3 Feb 2017

Ninaandika makala hii kama mtu ambaye huko nyuma nilishawahi kushiriki katika mapambano dhidi ya biashara ya kulevya, nilipokuwa mtumishi wa umma katika taasisi moja ya serikali.

Vilevile, kwa muda mrefu nimekuwa miongoni mwa sauti chache za kukemea ufisadi na uhalifu katika Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuipigia kelele jamii na serikali kuhusu biashara ya madawa ya kulevya.

Makala hii imegawanyika sehemu mbili. Ya kwanza inaongelea tangazo la RC Makonda kuhusu vita dhidi ya madawa ya kulevya. Sehemu ya pili inaongelea hatua muhimu ambayo nimechukua kuunga mkono jitihada za RC Makonda, na inayohitaji ushiriki wako.

Japo siwezi kuingia kwa undani kuhusu uzoefu wangu kama mtumishi wa umma (kwa sababu za kimaadili), ninachoweza kueleza ni kwamba watu wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya ni watu wenye uwezo mkubwa kupindukia kifedha. 


Uwezo huo sio tu unawapa jeuri ya kumwona kila binadamu kama bidhaa inayoweza kununuliwa au hata kuteketezwa, bali pia unawapa u-mungu mtu flani: wanaweza kununua kila kitu pamoja na uhai wako!

Naam, kuna matukio kadhaa ya 'vifo' yaliyotokea huko nyumbani Tanzania ambayo hayakuwa ya vifo vya asili bali mauaji yenye mkono wa wahusika wa biashara ya madawa ya kulevya.

Katika utumishi huo wa umma, nilipata fursa nyingi tu za kufanya kazi na watumishi wengine wa umma kwenye taasisi zinazohusika na mapambano dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya. Uzoefu nilioupata huko ulionyesha jinsi nguvu ya fedha za 'wauza unga' ilivyopenya na kuota mizizi kwenye baadhi ya taasisi hizo. 

Kwa mfano, baadhi ya askari polisi walieleza jinsi baadhi ya wenzao walivyowekwa mfukoni na watu wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya. Wakati fulani, nikiwa kwenye basi, nilionyeshwa askari polisi aliyekuwa na kifurushi ambacho nilielezwa kuwa ni madawa ya kulevya, na mhusika alikuwa akiyapeleka kwa mhusika maeneo ya Kinondoni. Na kweli, alishuka Kinondoni katika eneo linalosifika kwa biashara hiyo haramu.

Niliwahi pia kukutana na watu waliokuwa wanajihusisha na baishara hiyo, wale wanaoitwa 'mapapa' na wale wanaoitwa 'mapusha.' Na takriban kila mara nilibaini vitu viwili: fedha nyingi kupita maelezo, fedha ambayo ni vigumu mno kuipata katika shughuli halali au isiyo halali. Na fedha hiyo inaingia mara kadhaa kila siku, pengine laki kadhaa kama sio mamilioni.

Kingine ni wahusika kuwa tayari kwa lolote. Kwanza wanatambua kuwa wanaweza kukamatwa, kwahiyo wapo tayari kutumia kila njia kuhakikisha hilo halitokei, Licha ya kutumia fedha nyingi kununua 'usalama wao,' pia waliwekeza vya kutosha kwenye ushirikina. Usalama ulijumuisha pia watu wenye kupewa maagizo aidha kwenda kudai fedha inayodaiwa au kumshughulikia 'msaliti.' Kama ambavyo wauza unga hawana huruma kwa maisha ya 'mateja,' ndivyo amabvyo hawana huruma kwa watu wanaowaona tishio kwa biashara yao ya madawa ya kulevya.

Labda siku moja nitapata nafasi ya kusimulia kwa kirefu matukio ya aina hiyo kwenye kitabu, lakini kwa leo ninachokuomba msomaji mpendwa utambue ni ukweli kwamba mapambano dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya ni moja ya vitu hatari kabisa.

Jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bwana Paul Makonda, alinukuliwa akieleza kuwa ameamua kujitoa mhanga, na kuwekeza nguvu zake katika vita dhidi ya madawa ya kulevya.
Kwa hakika ni kauli zenye uzito mkubwa. Lakini tatizo la kwanza, na ambalo naomba kukiri kuwa nilikumbana nalo, sio ujumbe uliomo kwenye kauli hizo bali wasifu wa mtoa ujumbe.

Kwa bahati mbaya au pengine makusudi tu, RC Makonda ameshatoa lundo la maagizo - kuanzia zuio la uvutaji shisha hadi ishu ya ombaomba hadi vita dhidi ya mashoga, na maagizo mengineyo. Pamoja na nia yake nzuri, wingi wa maagizo hayo na utekelezaji wake ZIRO, imepelekea kuwafanya watu wengi tu kutozichukulia kauli za Bwana Makonda kwa uzito.  Amekuwa akionekana kama mtu wa kukurupuka na maagizo mapya kila kukicha ilhali yale aliyoyatoa awali bado yanasuasua.

Ndio maana sishangazwi na mapokeo hasi kwa tangazo lake la vita dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya. Mapokeo hayo hasi yamechangiwa zaidi wa uzeofu wa matamko yake mengine huko nyuma.

Hata hivyo, kwa mtizamo wangu, tamko la RC Makonda safari hii, hili la kutangaza vita dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya, lina dhamira na umakini. Ninajipa matumaini hayo kwa sababu katika historia ya vita dhidi ya madawa ya kulevya, feki na za dhati, hakuna mwanasiasa aliyefikia hatua ya kuwataja bayana baadhi ya wahusika.

Sawa, kuna wanaosema "ah sasa kuwataja hao 'vidagaa' inasaidia nini ilhali mzizi wa tatizo ni mapapa?" Naelewa hoja yao lakini ukweli ni kwamba tatizo sio kuanza na vidagaa au mapapa bali tatizo ni dhamira ya dhati ya kupambana dhidi ya biashara hiyo haramu. Tunaelewa kuwa penye nia pana njia. Penye nia ya kufika mahali flani haijalishi kama barabara ni ya lami au isiyo na lami au ni kupita porini.

Sasa je Bwana Makonda ana nia ya dhati? Mie kama nilivyoeleza hisia zangu hapo juu, ninahisi kuwa ana dhamira thabiti. Na sababu kubwa ni hiyo ya kudiriki kuwataja akina 'Madam' na wenzake.

Kuna wanaosema "ah sasa kuwataja hao kina Madam na kuwaita ofisini kwake, kisha si itaishia kuwa stori tu?" Kuna wengine wanaomkosea heshima Bwana Makonda na kudai kuwa tangazo lake hilo ni la "kujiweka karibu na 'Madam'" Tatizo ni kwamba baadhi ya watu wameshamgeuza Bwana Makonda kuwa 'punching bag' lao. Akifanya zuri watamkemea, akifanya baya ndio zaidi. Hata hivyo, pengine ule utitiri wa maagizo yake umechangia hali hiyo, japo ni vema kumhukumu on case-to-case basis.

Alichokifanya Bwana Makonda jana ni kuiweka rehani roho yake kwa ajili ya maisha ya ndugu zetu wanaoteketea kwa unga. Na hiyo "kuweka rehani roho" sio maneno yangu tu, hata yeye mwenyewe ametanabaisha hilo. Kadhalika, katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge, Rais Dkt John Magufuli alieleza kuhusu aina ya watu wanaojihusisha na biashara hiyo hatari. Wana uwezo mkubwa, na wanaweza kufanya lolote.

Hebu pata picha: mtu ambaye kutokana na unga ana uwezo wa kubadili magari ya kifahari kadri anavyojiskia, anaporomosha majumba kila anapojiskia, anapangisha mabangaluu kwa rundo la michepuko yake, na ana fedha ya kumnyanyasa kila mtu. Huyu mtu hawezi kukubali kirahisi kubadilishiwa maisha ya aina hiyo. Na sio kwamba ni dhambi kuishi ki-anasa kiasi hicho lakini kinachomwezesha kuishi ki-anasa kiasi hicho ni biashara ya madawa ya kulevya. Na amin nakuambia, watu hawa sio tu hawako tayari kupoteza anasa hizo bali wapo tayari kupambana kufa na kupona kuzilinda, kwa gharama yoyote ile. Na hilo ndio linafanya kila anayejipa uthubutu kupambana na wahusika wa biashara hiyo anakuwa amejitoa mhanga, anatembea na roho yake mkononi.

Kuna wanaomkebehi Bwana Makonda kuwa amekurupuka na suala hilo ili 'kuua soo' la matokeo mabaya ya kidato cha nne katika mkoa wa Dar es Salaam. Hoja hiyo haina mashiko, kwa sababu Bwana Makonda angeweza aidha kukaa kimya tu, au akarusha lawama kwa wakuu wa wilaya za mkoa huo, au ma-DAS au walimu wakuu. Hivi kweli hatuijui Tanzania yetu kiasi hicho? Nani asiyejua kuwa habari ya matokeo ya kidato cha nne ilishasahaulika masaa machache tu baada ya kuwekwa hadharani? 

Lakini hata kama matokeo hayo mabovu ndio yangekuwa sababu ya Bwana Makonda kutoa tangazo hilo la vita dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya, kwa mtazamo wangu naona tatizo hilo la matokeo mabaya yakidato cha nne lipo zaidi katika ngazi ya kifamilia na kutapakaa hadi ngazi ya shule, na vitu vingine ambavyo labda sie tuliosoma shule za vijijini, bila umeme, bila maabara, bila chochote lakini tukapata division one ndio twaweza kueleza vizuri.

Kwahiyo, japo wanaodhani kuwa Bwana Makonda 'anafanya usanii' wanaweza kuwa sahihi - time will tell - mie ninabaki na imani kubwa kuwa Bwana Makonda amepata maono ya aina flani na kuwa mrithi wa marehemu Amina Chifupa, mwanasiasa pekee aliyejitolea mhanga kupambana kwa dhati dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya. Kama Bwana Makonda 'anatuzuga,' muda utatujulisha. Lakini pengine ni vema kumpa, kile Waingereza wanaita 'benefit of the doubt.'

Sasa lengo la makala hii sio kumpongeza tu RC Makonda bali kwenda mbali zaidi na kumuunga mkono kwa vitendo. Kwa kuanzia, iwapo una taarifa zozote za uhakika kuhusu biashara hiyo ya madawa ya kulevya, fanya kuwasiliana nami aidha kwa DM huko Twitter, au meseji huko Facebook au kwa baruapepe yangu iliyo salama kupindukia evarist@protonmail.ch  

Naamini kuwa ninaaminika kwa wengi wenu hasa kwa sababu nimekuwa miongoni mwa sauti adimu zinazopambana na ufisadi na uhalifu kama huo wa biashara ya madawa ya kulevya, na sina sababu ya kumsaliti mtu atakayenipatia taarifa za 'wauza unga.'

Nikishapatiwa taarifa hizo nitaziwasilisha kwa Bwana Makonda lakini bila kujumuisha jina la mtoa taarifa. Ukiniamini nifikishie taarifa, usiponiamini kaa nazo ila tutambue kuwa unga unawamaliza ndugu zetu. Na hata kama hujawahi kuridhishwa na maagizo ya Bwana Makonda, fanya kumpa 'benefit of the doubt,' tuungane sote kupambana na janga hili.

Sie ni wepesi sana wa kulaumu. Na katika hili la biashara ya madawa ya kulevya, sie kama jamii hatuwezi kukwepa lawama. Ni wangapi miongoni mwa mnaomdhihaki RC Makonda mlikuwa mnawajua 'mateja' na 'mapusha' aliowataja lakini mkakaa kimya? Au ni wangapi ambao kamwe hamjawahi kufungua vinywa vyenu au kutumia vidole vyenu kukemea kuhusu janga la madawa ya kulevya? Tuache unafiki. Angalau RC Makonda amemudu kufanya kitu ambacho mamilioni ya Watanzania hawakifanyi, sio kwa vile hawawezi bali UNAFIKI.

Ni nani anayewalinda wauza unga huko mtaani kama sio ndugu, jamaa na marafiki wa hao wauza unga? Ni wangapi wanawachukia kwa dhati wauaji hao kiasi cha kuwakwepa na kutotaka ukaribu nao? Ni nani anayewaenzi wahalifu hao kwa cheo cha "wazungu wa unga" kama sio miongoni mwa wanafiki ambao leo wanamnyooshea kidole Bwana Makonda?

Nimalizie makala hii kwa kumpongeza kwa dhati RC Makonda, huku nikiahidi full support kwake, hususan kwa kuhamasisha uwasilishaji wa majina ya wahusika. Kwa pamoja tukiungana kama jamii basi lazima tutashinda kwa sababu genge hilo la wauaji ni dogo tu linalopata usalama katika unafiki wa baadhi ya wenzetu.

TANZANIA BILA MADAWA YA KULEVYA INAWEZEKANA


1 comment:

  1. Hakika nimesoma makala hii. Imeniongezea madini mengi kichwani. Mungu akubariki.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Philemon Chahali 2006-2014

JUMUIKA NAMI TUMBLR

  Sehemu Ninahifadhi Nyaraka Zangu!

Powered by Blogger.

NUNUA KITABU HIKI

NUNUA NAKALA YA KIELEKTRONIKI (EBOOK)

Download "Chahali Blog ANDROID App"

UNGANA NAMI FACEBOOK

Instagram