18 Mar 2016

NIANZE makala hii kwa kuomba radhi kutokana na safu hii kutochapishwa wiki iliyopita. Hali hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.

Miongoni mwa mada zinazotawala katika mijadala mbalimbali ya Watanzania hususan katika mitandao ya kijamii ni pamoja na suala linalofahamika kama ‘Kiingereza cha Rais John Magufuli.’ Mjadala huo umepamba moto zaidi kwenye mitandao ya kijamii ya Jamii Forums na Facebook. Mjadala huo ulianza rasmi baada ya kikao cha wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo hotuba ya Rais Magufuli ilizua hoja kuwa ‘Kiingereza chake kina kasoro.’ 

Kama Mtanzania mwenye makazi hapa Uingereza, nchi ambayo ndio ‘wenyeji wa Kiingereza,’ na ambaye kwa sasa ninafundisha kundi la watafiti (profesa mmoja, wahadhiri saba na wanafunzi wa shahada ya uzamivu wanane) wanaotarajia kuja huko nyumbani kwa ajili ya utafiti, nimeguswa sana na mjadala huo. 

Kwanza tuweke rekodi sawa. Kimsingi, Kiingereza alichoongea Rais Magufuli kinakubalika. Sawa, kinaweza kuwa sio timilifu lakini moja ya ‘siri’ za kuongea lugha ya kigeni, ikiwa ni pamoja na Kiingereza kwetu, ni uwezo wa kueleweka.

Pili, bila kuonekana ninamtetea Rais Magufuli, ni muhimu tukumbuke kuwa asili yake kitaaluma ni mwanasayansi. Na japo si kila mwanasayansi anasumbuliwa na Kiingereza, sio jambo la kushangaza kukutana na Wanasayansi ambao hawamudu Kiingereza vizuri. Hii inatokana na ukweli kuwa masomo yao sio ya lugha, na Kiingereza wanachotumia ni cha kitaalamu zaidi kuliko cha maongezi ya kawaida. 

Lakini tatu, na hili ni la muhimu zaidi, Kiingereza sio lugha yetu ya asili. Katika hili nitoe mfano ufuatao. Nilipoombwa kufundisha kundi hilo la watafiti wanaotarajia kuja huko nyumbani, awali nilidhani ni kundi la wanafunzi wa shahada ya uzamifu pekee. Kwa hiyo, licha ya ukweli kwamba sijafundisha darasani kitambo, nilijipa matumaini kuwa jukumu lililo mbele yangu sio gumu sana kwa vile nitakuwa nafundisha wanafunzi pekee.

Hata hivyo, kabla ya kuanza kufundisha kozi hiyo, nilipatiwa orodha ya ‘wanafunzi’ wangu, ambapo kwa mshangao, ilijumuisha profesa na wahadhiri kadhaa (wahitimu wa shahada ya uzamivu ambao miongoni mwao wapo wanaofanya kitu kinachojulikana kama ‘post-doctorate.’) Kwa hiyo, kule kujiamini kwangu kwa awali kuliyeyuka ghafla kwani kumfundisha mwanafunzi ni suala moja, lakini kumfundisha mhadhiri, hususan huyo profesa, ni shughuli pevu. 

Lakini mkuu wa idara inayohusika na ufundishaji wa kozi za lugha za kigeni alinipa maneno haya ya kutia moyo; “…bila kujali kuna profesa na wahadhiri, wewe ndiye mwalimu wao. Uprofesa na uhadhiri ni kwenye fani zao, lakini katika Kiswahili hao wote ni wanafunzi wako.” Hiyo ilinipa moyo, na kozi hiyo imekuwa ikiendelea kwa ufanisi mkubwa.

Lengo la mfano huo ni kuonyesha kuwa linapokuja suala la lugha ya kigeni, Haijalishi fulani ni kiongozi wa nchi au profesa, kwa sababu ni watu wachache tu wanaomudu vilivyo lugha zisizo zao. Hao ‘wanafunzi’ wangu ni wasomi waliobobea katika fani zao, lakini hawajui Kiswahili japo cha kuombea maji. Na huwezi kuwalaumu kwa sababu lugha hiyo ni ngeni kwao.

Kuna kasumba moja inayokera sana kuhusu baadhi ya ‘wasomi’ wetu wa Kitanzania, ambapo kuongea Kiingereza kunawafanya wajione wapo daraja la juu zaidi ya wasiomudu vema lugha hiyo au wasioiongea kabisa. Kwa sisi wengine ambao tunaamka, tunashinda, na tunakwenda kulala huku tunasikia Kiingereza, tunakerwa na mazingira ambapo unakutana na Mswahili mwenzako, badala ya kukupatia fursa mwanana ya kuongea naye lugha yetu ya asili, anatumia Kiingereza.

Ni kasumba iliyoshamiri mno kwenye mitandao ya kijamii ambapo baadhi ya wenzetu hawataki kabisa kuzungumza Kiswahili. Mara kadhaa nimekuwa nikiwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa sijawahi kuwaona Waingereza wakifanya maongezi kwa lugha ya kigeni labda iwe ni kwa minajili ya kujifunza tu. Tena kimsingi, Waingereza wanashutumiwa vikali na wenzao wa nchi mbalimbali za Ulaya kwa kupuuza lugha nyingine na kuiendekeza lugha yao.

Tofauti na sisi, wenzetu Wakenya wapo mahiri sana katika kukienzi na kukiendeleza Kiswahili. Kwa hapa Uingereza, Wakenya wengi wanajihusisha na shughuli za utafsiri wa Kiswahili kwenda Kiingereza au kinyume chake, kwa sababu wanamudu vema lugha zote mbili. Lakini kubwa zaidi ni mapenzi yao kwa Kiswahili, licha ya ukweli kuwa Kiswahili chetu Watanzania ni bora zaidi cha majirani zetu hao.

Ni nadra kwa hapa kukutana na Mkenya akazungumza nawe kwa Kiingereza. Atajikakamua hivyo hivyo na Kiswahili ‘chao’ lakini la muhimu mtaweza kuelewana. Sasa sisi Kiingereza chenyewe ni mgogoro mkubwa, lakini watu wapo radhi kujikakamua, na wengine kutokwa macho kama mjusi aliyebanwa na mlango, ili tu waongee ‘kimombo.’ Kwani wakizungumza Kiswahili wanapungukiwa na nini hasa?

Nimeambiwa kuwa katika hotuba yake kwenye dhifa ya kumkaribisha Rais wa Vietnam, Troung Tang Sang, Rais Magufuli alihutubia kwa Kiswahili. Nadhani huo ni mwanzo mzuri, na ninamsihi aendelee kuenzi lugha yetu ya taifa kwa sababu tusipoienzi sisi ‘wamiliki,’ ni dhahiri itapuuzwa na wengineo.

Inakadiriwa kuwa Kiswahili kinazungumzwa na takriban watu milioni 50 duniani. Ni lugha ya kimataifa. Wenye jukumu kubwa la kukienzi, kukiendeleza na kukitangaza ni Watanzania ambao kimsingi ndio tunaozungumza Kiswahili fasaha zaidi ya wenzetu wengine katika nchi kama Kenya, Uganda au Burundi.

Nimalizie makala hii kwa kuhitimisha kuwa pengine ‘lawama’ hizo zinazoelekezwa kwa Rais Magufuli kwa ‘Kiingereza chake’ zinaweza kuleta kitu Waingereza wanaita ‘blessing in disguise,’ yaani pale kitu kisichopendeza kinapoleta matokeo chanya. Kwa mfano, iwapo ‘lawama’ hizo zitasababisha Rais wetu sio tu kutumia zaidi Kiswahili katika matukio ya kimataifa bali pia kuhamasisha matumizi ya lugha yetu hiyo ya taifa.

Tukumbuke, mkataa asili yake ni mtumwa.

2 comments:

  1. Ukweli siku zote utabaki kuwa ukweli tu hata ukijaribu kuutengenezea mazingira gani haukwepeki. Katika suala la lugha mzee ni dhaifu, lazima ukweli huo tuukubali tu. Nadhani hicho pia ni kigezo kizuri kwa mkuu wa nchi ili aweze kuhusiana vizuri na mataifa mengine. Kwamba kasoma sayansi, ni utetezi ambao hauna mashiko hasa kwa msomi wa ngazi ya uzamivu na ambaye ameshika nyadhifa za juu kitaifa kama uwaziri kwa miaka 20. Ikiwa katika baadhi ya nafasi za kazi tu mtu anakosa nafasi kwaajili ya udhaifu wa lugha je si zaidi sana katika nafasi iliyo ya juu kabisa katika nchi? Tuwe wakweli tusitake kuupamba uozo uonekane kuwa sawa.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.