dhidi ya CHADEMA au ni ajenda ya CCM.
Majuzi, uongozi wa CHADEMA ulitoa tamko linaloonyesha ‘mtandao’ mpana wa wahusika wa mkakati huo, ambapo licha ya Mwigulu, CHADEMA iliwataja watu wengine kadhaa wakiwemo watumishi waandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Kimsingi, hata kama CHADEMA wasingemtaja Mwigulu, au hata kama mwenyewe asingebainisha huko nyuma kuwa ana mkanda wa video unaothibitisha ‘mipango ya ugaidi’ ya CHADEMA, mtu yeyote anayefuatilia siasa za Tanzania kwa karibu, au anayemfahamu vyema mwanasiasa huyo, asingeshindwa kuhisi kuwa anahusika kwa namna moja au nyingine.
Ni rahisi kuhitimisha kuwa ajenda kuu kichwani mwa Mwigulu ni kuiangamiza CHADEMA kwa namna mbaya kabisa. Chuki za mwanasiasa huyo kwa CHADEMA ni kubwa zaidi ya waliyokuwa nayo Watanzania dhidi ya mkoloni, kaburu au nduli Idi Amin.
Lakini wakati ninamshutumu Mwigulu ni vema kujiuliza, “Je uongozi wa juu wa CCM, ikiwa ni pamoja na Rais Kikwete, wana mtizamo tofauti na wa Mwigulu?” Au “je Mwigulu anatumia tu vibaya nafasi yake ndani ya chama hicho au anatekeleza tu matakwa na maelekezo ya chama hicho tawala?”
Ni vigumu kuamini kuwa Mwigulu haungwi mkono na viongozi wenziwe wa CCM (ukiweka kando Wassira na Nape) kwa sababu laiti ingekuwa hivyo basi angeshakemewa au ‘kuwekwa sawa.’
Vyovyote ilivyo, hatua iliyofikiwa na Mwigulu na wenzie kutengeneza mazingira ya uhalifu (criminalisation) dhidi ya CHADEMA yaweza kuwa na madhara yasiyokusudiwa. Nimeandika mara kadhaa kuwa kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa kwa CHADEMA kunatokana na udhaifu, ubabaishaji, uzembe, ufisadi, nk ndani ya CCM.
Kinachokiweka CHADEMA karibu na Watanzania wengi hivi sasa ni mafanikio ya chama hicho kuwaonyesha bayana wananchi jinsi CCM ilivyoifikisha nchi hapa tulipo, kwa kuibua ufisadi unaowahusisha baadhi ya viongozi wa CCM na kupigania marekebisho ya kimfumo (kwa mfano marekebisho ya Katiba) yatakayoleta uongozi wa hali na wa uadilifu.
Kwa kukihujumu CHADEMA, Mwigulu na wenziwe wanaweza kuwa wanawahujumu Watanzania, kwa sababu wakati CCM kimekuwa kikiwashawishi Watanzania kuwa CHADEMA hakifai, wenzao wa CHADEMA nao wamekuwa wakiwaamsha Watanzania kuhusu hali ilivyo sasa na hatma ya nchi yao, na nini kinapaswa kufanyika kuifikisha Tanzania yetu mahali inapostahili.
Ninatafsiri mkakati wa kufanya CHADEMA kionekane chama cha kigaidi umelenga kujenga hoja mbadala dhidi ya ile ya CHADEMA kuwa CCM ni chama cha mafisadi. Kwamba CHADEMA wakisema “CCM ni mafisadi” CCM nao watakuwa na cha kusema, kuwa “CHADEMA ni chama cha kigaidi.” Ikumbukwe, kabla ya ‘mkakati huu wa ugaidi’ CCM ilijaribu bila mafanikio kujenga picha kuwa CHADEMA ni chama cha kifamilia, baadaye kikabila, na hatimaye cha kidini. Mkakati huo wa kuifanya CHADEMA ionekane chama cha kidini umechangia sana kutufikisha katika vuguvugu la udini linaloendelea huko nyumbani. 
Nitahitimisha makala hii katika toleo lijalo kwa kuhusisha hatari ya vitendo vya Wassira, Nape na Mwigulu na uhuni unaoendelea huko bungeni, sambamba na kujadili kwa kifupi ‘nyongeza katika orodha ya wanasiasa hatari’ (yaani zaidi ya hao watatu, na kuwatupia macho Spika Anne Makinda, Naibu wake Job Ndugai na mbunge Peter Serukamba ambaye ameweka historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kutumia ‘the F-word’ katika Bunge tukufu la Jamhuri ya Muungano).
Kwa kifupi, kilichojiri bungeni hivi karibuni ni mwendelezo tu wa yale yanayofanywa na akina Wassira, Nape na Mwigulu kwenye harakati zao za kila siku za kuendeleza siasa za chuki. Wanapuliza sumu nje ya bunge lakini upepo umefanikiwa kurejesha sumu hiyo ndani ya bunge, na kwa hakika hatma ya taasisi hiyo tukufu-na nchi yetu kwa ujumla si njema.
Itaendelea.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.