Showing posts with label BENKI. Show all posts
Showing posts with label BENKI. Show all posts

18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI

Asalam aleykum,

Siku za nyuma niliahidi kwamba iko siku nitawaletea stori kuhusu “mateja” wa huku Ughaibuni.Ndio,tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya linawaumiza vichwa watu kadhaa huku Ughaibuni.Kuna vijana wadogo kabisa ambao wanashawishika kujiingiza katika kubwia unga.Ni vigumu kutabiri mafanikio ya jitihada za serikali na taasisi mbalimbali katika mapambano yao dhidi ya ulevi huo haramu na hatari.

Hivi karibuni nilipewa habari za kusikitisha sana.Kijana mmoja mwenye umri usiozidi miaka 18 alikutwa amekufa huku sindano aliyoitumia kujidungia adawa ya ulevya ikiwa inaning’inia kwenye mkono wake.Huyo kijana namfahamu vizuri kwa vile siku moja aliwahi kufika hapa ninapoishi akiwa ameongozana na rafiki yangu mmoja mwenye asili ya Afrika Mashariki.Kilichonivutia zaidi kuhusu kijana huyo ni kauli zake ambazo lazima nikiri kuwa mara nyingi kwa hapa zinatolewa na wanasiasa kuliko wananchi wa kawaida.Alikuwa akionyesha kuchukizwa kwake na watu wanaowabagua wenzao kwa vile tu ni wageni au wana rangi tofauti na wao.Kimsingi,alikuwa akilaani suala zima la ubaguzi.Kwa umri wake mdogo,nilimwona kama ni mtu mwenye upeo mkubwa sana.Kwa wakati huo sikujua kabisa kuwa pamoja na busara zake,kijana huyo alikuwa akiweka rehani roho yake kwa kubwia unga.Pengine lishe bora na huduma mbalimbali zinazopatikana kirahisi ndizo zilikuwa zinamsaidia kuficha “uteja” wake,kwani kama tujuavyo wengi si vigumu kumtambua m-bwia unga kwa kumwangalia tu.

Alienisimulia kuhusu mauti yaliyomkumba kijana huyo alinijulisha kwamba aliemletea marehemu madawa hayo ya kulevya alikuwa ni rafiki yake ambae walikuwa wanasoma darasa moja.Kwa lugha nyingine,wawili hao walishirikiana katika kuleta mauti ya mmoja wao.Huo ni ushirika wa mauti,na hilo ndio linanipeleka kwenye mada yangu ya pili kuhusu ujambazi uliotokea hivi karibuni pale Ubungo uliopelekea vifo na majeraha kwa waliosalimika.

Kuonyesha yeye ni kiongozi anaewajali mno wananchi wake,matra baada ya kurejea nchini akitoka ziarani kusini mwa Afrika,Rais Jakaya Kikwete alikwenda kuwajulia hali waliojeruhiwa na majambazi katika tukio hilo la Ubungo.Mheshimiwa Kikwete alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba anaamini kuwa kulikuwa na njama ndani ya benki iliyoibiwa fedha hizo kwa vile isingekuwa rahisi kwa majambazi hayo kuvamia tu gari lenye fedha bila kuwa na taarifa sahihi.Wafanyakazi waliohusika kuvujisha taarifa za fedha hizo kwa majambazi watakuwa hawana tofauti na yule kijana aliempelekea unga rafiki yake na hatimaye kumsababisha mauti.Waliovujisha taarifa hizo walikuwa na ushirika wa mauti na majambazi waliofanya unyama huo.Hivi tunapokuwa kazini si huwa tunaunda kitu kama undugu kwa vile muda mwingi tunautumia tukiwa pamoja na pengine kushirikiana katika mambo ya nyumbani kama vile harusi na misiba?Sasa unapotoa taarifa kwa majambazi wenye silaha za moto ili kuwawezesha kuvamia gari ambalo mfanyakazi mwenzio yupo humo si ni kama unamtengenezea mauti mwenzio?Jamani,hivi fedha zinatupeleka kupoteza utu wetu na kutothamini uhai wa wenzetu!Kwa hakika walioshiriki kwa namna yoyote katika kufanikisha uporaji huo wanastahili kusakwa kwa udi na uvumba na hatimaye kupatiwa kibano wanachostahili.Kwa “waliouza ishu” hiyo kwa majambazi wanakuwa wametenda dhambi kuu mbili:kuwasaliti wafanyakazi wenzao ambao aidha waliuawa au kujeruhiwa,na pia walishiriki katika ujambazi huo kwa vile wao ndio hasa waanzilishi wa mpango mzima.Hiyo si kusema kwamba majambazi waliohusika hawana hatia,lakini iwapo waliotoa taarifa hizo wasingewajulisha majambazi kwamba siku flani,muda flani,katika gari flani kutakuwa na shilingi bilioni moja ni dhahiri kwamba tukio hilo lisingetokea.

Kwa upande mwingine,ni muhimu kwa taasisi zetu za fedha kuwa makini zaidi wanaposafirisha fedha kutoka sehemu moja kwenda nyingine.Hivi kweli benki kama NMB inashindwa kununua gari moja ambalo ni maalumu kwa ajili ya kusafirishia fedha?Uzuri wa magari kama hayo ni kwamba licha ya kutoa usalama mkubwa kwa mali inayosafirishwa,maisha ya wanaosafirisha mali hiyo nayo yanakuwa salama zaidi ukilinganisha na magari ya kawaida.Natambua kuwa yapo makampuni binafsi ya ulinzi ambayo yanamiliki magari ya aina hiyo.Lakini siwezi kuilaumu NMB moja kwa moja kwa kutokodi huduma hiyo kwa vile kumbukumbu zinaonyesha kuwa siku za nyuma walinzi wasio waadilifu walishawahi kuingia mitini na mamilioni ya fedha wakiwa katika gari maalumu la kusafirishia fedha.

Hata hivyo,kuwa na gari maalumu la kusafirishia fedha bila kuwa na watumishi waadilifu ni sawa na kulala ukiwa kwenye chandarua chenye dawa lakini kimekufunika kuanzia kichwani hadi kiunoni tu,na hapohapo kuamini kuwa unawadhibiti mbu.Uaminifu,uadilifu na kuthamini maisha ya wenzetu ni vitu muhimu sana na lazima kwa kila Mtanzania.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa makala hii.

Leo nina hasira.Muda mfupi kabla ya kuandika makala hii niliongea na mzazi wangu huko Ifakara.Akanisimulia stori mmoja ambayo kimsingi ndio iliyonifanya niwe na hasira.Hata hivyo,naomba niwatoe hofu kwamba hasira nilizonazo haziwezi kupoteza ladha ya makala hii.

Mzee ana matatizo ya moyo.Sasa kama unavyojua mambo ya miji midogo kama Ifakara.Hospitali zipo lakini wataalamu ni wachache.Lakini kwa kumbukumbu zangu wakati flani aliwahi kunieleza kwamba kuna daktari mmoja mwenye zahanati yake binafsi mjini hapo ambae inaaminika kuwa ni mtaalam wa mambo ya moyo.Katika maongezi yetu kwenye simu aliniambia kuwa moyo bado unamsumbua.Nikamuuliza kwanini asiende kwa huyo mtaalam wa magonjwa ya moyo.Jibu alilonipa ndilo lililonifanya nipandwe na hasira niliyonayo hadi sasa.Anasema kwamba jirani yake aliyekuwa akisumbuliwa na matizo ya moyo alikwenda kumuona huyo daktari hivi karibuni,lakini jibu alilopewa lilimfanya mgonjwa huyo kurudi nyumbani akiwa na ugonjwa mwingine mpya:hofu ya kufa.Kisa?Aliambiwa na mtaalamu huyo wa moyo kwamba hivi “kwanini wewe ambaye umebakiwa na wiki mbili tu za kuishi (kutokana na umri wako mkubwa) unataka kutibiwa moyo badala ya kuuacha usimame wenyewe muda ukifika”!

Laiti maelezo hayo ya mzazi wangu yangekuwa yanatoka kwa mtu wa kawaida tu nisingeamini kwamba nchi yetu ina baadhi ya watu wanaojiita madaktari ambao wanaweza kukiuka maadili ya kazi yao kwa kiwango hicho!Nadhani hata ukienda gereji na gari lililochoka sana,bado mafundi makenika watakupa matumaini ya namna flani badala ya kukibilia kukwambia kwamba ukalitupe gari lako.Na hapo tunazungumzia kitu ambacho unaweza kukinunua kipya.Maisha hayawezi kununuliwa upya.Tukirudi kwenye stori niliyopewa na mzee,basi jirani yake (ambaye si kama amekula chumvi sana) tangu alipoambiwa na daktari kwamba amebakiwa na wiki mbili kufa,amepatwa na hofu ya ajabu.Kwani kuna mtu ambaye haogopi kufa?Na hasa kama umepewa tahadhari kama hiyo na daktari.Mzee wangu baada ya kusikia stori hizo kutoka kwa jirani yake alinieleza bayana kwamba bora aendelee kuugua kuliko kwenda kwa daktari ambae amegeuka kuwa mtabiri wa urefu wa maisha ya wagonjwa.Nilimpoza kwa kumwambia kuwa naamini huyo daktari alieongea upuuzi huo hajui wajibu wake na anakiuka tu maadili ya kazi yake.

Laiti jirani ya mzee wangu angekuwa amekumbana na kioja hicho hapa Ughaibuni huenda angejikuta anapata utajiri wa ghafla endapo angefungua mashtaka dhidi ya daktari aliemtishia uhai wake.Sio siri,hawa wenzetu wanatoa kipaumbele kikubwa sana kwa suala la afya sambamba na kuhakikisha kuwa watumishi katika sekta ya afya wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata maadili.Na sio katika sekta ya afya pekee bali sehemu nyingi zinazotoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi zinabanwa sana kuhakikisha kuwa huduma hizo zinatolewa katika kiwango stahili.Pengine kingine kinachowasaidia viongozi katika taasisi mbalimbali za huduma hapa Ughaibuni ni ile tabia ya kufuatilia nini kinachoongelewa kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi zao.Mganga mkuu akisoma gazeti na kukuta malalamiko kuhusu hospitali yake,hapuuzi bali atakimbilia kumjibu mlalamikaji huyo kuwa atachunguza suala lililolalamikiwa.Na haishii kutoa ahadi tu bali hatua lazima zitachukuliwa.Lakini kinachosikitisha huko nyumbani ni ile kuona gazeti flani limeripoti kuwa hospitali flani “imeua” mgonjwa na wala husikii habari hiyo ikikanushwa au kukubaliwa na uongozi wa hospitali husika.

Sehemu nyingi zinazotoa huduma huko nyumbani zina masanduku ya kutoa maoni.Lakini lile vumbi unaloliona kwenye mengi ya masanduku hayo linatosha kuthibitisha kuwa masanduku hayo ni sawa na urembo tu kwenye makorido ya sehemu husika.Kwa mtizamo wangu,nadhani tatizo la msingi ni ile tabia iliyojengeka kwa baadhi ya watumishi kwenda kazini kuonekana tu wamekwenda kazini na mwisho wa mwezi wapate mishahara yao,na si kwenda kutumikia wale wanaowafanya wapate mshahara.Unadhani mtumishi wa benki anaejua dhahiri kwamba ni fedha za wateja ndio zinaiwezesha benki hiyo kuwepo na kumlipa mshahara,atamdharau mteja anaekuja hapo kupata huduma?Kama mtumishi anajiona hataki “kubughudhiwa” na wanaohitaji huduma kazini kwake,si alale tu nyumbani,au aache kazi?Tuone kama hatakufa kwa njaa.Kumbe basi kinachompa shibe (kazi) ni sharti akiheshimu na kukitumikia kwa moyo wake wote.

Alamsiki

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.