Showing posts with label ARUSHA. Show all posts
Showing posts with label ARUSHA. Show all posts

15 Jun 2013




Habari zilizotufikia hivi punde bomu limelipuka katika eneo la Soweto mkoani Arusha kwenye mkutano wa Chadema leo, na kusababisha watu wanne  kufariki  Dunia.

Mlipuko huo umetokea majira ya saa 12:00 na  majeruhi ni zaidi ya 10 wamekimbizwa katika Hospitali ya Mount Meru STK 8493 kwa matibabu zaidi.

Bomu hilo ambalo lilikuwa limetegewa katika mkutano huo lilipuka na kusababisha mauti na kujeruhi watu zaidi 10.

Pia gari limevunjwa vioo na wananchi kwa madai ya kwamba limeshindwa kuokoa maisha ya majeruhi.
 
Inaonekana bomu lilitegwa karibu na gari la matangazo, Mtoto aliyelipukiwa na bomu amefariki uwanjani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Abbas amesema kwamba watu wawili ndio wamepoteza maisha.




13 Jan 2011

MSIBA WA MASHUJAA WALIOUAWA KWA AMRI YA DIKTETA JAKAYA KIKWETE

 











































































SARAFINA THE FUNERAL SONG



PICHA NA VIDEO KWA HISANI KUBWA YA MTANDAO NAMBARI WANI Jamii Forums.KWA HABARI KAMILI SOMA HAPA.

11 Jan 2011



Pengine wakati uongozi wa Chadema mkoani Pwani ulipochukua uamuzi wa kuahirisha mkutano wao wa hadhara-baada ya "intelijensia yao kubainisha kuwa jeshi la polisi lilikuwa na njama za kuzusha zahma kama ile ya Arusha-hawakufahamu kuwa actually wanavumbua mbinu inayoweza kuwatwanga misumari wadhalimu pale inapouma zaidi (hitting where it hurts most).

Ofkozi,yayumkinika kuamini kuwa Chadema mkoani Pwani waliingia gharama kuandaa mkutano huo,na kuuahirisha kumewatia hasara.Lakini ni dhahiri kuwa upande uliopata hasara kubwa ni Serikali iliyoamua kutuma rundo la askari kwenda "kutoa kipigo" kwa wananchi wasio na hatia,lakini target ikayeyuka.

Mbinu hii inaweza kuwa na ufanisi mkubwa.Kutangaza maandamano au mkutano mkubwa,kisha kama kawaida Serikali inaingia gharama za kuandaa operesheni ya kwenda kuangamiza watakaohudhuria maandamano/mkutano husika,lakini hatimaye nguvu ya tembo kukanyaga sisimizi inaishia kukanyaga hewa tupu.

Ili mpango huu ufanikiwe kunahitajika intelijensia bora zaidi ya vyombo vyetu vya usalama vilivyosheheni vihiyo wa taaluma ya usalama.Intelijensia inayohitajika ni ya kuhakikisha ujumbe kuwa kutakuwa na maandamano au mkutano umefika kwa wakandamizaji hao wa haki za binadamu.Ujumbe ukifika,raslimali na nguvu kazi ya kukandamiza jamii itaandaliwa chapchap,only for them kuishia kukandamiza hewa (uwanja au ukumbi mtupu).

Good news is,viongozi wengi-kama sio wote- wa vyombo vyetu vya usalama ni vihiyo wa taaluma ya usalama.Kwao,usalama ni kwa vigogo na mafisadi tu ilhali kinachowezesha wanausalama hao kulipwa mishahara na marupurupu lukuki ni fedha zinazotokana na kodi za walalahoi (vigogo na mafisadi wakilipa kodi ni kwa hisani tu,si lazima kwa vile hakuna sheria dhidi yao).Ukihiyo wa viongozi hao ni muhimu katika mkakati huu kwani,kama ilivyothibitika katika intelijensia yao ya kiwendawazimu kabla ya mauaji ya Arusha,wakishaskia kuna maandamano au mkutano basi badala ya kufanya analysis makini ya kiusalama za kuwawezesha kubashiri matishio la usalama na namna ya kuyadhibiti,wao wanakimbilia kuamrisha askari polisi wajiandae kwa vita huku magari ya mapambano na yale yenye maji ya upupu yakijazwa mafuta tayari kwa "vita".

Sasa kama kila baada ya wiki mbili wanyanyasaji hawa wanaingia mkenge na kujitwisha gharama za kudhibiti maandamano au mikutano hewa,ni dhahiri kuwa sio tu itavunja morali wa polisi wanaomtumikia kafiri ili mkono uende kinywani bali pia itaikamua serikali ambayo imeshatumia mabilioni kuchakachua uchaguzi uliopita,let alone gharama za kumudu lifestyles za kifahari za watawala wetu.

Wito wa blogu hii kwa Chadema ni simple: moto mlioanzisha haupaswi kuzimika mpaka kieleweke.Kwa upande mmoja,kuuzima moto huo kutamaanisha kusalimu amri kwa utawala wa kidikteta wa Kikwete.Na kwa upande mwingine,kuzima moto huo kutamaanisha uhai wa wazalendo waliouawa na polisi umepotea bure.Sio tu kwamba vuguvugu lililoanzishwa likiendelea kwa muda mrefu litapelekea Serikali kuishiwa nguvu ya kupiga na kuua kila kunapokuwa na mkutano au maandamano bali pia linaweza kuwafanya polisi wanaotumwa kuua Watanzania wenzao kupatwa na akili ya kutambua kuwa wanatumika vibaya kukandamiza raia wasio na hatia.Unaweza kudhani polisi hawa katili hawawezi kupatwa na roho ya kibinadamu.Hilo linawezekana,na dalili kuwa mwenye nguvu anaweza kutalikiwa na mnyonge kukumbatiwa inaonekana katika uamuzi wa diwani wa CCM huko Arusha aliyeamua kukitosa chama hicho tawala na kujiunga na Chadema.Uthibitisho mwingine ni kitendo cha Naibu Meya wa Arusha aliyeamua kubwaga manyanga kwa vile hayuko tayari kuwasaliti Watanzania wenzie.Trust me,vuguvugu hili likiendelea tunaweza kusikia stori kwamba polisi kadhaa wameamua kubwaga silaha kukwepa kwenda kuwaadhibu Watanzania wenzao wasio na hatia.

Kama alivyoandika mwanahabari mahiri Ansbert Ngurumo katika safu yake ya "Maswali Magumu" katika toleo la juzi la gazeti la Tanzania Daima,uamuzi wa Rais Kikwete na IGP wake Said Mwema kukandamiza wananchi kwa kipigo na risasi kitasaidia kuchochea hamasa kwa Watanzania wengi zaidi,na-kama alivyobainisha mwanahabari mwingine mkongwe Padri Privatus Karugendo- polisi hawana uwezo wala raslimali za kupiga risasi kila Mtanzania.Tupo wengi kuliko wao,na pia kama sera ya chinja chinja itaendelea basi mwishowe polisi hao watajikuta wanaua wazazi wao kama sio memba wengine wa familia zao.

Naanza kuhisi joto la ukombozi wa pili ikijongea kwa kasi.Na kichocheo cha joto hilo si kingine bali damu za wazalendo na mashujaa zilizomwagwa na askari waliotumwa na Kikwete kudhibiti raia wema huku mafisadi wakipewa hifadhi na fidia (rejea mabilioni kwa Dowans).

10 Jan 2011



Tanzania tuna tatizo kubwa.Hakuna haja ya kunyoosheana vidole as to nani amechangia tatizo hilo bali cha muhimu na haraka ni namna tutakavyoweza kutatua tatizo hili.Nisimung'unye maneno: tatizo kubwa linaloikabili ni kuwa na Rais ambaye takriban miaka sita tangu aingie Ikulu haelewi wajibu wake.

Hivi msomaji mpendwa wa blogu hii utamuelezeaje Jakaya Kikwete,Rais wetu,baada ya kumsikia akijitetea kwa mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania kuwa "unyama wa hali ya juu uliofanywa na polisi huko Arusha,na kusababisha vifo vya Watanzania wasio hatia,ni BAHATI MBAYA"!!!

Yani Kikwete aliishiwa kabisa na cha kudanganya mpaka akakurupuka na excuse dhaifu kiasi hiki!Bahati mbaya kwa maana gani?Bahati mbaya IGP Said Mwema kutengua dakika za majeruhi ruhusa ya maandamano iliyotolewa na RPC wa Arusha?Bahati mbaya polisi kuachana na jukumu la kusindikiza maandamano ya amani na badala yake kuanza kuwaadhibu wananchi wasio na hatia ambao "kosa" lao lilikuwa kutumia haki yao ya kikatiba kuandamana kwa amani?Bahati mbaya kupuuza miito kutoka kada mbalimbali juu ya umuhimu wa kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa umeya wa Arusha?Au bahati mbaya kwa risasi kutoka kwenye mitutu ya bunduki na hatimaye kutoa uhai wa Watanzania wasio na hatia?

Au Kikwete alikuwa anamaanisha kwamba unyama wa polisi wake dhidi ya wafuasi wa CUF walipoandamana,au vitendo vya udhalilishaji vya polisi hao dhidi ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki,au unyanyasaji uliozoeleka dhidi wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kila wanapoandamana,ni BAHATI NZURI kwa vile hakuna aliyeuawa?

Nashindwa hata kuhisi mabalozi walipatwa na mawazo gani walipomsikia mkuu wa nchi anatoa kauli ya ajabu kiasi hicho.Nahisi kuna waliomhurumia kwa kijibebesha jukumu asiloweza.Hii inanikumbusha wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 (ambazo zilinikuta nikiwa huko nyumbani kwa miezi kadhaa).Kuna baadhi ya wajuzi wa siasa za Tanzania waliniambia kuwa Kikwete anaweza kushinda urais kwa vile ana timu ambayo iko tayari kufanya lolote kuhakikisha anapata ushindi LAKINI urais wake utakuwa kituko.Na kituko amekuwa.

Kuna watakaosema wa kulaumiwa ni washauri wake.Lakini hao watakuwa wamesahau kuwa alipoanguka Mwanza alitanabaisha kuwa huwa anapuuza ushauri wa washauri wake (ambapo tulielezwa walimshauri apumzike kabla ya kukumbwa na zahma hiyo).Sasa inawezekana kabisa kuwa hata kabla ya kuongea na mabalozi hao,washauri wake walimshauri kitu sensible cha kuongea lakini akapuuza.Au pengine waliona hakuna haja ya kumshauri mtu ambaye ni "haambiliki".

Lakini tukiweka kando excuse hiyo ya kitoto iliyotolewa na mtu tuliyemkabidhi jukumu la kutuongoza Watanzania takriban milioni 50,ukweli kwamba Kikwete amediriki kujiumauma kwa mabalozi unapigia mstari ushauri niliotoa kwenye makala yangu iliyopita.Katika makala hiyo niliwashauri Watanzania wanaoishi katika nchi wafadhili wa Tanzania kuwasiliana na wabunge/wawakilishi wao na kuwafahamisha udikteta wa Kikwete,kisha kuwaomba wafikishe kilio cha Watanzania kwa serikali za wafadhili hao.Kikwete amelazimika kuokoteza excuses kwa vile anatambua bayana kuwa ni lazima awapoze wafadhili kwani mchango wa wafadhili hao ni muhimu sana kwa ustawi wa taifa letu.Ni muhimu zaidi kwa ustawi wa Kikwete na serikali yake inayosifika kwa matumizi ya anasa yanayozidi mapato.Wafadhili wakiamua kusitisha misaada,serikali itaanguka within months if not weeks.Lakini idea yangu ya kufikisha ujumbe kwa nchi wafadhili haikulenga kuwashawishi wasitishe misaada bali naamini wao wanaweza kumbana dikteta huyu aanze kuheshimu haki za binadamu.

Na kuthibitisha kuwa Kikwete alikuwa anawazuga mabalozi hao,gazeti la Tanzania Daima lina habari kuwa jeshi la polisi limezuia maandamano ya amani huko Songea yaliyoandaliwa na Chadema kupinga ufisadi katika sekta ya kilimo. Huu ni uthibitisho tosha kuwa unyanyasaji wa raia wasio na hatia na ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na polisi sio suala la BAHATI MBAYA kama anavyozuga Kikwete.Ni utekelezaji wa maagizo ya serikali iliyopo madarakani inayoongozwa na Kikwete huyohuyo.

Hivi Kikwete ameshindwa angalau kuwatosa Waziri wa Mambo ya Ndani Shamsi Vuai Nahodha,IGP Mwema na RPC wa Arusha kuwa "mbuzi wa kafara" ali mradi imsaidie kudanganya kuwa yeye hahusiki na maagizo yaliyopeleka polisi kuua.Hawezi kuwatosa kwa vile ni kiongozi anayeendekeza ushkaji.Sasa kama familia haiwezi kuongozwa kishkaji,nchi ikiongozwa kwa mtindo huo inakuwaje?

Na kuna kila dalili kuwa hivi sasa Kikwete anaongoza nchi na CCM yake kwa mtindo wa "bora liende".Hebu angalia jinsi ishu ya fidia kwa Dowans inavyoonyesha mparaganyiko kwenye kabineti ya Kikwete.Wakati Waziri William Ngeleja anatweta kuwakikishia mafisadi wa Dowans kuwa lazima walipwe kwa utapeli wao,Waziri Samuel Sitta anatangaza hadharani kuwa kuwalipa Dowans ni jambo la hatari.Uwajibikaji wa pamoja Kikwete's cabinet style!Huko CCM,Katibu wa chama hicho mkoani Arusha,Mary Chatanda anawawakia viongozi wa dini akiwataka wavue majoho yao wajiunge na siasa badala ya kukemea maovu (mpuuzi huyu anakosa adabu hata kwa Watumishi wa Mungu!).Kwa upande mwingine,Katibu Mkuu wa chama hicho,Yusuph Makamba,anadai kila mtu ana uhuru wa kutoa mawazo yake including viongozi wa dini.Na yote hayo yanatokea huku yakiweka kivuli kwenye tukio la kihistoria la diwani wa CCM kujiunga na Chadema.Tukio hili linapaswa kuchukuliwa kama ugonjwa nyemelezi kwa mwathirika wa ukimwi: linaashiria mwanzo wa mwisho wa CCM.

NIMALIZIE KWA KUKUMBUSHIA WITO WANGU KWA WATANZANIA WENZANGU WANAOISHI NCHI ZA WAFADHILI WA TANZANIA.KUWA MBALI NA NYUMBANI ISIWE SABABU KWETU KUSHINDWA KUSAIDIA UPATIKANAJI WA UHURU WA PILI WA TANZANIA (wa kwanza ulikuwa wa kumwondoa mkoloni,wa pili ni wa kuondoa udhalimu,ufisadi,ubabaishaji,unyanyasaji,ukiukwaji haki za binadamu,udikteta na kila baya unalofahamu).TUWASILIANE NA WABUNGE/WAWAKILISHI KATIKA MAENEO TUNAYOISHI NA KUWAOMBA WATUFIKISHIE KWA SERIKALI ZAO VILIO VYA WATANZANIA WENZETU WANAONYANYASIKA KWA KILA HALI CHINI YA UTAWALA WA KIKWETE NA CCM YAKE

8 Jan 2011







Mbunge wa zamani kutoka chama cha Labour hapa Uingereza,David Chaytor (pichani juu),leo amelala usiku wa kwanza akiwa jela kama mfungwa baada ya kuhukumiwa kifungo cha miezi 18 kutokana na kukutwa na hatia ya ubadhirifu wa fedha za umma takriban pauni 20,000 (takriban shilingi 45 milioni za Tanzania).Ubadhirifu wa fedha hizo za umma ni kutokana na matumizi mabaya ya fedha za posho kwa wabunge.


Wakati hayo yakijiri hapa,huko nyumbani Waziri wa Nishati na Madini,William Ngeleja alivunja mzizi wa fitina kwa kutangaza hadharani kuwa hatimaye serikali italipa shilingi 95,000,000,000 (bilioni tisini na tano) kwa kampuni ya kifisadi ya Dowans kufuatia hukumu ya kiini macho iliyotoa ushindi kwa kampuni hiyo licha ya rundo la utata linaloendelea kuizunguka.



Ngeleja,bila haya wala uoga,alieleza kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Frederick Werema) ameridhia hukumu hiyo ya miujiza kabisa na ushauri wake wa kitaalam (ya sheria) ni kuilipa kampuni hiyo.

Wote,Ngeleja na Werema ni wateuliwa wa Rais Jakaya Kikwete,ambaye kwa makusudi kabisa aliepuka kuzungumzia suala la Dowans katika hotuba yake ya kukaribisha mwaka mpya 2011.Ni dhahiri kuwa Kikwete ameridhia Dowans ilipwe na ndio maana Ngeleja na Werema wanatoa maamuzi yao bila hofu wala aibu. Na kama umesahau,ni Kikwete huyuhuyu aliyeahidi wakati wa kampeni zake kuwa ana dhamira ya kuboresha maisha ya Watanzania.Nadhani labda alichomaanisha ni kuboresha akaunti za mafisadi kwa mgongo wa walalahoi.

Napata shida kutumia lugha ya kistaarabu kushangazwa na uwendawazimu huu!Hivi hawa viongozi wetu wamerogwa na mafisadi au ni matokeo ya kupokea fadhila za mafisadi kupita kiasi kwamba sasa wanalazimika kulipa fadhila hizo kwa gharama yoyote ile?Hizi sio tamaa za kawaida tulizozowea kuziona kwa watawala wetu.Hiki ni kichaa hatari ambacho pasipo hatua za haraka kinaweza kupelekea nchi nzima kuuzwa,kisha akina Werema wakaja kutuambia gharama za kuzuia kuuzwa kwa nchi yetu ni kubwa kuliko uamuzi wa kukubali nchi iuzwe.

Blogu hii ilifanya kila ilichoweza kuhamasisha wapiga kura waiepuke CCM na mgombea wake Kikwete.Sio kwamba blogu hii ilifanya utafiti wa kina kubaini athari za kuirejesha CCM madarakani bali taarifa kuhusu uhuni wa chama hicho,sambamba na kilivyojipa jukumu la kuwa kichaka cha kuhifadhi mafisadi,zilikuwa bayana kwa kila mwenye macho.Hivi kuna Mtanzania asiyefahamu kuwa ujio wa kampuni ya kijambazi ya Richmond (iliyopelekea ujambazi mwingine wa Dowans) ulikuwa na baraka za Kikwete pamoja na swahiba wake Lowassa na "kubwa la maadui" Rostam Aziz?





Ndio maana majuzi baada ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,Dkt Wilbroad Slaa,kurejea kauli yake kuwa Kikwete ni mmiliki wa Dowans,hasira za mkuu huyo zikaishia kwa kuamuru polisi wake kutoa kipigo kwa raia wasio na hatia huko Arusha na kupelekea vifo kadhaa (Polisi wanadai wameua watu watatu tu lakini tangu lini wauaji wakaaminika?).


Na kama adhabu ya Kikwete kwa Chadema na wana-Arusha haijatosha,kaamua kuwadhihaki Watanzania wote kwa kuidhinisha Dowans ilipwe mabilioni hayo,huku swahiba wake Rostam akidhihaki Watanzania kwa kudai hizo bilioni kadhaa ni fedha kiduchu tu kwake.Huwezi kumlaumu kwani kaiweka serikali mfukoni na anaendesha nchi kwa remote control.

Blogu hii iliwaasa wapiga kura kuhusu madhara ya kumpatia Kikwete miaka mitano mingine baada ya awamu yake ya kwanza kugubikwa na ufisadi wa kutisha.Lakini hata kwa viwango vilivyozoeleka vya ufisadi hakuna aliyetarajia kuwa hata kabla miezi mitatu haijapita tangu arejee madarakani,Kikwete angediriki kuruhusu Watanzania wenzie wabakwe kiuchumi kwa mtindo huu wa Dowans.Lakini kwa vile Katiba tuliyonayo inampa madaraka mithili ya mungu-mtu,na kwa vile anafahamu fika kuwa Watanzania ni wepesi wa kusahau na ndio maana wengi wao wakampigia kura licha ya maumivu aliyowasababishia tangu aingie madarakani Desemba 2005,ameruhusu ujambazi huu wa mabilioni ya fedha za walipa kodi pasi soni.

Tusipochukua hatua za haraka tutashtukia tumefikishwa mahala ambapo hatutokuwa na namna ya kurekebisha mambo.Kama less than three months tangu Kikwete arejee madarakani tumeshashuhudia Dowans ikizawadiwa mabilioni kama asante ya kututapeli,na tumeona hasira za Kikwete kwa ukatili na mauaji yaliyofanywa na polisi wake (kisa kasutwa kuwa analea ufisadi),ni wazi kuwa hali itazidi kuwa mbaya na yawezekana ikawa ya kutisha kabla Kikwete hajamaliza muda wake hapo 2015 (assuming hatachakachua Katiba kutaka aongezewe muda).

Moja ya hatua inayoweza kuzaa matunda ni kufikisha kilio chetu kwa nchi wahisani.In addition to malezi anayotoa Kikwete kwa mafisadi,sasa tuna jambo jingine zito ambalo linaweza kuvuta hisia za wahisani,nalo ni ukiukwaji wa haki za binadamu kama ilivyodhihirika huko Arusha.



Kwa kuanzia,blogu hii inamwomba kila mzalendo anayeishi katika nchi mfadhili kwa Tanzania,kuwasiliana na mbunge wake na kumwomba afikishe kilio cha wanyonge wa Tanzania.Toa chapa ya picha za matukio ya Arusha pamoja na habari zinazobainisha ukiukwaji wa haki za binadamu,na ufisadi,kisha mfahamishe mbunge huyo kuwa hii ndio hali halisi ya Tanzania chini ya utawala wa Kikwete.Kama utahitaji maelezo zaidi ya namna ya kuwasilisha ujumbe wako kwa mbunge wa sehemu unayoishi,usisite kuwasiliana nami.

KWA USHIRIKIANO WETU,TUNAWEZA KUPAMBANA NA UTAWALA DHALIMU AMBAO LICHA YA KUUA RAIA WASIO NA HATIA HUKO ARUSHA,UNATOA ZAWADI YA SHILINGI BILIONI 95 KWA DOWANS KANA KWAMBA HIYO NDIO RAMBIRAMBI KWA WALIOUAWA NA POLISI HUKO ARUSHA.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.