21 Oct 2015




OKTOBA 25 mwaka huu, Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani. Mchuano mkali zaidi unatarajiwa kuwa katika nafasi ya urais, ambapo licha ya vyama vinane kusimamisha wagombea wao katika nafasi hiyo, ushindani mkali ni kati ya mgombea wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, na yule wa umoja wa vyama vinne vya upinzani (Ukawa), Edward Lowassa.
Ushindani huo unatokana na unachangiwa zaidi na ukweli kwamba mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa, Lowassa, awali alijaribu kuwania nafasi hiyo akiwa mwanachama wa CCM, lakini jina lake halikupitishwa, na hatimaye alijiunga na moja ya vyama vinavyounda Ukawa, Chadema, na kupitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya umoja huo unaojumuisha pia chama cha National League for Democracy (NLD), NCCR- Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF).
Yayumkinika kuhitimisha kuwa Rais wa Tano wa Tanzania, atakayemrithi Rais wa sasa, Jakaya Kikwete, atakuwa kati ya Dk. Magufuli au Lowassa, huku mgombea urais kwa tiketi ya chama kipya cha Alliance for Change and Transparency (ACT- Wazalendo), Anna Mghwira akitarajiwa kushika nafasi ya tatu.
Dalili kuwa uchaguzi huo ungekuwa na ushindani mkubwa zilianza kujitokeza katika mchakato wa CCM kumpata mgombea wake, ambapo licha ya baadhi ya wanasiasa wa chama hicho waliokuwa na nia ya kuwania urais kujitokeza kutangaza nia takriban mwaka mzima kabla ya kuanza rasmi kwa mchakato huo, jumla ya makada 43 walichukua fomu za kuwania kuteuliwa kuwa wagombea urais, huku 38 kati yao wakifanikiwa kurejesha fomu.
Kwa upande wa Lowassa, jina lake lilianza kusikika katika duru za siasa za Tanzania kuhusu mrithi wa Rais Kikwete, mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Ikumbukwe pia kuwa Lowassa alikuwa na mchango mkubwa katika kampeni za urais mwaka 2005, ambapo hatimaye Rais Kikwete alishinda. Kadri Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ulivyozidi kujongea, ndivyo jina la Lowassa lilivyozidi kuvuma. Kimsingi, mchakato wa CCM kupata mgombea wake uligubikwa zaidi na shauku ya Watanzania iwapo Lowassa angepitishwa au la.
Hata hivyo, hatimaye jina la Lowassa halikupitishwa, na badala yake akapitishwa Magufuli, hatua ambayo pia ilihitimisha tetesi za muda mrefu kuwa urafiki kati ya Lowassa na Rais Kikwete ulikuwa umefikia kikomo, hasa ikizingatiwa kuwa hoja iliyokuwa na nguvu katika harakati za Lowassa kuwania urais kupitia CCM ni hisia kuwa huenda Kikwete angemsaidia Lowassa kuwa mrithi wake.

Kwa upande wa Ukawa, umoja wa vyama vinne vya upinzani ulioundwa katika Bunge Maalumu la Katiba mwaka jana kwa lengo la kushinikiza matakwa ya wananchi yaheshimiwe katika mchakato wa kupata Katiba mpya, mchakato wa kumpata mgombea wao wa urais ulitawaliwa na ukimya kwa muda mrefu, kabla ya Lowassa kujiunga na Chadema na hatimaye kupitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya umoja huo. Ujio wa Lowassa uliamsha hamasa kubwa miongoni mwa wafuasi wa vyama vinavyounda umoja huo, sambamba na kuleta ushindani mkubwa dhidi ya CCM.
Hata hivyo, uamuzi wa Chadema kumpokea Lowassa, mwanasiasa ambaye chama hicho kilimwandama na tuhuma za ufisadi kwa muda mrefu, ulipokelewa kwa hisia tofauti na Watanzania wengi, huku baadhi wakiuona umaarufu wake kama mtaji muhimu kuwezesha kuishinda CCM, huku wengine wakidhani kitendo hicho ni cha usaliti, hususan kwa Chadema ambayo ajenda yake kuu ilikuwa kupambana na ufisadi.
Licha ya uamuzi wa Lowassa kujiunga na umoja huo wa wapinzani, ukweli kwamba kwa mara ya kwanza, vyama vya upinzani nchini humo vimeweza kushirikiana kwa kusimamisha wagombea mbalimbali katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani, imeufanya uchaguzi huo kuwa wa kwanza katika historia ya Tanzania ambapo nafasi ya ushindi kati ya chama tawala na upinzani zinakaribiana.
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya Watanzania sio wanachama wa chama chochote cha siasa. Na kundi hili licha ya kutarajiwa kuwa muhimu katika kuwezesha ushindi katika uchaguzi huo, pia linajumuisha wapiga kura wanaokabiliwa na uamuzi mgumu kujiunga mkono CCM na mgombea wake licha ya chama hicho kutuhumiwa kuwa kumechangia matatizo mengi yanayoikabili nchi hiyo, au kujiunga mkono Ukawa ambayo mgombea wake wa urais, Lowassa, licha ya kuhubiri kuhusu mabadiliko, anaonekana kama hana tofauti na chama hicho tawala, hasa ikizingatiwa alikuwa huko kwa muda mrefu.
Kwa tathmini hadi wiki hii ya mwisho kabla ya uchaguzi huo, chama tawala CCM 

kinatarajiwa kufanya vizuri zaidi ya vyama vya upinzani katika nafasi zote, yaani urais, ubunge na udiwani. Kwa upande wa urais, nguvu za CCM zimekuwa katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na kujenga picha kuwa mpinzani wao mkuu, Lowassa, hafai ndio maana jina lake lilikatwa katika mchakato wa chama hicho kupata mgombea wake.
Kujenga picha kuwa Lowassa, pamoja na viongozi wachache wa CCM walimfuata huko upinzani ni wenye uchu wa madaraka, wanaotumia malalamiko ya wananchi dhidi ya CCM kwa manufaa yao kisiasa.
Tuhuma za ufisadi dhidi ya Lowassa ambazo kimsingi zilitangazwa zaidi na vyama vya upinzani hususan Chadema. Katika hoja hiyo, CCM pia imejaribu kuionyesha Chadema na Ukawa kwa ujumla kama wanasiasa wasio na msimamo na walioikimbia ajenda yao ya kupinga ufisadi ili ‘kumsitiri’ Lowassa.
Kutofanikiwa kwa Lowassa na Ukawa kuelezea kwa undani kuhusu ajenda yao ya mabadiliko. CCM na mgombea wake Magufuli wamekuwa wakitumia muda mwingi kubainisha sera zao na jinsi watakavyotekeleza.
Takriban asilimia 85 ya Watanzania wanaishi maeneo ya vijijini ambayo kiasili ni ngome kubwa ya CCM kwenye chaguzi. Kwa upande mwingine, Ukawa hawajafanikiwa kujipenyeza vya kutosha katika maeneo hayo, ambapo pia kuna uelewa mdogo kuhusu muundo wa umoja huo.
Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, idadi ya wanawake –kundi ambalo kiasili ni ngome muhimu ya CCM – ni kubwa zaidi ya wanaume, na hii inatarajiwa kukinufaisha chama hicho tawala na mgombea wake Magufuli.
Magufuli, amekuwa waziri kwenye awamu mbili za urais Tanzania, Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa, na hii ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, na anasifika kwa uchapakazi. Kwa upande mwingine, ugombea wa Lowassa umeendelea kugubikwa na kashfa ya Richmond iliyosababisha ajiuzulu Uwaziri Mkuu mwaka 2008.
Kadhalika, licha ya kuwa na mtandao mkubwa nchi nzima, kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa, CCM inanufaika na hoja inayojiri kwenye kila uchaguzi mkuu, kuwa kuwapa ushindi Wapinzani ni sawa na kuwapa fursa ya kufanya majaribio ya uongozi ilhali CCM ina uzoefu wa kutosha.
Mapema wiki hii ziliibuka tena taarifa kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa Chadema alihamisha mabilioni ya shilingi kwenda nje ya nchi, fedha zinazodaiwa zilipatikana baada ya kiongozi huyo ‘kukiuza chama hicho’ kwa Lowassa.
Hata hivyo, changamoto kubwa kwa CCM ni kinachotafsiriwa kama hasira za Watanzania wengi kutokana na matatizo mbalimbali yanayoikabili nchi hiyo, ambayo CCM inabebeshwa lawama, kubwa zaidi likiwa ufisadi unaotajwa kama chanzo kikuu cha umasikini.
Wachambuzi mbalimbali wa siasa za Tanzania wanatafsiri kuwa ufuasi mkubwa kwa Lowassa na Ukawa unachangiwa zaidi na manung’uniko ya wananchi wengi dhidi ya CCM, kiasi cha kuwa radhi kumwamini mwanasiasa ambaye kwa muda mrefu ameandamwa na tuhuma za ufisadi. Kauli kama ‘bora kulipigia kura jiwe kuliko CCM’ sio tu imekuwa ikisikika mra kwa mara miongoni mwa wafuasi wa upinzani bali pia inaashiria manung’uniko hayo.
Kadhalika, kwa vyama vinne vya upinzani kuweza kushirikiana na kumsimamisha mgombea mmoja wa urais, na kuongezewa nguvu na ujio wa Lowassa pamoja na makada kadhaa waliohama CCM, kwa mara ya kwanza Wapinzani wanaona kuna uwezekano wa kukishinda chama hicho tawala. Mikutano yao ya kampeni imeshuhudia umati mkubwa japokuwa lawama kwa Lowassa imekuwa ni kuhutubia kwa muda mfupi mno.
Wakati Magufuli na CCM wanaonekana kujiamini na kuwa na uhakika wa ushindi, kwa upande wa Lowassa na Ukawa, licha ya kuwa na matumaini makubwa ya kushinda, wanaonekana kuwa na hofu ya kuhujumiwa na chama hicho tawala.
Kwenye nafasi za ubunge na udiwani, CCM inatarajiwa kusinda viti vingi zaidi kwa sababu licha ya kuwa na mtandao mzuri majimboni, Ukawa inaonekana kuwekeza nguvu zaidi katika kumnadi Lowassa kuliko katika kampeni zake majimboni. Kadhalika, takwimu zinaonyesha kuwa mgombea wa CCM, Magufuli, ametembelea maeneo mengi zaidi ya mgombea wa Ukawa, Lowassa.
Kwa upande wa vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi huo, inatarajiwa kuwa ACT-Wazalendo kitashika nafasi ya tatu nyuma ya CCM na Ukawa, na kinatarajiwa kuimarika zaidi baada ya uchaguzi huo hasa kwa vile inahisiwa kwamba iwapo Ukawa itashindwa, wafuasi wake wengi wanaweza kuiona ACT-Wazalendo kama mpinzani wa kweli dhidi ya CCM.
Kwa hitimisho, changamoto kubwa kwa chaguzi nyingi barani Afrika huwa kwa chama cha kikuu cha upinzani kukubali matokeo pindi kikishindwa. Kwa mara ya kwanza, Tanzania inafanya uchaguzi wake mkuu huku kambi ya upinzani ikiwa na imani kubwa kuwa itaibuka na ushindi.
Kadhalika, kadri uchaguzi unavyozidi kukaribia ndivyo Wapinzani (hasa Ukawa) wanavyozidi kuonyesha kutokuwa na imani na mfumo mzima wa uchaguzi. Bila kujali upande gani utakaoibuka na ushindi, mustakabali wa Tanzania unategemea busara za viongozi na wafuasi wa kila chama kuhamasisha amani badala ya vurugu. Ushindi mkubwa katika uchaguzi huo ni kwa Watanzania kuendelea kubaki na umoja na amani.
Pia, mshindi katika uchaguzi huo atakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoikabili Tanzania, kubwa zaidi ikiwa kuleta uwiano kati ya utajiri wa raslimali lukuki katika nchi hiyo na hali ya maisha ya wananchi, kupunguza pengo kati ya matajiri na masikini, na kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja baada ya uchaguzi huu ambao kwa kiasi kikubwa umejenga mpasuko kijamii na kisiasa.
Mwisho, kwa vile hii ni makala yangu ya mwisho kabla ya uchaguzi huo hapo Jumapili, na kwa vile safu hii imekuwa ikifuatilia maendeleo ya uchaguzi huo tangu mwanzo, basi si vibaya kufanya ubashiri wa matokeo katika nafasi ya urais. Na ubashiri kuwa Magufuli atashinda urais, na CCM itashinda viti vya jumla katika nafasi za ubunge na udiwani, huku Ukawa, hususan Chadema, ikipata viti pungufu zaidi ya ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliopita.
Hata hivyo, mshindi halisi katika uchaguzi huo ni Tanzania na Watanzania wenyewe. Kuna maisha baada ya uchaguzi, kwa hiyo ni muhimu kwa upande utakaoshindwa kutanguliza mbele maslahi ya taifa, badala kufanya vurugu.
MUNGU UBARIKI UCHAGUZI MKUU. MUNGU IBARIKI TANZANIA.

1 comment:

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.