Showing posts with label BALLALI. Show all posts
Showing posts with label BALLALI. Show all posts

11 Feb 2008

Uongozi wa kisiasa wa Tanzania,kama ilivyo sehemu mbalimbali duniani,umekuwa ukitegemea watu kutoka fani mbalimbali za maisha.Tuna viongozi wa dini (kama Mchungaji Lwakatware),Wasomi (kama Prof Mwandosya,Prof Msola,Prof Mwakyusa),wanajeshi (kama Kapteni John Komba,Kapteni Jaka Mwambi,Luteni Yusufu Makamba) na hata wasanii kama Khadija Kopa .Hivi karibuni,JK alielezea kutoridhishwa kwake na athari zinazoweza kutokana na kuwa na viongozi ambao pia ni wafanyabisahara.Ana hoja ya msingi hapo,lakini nadhani tatizo la msingi sio fani aliyotoka au anayoendela nayo kiongozi husika bali ni utashi alionao katika kuwahudumia Watanzania wenzake.Kadhalika,mkanganyiko uliopo kwenye kanuni za maadili ya uongozi ziko shaghala baghala,hasa baada ya kuuawa kwa Azimio la Arusha na kuzaliwa Azimio la Zanzibar.Endelea na makala yangu hii kwenye gazeti la Mtanzania.
MTANZANIA UGHAIBUNI-

Watanzania wengi wameipokea kwa furaha kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu umuhimu wa kutenganisha biashara na utumishi wa umma.Ni kauli mwafaka kwani hata katika Maandiko Mtakatifu tunafundishwa kwamba ni vigumu kutumikia mabwana wawili.

Naamini kwa mtazamo wa wengi,wafanyabiashara kama Watanzania wengine wana kila haki ya kushiriki katika shughuli za siasa ikiwa ni pamoja na kugombea ubunge au hata kuteuliwa mawaziri.Tatizo linakuja pale maslahi ya biashara zao yanapoingiliana na utekelezaji wa majukumu yao katika kuuhudumia umma.

Inaweza kuwa sio sahihi kuwalaumu wafanyabisahara wanaochanganya biashara na siasa pale ilhali hakuna miongozo maalumu (kama ya Marekani na Uingereza).Ndio maana wazo la kufanyika mchakato wa kuleta sheria na kanuni zitakazoweka bayana mazingira ambayo kwa upande mmoja hayatawanyima nafasi wafanyabiashara kushiriki kwenye siasa,na upande mwingine biashara zao kutoathiri majukumu waliyokabidhiwa na taifa,lina umuhimu mkubwa.

Pamoja na pongezi hizo ni muhimu kuangalia chanzo cha tatizo lililopo hivi sasa.Ni ukweli usiopingika kwamba wakati wanasiasa wengi wameendelea kuhubiri kwamba siasa ya Ujamaa na Kujitegemea bado ni mhimili wa taifa letu,hali halisi tuliyo nayo sasa inapingana kabisa na matamshi hayo.

Azimio la Arusha lilisaidia kuweka wazi mwelekeo wa taifa letu.Makala moja kama hii haiwezi kutosha kuelezea undani wa Azimio hilo lakini kilicho wazi ni kwamba Baba wa Taifa,ambaye kimsingi ndiye anayekubalika kama mwasisi wa itikadi hiyo,alikuwa na ndoto ya kuona jamii ya Watanzania inayoishi kwa usawa na haki.

Baadaye likaja Azimio la Zanzibar.Pengine mie ni mzembe wa kujua kilichomo katika Azimio hilo lakini naamini kwamba kuna Watanzania wengi ambao hadi leo hawajui kilichomo kwenye Azimio hilo.Labda ni kutokana na ufahamu mdogo uliopo miongoni mwa wananchi wengi kuhusu Azimio la Zanzibar ndio maana wengi wetu tunarahisisha majibu kwamba lilikuwa tamko rasmi la kifo cha Azimio la Arusha.Na katika hili,CCM inastahili kubeba lawama zote kwani haijafanya jitihada zozote za makusudi kuuelewesha umma kuhusu madhumuni na kulichomo kwenye Azimio hilo (la Zanzibar).

Kuna mapungufu makubwa katika suala zima la uwazi pindi yanapojiri masuala nyeti kwa taifa letu.Mfano mzuri ni kwamba wengi wetu tulikuwa hatufahamu kwamba hadi uteuzi wake unatenguliwa na Rais,aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu aliyeondolewa madarakani,Dkt Daudi Ballali,hakuwa mtumishi wa serikali.Pengine taratibu zinasema hivyo lakini kwa vile mtu anayekalia nafasi hiyo ndiye mwenye kushika dhamana ya fedha za Watanzania wote,nadhani kulikuwa na kila sababu ya wenye fedha zao (Watanzania) kufahamishwa kuhusu hilo badala ya kusubiri mpaka litokee tatizo la ufisadi kwenye taasisi hiyo muhimu kwa taifa.

Hadi muda huu,ukiwauliza viongozi wa CCM kwamba je Azimio la Arusha bado ni mwongozo muhimu kwa maendeleo na mwelekeo wa taifa,sanasana utachoambulia ni hadithi ndefu zisizotosha kutoa jibu moja la kueleweka.Ni dhahiri muuliza swali atakumbana na ugumu wa aina hiyohiyo pindi akiuliza iwapo nchi yetu bado inafuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.Na haiishii hapo kwani majibu yataendelea kuwa tete pindi mtu akiuliza iwapo CCM bado ni chama cha wakulima na wafanyakazi.

Na ni katika hilo la wakulima na wafanyakazi ndipo napoona kuna tatizo la msingi.Inasemekana Azimio la Zanzibar lilihalalisha watumishi wa umma (wafanyakazi) kumiliki mali kinyume na katazo lililowekwa na Azimio la Arusha.Laiti wakati wanasiasa wetu walipokutana Zanzibar kuua Azimio la Arusha wangeangalia mbali,ni dhahiri wangebaini uwezekano wa kutokea mgongano kati ya biashara na utumishi wa umma.Haraka ya kupitishwa Azimio hilo inaweza kuwa sababu muhimu ya wanasiasa hao kutoangalia mbali.Lakini pia haraka hiyo inaweza kuwa ilichochewa na ukweli kwamba wakati wanasiasa wengi walikuwa wakituimbia ngonjera za Ujamaa na Kujitegemea majukwaani,majumbani mwao walikuwa wakicheza ngoma za ubepari.

Dhana hapo ni kwamba Azimio la Zanzibar lilipitishwa chapchap ili wajamaa wa hadharani waliokuwa mabepari wa kificho waweze kuendesha maisha yao bila hofu na bughudha ya kuonekana wanatenda kinyume na imani ya taifa letu kwa wakati huo.Hawa ni pamoja na wale ambao walikuwa wakituaminisha kwamba ni watu wa karibu na Baba wa Taifa kumbe moyoni walikuwa wakiomba dua Mwalimu aondoke madarakani ili watumie vile walivyokuwa wakikusanya kwa kificho katika zama hizo za Ujamaa na Kujitegemea.Na wengine japo Mwalimu aliwasaidia kuwaingiza madarakani akidhani ni waumini wa siasa zake,wamestaafu wakiacha skandali lukuki.

Kama kuna madhara mabaya zaidi ya mfumo wa chama kimoja basi ni kule kutoruhusu mawazo tofauti na ya watawala,hata kama mawazo hayo ni ya kuchochea maendeleo ya taifa.Kinadharia kila Mtanzania ana uhuru wa kutoa mawazo yake alimradi asivunje sheria halali za nchi,lakini kiuhalisia bado kuna chembechembe zilizorithiwa kutoka katika mfumo wa chama kimoja ambapo mawazo tofauti ni sawa na uhaini.

Katika zama za chama kimoja,hoja kama ile ya “chama kushika hatamu” zilisaidia baadhi ya mafisadi wa wakati huo kupata kinga dhidi ya wale maovu yao.Sote tulikuwa ni Watanzania tusio na tofauti,tunaoamini kwamba ili nchi yetu iendelee tunahitaji ardhi,watu,siasa safi na uongozi bora.Mwalimu aliamini kuwa hiyo ni njia sahihi ya maendeleo kwani alishuhudia namna ilivyofanikiwa sehemu kama China na Cuba.Kosa lake ni kuamini kwamba walio karibu yake walikuwa na imani ya dhati kama yeye.Angalau leo tunawajuwa wanafiki hawa,lakini kwa sababu za “kulinda umoja wa kitaifa” na kutaka “wapumzike kwa amani” tunaendelea kuwaheshimu kwa kutowaumbua hadharani.

Kumkosoa mzazi ni kosa,na kwa mwananchi wa kawaida au hata kiongozi kumkosoa Rais inaweza kutafsiriwa kuwa ni utovu wa nidhamu.Hata hivyo,kutoa ushauri kwa heshima na taadhima ni jambo linalokubalika.Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana naamini kwamba wakati Watanzania wengi wanakubaliana na mtizamo wa Rais Kikwete kuhusu kutenganisha siasa na biashara,ni vema katika utekelezaji wa dhamira yake hiyo akaweka maanani namna Baba wa Taifa alivyosalitiwa na baadhi ya watu wake wa karibu.

Nasema hivyo kwa sababu naamini hata zikiwekwa sheria nzuri namna gani za maadili ya uongozi,pasipo kutengeneza mazingira yatakayozuia wasimamizi wa sheria hizo kuzihujumu,itakuwa ni kazi bure.Mwanasiasa anaweza kabisa kutangaza kwamba biashara zake za awali zimekabidhiwa kwa wadhamini flani,lakini pasipo usimamizi mzuri mfanyabiashara huyo anaweza kuendelea kuendesha biashara zake huku akiwa mwanasiasa japo machoni mwa umma anaonekana ametekeleza sheria hiyo tarajiwa ya kutenganisha biashara na siasa.

Mfano mzuri wa ninachosema ni hili sakata linaloendelea la fedha za EPA huko Benki Kuu.Yayumkinika kubashiri kwamba kama itafikia hatua ya watu flani kupelekwa mbele ya vyombo vya sheria,kuna uwezekano watu hao wakawa ni wamiliki “hewa” ambao majina yao yalitumika tu kuficha wamiliki halali.Katika mazingira ambapo taasisi kama TAKUKURU ilikuwa ya kwanza kudai mradi wa Richmond haukuwa na harufu ya rushwa ilhali sasa tunaona suala hilo likiwaka moto huko bungeni,tutarajie nini pindi wakipewa jukumu la kuhakikisha mfanyabishara anayetaka kuingia kwenye siasa kweli amekabidhi biashara yake kwa wadhamini kama sheria itakavyokuwa inataka?

Mwisho,kikao kinachoendelea cha bunge kimeonyesha dalili kwamba baadhi ya wawakilishi wetu wamechoka kupiga mihuri kupitishwa miswada inayoonekana mizuri machoni lakini inaishia kwa mashirika kama ATC kununua ndege mbovu,TANESCO kujikuta hohehahe kwa kulipa madeni yaliyosababishwa na walafi flani wasio na uchungu na taifa au kuletewa umeme hewa ulioahidiwa na makampuni ya kisanii.Hoja hapa sio kuitupilia mbali miswada ya manufaa kwa taifa au kuchochea upinzani dhidi ya serikali bali kuwabana mafisadi wote wananaotumia nyadhifa zao kulikamua taifa letu.
BAADA YA POLITIKI ZA BONGO,HEBU ANGALIA HIZI ZA NAS KUHUSU THE N-WORD


20 Jan 2008

Makala hii ilitoka kwenye gazeti la Mtanzania siku ya Alhamisi 17Jan 2008.

Hatimaye ugavana wa Dkt Daudi Ballali katika Benki Kuu ya Tanzania umetenguliwa.Sijui kama utenguzi huo ni sawa na tunachosoma,kuona na kusikia kwenye vyombo mbalimbali vya habari kwamba Balali amefukuzwa kazi.Pengine la muhimu kwa sasa ni kwamba mtu huyo ametolewa katika wadhifa huo japo la muhimu zaidi ni kuweka rekodi vizuri kwa minajili ya kuondoa utata uliojitokeza hasa katika neno “KUTENGUA”.

Kuna wanaosema kwamba Ballali ametolewa kafara hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba sio rahisi wizi mkubwa namna hiyo uwe umefanywa na mtu mmoja tu.Ni vigumu pia kuamini kwamba uamuzi wa gavana huyo wa zamani kuyazawadia makampuni yaliyotajwa kwenye ufujaji wa fedha hizo ulifanywa na mtu mmoja pekee (Balalli).

Sakata hili lilisabaisha,linasababisha na litaendela kusababisha maswali mengi zaidi kuliko majibu.Sijui kuna wazalendo wangapi hapo Benki Kuu, lakini nashawishika kuhoji uzalendo wao kwani japo si kila mtumishi angeweza kufahamu alichokuwa akifanya Balali na washirika wake,ni dhahiri wapo waliokuwa katika nafasi ya kutoa taarifa kwa vyombo husika lakini wakaamua kukaa kimya.

Nadhani kuna waliojua kinachoendela lakini wakaa kimya kwa vile nao walikuwa washiriki katika ufisadi huo.Hawa hawana cha kujitetea kwani hawana tofauti na Balalli na wanachostahili ni adhabu tu.Kikwazo kikubwa kinachojitokeza katika uwezekano wa kuwaadhibu waungwana hawa ni ukweli kuwa baadhi yao wamepewa nafasi ya kujichunguza wenyewe (kwa vile bado wako madarakani) na sote tunaelewa kwamba hawawezi kujihukumu.Sanasana wataishia kuharibu ushahidi muhimu katika uchunguzi mzima wa ufisadi huo.

Kundi la pili ni wale waliokuwa wakifahamu kinachoendelea lakini hawakuchukua hatua kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kauli za utetezi zilizokuwa zikitolewa na watu mbalimbali pindi tuhuma za ufisadi huo zilipoanza kuibuka.Tunakumbuka kwamba kuna wakati huko bungeni lilitolewa tishio la kumfikisha Dr Slaa mbele ya vyombo vya sheria akituhumiwa kwamba ameghushi nyaraka zinazohusiana na sakata hilo.Yayumkinika kusema kwamba kauli kama hizo zinaweza kuwa ziliwakwaza baadhi ya watumishi wa Benki Kuu (waliokuwa na ufahamu wa ufisadi huo) kuripoti kuhusu uhuni uliokuwa ukiendelea hapo.
Imeripotiwa pia kwamba moja ya makampuni ya ukaguzi wa mahesabu ya benki hiyo iliripoti kuhusu kasoro zilizokuwepo lakini ikaishia kuona mkataba wake na benki hiyo ukisitishwa.Ni rahisi kukubaliana na “busara” hii kwamba kama kampuni iliyolipwa kuchunguza mahesabu imepuuzwa je “nani atanisikiliza mie niliyeajiriwa kufanya majukumu mengine katika Benki Kuu”.

Miongoni mwa madhara ya kulea ubadhirifu ni kujengeka kwa imani (miongoni mwa wasiojihusisha na ubadhirifu huo) kwamba ubadhirifu sio dhambi kwani ingekuwa haukubaliki basi wahusika wasingeendelea nao pasipo kuchukuliwa hatua.Yeyote aliyehusika na skandali hiyo lakini bado yuko madarakani ni sawa na kansa ambayo isipodhibitiwa inasambaa katika mwili mzima.Ni kama katika familia yenye watoto kadhaa na baadhi yao wanajihusisha na tabia zisizofaa.Ni dhahiri wale wanaoepuka tabia hizo (ilhali wenzao wanaendelea nazo) wanaweza kushawishika kuiga tabia hizo hususan kama wanaona wenzao wananufaika kwa namna flani.

Nakumbuka hivi karibuni,mkongwe wa siasa Mzee Kingunge Ngombale Mwiru alinukuliwa na gazeti moja akieleza masikitiko yake kuhusu namna uzalendo unavyopungua miongoni mwa Watanzania.Ni kweli uzalendo umepungua sana na tusipokuwa makini utapotea kabisa lakini kuwa na wasiwasi au kulalamika pekee hakuwezi kusaidia kurekebisha mambo.Ni dhahiri kwamba moja ya mambo yanayochangia kupungua uzalendo ni pamoja na ufisadi kama huo uliofanyika hapo Benki Kuu.

Hivi mtu atakuwaje mzalendo iwapo wakati yeye anahangaika kutafuta fedha za kumwezesha kupata angalau mlo mmoja wa siku kuna wajanja wanatumbukiziwa mamilioni ya shilingi kwenye makampuni yao pasipo kuvuja tone moja la jasho.Kibaya zaidi na pengine katika kuwaringia walipa kodi wanaoibiwa,mafisadi hawaogopi kuonyesha namna wizi wao “unavyolipa” kwa kuporomosha mahekalu ya gharama kubwa,magari ya thamani ya kutisha na vimbwanga vingine chungu mbovu.Ni kama mtu anakupora mke halafu kesho yake unamwona anatamba nae mtaani.Hii inaongeza chuki na hasira kwa aliyeibiwa.

Kila zinapojitokeza tuhuma za ufisadi huwa nashindwa kujizuia kuhoji uwezo wa TAKUKURU katika jukumu lake la kuzuia na kupambana na rushwa.Taasisi hii imekuwepo kwa muda mrefu sasa lakini bado ni legelege licha ya jitihada kadhaa zilizokwishafanywa iwe na ufanisi zaidi.Naafikiana na baadhi ya hoja kwamba matendo mengi ya ulaji fedha za umma hayafanyiki hadharani,hivyo kusababisha ugumu katika kuyabaini.Hata hivyo,katika sakata hili la ufisadi hapo BoT,tetesi zilikuwepo mtaani na magazetini kwa muda mrefu.Kama ilivyozeleka,kauli za TAKUKURU zilikuwa “taarifa hizo tunazo na tunazifanyia uchunguzi”.Ikumbukwe kwamba katika mazingira ambayo matatizo yanazaliana kila kukicha,kuchelewa kutatua tatizo moja ni sawa na kutengeneza mlima wa matatizo hayo ambapo mwisho wake itakuwa ni suala lisilowezekana kabisa kuyaondoa.

Pengine umefika wakati mwafaka kwa wawakilishi wetu huko bungeni kuhoji uhalali wa kuendelea kuwa na taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa.Kanuni ya haki katika sheria inatamka waziwazi kwamba haki sio tu itendeke bali pia ionekane imetendeka.Tunaweza kuitumia kanuni hiyo kwa TAKUKURU pia kwamba mapambano dhidi ya rushwa yasiishie tu kuwa ya dhamira bali yaonekane hadharani kuwa yapo na yana ufanisi unaotarajiwa.

Naweza kuonekana mtu wa ajabu iwapo nitashauri kuvunjwa kwa TAKUKURU lakini nina hoja ya msingi napofikiri hivyo.Mamilioni ya fedha yanayoelekezwa kwa taasisi hiyo kupambana na rushwa hayajasaidia lolote katika kupunguza tatizo hilo.Mabadiliko mbalimbali ya kisheria yaliyolenga kuipa meno taasisi hiyo nayo yameshindwa kuifanya iwajibike ipasavyo.Binafsi sioni cha ziada kinachoweza kubadili ulegelege wa taasisi hiyo zaidi ya kuivunjilia mbali na kasha majukumu yake kuhamishiwa kwenye taasisi nyingine kama vile kitengo cha upelelezi katika jeshi la polisi (CID).

Kwa kuzingatia rekodi ya TAKUKURU katika uendeshaji wa kesi inazopeleka mahakamani,sintoshangaa iwapo wanaotajwa kwenye sakata hilo wataishia kuibuka washindi kwenye kesi hizo.Tumeshuhudia namna taasisi hiyo ilivyokuwa “ikipelekeshwa” kwenye kesi dhidi ya Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia.Kama kesi ya mtu mmoja imekuwa ngoma nzito namna hiyo,tutarajie nini kwenye lundo la kesi linalowahusu watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha?

Wengi wanatafsiri vurugu zinazoendelea nchini Kenya kuwa ni matokeo ya ukabila.Lakini baadhi ya wachambuzi wa uchumi wananyumbulisha kwamba vurugu hizo ni sehemu tu ya mapambano ya kiuchumi kati ya wenye nacho na wasio nacho.Migongano ya kidini au kikabila hujichomoza zaidi kwenye jamii isiyo na uwiano wa kimapato kwani mara nyingi washiriki kwenye vurugu hizo huamini kwamba pindi zikifanikiwa zitarekebisha maisha yao ya kila siku.Tuna kila sababu ya kuzuia nchi yetu inayosifika kwa amani na utulivu isiingie kwenye machafuko yanayoweza kusababishwa na wengi wanaoona wachache wakinufaika kwa “ulafi wa kula keki ya taifa” huku wao (wengi hao) wakiendelea kutaabika.Kinachowezekana leo kisingoje kesho.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.