Showing posts with label BENSON BANA. Show all posts
Showing posts with label BENSON BANA. Show all posts

9 Oct 2010


Majuzi tumemsikia Mwenyekiti Mwenza wa REDET,Dokta Benson Bana akilipuka tena na utafiti wao wa kuchakachua kuhusu mwenendo wa uchaguzi,ambapo kwa mujibu wao wanadai mgombea wa CCM,Jakaya Kikwete anaongoza kwenye kura za maoni.

Huko nyuma nilishawahi kuandika post moja kuhusu Dokta Bana,na tabia yake ya ulipukaji.Katika post hiyo nilikuwa nazungumzia kauli ya Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwamba tuhuma zilizokithiri dhidi ya ufisadi zinaweza kusababisha taifa kukosa viongozi wazuri.Yani mhadhiri mzima alikosa busara ya kufahamu kuwa kukalia kimya ufisadi hakuwezi kusababisha taifa kupata viongozi wazuri.

Bana na Redet yake wanadhani Watanzania ni wajinga ndio maana wakakurupuka na uchakachuaji huo wakiamini wanaisaidia CCM na Kikwete.Sio ubishi wala kulazimisha matokeo tunayotaka sie bali hali halisi ya mwenendo wa kampeni inaonyesha dhahiri kuwa CCM na Kikwete wamekaliwa kooni na Dokta Wilbroad Slaa na Chadema,huku uthibitisho mkubwa ukiwa kwenye vioja kama kauli ya vitisho ya Mnadhamu Mkuu wa JWTZ Brigedia Jenerali Shimbo.

Hivi huyo Kikwete angekuwa 'anapendwa' na zaidi ya asilimia 70 ya wapiga kura watarajiwa (potential voters) angekuwa anahangaika huku na kule ku-recycle lundo la ahadi zake za mwaka 2005?

Lakini tungetarajia nini kutoka kwa Dokta Bana na REDET yake?Waseme umaarufu wa Kikwete umeshuka?Waseme Dokta Slaa anaongoza kura za maoni?Hayo hayawezekani katika utawala huu wa kifisadi unaotaka kusikia habari njema tu hata kama hazina ukweli.Tunafahamu kuwa Synovate walishindwa kutueleza nani anaongoza kura za maoni kwa vile CCM ilihofia matokeo ya ripoti hiyo yangewaadhiri.Sasa kwa vile REDET 'wameshafungulia mbwa' sintoshangaa Synovate nao wakikurupuka na ripoti yao iliyochakachuliwa itakayoonyesha Kikwete na CCM wanaongoza.

Haina haja ya kuwashutumu wachakachuaji hawa.Dawa yao iko kwa wapiga kura waliochoshwa kuona nchi yao ikigeuzwa maabara ya uchakachuaji kwenye kila eneo.Hebu pata picha iwapo kila Mtanzania aliyechoshwa na ufisadi akipiga kura ya kuwaadhibu mafisadi na hatimaye Kikwete akan'goka madarakani,Dkt Bana na REDET yake watakuwa katika hali gani!

Hilo linawezekana.Wapiga kura wasianze kukata tamaa kuwa CCM wataiba kura.Of course wataiba lakini ili 'kura zitoshe' watalazimika kufanya wizi wa 'mchana mweupe' (day light robbery) jambo ambalo sio rahisi sana,japo linawezekana.Wanaweza tu kuchakachua matokeo kama,kwa mfano Dokta Slaa akipata asilimia 51 na Kikwete asilimia 49.Hapo watarejea uchakachuaji kama ule wa Zanzibar.Lakini kama ni tofauti ya double digits,wanaweza kupatwa na kigugumizi katika kufanikisha ujambazi huo.

Ni muhimu kutovunjwa moyo na hujuma hizi.Yatupasa kufahamu kuwa Kikwete na CCM yake ni kama mgonjwa mahututi ambaye yuko tayari hata kuning'inia kwenye uzi ili asalimike.Tutashuhudia vituko zaidi ya huo uchakachuaji wa REDET au vitisho vya akina Brigedia Shimbo.Cha muhimu ni kusimamia dhamira yetu.

Inawezekana.Timiza wajibu wako

19 Apr 2010

Kuna busara moja inayotuasa kuwa mpuuzi husema kwa vile anajiskia kusema (hata kama ni upuuzi) ilhali mwenye busara husema tu pale anapokuwa na kitu cha kusema (ikimaanisha kama hana cha kusema,au haoni umuhimu wa kusema kitu,atakaa kimya. Busara zaidi zinatuasa kuwa makini na tunayosema hadharani kwa vile mara nyingi jamii humtambua zaidi mtu kwa kauli zake.Sema upuuzi,utaonekana mpuuzi.Sema ya busara,utaonekana mwenye busara.Sasa kuna huyu msomi,Dokta Benson Bana,ambaye licha ya kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam,ni mkuu wa idara ya Sayansi za Siasa na Uongozi na pia ni Mwenyekiti Mwenza wa REDET.Yayumkinika kusema Dkt Bana amekuwa mahiri zaidi wa kutoa kauli zisizoendana na wasifu wake kitaaluma kuliko umahiri wa wa usomi wake

Na leo,kwa mujibu wa habari katika gazeti la Mwananchi,msomi huyo 'amelipuka' tena kwa kauli kwamba tuhuma zilizokithiri dhidi ya ufisadi zinaweza kusababisha taifa kukosa viongozi wazuri wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba.Huhitaji kuwa na hata asilimia moja ya kiwango cha elimu ya Dkt Bana kutambua kuwa tuhuma zilizotapakaa kuhusu ufisadi ni matokeo ya kuwepo kwa ufisadi.Msomi huyu anaishi Tanzania lakini yaelekea hafahamu mazingira yanayomzunguka,na hilo linaleta wasiwasi mkubwa kuhusu mchango wa wanataaluma katika maendeleo ya nchi yetu.

Katika habari hiyo Dk Bana aliwataka watu "waaache siasa chafu za kuhubiri na kudai kuwa watuhumiwa wa ufisadi hawafai kupewa kura au kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi kana kwamba wameshathibitika".Huu ni zaidi ya ubabaishaji wa kitaaluma,na kwa kiasi flani inaaibisha Udaktari wa Filosofia tunaohenyea akina sie.Kwanza,Dkt Bana amepata wapi mamlaka ya kuwataka wananchi waache kulalamikia ufisadi?Usomi hautoi mamlaka ya kuizuia jamii kulalamikia maovu yanayoisumbua.Pili,kwa mtizamo wa msomi huyu,kwa vile tuhuma za ufisadi hazijathibitika basi watu wakae kimya hadi 'miujiza itapotokea kwa watawala wetu kuamua kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mafisadi'!Hii ni sawa na kuingiliwa ndani na kibaka halafu ukakaa kimya kwa vile tu wewe sio chombo cha sheria.Ukifanya hivyo,hata hao polisi watakuona mpumbavu na unawapotezea muda.La kufanya ni kumdhibiti kibaka au kupiga kelele kuwashtua majirani wakusaidie kumdhibiti.

Binafsi,pamoja na kuheshimu uhuru wa kutoa mawazo,nadhani tatizo kubwa la Dkt Bana ni tabia yake ya 'kusema chochote' hata kama hana cha kusema.Inaelekea aidha hafahamu athari za tabia hiyo au anapuuza tu.Matokeo yake ni kuonekana mbabaishaji wa namna flani.Si lazima jina lake lionekane magazetini au kusikika radioni kama hana la muhimu kuieleza jamii.Eti anatuasa kuwa "si vizuri kwa watu kunyimwa kura kwa sababu ya kutuhumiwa kwa ufisadi hadi hapo watakapothibitika na kutaka wanasiasa waache kuhukumu wenzao bila kosa".Kwanini hajiulizi inakuwaje watu hao wanatuhumiwa ufisadi in the first place?Kwanini ni wao na si Dokta Bana,kwa mfano?

Hivi lipi lililo muhimu zaidi kwa Tanzania kama taifa: kukosa viongozi bora kwa vile wanatuhumiwa kwa ufisadi au kupata viongozi bora watakaowajibika kulitumikia taifa kupambana na ufisadi?Wasiwasi wa Dkt Bana ulipaswa kuwa kwenye athari za ufisadi kwa jamii na sio tuhuma za wananchi dhidi ya mafisadi.Ni mlevi tu atakayeshindwa kuelewa kuwa kinachoumiza Watanzania kwa sasa ni UFISADI na sio TUHUMA DHIDI YA MAFISADI.

Mwanataaluma huyu anaongoza taasisi ya REDET ambayo mara imekuwa ikishutumiwa kwa upendeleo inapotoa taarifa za kura zake za maoni (opinion polls) kuhusu CCM na vyama vingine vya siasa.Sina hakika kuwa matokeo ya kura hizo huwa 'yanapikwa' ili kuridhisha watawala lakini kinachozua maswali dhidi ya polls hizo ni kutoendana na hali halisi na dalili za upendeleo.

Wito wangu kwa Dkt Bana ni huu: wakati mwingine jaribu kuitendea haki taaluma yako kwa kukaa kimya pale usipokuwa na cha kuongea.Kwa kufanya hivyo,utawatendea haki pia wasomi wenzako,taasisi unazoongoza na fani nzima ya usomi.Ni muhimu pia unapotoa matamshi mazito ukajitahidi kutumia theories za kusapoti matamshi hayo badala ya kutoa hisia zenye mwelekeo wa kijiweni.


.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.