Showing posts with label CCM. Show all posts
Showing posts with label CCM. Show all posts

27 Oct 2020



Pengine umeshawahi kusikia jina la Profesa Allan Lichtman wa Marekani ambaye ana rekodi ya miaka 30 ya kutabiri kwa usahihi kabisa matokeo ya urais katika nchi hiyo. 



Pengine utabiri uliompatia umaarufu zaidi ni wa mwaka 2016 ambapo takriban kila kura ya maoni ilionyesha kuwa mgombea wa chama cha Democrats, Hillary Clinton, angemshinda mpinzani wake wa chama cha Republican, Donald Trump.

Profesa huyo anatumia vipengele 13 vinavyopatikana kwenye kitabu chake kiitwacho "The Keys To The White House" (funguo za kuingilia Ikulu ya Marekani).

Katika vipengele hivyo 13 ni kauli zenye mrengo wa ushindi kwa mgombea aliyepo madarakani. Kwa muktadha wa Tanzania, vipengele hivi hapa chini vinamhusu Rais John Magufuli wa chama tawala CCM anayechuana vikali na mpinzani wake mkuu, Tundu Lissu wa Chadema.

Endapo majibu ya SI KWELI (FALSE) ni matano au pungufu kwa vipengele hivyo, basi mgombea aliyepo madarakani anatabiriwa kushinda. Lakini endapo majibu ya SI KWELI (FALSE) yatakuwa sita au zaidi, basi mgombea huyo ataanguka kwenye uchaguzi husika.

Naomba nitahadharishe kuwa hii ni mara ya kwanza kwa kanuni hii kutumika kutabiri matokeo ya urais nchini Tanzania. Hata hivyo nimejiridhisha kuwa japo Profesa Lichtman alilenga chaguzi za rais wa Marekani, zaweza pia kutumika kwa muktadha wa Tanzania.

18 Mar 2019


 
Leo Machi 18, 2019 ni siku ambayo lazima iingie kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa sababu kuu tatu, ambazo zote zinamhusu mwanasiasa mkongwe Seif Sharif Hamad na Chama cha Wananchi (CUF)

Sababu ya kwanza, leo ni siku ambayo mwanasiasa huyo, maarufu kwa jina la Maalim Seif, "ametimuliwa" rasmi kutoka chama alichoshiriki kukiasisi (CUF).
Kibaya zaidi, "kutimuliwa" huko kumekuwa na baraka kisheria, baada ya Mahakama Kuu kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho.

Ikumbukwe tu Lipumba alitangaza kujiuzulu uenyekiti kwa sababu anazozijua yeye kabla ya kuamua kurejea kwenye wadhifa huo "kwa mabavu." Kwa bahati mbaya – au pengine makusudi – sheria na kanuni za CUF zilikuwa zinatoa mwanya kwa Lipumba (au mwanasiasa mwingine yeyote yule) kufanya "uhuni" kama huo.

Sababu ya pili, ni kwamba leo CUF imekabidhiwa rasmi kwa Lipumba. Kisheria. Mahakama imetenda haki kwake kwa sababu japo alichofanya ni uhuni, kisheria uhuni huo ulihalalishwa na CUF yenyewe.

Hili la Lipumba kukabidhiwa chama si jambo dogo. Kuna mawili hapa. Moja, hii inaweza kuwa fursa nzuri kwa Lipumba kukijenga chama hicho na hatimaye kukirejesha kwenye nafasi ya kuaminika kama "mbadala wa CCM."

Lakini la pili, na hili ndilo ninahisi litatokea, ni mwanzo wa mwisho wa CUF. Sio siri kuwa Lipumba amesaidiwa sana na CCM kuipora CUF kutoka mikononi mwa Maalim Seif. CCM hawajafanya hayo kwa vile wanampenda Lipumba.Hapana. Wanamtumia tu kumdhibiti Maalim Seif ambaye licha ya kila hujuma zilizokuwa zikifanywa na CCM na taasisi zake, ameendelea kuwa mwanasiasa maarufu zaidi kuliko wote katika siasa za Zanzibar.

Sasa, baada ya Lipumba kutumika "kummaliza Seif ndani ya CUF," kuna uwezekano wa aina mbili tu. Wa kwanza ni kwa mwanasiasa huyo msomi kukubali kuendelea kutumika kama kibaraka wa CCM huku CUF ikigeuka kuwa CCM-B, na wa pili, ni kujaribu kusimama kama chama halisi cha upinzani na hapohapo "kumwagiwa radhi na CCM" na hatimaye kupelekea kifo cha chama hicho.

Uwezekano mkubwa zaidi ni huo wa kwanza - ukibaraka. Kwamba CUF haitokufa. CUF itaendelea kushiriki chaguzi mbalimbali. CUF itajenga taswira ya chama kamili cha upinzani. Lakini uwepo huo wa CUF hautokuwa kwa manufaa ya chama hicho au siasa za upinzani bali kwa manufaa ya CCM.

Kuna kila dalili kuwa CCM itaisaidia CUF kujitanua nchi nzima kwa sababu moja kuu: uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utakuwa mbovu kuliko chaguzi zote zilizowahi kutokea Tanzania. Kuna uwezekano mkubwa tu kwa baadhi ya vyama vikuu vya upinzani kutishia kususia uchaguzi huo. Na hapo ndipo CUF ya Lipumba itakapotumika kuhalalisha "ushindi wa Magufuli/CCM."

CCM itaisaidia CUF kuweza kusimamisha wagombea takriban kila jimbo kwa upande wa Tanzania Bara. Lakini pia CCM itaisaidia CUF kuendelea kuwa chama imara cha upinzani huko Zanzibar, ambako uimara wake utasaidia kugawa kura dhidi ya CCM na wagombea wake.

Hata hivyo, "laana ya kutumika" itaikumba CUF baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kama isipoishia kusambaratika basi itabaki "chama jina" kama TLP ya Mrema.

Kuhusu uamuzi wa Maalim Seif kuhamia ACT- Wazalendo, japo hatua hiyo inaweza kuwashangaza baadhi ya watu, ukweli mchungu baada ya Mahakama Kuu kuhalalisha "uhuni" wa Lipumba, sambamba na "uhuni" wake mwingine majuzi ambapo "alijitangaza" kuwa Mwenyekiti kupitia "uchaguzi mkuu hewa" ambao pia "ulimtimua Maalim Seif" kwa kuteua mtu mwingine kushika wadhifa wa Katibu Mkuu.

Kwa kuzingatia muda mfupi uliosalia kabbla ya uchaguzi mkuu wa mwakani, Maalim Seif kuendelea kutafuta haki yake mahakamani kungeweza kumkuta akiwa bado kwenye korido za mahakama wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ujao. Ni vigumu mno kwa chama cha siasa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi mkuu huku kikiwa kinakabiliwa na mpasuko katika uongozi wake wa juu.

Kwahiyo, kimkakati, uamuzi huo wa Maalim Seif unaeleweka, na unaweza kuwa ni mbinu muhimu kwake kuendelea kuwa relevant kisiasa.

Hata hivyo, kuna uwezekano wa aina mbili kuhusu mustakabali wa Maalim Seif na wa chama chake kipya cha ACT- Wazalendo.

Uwezekano wa kwanza ni kwa chama hicho kuibuka kuwa tishio katika siasa za Tanzania. ACT – Wazalendo ni chama kizuri lakini ambacho hakikui. Kimeendelea kuwa "chama cha mtu mmoja" chini ya uongozi wa Zitto Kabwe. Kwa muda mwingine, chama hicho kimekuwa cha kiharakati zaidi kuliko cha kisiasa.

Mapungufu hayo yanaweza kubadilika kwa njia kuu tatu. Kwanza, Maalim Seif hajawahi kupata fursa nzuri ya kunadi mvuto wake kwenye majukwaa ya siasa za Tanzania Bara. ACT-Wazalendo wanaweza kuwa Jukwaa muhimu katika hilo.

Pili, Zitto  hajawahi kupata jukwaa mwafaka kunadi mvuto wake wa kisiasa huko Zanzibar. Kwa kuungana na Maalim Seif, hii inaweza kuwa ndio fursa mwafaka kwake.

Tatu, ACT-Wazalendo kama chama inaweza kupata fursa mwafaja kabisa ya kuwa chama cha kitaifa badala ya kuwa "chama cha Kigoma."

Haya yote yatawezekana tu endapo kutakuwa na "kujitoa mhanga" kati ya mwenyeji Zitto na mgeni Maalim Seif. Kwa mara ya kwanza, Zitto atajikuta akiongoza chama ambacho ndani yake kuna mwanasiasa maarufu zaidi yake. Naam, Maalim Seif ni mkongwe zaidi kisiasa kuliko Zitto. Endapo Zitto "atajitoa mhanga" (make a sacrifice) na kukubali "kumezwa" na umaarufu wa Maalim Seif, basi chama hicho kitakuwa na fursa kubwa ya kupanuka zaidi na hata kuja kuwa chama kikuu cha upinzani katika pande zote za Muungano.

Lakini endapo kutakuwa na mgongano wa ego kati ya wanasiasa hao, basi mustakabali wa chama hicho utakuwa mashakani. Lakini pengine uwezekano wa hili kutokea ni mdogo kutokana na ukweli kwamba suala la Maalim Seif kujiunga na ACT-Wazalendo sio limetokea tu ghafla. Ni dhahiri kuwa kulikuwa na majadiliano ya muda mrefu na yayumkinika kuhisi kwamba tofauti kati ya wanasiasa hao wawili (Maalim Seif na Zitto) zilifanyiwa kazi wakati wa majadiliano hayo.

Suala jingine ambalo linaweza kuijenga ACT-Wazalendo "mpya" (ya Zitto na Maalim Seif) au kuibomoa ni mtihani ulioikumba Chadema mwaka 2015.

Kwa mwelekeo ulivyo ndani ya CCM ambapo Magufuli hafanyi siri kuwa anataka chama hicho kiwe chini ya uongozi wa watu wake (wengi wao wakiwa wana-Kanda ya Ziwa wenzake), kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka wimbi kubwa tu la wanasiasa wenye majina watakaotaka kuhamia Upinzani. Na endapo Zitto na Maalim Seif watakuwa "dream team" ya kuaminika, basi ACT-Wazalendo inaweza kuwa na mvuto zaidi kwa "wakimbizi kutoka CCM" kuliko Chadema.

Si ajabu kwa wanasiasa kama Nape Nnauye, Mwigulu Nchemba, Bernard Membe kujiunga na ACT-Wazalendo endapo chama hicho kitaonekana kuwa kinaweza kutoa ushindani wa dhati dhidi ya CCM hapo mwakani.

Sasa, wakati kupokea "majina makubwa" kutoka CCM husaidia kuongeaza umaarufu wa chama, uzoefu umeonyesha kuwa wengi wao wenye majina hayo makubwa ni wanafiki wanaokwenda upinzani kwa sababu zao binafsi na sio kwa maslahi ya vyama husika vya upinzani.
Kibaya zaidi, kila ujio wa "wahamiaji" hao ni fursa mwafaka kwa CCM kupandikiza "mamluki" wake kama ilivyotokea kwa Chadema ilipompokea Lowassa mwaka 2015.

Je ACT-Wazalendo "mpya" inaweza kutoa upinzani wa dhati dhidi ya CCM hapo mwakani? Jibu fupi ni "muda ndio utaongea" (time will tell). Jibu pana zaidi ni kwamba japo uwezekano huo upo lakini sidhani kama muda unatosha kukitanua chama hicho nchi nzima hususan katika kipindi hiki ambacho chama pekee cha siasa kinachoruhusiwa kufanya shughuli za siasa ni CCM tu.

Hata hivyo, endapo mkazo wa ACT-Wazalendo utakuwa katika sio tu kuongeza idadi ya wanachama bali kujenga kuaminika kwa "Watanzania wasio na vyama," basi huenda chama hicho kikafanya vizuri kwenye uchaguzi mkuu huo.

Ni hivi, kundi muhimu kabisa la wapigakura katika uchaguzi mkuu wowote ule nchini Tanzania ni "Watanzania wasio na vyama." Kwamba, hakuna chama cha upinzani kinachohitaji kupoteza muda wake kuwashawishi wafuasi wa CCM wakipigia kura, kama ambavyo CCM haina muda na wafuasi wa upinzani kuwashawishi waipigie kura. Vilevile, si CCM wala vyama vya upinzani vinavyohitaji kuwashawishi wanachama/wafuasi wao wapigie kura vyama vyao. Watu wanaohitaji kushawishiwa ni hao wasio na vyama. Na habari njema ni kwamba kundi hilo ndilo lwenye idadi kubwa zaidi ya wapiga kura.

Kwa mujibu wa takwimu zisizo rasmi, CCM ina takriban wanachama milioni 8 ilhali wapinzani wana wanachama takriban milioni 5. Kwa makadirio, takriban Watanzania milioni 25 walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Kwahiyo, milioni 8 wa CCM jumlisha milioni 5 wa upinzani jumla inakuwa milioni 13. Ukichukua milioni 25 kutoa miloni 13 unabakiwa na milioni 12. Kwa makadirio, hawa ni "wapigakura wasio na vyama." Na kimahesabu, hata nusu tu ya kundi hili likielemea upande mmoja, upande huo unaweza kabisa kushinda uchaguzi husika. Of course, hapo tunaweka kando hujuma za kawaida za kuibeba CCM kwenye takriban kila uchaguzi mkuu.

Nimalizie kwa kukumbusha kuwa uchambuzi huu sio exact science. Umeelemea kwenye uelewa wa kutosha wa mchambuzi kuhusu siasa za Tanzania.

Kadhalika, uchambuzi huu ni endelevu. Utafanyiwa marejeo mara kwa mra kila kutakapokuwa na umuhimu wa kufanya hivyo


18 Feb 2018


Nianze makala hii kwa kutoa salamu zangu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Daniel John, ambaye hadi alipouawa kinyama alikuwa Katibu wa Chadema kata ya Hananasifu, na pia kwa familia, ndugu,jamaa na marafiki wa marehemu Acqulina Akwilin (samahani kama nimekosea jina).

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, mwili wa marehemu Daniel uliokotwa kwenye ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam ukiwa na majeraha. Alieleza kuwa awali marehemu alichukuliwa na Land Rover nyeupe na watu waliohifanya askari polisi, lakini tangu wakati huo Polisi hawakuwa na taarifa zozote za kiuchunguzi, na hata jitihada za kupatikana mwili huo zilifanywa na Chadema wenyewe.




Kwa upande wa marehemu Acquilina, kifo chake kilisababishwa na kasumba hatari inayozidi kuzoeleka kwa watumishi wa vyombo vya dola kufanya mzaha katika matumizi ya silaha za moto, ambapo katika tukio husika, polisi waliokuwa wakizuwia maandamano ya wafuasi wa Chadema, walitumia risasi za moto,na moja kati ya risasi hizo ilipelekea kifo cha binto huyo, ambaye hadi mauti yanamfika alikuwa mwanafunzi katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) akisomea shahada ya ununuzi na ugavi.
Ni muhimu kutambua kuwa vifo vyote hivi viwili vingeweza kuepukika laiti utu na ubinadamu wetu ungewekwa mbele ya chuki za kisiasa. Huhitaji kuwa mjuzi wa uchunguzi wa mauaji kufahamu kuwa vifo hivyo ni matokeo ya chuki, hujuma, uonevu na kila aina ya baya dhidi ya chama kikuu cha upinzani, Chadema, kuhusiana na kampeni za uchaguzi mdogo katika jimbo la Kinondoni, ambalo kama ilivyo kwa jimbo la Siha, ni "piga ua" kwa CCM ishinde. Yaani chama hicho tawala kilitarajiwa kutumia kila mbinu kuhakikisha inashinda katika majimbo hayo mawili.

Lakini kabda sijaingia kwa undani katika mada hii - ambayo lazima nikiri kwamba inanipa wakati mgumu sana kuiandika kwa sababu nimebanwa na mchanganyiko wa majonzi na hasira, sambamba na hofu ya kuona taifa langu likisukumwa kuelekea kwenye upotevu wa amani na mshikamano wetu – naomba kuweka wazi masuala matatu ya msingi kunihusu mie mwandishi wa mwakala hii.

Kwanza, mimi licha ya kuwa na makazi nje ya Tanzania kwa takriban miaka 15 sasa bado no Mtanzania. Utanzania wangu ni haki nilioirithi kutoka kwa wazazi wangu, na itabaki hivyo milele. Naeleza hili kwa sababu kuwa wabaguzi wanaopenda kutuhukumu Watanzania tunaoishi huku ughaibuni, na kutaka tuonekane kama Utanzania wetu sio kamili. Kwa mantiki hiyo, kama Mtanzania, nina kila haki ya kutoa maoni yangu kuhusu mustakabali wa taifa letu, hususan katika nyakati hizi ambapo kuna dalili za wanaotaka kulipeleka kubaya taifa letu.

Pili, mwaka 2015 nilishiriki kikamilifu katika kampeni zilizomwingiza madarakani Rais John Magufuli. Kwa upande mmoja nililazimika kumkampenia Magufuli kwa vile nilikuwa nina "sababu binafsi" dhidi ya aliyekuwa mpinzani wake mkuu, mgombea urais wa tiketi ya UKAWA, Edward Lowassa. Wanasema "adui ya adui yako ni rafiki yako."Kwa upande mwingine, nililipwa kutoa huduma ya ushauri wa kitaalamu (usadi, yaani consultancy kwa kimombo) hususan kwenye mitandao ya kijamii. Natanabaisha hili ili asije akakurupuka mtu na kusema "ah ulishiriki kutupigia kampeni kwa vile tulikupa pesa."

Tatu, huko nyuma nilikuwa mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa. Na kabla ya kuanza utumishi katika taaluma hiyo muhimu na nyeti, nilikula kiapo kwa nchi yangu, kiapo ambacho nitaishi nacho hadi ninaingia kaburini. Kiapo hicho sio cha kukitumikia chama flani au viongozi wake bali Tanzania yetu. Nchi ni muhimu  kuliko vyama vya siasa au wanasiasa.

Mtu aliyepikwa na kuiva kwenye taaluma ya uafisa usalama wa taifa, katika nchi yoyote ile, anapaswa kubaki kuwa mtiifu kwa nchi yake bila kujali yupo ndani au nje ya ajira ya taasisi inayohusika na usalama wa taifa wa nchi husika.

Wanasema hata nje ya ajira rasmi, kila mtu aliyewahi kuwa afisa usalama wa taifa anaendeshwa na "sense of public duty born in their previous lives" yaani wajibu kwa umma uliozaliwa katika maisha yao huko nyuma. Jasusi mmoja mstaafu anaeleza “...I have obligations, professional obligations. If there’s a national security emergency or possible national security issue, I should report it."


Kwahiyo, hata kama "maafisa wenzangu wa zamani" wataamua kukaa kimya kwa sababu moja au nyingine – wengi wanahofia usalama wa maisha yao – sie wengine hatuwezi kukaa kimya, hasa kwa vile baadhi yetu tumeshalipa gharama kubwa kwa kelele zetu. Kukaa kimya ni sawa na kuafiki uhuni unaoendelea ambao ni tishio kwa usalama wa taifa.

Lakini licha ya wajibu huo unaotokana na utumishi wetu kwa nchi huko nyuma, Rais Magufuli amefanikiwa kuvifunga mdomo vyombo vya habari kiasi kwamba haviwezi kusema lolote kuhusu "mabaya" yake, na amefanikiwa kuvijengea nidhamu ya uoga vyombo hivyo vya habari kiasi kwamba habari pekee zenye umuhimu kwao ni za kumtukuza na kumpamba "mungu-mtu" huyo. Kwahiyo na sie tuliopikwa na kuiva kuhusu ujasiri, kujitoa mhanga na kutokuwa waoga tukiufyata na kukaa kimya - ilhali media zetu ndio zishapigwa kufuli - hali itazidi kuwa mbaya.


Baada ya kuweka wazi nafasi yangu, sasa tuangalie kwa kina kinachoendelea huko nyumbani hasa kuhusiana na uchaguzi mdogo kwenye jimbo la Kinondoni na Siha na kuuawa kwa Daudi na Acquiline.

Ni muhimu kutambua kwamba ukandamizaji dhidi ya vyama vya upinzani sio kitu kilichoanza chini ya utawala wa Magufuli bali hali hiyo imedumu mfululzo tangu kuanzishwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1992. Labda kilicho tofauti kwa zama hizi ni "ujasiri" wa Magufuli kutoficha chuki yake dhidi ya vyama vya upinzani. Yaani angalau akina Mwinyi,Mkapa na Kikwete walikuwa "wanauma na kupuliza." Kwamba angalau walikuwa na "mshipa wa aibu" na walijitahidi japo kutowaonea Wapinzani waziwazi.

Kwa wanaojua "yanayojiri nyuma ya pazia" watakwambia kuwa hujuma dhidi ya vyama vya upinzani ni miongoni mwa vipaumbele vikubwa kwa CCM na serikali zake, na hiyo imepelekea kujengeka "symbiotic relationship" kati ya chama hicho tawala na taasisi za dola, ambapo kila mmoja anategemea uhai wa mwenzie.

Lakini kama kuna kitu kinachokera zaidi kuhusu hujuma dhidi ya demokrasia ni pale CCM na taasisi zake hasa za dola wanapoweka mbele maslahi yao mbele ya utu na uhai wa Watanzania. Na hili halijaanza jana au katika kampeni za chaguzi ndogo katika majimbo ya Kinondoni na Siha.

Uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 ulihusisha matukio mengi tu ambayo kwa makusudi hayapo kwenye kumbukumbu za wazi (japo yamehifadhiwa mahala flani).

Lakini kama wanavyosema "amekula asali sasa anachonga mzinga," baada ya hujuma za kimyakimya za mwaka 1995 kuzaa matunda, CCM na taasisi zake ikanogewa, na matokeo yake ni kwamba uchaguzi mkuu uliofuata, mwaka 2000 uliweka doa kubwa kwa historia ya Tanzania yetu ambapo kwa mara ya kwanza nchi yetu ilizalisha wakimbizi kufuatia unyama uliofanyika huko Zanzibar na kupelekea vifo kadhaa (idadi halisi ya vifo haijawahi kuwekwa hadharani japo "wenyewe" walisema zaidi ya watu 19 ndio waliokufa kwenye machafuko hayo. Wasichosema pia ni idadi ya watu waliobakwa, kuteswa na kuwekwa kizuizini.

Kwamba hujuma hizo za CCM dhidi ya demokrasia zilipelekea vifo na majeruhi ni kitu kibaya kabisa. Lakini kitu kingine kibaya ni ukweli kwamba hakuna mtu hata mmoja aliyechukuliwa hata kutokana na unyAma waliofanyiwa Wazanzibari hao.

Kwa namna ya kipekee, CCM ikawa kama imepewa ruhusa ya kutumia vyombo vyake vya dola kufanya lolote itakalo ili ifanikishe hujuma zake dhidi ya Wapinzani na demokrasia kwa ujumla, kisha iibuke na ushindi.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ulikuwa na "uchafu kupindukia." Kundi lililofahamika kama "mtandao" lilijipenyeza katika kila sekta, kuanzia kwenye vyombo vya habari, taasisi za dola hadi kwenye taasisi za dini. Yayumkinika kabisa kuhitimisha kwamba yaliyojiri wakati "mtandao unafanya jitihada za kumwingiza mtu wao Ikulu" ni mabaya zaidi ya haya tunayoshuhudia sasa tangu Magufuli aingie madarakani.

Kwanini basi hayo yaliyojiri kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 hayajulikani? Jibu ni kwamba, wakati mbinu iliyotumika mwaka 1995 na 2000 ilitegemea zaidi vyombo vya dola, uchaguzi wa mwaka 2005 na 2010 ulitegemea zaidi nguvu ya fedha, nyingi zikiwa fedha haramu. Na sehemu ya fedha hiyo ilitumika "kununua ukimya" wa wanahabari wengi tu. 

Lakini si fedha tu bali pia kuna hujuma mbalimbali – nyingine chafu na za kuchefua – zilizotawala safari za ushindi wa chama tawala kwenye chaguzi hizo.


Image result for lowassa kikwete 2005

Labda tofauti nyingine kuhusu mwaka 2005 na 2010 ni ukweli kwamba wakati chaguzi hizo zilihusisha "kikundi binafsi" yaani hicho cha wanamtandao ambacho hakikuwa taasisi ya serikali au chama.

Lakini muda wote huo, CCM ilikuwa kama imepwa ruhusa na Watanzania kuendeleza hujuma zake dhidi ya Wapinzani na demokrasia kwa ujumla. Hakujawahi na utashi miongoni mwa Watanzania kutaka kukabiliana kwa dhati za uhuni/uhalifu wa kisiasa. Na kwa bahati mbaya, kwa vile vipaumbele vya Watanzania wengi ni kwenye "ubuyu" na "kubeti/mkeka" basi habari mbaya ni uwezekano wa CCM kuendelea kufanya itakavyo kwa muda mrefu sana.

Sio kama kwa kubashiri kuwa unyanyasaji wa CCM utaendelea muda mrefu sana ninamaanisha kuwa nimekata tamaa. Hapana. Ninakuwa mkweli tu. Tatizo ni zaidi ya CCM na uhuni wake. Watanzania wenyewe ni sehemu ya mfumo unaowezesha CCM kufanya uhuni/uhalifu huo.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ulihusisha pia matuki kadhaa yaliyojiri "nyuma ya pazia." Na ukitaka kufahamu kuwa Tanzania yetu haijawahi kuhangaishwa na mauaji ya kisiasa – kuanzia yale ya mwaka 2001 huko Zanzibar hadi haya ya Daudi wa Hananasifu na dada Acquilina – ni kifo cha Mchungaji Christopher Mtikila.


Kwahiyo, na ninaandika haya kwa uchungu mkubwa uliochanganyika na hasira, kuuawa kwa Daudi na Acquilina kutaishia kuwa moja tu ya matuko yaliyowahi kutokea katika Tanzania yetu. Tutawasikia wanasiasa wetu wa vyama vya upinzani wakiongea kwa hisia kubwa. Tutashuhudia pia wanafiki wengi tu miongoni mwa wasanii wetu nao wakijifanya kuguswa na vifo hivyo, lakini wakiwa makini kuepuka kumuudhi "Bashite na baba yake" au kuitibua CCM. Tutashuhudia pia kundi la wanafiki hatari ndani ya CCM wakijifanya kuumizwa na mauaji hayo, na kutaka uchunguzi ufanyike, ilhali nao ni kondoo waliojivika ngozi ya mbwa mwitu.



Kama ambavyo "mauaji mengine ya kisiasa" yalivyoruhusiwa kupita kimyakimya, ndivyo unyama huu uliofanywa dhidi ya Daudi na Acquilina utakavyoruhusiwa uishe kimyakimya.

Kwa upande mmoja tusitarajie Rais Magufuli awajibike – sio kwa yeye binafsi kujiuzulu kwa sababu hilo litakuwa kutarajia zaidi ya muujiza – kwa kumtimua Waziri husika na watendaji katika jeshi la polisi. Kwa upande mwingine, hakuna wa kumshinikiza Rais Magufuli achukue hatua stahili dhidi ya wahusika.

Na nisingependa kuuma maneno hapa. Yeye Magufuli mwenyewe ni chanzo muhimu cha siasa hizi za uhasama zinazoendelea kuitafuna Tanzania yetu. Huyu ni mtu ambaye wala hapati shida kuonyesha chuki zake za waziwazi dhidi ya Wapinzani, Upinzani na demokrasia kwa ujumla.


Kama ilivyo kwa madikteta wengine duniani, Magufuli amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutumia ajenda yake ya ufisadi kama kisingizio cha kusigina haki za binadamu nchini Tanzania, na kubinya kila fursa ya haki za kidemokrasia na uhuru wa habari. Kama nilivyoeleza awali, amefanikiwa kuviziba midomo vyombo vya habari na ndio maana hata habari za kusikitisha kuhusu mauaji ya Daudi na Acquiline hazijaripotiwa vya kutosha.

Kwa kuviziba midomo vyombo vya habari Magufuli amefanikiwa kuzuwia "habari asizozipenda" na ndio maana hadi muda huu ni Watanzania wachache tu wanaofahamu kilichojiri huko MKIRU katika kilichoitwa "operesheni dhidi ya ugaidi." Kuna siku yaliyojiri huko – na ambayo yamechangia "kupotea" kwa mwandishi wa gazeti la Mwananchi Azory Gwanda – yatajulikana hadharani. Haijalishi itachukua miaka mingapi.


Lakini "yaliyojiri MKIRU" ni uthibitisho mwingine wa hicho nilichoeleza hapo juu kuwa Watanzania wenyewe ndio wanaopaswa kubeba lawama nyingi katika kasumba ya CCM kutojali uhai katika harakati zake za kukandamiza demokrasia. Kwamba kama yaliyojiri MKIRU yameachwa yaishe kienyeji, kwanini tutegemee hali tofauti kwa vifo vya Daudi na Acquiline?

Kama ndugu zetu wa Chadema (na kila mpenda haki) "wamekubali yaishe" kuhusu kifo cha Kamanda Mashaka, "kupotea" kwa kada Ben Saanane (hata zile kampeni za #BringBackBenAlive zimejifia kifo cha asili), na hawasumbuliwi na serikali ya Magufuli kupuuzia jaribio la mauaji dhidi ya Tundu Lissu, kwanini tutarajie jipya katika mauaji yaliyofanywa dhidi ya Daudi na Acquiline?

Yaani Mnadhimu Mkuu wa upinzani anamwagiwa risasi hadharani wakati mkutano wa bunge unaendelea huko Dodoma, na tunaambiwa kuwa tukio hilo lilitokea katika eneo lenye ulinzi mkubwa na lenye CCTV, kwanini basi wanaosumbuliwa na tukio hilo wasitafute njia stahili za japo kuifanya serikali ione aibu na kufanya japo "uchunguzi wa kizushi"?

Kuhusu hujuma "za kawaida" za uchaguzi, kama kila aina ya uhuni uliofanywa na CCM kwenye chaguzi ndogo za madiwani katika kata 43 uliofanyika Novemba mwaka jana uliruhusiwa upite "kimya kimya" – kwa maana kwamba hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya uhuni huo – kwanini basi chaguzi hizi ndogo katika jimbo la Siha na Kinondoni zilitarajiwa kuwa tofauti?

Na katika hili, inapaswa wana-Chadema wajiulize kuhusu busara za viongozi wao kuamua kushiriki katika chaguzi hizo ndogo Siha na Kinondoni ilhali mazingira yaliyokuwepo yalikuwa yaleyale yaliyopelekea chama hicho kususia chaguzi nyingine ndogo tatu katika majimbo ya Longido, Singida Kaskazini na Songea Mjini uliofanyika mwezi uliopita.

Hadi wakati ninaandika makala hii, tayari Tume ya Uachaguzi ilikuwa imeshamtangaza mgombea wa CCM jimbo la Siha, Godwin Mollel kuwa mshindi kwa tofauti kubwa tu ya kura dhidi ya mgombea wa Chadema. Hata kama CCM wameiba kura, ukubwa wa tofauti kati ya kura za mgombea wao na huyo wa Chadema zinaashiria kuwa chama hicho kikuu cha upinzani kilipitisha mgombea fyongo.


Na kama ilivyotarajiwa mgombea wa CCM jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia, naye ametangazwa mshindi.


Mie mtumishi wako nilishabashiri mapema tu kuwa chama hicho tawala kingeshinda majimbo hayo, "iwe isiwe."

Ushindi kwa wagombea hao wa CCM ulipaswa kupatikana kwa gharama yoyote kwa sababu laiti wangeshindwa, kinachoelezwa kama "mkakati wa Magufuli kuua upinzani kwa kununua wabunge na madiwani wa Upinzani"  kingemfanya achekwe hata huko kwenye chama chake.

Na kwa vile hadi sasa wabunge na madiwani waliohama upinzani na kujiunga na CCM wamefanikiwa kurudi madarakani baada ya chama hicho tawala kuwapa fursa ya kuwa wagombea wake kwenye chaguzi ndogo, na kuwasaidia kwa hali na mali washinde, tutarajie wabunge na madiwani wengin zaidi kuhama vyama vya upinzani na kujiunga na CCM. Kisa? "Dili hilo linalipa," kwa CCM na kwa wanasiasa hao wanaohama.

Na unadhani mbunge au diwani "mwenye moyo mwepesi" akiona jinsi chama chake "kilivyochukulia poa" yaliyowasibu akina marehemu Mashaka na Daudi, na yaliyowasibu Ben Saanane na Lissu, kwanini iwe ngumu kwake kushawishika kuhama?

Ningetamani sana kuhitimisha makala hii kwa kushauri nini kifanyike lakini itakuwa kupoteza muda wangu na muda wako msomaji. Ni vigumu mno kuwashauri watu waliokubali kwamba mgao wa umeme ni stahili yao kwa zaidi ya miaka kumi sasa, na ambao kila mara umeme unaporudi wanashangilia kana kwamba wamepewa upendeleo flani.

Kama Watanzania wameshindwa kuilazimisha Tanesko iache mgao wa umeme, wataweza kweli kuilazimisha CCM iache hujuma dhidi ya vyama vya upinzani na demokrasia kwa ujumla? Ndio maana bila utu wala aibu, chama hicho tawala kinapata ujasiri wa kukifanyia mzaha kifo cha Acquiline ambapo kwa kudai polisi (haohao waliomuua binti huyo) wachukue hatua dhidi ya Mbowe. Utterly disgusting!


Na kama mauaji mbalimbali ya kisiasa huko nyuma yameachwa yapite na kusahaulika, kwanini tutarajie miujiza kwenye mauaji haya ya sasa dhidi ya wapendwa wetu Daudi na Acquline?

Na ukweli mchungu ni kwamba Magufuli ataendelea kuwapelekesha Watanzania atakavyo ka sababu si watangulizi wake -Mwinyi, Mkapa na Kikwete – wenye jeuri ya kumwambia "Ee bwana ee, huku unakoipeleka nchi siko." Hawawezi kwa sababu nao ni kama "mateka." Madhambi waliyofanya kwenye tawala zao yanawafanya wahofie hatma yao pindi wakimkosoa "mungu-mtu" aliyepo madarakani.

Na wakati wastaafu au watumishi wa zamani wa Idara za Usalama wa Taifa kwenye nchi kama Marekani wamekuwa mstari wa mbele kukemea kila tendo linalotishia usalama wa nchi hiyo – kwa mfano 'ndoa' kati ya Rais Donald Trump na Russia – wastaafu wetu sie hawana jeuri ya kufungua mdomo sio tu kwa vile wanahofia kuathiri posho na marupurupu yao bali kwa vile nao ni mateka wa "madudu" waliyofanya walipokuwa madarakani. Ukiwa mchafu unajinyima uhuru wa kukemea uchafu.


Basi niishie hapa kwa kurejea tena salamu zangu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Daudi na Acquiline. Ni vigumu kuwaambia maneno yanayotosha kuwaliwaza lakini la muhimu ni kuendelea kuzikumbuka roho za marehemu hao, hasa katika kipindi hiki cha Kwaresma ambapo sisi Wakristu tunaadhimisha mateso ya Bwana Yesu Kristo. Pumziko la Milele awape Bwana, na Mwanga wa Milele awaangazie, wapumzike kwa amani. Amen


31 Oct 2017



Pasipo kutarajiwa, jana, Jumatatu ya Oktoba 30, 2017, anga za habari huko nyumbani Tanzania zilitawaliwa na habari moja nzito: mmoja wa wana-CCM maarufu, Mbunge kwa tiketi ya chama hicho tawala anayewakilisha jimbo la Singida Kaskazini, na Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Nne, Bwana Lazaro Nyalandu, alitangaza kujivua uanachama wa CCM na kuomba kujiunga na chama kikuu cha upinzani cha Chadema.


Tukio hilo lilileta mshangao mkubwa kwa sababu kadhaa. Kwanza, licha ya matamshi ya hivi karibuni ya Nyalandu kuhusu haja ya kurejeshwa mchakato wa Katiba mpya, sambamba na kuwasihi wabunge wenzie wa CCM kupinga kwa nguvu zote jaribio la kurefusha muda wa Rais madarakani, hakukuwa na dalili kubwa na za waziwazi iwapo kuna ‘kutofautiana’ kati ya Nyalandu na chama chake.


Na hata kama kungekuwa na dalili hizo – kwa kificho au wazi – bado wananchi wengi wangepokea habari hizo kwa mshtuko mkubwa.

Sababu ya pili ya mshangao kuhusu tukio hilo ni ukweli kwamba mwanasiasa wa chama tawala kuamua kujiunga na upinzani, tena miaka mitatu hivi kabla ya uchaguzi mkuu, ni suala ambalo licha ya kuhitaji ujasiri mkubwa pia linaacha maswali kadhaa ambayo pengine sio rahisi kuyapatia majibu.

Hadi wakati ninaandika uchambuzi huu, kilicho bayana kuhusu sababu za Nyalandu kuchukua uamuzi huo ni sababu alizotanabaisha mwenyewe katika tamko lake kwa umma.

Akizungumza jana, mwanasiasa huyo alidai sababu ya kuchukua uamuzi huo ni kutokuridhishwa na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa Watanzania na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi ya mihimili ya dola yaani Serikali, Bunge na Mahakama.

Lakini hata kabla ya kuchukua uamuzi huo jana, Nyalandu alishaonyesha dalili ya kutofautiana na wana-CCM wenzie, hasa kwa uamuzi wake wa kumtembelea Mbunge Tundu Lissu wa Chadema aliyelazwa huko Nairobi, Kenya kufuatia jaribio la kumuua. Hadi sasa, Nyalandu anabaki kuwa kiongozi wa ngazi za juu wa CCM kumtembelea Lissu huko Kenya.


Huku kukiwa na tetesi kwamba uongozi wa juu wa CCM umewapiga marufuku viongozi wake kujihusisha na suala la Lissu, uamuzi wa Nyalandu kwenye Kenya ‘kinyume na maagizo ya chama chake’ ulihisiwa kuwa ungemwingiza matatizoni.

Dalili nyingine kuwa mwanasiasa huyo hakuwa akipendezwa na baadhi ya mienendo ndani ya CCM ni pale alipoibuka kuhamasisha haja ya kuanzisha upya mchakato wa kupatikana Katiba mpya, sambamba na kuhamasisha wana-CCM wenzake dhidi ya jitihada za chini chini kuongeza muda wa Rais madarakani.

Masuala yote hayo mawili yalitarajiwa ‘kumsababishia matatizo’ mwanasiasa huyo.

Hata hivyo, kuna ‘sababu mbadala’ kuhusu uamuzi wa Nyalandu kujiuzulu. Kuna taarifa kwamba kuna uchunguzi unaofanyika dhidi ya mwanasiasa huyo kuhusiana na utumishi wake kama Waziri wa zamani wa Maliasi na Utalii. Taarifa hizo ambazo bado ni tetesi hadi muda huu, zinaweza kupewa uzito zaidi na ‘screenshot’ inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikidaiwa kuwa ni ya mazungumzo ya kundi la Whatsapp la viongozi wanawake wa CCM.

Katika ‘chat’ husika, mmoja wa makada wa kike wa CCM anadai kuwa kuna uchunguzi unaofanyika dhidi ya Nyalandu alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, na kwamba uamuzi wa kujiondoa CCM na kuomba kujiunga na Chadema una lengo la kugeuza suala hilo kuwa la kisiasa pindi akichukuliwa hatua.

Pengine swali muhimu linaloendelea kutawala vichwa ni “kwanini HASWA Nyalandu amejiuzulu?” Kuna sababu alizotoa yeye mwenyewe, ambazo kwa kiasi kikubwa zinaleta mantiki, lakini pia kuna hiyo tetesi kuwa amechukua uamuzi huo kama tahadhari pindi akianzishiwa tuhuma za ufisadi.

Tuchambue sababu zote mbili, yaani alizotoa mwenyewe na hizo tetesi. Kwa vile hatuna maelezo yenye uhakika yaliyo kinyume na sababu alizotoa Nyalandu, nadhani kwa kuzingatia busara tu, itakuwa sio sahihi kudhani anaongopa. Unapopinga kauli ya mtu basi shurti uwe na kauli mbadala yenye uthibitisho. Kwahiyo, angalau kwa muda huu, hakuna sababu za msingi za kupinga sababu alizotoa mwanasiasa huyo.

Kuhusu tetesi za kuwepo kwa mchakato wa ‘kumshughulikia kutokana na tuhuma za ufisadi,’ kuna mantiki kwa mbali, na utata kwa mbali pia. Sio siri kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii ilikuwa kama ‘makao makuu’ ya ufisadi. Wizara hiyo ilikuwa kama ile ya Nishati na Madini, ambapo mawaziri lukuki walihamishwa au kuondolewa madarakani kutokana na tuhuma za ufisadi.

Kwamba Nyalandu alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kulikuwa na tuhuma za ufisadi, hilo halina mjadala. Lakini kwa kuzingatia kanuni ya asili ya haki, tuhuma hizo zinabaki tuhuma tu mpaka zitakapothibitishwa.

Kwahiyo, hadi hapa, mantiki ya mbali kuhusu uwezekano wa uchunguzi wa tuhuma za ufisadi dhidi ya Nyalandu ipo. Hata hivyo, utata wa mbali ni kwamba katika mazingira ya kawaida tu, na tukijifanya kuamini (angalau kwa minajili ya uchambuzi huu) kwa Nyalandu anafahamu kuhusu uchunguzi huo, je isingekuwa mwafaka kwa yeye kupambana na suala hilo akiwa CCM kuliko nje ya chama hicho tawala?

Sawa, kuna hiyo hoja ya “amehama CCM na anataka kuhamia Chadema ili pindi akichukuliwa hatua, suala hilo lionekane la kisiasa,” lakini ikumbukwe kuwa suala la muhimu sio “suala lionekane la kisiasa” bali “lisitokee kabisa.” Na katika mazingira ya kawaida, huo uamuzi wa tu Nyalandu kuhama CCM na kuikosoa hadharani unatosha kuipa serikali ya chama hicho tawala na taasisi zake “hasira” dhidi ya mwanasiasa huyo. Na hapo hatujagusia uwezekano wa mwanasiasa huyo kujiunga na “adui nambari moja wa CCM” yaani Chadema.

Kwa mtazamo wangu, kama ni kweli kuna uchunguzi unaoendelea au unaotarajiwa kufanyika kuhusu Nyalandu basi yayumkinika kuhisi kwamba ingekuwa rahisi zaidi kwa yeye kupambana na suala hilo akiwa ndani ya CCM kuliko nje ya chama hicho chenye historia ya siasa za kinyongo, visasi na majitaka.

Lakini kuna ‘angle’ kubwa zaidi katika uamuzi huo wa Nyalandu. Yawezekana amesoma vema upepo wa kisiasa huko nyumbani chini ya utawala wa Rais Magufuli, na kubaini vitu kadhaa. Moja laweza kuwa kinachoonekana kama wananchi wengi kutoridhishwa na utawala wa Magufuli, ndani na nje ya CCM. Keyword hapa ni ‘kinachoonekana,’ nikimaanisha pengine ni hisia tu kuwa kuna wananchi wengi wasioridhishwa ilhali ukweli ni kinyume na hisia hiyo.

Kwa minajili ya uchambuzi huu, tufanye kuwa hisia hizo zipo kweli. Kwahiyo, kwa vile Nyalandu alikuwa miongoni mwa makada wa CCM walioomba ridhaa ya chama hicho kuwa wagombea wa urais mwaka 2015 lakini haukufanikiwa, basi pengine anataka kutupa kete yake kupitia upande wa upinzani.

Lakini sio tu kusukumwa na nia ya kuwania urais, lakini yayumkinika kuhisi kuwa mazingira yaliyopo muda huu yanampatia mwana-CCM yeyote nafasi nzuri ya kukikimbia chama hicho. Sio siri kuwa hisia kwamba Magufuli ana dalili za udikteta zinazidi kushika hatamu. Kwa maana hiyo, hata mtu mwenye sababu zake binafsi akikurupuka na kutamka “ninahama CCM kwa sababu utawala wa Magufuli ni wa kidikteta” ataeleweka kirahisi, na anaweza kuungwa mkono kirahisi pia.

Kwamba Nyalandu anaweza “kuruka kutoka kwenye ngalawa na kuingia majini kwenye bahari yenye papa na nyangumi” sio suala dogo. Kama kuikosoa CCM ukiwa ndani ya chama hicho ni hatari, sote twafahamu nini kinachoweza kumkumba anayediriki sio kukosoa tu bali pia kuhama chama hicho tawala. Kwa mantiki hiyo, kwa sababu yoyote ile – iwe hizo alizotaja mwenyewe au tetesi za uchunguzi wa ufisadi – mwanasiasa huyo amefanya maamuzi magumu, na yayumkinika kuamini kuwa amejiridhisha vya kutosha kabla ya kuchukua uamuzi huo.

Kuna mambo matatu yanayoweza kutoa mwangaza kidogo. Kwanza, hivi karibuni, Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Dokta Hamis Kigwangallah alinukuliwa akisema kwamba anayo orodha ya watu mashuhuri, viongozi wastaafu na wabunge wanaojihusisha na ujangili, na atahakikisha anawashughulikia.

Pili, jana katika hotuba yake akiwa huko Mwanza, Rais Magufuli alikumbushia kuhusu Mahakama Maalum ya Ufisadi, ambayo pasi kuuma maneno, imekuwa kama kichekesho kutokana na kukosa kesi. Rais kuitaja mahakama hiyo ‘isiyo na ufanisi angalau hadi sasa’ inaweza kumaanisha kilekile alichokigusia Waziri Kigwangallah kuhusu ujangili.

Na tatu, ‘vijana wa Lumumba’ (makada wa CCM kwenye mitandao ya kijamii) walishaanza kuzungumzia ‘ufisadi wa Nyalandu’ mara tu alipoenda Nairobi kumjulia hali Lissu. Na kasi yao ya mashambulizi dhidi ya Nyalandu imepamba moto zaidi jana baada ya mwanasiasa huyo kutangaza kujiondoa katika chama hicho tawala.

Lakini pia kuna tamko la Humprey Polepole, ‘katibu Mwenezi’ wa CCM kuhusu uamuzi huo wa Nyalandu. Binafsi nilitarajia tamko kali na pengine lililosheheni kebehi kama sio kashfa (na Polepole ni hodari sana kwenye maeneo hayo), lakini reaction ya msemaji huyo wa CCM imekuwa ‘muted.’ Sana sana ameishia kudai kuwa Nyalandu amejiondoa kwa sababu ameshindwa kuendana na kasi ya awamu ya tano. Pia amejaribu kuonyesha kuwa mwanasiasa huyo sio ‘mtu mkubwa’ ndani ya chama hicho tawala. Huyu si Polepole tunayemfahamu kwa umahiri wake wa ‘kusema ovyo.’ Huenda ‘upole’ wake una sababu flani.

Japo kauli ya Kigwangallah na ya Rais Magufuli, sambamba na ‘vijana wa Lumumba’ kumwandama Nyalandu, na ‘upole’ wa Polepole yanaweza kuwa mambo ya kawaida tu, lakini pia yanaweza kutoa mwangaza kuhusu uamuzi huo wa Nyalandu. Hata hivyo, kama nilivyotanabaisha awali, sidhani kama mazingira hayo yangetosha kumfanya Nyalandu kuchukua uamuzi huo mzito.

Kwamba Nyalandu ataandamwa baada ya kuchukua uamuzi huo, hilo halina mjadala. Kama asipoandamwa na ngazi za juu za CCM au kupitia taasisi za dola/umma basi ‘vijana wa Lumumba’ watakesha mitandaoni kumchafua. Pamoja na ukongwe wake katika siasa si Tanzania tu bali barani Afrika kwa ujumla, kwa kiasi kikubwa CCM inaendekeza mno siasa za kisasi, kinyongo na adui mkubwa wa ukweli. Kuikosoa CCM au serikali yake ni kama kusaini ruhusa ya kusumbuliwa kwa kila namna.



Na ni muhimu kutambua kuwa Nyalandu alikuwa akifahamu kuhusu ‘mabalaa’ yanayomsubiri baada ya kuchukua uamuzi huo mzito. Angalia yanayomsibu Yusuph Manji, mtu aliyemwaga mamilioni ya fedha kuifadhili CCM lakini amebaki kuwa ‘kielelezo cha hasira za CCM.’

Je CCM wakiamua kulipa kisasi kwa Nyalandu watafanikiwa? Inategemea sana busara za Magufuli. Yote yanayoelezwa kuwa ‘ufisadi wa Nyalandu’ yailikuwa na baraka za mtangulizi wa Magufuli, yaani Rais Kikwete. Kwahiyo, kama ambavyo jitihada zozote za kumbana Lowassa zilivyoshindikana kwa vile zingeishia kumchafua pia Kikwete, ndivyo jaribio la ‘kulipiza kisasi kwa Nyalandu’ linavyoweza kumtia matatani JK.


Licha ya kuelezwa kuwa Nyalandu alikuwa mmoja wa watu wa karibu wa JK, pia ni muhimu kutambua kuwa mmoja wa watu wake wa karibu ni mke wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa, Mama Anna. Mara baada ya kurejea Tanzania kutoka Marekani, Nyalandu alikuwa miongoni mwa washauri Mama Anna Mkapa, katika uendeshaji wa taasisi ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF).

Kwa maana hiyo, jaribio lolote la ‘kumwandama Nyalandu’ linaweza kuzua kile Waingereza wanaita ‘unintended consequences,’ au ‘matokeo yasiyokusudiwa kwa Kiswahili.

Pia ni muhimu kutambua u-kimataifa wa Nyalandu. Mwanasiasa huyo ana mahusiano mazuri na wanasiasa wenye nguvu kubwa hususan nchini Marekani. Japo ‘nguvu’ zao zinaweza kutofua dafu kwa Magufuli, lakini sote twafahamu kuwa ni vigumu kwa Tanzania yetu kuwa na ‘jeuri’ katika umasikini wetu.


Hatma ya Nyalandu akifanikiwa kuhamia Chadema ikoje? Binafsi, ninahisi mambo makuu mawili. Kwanza, ujio wake katika chama hicho kikuu cha upinzani unaweza kuamsha msisimko mpya wa siasa za ndani na nje ya chama hicho, na Tanzania kwa ujumla.

Kwa upande mmoja, anaweza kuendeleza hoja zake kama hiyo ya kudai kurejeshwa kwa mchakato wa Katiba mpya, suala ambalo Chadema na washirika wake wa UKAWA ni kama wamelitelekeza.

Lakini pengine kubwa zaidi ni uwezekano mkubwa wa Nyalandu kuwa mmoja wa wagombea wa Urais kwa tiketi ya Chadema katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020. Kwamba amejiondoa CCM kwa hiari yake (angalau kwa mujibu tunachofahamu hadi muda huu) na kujiunga na Chadema kwa hiari yake, anaweza kuwa na faida ya ziada kuliko majina mengine mawili yanayotajwa kuhusu urais mwaka 2020 kupitia Chadema, Mawaziri Wakuu wa zamani, Lowassa na Sumaye.


Kwamba Nyalandu ni ‘mwana-CCM pekee aliyemjali Lissu kwa kumtembelea huko Nairobi,’ na ukweli kuwa yeye na Lissu wanatoka mkoa mmoja, wanaweza kujenga ‘dream team’ inayoweza kuirejesha Chadema enzi za kina Dkt Slaa, Zitto na Mbowe.

Lakini pia katika mazingira yaliyopo sasa, Chadema imekuwa kama haina mpango wa kushiriki uchaguzi mkuu ujao. Maandalizi yanayopaswa kufanyika sasa – miezi 36 tu kabla ya uchaguzi huo – ni kama hayapo. Ndiyo, Magufuli kapiga marufuku shughuli za kisiasa, lakini ni lini Rais kutoka CCM aliwahi kuridhika shughuli za wapinzani?

Kwa maana hiyo, ujio wa Nyalandu unaweza kuamsha matumaini kwa chama hicho kikuu cha upinzani kuhusu nafasi yake katika uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo, kuna vikwazo vikuu viwili. Cha kwanza, ni lile lililojiri baada ya Lowassa kujiunga na CCM, Kwa minajili ya kumbukumbu tu, Chadema ilimwandama Lowassa kuwa ni ‘baba wa ufisadi’ kwa takriban miaka 9 mfululizo, kisha ghafla wakampokea na kumfanya mgombea wao wa Urais katika uchaguzi mkuu uliopita. Kwa busara za kawaida tu, huwezi kumchafua mtu kwa muda wote huo kisha ukategemea kumsafisha ndani ya miezi mitatu. Japo makada wa chama hicho hawataafiki, athari za kumpokea Lowassa na kumfanya mgombea wao zinaendelea kukisumbua chama hicho.

Kama ilivyokuwa kwa Lowassa, baadhi ya viongozi wa Chadema walishawahi ‘kumpaka’ Nyalandu wakimwita fisadi, hali inayoweza kutumiwa na CCM kudai kuwa ‘Chadema ni kimbilio la mafisadi.’ Hata hivyo ni rahisi kwa chama hicho cha upinzani kuwauliza CCM, “mpaka mwanasiasa awakimbie na kujiunga nasi ndio mnaanza kumwita fisadi?” Ni hoja inayoingilia akilini.


Je Nyalandu atapata mapokezi mazuri huko Chadema? Kama kauli ya Lowassa jana kuwa Chadema itakuwa ‘imelamba dume’ pindi Nyalandu akijiunga na chama hicho inaashiria chochote basi kuna uwezekano mkubwa wa mafanikio makubwa kwa mwanasiasa huyo.

Hata hivyo, ukweli kwamba Nyalandu ni miongoni mwa watu wenye sifa na uwezo wa kuwa wagombea urais kwa tiketi ya Chadema mwaka 2020 unaweza kupelekea mgongano dhidi yake na majina mengine yanayotarajiwa kuwemo kwenye kinyang’anyiro hicho, yaani Lowassa, Sumaye na Lissu.

Hili sio tatizo kubwa sana iwapo maslahi ya Chadema – badala ya maslahi ya mtu au kikundi binafsi – yakiwekwa mbele. Kwamba kufanyike tathmini ya kutosha kufahamu nani anayeweza kukiwezesha chama hicho kuing’oa CCM madarakani hapo mwaka 2020.

Kwamba Nyalandu anaweza kuleta hamasa kwa wana-CCM wengine (Membe?) kujiunga na Chadema, na kama ujio wake huko Chadema utaleta matokeo chanya, ni suala la muda. Lililo bayana hadi muda huu, uamuzi wake huo wa ghafla umetushtua wengi ikiwa ni pamoja na CCM na makada wake. Na yayumkinika kuamini kuwa uamuzi huo utaleta msisimko mpya katika siasa za Tanzania.

Mwisho, uchambuzi huu umetokana na uelewa wangu wa siasa za Tanzania, na unaweza kuwa sio sahihi kulingana na mitazamo tofauti. Jiskie huru kuchangia maoni, kunikosoa au hata pongezi zinaruhusiwa. Siku zote ninajitahidi kwenda mbali zaidi ya kuripoti tu matukio badala ya kuyachambua kwa undani zaidi. Asanteni na siku njema



Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.