20 Apr 2017


NIANZE makala hii kwa kutoa salamu za rambirambi kwa familia za askari wanane wa Jeshi la Polisi waliouawa kinyama wiki iliyopita, wilayani Kibiti, mkoani Pwani.
Huu ni msiba wa kitaifa, japo hakuna maombolezo ya kitaifa – sijui kwa vile hatuthamini uhai wa Watanzania wenzetu au tumekwishazoea sana vifo kama vile vya ajali.
Katika moja ya vitu nilivyojifunza katika miaka yangu kadhaa ya kuishi hapa Uingereza ni jinsi wenzetu wanavyothamini uhai. Laiti tukio hili la kuuawa polisi wanane huko Kibiti ndio lingekuwa limetokea hapa, basi huenda kila kitu kingesimama.
Na si hapa Uingereza pekee. Kwa hali ilivyo sasa katika baadhi ya mataifa ya Ulaya Magharibi sasa ni kama "tumekwishaanza kuzoea” matukio ya kigaidi, maana yanatuandama mno, hasa Ufaransa, Ubelgiji na Ujerumani, na majuzi hapa Uingereza.
Katika kila tukio, bila kujali idadi ya waathirika, takriban ndani ya saa moja tangu kutokea tukio husika, Rais au Waziri Mkuu wa nchi husika huongea na wananchi katika runinga mubashara, kutoa pole kwa waathirika, kuwahakikishia usalama wananchi, na kuwaonya wahusika kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao. Huu ndio uongozi.
Je, sisi hali ikoje? Sana sana ni taarifa ya salamu za rambirambi kutoka kwa Rais, matamko ya hapa na pale ya Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba, na kauli za vitisho za IGP Ernest Mangu – sio kwa “majambazi” bali “wananchi wanaochekelea vifo vya polisi hao waliouawa.”
Japo sio busara kwa mtu yeyote kufurahia kifo cha mtu mwingine – hata kama sio polisi – lakini hilo sio kosa la jinai. Kadhalika, ni vema nguvu ikaelekezwa kwenye tatizo halisi, ambalo Jeshi la Polisi chini ya uongozi wa IGP Mangu haliwezi kukwepa lawama, kwa sababu tishio la usalama mkoani Pwani limedumu kitambo sasa bila kupatiwa ufumbuzi, kuliko ‘tatizo la kufikirika’ (kuwa kuna watu wanafurahia vifo vya polisi hao)
Saa kadhaa baada ya kupatikana taarifa za mauaji hayo, Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani, alizungumza na waandishi wa habari, ambapo pamoja na mambo mengine alinukuliwa akisema kuwa jeshi hilo "halitokuwa na mzaha wala msamaha" katika operesheni maalumu kuhusiana na tukio hilo. Je, kulikuwa na mzaha na msamaha kabla ya tukio hilo, ambao sasa hautakuwepo wakati wa operesheni husika?
Tukiweka kando kasoro hizo, jambo moja lililonigusa mno ni kukosekana kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwenye tukio la kuaga miili ya polisi hao. Badala ya kujumuika na wafiwa, Rais alihudhuria hafla mbili (ambazo zingeweza kabisa kusogezwa mbele) za uzinduzi wa hosteli za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na makazi katika kitongoji cha Magomeni.
Sambamba na hilo, tukilinganisha na matukio makubwa mawili ya hivi karibuni – uvamizi uliofanywa na RC Makonda kwenye kituo cha Clouds na "kutekwa" kwa msanii wa bongofleva, Roma Mkatoliki – mauaji hayo ya polisi hao wanane yalipewa uzito mdogo na Watanzania wengi, angalau huko mtandaoni.
Hali hiyo inasikitisha lakini haishangazi. Sababu moja kuu ya "wananchi wengi kutoonekana kuguswa na mauaji hayo ya polisi wanane" ni ukweli kwamba uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi wengi sio mzuri. Polisi wetu kwa kiasi Fulani wamekuwa wakisifika kwa unyanyasaji dhidi ya raia wasio na hatia.
Na kama kuna kitengo cha polisi wetu "kinachochukiwa mno" ni hicho cha FFU (Kikosi cha Kuzuia Ghasia) ambacho askari hao wanane walikuwamo. Japo siungi mkono "chuki" hiyo, lakini naelewa jinsi gani Watanzania wengi wasivyopendezwa na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.
Kwa upande mwingine, jeshi hilo limekuwa likionekana kama "adui wa kudumu" dhidi ya vyama vya upinzani, huku likifanya upendeleo wa wazi kwa chama tawala CCM.
Kwa hiyo, wakati tunaomboleza vifo hivyo vya polisi hao wanane, ni muhimu mno kwa wahusika kuchukua hatua za makusudi kuondoa "uhusiano wa chuki na shaka" uliopo kati ya Jeshi la Polisi na asilimia kubwa ya Watanzania.
Kana kwamba uhusiano bora kati ya Jeshi la Polisi na wananchi sio muhimu ‘sana,’ moja ya nyenzo muhimu ya kujenga na kuimarisha ushirikiano huo, mpango wa Polisi Jamii, ulifutwa kwa sababu wanazozijua wahusika. Polisi jamii ilikuwa kiungo muhimu kati ya polisi wetu na jamii.
Kioperesheni, japo tukio hilo la mauaji ya polisi wanane linaelezwa kuwa ni la kijambazi, binafsi ninahisi kuwa kuna tatizo zaidi ya ujambazi. Na kwa tafsiri ninayoelewa kuhusu ugaidi, basi tukio hilo linastahili kabisa kuitwa la kigaidi. Ni majambazi gani wenye ujasiri wa kuwavizia polisi na kuwaua kwa namna hiyo ya uvamizi wa kushitukiza?
Halafu, hilo sio tukio la kwanza. Na hao polisi wanane sio polisi wa kwanza kuuawa katika eneo hilo, sambamba na wakazi wengine. Yayumkinika kuhitimisha kuwa Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani hawawezi kukwepa lawama, kwa kushindwa kukabili kushamiri kwa mauaji katika eneo hilo.
Sijui Rais Magufuli ameishiwa na zile sindano zake za kutumbulia majipu, au kaishiwa pumzi ya “TumbuaMajipu” lakini ni wazi kuna matatizo ya msingi katika uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kwa ujumla. Ukimya wa polisi katika uvamizi huko Clouds, na "kutekwa" kwa Roma, na sasa hili la Kibiti, vilipaswa kumfanya Rais Magufuli achukue hatua.
Moja ya sababu maarufu ya polisi wetu wanapozuia mikutano au maandamano ya vyama vya upinzani huwa "intelijensia." Sasa kama intelijensia ipo kwenye kudhibiti shughuli halali za vyama vya siasa, kwa nini intelijensia hiyo isitumike kwenye kukabiliana na "magaidi" hao wanaotikisa Mkoa wa Pwani?
Nihitimishe makala hii kwa kurejea salamu zangu za rambirambi kwa familia za askari hao waliouawa kinyama. Pamoja na upungufu wote nilioutanabaisha katika makala hii, hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha unyama waliofanyiwa askari hao.
Lakini pia wakati tunaomboleza vifo vyao, ni vema tukatafakari kama taifa kuhusu uhusiano kati ya Jeshi la Polisi (na vyombo vyote vya dola kwa ujumla) na raia, ambao ukiwa bora, unaweza kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na taifa kwa ujumla

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.