Showing posts with label BERNARD MEMBE. Show all posts
Showing posts with label BERNARD MEMBE. Show all posts

29 Jan 2016

KATIKA tasnia ya ushushushu kuna kitu kinachoitwa Moscow Rules (yaani Kanuni za Moscow). Hizi ni kanuni za zama za Vita Baridi ambazo majasusi waliopangiwa kazi nchini Urusi walipaswa kuzizingatia, kwa sababu nchi hiyo ilikuwa nguli wa kukabiliana na majasusi. Moja ya kanuni hizo inasema; “Once is an accident. Twice is a coincidence. Three times is an enemy action.” Kwa tafsiri isiyo rasmi; kitu kinachojiri mara moja ni ajali; kikijiri mara ya pili ulinganifu wa bahati mbaya, sio makusudi; kikijiri mara ya tatu ni kitendo cha adui.”

Nimeanza makala hii na angalizo hilo kwani ndio wazo lililoniingia kichwani mara baada ya kusoma kauli za aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, katika Serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe.

Wiki iliyopita, Membe alinukuliwa na vyombo vya habari akimkosoa Rais Dk. John Magufuli, angalau katika maeneo matatu. Kwanza, Membe alidai kuwa kiuhalisi, Dk. Magufuli hajapunguza idadi ya wizara kama alivyoahidi bali amepunguza idadi ya mifuko, na kutanabaisha kuwa Rais hajabana matumizi yoyote kwa kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri, bali alichofanya ni kupunguza idadi ya mawaziri na sio wizara.

Alichofanya ni sawa na kuwa na mayai kumi halafu ukaamua kuyaweka kwenye mifuko kumi, maana yake ni kwamba utakuwa na mifuko kumi yenye mayai,” alisema waziri huyo wa zamani ambaye pia alikuwa miongoni mwa makada wa CCM waliowania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.

Lakini unaweza kuwa na idadi hiyo hiyo ya mayai na ukaamua kuyagawanya; mayai matatu unayaweka kwenye mfuko mmoja, mawili kwenye mfuko mwingine na yaliyobaki kwenye mfuko mmoja. Maana yake ni kwamba utaendelea kuwa na mayai kumi lakini idadi ya mifuko imepungua. Hapa sasa utakuwa hujapunguza gharama za kuyatunza hayo mayai,”aliongeza Membe.

Membe alidai kwamba Magufuli ameendeleza wizara zile zile lakini kaamua kuzikusanya pamoja, na kuona kuwa mfumo huo mpya wa wizara unaweza kuathiri uwasilishaji wa bajeti bungeni kwa vile mawaziri sasa watahitaji muda mwingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Hilo tutaliona kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka huu. Tuone kama bajeti itaongezeka au itapungua? Kwa sababu kama wizara zimepungua kama tunavyoamini, lazima bajeti ipungue, sasa bajeti ikiongezeka au ikibaki vile vile maana yake hakuna kilichofanyika,”alitahadharisha.

Eneo la pili ambalo Membe alimkosoa Magufuli ni udhibiti wa safari za nje, akidai kuwa Tanzania si kisiwa. Membe, aliyekuwa mtetezi mkuu wa safari mfululizo za Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete nje ya nchi, alisema kuwa safari za nje zina manufaa kwa taifa, na kusisitiza kuwa lazima Rais Magufuli asafiri kwenda nje ya nchi.

Tanzania si kisiwa, hata ukiwa tajiri namna gani lazima utoke nje ya nchi yako,” alisema Membe, na kutahadharisha kuwa nchi yetu inaweza kuwa kama Zimbabwe kwani ukijitenga, utatengwa.
Alisema nchi ina mabalozi 36 tu duniani kote kati ya nchi 194 zinazohitaji uwakilishi huo na kibaya zaidi, mabalozi hawaruhusiwi kuingia kwenye baadhi ya vikao, na hata wakiingia wakifika kwenye hatua ya uamuzi watazuiwa kushiriki.

Eneo la tatu ambalo japo hakumtaja Magufuli wala kukosoa moja kwa moja lakini linaloweza kutafsiriwa kama kuikosoa serikali kuhusu wafanyabiashara, ambapo alitahadharisha serikali kutowachezea.

Waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Mtama (CCM) alipongeza kasi ya Magufuli katika vita dhidi ya ufisadi na kudhibiti mianya ya kukwepa kodi lakini akatahadharisha kuhusu haja ya kuwa mwangalifu katika kuwashughulikia wafanyabiashara. Alidai kuwa wafanyabiashara wana masikitiko makubwa dhidi ya serikali, na anaona suala hilo litaibuka kwa kishindo bungeni.

Licha ya maeneo hayo matatu, Membe alizungumzia kauli ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa, aliyedai wafanyabiashara waliomuunga mkono wananyanyaswa. Alieleza kuwa si dhambi kwa wafanyabiashara kufadhili vyama vya siasa wakati wa uchaguzi, na kwamba serikali ya chama kilichoshinda uchaguzi inapaswa kuwakusanya wafanyabiashara wote na kufanya nao kazi na sio kuwaburuza.

Kadhalika, mwanasiasa huyo alizungumzia kuhusu “timua timua” ya watumishi wa umma wanaohusishwa na tuhuma za ufisadi.

Ni rahisi kumshughulikia mtu usiyemfahamu lakini siyo rahisi kumshughulikia mtu unayemfahamu,” alidai Membe, na kuongeza kuwa haitokuwa shida kwa Magufuli kuwashughulikia watendaji aliowakuta serikalini ambao kimsingi hakuwateua, na hawafahamu. Alihoji iwapo Rais ataweza kuwatimua aliowateua mwenyewe.

Kauli hizo za Membe zimezua mjadala mkubwa, hususan kwenye mitandao ya kijamii. Japo kabla yake, aliyekuwa Naibu wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Makongoro Mahanga, alimkosoa Magufuli kuhusu ukubwa wa kabineti yake, ukweli kwamba Membe bado ni kiongozi wa juu wa CCM ilhali Mahanga alihamia upinzani, unaashiria mengi.

Lakini binafsi sikushangazwa na kauli hizo za Membe, hasa kwa vile awali, katika kitabu nilichokichapisha hivi karibuni kuhusu safari ya urais wa Magufuli, mafanikio na changamoto katika urais wake, nilibainisha kuwa moja ya changamoto zinazoweza kumkabili Rais huyo wa Awamu ya Tano ni maadui wa ndani ya chama chake.

Kimsingi, hoja zote za Membe hazina mashiko. Kuhusu anachoita ukubwa wa baraza la mawaziri, la muhimu kwa Watanzania si ukubwa au udogo bali uchapakazi. Ni bora kuwa na mawaziri, manaibu na makatibu wakuu hata 1,000 wachapakazi, kuliko kuwa na serikali ndogo inayokumbatia mafisadi.
Pia Membe alipaswa kufahamu kuwa utendaji kazi wa viongozi wa serikali unategemea sana utendaji kazi na msimamo wa bosi wao, yaani Rais aliyewateua. Ni dhahiri kuwa Membe anatambua kuwa Magufuli si mtu wa porojo, mtoa ahadi anazoshindwa kuzitekeleza mwenyewe (rejea kauli ya “ninawajua wala rushwa kwa majina” ya Kikwete), na kimsingi Watanzania na dunia nzima wanafahamu kuwa kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu ya Magufuli ni tofauti na zama za nchi kujiendesha yenyewe (on autopilot).

Kuhusu safari za nje, Membe amepotoka mno, pengine kwa sababu kwa wadhifa wake wakati huo, alikuwa mmoja wa wasafiri nje ya nchi mara kwa mara. Kwanza, Rais Magufuli hajawahi kutamka kuwa hatosafiri. Kwa hiyo, kauli ya Membe kuwa lazima atasafiri ni fyongo.

Pili, zuio la safari za nje sio ‘blanket ban’ bali ni kwa safari zisizo na tija. Lakini kwa nini tushangazwe na kauli hiyo ya Membe ilhali tunafahamu misafara ya serikali iliyopita ilivyosheheni wajumbe kwa kutumia fedha za umma? Ni mtu mwenye matatizo tu anayeweza kutetea safari zenye manufaa zinazoligharimu taifa matrilioni ya shilingi huku faida tarajiwa zikiwa pungufu ya gharama husika.

Mwanadiplomasia msomi kama Membe alipaswa kuangalia hapo jirani tu kwa Rais Paul Kagame, kulinganisha idadi ya safari zake nje na zile za Kikwete kisha kuangalia hali ya uchumi kati ya nchi hizo mbili.

Vilevile ni rahisi kwa Membe kuzungumzia mafanikio ya safari hizo kwa vile ni Watanzania wachache wanaofahamu vituko vilivyoambatana na safari hizo. Ni mara ngapi safari hizo za ‘manufaa’ zilijumuisha shopping, kuhudhuria birthday parties, na matukio mengine yasiyo na tija kwa serikali?

Kuhusu wafanyabiashara, ni upuuzi wa hali ya juu kuhisi tu kuwa kuna uonevu dhidi ya mfanyabiashara yeyote. Kama kuwabana wafanyabiashara wakwepa kodi ni uonevu basi Magufuli aongeze dozi, maana hizi sio zama za Tanzania kuwa shamba la bibi.

Membe anadai wafanyabiashara wana masikitiko na suala hilo linaweza kuibuka bungeni. Anamaanisha Bunge limejaa wafanyabiashara au? Na kama masikitiko yao ni kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano kuwabana ili wasikwepe kodi na kwamba masikitiko hayo yanaweza kusababisha kupoteza wawekezaji, basi na waondoke hata kesho. Hatuhitaji wakwepa kodi nchini. Kimsingi, wanaolalamika wala hawastahili kuitwa wafanyabiashara bali wahujumu wa uchumi wetu.

Na hoja yake kuhusu ‘timua timua’ haishangazi kwani moja ya udhaifu wa serikali ambayo Membe alikuwa waziri ilikuwa ni kuwaonea aibu wanaoboronga, na matokeo yake hali hiyo ilivutia waborongaji wapya kwani walishabaini kuwa hakuna wa kuwachukulia hatua. Hivi Membe anaweza kutuambia lolote kuhusu ahadi ya Riais Kikwete aliyoitoa Februari 2006 kwamba anawafahamu wala rushwa kwa majina na anawapa muda wajirekebishe? Sawa, Magufuli alipoingia Ikulu alikuta orodha hiyo ya wala rushwa aliowajua Kikwete na kuamua kuifanyia kazi?

Nimeeleza awali kuwa nimelizungumzia suala hilo kwa kirefu kitabuni. Sitaki kabisa kuamini kuwa kauli za Membe ni zake peke yake. Hisia zinanituma kuamini kuwa huu ni moshi tu unaoashiria moto unaowaka ndani kwa ndani ya CCM kati ya makundi makuu mawili: la Hapa Kazi Tu la Magufuli linalotaka kuiondoa Tanzania katika lindi la ufisadi unaoifanya nchi yetu kuzidi kuwa masikini, na kundi la wanufaika wa ufisadi linalomwona Magufuli kama mtu anayewaziba pumzi. Naam, ufisadi ni ‘lifeline’ ya watu walioigeuza nchi yetu Shamba la Bibi, wakivuna wasichopanda.

Nimalizie makala hii kwa kutoa wito kwa makada wa CCM, ambao wengi wao wanaimba Hapa Kazi Tu, lakini wakisikia madhambi yaliyofanywa na mwana-CCM fulani wanakimbilia kuwanyooshea vidole wapinzani. Wapinzani wakuu wa Magufuli hawapo Chadema au nje ya nchi bali wapo ndani ya chama hicho tawala. Na njia pekee ya kupambana nao ni kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya kutanguliza umoja na mshikamano wa chama. Kuna usemi mchawi akimaliza kuroga mtaa hugeukia familia yake. Majipu yaliyomo ndani ya CCM yasipotumbuliwa mapema yatamkwaza Magufuli na nchi yetu kwa ujumla.


28 Nov 2013


MAKALA hii ni mwendelezo wa ile iliyochapishwa katika toleo lililopita la gazeti hili, iliyobeba kichwa cha habari ‘Nani kinara wa CCM urais 2015?’
Lakini kabla sijaingia kiundani, nadhani ni vema nikarejea nilichoandika katika makala iliyopita kuhusu kukua kwa uwezekano wa CCM kubaki madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu ujao. Wiki iliyopita ilishuhudia chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA, kikiingia katika mtafaruku mkubwa ambao licha ya kutishia uhai wake unazidi ‘kupapalia’ mazingira mwafaka ya ushindi kwa CCM.
Awali, CHADEMA ilitangaza kuwavua madaraka viongozi wake waandamizi watatu, Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba na kuwapa siku 14 kujieleza kwa nini wasivuliwe uanachama baada ya kupatikana kwa nyaraka inayodaiwa kulenga kukihujumu chama hicho.
Jumapili iliyopita, Zitto na Kitila waliitisha mkutano na waandishi wa habari ambao kimsingi haikusaidia japo kupunguza moto unaozidi ‘kuunguza nyumba ya CHADEMA.’ Kwa kifupi, wanasiasa hao wawili walipinga vikali shutuma zilizoelekezwa kwao na kuhalalisha kile kilichotafsiriwa na uongozi wa chama hicho kama hujuma, huku wao wakibainisha kama matumizi ya demokrasia kwa minajili ya kuiboresha CHADEMA.
Pasi haja ya kuingia kwa undani katika sokomoko hilo, ni wazi kwamba uamuzi wa kuwavua madaraka viongozi hao na msimamo uliotolewa na ‘wahanga’ hao unaendeleza mapambano ya madaraka ndani ya CHADEMA. Kubaki au kuondoka kwa akina Zitto hakuwezi kukirejesha chama hicho katika mahala kilipokuwa. Kibaya zaidi, japo hakuna tathmini yoyote iliyokwishafanywa kuhusu athari za mgogoro huo, ni wazi Watanzania wengi wameanza kupoteza matumaini kwa chama hicho kilichotarajiwa sio tu kutoa upinzani mkubwa kwa CCM bali pia hata kuweza kuingia Ikulu mwaka 2015.
Nihitimishe suala hili la CHADEMA kwa kutanabaisha kuwa japo inafahamika kuwa lolote linawezekana katika siasa, ukweli kwamba tumebakiwa na takriban mwaka na ushee tu kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao, sambamba na ukweli kuwa hakuna dalili ya mgogoro huo wa CHADEMA kumalizika hivi karibuni, itakuwa vigumu mno kwa chama hicho kujipanga upya na vyema, kuweza kutoa ushindani wa maana katika Uchaguzi Mkuu ujao. Nitaijadili kwa kirefu hatma ya CHADEMA katika makala zijazo.
Tukiendelea na mada ya urais kwa tiketi ya CCM, niliahidi kuwa wiki hii nitajadili ‘odds’ (uwezekano wa kufanikiwa au la) zinazowakabili wanasiasa wawili ambao tathmini yangu inawaona kama ndio vinara katika mbio za kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete kupitia CCM, yaani Edward Lowassa na Bernard Membe.
Pengine hadi siku chache zilizopita, kikwazo kikubwa kwa wote wawili kingeweza kuwa uwezekano wa CCM kubwagwa na CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu ujao. Lakini kwa kuzingatia mwenendo ulivyo katika chama hicho kikuu cha upinzani, yayumkinika kuhitimisha kuwa kikwazo hicho ni kama kimekufa kifo cha asili.
Kwa upande wa Lowassa, doa kubwa linaloonekana kuendelea ‘kuchafua’ jina na wasifu wake ni tuhuma za ufisadi wa Richmond. Bila kujali kuwa uamuzi wake wa kujiuzulu uwaziri mkuu kufuatia kashfa hiyo ni ‘kutolewa kafara’ au ‘alivuna alichopanda,’ tafsiri ya haraka kwa wananchi wengi wa kawaida inabaki kuwa ‘ni vigumu kumtenganisha mwanasiasa huyo na moja ya matatizo makubwa kabisa yanayoikabili nchi yetu, yaani ufisadi.’
Ukweli kwamba Tanzania yetu sio tu ni moja ya nchi masikini sana bali pia inazidi kuwa masikini huku ufisadi ukizidi kushamiri, umesababisha kujengeka kwa hisia (pengine zisizopendeza) kuwa kila mwenye uwezo wa kifedha ni fisadi. Hisia hizo hazimsaidii Lowassa ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa mstari wa mbele katika harambee za kuchangisha mamilioni ya fedha hususan kwenye taasisi za dini. Badala ya ukarimu wake kumjenga kama kiongozi anayejali, kuna wanaotafsiri jitihada zake hizo kama ‘rushwa’ ya kutaka urais mwaka 2015.
Kadhalika, kuna hisia hasi kuwa hata hizo fedha anazotoa kusaidia miradi mbalimbali ‘ni chafu’ kwa maana ya hisia kuwa huenda ni zile zilizotokana na tuhuma za ufisadi. Kibaya zaidi, kutofahamika chanzo cha kinachotajwa kama utajiri mkubwa wa mwanasiasa huyo kunaimarisha hisia hizo za ufisadi.
Vile vile, na hili linawagusa wote-Lowassa na Membe- ukweli kwamba wanasiasa hao wanatajwa kama sehemu muhimu ya ‘mtandao’ uliomwingiza madarakani Rais Kikwete mwaka 2005, unaleta hisia za ‘mvinyo mpya kwenye chupa ya zamani’ (kwa wasiofahamu, thamani ya mvinyo inaelemea sana kwenye ‘ukale’ wake na si upya wake)
Sasa, kama tukiafikiana kuwa mtizamo wa Watanzania wengi ni kuwa utawala wa Kikwete (ambao uliingizwa madarakani na ‘mtandao’ uliowashirikisha Lowassa na Membe) umetawaliwa zaidi na tuhuma za ufisadi huku hali ya maisha ya Mtanzania ikizidi kuwa ngumu, kwa nini basi watu hao wapewe fursa ya kuboronga mambo zaidi?
Faraja kubwa kwa Lowassa (na hata Membe kwa ‘uhusika wake katika mtandao) kuhusu tuhuma za ufisadi ni ukweli mchungu kuwa Watanzania ni wepesi kusahau ‘mabaya.’ Wanasiasa wetu wengi wanafahamu kuhusu udhaifu huo ambao kwa kiasi kikubwa umewasaidia wengi kuendelea kuwapo madarakani licha ya ‘madudu’ yao.
Iwapo ‘kete ya fedha’ niliyobainisha katika makala iliyopita kuwa inamsaidia sana Lowassa itaendelea kutumika, basi kuna uwezekano mkubwa wa mwendelezo wa ‘who cares?’ (nani anajali?) ambapo mahitaji ya muda mfupi kama vile sukari, khanga, mchele na mengine kama hayo yatafunika mahitaji ya muda mrefu kama vile kuondokana na umasikini sambamba, kupambana na ufisadi, na hatma ya taifa letu kwa ujumla.
Kwa upande wa Membe, kikwazo kikubwa kwake ni kutokuwa maarufu ndani na nje ya CCM. Na ukubwa wa kikwazo hicho unatokana na ukweli kwamba ‘mpinzani’ wake, yaani Lowassa, ni mwanasiasa maarufu kuliko wote ndani ya CCM hivi sasa (bila kujali umaarufu huo ni stahili au la). ‘Wajuzi wa mambo’ wanaeleza kuwa inahisiwa Lowassa anaungwa mkono na zaidi ya asilimia 75 ya viongozi wa chama wenye uwezo wa kufanya uamuzi, huku wengi wao wakiwa watu waliofanyiwa fadhila zilizosababisha wawepo madarakani hivi sasa.
Tegemeo pekee kwa Membe dhidi ya Lowassa ni lile nililogusia katika makala iliyopita; nafasi ya Idara ya Usalama wa Taifa katika kumpata mgombea urais ajaye (ndani ya CCM). Kama kuna kitu chochote kinachoweza kumzuia Lowassa kuingia Ikulu, na pengine kumsaidia Membe kupata fursa hiyo, ni pale Idara hiyo itakapoamua ‘kumbeba mwenzao’ (Membe ni shushushu mstaafu). Na hilo si gumu kama inavyoweza kudhaniwa. Moja ya maeneo ambayo mashushushu wetu wanayomudu sana ni hujuma (sabotage) na uzandiki (subversion).
Ni hivi, kwa vile tayari kuna hisia za ‘uchafu’ kuhusu Lowassa (yaani tuhuma za ufisadi) basi haitokuwa vigumu kwa mashushushu kuzikuza na kuziendeleza katika namna ya kile kinachofahamika kama character assassination. Lakini kwa vile Lowassa bado yupo katika ‘himaya’ ya Idara ya Usalama wa Taifa (kama waziri mkuu wa zamani, anapatiwa huduma za ulinzi na Idara hiyo) ni rahisi kwa mashushushu kuibua mengi (ya kweli au hata ya kutunga) dhidi yake, iwapo wataona haja ya kufanya hivyo.
Kwa hiyo, kwa kifupi, kufanikiwa kwa Membe kutategemea kukwama kwa Lowassa. Na pengine katika hatua hii, ni vema nikitanabaisha waziwazi kuwa mwana-CCM anayeongoza katika kinyang’anyiro hicho ni Lowassa akifuatiwa kwa karibu kiasi na Membe.
Nihitimishe makala hii kwa kueleza kuwa mada hii ni endelevu, kwa maana ya kuwa nitaendelea na uchambuzi na mjadala huu kadri tunavyoelekea Uchaguzi Mkuu ujao. Hata hivyo, ninapenda kurejea tena mtizamo wangu kuwa CCM kurejea tena madarakani mwaka 2015 ni janga kwa Watanzania. Chama hicho tawala sio tu kimeishiwa na kila mbinu ya kuongoza nchi lakini pia hakipo kwa ajili ya maslahi ya Watanzania. Na kama uchambuzi huu ulivyoonyesha kuwa uwezekano mkubwa wa aidha Lowassa au Membe kuwa mgombea kwa tiketi ya chama hicho ni kwa aidha fedha au ‘sanaa za giza’, yeyote kati yao atakapopata urais hatokuwa tofauti na utawala uliopo madarakani hivi sasa ambao nao ulitumia mbinu ya ‘mtandao.’
Kwa bahati mbaya au makusudi, watu tuliodhani wangeweza kutusaidia kuiondoa CCM madarakani, yaani CHADEMA, wanaonekana kuwa ‘bize’ kupigana ngwala kugombea madaraka ndani ya chama chao. Sasa kama zoezi dogo tu la kupata uongozi wa chama linasababisha ‘watiane vidole machoni’ kwenye uongozi wa nchi itakuwaje? Ni ukweli mchungu lakini usioepukika na hivyo ni vema kujiandaa kisaikolojia kuendelea kuwa chini ya utawala wa CCM (ninatamani kuwa na suluhisho mbadala lakini sijalipata hadi muda huu)

Soma zaidi kuhusu:

- See more at: http://raiamwema.co.tz/nani-kinara-wa-ccm-urais-wa-2015-ii#sthash.RAQui2j5.dpuf

24 Nov 2013


KAMA nilivyoahidi katika makala yangu ndani ya toleo lililopita la gazeti hili maridhawa, wiki hii nitafanya uchambuzi kuhusu kinyang’anyiro cha kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2015.
Kwa wanaofuatilia safu hii, niliwahi kugusia mada hii katika toleo la Oktoba 26, 2011 ikibeba kichwa cha habari “Mizengwe na mitego ya mgombea urais kutoka CCM.” Mengi yametokea kati ya wakati huo na sasa, na kwa vile Uchaguzi Mkuu unazidi kujongea, nimeona ni muhimu kurejea tena mada hii.
Pengine msomaji unaweza kubaini mabadiliko kidogo katika mtizamo wangu kuhusu uwezekano wa CCM kung’oka madarakani 2015. Ninaomba kukiri kwamba chokochoko zisizo na msingi zinazoendelea ndani ya chama kikuu cha upinzani (na tegemeo la wengi kuiondoa CCM madarakani, CHADEMA, zinanifanya nikubaliane na ukweli mchungu kuwa fursa za chama tawala kushinda tena katika uchaguzi mkuu ujao zinazidi kuongezeka.
Na moja ya mambo ya kusikitisha zaidi kuhusu CHADEMA ni kuibuka kwa kundi la ‘wahuni wa kisiasa’ waliojipachika joho la uanaharakati. Kwa wababaishaji hao, kuanza kukubalika kwa chama hicho kumetoa fursa kwao kufahamika kwa namna moja au nyingine. Ni tatizo lilelile sugu katika jamii yetu la kusaka umaarufu hata kwa mambo ya kipuuzi, Waingereza wanasema ‘famous for nothing.
Sasa ‘wahuni’ hawa wamebinafsisha ajenda ya CHADEMA kupambana na ufisadi na kujipa hakimiliki kuwa wao pekee ndio wenye uelewa na mbinu za kukiwezesha chama hicho kufanikisha ajenda hiyo. Pasi kujali madhara ya uhuni wao kwa hatma ya chama hicho, wamejikuta wakitumiwa na maadui wa CHADEMA kwa njia isiyo ya moja kwa moja - kwa ‘remote control.’
Lakini kuashiria kuwa chama hicho kina wakati mgumu japo uongozi wake wa juu unaendeleza porojo za “njama za CCM na Usalama wa Taifa,” imefika mahala Mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya mkoa anabandika tuhuma nzito dhidi ya Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, kwenye blogu yake. Hivi pamoja na madudu ya CCM unatarajia ‘utoto’ wa aina hiyo?
Tuelekee huko CCM sasa. Kwanza ninaomba kuweka bayana kuwa uchambuzi huu umeelemea katika uelewa wangu wa siasa za huko nyumbani, maongezi yangu na watu walio karibu na siasa hizo, na taarifa mbalimbali katika vyombo vya habari (vya ‘asili’ na vya ‘kisasa’)
Kwa mtizamo wangu, hadi muda huu wanasiasa wawili wanaoongoza katika kinyang’anyiro cha kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete hapo 2015 ni aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Kwa ‘pembeni’ kidogo kuna Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta. Kimsingi, majina mengine yanayosikika kama William Ngeleja, John Magufuli na wengineo ni ya ‘kuchangamsha gumzo’ zaidi kuliko kuwa na uzito wowote wa maana.
Pengine baadhi ya wasomaji wangetamani nisiandike hivi lakini kimsingi hauepukiki, kama mazingira yatabaki kama yalivyo muda huu (constant) ni vigumu kwa mwanasiasa yeyote yule ndani na nje ya CCM kumzuia Lowassa kuwa rais mwaka 2015. Ninaomba nikiri kuwa ninatamani isiwe hivyo (kwa sababu binafsi ninaamini kuwa hafai kuwa Rais) lakini ukweli una tabia moja: kuuchukia hakuufanyi uwe uongo.
Turufu kubwa ya Lowassa ni uwezo wake mkubwa wa kifedha japo mwenyewe amekuwa akikanusha na kudai kuwa mamilioni anayoyamwaga katika harambee mbalimbali ni michango ya rafiki zake (hajawahi kuwataja wala kutueleza vyanzo vya utajiri wao).
Inaelezwa pia kuwa mwanasiasa huyo amejijenga mno ndani ya CCM kiasi cha kuwa sahihi kuhitimisha kuwa ana nguvu zaidi ya Mwenyekiti wa Taifa, Kikwete.
Sasa, huhitaji japo kozi ya muda mfupi ya siasa za nchi yetu kufahamu kuwa katika zama hizi fedha ndio nyenzo muhimu zaidi ya kumwezesha mwanasiasa kushinda uchaguzi kuliko kitu chochote kile. Mpigakura mwenye njaa hana habari na sera ya chama bali anachofikiria ni pishi ya mchele, doti ya khanga au kilo ya sukari.
Kwa upande wa Membe, turufu zake muhimu zaidi ni tatu. Kwanza, nafasi yake kama Waziri wa Nje inamweka karibu sana na Rais Kikwete kwani wanasafiri pamoja takriban katika kila ziara ya Rais nje ya nchi. Huhitaji kuwa mdadisi kufahamu kuwa watu wanaosafiri pamoja kwa miaka 10 mfululizo wana ukaribu kiasi gani.
Pili, kuna taarifa zisizo rasmi kuwa Membe anaungwa mkono na familia ya Kikwete. Katika moja ya mahojiano, mmoja wa watoto wa Kikwete, Ridhiwani, alikiri bayana kuwa anadhani Membe anaweza na anafaa kuwa Rais. Siasa za kifamilia zinaweza kubadilika lakini kwa angalau kwa sasa hali ipo hivyo.
Tatu, na kwangu hii ndio turufu muhimu zaidi, Membe ni ‘shushushu mstaafu.’ Pengine ni vigumu kuelezea kwa undani umuhimu wa kigezo hiki, lakini kwa kifupi, ni vigumu sana kwa mwanasiasa kuingia Ikulu pasi kuungwa mkono na Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi husika (angalau katika ‘demokrasia changa’). Mashushushu, kama watumishi wengine wa vyombo vya dola, wana tabia moja ya kumuunga mkono ‘mwenzao.’
Lakini sambamba na hilo ni kile kinachofahamika kama ‘sanaa za giza’ (dark arts), yaani kwa lugha ya kawaida, zile mbinu zinazosababisha kura kuyeyuka katika mazingira ya ajabu. Tukiamini kuwa mashushushu watamuunga mkono Membe, kwa nini basi wasiende mbali zaidi kuhakikisha kuwa anashinda kwa ‘gharama yoyote’ (na ‘gharama’ hapa si lazima iwe fedha)?
Kwa hiyo licha ya uwezo mkubwa wa kifedha wa Lowassa (tukiweka kando kukanusha kwake kuwa yeye si tajiri), Membe anaweza kumshinda kwa mbinu (ambazo kwa mtizamo wangu zinaweza kuhusisha watumishi wa sasa na wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa)
Kuhusu Sitta, nafsi yangu inanituma kuamini kuwa haitokuwa jambo la kushangaza endapo miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 tukakutana na kichwa cha habari kama hiki “Sitta: Lowassa ni chaguo la Mungu.” Kwa nini nina hisi hivyo? Binafsi ninamwona kama mwanasiasa asiyeaminika, anayeendeshwa na siasa za kusaka umaarufu na hata ‘rahisi kutulizwa.’ Kwa kifupi, Sitta anaendeshwa zaidi na imani (kuwa anaweza kuwa rais) kuliko uhalisia.
Kwa Sumaye, japo pengine ni mapema mno ‘kumpuuza,’ nafasi pekee ya yeye kuwa rais ni nje ya CCM. Tatizo kubwa kwa mwanasiasa huyu ni kwamba lugha anayoongea haieleweki ndani ya chama hicho. Naam, amejitokeza kuwa msemaji wa wanyonge na mkemeaji mkubwa wa ufisadi lakini sote tunafahamu kuwa hiyo sio sera ya CCM (angalau kwa vitendo na si kauli za majukwaani).
Nafasi hairuhusu kuangalia ‘odds’ dhidi ya Lowassa na Membe (ninataraji kufanya hivyo katika matoleo yajayo), lakini muda mfupi kabla ya kuandaa makala hii nilishiriki katika mjadala mzito kuhusu hatma ya Tanzania yetu hususan jinsi ya kuzuia uwezekano wa kumpata Rais atakayetokana na rushwa. Pia tulijadili tatizo la rushwa na namna ya kulimaliza.
Kwa bahati nzuri, mjadala huo uliofanyika katika mtandao wa kijamii wa Twitter ulimvutia mwanasiasa kijana na Mbunge wa Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki, Abdullah Mwinyi. Kwa kifupi, alitueleza kiini cha tatizo la rushwa, na nini kinaweza kufanyika kupambana na tatizo hilo sugu. Bila kuingia undani kuhusu mjadala huo, ulipofikia tamati takriban kila mshiriki alikiri kuwa “kumbe CCM bado ina hazina zaidi ya hayo majina tunayoyasikia kila siku.”
Je, wanasiasa kama Abdullah, mtoto wa Rais wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi wanaweza kuwa chaguo mbadala (alternative choice) hasa ikizingatiwa kuwa hawana ‘mawaa’ kama ya Lowassa au Membe (nitayajadili mbeleni)?
Nihitimishe makala yangu kwa kusisitiza jambo moja: japo kwa jinsi hali ilivyo ni muhimu kujiandaa kisaikolojia kuiona CCM ikiendelea kuwa madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu ujao, bado kuna umuhimu mkubwa kwa chama hicho kikongwe kupumzishwa kwani kimeshindwa kazi.
Si Lowassa, Membe, Sitta au Sumaye anayeweza kuibadili CCM irejee misingi aliyoasisi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Tegemeo dogo katika chama hicho ni damu mpya kama za akina Abdulla Mwinyi, japo pengine ni mapema mno kuhitimisha hilo.
ITAENDELEA...


- See more at: http://raiamwema.co.tz/nani-kinara-wa-ccm-urais-wa-2015#sthash.fO09a0nd.dpuf

7 Aug 2013



 

Picha kwa hisani ya Ndugu ASSAH MWAMBENE, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali


26 Jun 2013

The Minister for Foreign Affairs and International Cooperation, Hon Bernard Membe has paid tribute to the ailing South African Father of the Nation, Mr Nelson Mandela saying Africa and the world still needs a healthy Mandela and his wisdom.

Speaking in a live Radio Clouds interview in Dar es alaam yesterday the Minister said Mr Mandela is one of the statesman on record for devising a successful peace and reconciliation with people who jailed him for nearly three decades.

"The world needs Mandela and pray to God for his quick recovery" the Minister noted in the Clouds' most popular program ' power breakfast'.

The Minister also said in the next one week Tanzania is going to host three major events, starting with the Smart partnership dialogue, the historic visit of the US President, Baraka Obama and First ladies Summit to be attended by George W. Bush, the former US President and his wife Laura.

Source: Mr Assah Mwambene, Director of Tanzania Information Service (Maelezo)/ Government Spokesman


4 Nov 2011



Waziri Membe asema kama ni misaada yao basi
Raymond Kaminyoge 
TANZANIA imesema ipo tayari kukosa  misaada yote kutoka Serikali ya Uingereza  na kamwe haiwezi kuruhusu sheria inayotambua mashoga na kuhalalisha ndoa za jinsia moja.Msimamo huo mzito wa serikali umekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kutamka kwamba nchi yake ina mpango wa kusitisha misaada yake kwa nchi ambazo sheria na katiba zao, hazitambui mashoga na ndoa za jinsia moja.

Cameron alikaririwa akithibitisha kuwa tayari amewajulisha juu ya suala hilo Wakuu  wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola waliokuwa wakihudhuria mkutano wa Jumuiya hiyo uliomalizika siku nne zilizopita,  mjini Perth , Austaralia ambao pia ulihudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete.

Waziri Mkuu huyo kutoka chama cha Conservative ambacho kilishinda uchaguzi Mei mwaka jana, alisema  suala hilo la mashoga na ndoa za jinsi moja ni moja ya mambo yanayoongoza sera ya serikali yake kuhusu misaada kwa mataifa mbalimbali na kwamba tayari imeanza kutekelezwa katika maeneo kadhaa duniani.

Kauli ya Cameron imechukuliwa kama kielelezo cha ukoloni mamboleo ambao Uingereza inajaribu kuupandisha daraja  kwa mataifa yanayoendelea kwa kigezo cha misaada  

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe,  alisema pamoja na umasikini wake, Tanzania kamwe haitaruhusu upuuzi huo kwa kigezo cha misaada.

“ Tanzania ni nchi maskini lakini hatutakubali kuruhusu upuuzi huo eti kwa sababu ya misaada yake na fedha zao, lakini ushoga si utamaduni wetu, hata sheria zetu zinakataa,” alisema Membe.

Alifafanua kuwa katika kuonesha msimamo wa kutokukubaliana na masharti hayo, Tanzania imeshikilia msimamo thabiti kupinga  upuuzi huo ambapo  Januari mwaka huu,  ilimkataa balozi shoga ambaye aliteuliwa na nchi yake kuja kuiwakilisha hapa  nchini. Hata hivyo Waziri Membe hakutaja jina la balozi huyo wala nchi  anayotoka.
“Niwape siri moja ambayo tuliificha lakini leo ngoja niwaambie, mwanzoni mwa mwaka jana nililetewa barua  kunijulisha ujio wa balozi mmoja anayekuja kuiwakilisha nchi yake, mwanamume mwenye ndoa ya jinsia moja. Nilikwenda kumweleza Rais Jakaya Kikwete kuhusu wasifu wa balozi huyo mtarajiwa naye akajibu kwa maneno matatu, yarabi toba! Mkatae!” 
Waziri Membe alifafanua kuwa serikali ilimkataa balozi huyo kwa kuwa ni kinyume cha utamaduni wetu na sheria za nchi kuwa na watu wenye tabia hizo.

Alisema alimjulisha waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kwamba balozi huyo haruhusiwi kuja kufanya kazi nchini kwa kuwa ni kinyume na utamaduni wetu.  “ Waliendelea kuniomba kwamba balozi huyo akija hatatoka kwenye makazi yake akiwa na mwenza wake hivyo watu hawatamuona lakini tulimkataa kabisa, wakatuelewa,” alisema Membe.

 Alieleza kuwa  tamko hilo la Waziri Mkuu Cameron linaweza kusababisha hatari ya kuvunjika kwa uhusiano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola na koloni mama  Uingereza na waziri huyo atabeba lawama hizo

 Akisisitiza msimamo huo wa serikali, Membe,  alisema  Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha tisa, kinatambua ndoa ya jinsia mbili tofauti,  yaani mume na mke.  “ Sheria hizi tunazozitumia hivi sasa tumezirithi kutoka Uingereza ambako leo wanatukuza ndoa za jinsia moja na ushoga,” alisema Membe.
Suala la kile kinachoitwa haki za binadamu kuhusu ushoga ilikuwa moja ya ajenda ambazo viongozi kadhaa walishindwa kuafikiana katika mkutano  Perth .
Hoja ya  kukomesha vizuizi dhidi ya ushoga na ndoa za jinsi moja lilikuwa moja ya mapendekezo yaliyokuwamo katika ripoti ya ndani kuhusu matarajio ya baadaye ya Jumuiya hiyo ya Madola.
  
Itakumbukwa kwamba, Malawi tayari imeathirika na mpango huo wa Uingereza kwa sehemu ya misaada yake kusitishwa kutokana na msimamo wa nchi hiyo kuhusu kile Uingereza na nchi za Magharibi zinazokiita haki za mashoga. Ikumbukwe pia kuwa, mjadala mzito ulioibuka katika Bunge la Uganda mwaka 2009 kuhusu ndoa za jinsi moja ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa sera hiyo ya Uingereza na washirika wake.
CHANZO: Mwananchi

9 May 2011



Mkutano wa tatu wa Diaspora umemalizika majuzi jijini London huku,kama ilivyokuwa kwa Diapora I na Diaspora II,tumeishia kushuhudia zaidi picha za matukio kuliko maelezo ya mambo muhimu yaliyojiri katika mkutano huo (if there were any).Sina tatizo na watu wanaopenda kupiga picha na viongozi kwani huo ni uhuru wao wa kikatiba.Hata hivyo,nina tatizo kubwa na wale wanaodhani picha na viongozi ni muhimu kuliko kuwabana viongozi hao,hususan wanaposhindwa kutoa maelezo ya kueleweka.

Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe amekuwa sura iliyozoeleka kwenye mikutano hiyo ya Diaspora.Kwa wadhifa wake,ni mtu mwafaka kuiwakilisha serikali,sambamba na kusikia maoni,ushauri,maswali,nk kutoka kwa Watanzania wanaoshi nje ya nchi.Lakini kwa mwenendo wa ushiriki wake kwenye mikutano hiyo,yayumkinika kusema kuwa Membe amekuwa kama mtalii tu wa kutoa porojo moja baada ya nyingine badala ya kuwaeleza washiriki wa Diaspora Forums mafanikio yaliyokwishapatikana kutokana na uwepo wake au umuhimu wa mikutano hiyo (kama upo).

Usanii wa kwanza wa Membe ni katika kauli yake kuwa moja ya changamoto zinazoikabili serikali anayoitumikia ni kujua idadi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi.Huu ni usanii wa kitoto kwa vile Watanzania hao hajawaanza kuja nje wiki iliyopita,wala balozi za Tanzania nje-ambazo Membe ameziagiza kubuni mikakati ya kuwezesha kupata idadi ya Watanzania wanaoishi nje-hazijafunguliwa mwezi huu.

Badala ya kupachika jina la CHANGAMOTO,Membe alistahili kueleza bayana kuwa kutofahamika kwa idadi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi ni moja tu ya UZEMBE ULIOZOELEKA kwenye balozi zetu.Ni uzembe kwa vile umuhimu wa kufahamu idadi hiyo ya wana-diaspora umekuwepo tangu zamani hizo na sio mwaka huu tu au kwenye Diaspora Forums pekee.

Laiti washiriki wa Disapora hiyo wangekuwa serious,wangemkalia kooni Membe kumhoji kwanini zoezi hilo la kufahamu Watanzania waliopo nje ya nchi halijafanyika huko nyuma,na kwanini tuamini kuwa sasa litafanyika?Ikumbukwe Membe amekuwa Waziri wa Nje kwa miaka sita sasa,hivyo kukurupuka wiki iliyopita kukumbuka umuhimu wa kuwa na idadi ya Watanzania nje ya nchi ni sehemu tu ya ubabaishaji wake.

Membe anadai kuwa sababu ya yeye kuja London kuhudhuria mkutano huo ni kukusanya hoja kutoka kwa wadau ili ziweze kusaidia tatizo la Diaspora kupelekwa Bungeni na hatimaye kuingizwa kwenye Katiba.Come on,Membe!That's too cheap politicking even in your own standards.Yaani kukusanya hoja za Watanzania wanaoishi ughaibuni ni lazima kufanywe na waziri ilhali tuna balozi zetu na vyama mbalimbali vya Watanzania?

Na hata tukimpa Membe benefit of a doubt,kwanini asituambie namna alivyokwisha shughulikia hoja alizokusanya kwenye Diaspora I na Diaspora II kabla ya kukurupuka na usanii mwingine kwenye Diaspora III?Kama hoja za nyuma hazijafanyiwa kazi,how come hizo mpya au mwendelezo wa zile za zamani zitashughulikiwa sasa?

Japo Membe anastahili lawama,lakini washiriki wa Diapora Forums nao wanapaswa kulaumiwa kwa kuruhusu cheap lies kutoka kwa same crooked politicians year in year out.Yayumkinika kuamini kuwa udhaifu wa wahudhuriaji wa Diaspora Forums kuuliza maswali magumu yanayostahili majibu ya msingi unachangia sana kumfanya Membe awe "MGENI RASMI WA KUDUMU" kwenye mikutano hiyo kwani anajua he would easily get away with usanii wake.Unadhani angejua kuwa atakaliwa kooni kuhusu ubabaishaji wake,kwa mfano kwenye suala la dual nationality,angetia mguu kwenye Diaspora Forum iliyopita majuzi?

Lakini kilichonikera zaidi katika usanii wa Membe ni kauli yake ya kitoto kuwa eti changamoto nyingine inayoikabili Diaspora ni "WATU WENGI HAWAFAHAMU VIZURI MAANA YA DIASPORA".Utterly rubbish!Hivi Membe anaweza kutueleza amejuaje kuwa watu wengi hawafahamu maana ya Diaspora?Au,je anaweza kutuambia kwanini hawafahamu maana ya neno hilo ambalo lipo kwenye kamusi?Ungetarajia waliohudhuria mkutanio huo wamzomee Membe kwa kauli hiyo isiyo na kichwa wala miguu.Na Membe ana lipi la kutuambia katika madai yake kuwa neno Diaspora halifahamiki kwa wengi,i.e. kutofahamu maana ya neno hilo kunakwamishaje maazimio ya Diaspora Forums zilizopita?

Haya ndio matatizo ya kualika wageni rasmi wanaokuja kutalii badala ya kuzungumza mambo ya msingi.Ni dhahiri kuwa laiti waandaaji wa Diaspora Forums wangetaka mkutano huo uwe na maana wangeandaa mazingira ya kuepuka wababaishaji kama Waziri Membe ambao ni mahiri sana katika kutoa hotuba za kuleta matumaini lakini hotuba hizo zinabaki kuwa hotuba tu,na kusahaulika mara baada ya kumalizika kwa shughuli husika.

Kama kupiga konzi kwenye kidonda kibichi,Membe pasi aibu aligusia suala la uraia pacha (dual nationality).Akaanza kwa kueleza umuhimu wa uraia pacha,na kusema kuwa nchi zilizoruhusu uraia pacha zimewafanya watu wao kupata kazi nzuri zenye mishahara mikubwa na hivyo kuwawezesha kutuma fedha nyingi katika nchi wanazotoka.Huu ndio uelewa wa Waziri wa Mambo ya Nje kuhusu umuhimu wa Diaspora!!!

Labda hakupitia speech notes zake vizuri,labda hakufanya brainstorming ya kutosha kabla ya kutoa hotuba yake kwa wana-Diaspora,lakini ni wazi Membe anafahamu fika kuwa umuhimu zaidi wa uraia pacha ni suala la haki za binadamu kuliko mishahara mikubwa au kazi nzuri.Nani aliyemwambia Membe kuwa wana-Diaspora wana kazi za ovyo ovyo zisizolipa mishahara mizuri kwa vile tu hawana uraia pacha?

Kwa hoja hizi mfu,ni wazi kuwa Membe si mwakilishi mzuri wa wana-Diaspora katika kilio chao cha muda mrefu cha uraia pacha.Membe amegeuza Diaspora Forums kuwa sehemu ya kuwapa matumaini kuhusu suala hili ilhali hafanyi jitihada zozote kuhakikisha suala hilo linahama kutoka kuwa ahadi hewa na kuwa sheria kamili inayotekelezeka.

Kuhusu changamoto ya kuwawezesha Watanzania walio nje ya nchi kuchangia maendeleo ya Tanzania,Membe anapswa kufahamu kuwa kila Mtanzania aliye nje ya nchi ana connection na Tanzania.Wengine tuna wazazi,kaka,dada,wadogo,nk huko nyumbani na licha ya nchi yetu kujifanya haitambua umuhimu wa Watanzania walio nje,wameendelea kupunguza makala ya ufisadi kwa ndugu na jamaa zao huko nyumbani kwa kuwatumia fedha za matumizi na misaada mingineyo.

Katika mkutano huo,mmoja wa wajumbe alipendekeza uanzishaji wa kumbukumbu mkeka ya ujuzi na fani wazizonazo Watanzania waishio nje.Wazo zuri lakini nadhani mtoa hoja amesahau umuhimu wa data protection,na namna taarifa hizo binafsi za Watanzania walio nje zinavyoweza kuishia mtaa wa Mkwepu kwa wanaotengeneza vitambulisho feki.I would never trust fisadi awe na taarifa zangu binafsi ilhali nafahamu fika kuwa zitaozea tu kwenye mafaili kama sio kufungiuwa vitumbua na maandazi.

Kama taafira zilizokusanywa kufahamu chanzo cha milipuko ya mabomu huko Mbagala na Gongo la Mboto zimepuuzwa,mtoa hoja anataraji mijuiza gani  kwa taarifa za Watanzania walio nje kutumiwa ipasavyo?Nadhani kuna baadhi ya Watanzania wenzetu walio nje hawajishughulishi kufahamu uharamia,ufisadi,ubabaishaji,uzembe na utapeli wa kisiasa unaendelea huko nyumbani kiasi kwamba wanaweza kupoteza muda wao kuwasikiliza akina Membe "wakiuza sura" kwenye Diaspora Forums.

Unajua kwanini nasema Membe anafanya usanii kwenye suala la uraia pacha?Ameshatoa kauli kadhaa za kibabaishaji kuhusu suala hilo,moja ikiwa aliyoitoa Januari mwaka huu kwenye mkutano wa IOM ambapo alidai kuwa utafiti uliofanyika umehitimisha umuhimu wa uraia pacha,Wizara yake imeanzisha kitengo cha kushughulikia suala la Diaspora,na sheria ipo mbioni kuanzishwa.

Lakini kwenye mkutano wa Diaspora uliomalizika wiki iliyopita,Membe wala hakugusia ni lini sheria hiyo itaanza kufanya kazi.Katika mkutano huohuo wa IOM,Membe aliwazuga wajumbe kwa kuahidi kuwa sheria ya uraia pacha ingekuwa tayari kufikia mwisho wa mwaka jana.Amekuja London miezi mitano baadaye na kuendelea ngonjera hizo hizo.

Hebu sikiliza porojo za Membe kwenye Diaspora Forum II iliyofanyika mwaka jana



Na hapa pamoja na kuongelea mambo mengine,mwishoni mwa clip ifuatayo anajibu swali na Freddy  Macha kwa kuahidi tena "MWISHO WA MWAKA HUU" kama alivyoahidi mwaka jana kuwa "MWISHO WA MWAKA HUO 2010".



Enewei,kulikuwa Diaspora Forum I,ikamalizika na picha tukaona.Ikaja Diaspora Forum II,ikamalizika na picha tukaonyeshwa.Na majuzi imemekuja Diaspora Forum III,imemalizika wiki iliyopita na picha tumeziona.Tusubiri Diaspora Forum IV...bila shaka tutaendelea kushuhudia picha nyingine na usanii mwingine unaohanikizwa na maneno kama "mchakato","changamoto","vipaumbele" na usanii mwingine kama huo.Blogu hii inatoa wito kwa wana-Diaspora kujaribu kuwaonyesha Watanzania wenzatu walio nyumbani kuwa licha ya kutopendezwa na ubabaishaji wa baadhi ya viongozi wetu huko nyumbani,hatuwezi kutoa fursa kwa ubabaishaji huo kuwa exported hadi huku ughaibuni.Ili Diaspora Forums ziwe na manufaa,they need to go beyond being just another photo-ops.

26 Feb 2011


Yayumkinika kuhisi kuwa laiti Baba wa Taifa angefufuka leo huenda angeishia kutoa machozi.Taifa alilohangaika na wenzie kulipigania uhuru limegeuka kituko.Upande mmoja tunamwona Rais wetu akijibidiisha kusaka amani Ivory Coast ilhali wakazi wa Gongo la Mboto wanaporwa amani na usalama wao na wazembe wa Jeshi la Wababaishaji Tanzania...ooops,I meant Jeshi la Walipua mabomu...oh,not again.Nilitaka kuandika Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).Kwa upande mwingine ni ziara ya haramia wa Dowans ambaye licha ya kukimbia ukombozi wa Wazanzibari baada ya Mapinduzi amemudu kututapeli,kabla ya kuja kutuhubiria namna ya kuzalisha umeme,na kukumbushia fidia anayopaswa kulipwa kwa kututapeli!

Huku baadhi yetu tukizidi kusononeshwa na namna ombwe la uongozi linavyozidi kufidiwa kwa vitendo vya ufisadi,tunashuhudia eneo jingine ambalo lilisaidia sana kuifanya Tanzania ya Nyerere iheshimike kwa msimamo wake thabiti.Hapa nazungumzia sera za nje za nchi yetu.

Baada ya Mwalimu kung'atuka na nafasi yake kurithiwa na watu ambao kama Urais ni somo basi kwao halikuwemo kwenye silabasi (maana angalau anayepata zero anakuwa amesoma lakini hakufaulu),nchi yetu imegeuka kichekesho linapokuja suala la msimamo wetu kama taifa huru.

Na ukidhani naandika haya kama uzushi basi soma habari hii inayoeleza kuwa Tanzania imeogopa kutoa msimamo wake kuhusu uanaharamu wa dikteta Muamar Ghaddafi dhidi ya wananchi wake wanaodai mabadiliko nchini Libya.


Kwa mujibu wa habari hiyo,Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa Bernard Membe amedai kuwa


Tanzania kama nchi haiwezi kujitokeza wazi wazi kuunga mkono ama kupinga kinachotokea nchini humo kwa sababu ina raia wake wanaoishi huko hivyo kitendo chochote cha kushabikia kwa kuunga mkono ama kupinga kinahatarisha maisha yao.




Katika habari hiyo,Membe amenukuliwa akisema:
Unajua tuna raia wetu kule sasa siyo vizuri kuonyesha utashi wetu inaweza kuhatarisha maisha ya wananchi wetu kwani hii ilitokea kule Misri kwa wale waliojitokeza kuunga mkono waliweza kushambuliwa na kuharibiwa biashara zao

Ungetegemea Membe angejaribu angalau kuficha ombwe katika sera yetu ya nje kwa angalau kudanganya kama mwanadiplomasia kwamba "tunafuatilia kwa karibu matukio ya nchini Libya na tuko katika mchakato wa kuweka bayana msimamo wetu".

Yaani Membe anataka kutuzuga kwamba laiti Tanzania ikilaani unyama wa Ghaddafi dhidi ya raia wake basi kiongozi huyo wa Libya atalipa kisasi kwa kuwadhuru Watanzania 26 (kwa mujibu wa takwimu zake) waliopo nchini humo?

Kichekesho ni kwamba serikali ya CCM ambayo Membe ni miongoni mwa Waziri wake ilimudu kulaani "vurugu zilizosababishwa na Chadema huko Arusha" (ilhali waliopaswa kulaaniwa ni polisi wanaoamini katika ubabe kama wa Ghaddafi) japokuwa kuna Watanzania waliouawa na kujeruhiwa ni Watanzania pia (pamoja na raia mmoja wa Kenya).

Labda nitoe mfano bora zaidi.Hivi wakati Nyerere alipoweka wazi msimamo wake dhidi ya Makaburu wa Afrika Kusini hakukuwa na maslahi yoyote ya Tanzania katika nchi hiyo?Au,je tulipoamua kukabiliana na nduli Idi Amini hakukuwa na Mtanzania huko Uganda?

Ukweli ulio bayana ni kwamba si Membe wala bosi wake Kikwete wenye uthubutu wa kulaani unyama unaofanywa na Ghaddafi.Na si ajabu wanaombea afanikiwe kuteketeza raia wake na kubaki madarakani kisha wajipendekeze kwa kupitisha bakuli huko.

Lakini kwa upande mwingine kumlaumu Membe katika hili ni sawa na kumtaka mwanafunzi wa chekechea aandike thesis kuhusu mada ngumu kama Quantum Physics.Hivi kwa watu wanaoshindwa japo kumkemea mwarabu Adawi anayeifanya nchi yetu kama darasa la majaribio ya kudalilisha uhuru wa taifa,na badala yake wanampa fursa ya mwaliko hapo Ikulu kukutana na Makamu wa Rais (bila kusahau dokezo lake kuwa asipigwe picha),wataweza vipi kumudu mambo mazito kama uhusiano wa kimataifa?

Unapoona kiongozi wa nchi anashindwa kuwawajibisha Waziri wa Ulinzi Dkt Hussein Mwinyi,Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange,na wazembe wote waliogeuza makazi ya raia yaliyo jirani na kabi za jeshi kuwa viwanja vya mazoezi ya kulipua mabomu,basi ni wazi kumtegemea aongoze vema nchi katika masuala ya kimataifa ni sawa na kutarajia damu kutoka kwenye jiwe.

Mwinyi,Mkapa na sasa Kikwete wamefanikiwa sana kuifuta Tanzania kutoka katika nafasi yake kama taifa lenye msimamo na uongozi dhidi ya tawala dhalimu,mfano wa kupigiwa mstari ukiwa nafasi ya Tanzania katika mapambano ya ukombozi Kusini mwa Afrika.

Katika stadi za siasa tunafundishwa kwamba sera imara ya mambo ya nje inategemea sana uimara katika sera za mbalimbali za ndani ya nchi.Sasa kwa mwenendo huu ambapo Taifa letu lipo katika hatari ya kugeuzwa koloni binafsi la mafisadi ambao wanarahisishiwa azma hiyo na uongozi dhaifu wa Kikwete (anayechelea kuwaudhi maswahiba zake wanaoliingiza mkenge taifa letu),itakuwa ni njozi za mchana za mtu mwenye njaa kutegemea nchi hii irejee zama za Mwalimu ambapo tulimudu kujitengenezea heshima kubwa kutokana na misimamo thabiti na isiyoendekeza kujikomba,uoga,unafiki au ubabaishaji.

Kwa mwenendo huu,nalazimika kuafikiana na kauli za Sheikh Yahya kuwa nchi yetu inaweza kukumbwa na mabalaa makubwa huko mbeleni (japo nawalaumu waandishi wa habari walioshindwa kumhoji mnajimu huyo kuhusu utabiri wake kwamba mtu yeyote ambaye angejitokeza kugombea dhidi ya Kikwete katika uchaguzi mkuu uliopita angekufa).


9 Jul 2010

UJUMBE KUTOKA URBAN PULSE: Karibuni tena wadau wote wa kuangalia sehemu ya pili ya mada ya Uraia Pacha kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe wakati akitoa hotuba kwenye Diaspora hapa Mjini Ukerewe tarehe 26.3.2010

Pia Mh Membe alisoma ujumbe kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Jakaya Kikwete akiwasifu na Kuwapongeza Watanzania katika Diaspora. Tafadhali Bonyeza chini kuangalia Video

7 Jul 2010


Demokrasia katika jamii isiyojali utawala bora ni sawa na kufukia makaratasi ardhini kwa matarajio ya kuota mmea wenye matunda ya noti.Ni mithili ya kualika timu ya Taifa ya Brazil kwa mabilioni ya shilingi kisha mechi husika ituache na bili kubwa pasipo manufaa yoyote.Hebu tafakari.Mwezi Oktoba Watanzania kwa mamilioni yao watapiga kura kumchagua Rais na Wabunge.Japo shughuli hiyo ni ya siku moja tu,maandalizi yake yanagharimu mabilioni ya shilingi.Wenyewe wanasema ndio gharama ya demokrasia.Lakini baada ya uchaguzi,wengi-kama sio wote-wa tutakaowachagua watasahau kabisa kwanini tumewachagua,huku wakiwa bize kutafuta namna ya kufidia gharama walizotumia kuingia madarakani.

Zamani hizo tuliambiwa kuwa demokrasia ni pamoja na uwepo wa vyama vingi vya siasa.Takriban miongo miwili baadaye Watanzania wameshuhudia namna uwepo wa vyamahivyo vingi vya siasa ulivyoshindwa kulikwamua taifa letu kutoka kwenye lindi la umasikini.Sanasana umasikini umekuwa ukizidi kuongezeka huku wanasiasa wetu wakibadili kauli mbiu kila baada ya muhula (kwa mfano kutoka Ari Mpya,Kasi Mpya na Nguvu Mpya kuwa Ari Zaidi,Kasi Zaidi na Nguvu Zaidi).Tumeshuhudia pia mlolongo wa sera,mikakati,mpingo na vitu kama hivyo,from MKUKUTA to MKURABITA to KILIMO KWANZA.Na kwa mawazo mapya hatujambo,shughuli ipo kwenye utekelezaji.

Siku chache zilizopita nilitundika makala kuhusu utata wa kauli za Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe na zile za Makamu Mwenyekiti wa CCM Pius Msekwa kuhusu suala la uanzishwaji Mahakama ya Kadhi.Wakati Waziri Chikawe aliahidi kuwa mahakama hizo zingeanza kazi mwakani,Msekwa alitamka bayana kuwa suala hilo haliwezekani.Hadi leo hakuna ufafanuzi uliotolewa kuhusu suala hilo ila kilicho bayana ni kuwa CCM imeamua kuachana nalo baada ya kuliingiza kwenye manifesto yake ya Uchaguzi mwaka 2005.Kwa vile sie ni mahiri zaidi wa kuhangaika na mambo kwa mtindo wa zimamoto tunasubiri liwake la kuwaka ndipo tuanze kuhangaika namna ya kudhibiti.Taasisi zenye majukumu ya kuwa proactive (yaani kuazuia majanga kabla hayajatokea) ziko busy zaidi na kuhakikisha CCM inarejea madarakani kwa ushindi wa kishindo badala ya kujishughulisha na jukumu lao la msingi la kulinda na kutetea ustawi wa taifa letu.Kwao,siasa (yaani CCM) ndio nchi na ndio kila kitu.

Majuzi umejitokeza utata mwingine wa kauli kati ya mawaziri wawili waandamizi kuhusu suala la uraia wa nchi mbili (dual citizenship).Na kichekesho ni kwamba tofauti na ule mgongano wa kauli kati ya Chikawe na Msekwa,safari hii mgongano wa kauli za mawaziri hao umejiri ndani ya jengo la Bunge katika kikao kinachoendela cha bajeti ya mwaka 2010/11.Awali,Waziri wa Mambo ya Ndani Lawrence Masha alilieleza Bunge Tukufu kuwa serikali imeamua kuwa huu sio wakati mwafaka kwa suala la uraia wa nchi mbili,na kwamba serikali anaangalia uwezekano wa kuanzisha ukaazi wa kudumu (permanent residency).Waziri Masha alieleza kuwa serikali inaandaa hoja kuhusu suala hilo la permanent recidency kwa minajili ya kuileta bungeni ijadiliwe. "Huu sio wakati mwafaka kuruhusu uraia wa nchi mbili,serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha ukaazi wa kudumu badala ya uraia wa nchi mbili", alisema Masha.

Wakati Masha akisema hivyo,Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe alilieleza Bunge hilohilo kuwa serikali imeridhia suala la uraia wa nchi mbili na kwamba Wizara yake iko kwenye mchakato wa kuwasilisha suala hilo kwenye kikao cha Barza la Mawaziri.Pia Membe alieleza kuwa anafanya mawasiliano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ili kupata baraka zao kutokana na suala hilo kuwa la Muungano.Akihitimisha hoja ya bajeti ya wizara hiyo, kwa mwaka wa fedha 2010/2011, Waziri Membe alisema siyo dhambi, Watanzania kutafuta riziki nje ya nchi na ni haki yao kubaki na uraia wa Tanzania.Alisema wakati umefika kwa Watanzania, kupatiwa haki yao ya msingi kwani licha ya kuwa ni manufaa kwao pia ni manufaa kwa nchi kutokana na fursa ya kuongeza pato la taifa.

Kadhalika,inadaiwa kuwa Waziri Membe aliwaeleza Watanzania waliohudhuria mkutano wa Diaspora jijini London hivi karibuni kwamba suala hilo limeshajadiliwa na baraza la mawaziri na linasubiri kuwasilishwa bungeni ili upitishwe au kupingwa na wabunge.Mimi sikuhudhuria Mkutano huo wa Diaspora kwa vile niliamini ungenipotezea muda wangu tu kwa sababu viongozi wetu ni mahiri sana katika kuahidi mambo mazuri kwenye hadhara,na hujifanya wasikivu sana lakini utekelezaji ni zero,sifuri,zilch!

Ni dhahiri kwamba mmoja kati ya mawaziri hawa anadanganya.Wakati sina la kusema kuhusu kauli ya Waziri Masha,kauli za Waziri Membe huko Bungeni na London zinaleta utata unaoweza kuyumkinisha kuwa kuna urongo wa namna flani.Je kauli ipi ni sahihi kati ya hiyo alotoa London kuwa suala hilo limeshajadiliwa na Baraza la Mawaziri na hiyo ya bungeni kuwa suala hilo bado liko wizarani huku likifanyiwa mchakato wa kulipeleka kwenye Baraza la Mawaziri?

Unajua kwanini mmoja wao anadanganya?Sababu ni kadhaa,lakini kwa ufupi,moja,ni kwa vile mdanganyifu huyo anafahamu bayana kuwa wabunge wanaoelezwa suala hilo wapo bize zaidi kufikiri namna watakavyorudi bungeni baada ya uchaguzi (sambamba na kuwazia posho zao nono za vikao vya bunge) kuliko kumkalia kooni waziri aeleze kinagaubaga.Ndio maana mwanzoni mwa makala hii nilibainisha uselessness ya demokrasia yetu.Tunapoteza mabilioni ya shilingi (sambamba na muda wetu kusikiliza porojo za "mkituchagua tufafanya hiki na kile") kuwachagua watu wa kutuwakilisha bungeni lakini wakishafika huko wanakuwa bize zaidi na maslahi yao binafsi.

Pili,anayedanganya kati ya mawaziri hao anafahamu kuwa aliyemteua hatamwajibisha.Kama kuna mtu alimudu kumzuga Rais kwa kuchomekea ishu kadhaa kwenye muswada wa sheria za gharama za uchaguzi na kisha akasalimika,kwanini basi mdanganyifu huyo katika suala hili la uraia mbili awe na hofu?

Tatu,waziri anayedanganya kati ya hao wawili anafahamu udhaifu wa Watanzania katika kudai haki zao za msingi.Kiongozi anaweza kudanganya waziwazi kwenye umati wa watu lakini bado akaishia kupigiwa makofi na vigeregere.Ule wimbo wa "Ndio Mzee" wa Profesa Jay unawakilisha hali halisi ya namna Watanzania wengi wanavyoridhia kuzugwa na wanasiasa wababaishaji.Hebu angalia namna harakati za kuirejesha tena madarakani CCM zinavyopamba moto huko nyumbani.Kwa mgeni,anaweza kudhani labda chama hicho ni kipya na hakihusiki kabisa na kashfa za ufisadi,kubebana,kubomoa uchumi wetu na madudu mengine chungu mbovu yanayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi masikini kabisa duniani licha ya raslimali lukuki iliyojaaliwa kuwa nazo.Binafsi naamini kuwa unyonge huo wa Watanzania umechangiwa sana na siasa za chama kimoja ambapo kiongozi alikuwa mithili ya Mungu-mtu,hakosei,lazima ashangiliwe hata akiongea utumbo,sambamba na suala la kujikomba kwa viongozi kwa matarajio ya kujikwamua kwa namna moja au nyingine.

Na kwa vile vyama vya upinzani vimetuthibitishia kuwa uwezo wao katika kuing'oa CCM madrakani ni kama haupo,basi mazingaombwe kama hayo ya Chikawe na Msekwa,na haya ya sasa kati ya Masha na Membe yataendelea kuwepo kwa muda mrefu sana.Unaweza kuhisi kama nimekata tamaa vile kwa namna ninavyoandika.Hapana,ila safari yetu ni ndefu sana,na tatizo sio urefu tu bali ni kiza kilichotanda kwenye njia yetu ambayo imejaa mashimo kadhaa.Ni sawa na kipofu kumsaka paka mweusi kwenye chumba chenye giza ilhali paka huyo hayumo chumbani humo.

8 Dec 2008


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ameonya kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinaweza kusambaratika ikiwa uadui uliopo ndani yake unaoendelezwa na makundi hautadhibitiwa. 

Membe alisema uadui huo unasababishwa na vitendo kama vile hujuma za kuangushana katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika chama hicho. 

Waziri huyo alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Dar es Salaam. 

Membe, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM, alisema ni dhana potofu kuamini kuwa uadui wa aina hiyo unasababishwa na vyama vya upinzani. 

``Maadui wapo ndani, ni wenzetu sisi wenyewe, tunakaa nao lakini wanashiriki kupanga kuangushana, majungu yamekithiri hiyo ni kielelezo cha ugonjwa wa chama kusambaratika,`` alionya Membe ambaye pia ni Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje ya CCM. 

Membe, alisema uzoefu ywa miaka miwili aliopata tangu ateuliwe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, umemuonyesha kuwa vyama vingi vilivyotawala kwa muda mrefu vinaweza kuondoka madarakani kutokana na udhaifu uliopo, na si nguvu ya upinzani. 

``Mara nyingi sana vyama tawala vinajiua vyenyewe, si kwa sababu ya upinzani,`` alisema Mbunge huyo wa Mtama,. 

`` Tunapotafunana, kutoaminiana, kama CCM na jumuiya zake hatushikamani, tukagawanyika, hatuwezi kuwa chama imara, tutameguka,`` alisema. 

Membe alisema machafuko yanayotokea baada ya chaguzi barani Afrika, yanachochewa na kasumba ya kutokukubali matokeo. 

Alisema hali hiyo inawafanya watu wengine kuingia msituni ama kufikia hatua ya kufanya mapinduzi ya kijeshi. 

Alitoa mfano kuwa katika kipindi cha takribani miaka 50, viongozi 32 barani Afrika, waliuawa kutokana na mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa katika nchi zao na kwamba vyama vilivyopo madarakani, vina fursa nyingi za kufanikisha kubaki katika uongozi. 

Kwa mujibu wa Membe, baadhi ya fursa hizo ni kueleweka kwa sera zake, uwepo wa viongozi bora na jumuiya imara. 

Wakati Membe akitoa tahadhari hiyo, baadhi ya wajumbe wa mkutano huo nusura wapigane hadharani, kutokana na tofauti za kuwaunga mkono wagombea katika nafasi mbalimbali za UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam. 
Hali hiyo ilijitokeza jana asubuhi, kabla ya Membe kuwasili kufungua mkutano huo. 

Taarifa za ndani zilidai kuwa kundi linalomuunga mkono mmoja wa wagombea wa uenyekiti, lilipanga njama za kuhujumu uchaguzi huo ili kutoa fursa kwa `mtu wao` kushinda. 

Miongoni mwa hujuma hizo, ni kusimamishwa kwa wajumbe zaidi ya 10, ili wasishiriki kupiga kura. 
Hata hivyo, baada ya kugundulika, baadhi ya vijana kutoka wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke, waligoma kuingia ukumbini. 

``Hatuingii ukumbini kama wenzetu waliosimamishwa hawatapewa vitambulisho, hatukubali kuburuzwa,`` walisikika baadhi yao wakisema. 

Hakuna kiongozi yeyote wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo, isipokuwa wanachama wengine wa umoja huo walisikika wakilalamikia kundi walilodai kwamba liliongozwa na mmoja wao. 

Baadaye, taarifa zilieleza kuwa vijana waliozuiwa kupiga kura, waliruhusiwa na kupewa vitambulisho.

CHANZO: Nipashe

WAKITAHARIDHISHANA WENYEWE INAKUWA SALAMA,MAANA KAZI HIYO IKIFANYWA NA WACHAMBUZI WA SIASA WANAISHIA KUNYOOSHEWA VIDOLE WAKITUHUMIWA KWA UCHOCHEZI.

JAPO MEMBE ANASTAHILI PONGEZI KWA KUJITOA MHANGA KUSEMA HAYO ALOSEMA NDANI YA CHAMA KILICHOZOWEA KUSIFIWA TU HUKU CRITICISM YA AINA YOYOTE IKITAFSIRIWA KUWA NI MITHILI YA UHAINI,ALIPASWA PIA KUONGELEA NAMNA CCM INAVYOJIMALIZA KWA KUKUMBATIA MFUMO  USIO RASMI AMBAPO ASIYE NA FEDHA HAWEZI KUSHINDA CHAGUZI YOYOTE YA CHAMA HICHO.RUSHWA IMEKITHIRI MNO NDANI YA CHAMA HICHO KIKONGWE.

MADHARA YA MUDA MFUPI (IMMEDIATE) YA RUSHWA KATIKA CHAGUZI HIZO NI NI PAMOJA NA UWEZEKANO WA KUPATA VIONGOZI WASIO NA SIFA STAHILI NA AMBAO WANAWEZA KUTOWAJIBIKA IPASAVYO KWA VILE WANAJIONA KAMA WAMENUNUA UONGOZI NA WANA HAKI YA KUFANYA MAMBO WAPENDAVYO.MADHARA YA MUDA MREFU (LONG TERM) NI REPRODUCTION YA MAFISADI.CCM NDIO CHANZO KIKUBWA CHA VIONGOZI WA NGAZI MBALIMBALI NCHINI.KWA MAANA HIYO,CHAMA HICHO KIKIZEMBEA KAMA SASA NA KUACHIA VIONGOZI WAPATIKANE KWA NJIA YA RUSHWA BASI TAIFA NALO LITAENDELEA KUPATA SUPPLY KUBWA YA VIONGOZI WALIONUNUA CHAGUZI AMBAO HAWATASHINDWA KULIFISADI TAIFA.

HABARI MBAYA NI KWAMBA HAKUNA DALILI YA CCM KUPAMBANA NA RUSHWA KATIKA CHAGUZI ZA CHAMA HICHO.NA KIKWAZO KIKUBWA CHA JITIHADA HIZO NI HIZI SIASA MUFILISI ZA MITANDAO.KWAMBA,UKIJITAHIDI KUSIMAMIA HAKI UTALIPULIWA NA WALE WANAOJUA UMEFIKAJE HAPO ULIPO.NDIO MAANA WANASIASA MAKINI HUJITAHIDI SANA KUEPUKA MAKUNDI YA KUSAIDIA USHINDI KWA VILE KUJIHUSISHA NAYO HUMGEUZA MWANASIASA HUSIKA KUWA MTUMWA WA MAKUNDI YA AINA HIYO.

31 Oct 2008

Picha kwa hisani ya BONGOPICHA

WAKATI serikali ikishutumiwa na viongozi wa madhehebu ya Kikristo, juu ya Tanzania kutaka kujiunga na Jumuiya ya nchi za Kiislamu (OIC) na kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amekutana kwa siri na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kujadili masuala hayo.

Kikao hicho cha faragha cha viongozi hao wawili, kilichukua zaidi ya saa moja katika mazungmzo yao yaliyofanyika jana katika ofisi za Jimbo Kuu la Dar es Salaam, kuanzia saa 10:30 jioni hadi saa 11:30.

Membe alikutana na Pengo jana ikiwa ni siku moja baada ya kardinali huyo kurejea nchi akitokea Vatican ambako alikwenda kwa shughuli za kanisa.

Akizungumza na Tanzania Daima, baada ya kumalizika kwa kikao hicho nyeti, Waziri Membe alikiri kuwa na kikao cha faragha na kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki nchini, lakini hakuwa tayari kusema nini walichojadiliana, kwa madai kuwa, hayapaswi kuwekwa hadharani kwa sasa.

“Unajua Kardinali Pengo ni kiongozi wa kiroho wa ngazi ya juu sana, kila tunapokuwa na masuala mazito ya kitaifa, tunapenda kupata ushauri wake pamoja na viongozi wengine wa kiroho ili kuona wanasemaje,” alisema Waziri Membe.

“Mbali na suala la OIC na Mahakama ya Kadhi, tumezungumza mambo mengi ya kitaifa ambayo mimi sipaswi kueleza zaidi kwa undani, kwani unaweza kumuuliza Baba Kardinali mwenyewe kama atataka kukueleza, lakini ni mambo ambayo yanahusiana na maisha ya Watanzania wote,” alisema Waziri Membe.

Kuhusu mjadala unaoendelea juu ya Tanzania kujiunga na OIC na jinsi hali ilivyo kwa sasa nchini, Waziri Membe alisema ni mambo ya kupita na utulivu utarejea hivi karibuni.

“Hali ya amani na utulivu itarudi hivi karibuni, hakuna shida, serikali ina amini na inawahakikishia wananchi kuwa hakuna vurugu kuhusiana na hilo wala suala lingine lolote.

“Watu watulie, wafanye kazi, serikali itakutana na wadau wote na nasema tena, hakuna tatizo kubwa hapa, tutahakikisha suala hili linaisha kwa amani bila kusababisha vurugu zozote,” aliongeza Membe.

Akizungumzia madai yaliyotolewa na Jumuiya ya Maaskofu wa CCT, kumtaka ajiuzulu hivi karibuni, alisema kuwa hilo hataki kuliongelea kwani amechoka, aachwe apumzike kwanza.

Jitihada za kumtafuta Kardinali Pengo, kuzungumzia juu ya kikao hicho cha siri ziligonga mwamba baada ya kuambiwa kuwa, ameingia kwenye kikao kingine na uongozi wa Kanisa la Mt. Joseph na haijulikani kingeisha saa ngapi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita maaskofu wanaounda Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), walielezea kusikitishwa, kushtushwa na kupinga ushawishi unaojengwa na serikali wa kutaka Tanzania iridhie kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC).

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Askofu Peter Kitula ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, alisema hawatakuwa tayari kukubalia kwa vyovyote vile kuona chama fulani cha siasa kikijaribu kutafuta ridhaa ya wapiga kura kwa gharama ya kutishia umoja wa kitaifa na amani ya nchi.

“Hapa ieleweke kuwa ni hatari na kamwe isiruhusiwe njia hii kutumika ili mradi chama fulani kishike dola hata kama ni kwa gharama ya kuvunjika kwa umoja wa kitaifa na amani ya nchi hii! Jambo hili hatutalikubali kwa vyovyote vile kwa chama chochote kitakachokubali mambo haya mawili aidha wakati wa kampeni za uchaguzi au wakati wowote ule,” lilisema tamko hilo la CCT lililoambatanishwa na majina ya maaskofu 64 wa nchi nzima.

Pasipo kufafafanua huku wakisema kwamba CCT, haifungamani na chama chochote cha siasa, maaskofu hao katika tamko lao walisema, iwapo itafikia hatua ya Tanzania kujiunga na OIC na Mahakama ya Kadhi kuridhiwa, basi wao watalazimika kufikiria upya jinsi ya kukishauri chama hicho tawala kwa kuzingatia kile walichokieleza kuwa ni manufaa ya Watanzania.

“Kipekee wakati huu, kutokana na yanayoendelea kujadiliwa bungeni, tunatoa tahadhari kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kutoruhusu kabisa kuendelea kwa mjadala huu kama ambavyo tumekuwa tukiomba mara kwa mara kwa nyakati tofauti zilizopita,” linasema tamko hilo.

Pamoja na hilo, maaskofu hao walimtaka Waziri Membe, kujiuzulu wadhifa wake kutokana na hatua yake ya kujenga ushawishi wenye mwelekeo wa kidini wa kuiingiza nchi katika OIC.

Mbali ya hayo, tamko lilisema kuwa hatua ya Tanzania kujiunga OIC inakwenda kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 19 (2) na Sheria ya Vyama vya Siasa nchini.

Askofu Kitula alisema, wanapinga Tanzania kujiunga na OIC kwa maelezo kuwa, katiba ya jumuiya hiyo imejipambanua wazi kuwa na malengo ya kuendelea na kuulinda Uislamu, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa taifa, lenye watu wa imani nyingine za dini.

Akifafanua askofu huyo alisema, katika Ibara ya 1 (11) ya Katiba ya OIC, kuna kipengele kinachosomeka ‘kusambaza, kuendeleza na kuhifadhi mafundisho ya dini ya Kiislamu….kuendeleza utamaduni wa Kiislamu na kuulinda urithi wake’, maelezo ambayo ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ambayo inahimiza uhiari na uhuru wa mtu binafsi katika masuala yanayohusu kueneza dini au masuala ya imani.

Askofu Kitula ambaye alisoma tamko hilo kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCT, Akofu Donald Mtetemela, aliyesaini tamko hilo, alisema uamuzi wa kujiingiza katika masuala ya namna hiyo ni wa hatari, kwani yanaweza kuleta migogoro kutokana na kuwapo kwa dhana ya udini.

Maaskofu hao walimtaka Waziri Membe kuachana na kauli zake juu ya umuhimu wa kuingia kwenye jumuiya hiyo ya Kiislamu na kuhoji aliyemtuma kufanya hivyo.

CHANZO:Tanzania Daima

24 Oct 2008


Na Peter Edson
JUMUIYA ya Kikristo Tanzania (CCT) imemuonya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuwa kauli zake kuhusu kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi za Kiislamu (OIC) zinaweza kusababisha mgawanyiko wa kitaifa na kumtaka aachane nazo au ajiuzulu wadhifa wake.

Tamko hilo la maaskofu wa makanisa ya Kikristo imekuja baada ya Waziri Membe kukaririwa akisema kuwa hakuna athari zozote kwa Tanzania kujiunga na taasisi hiyo, ambayo madhumuni yake ni kutetea binadamu na hasa Waislamu na sehemu takatifu.

Membe alisema hakuna haja ya kuwa na woga wa kujiunga na taasisi hiyo wakati katika mchakato wake wakristo na waislamu watanufaika na miradi itakayokuwa ikisimamiwa na OIC, na akashangaa ujasiri wa Watanzania wa kupambana na matatizo umekwenda wapi kiasi cha kuogopa nchi kujiunga na jumuiya hiyo.

Suala hilo liliwahi kuibuka mwishoni mwa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi wakati vyombo vya habari vilipofichua kuwa serikali ilijiunga kinyemela na jumuiya hiyo. Baadaye viongozi wa serikali walikiri kufanya hivyo kabla ya kujiondoa, lakini safari hii upinzani umekuwa mkubwa zaidi.

Wakitoa tamko lao kwa waandishi wa habari jana, maaskofu hao kutokana makanisa ya kiprotestanti walisema kauli ya Waziri Membe ina lengo la kutetea maslahi ya watu wachache.

Maaskofu hao walisema kwa kuwa katiba ya OIC hiyo inaeleza bayana kuwa italinda mila, desturi na tamaduni za kiislamu, kujiunga na jumuiya hiyo itakuwa ni kukiuka katiba ya nchi inayoeleza kuwa dini ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na kwamba shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchini.

"Kama serikali ikikubali, kutakuwa ni mwanzo wa kuruhusu kubomoka na kuvunjika kwa amani ya nchi kwa sababu yanagusa hisia na itikadi za wananchi," alisema Askofu Peter Kitula, ambaye ni makamu mwenyekiti wa kwanza wa CCT.

Askofu Kitula, ambaye alisoma tamko hilo la maaskofu, alisema baada ya kutafakari kwa roho ya kiutume na kinabii wameamua kupinga kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi pamoja na mchakato wa kujiunga na OIC.

Alisema katiba ya Tanzania ibara ya 19 kifungu cha 2 inaeleza wazi kuwa kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchini.

"Ibara hii ni muhimu sana kwa ajili ya kusimamia na kuhakikisha kwamba mambo ya dini yanatenganishwa kabisa na shughuli za uendeshaji wa nchi," alisema.

Alisema sehemu hiyo ya katiba inapingana na ibara ya 1 kifungu cha 11 ya katiba ya OIC kinachosema kuwa jumuiya hiyo inatetea mila, tamaduni na desturi za kiislamu, kuwalinda na kuwaelimisha wananchi kuhusu uislamu nchini, jambo ambalo askofi huyo alisema linaonyesha wazi kuwa kujiunga na IOC itakuwa ni ukiukwaji wa katiba.

Alisema siku za hivi karibuni Bunge la Jamuhuri ya Muungano limekuwa likijadili miswada ya sheria ya kuanzisha au kujihusisha na vyombo hivyo viwili, lakini akasema kuwa kushinikiza kukubalika kwake ndani ya bunge ni kwenda kinyume na katiba.

Naye Owdernburg Mdegela, askofu wa dayosisi ya Iringa ya Kanisa la Kiinjili la Kilutherani Tanzania (KKKT), alisema kitendo cha Waziri Membe kulizungumza jambo hilo bila kulionea haya ni kutetea maslahi ya watu wachache na kuvunja katiba.

Alisema Tanzania ina rasilimali za kutosha hivyo kujiunga na umoja huo kwa lengo la kutafuta misaada ama kutafuta kula na baadaye kupoteza mwelekao wa taifa, ni kujiingiza katika mtego ambao kujinasua kwake kunahitaji gharama ambayo ni kumwaga damu.

"Sisi tunasimama kama viongozi wa kanisa tukimwambia Membe kuwa hafai wadhifa huo, hivyo ni vema akaacha mara moja kutoa kauli zake zisizo na mantiki. Lakini kama hawezi, basi inampasa ajiuzulu," alisema Askofu Mdegela.

Naye askofu wa kanisa pentekoste, Sylivester Gamanywa alisema Waziri Membe anatoa kauli ambazo zina lengo la kuweka hisia binafsi na mgawanyiko wa kitaifa pamoja na kuvunjika kwa amani.

Alisema kitendo cha waziri huyo kusema kuwa serikali inaruhusu fedha chafu na kwamba kama mtu akikuta fedha za shetani inampasa kuzichukuwa, ni kuwadhalilisha Watanzania na taifa lao kwa ujumla.

Naye askofu wa Anglikana, Dk. Stephen Munga alisema kuwa waziri Membe hafai katika kushughulikia masuala ya kitaifa kwani hakuna mamalaka yoyote iliyomuagiza aende kuzungumzia suala la kuaanzishwa kwa OIC.

"Inampasa Waziri Membe afahamu kuwa sisi ni Tanzania na tutafuata mambo yetu na si kuiga masuala ya nje. Anavyosema tuwaige Waganda si jambo sahihi," alisema Dk. Munga.

Alisema kama kanisa msimamo wao ni kuyakataa mambo hayo mawili na kuitaka Serikali na mamlaka zake zote kuacha kuendelea kukaribisha mijadala ya mambo hayo kwani kufanya hivyo ni kupoteza muda wa wenye dhamana ya mamlaka ya nchi hii na rasilimali zake.

"Tunauhakika kuwa yaliyomo ndani ya OIC ni hatari kabisa, kwani endapo yakikubalika katiba ya nchi itakuwa imevunjwa na Watanzania watakuwa wameingia katika migogoro itakayoua maridhiano, mshikamano, utengemano na umoja wa kitaifa," alisema Askofu Kitula.

"Kwa kuzingatia wajibu wetu wa kinabii na kiutume, tunatoa wito kwa bunge kutoruhusu kamwe uanzishwaji wa mahakama ya kadhi kwa kupitia mchakato wa utendaji wa mamlaka ya nchi, pia kutoridhia uanachama wa Tanzania katika OIC."

Akizungumzia tamko la maaskofu, mwenyekiti wa kamati ya msikiti wa Idrissa, Sheikh Ally Basaleh alisema kuwa awali kabla ya kuanza kwa mchakato wa masuala hayo serikali ilishafanya uchambuzi wa kina na kugundua umuhimu wa kuanzishwa kwa vyombo hivyo.

"Kauli za maaskofu hawa na viongozi wa kanisa zinadhihirisha kuwa wanakataa maamuzi yao ya awali kwamba Rais Jakaya Kikwete ni mteule wa Mungu, kwani ndiye anayesimamia masuala haya yote," alisema Basaleh.

Alisema waislamu ni sehemu ya jamii hivyo wao kama viongozi wa dini wanaandaa mchakato wa kutoa tamko litakalokuwa likitoa mchanganuo kuhusu uhalali wa kuanzishwa kwa vyombo vyote hivyo viwili nchini.
CHANZO: Mwananchi

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.