25 Mar 2017


Kuna wanaotusimanga tuliompigia kampeni Rais John Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015. Kwamba sie ndo tumemleta Magufuli. Kwamba bila sie kumnadi, Tanzania isingeshuhudia kipindi hiki cha 'maajabu' ambapo kwa mara ya kwanza tumeshuhudia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam'anayebebwa na Magufuli' akiwa na uhuru wa kuvunja sheria, na yeyote atakayemkemea atakuwa amenunua ugomvi na Magufuli.

Wanaotusimanga wanasahau kitu kimoja. Laiti Upinzani ungekuwa na mgombea imara katika uchaguzi mkuu uliopita, kazi ya kuiangusha CCM ilikuwa rahisi kuliko wakati mwingine wowote ule.

Nakumbuka kada mmoja mwandamizi wa CCM alinieleza wakati wa kampeni kuwa "laiti Wapinzani walivyoungana na kumsimamisha mtu asiye na rekodi yenye mawaa, kwa mfano Dokta Slaa hivi, basi uchaguzi huu ungekuwa mgumu sana kwetu." Alieleza kuwa UKAWA uliirahisishia CCM kampeni ya kumnadi mgombea wake kwa vile, pamoja na sababu nyingine, mgombea wa UKAWA -Lowassa- alikuwa akijulikana vizuri mno huko CCM, kitu kilichowarahisishia kumshinda 'kirahisi.'

Kwahiyo, kabla ya kuachana na suala la lawama hizo, niseme hivi: sie tuliomnadi Magufuli hatukujua kuwa angekuja kubadilika kiasi hiki, lakini laiti Upinzani ungesimamisha mgombea bora, sie wengine wala tusingekimbia, tungefanya kampeni kama mwaka 2010, na kwa vile kwa kiasi kikubwa Upinzani auliamia kuweka kando tofauti zao, basi uwezekano wa kuiangusha CCM ulikuwa mkubwa. Ila hayo yameshapita sasa, tugange yaliyopo na yajayo.

Na yaliyopo tunayaganga vipi? Ni kwamba wakati tunaendelea kukuna vichwa kufahamu kitu gani kilichomsibu Rais Magufuli, aliyeingia kwa kishindo kikubwa sio Tanzania tu bali kimataifa pia, na hadi kutawala dunia na alama ya reli #WhatWouldMagufuliDo hadi kufikia hatua aliyofikia sasa ya kutawala kwa vitisho, jazba, ubabe na kutetea waziwazi uvunjifu wa sheria uliofanywa na RC Makonda, ni vema basi tujipange imara kuzuwia jitihada zozote za kiongozi huyu kuwa wa kutumia mabavu tu.

Kuna mwanafalsafa mmoja aliusia huko nyuma kuwa "ili maovu yashamiri, yahitaji tu watu wema kutofanya lolote." Wenye uwezo wa kupiga sauti dhidi ya maovu tukikaa kimya, labda kwa vile tu tuliwahi kumpigia kampeni Magufuli, au kwa vile "yatapita tu," kuna kila dalili kuwa tunakoelekea sio kuzuri.

Moja ya mambo yanayotatiza sana kuhusu Rais Magufuli ni kile kinachoonekana kama kupenda ugomvi usio wa muhimu. Hilo nimelieleza kwa kirefu katika makala ninayoiambatanisha hapo chini ambayo ilipaswa kuchapishwa na gazeti la Raia Mwema toleo la wiki hii lakini ninahisi haikuchapishwa (njia pekee ya mie kufahamu imechapishwa au la ni kuona makala husika kwenye tovuti ya gazeti hilo, na wiki hii haipo).

Kati ya nilipoandika makala hiyo na leo, kuna matukio makubwa manne yaliyojitokeza. Kwanza ni Waziri wa Habari (na masuala mengine)  Bwana Nape Nnauye kusimamia vema wajibu wake kama waziri husika, kufuatilia uvamizi uliofanywa na RC Makonda kwenye kituo cha redio na televisheni cha Clouds. Nape alipokea ripoti ya Tume aliyounda, na licha ya msimamo wa Magufulikujulikana mapema kuwa "anambeba Makonda," Nape alionyesha ujasiri na kuiweka hadharani ripoti hiyo ambayo awali baadhi yetu tulidhani ingekuwa 'changa la macho.'

Tukio la pili ni uamuzi wa Rais Magufuli kumfukuza kazi Nape kwa kufanya mabadiliko kwenye kabineti yake, na nafasi ya Nape kukabidhiwa Dkt Harrison Mwakyembe, ambaye majuzi tu 'alilikoroga' kwa kupiga marufuku kufunga ndoa bila cheti cha kuzaliwa. Amri hiyo ya kizembe ilitenguliwa na Magufuli siku chache baadaye.

Tukio la tatu ni mkutano wa Nape na waandishi wa habari, ambao tukiweka kando aliyoyasema mwanasiasa huyo, kubwa zaidi lilikuwa kitendo cha afisa mmoja wa usalama (haijulikani kwa hakika kama alikuwa polisi au taasisi nyingine ya dola) kumtolea bastola Nape hadharani. Tukio hilo la kutisha, na lile na Makonda kuvamia Clouds, yatabaki kuwa historia isiyopendeza kwa taifa letu kwani hayajawahi kutokea...labda zama za ukoloni.

Tukio la nne ni 'mafuriko' ya maneno yasiyopendeza kutoka kwa Rais Magufuli katika hotuba yake aliyoitoa jana wakati anawaapisha Mwakyemba na Profesa Kabudi, aliyerithi nafasi ya Mwakyembe. 

Sitaki kurudia vitisho alivyotoa Rais Magufuli lakini nachoweza kutahadharisha ni kuwa tunakoelekea sio kuzuri. Unapoona Rais anakerwa kwa vile habari zinazomhusu hazijapewa kipaumbele kwenye vyombo vya habari vingi, basi ujue tuna tatizo kubwa. Unapoona Rais anaamini kuwa habari za maandamano ya wafugaji na wakulima kuhusu migogoro ya ardhi ni "habari mbaya mbaya" basi ni wazi huyu si yule tuliyedhani ni tetezi wa wanyonge.

Tulipasw akuona dalili hizo mapema, kupitia baadhi ya kauli zake kama "I wish I could be Jaji Mkuu" na "I wish I could be IGP." Ukiona Rais anatamani madaraka zaidi ya aliyonayo, hiyo ni hali ya hatari.

Nihitimishe makala hii kwa kumshauri Rais Magufuli asikilize ushauri anaopewa na "wataalamu kuhusu hali ilivyo huko mtaani." Kadhalika, ninamsihi Rais wangu apunguze jazba. Hazitamfikisha popote. Aache kasumba ya kutafuta 'mabifu' yasiyo na msingi. Lakini jingine ni ukweli kwamba hatoweza 'kumbeba Makonda' milele, na kuendelea kumkumbatia kijana huyo kunaweza kumgharimu yeye Magufuli binafsi. 

SOMA MAKALA ILIYOPASWA KUTOKA KATIKA RAIA MWEMA TOLEO LA WIKI HII (JUMATANO 23/03/2017) LAKINI HAIKUTOKA (KWA SABABU WANAZOJUA WAMILIKI WA GAZETI HILO)


MAKALA YA RAIA MWEMA TOLEO LA MACHI 22, 2017

Disemba 31 mwaka juzi, siku ya mkesha wa ‘mwaka mpya 2016, nilichapisha kitabu cha kielektroniki kilichobeba jina “Dokta John Magufuli: Safari ya Urais, Mafanikio na Changamoto Katika Urais Wake.”

Pamoja na watu wengi waliokisoma kitabu hicho kukipongeza, wapo pia walionikosoa, hoja yao kuu ikiwa “ni mapema mno kutathmini Urais wa Magufuli katika muda huu mfupi aliokaa madarakani.”
Kwa wakati huo, sikuafikiana na ukosoaji huo, hasa kwa vile tathmini ya uongozi ni kama maadhimisho ya siku ya kuzaliwa: yanaweza kufanywa siku 40 baada ya kuzaliwa, kila mwezi, na kila mwaka kama wote tunavyofanya.

Kwahiyo, sikuona tatizo katika kufanya tathmini ya urais wa Dokta Magufuli, hasa ikizingatiwa kuwa aliingia na “kasi ya kutisha.” Kati ya siku aliyopishwa, Novemba 5, 2015 hadi nilipochapisha kitabu hicho – takriban miezi miwili hivi – Rais Magufuli alimudu kukonga nyoyo, sio za Watanzania tu, bali dunia nzima kwa ujumla kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya uzembe, rushwa, ufisadi, sambamba na ari yake kubwa ya kubana matumizi.

Naamini sote tunakumbuka alama ya reli (hashtag) ‘iliyotikisa’ dunia nzima ya #WhatWouldMagufuliDo ambayo watumiaji mbalimbali wa mtandao wa kijamii wa Twitter katika kila kona ya dunia walijaribu kuonyesha jinsi gani Dokta Magufuli alivyo bora zaidi ya viongozi wengine duniani.

Lakini sababu nyingine ya kuandika kitabu hicho ilikuwa ushiriki wangu binafsi kwenye kampeni za kumnadi Dokta Magufuli kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Pamoja na sababu nyingine, niliamua kumnadi kutokana na sababu zangu binafsi dhidi ya mpinzani wake mkuu.

Na haikuwa kazi rahisi kumnadi mwanasiasa huyu, kwa sababu baadhi ya watu walishindwa kabisa kunielewa, huku wengine wakihoji “kwanini unaweza kutusaliti wapinzani na kumpigia debe mgombea wa chama tawala, ambacho wewe binafsi ni mhanga wa unyanyasaji unaofanywa na serikali yake dhidi ya wanaoikosoa?” Na kilichoambatana na kauli hizo ni matusi mazito, udhalilishaji usiomithilika, na mengineyo yasiyostahili kukumbukwa.

Takriban miaka miwili baadaye, nimeshikwa na bumbuwazi baada ya kumsikia Rais Magufuli “akimkingia kifua” Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambaye majuzi ameandika historia ya matukio ya kisiasa nchini Tanzania kwa kuvamia ofisi za kituo cha habari cha Clouds, akiambatana na askari wenye silaha nzito.

Niweke rekodi sahihi. Awali nilimtetea RC Makonda katika nilichoamini kuwa ni jitihada zake dhidi ya biashara haramu ya madawa ya kulevya. Niliamini kuwa suala la ‘utata wa elimu yake’ ni sehemu tu ya mikakati za kumwondoa kwenye ajenda hiyo muhimu.

Hata hivyo, baada ya mawasiliano na “wenye uelewa wa yanayojiri nyuma ya pazia la siasa za Tanzania,” nilithibitishiwa kuwa tuhuma dhidi ya kiongozi huyo zina ukweli, na nikaelezwa kuwa “hata Dokta Magufuli anafahamu hilo.” Na kimsingi, awali nilipanga makala hii iwe ya ushauri kwa Rais kuchukua hatua stahili dhidi ya mteuliwa wake huyo “ili kuwatendea haki wanaomshauri.”

Lakini kabla sijawasilisha makala hiyo, ambayo ililenga zaidi kwenye kusisitiza haja kwa viongozi wetu kuzingatia ushauri wa kitaalamu badala ya kuendekeza ajenda binafsi, kukajitokeza tukio la RC Makonda kuvamia huko Clouds.

Nitumie fursa hii kuupongeza uongozi wa kampuni ya Clouds, hususan Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga, kuwa kufanya kile kilichotamaniwa na Watanzania wengi waliokuwa wakisubiri tamko la kampuni hiyo kuhusu tukio hilo la uvamizi wa Makonda, kwamba wasimamie ukweli.

Na kwa hakika, Ruge na Kusaga hawakuwaangusha watumishi wenzao wa Clouds na Watanzania kwa ujumla, wakaeleza “A hadi Z” ya kilichotokea wakati wa uvamizi huo ambao, kwa kumbukum bu zangu, ni wa kwanza kabisa kutokea nchini mwetu.

Ingeweza kuwa rahisi tu kwa viongozi hao wa Clouds “kuweka mbele maslahi yao binafsi” na kubadili maelezo, hasa ikizingatiwa kuwa lolote ambalo wangesema lingeweza kuaminika, lakini wakaamua kuhatarisha uhusiano wao na Makonda pamoja na shabiki mkubwa wa kituo hicho, yaani Rais Magufuli mwenyewe.

Akiongea kwenye uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa barabara za juu, pamoja na mambo mengine Rais Magufuli aliwaomba Watanzania kujielekeza kwenye vitu vya maendeleo badala ya kujielekeza zaidi kwenye udaku. Ikumbukwe kuwa siku chache tu zilizopita, Rais alipiga simu kwenye kituo cha televisheni cha Clouds na kueleza kuwa yeye pia ni shabiki wa kipindi cha Shilawadu, ambacho ni cha “udaku” huo huo anaokemea Rais.

Suala hapa sio tu “kama ni sahihi kwa Rais kuwa shabiki wa kipindi cha udaku, basi isiwe dhambi kwa wananchi kupenda udaku” bali “kitendo cha Makonda kuvamia Clouds sio kujielekeza kwenye maendeleo.”

Dokta Magufuli alikumbusha pia kuwa “kampeni zimekwisha, ulie lakini Rais ni Magufuli, mimi kwangu hapa ni kazi tu, maendeleo.” Hivi kweli Rais anaamini kelele za kutaka Makonda achukuliwe hatua kutokana na uvamizi huko Clouds ni mwendelezo wa kampeni? Au ni “kelele za wasiojua kuwa Rais ni Magufuli”? Na sitaki kabisa kuamini kuwa Rais anaamini kitendo cha uvamizi wa Makonda huko Clouds ni sehemu ya “hapa ni kazi tu.”

Kilichonisikitisha zaidi ni kauli ya Dokta Magufuli kwamba “mnahangaika na viposti vyenu mara hili mara lile, mpaka wengine wanaingilia uhuru wangu kwamba nifanye hivi, ukiniingilia ndio unapoteza kabisa.”

Kwangu binafsi, nimeoiona kauli hiyo ya Rais kuwa kama dhihaka dhidi ya baadhi yetu tulioshiriki kikamilifu kumpigia kampeni mwaka 2015 kwa kutumia “viposti” hivyo hivyo anavyovidharau. Na sio sahihi kwa Rais kudai tunamwingililia uhuru wake. Yeye ni mtumishi wetu, na tuna haki ya kumweleza matakwa yetu. Huko sio kumwingilia uhuru wake bali kudai stahili yetu kutoka kwake.

Rais alitukumbusha pia kuwa yeye hapangiwi mambo, anajiamini, na ndio maana siku ya kuchukua fomu alikwenda peke yake. Kumtaka amwajibishe mteule wake aliyevamia kituo cha habari sio kumpangia mambo bali kumkumbusha wajibu wake kama kiongozi. Na kupangiwa mambo kama “mwajiriwa wa Watanzania” sio kosa, isipokuwa tu pale “kumpangia mambo” huko kunalenga kuidhuru nchi yetu.

Sawa, Dokta Magufuli alikwenda peke yake kuchukua fomu za kuwania urais, lakini hakufanya kampeni peke yake. Na kwenda kwake pepe yake kuchukua fomu hakumpi ruhusa ya kutuongoza peke yake, bali kwa ushirikiano kati yetu waongozwa na yeye kiongozi. Hivi, sio Dokta Magufuli huyuhuyu ambaye kila mara anatusihi tumwombee, lakini leo anatuona tunamwingilia?

Kadhalika, Rais alimuunga mkono RC Makonda kwa kumwambia kuwa yeye (Rais) ndio anayepanga nani akae wapi na afanye nini…kwahiyo RC Paul Makonda achape kazi. Hivi Rais amesahau kuwa sio yeye kama Magufuli bali taasisi ya Urais ndiyo inayompa nguvu kufanya maamuzi kwa maslahi ya Watanzania wote?

Na je Dokta Magufuli anataka kutuaminisha kuwa ameridhia kitendo cha Makonda kuvamia kituo cha habari akiwa na askari wenye silaha, kiasi cha kumtaka Mkuu huyo wa mkoa “aendelee tu kuchapa kazi”? Je hiyo haitompa jeuri Makonda, na hata wengineo, kufanya “abuse of power” kwa vile “Rais kuruhusu”?

Nimalizie makala hii kwa ushauri huu kwa Dokta Magufuli: kwanza, hakuna tija katika kusaka ugomvi usio na umuhimu (picking up cheap fights). Uamuzi wa kuzuwia kurushwa matangazo ya bunge mubashara, kuzuwia mikutano ya vyama vya siasa vya upinzani, kuwaambia wahanga wa tetemeko Kagera kuwa “serikali haikuleta tetemeko hilo” na “kila mtu abebe msalaba wake mwenyewe”, kuwaambia wananchi wanaolalamikia njaa kuwa “wewe Rais huwezi kuwapikia,” nk sio tu ni “kusaka ugomvi usio wa lazima” lakini haziendani na matarajio ya Watanzania kwako Rais wetu.

Vilevile ninaomba sana kumshauri Rais kuzingatia ushauri wa kitaalamu anaopatiwa na wasaidizi wake. Ni vigumu kufafanua katika hili, lakini ninaamini “nimeeleweka.” Taifa litakuwa katika hali mbaya itapofika mahala “washauri watakapotumia njia mbadala kukufikishia ujumbe.” Na ndicho kinachotokea kuhusu “viposti.”

Mwisho, siku zote Rais wetu umekuwa ukimtanguliza Mungu katika hotuba zako mbalimbali na kuwasihi Watanzania wakuombee. Wewe ni Mkristo, na hii ni Kwaresma. Ni kipindi cha maungamo, kusamehe waliotukosea, kuangalia tulikotoka, tulipo na tuendako. Penye Mungu pana upendo, na penye upendo pana haki. Japo hupangiwi cha kufanya, naomba kukushauri uwapatie haki Watanzania kwa kumwajibisha RC Makonda kwa kuvunja haki za Clouds kutokana na uvamizi aliofanya.
Mungu Ibariki Tanzania


Baruapepe: [email protected] Tovuti: www.chahali.com Twitter: @cha



1 comment:

  1. Uchaguzi haukua wa huru na haki nadhan unakumbuka mengi kuhusu kukamatwa kura masanduku yaliyokwishapigiwa kura matokeo idadi ya watu wachache kura nyng

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.