Showing posts with label Ambisikile Mwasakile. Show all posts
Showing posts with label Ambisikile Mwasakile. Show all posts

26 Mar 2011

Habari na picha hii zimetumwa na mdau wa Mbeya yetu,nami naiwasilisha kama ilivyo...with no comment!



Mganga mwingine wa tiba za magonjwa Sugu aliyefahamika kwa jina la Jafar Welino(17) mkazi wa mtaa wa Mianzini Kitongoji cha Mabatini jijini Mbeya ameibuka na kutoa tiba kwa mamia ya wakazi wa jiji la Mbeya na viotongoji vyake.



Umati wa watu ulionekana katika nyumba anayoishi kijana huyo wakisubiri kupatiwa tiba hiyo huku wakiwa na vikombe vyao mikononi. Baadhi ya wananchi waliofika eneo hilo walidai kuwa wamefika hapo kutokana na taarifa za kuwa kijana huyo anatibu magonjwa Sugu bure kama vile ambavyo anatibu Mchungaji mstaafu wa Loliondo Mzee Ambilikile Mwasapila.



Akizungumza kwa niaba ya kijana huyo mama mkubwa wa mganga huyo aliyejitambulisha kwa jina la Edina Sanga alisema kuwa kijana huyo alianza tiba hiyo wiki mbili zilizopita ambapo kabla ya kuanza kutibu alimueleza mama yake huyo kuwa alitokewa na mama yake mzazi a,mbaye kwa sasa ni marehemu akimuelekeza kurithi mikoba yake.



Bi.Sanga alisema kuwa mama yake kijana huyo ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa ni mtu mwenye maruhani ambapo kwa kutumia maruhani hayo alikuwa akitoa tiba kwa wakazi mbalimbali mjini Mbeya.Alisema kijana huyo ambaye wamezaliwa mapacha na dada yake aliyemtambulisha kwa jina la Hadija Welino kwamba yeye anasoma kidato cha Nne katika shule ya sekondari Itende.

Hata hivyo Bi.Sanga alisema kuwa kijana huyo aliitwa katika ofisi ya Ofisa Mtendaji ili kutoa maelezo ya namna ambavyo anaendesha tiba hiyo na kuwa hata hivyo anaendelea kutoa tiba kwa watu kwa kunywa vikombe viwili kwa muda wa siku mbili. Alisema kuwa dawa hiyo aliifuata katika kijiji cha Iyula kilichopo wilayani Mbozi na kuwa mara alipofika alianza kuichemsha na kuwagawia wananchi wanaosumbuliwa na maradhi sugu. Aidha umati wa watu walikuwa wamejipanga katika mistari kusubiri tiba hiyo ambapo


Mwenyekiti wa mtaa wa Mianzini Bi.Elizabethy Mwakabungu aliweka utaratibu wa wananchi kupata tiba ikiwa ni pamoja na kuchangia fedha kidogo kwa ajili ya kununulia kuni za kuchemshia dawa hiyo.Akizungumza na umati wa watu waliokuja kujipatia tiba hiyo Mwenyekiti huyo wa mtaa alisema kuwa kila ambaye atapata kikombe kimoja cha dawa anatakiwa kupata kikombe cha pili siku inayofuata.



‘’Mganga katuagiza kuwa kila anayekunywa kikombe kimoja anatakiwa kunywa kikombe cha pili siku inayofuata…yeyote atakayekunywa hatakiwi kunywa pombe kwa muda wa siku saba,’’alisema Bi. Mwakabungu


Wakipata kikombe

maelekezo ya kufika eneo hilo

Pamoja tunaendeleza kupashana Habari


HABARI NA PICHA: Mbeya Yetu

14 Mar 2011


TIBA inayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa KKKT (Babu), Ambilikile Mwasapile katika kijiji cha Samunge, Loliondo, imeendelea kuonyesha maajabu yake baada ya wagonjwa kadhaa wa hospitali mbili kubwa nchini kukutana na madaktari wao kwenye foleni, kila mmmoja akitafuta uponyaji.
.

Wakati hayo yakiendelea, Mbunge wa Kilindi mkoani Tanga, Bi. Beatrice Shellukindo ametoa ushuhuda tiba hiyo ya Babu si jambo la mzaha bali inaponya, yeye amenufaika nayo, pamoja na ndugu zake 18 alioongozana nao.

Wakizungumza na majira kwa nyakati tofauti siku chache baada ya kurudi walikokwenda kufuatilia tiba hiyo, baadhi ya wanachi walithibitisha wagonjwa hao kupigana vikumbo na madaktari wao kwenye foleni kila mtu akijaribu kutatua tatizo lake.

“Sisi tulikwenda baada ya kushauriwa na daktari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambaye anamtibu ndugu yangu. alitwambiwa moja kwa moja ya kwamba tumpeleke mgonjwa wetu kwa Babu,” alisema Timothy Ndalichako, mkazi wa Njoro, mjini Moshi.

Alisema siku chache baada ya kupewa ushauri huo ambao ulitiwa chumvi na kuenea kwa taarifa za huduma ya Babu, walitafuta taratibu za kumpeleka ndugu mgonjwa huyo Loliondo na kufanikiwa kuipata baada ya siku mbili kwa kuwa wakati huo msongamano ulikuwa haujawa mkubwa.

“Tukiwa kwenye foleni siku ya pili, ndipo tukamuona daktari aliyetushauri akiwa ameandamana na wenzake kwenye gari, nao wakiwa wanaingia eneo la tiba Loliondo,” alisema.

Aidha alisema alichogunduwa ni kwamba madaktari wengine kutoka hospitali hiyo maarufu hapa nchini na nje ya nchi pamoja na wale wa hospitali nyingine za mjini Moshi, walishafika na wengine walikuwa wakiendelea kufika eneo hilo kufuatia tiba hiyo mbadala.

Kwa upande wake, Bw. Manase Kiara, alidai kukutana na daktari bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, aliyekwenda Loliondo kufuatia tiba hiyo.

“Niliondoka na wenzangu baada ya kujipanga kwenda kupata tiba baada ya kuhangaikia kwa muda mrefu Muhimbili. Kufika huko mimi na wenzangu tulikutana na dokta wetu ambaye baada ya kusalimiana naye tu alituambia mpeni Mungu yaliyo yake Mungu na ya Kaisari mpeni Kaisari,” alisema.

Wakati huo huo baadhi ya wananchi wa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro wameipongeza serikali kwa tamko lake kuwa haijazuia huduma ya tiba inayotolewa Mchungaji Mwasapile kwa miezi kadhaa sasa.

Shellukindo atoa ushuhuda wa tiba

Mbunge wa Jimbo la Kilindi mkoani Tanga, Bi. Beatrice Shelukindo amesema akiwa na ndugu zake 18 wakiwa na matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwemo yeye mwenyewe kusumbuliwa na magonjwa mbalimbali kwa muda mrefu, wamefika kwa Babu na kupata tiba.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu akiwa Arusha jana baada ya safari iliyomchukua wiki nzima, Bi. Beatrice alisema sio jambo la mzaha, dawa ya Babu inaponya.

Bi. Shelukindo alisema walifika katika Kijiji cha Samunge wilayani Ngorongoro Machi 7, mwaka huu, lakini kutokana na wingi wa wagonjwa walipata tiba Machi 11 yeye na ndugu zake, na baada ya hapo kila mtu akajisikia amepona, wakiwemo waliokuwa wanasumbuliwa na saratani.

"Mimi mwenyewe nilikuwa nasumbuliwa na presha na vidonda vya tumbo kwa muda mrefu, lakini baada ya kunywa kikombe kile cha dawa nilipona, tangu Ijumaa sijagusa kabisa kidonge cha aina yeyote, iwe kwa ajili ya vidonda vya tumbo au presha.

"Lakini maajabu yapo kwa mtoto wangu wa kike, akiwa na miaka 37 tulimpeleka hajiwezi na hajaweza kula wala kusema kwa miezi sita, zaidi ya kunywa uji tu kwa vile alikuwa anasumbuliwa na kansa, lakini baada ya kutoka hapo, kwanza tulishangaa baada ya kutaka tumpe chakula.

"Na kutokana na shida ya safari, wakati wa kurudi tulimuandalia ndege ya kurudi Dar es Salaam alikataa na jana Jumamosi (Machi) amerudi kwa basi. Mwingine ni mama mdogo alikuwa anasumbuliwa na presha mbaya, lakini ghafla amepona," alisema Bi. Shelukindo.

Bi. Shelukindo alisema pia alikwenda na ndugu yake mwanaume, yeye alikuwa anaumwa macho kiasi ambacho moja lilipasuka, lakini alipofika kwa Babu na kunywa dawa amepona, na ndugu zake wote aliokwenda nao wanaendelea vizuri.

"Yusuph (mwandishi) nakusihi sana uende kwa yule mchungaji. Sio vitu vya kubuni, dawa yake inaponya. Hakika ndugu zangu wote wamepona. Ni kweli imani pia ni muhimu katika kutumia dawa hiyo, lakini yenyewe bado inaponya, na inaanza kufanya kazi siku moja mpaka saba tangu unywe dawa hiyo," alimaliza kwa kutoa ushuhuda huo Bi. Shelukindo.


Mazingira yaanza kuwekwa sawa

Hofu ya usalama ilikuwa imetanda kwenye Kijiji cha Samunge imeanza kuondoka baada ya serikali wilayani Ngorongoro
imesema kuanza uboresha wa miundombinu, usafi wa mazingira na kuweka utaratibu mzuri wa wagonjwa kupata tiba.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Elias Wawa Lali alisema jana kuwa
siku chache tu zijazo wananchi watapata tiba hiyo kwa muda mfupi na katika mazingira safi na salama kwa kuwa tayari wameanza jitihada za kukamilisha mpango huo kwa kushirikiana na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati.

Kwa mujibu wa DC huyo kanisa hilo limesema kuwa watahakikisha wananchi hawapati tena taabu walizokuwa wakizipata siku kadhaa zilizopita za kukaa siku zaidi ya tano bila tiba huku wakitishiwa na hatari ya kimazingira kwa afya zao.

“Kila mmoja anazungumza habari ya Loliondo hata yule ambaye hana taarifa sahihi za huko, lakini uhakika ni kwamba tayari mipango yetu inakwenda vizuri tunachozubiri na
wataalamu hao wa ujenzi kutuletea tathimini nzima ya kinachohitajika huko,” alisisitiza DC.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Askofu Thomas Laiser alisema kanisa hilo katika kuhakikisha azma yao inatimia linatarajia kutumia zaidi ya sh milioni 75
katika kuboresha mazingira ya tiba hiyo.

Fedha hizo ni kwa ajili ya kujenga majengo maalumu yenye uwezo wa kuhudumia watu zaidi ya 600 kwa wakati moja, huku kukiwa na huduma bora za matundu ya vyoo na maji safi na salama ya kutosha.

Aliongeza wachoraji na wasanifu wa majengo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi hiyo, Bw. Ezrael Kariyongi hivi sasa wapo kijijini Samunge wakifanya tathimini ya mradi huo.

Alisema kuwa hata hivyo bajeti hiyo itategemea taarifa ya mchanganuo wa ujenzi huo ambapo utekelezaji wake utafanyika ndani ya wiki mbili zijazo ambapo mchungaji huyo ataendelea na tiba hiyo.

Imeandaliwa na Yusuph Mussa, Korogwe; na Heckton Chuwa,
Moshi; na Said Njuki, Arusha

CHANZO: Majira


MWENYEKITI wa TLP, Augustine Mrema, ametinga Loliondo kwa Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Ambilikile Mwasapile kunywa dawa na kutamba ni kwa ajili ya kuongeza nguvu ya mwili kupambana na ufisadi

Mrema, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), alisema jukumu alilokabidhiwa kuzunguka nchi nzima ni kubwa linalohitaji kuimarisha afya yake.

“Kazi niliyokabidhiwa ni kubwa, kuzunguka nchi nzima kupambana na ufisadi kunahitaji kuimarisha afya yangu,” alisema Mrema na kuongeza:

“Bila kuimarisha afya huwezi kufanya kazi hii niliyokabidhiwa, waeleze Watanzania kuwa nimeimarisha afya sasa nikupambana na mafisadi kwenye halmashauri nchini kwa kwenda mbele.”

Alisema Watanzania wanatakiwa kumshukuru Mungu kwa ‘kuwashushia’ Mchungaji mstaafu Ambilikile Mwasapile (76), kwa sababu hawatumii gharama kubwa zaidi ya 500.

“Kama angekuwa Marekani tungeenda kwa Sh500? dawa yake haina kuchakachua unakunywa. Dawa nimekunywa na nimerudi na picha nimepiga naye ” alisema Mrema kwa kujiamini.

Hata hivyo, Mrema hakubainisha magonjwa yanayomsumbua hadi kwenda kwa Mchungaji Mwasapile, ingawa anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa muda mrefu. Siku za hivi karibuni vigogo wengi wa Serikali na CCM wamekuwa wakienda Loliondo kwa ajili ya tiba.

CHANZO:Mwananchi

7 Mar 2011


Kwa siku kadhaa sasa kumekuwa na taarifa kuwa Mchungaji mmoja mstaafu huko Monduli,mkoani Arusha anatoa tiba ya Ukimwi kwa gharama nafuu ya shilingi 500.Inaelezwa kuwa maelfu kwa maelfu ya watu wamekuwa wakimiminika kwa Mchungaji huyo Ambilikile Mwasakile kujipatia tiba ya gonjwa hilo hatari .

Japo kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa Ukimwi unadhibitika kwa sasa kutokana na uvumbuzi wa dawa zenye ufanisi zaidi katika kudhibiti athari za ugonjwa huo,tiba rasmi haijapatikana.Hata hivyo,ukweli huu haumaanishi kuwa tiba ya Mchungaji Mwasakile ni feki kwa vile hadi sasa hakuna mtu au taasisi iliyopinga madai yake.

Pia,huwezi kuwashangaa maelfu ya watu wanaofurika kwa Mchungaji huyo kusaka tiba.Kama malaria tu inawafanya watu wakimbilie mahospitalini,sembuse waathirika wa Ukimwi!

Lakini kama kichwa cha habari kinavyohoji,ukimya wa Wizara ya Afya na serikali kwa ujumla kuhusu madai hayo unaweza kuzua zahma kama ile ya upatu maarufu wa DECI.Katika sakata hilo la "kupanda mbegu",watumishi kadhaa wa Mungu walifanikiwa kuhamasisha maelfu kwa maelfu ya Watanzania "kupanda mbegu" zao kwa matarajio ya kuvuna mamilioni.Sote tunajua kilichofuata.

Serikali ilikuwa ikifahamu uwepo wa DECI lakini haikuchukua hatua stahili (kuruhusu au kuharamisha) hadi pale ilipozinduka na kupiga marufuku upatu huo,hatua iliyowaacha wananchi lukuki wakiwa wamepoteza fedha zao "za ngama".

Sasa japo katika suala hili la tiba ya ukimwi,malipo ni shilingi 500 tu,unyeti wa suala hilo na faida au athari zake unalazimisha serikali kutoa kauli rasmi.Tunafahamu ombwe kubwa la uongozi linaloikabili serikali yetu lakini si kwa kiwango cha kushindwa kusema lolote kuhusu suala hili "dogo" japo linaloweza kuwa na athari kubwa kwa jamii.

Hivi kwa mfano tiba ya Mchungaji huyo ni feki,je hiyo haitoathiri watu wanaoweza kusitisha matibabu ya dawa za kudhibiti virusi vya Ukimwi (ARVs?Serikali yoyote yenye kujali watu wake inapaswa kutoa kauli ya mwongozo kwa wananchi wake kuhusu ukweli au uongo wa madai hayo ya kupatikana kwa tiba ya ukimwi.

Japo kujaribu kuhalalisha au kupinga madai hayo si kazi nyepesi,mazingira yafuatayo yanaweza kutoa mwanga japo kidogo:

Kwanza,katika imani za kidini,kuna uwezekano kwa binadamu kujaliwa karama za kufanya miujiza.Nadhani baadhi ya wasomaji wanafahamu kazi za watu kama Father Nkwera na yule mama wa Mikocheni (anadhani alikuwa anaitwa Esther kama sikosei).Kadhalika,wengi wetu tumesikia miujiza ya Sheikh Shariff.

Pili,kuna watu wanaoaminika kuwa na uwezo wa kutibu maradhi mbalimbali kwa kutumia tiba za asili.Katika ukoo wetu,kuna ndugu yangu mmoja ambaye amekuwa akitoa tiba za asili katika eneo la Kiberege huko Morogoro.Kila nilipokuwa namtembelea nilikuwa nashuhudia namna anavyotibu watu wenye matatizo mbalimbali,ya kiafya na kimaisha.Hata hivyo,hapo kwenye "zahanati" yake kuna tangazo kuwa yeye hana uwezo wa kutibu ukimwi.

Tatu,ni rahisi kuzusha jambo na likaaminika miongoni mwa wengi.Na kama jambo lenyewe ni habari njema basi si ajabu "waaminifu" wa awali wakasambaza habari hizo "njema" na kupelekea tetesi zisizo na ukweli kupata uaminifu.Waingereza wana msemo kwamba uongo usipokemea unaishia kupata hadhi ya kuwa ukweli.Sasa ikitokea kuwa madai ya Mchungaji huyo si ya kweli,lakini hakuna anayekanusha,basi madai hayo yanaweza kuchukua hadhi ya "ukweli".

Kinachonipa wasiwasi ni kauli ya Mchungaji Mwasakile kuwa alianza kutoa matibabu hayo mwezi Agosti mwaka jana baada ya kuoteshwa na Mungu.Kwa maana hiyo,kuna watu kadhaa ambao wanaweza kuwa mashuhuda wa ufanisi wa dawa anazotoa kwa wagonjwa wake.Kwanini habari hizo hazikufahamika hadi majuzi,inabaki kuwa muujiza kama habari yenyewe ya tiba.

Pengine unaweza kusema si rahisi mtu kutapeli kwa kutoza shilingi 500 tu.Lakini ukifanya hesabu za chap chap utagundua kuwa laiti wagonjwa 2000 tu wakilipa kiwango hicho,Mchungaji atakuwa ametengeneza shilingi milioni moja.Na kwa mujibu wa taarifa za idadi ya watu wanaoelekea kwa Mchungaji huyo,yawezekana ameshachuma shilingi milioni kadhaa hadi sasa.


Ni mapema mno kubaishiri lolote kuhusu madai hayo.Kwa upande mmoja tiba kwa nguvu za kiroho au dawa asilia inawezekana,japo sina hakika kama ukimwi nao unatibika kwa njia hizo.Lakini,again,katika Mungu yote yanawezekana.

Serikali inaweza kuwasaidia Watanzania kwa kutoa tamko rahisi kuhusu madai hayo.Na licha ya ombwe la uongozi linaloikabili serikali yetu,suala hili linaweza kuwa rahisi zaidi hasa kwa vile taarifa zinaeleza kuwa vigogo kadhaa wameonekana wakielekea kwa Mchungaji huyo kwenda kujipatia tiba.Hawa wanaweza kuwa mashuhuda wazuri katika suala hilo.


Wakati jamii inasubiri uthibitisho wa madai ya Mchungaji huyo ni vema kubaki na msimamo rasmi wa kitabibu kuwa ukimwi hauna tiba.Na kwa waliokwishapewa "tiba" ya Mchungaji huyo,ni muhimu kwao kufanya vipimo vya kitaalamu kuthibitisha kama kweli wamepona.Na kama wakipona basi iwe fundisho kwao badala ya "kurejesha libeneke kwa kasi mpya,nguvu mpya na ari mpya"

Picha zote kwa hisani ya Michuzi

Kwa habari na picha zaidi soma hapa kwa Miss Jestina

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.