31 Oct 2017



Pasipo kutarajiwa, jana, Jumatatu ya Oktoba 30, 2017, anga za habari huko nyumbani Tanzania zilitawaliwa na habari moja nzito: mmoja wa wana-CCM maarufu, Mbunge kwa tiketi ya chama hicho tawala anayewakilisha jimbo la Singida Kaskazini, na Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Nne, Bwana Lazaro Nyalandu, alitangaza kujivua uanachama wa CCM na kuomba kujiunga na chama kikuu cha upinzani cha Chadema.


Tukio hilo lilileta mshangao mkubwa kwa sababu kadhaa. Kwanza, licha ya matamshi ya hivi karibuni ya Nyalandu kuhusu haja ya kurejeshwa mchakato wa Katiba mpya, sambamba na kuwasihi wabunge wenzie wa CCM kupinga kwa nguvu zote jaribio la kurefusha muda wa Rais madarakani, hakukuwa na dalili kubwa na za waziwazi iwapo kuna ‘kutofautiana’ kati ya Nyalandu na chama chake.


Na hata kama kungekuwa na dalili hizo – kwa kificho au wazi – bado wananchi wengi wangepokea habari hizo kwa mshtuko mkubwa.

Sababu ya pili ya mshangao kuhusu tukio hilo ni ukweli kwamba mwanasiasa wa chama tawala kuamua kujiunga na upinzani, tena miaka mitatu hivi kabla ya uchaguzi mkuu, ni suala ambalo licha ya kuhitaji ujasiri mkubwa pia linaacha maswali kadhaa ambayo pengine sio rahisi kuyapatia majibu.

Hadi wakati ninaandika uchambuzi huu, kilicho bayana kuhusu sababu za Nyalandu kuchukua uamuzi huo ni sababu alizotanabaisha mwenyewe katika tamko lake kwa umma.

Akizungumza jana, mwanasiasa huyo alidai sababu ya kuchukua uamuzi huo ni kutokuridhishwa na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa Watanzania na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi ya mihimili ya dola yaani Serikali, Bunge na Mahakama.

Lakini hata kabla ya kuchukua uamuzi huo jana, Nyalandu alishaonyesha dalili ya kutofautiana na wana-CCM wenzie, hasa kwa uamuzi wake wa kumtembelea Mbunge Tundu Lissu wa Chadema aliyelazwa huko Nairobi, Kenya kufuatia jaribio la kumuua. Hadi sasa, Nyalandu anabaki kuwa kiongozi wa ngazi za juu wa CCM kumtembelea Lissu huko Kenya.


Huku kukiwa na tetesi kwamba uongozi wa juu wa CCM umewapiga marufuku viongozi wake kujihusisha na suala la Lissu, uamuzi wa Nyalandu kwenye Kenya ‘kinyume na maagizo ya chama chake’ ulihisiwa kuwa ungemwingiza matatizoni.

Dalili nyingine kuwa mwanasiasa huyo hakuwa akipendezwa na baadhi ya mienendo ndani ya CCM ni pale alipoibuka kuhamasisha haja ya kuanzisha upya mchakato wa kupatikana Katiba mpya, sambamba na kuhamasisha wana-CCM wenzake dhidi ya jitihada za chini chini kuongeza muda wa Rais madarakani.

Masuala yote hayo mawili yalitarajiwa ‘kumsababishia matatizo’ mwanasiasa huyo.

Hata hivyo, kuna ‘sababu mbadala’ kuhusu uamuzi wa Nyalandu kujiuzulu. Kuna taarifa kwamba kuna uchunguzi unaofanyika dhidi ya mwanasiasa huyo kuhusiana na utumishi wake kama Waziri wa zamani wa Maliasi na Utalii. Taarifa hizo ambazo bado ni tetesi hadi muda huu, zinaweza kupewa uzito zaidi na ‘screenshot’ inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikidaiwa kuwa ni ya mazungumzo ya kundi la Whatsapp la viongozi wanawake wa CCM.

Katika ‘chat’ husika, mmoja wa makada wa kike wa CCM anadai kuwa kuna uchunguzi unaofanyika dhidi ya Nyalandu alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, na kwamba uamuzi wa kujiondoa CCM na kuomba kujiunga na Chadema una lengo la kugeuza suala hilo kuwa la kisiasa pindi akichukuliwa hatua.

Pengine swali muhimu linaloendelea kutawala vichwa ni “kwanini HASWA Nyalandu amejiuzulu?” Kuna sababu alizotoa yeye mwenyewe, ambazo kwa kiasi kikubwa zinaleta mantiki, lakini pia kuna hiyo tetesi kuwa amechukua uamuzi huo kama tahadhari pindi akianzishiwa tuhuma za ufisadi.

Tuchambue sababu zote mbili, yaani alizotoa mwenyewe na hizo tetesi. Kwa vile hatuna maelezo yenye uhakika yaliyo kinyume na sababu alizotoa Nyalandu, nadhani kwa kuzingatia busara tu, itakuwa sio sahihi kudhani anaongopa. Unapopinga kauli ya mtu basi shurti uwe na kauli mbadala yenye uthibitisho. Kwahiyo, angalau kwa muda huu, hakuna sababu za msingi za kupinga sababu alizotoa mwanasiasa huyo.

Kuhusu tetesi za kuwepo kwa mchakato wa ‘kumshughulikia kutokana na tuhuma za ufisadi,’ kuna mantiki kwa mbali, na utata kwa mbali pia. Sio siri kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii ilikuwa kama ‘makao makuu’ ya ufisadi. Wizara hiyo ilikuwa kama ile ya Nishati na Madini, ambapo mawaziri lukuki walihamishwa au kuondolewa madarakani kutokana na tuhuma za ufisadi.

Kwamba Nyalandu alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kulikuwa na tuhuma za ufisadi, hilo halina mjadala. Lakini kwa kuzingatia kanuni ya asili ya haki, tuhuma hizo zinabaki tuhuma tu mpaka zitakapothibitishwa.

Kwahiyo, hadi hapa, mantiki ya mbali kuhusu uwezekano wa uchunguzi wa tuhuma za ufisadi dhidi ya Nyalandu ipo. Hata hivyo, utata wa mbali ni kwamba katika mazingira ya kawaida tu, na tukijifanya kuamini (angalau kwa minajili ya uchambuzi huu) kwa Nyalandu anafahamu kuhusu uchunguzi huo, je isingekuwa mwafaka kwa yeye kupambana na suala hilo akiwa CCM kuliko nje ya chama hicho tawala?

Sawa, kuna hiyo hoja ya “amehama CCM na anataka kuhamia Chadema ili pindi akichukuliwa hatua, suala hilo lionekane la kisiasa,” lakini ikumbukwe kuwa suala la muhimu sio “suala lionekane la kisiasa” bali “lisitokee kabisa.” Na katika mazingira ya kawaida, huo uamuzi wa tu Nyalandu kuhama CCM na kuikosoa hadharani unatosha kuipa serikali ya chama hicho tawala na taasisi zake “hasira” dhidi ya mwanasiasa huyo. Na hapo hatujagusia uwezekano wa mwanasiasa huyo kujiunga na “adui nambari moja wa CCM” yaani Chadema.

Kwa mtazamo wangu, kama ni kweli kuna uchunguzi unaoendelea au unaotarajiwa kufanyika kuhusu Nyalandu basi yayumkinika kuhisi kwamba ingekuwa rahisi zaidi kwa yeye kupambana na suala hilo akiwa ndani ya CCM kuliko nje ya chama hicho chenye historia ya siasa za kinyongo, visasi na majitaka.

Lakini kuna ‘angle’ kubwa zaidi katika uamuzi huo wa Nyalandu. Yawezekana amesoma vema upepo wa kisiasa huko nyumbani chini ya utawala wa Rais Magufuli, na kubaini vitu kadhaa. Moja laweza kuwa kinachoonekana kama wananchi wengi kutoridhishwa na utawala wa Magufuli, ndani na nje ya CCM. Keyword hapa ni ‘kinachoonekana,’ nikimaanisha pengine ni hisia tu kuwa kuna wananchi wengi wasioridhishwa ilhali ukweli ni kinyume na hisia hiyo.

Kwa minajili ya uchambuzi huu, tufanye kuwa hisia hizo zipo kweli. Kwahiyo, kwa vile Nyalandu alikuwa miongoni mwa makada wa CCM walioomba ridhaa ya chama hicho kuwa wagombea wa urais mwaka 2015 lakini haukufanikiwa, basi pengine anataka kutupa kete yake kupitia upande wa upinzani.

Lakini sio tu kusukumwa na nia ya kuwania urais, lakini yayumkinika kuhisi kuwa mazingira yaliyopo muda huu yanampatia mwana-CCM yeyote nafasi nzuri ya kukikimbia chama hicho. Sio siri kuwa hisia kwamba Magufuli ana dalili za udikteta zinazidi kushika hatamu. Kwa maana hiyo, hata mtu mwenye sababu zake binafsi akikurupuka na kutamka “ninahama CCM kwa sababu utawala wa Magufuli ni wa kidikteta” ataeleweka kirahisi, na anaweza kuungwa mkono kirahisi pia.

Kwamba Nyalandu anaweza “kuruka kutoka kwenye ngalawa na kuingia majini kwenye bahari yenye papa na nyangumi” sio suala dogo. Kama kuikosoa CCM ukiwa ndani ya chama hicho ni hatari, sote twafahamu nini kinachoweza kumkumba anayediriki sio kukosoa tu bali pia kuhama chama hicho tawala. Kwa mantiki hiyo, kwa sababu yoyote ile – iwe hizo alizotaja mwenyewe au tetesi za uchunguzi wa ufisadi – mwanasiasa huyo amefanya maamuzi magumu, na yayumkinika kuamini kuwa amejiridhisha vya kutosha kabla ya kuchukua uamuzi huo.

Kuna mambo matatu yanayoweza kutoa mwangaza kidogo. Kwanza, hivi karibuni, Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Dokta Hamis Kigwangallah alinukuliwa akisema kwamba anayo orodha ya watu mashuhuri, viongozi wastaafu na wabunge wanaojihusisha na ujangili, na atahakikisha anawashughulikia.

Pili, jana katika hotuba yake akiwa huko Mwanza, Rais Magufuli alikumbushia kuhusu Mahakama Maalum ya Ufisadi, ambayo pasi kuuma maneno, imekuwa kama kichekesho kutokana na kukosa kesi. Rais kuitaja mahakama hiyo ‘isiyo na ufanisi angalau hadi sasa’ inaweza kumaanisha kilekile alichokigusia Waziri Kigwangallah kuhusu ujangili.

Na tatu, ‘vijana wa Lumumba’ (makada wa CCM kwenye mitandao ya kijamii) walishaanza kuzungumzia ‘ufisadi wa Nyalandu’ mara tu alipoenda Nairobi kumjulia hali Lissu. Na kasi yao ya mashambulizi dhidi ya Nyalandu imepamba moto zaidi jana baada ya mwanasiasa huyo kutangaza kujiondoa katika chama hicho tawala.

Lakini pia kuna tamko la Humprey Polepole, ‘katibu Mwenezi’ wa CCM kuhusu uamuzi huo wa Nyalandu. Binafsi nilitarajia tamko kali na pengine lililosheheni kebehi kama sio kashfa (na Polepole ni hodari sana kwenye maeneo hayo), lakini reaction ya msemaji huyo wa CCM imekuwa ‘muted.’ Sana sana ameishia kudai kuwa Nyalandu amejiondoa kwa sababu ameshindwa kuendana na kasi ya awamu ya tano. Pia amejaribu kuonyesha kuwa mwanasiasa huyo sio ‘mtu mkubwa’ ndani ya chama hicho tawala. Huyu si Polepole tunayemfahamu kwa umahiri wake wa ‘kusema ovyo.’ Huenda ‘upole’ wake una sababu flani.

Japo kauli ya Kigwangallah na ya Rais Magufuli, sambamba na ‘vijana wa Lumumba’ kumwandama Nyalandu, na ‘upole’ wa Polepole yanaweza kuwa mambo ya kawaida tu, lakini pia yanaweza kutoa mwangaza kuhusu uamuzi huo wa Nyalandu. Hata hivyo, kama nilivyotanabaisha awali, sidhani kama mazingira hayo yangetosha kumfanya Nyalandu kuchukua uamuzi huo mzito.

Kwamba Nyalandu ataandamwa baada ya kuchukua uamuzi huo, hilo halina mjadala. Kama asipoandamwa na ngazi za juu za CCM au kupitia taasisi za dola/umma basi ‘vijana wa Lumumba’ watakesha mitandaoni kumchafua. Pamoja na ukongwe wake katika siasa si Tanzania tu bali barani Afrika kwa ujumla, kwa kiasi kikubwa CCM inaendekeza mno siasa za kisasi, kinyongo na adui mkubwa wa ukweli. Kuikosoa CCM au serikali yake ni kama kusaini ruhusa ya kusumbuliwa kwa kila namna.



Na ni muhimu kutambua kuwa Nyalandu alikuwa akifahamu kuhusu ‘mabalaa’ yanayomsubiri baada ya kuchukua uamuzi huo mzito. Angalia yanayomsibu Yusuph Manji, mtu aliyemwaga mamilioni ya fedha kuifadhili CCM lakini amebaki kuwa ‘kielelezo cha hasira za CCM.’

Je CCM wakiamua kulipa kisasi kwa Nyalandu watafanikiwa? Inategemea sana busara za Magufuli. Yote yanayoelezwa kuwa ‘ufisadi wa Nyalandu’ yailikuwa na baraka za mtangulizi wa Magufuli, yaani Rais Kikwete. Kwahiyo, kama ambavyo jitihada zozote za kumbana Lowassa zilivyoshindikana kwa vile zingeishia kumchafua pia Kikwete, ndivyo jaribio la ‘kulipiza kisasi kwa Nyalandu’ linavyoweza kumtia matatani JK.


Licha ya kuelezwa kuwa Nyalandu alikuwa mmoja wa watu wa karibu wa JK, pia ni muhimu kutambua kuwa mmoja wa watu wake wa karibu ni mke wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa, Mama Anna. Mara baada ya kurejea Tanzania kutoka Marekani, Nyalandu alikuwa miongoni mwa washauri Mama Anna Mkapa, katika uendeshaji wa taasisi ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF).

Kwa maana hiyo, jaribio lolote la ‘kumwandama Nyalandu’ linaweza kuzua kile Waingereza wanaita ‘unintended consequences,’ au ‘matokeo yasiyokusudiwa kwa Kiswahili.

Pia ni muhimu kutambua u-kimataifa wa Nyalandu. Mwanasiasa huyo ana mahusiano mazuri na wanasiasa wenye nguvu kubwa hususan nchini Marekani. Japo ‘nguvu’ zao zinaweza kutofua dafu kwa Magufuli, lakini sote twafahamu kuwa ni vigumu kwa Tanzania yetu kuwa na ‘jeuri’ katika umasikini wetu.


Hatma ya Nyalandu akifanikiwa kuhamia Chadema ikoje? Binafsi, ninahisi mambo makuu mawili. Kwanza, ujio wake katika chama hicho kikuu cha upinzani unaweza kuamsha msisimko mpya wa siasa za ndani na nje ya chama hicho, na Tanzania kwa ujumla.

Kwa upande mmoja, anaweza kuendeleza hoja zake kama hiyo ya kudai kurejeshwa kwa mchakato wa Katiba mpya, suala ambalo Chadema na washirika wake wa UKAWA ni kama wamelitelekeza.

Lakini pengine kubwa zaidi ni uwezekano mkubwa wa Nyalandu kuwa mmoja wa wagombea wa Urais kwa tiketi ya Chadema katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020. Kwamba amejiondoa CCM kwa hiari yake (angalau kwa mujibu tunachofahamu hadi muda huu) na kujiunga na Chadema kwa hiari yake, anaweza kuwa na faida ya ziada kuliko majina mengine mawili yanayotajwa kuhusu urais mwaka 2020 kupitia Chadema, Mawaziri Wakuu wa zamani, Lowassa na Sumaye.


Kwamba Nyalandu ni ‘mwana-CCM pekee aliyemjali Lissu kwa kumtembelea huko Nairobi,’ na ukweli kuwa yeye na Lissu wanatoka mkoa mmoja, wanaweza kujenga ‘dream team’ inayoweza kuirejesha Chadema enzi za kina Dkt Slaa, Zitto na Mbowe.

Lakini pia katika mazingira yaliyopo sasa, Chadema imekuwa kama haina mpango wa kushiriki uchaguzi mkuu ujao. Maandalizi yanayopaswa kufanyika sasa – miezi 36 tu kabla ya uchaguzi huo – ni kama hayapo. Ndiyo, Magufuli kapiga marufuku shughuli za kisiasa, lakini ni lini Rais kutoka CCM aliwahi kuridhika shughuli za wapinzani?

Kwa maana hiyo, ujio wa Nyalandu unaweza kuamsha matumaini kwa chama hicho kikuu cha upinzani kuhusu nafasi yake katika uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo, kuna vikwazo vikuu viwili. Cha kwanza, ni lile lililojiri baada ya Lowassa kujiunga na CCM, Kwa minajili ya kumbukumbu tu, Chadema ilimwandama Lowassa kuwa ni ‘baba wa ufisadi’ kwa takriban miaka 9 mfululizo, kisha ghafla wakampokea na kumfanya mgombea wao wa Urais katika uchaguzi mkuu uliopita. Kwa busara za kawaida tu, huwezi kumchafua mtu kwa muda wote huo kisha ukategemea kumsafisha ndani ya miezi mitatu. Japo makada wa chama hicho hawataafiki, athari za kumpokea Lowassa na kumfanya mgombea wao zinaendelea kukisumbua chama hicho.

Kama ilivyokuwa kwa Lowassa, baadhi ya viongozi wa Chadema walishawahi ‘kumpaka’ Nyalandu wakimwita fisadi, hali inayoweza kutumiwa na CCM kudai kuwa ‘Chadema ni kimbilio la mafisadi.’ Hata hivyo ni rahisi kwa chama hicho cha upinzani kuwauliza CCM, “mpaka mwanasiasa awakimbie na kujiunga nasi ndio mnaanza kumwita fisadi?” Ni hoja inayoingilia akilini.


Je Nyalandu atapata mapokezi mazuri huko Chadema? Kama kauli ya Lowassa jana kuwa Chadema itakuwa ‘imelamba dume’ pindi Nyalandu akijiunga na chama hicho inaashiria chochote basi kuna uwezekano mkubwa wa mafanikio makubwa kwa mwanasiasa huyo.

Hata hivyo, ukweli kwamba Nyalandu ni miongoni mwa watu wenye sifa na uwezo wa kuwa wagombea urais kwa tiketi ya Chadema mwaka 2020 unaweza kupelekea mgongano dhidi yake na majina mengine yanayotarajiwa kuwemo kwenye kinyang’anyiro hicho, yaani Lowassa, Sumaye na Lissu.

Hili sio tatizo kubwa sana iwapo maslahi ya Chadema – badala ya maslahi ya mtu au kikundi binafsi – yakiwekwa mbele. Kwamba kufanyike tathmini ya kutosha kufahamu nani anayeweza kukiwezesha chama hicho kuing’oa CCM madarakani hapo mwaka 2020.

Kwamba Nyalandu anaweza kuleta hamasa kwa wana-CCM wengine (Membe?) kujiunga na Chadema, na kama ujio wake huko Chadema utaleta matokeo chanya, ni suala la muda. Lililo bayana hadi muda huu, uamuzi wake huo wa ghafla umetushtua wengi ikiwa ni pamoja na CCM na makada wake. Na yayumkinika kuamini kuwa uamuzi huo utaleta msisimko mpya katika siasa za Tanzania.

Mwisho, uchambuzi huu umetokana na uelewa wangu wa siasa za Tanzania, na unaweza kuwa sio sahihi kulingana na mitazamo tofauti. Jiskie huru kuchangia maoni, kunikosoa au hata pongezi zinaruhusiwa. Siku zote ninajitahidi kwenda mbali zaidi ya kuripoti tu matukio badala ya kuyachambua kwa undani zaidi. Asanteni na siku njema



1 comment:

  1. Zangu ni pongezi nyingi Evarist kwa mtazamo wako uliokuwa makini na uelewa mkubwa wa mwenendo wa sayansi ya siasa za nyumbani. Kudos!

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.