12 Jan 2017

MIONGONI mwa kauli maarufu zaidi za Rais John Magufuli ni ile ya kuwaomba Watanzania wamwombee na msema kweli ni mpenzi wa Mungu.
Kwa bahati mbaya au pengine kwa makusudi, Rais amekuwa mtu wa kwanza kukiuka kauli hizo au kuziweka katika mazingira magumu kutekelezeka.
Nianze na hiyo kauli ya kuwataka Watanzania wamwombee. Pengine wakati ambao alielezea kwa undani mantiki ya kauli hiyo ni wakati wa uzinduzi wa bunge mwaka jana, ambapo alizungumzia kwa undani ugumu unaoikabili vita dhidi ya rushwa na ufisadi.
Katika hotuba hiyo, aliwafahamisha Watanzania kuwa wanaohusika na rushwa na ufisadi sio watu wadogo, kwa maana kwamba ni watu wenye uwezo mkubwa. Na kwamba licha ya dhamira yake na jitihada zake, angehitaji sio tu ushirikiano wa wananchi bali sala na dua zao pia.
Niwapeleke kando kidogo kabla ya kubainisha kwa nini nimeandika Rais amekuwa mtu wa kwanza kukiuka kali zake mwenyewe. Katika sosholojia, kuna kanuni moja inayofahamika kama ‘Social Exchange.’ Kwa kifupi, pamoja na mambo mengine, kanuni hii inaelezea kuhusu uhusiano (interactions) kati ya watu katika jamii.
Kanuni hiyo inatanabaisha kuwa uhusiano kati yetu katika jamii huongozwa na ‘zawadi’ (rewards) na ‘gharama’ (costs). Na watu wengi huongozwa na kanuni (formula) hii: thamani (ya mtu) = zawadi – gharama. ‘Zawadi’ ni vitu vizuri kama vile pongezi, shukrani, kuombewa dua, nk ilhali gharama ni hasara, mtendewa kutoonyesha shukrani, kupuuzwa, nk.
Mfano rahisi: ukipita mtaani, ukakutana na ombaomba, ukampatia hela kidogo, kisha akanyoosha mikono angani kukushukuru, basi kuna uwezekano mkubwa wa kumsaidia tena siku nyingine. Na si ombaomba tu, bali hata ndugu, jamaa au rafiki au ‘mtu baki’ ambaye anashukuru anaposaidiwa.
Lakini laiti ukimpatia msaada ombaomba, au mtu mwingine, kisha asionyeshe kujali msaada huo, basi uwezekano wa kumsaidia tena ni hafifu. Kwa mujibu wa kanuni yetu ya ‘thamani = zawadi – gharama,’ msaidiwa akionyesha shukrani inakuwa zawadi yenye thamani zaidi ya gharama, ilhali kwa asiyeonyesha shukrani gharama inakuwa kubwa kuliko zawadi. Natumaini hizi ‘hisabati’ hazijakuchanganya ndugu msomaji.
Kimsingi, kanuni hiyo inaambatana na matarajio ya ‘nipe nikupe’ (give and take). Kwamba katika kila tunalofanya, tunakuwa na matarajio fulani. Kwamba tunapokwenda kwenye nyumba za ibada, tuna matarajio ya kumridhisha Mola kwa vile tunafuata anachotarajia kwetu: sala/ibada kwake.
Tunapokuwa watu wa msaada, au wakarimu, au wema, nk tunatarajia wale tunaowafanyia hivyo wathamini tabia zetu hizo nzuri.
Turejee kwa Rais Magufuli. Hivi karibuni, akiwa ziarani mkoani Kagera, aliwaambia wananchi kuwa, ninamnukuu; “Serikali na wananchi kila mmoja abebe msalaba wake mwenyewe.’’ Alitoa kauli hiyo alipozungumzia misaada kwa waathirika wa tetemeko la ardhi lililoyakumba maeneo ya Ukanda wa Ziwa hususan Mkoa wa Kagera.
Mwaka jana nilipokuwa naomba kura kwenu, sikuomba tetemeko la ardhi litokee hapa, hili ni jambo ambalo liko nje ya uwezo wangu, tunaomba kila mmoja aweze kutumia msaada uliotolewa ili kurejesha miundombinu ya makazi yenu” alieleza Dk. Magufuli.
Bila kuingia kiundani kuchambua mantiki ya kauli hiyo ya Rais, yayumkinika kuhitimisha kuwa kama “kila mtu abebe mzigo wake mwenyewe” basi na ombi lake maarufu kwa wananchi la “mniombee” alibebe yeye mwenyewe. Ajiombee.
Naandika hivyo kwa sababu, kiustaarabu tu, kuna baadhi ya maneno hayastahili kusemwa katika mazingira ya maombolezo, misiba, nk. Rais ni kama mzazi. Na japo kila mzazi ana jukumu la kuwa mkweli, anapaswa pia kuwa na busara ya kuchagua maneno yanayoweza kuwasilisha ujumbe bila kuumiza mioyo ya watu.
Hivi Rais angeeleza kwa lugha ya upole kuwa uwezo wa serikali ni mdogo na haitomudu kumjengea nyumba kila mwananchi, lakini itashirikiana na wananchi kadri itakavyoweza, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha misaada kwa waathirika, asingeeleweka? Au angeonekana sio ‘Rais kamili’?
Kwa mujibu wa ‘social exchange theory,’ matarajio ya Watanzania wanaaombwa na Rais wao kuwa wamwombee si kumsikia akiwaambia “kila mtu abebe mzigo wake mwenyewe” hususan mbele ya watu wanaoendelea kukabiliana na athari za janga la tetemeko la ardhi.
Lakini kama hilo la “kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe” halitoshi, Rais Dk. Magufuli akakiuka kauli yake maarufu ya “msema kweli mpenzi wa Mungu” kwa kutoa maelezo yasiyo sahihi, kwamba (ninamnukuu) “Kuna nchi kama Japan na Italia, zimekuwa zikikumbwa na matetemeko mengi, haijawahi kutokea serikali yao ikawajengea nyumba upya isipokuwa inarejesha miundombinu ya taasisi za umma kama vituo vya afya, shule na barabara.”
Sio heshima wala nidhamu kusema “Rais amedanganya” lakini alichoongea kina kasoro. Kwa Italia, baada ya tetemeko lililotokea mwezi Agosti mwaka jana, Waziri Mkuu wa zamani Mateo Renzi alishughulikia upitishwaji wa sheria ya kuidhinisha Euro bilioni 4.5 kwa ajili ya waathirika na miundombinu. Euro bilioni 3.5 kwa ajili ya waathirika na euro bilioni kwa ajili ya majengo ya umma.
Kutegemea eneo, sheria iliidhinisha malipo kati ya asilimia 50 hadi 100 kwa wananchi ambao nyumba zao ziliharibiwa na tetemeko hilo.
Huko Japan nako, mara tu baada ya tetemeko kubwa la ardhi la mwaka 2011, serikali ilichukua hatua kadhaa kuwasaidia waathirika ikiwa ni pamoja na fedha za rambirambi kwa kila familia iliyopoteza ndugu katika janga hilo (Yen milioni 5), fedha kwa familia zenye majeruhi (Yen milioni 3), misaada ya fedha kwa kila familia na mikopo yenye masharti nafuu kwa kila familia (Yen milioni 3.5), mikopo maalumu kwa watu/biashara waliokuwa na madeni kabla ya tetemeko,  ahueni ya kodi mbalimbali kwa waathirika wote, malipo kwa waliopoteza ajira (unemployment benefits), mkakati maalumu wa utengenezaji ajira mpya, na hatua nyinginezo.
Kanuni za tawala zetu za kiafrika zipo wazi: “kiongozi huwa hakosei, na akikosea huwa amenukuliwa vibaya, na kama ikithibitika amekosea haina haja ya kumradhi.” Sitarajii kusikia tamko lolote kwamba “Kauli ya Rais kuwa ‘Kuna nchi kama Japan na Italia, zimekuwa zikikumbwa na matetemeko mengi, haijawahi kutokea serikali yao ikawajengea nyumba upya’ haikuwa sahihi. Anaomba radhi.”
Wakati wa kampeni zake za kuwania urais na hata baada ya kushinda urais, Dk. Magufuli amekuwa akituomba mara kwa mara kuwa tumsaidie. Makala hii ni mwitikio wa ombi hilo. Ni mchango wangu wa msaada kwake kumsihi ajaribu kuepuka lugha inayoweza kujenga tafsiri mbaya.
Kadhalika, suala la kusaidia wenzetu waliokumbwa na tatizo sio la kisheria, kisera au ki-kanuni, au kwa vile fulani hakufanya, bali ni suala la utu. Na utu ni kama pale Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alipomtembelea mzazi wa msanii Chid Benz, kuangalia uwezekano wa kumsaidia msanii huyo aliyeathirika na matumizi ya dawa za kulevya. Ni utu kwa sababu, kisheria, anachofanya msanii huyo (kununua na kutumia mihadarati) ni kosa la jinai (Ibara ya 15 ya Sheria mpya ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ya mwaka 2015).
Nihitimishe makala hii kwa kumshauri Rais Magufuli kwamba pamoja na dhamira yake nzuri kuitumikia nchi yetu kwa uwezo wake wote, na licha ya Watanzania kuwa na matumaini makubwa kwake, ni muhimu sana ajaribu ‘kupunguza makali’ kwenye lugha yake. Kama nilivyoeleza katika makala yangu iliyopita, ‘lugha ya ukali’ inaweza kujenga nidhamu ya uoga, kitu ambacho kitakwaza jitihada za Rais wetu kuijenga Tanzania tunayostahili. Ninatumaini Rais ataupokea ushauri huu na kutoona kuwa anakosewa heshima kwa kusahihishwa pale alipokosea.
Mungu ibariki Tanzania

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.