29 May 2016

Mama mpendwa,ilikuwa siku kama yale leo,miaka minane iliyopita,uliondoka hapa duniani wakati tunakuhitaji sana.Japo miaka minne inaweza kuonekana ni muda mrefu kusahau machungu,kwangu mwanao imeshindikana.Kila siku ya Mungu ninaposali kukuombea pumziko na raha ya milele huko ulipo,hujikuta napatwa na uchungu usioelezeka.Kwa kifupi,mama mpendwa,kila siku baada ya kifo chako-siku kama ya leo miaka minane iliyopita,imeendelea kuwa ni hudhuni na majonzi yasiyoelezeka.

Mama mpendwa,ulikuwa ni zaidi ya mama kwangu,kwa mumeo marehemu Baba Mzee Chahali (aliyeungana nawe huko peponi mwaka jana),na kwa wanao wote na ndugu na jamaa.Nakumbuka mwaka 2005 nilipokuja likizo nyumbani,ulirukaruka kwa furaha,ukanikumbatia na kunipakata mwanao,ukaniandalia maji ya kuoga,ukanifanya nijsikie kama mtoto mchanga. Sikujua kuwa furaha ile ya mzazi kumwona mwanae waliopoteana kitambo kidogo sintoipata tena maishani.Inaniuma sana.
Marehemu mama akicheza siku ya harusi ya mwanae wa nne. Yeye na marehemu baba walijaliwa kupata watoto tisa, mmojaalifariki  na tukabaki wanane, wanaume sita na wanawake wawili.
Nakumbuka wakati huo ambapo wewe na marehemu Baba mlikuwa mnasherehekea miaka 50 ya ndoa yenu,ulinipa mafundisho mengi kuhusu maisha,ndoa, upendo na zaidi ni kumweka mbele Mungu katika kila ninalofanya. Kabla ya kifo chako, nilikuwa nauangalia mkanda niliowarekodi wewe na  marehemu Baba,na kila nilipofanya hivyo niligundua kuwa nina bahati ya pekee kuwa na wazazi wanaonipenda kiasi hicho. Sikujua kuwa mahojiano yale ndio ulikuwa wosia wako na marehemu baba kwangu mwanenu. Kwa sasa sina nguvu ya kuangalia video hiyo, kwani kila nikijaribu naishia kububujikwa na machozi.

Nakumbua nilipokwenda chumba cha maiti na kukuona umelazwa kwenye zile friji wanzohifadhia maiti. Nilikugusa mama,nilitaraji muujiza kwamba ungeamka na ndoto ile mbaya ingeisha. Hukuamka hadi leo hii.

Hospitali Teule ya Mtakatifu Fransisko ambapo marehemu mama alilazwa akiwa amepoteza fahamu kwa zaidi ya miezi mitatu hadi alipofariki siku kama ya leo miaka minane iliyopita

Mama,inaniuma sana kwani nilipokuja kukuuguza Februari 2008 ulikuwa umeshapoteza fahamu. Ulipokuwa Muhimbili na baadaye St Francis, Ifakara,nilikuwa najaribu kukusemesha.Kama vile ulifahamu mwanao nimekuja kukuuguza,kuna nyakati ulikuwa unatoa tabasamu lako lenye mwanya ulionirithisha. Nikategemea ungemka na kunieleza japo neno moja.Kwa bahati mbaya hadi unafariki hukuweza kuniambia chochote. Iliniuma sana, inaniuma sana na itaendelea kuniuma sana, mama.

Kabla marehemu baba hajaungana nawe huko uliko, nilikuwa na wakati mgumu sana kila nilipopiga simu nyumbani kwa wakati wa uhai wako, nilizowea kuwa nikimaliza kuongea na Baba anakupa simu wewe tupige stori. Na kila nilipoongea nawe nilijisikia kudeka kutokana na upendo wako usiomithilika. Baada ya kifo chako, na kabla marehemu baba hajafariki, kila nilipompigia simu mzee huwa nilijikuta najisahau na nataka kumwambia Mzee akupe simu niongee nawe,kisha nakumbuka kuwa hauko nasi. Sasa ndio imekuwa uchungu maradufu kwani kila nikipiga simu nyumbani, ninatamani kuongea nawe na marehemu baba kisha nakumbuka kuwa hampo nasi.

Nyakati nyingine baadhi ya watu wangu wa karibu (ninao wengi kutokana na malezi bora uliyonipatia) huwa wananiona kama dhaifu ninapowaeleza uchungu nnilio nao takriban kila siku tangu ufariki wewe na baadaye marehemu baba.Siwalaumu,kwani wanachojitahidi kufanya ni kunishawishi nikubali ukweli kuwa hampo nasi na haiwezekani kuwarejesha. Kuna wakati wananichukiza kwani najihisi kama hawaelewi jinsi kifo chako kinavyoniathiri.Lakini baadaye akili hunirejea na kutambua wanachofanya ni kujaribu kunisaidia tu.


Mama mpendwa, sijui nisemeje. Rafiki zako wakubwa, wanao vitinda-mimba,Kulwa na Doto, ndio wananitia uchungu zaidi, Wanawa-miss mno wewe na marehemu baba kwa sababu ndio uhusiano wenu ulikuwa zaidi ya kati ya wazazi na vitinda-mimba wao. Nakumbuka siku zile nawapigia simu na kuwasikia mnacheka,mnataniana na kunipa kila aina ya faraja. Kwa sasa imebaki kumbukumbu tu.

Mama mpendwa,siku ya mazishi yako Padre alituambia maneno haya: "Mama Adelina alikuwa mtu wa watu, na kila anayemjua anafahamu hilo. Japo mnaomboleza kifo chake, lakini mnapaswa kupata faraja kuwa kutokana na matendo yake mema, Baba Yake wa Mbinguni Ameamua kumchukua.Sote tulimpenda lakini Mungu alimpenda zaidi,na ndio maana amemchukua." Maneno hayo ndio nguvu pekee inayonisaidia kumudu kufanya mambo mengine maishani. Nguvu nyingine niliyonanyo ni imani kuwa wewe na marehemu baba mnaendelea kutuombea huko mlipo.

Nyumba ya milele ya marehemu Adelina 

Basi naomba nikuage tena mama kwa kumwomba BWANA AKUPATIE NA MAREHEMU BABA PUMZIKO LA MILELE NA MWANGA WA MILELE AWAANGAZIE, MPUMZIKE KWA AMANI AMEEN.


2 comments:

  1. Asterehe kwa amani mama yetu Adelina tupo nawe kiroho na kwa maombi kila siku.

    ReplyDelete
  2. Amen dadangu mpendwa Yasinta. Asante kwa kuwa nasi kila tarehe hii tangu marehemu alipofariki. Ni upendo usiomithilika. Asante sana dadangu. Mungu akubariki sana.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.