21 Jul 2015




Juzi nilipatiwa uthibitisho wa kitu nilichokwishaambiwa awali: Idara yetu ya Usalama wa Taifa iliandaa operesheni dhidi ya mtu aliyepaswa kuja Tanzania kumzika baba yake. 

Nilipata taarifa kuhusu kinachoendelea katika Idara hiyo masaa kadhaa baada ya kutangaza kuwa baba yangu, Mzee Chahali amefariki. Afisa mmoja wa Idara hiyo alinipa ushauri kuwa nisije huko nyumbani kwa sababu kuna hujuma dhidi yangu. Kuthibitisha kuwa taasisi hiyo ni ya kibabaishaji, nilipata taarifa hizo muda mfupi tu baada ya maandalizi ya operesheni hiyo, and guess what, mie nipo Uingereza. Sasa kama mie nisiye na hatia yoyote na masikini nisiye na fedha za kuhonga, jiulize, ni wauza unga wangapi wenye mamilioni ya kuhonga  wanaopewa taarifa huko nyumbani kutoka katika Idara hiyo na taasisi nyingine za dola.

Sijawahi kuficha kuwa nilikuwa mtumishi wa taasisi hiyo. Nilikuwa mtumishi mwaminifu kwa takriban miaka 15 hadi mwaka 2008 nilipoamua kuachana nayo. Sijawahi kutamka nini kilichonifanya kuchukua uamuzi huo, lakini kwa kifupi maisha yangu yalikuwa hatarini baada ya kuzushiwa kosa ambalo ni sawa na uhaini. Kwa kifupi, ukiwa mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi yeyote ile, kosa la 'kutumikia Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi nyingine' ni kile kwa kimombo kinaitwa 'treasonable offence,' yaani kosa la kihaini. Kwanini nilizushiwa hilo, hiyo ni hadithi nyingine, ila sijawahi kuitumikia taasisi nyingine ya Usalama wa Taifa  zaidi ya hiyo ya nchi yangu.

Mwaka 2002, Idara hiyo ilinipatia skolashipu ya kuja kusoma shahada ya uzamili (Masters) huku Uingereza. Baada ya kumaliza shahada hiyo, niliomba ruhusa ya kusoma shahada ya uzamifu (PhD). Lakini kwa vile shahada ya uzamili niliyosoma haikuwa ya kiutafiti (research-based), ilinilazimu kusoma shahada nyingine ya uzamili (MRes) ambayo ni ya kiutafiti, na nilipomaliza nilijiunga na shahada ya uzamifu. Hayo yote yalifanyika kwa ruhusa ya taasisi hiyo.

Matatizo yangu na Idara hiyo yalianza Oktoba mwaka 2006, baada ya mie kuchapisha makala iliyokuwa ikimkemea aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa, kuhusu taarifa za vyombo vya habari vya huko nyumbani kuwa alikuwa akijaribu kuzima mjadala wa skandali ya Richmond. Mmoja wa Wakurugenzi katika Idara hiyo alinipigia simu ya vitisho akinituhumu kuwa 'ninawasidia wapinzani,' 'ninaikosoa serikali ilhali mie ni mtumishi wake (kwa wakati huo),' na kubwa zaidi, kuhoji iwapo ninaitumikia Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi nyinyingine. Kadhalika, press secretary wa Lowassa alisambaza makala kali kunikemea

Walinileta huku kusoma stadi za siasa, sasa mie kupevuka kifikra kuhusu vikwazo vya siasa yetu katika maendeleo ya taifa letu ikawa kosa. Uzalendo ulinishinda, ndio maana ikanilazimu kukosoa maovu mbalimbali yaliyokuwa yanawaumiza walalahoi wa Tanzania. Kichekesho ni kwamba kile nilichoandika 2006 na kushambuliwa vikali, ndicho kilichotokea miaka miwili baadaye, na kulazimisha Lowassa kujiuzulu. Na hakuna aliyenipongeza.

Mwaka 2008 nilikuja huko nyumbani kwa miezi kadhaa kumuuguza marehemu mama yangu. Nikidhani kuwa watumishi wenzangu katika Idara hiyo walikuwa wakielewa kilichokuwa kikinisibu wakati huo, wakanisumbua vya kutosha, na hatimaye njia pekee niliyobakiwa nao ilikuwa kuondoka huko nyumbani - japo baba alikuwa taabani kutokana na kifo cha mkewe aliyedumu nae kwenye ndoa kwa miaka 53. Na niliporudi huku, usumbufu ukaendelea: vitisho na upuuzi mwingine. Kwa ushauri wa taasisi za hapa, na kwa kuzingatia kuwa maisha yangu yalikuwa hatarini, nikaamua kuachana na taasisi hiyo. So ukiangalia hadi hapo, sikuwa nimefanya kosa lolote la kustahili kusumbuliwa kiasi hiki.

Kuhusu tukio la majuzi, masaa kadhaa baada ya kutangaza kuwa baba yangu amefariki, nililetewa taarifa ya uwepo wa operesheni maalum dhidi yangu, na aliyenipa taarifa hiyo alinisihi nisije huko nyumbani. Nimeambiwa kuwa Idara hiyo iliweka maofisa wake airport ili 'kunipokea.' Lakini baada ya kutoniona, walituma maafisa watatu, wawili wanaume na mmoja mwanamke, kwenda Ifakara 'kushirikiana nasi kwenye mazishi.' Wahuni hawa hata hawana ubinadamu.

Sijui wametumia kiasi gani cha fedha za walipakodi kukesha macho airport kunisubiri, na sijui hadi sasa washatumia kiasi gani huko Ifakara kuendeleza operesheni yao fyongo. Hawa wahuni hawataki kujifunza. Mwaka juzi, mwezi Februari, walituma watu kuja kunidhuru hapa Uingereza. Kwa vile Idara hiyo inaiendeshwa kishkaji, nadhani walituma wababaishaji walioishia kudakwa na mashushushu wa hapa Uingereza, ambao baadaye waliwafahamisha Polisi hapa Glasgow kuwa nichukue tahadhari muhimu. Na tangu wakati huo nimekuwa nikiishi na uelewa kuwa kuna mtu flani, siku flani atajaribu kunidhuru. Sio rahisi kuishi namna hiyo lakini sio impossible.Na hili tukio la majuzi limekuwa kama 'wake-up call' kwamba hujuma hizo dhidi yangu bado zipo hai.

Nilipokuwa mtumishi wa taasisi hiyo, niliitumikia kwa uadilifu mkubwa, na nilifanya kazi katika vitengo mbalimbali.Lakini kubwa zaidi, hadi ninaondoka huko nyumbani kuja huko kimasomo, nilikuwa Mkuu wa Kanda ya Kiintelijensia katika moja ya kanda zake jijini Dar. Huo si wadhifa mdogo, na ninakumbuka nilipowaambia maafisa wangu kuwa nakwenda Uingereza kimasomo, wapo walioniuliza 'sasa bosi unataka nini zaidi ya hiki ulichonacho sasa?' Japo wakati huo nilikuwa na shahada moja kutoka UDSM, dhamira yangu siku zote ilikuwa kukamata udaktari wa kitaaluma, na nilipopewa skolashipu kuja huku kimasomo, sikufikiria mara mbili.

Enough about that. Laiti Idara yetu ya Usalama ingekuwa na vipaumbele mwafaka basi ingehangaika na wahalifu waliokimbilia kwenye siasa na kuwadhibiti au ingehangaika na tishio la usalama wa taifa letu katika biashara ya madawa ya kulevya. Wanazidi kujaza mafaili kwenye masjala yao yenye majina ya wauza unga lakini wapo bize na watu kama sie tusio na hatia.

Wengi wenu mnanifahamu kama 'mropokaji' lakini kwa vile nilikula kiapo cha utiifu, hata siku moja sijawahi kuropoka kuhusu mambo mbalimbali niliyoshuhudia au kushiriki wakati nikiwa mtumishi wa taasisi hiyo. Sasa kwanini niendelee kuonekana adui? 

Hiyo operesheni fyongo ya mwaka juzi ilinishtua, lakini hii ya majuzi imenichukiza. Ushauri wangu pekee kwa Idara hiyo ni wa aina mbili: kwanza, fedha za Watanzania zinazopotezwa kufuatilia watu wasio na makosa zielekezwe katika kuimarisha uwezo wa Idara hiyo kupambana na wahalifu halisi wanaotishia usalama wa taifa letu, eg mafisadi , wauza unga, majangili, nk. Lakini pili, nimewashauri pia kwamba fedha zinazotumika kutufutilia akina sie' zielekezwe kwenye mafunzo ya maofisa wanaokabidhiwa majukumu ya aina hiyo. Walijaribu kuja kunidhuru hapa UK wakaishia kuumbuka. Na sasa wamejaribu kunishughulikia huko nyumbani, wameishia kupata hasara ya bure. Lakini wahuni hawa hawana uchungu na fedha wanazotumia kwa operesheni fyongo kwa vile hazitoki mfukoni mwao.

Sikupenda kzungumzia suala hili hadharani lakini imenilazimu kufanya hivyo hasa baada ya kufahamishwa kuwa familia yangu huko Tanzania inaishi kwa hofu baada ya kufahamishwa kuwa kuna watu wapo Ifakara kwa 'nia mbaya' dhidi yangu. Ninatambua hii ni vita ya sisimizi (mie) na tembo (Idara hiyo) lakini cha kutia matumaini ni vitu viwili: siku zote Mungu husimama na wanaonyanyaswa, na pili, mafunzo aliyopitia tembo ndio aliyopitia sisimizi. Hapa ni suala la akili ya nani iko mbele ya mwenzie, na ninaamini kuwa kamwe operesheni hizo fyongo hazitofanikiwa. Mlinifunza 'constant vigilance of an officer.' For your information, kwa hakika ninaitumia vizuri sana. This is a battle of wits...and sadly for you, I am still winning.

Sijaandika haya kusaka huruma ya mtu flani au taasisi hiyo. Nimeamua tu kuweka rekodi bayana. 

Asanteni kwa kuchukua muda wenu kunisoma

MESSAGE SENT AND DELIVERED.

1 comment:

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.