20 Aug 2016



Kwanza kabla ya kuingia kwa undani katika uchambuzi huu, ni vema nikaweka bayana uhusiano wangu na watu wawili ninaowaongelea katika makala hii: Rais John Magufuli na aliyekuwa RC wa Arusha Felix Ntibenda. 

Oktoba mwaka 2006, nilianza kufuatilia kilichokuja kujulikana baadaye kama 'skandali ya Richmond' (rejea HAPA na HAPA  na hatma yake HAPA). Kwa kifupi, nilikuwa bloga pekee niliyelivalia njuga suala la Richmond, tangu mwanzo wake hadi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alipolazimika kujiuzulu.

Wasichoelewa watu wengi ni kwamba uamuzi wangu wa kufuatilia suala hilo ulinigharimu mno, kikazi, kimasomo na kimaisha kwa ujumla. Laiti ningelipa kisogo suala hilo basi leo hii ningeendelea kuwa mtumishi wa umma. Hata hivyo, sijilaumu wala kusikitika kwa sababu mabadiliko yanahitaji kujitoa mhanga.

Lakini niwe mkweli, yaliyonisibu kutokana na ufuatiliaji wangu wa suala hilo yameniachia kinyongo, na ni kinyongo hicho kilichopelekea uamuzi wa kumuunga mkono mpinzani mkuu wa Lowassa katika kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais mwaka jana. Pamoja na 'tofauti zangu na CCM' haikuwa vigumu kwangu 'kuungana nao dhidi ya our common enemy.' Waingereza wanasema 'chuki ya pamoja na mwanzo wa urafiki.'

Hiyo ndio iliyokuwa sababu ya kumpigia debe mgombea wa CCM, Dkt John Magufuli. Na kwa vile kabla ya hapo nilikuwa nikiunga mkono harakati za vyama vya upinzani, hususan Chadema, uamuzi huo wa kumsapoti mgombea wa CCM ulipelekea mie kuonekana 'msaliti,' nikamwagiwa idadi kubwa tu ya matusi, huku baadhi ya 'waungwana' wakidai kuwa nilikuwa najikomba kwa ajili ya kutaka u-DC.

Kufupisha stori, sio tu kuwa kama Mtanzania nina haki na uhuru wa kupongeza au kumkosoa Rais Magufuli bali pia ukweli kuwa nilikuwa miongoni wa waliompigia kampeni unaniongezea haki na uhuru huo.

Na katika makala hii ninatumia uhuru huo na haki hiyo kwa kumkosoa kidogo Rais wangu katika 'tumbua majipu' yake. Ninasema 'kumkosoa kidogo' kwa sababu kwa ninamuunga mkono kwa kiasi kikubwa katika jitihada zake za 'kuinyoosha Tanzania yetu,' ikiwa ni pamoja na umuhimu wa utumbuaji majipu.

Waingereza wana msemo kwamba sio kila jambo sahihi ni zuri na sio kila jambo zuri ni sahihi.Ntakupa mfano. Ukitembelewa na mtu mwenye njaa kali, waweza kukimbilia kumpa chakula kingi ili aondoe njaa hiyo. Kwa kufanya hivyo waweza kumpelekea akavimbiwa au hata akapoteza maisha (yes, mlo 'wa ghafla' waweza kuuwa mtu). Kinachopaswa kufanyika katika hali hiyo ni kwanza kumpatia mwenye njaa huyo kimiminika cha moto, kama vile uji au chai kabla ya kumpatia mlo kamili.

Mfano huo unaonyesha kuwa jambo sahihi la kumpatia mlo mwenye njaa lingeweza kuwa na matokeo yasiyo mazuri, yaani kuvumbiwa kwa mwenye njaa au hata kupoteza maisha.  Na laiti mwenye njaa huyo angepewa kwanza uji badala ya mlo mzito, angeweza kuhisi kuwa mwenyeji wake 'amepuuza njaa yake' kwa kumpa uji badala ya ugali/wali. Kwahiyo hapa jambo sahihi linatafsiriwa kuwa sio zuri.

Kwa mantiki hiyohiyo, utumbuaji majipu wa Rais Magufuli ni jambo sahihi kabisa, lakini kuna nyakati utekelezaji wake unaleta taswira isiyo nzuri.

Na hapa nitolee mfano wa tukio lililotokea juzi ambapo wadhifa wa aliyekuwa Mkuu wa Arusha Felix Ntibenda ulitenguliwa pasipo kutolewa maelezo yoyote.

Kwanza kitendo tu cha kutengua wadhifa wa mwakilishi mkuu wa Rais katika mkoa, bila kujali kuwajulisha wananchi ni kuwanyima haki na pia kutomtendea haki aliyetenguliwa. Ikumbukwe kuwa penye ukosefu wa taarifa sahihi, majungu au uzushu huziba pengo hilo.

Nilibainisha awali kuwa ninafahamiana na Ndugu Ntibenda. Ni mtu aliyewahi kuwa 'mwalimu' na kiongozi wangu wakati nikiwa mtumishi wa serikali huko nyuma. Misingi aliyonipatia wakati nikiwa chini yake ilipelekea nami kupewa promosheni ambayo ilidumu hadi wakati ninaondoka huko nyumbani kuja huku Uingereza kimasomo. Na sio mie pekee bali Ndugu Ntibenda 'aliwapika' lundo la maafisa ambao wengi leo hii ni watu muhimu kabisa kwa usalama wa taifa letu.


Kwa tunaomfahamu, licha ya uchapakazi wake usio na mfano, Ndugu Ntibenda ana utu wa kipekee. Na hicho ndio kilichmfanya awe kiongozi mzuri. Walio chini yake walikuwa kama sehemu ya familia yake.

Niwe mkweli, niliposikia kada fulani wa CCM ameteuliwa kuwa mkuu wa wilaya katika mkoa wa Arusha uliokuwa chini ya Ndugu Ntibenda nilipatwa na hofu kuhusu hatma ya bosi wangu huyo wa zamani. Na sababu kubwa ni kuwa Mkuu wa wilaya huyo anafahamika kwa majungu na fitna, mmoja wa mtaji mkubwa wa makada wa CCM hasa wale waliopo au waliopitia Umoja wa Vijana wa CCM .

Na kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana, kuna kila dalili kuwa njama za kumhujumu Bwana Ntibenda zilichochewa na kada huyo wa CCM kwa kushirikiana na wenzie mkoani humo. Natambua kuwa ninaweza kuonekana mnafiki kwa 'kushikilia bango' suala la Bwana Ntibenda kwa vile tu ninafahamiana nae, lakini hiyo haina uzito kulinganisha na uzito wa suala lenyewe.



Ukiangalia jinsi wadhifa wake ulivyotenguliwa unaona bayana kuwa kuna hali kama ya kuumbuana makusudi.Kama Rais au Waziri Mkuu walikuwa wanafahamu 'makosa' ya RC Ntibenda, kwanini wamwondoe madarakani katika hali ya kumdhalilisha, na kwa uharaka kana kwamba ni gaidi or something? Isingewezekana kusubiri hadi mwisho wa siku ya kazi au baada ya kumaliza majukumu yake ya kazi katika siku hiyo? 




Na kubwa zaidi, kama tukiamini kuwa alifanya makosa yaliyopelekea wadhifa wake kutenguliwa, kwanini basi, kwanza, makosa hayo yafanywe siri, na pili, kwanini ahamishiwe Ofisi ya Waziri Mkuu? Akarudie tena makosa au ni kumdhalilisha tu?

Hii ni nje ya rekodi, lakini Bwana Ntibenda alifanya kazi kubwa sana katika uchaguzi mkuu uliopita.Siwezi kuandika hapa kwa sababu ni 'mambo yasiyoandikika hadharani' lakini 'wanaofahamu yanayoendelea behind the scene' wanafahamu fika mchango wa RC huyo wa zamani.

Nimalizie makala hii kwa kumshauri Rais Magufuli kuepuka kusikiliza majungu ya kisiasa, moja ya kansa inayoitafuna CCM kwa muda mrefu. Hao vijana wanaompelekea majungu, wakishamaliza kuwaharibia wengine watamgeukia yeye Rais. Kuna msemo wa kiswahili usemao: "Mchawi akimaliza kuroga mtaa mzima huigeukia familia yake."

Kilichojiri Arusha chaweza kuwa mwendelezo wa 'kuzadia uhuni,' kama ilivyokuwa kwa yule kijana aliyemfanyia vurugu Jaji Warioba akaishia kuzawadiwa ukuu wa wilaya,na leo ni Mkuu wa Mkoa. 



1 comment:

  1. Umeongea vizuri sana kaka ila ukiachia suala la fitina na majungu ndani ya CCM. Kansa nyingine inayosumbua ni hii ya kutaka kila mtumishi wa serikali awe na misuli mipana dhidi ya Upinzani. Na kushndwa kufanya hivyo ni kutumbuliwa. Sasa hii ni miongoni mwa kansa mbaya sana itakayoturudisha nyuma. Tumeacha kushguhulikia maendeleo, tunapeleka nguvu zetu nyingi kupambana na Upinzani. Tunasahau kuwa migongano ya kimawazo ndio nyenzo madhubuti ya kamaendeleo. Hata mitume wa Mungu walikuwa na wapinzani. Tujiulize kwa nini Mungu aliwapa upinzani mitume wake. Je, alikuwa hawapendi? Tutafakari.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.