21 Mar 2017



Baada ya tukio la Mkuu wa Mkoa Paul Makonda kuvamia ofisi za Kampuni ya Clouds jijini Dar, Ijumaa usiku, na kuahidiwa na uongozi wa Kampuni hiyo kuwa ungetoa taarifa rasmi jana, watu wengi - ikiwa ni pamoja nami- walihisi kuwa "sio rahisi kwa Clouds kumtosa Makonda, kwa vile ni mshkaji wao."

Sie hapa Uingereza tupo masaa matatu nyuma ya masaa ya Tanzania (japo Jumapili ijayo masaa yatabadilika), na jana nilipoamka, tayari uongozi wa Clouds chini ya Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga ulikuwa umeshatoa taarifa kuhusu kilichojiri Ijumaa iliyopita kuhusu Makonda.

Awali, nilitaka kupuuzia kufuatilia habari hiyo nikihofia "kuharibu siku yangu kwa kuianza na habari mbaya" nikidhani kuwa Ruge na Kusaga "wamemsafisha Makonda."

Hata hivyo, baada ya kutupia macho tweets za Millard Ayo aliyerusha press conference ya uongozi wa Clouds mubashara, nilibaini kuwa Ruge, Kusaga na Clouds kwa ujumla wamefanya kile ambacho kimekuwa kigumu mno kufanywa na Watanzania wengi: kuwa wakweli. Kuwa tayari kupoteza rafiki kuliko kupoteza ukweli.

Kwa wengi hilo linaweza kuwa suala dogo lakini kwa hakika lina umuhimu wa kipekee. Sote twafahamu ukaribu wa Makonda na Clouds, na hata Ruge amekiri kuwa yeye binafsi ni rafiki na Mkuu huyo wa Mkoa.

Kwahiyo, kama ilivyotarajiwa na wengi, ingekuwa rahisi zaidi kwa Clouds "kumbemba Makonda" (kama alivyobebwa na Rais Magufuli) na pengine "stori ingeishia hapo" kuliko kuamua kusimamia kwenye haki na ukweli.

Jana niliwapa angalizo ndugu zangu wa Clouds kuhusu "kukubali kutumika." Nili-tweet hivi


Lakini japo ni rahisi kulaumu kuliko kujihangaisha kujua kwanini flani kafanya kitu tunachomlaumu kukifanya, mazingira ya media zetu yanalazilazimisha kutumika. Kwahiyo, wakati ni rahisi kuwalaumu Clouds "wanapotumika" kuinadi CCM na serikali yake, ni muhimu twenda mbali na kufahamu kwanini wanafanya hivyo.

Ni kwamba, kwa kiasi kikubwa, uhuru wa habari Tanzania bado ni fadhila kutoka kwa watawala. Kwa kiasi kikubwa, chanzo kikuu cha mapato ya vyombo vya habari ni matangazo kutoka serikalini. Kwahiyo, chombo cha habari "kitakachoiudhi serikali" kinaweza kujikuta kinanyimwa matangazo. Hiyo inalazimisha "urafiki" kati ya vyombo hivyo na serikali.

Lakini licha ya matangazo, vyombo vyetu vya habari vinafanya kazi katika mazingira kandamizi, na kwa ridhaa ya watawala badala ya kanuni stahili. Ndio maana, kama tulivyoshuhudia jana, Waziri Nape anapigania "sheria" huku Bosi wake Magufuli anakumbatia ridhaa yake kama mtawala.

Kingine kinachohusiana na tukio hilo ni ukweli kwamba Rais wetu Dokta John Magufuli anaelewa kasoro za wasifu wa elimu ya Makonda...kwa sababu alishajulishwa ukweli huo na "wahusika." Laiti angefanyia kazi ushauri aliopewa, tusingefika hapa. 

Kuna tatizo pia katika jinsi Rais wetu alivyojitahidi kutuonyesha kuwa ni rafiki wa Clouds, na ameshapiga simu mara kadhaa na kurushwa hewani, 

na kusifiwa na watu kibao kuwa "ni mtu wa watu" lakini swahiba wake, Paul Makonda, alipovunja sheria kwa kuvamia ofisi za Clouds, akapuuza "urafiki wake na Clouds" na "kumbeba swahiba wake Makonda." 
Kasoro nyingine ni kudai kuwa yeye Rais anapenda kipindi cha "udaku" cha Shilawadu cha Clouds lakini jana anatuchamba kuwa "Watanzania tunaendekeza udaku." Je ni Rais pekee anayestahili kupenda udaku, lakini ni jinai kwa raia wa kawaida?


Nimalizie makala hii kwa kumshauri Rais Magufuli aache kupenda ugomvi usio na maana, Waingereza wanaita "cheap fights." Alizuwia "matangazo ya bunge mubashara," na majuzi kajisifu kwa hatua hiyo; lilipotokea tetemeko Kagera, akakaa muda mrefu bila kwenda kuwapa pole wahanga, na alipokwenda akawasemea ovyo, eti "yeye hakuleta tetemeko hilo" na "hakuna serikali duniani inayosaidia wahanga wa tetemeko" (kitu ambacho sio kweli).


Kana kwamba hayo hayakutosha kutibua watu, alipokuwa ziarani mikoani, wananchi walisikika wakimwambia "njaa baba!" akawasemea ovyo "njaa mnataka mie niingie jikoni kuwapikia?" Na jana, amejigamba kuwa anajiamini, ndio maana alikwenda kuchukua fomu ya kuwania urais peke yake. Anajifanya kusahau kuwa hakujipigia kampeni peke yake, na kuna tuliotukanwa mtandaoni tukihangaika kumpigia kampeni.

Nilishaandika kwenye jarida la Raia Mwema kumsihi Rais Magufuli azingatie umuhimu wa kutumia lugha ya kidiplomasia badala ya kuendekeza ukali usio na maana, hasa katika mazingira kama ya jana ambapo hakupaswa kumlinda Makonda kwa uhuni aliofanya huko Clouds. Kusema "hapa ni kazi tu" kwa minajili ya kumlinda Makonda kinatufanya tuliosapoti kauli mbiu hiyo ya "hapa ni kazi tu" kujiskia kichefuchefu. Yaani "hapa ni kazi tu" kwa Mkuu wa Mkoa kuvamia kituo cha habari akiwa na askari wenye silaha?


Lakini kosa kubwa alilofanya Magufuli jana sio kumtetea Makonda bali kutupa jawabu la wazi kuwa jeuri ya Makonda inatoka kwa bsoi wake, yaani Magufuli. Kwanini Magufuli anamlinda Makonda kiasi hicho? Baadhi yetu twaelewa lakini huu sio muda mwafaka kuyaongelea hayo. Ila tu Rais wetu afahamu kuwa sapoti ya baadhi ya watu kwake ina ukomo, itafika mahala "akimwaga mboga, watamwaga ugali." I hope hatutofika huko. I hope Rais wetu atatumia busara, kufanyia kazi mapungufu yake eg kuwabwatukia watu ovyo huku anawalea watu kama Makonda, na kuepuka kusaka ugomvi usio na maana.

Historia ina mafundisho mengi kuhusu viongozi walioendekeza jeuri, kiburi, ubabe, dharau na kujiona majabali, na hatma yao haikuwa nzuri.

Waingereza wanasema WRONG IS JUST THAT, WRONG (Kitu kisicho sahihi kiko hivyo tu, hakiko sahihi). Alichofanya Makonda was wrong. Utetezi wa Rais Magufuli kwa Makonda was wrong too. Huo ni ukweli hata kama utamchukiza Mheshimiwa Rais.





1 comment:

  1. Makala nzuri ndugu Chahali...let's hope kuwa Le Prezidaa ataanza kutega masikio na kusikiliza mawazo tofauti

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.