Showing posts with label HATMA YA NCHI YETU. Show all posts
Showing posts with label HATMA YA NCHI YETU. Show all posts

15 Apr 2010

Nimekuletea habari sita zilizopelekea nijiulize swali hilo hapo juu:TUNAELEKEA WAPI kama Taifa?Tutafakari pamoja...

Mwananchi: Polisi waibiana Sh3 bilioni za posho

Salim Said
SIRI ya kuchelewa kwa posho za askari polisi mwezi Febuari mwaka huu imefichuka baada ya kudaiwa kuwa maafisa watatu wa jeshi hilo walitoweka na hundi ya malipo hayo yanayofikia Sh3 bilioni.

Baadhi ya maofisa wa polisi waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti wiki hii, walielezea mazingira ya wizi huo na kusisitiza kuwa ngazi ya juu ya jeshi hilo imekuwa ikificha taarifa hizo, kwa hofu ya kuchafua sifa ya chombo hicho cha dola.

Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, walisema fedha hizo ziliibwa na maofisa hao watatu baada ya kubadili maelezo kwenye hati ya malipo na kuielekeza katika akaunti za mmoja wao.
MwananchiTanesco yapoteza umeme wa Sh 100 bilioni kwa mwaka



Sadick Mtulya
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (Cag), Ludovick Utouh amesema kuwa upo uwezekano wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kufilisika baada ya kubaini kuwa kila mwaka linakabiliwa na upotevu wa Sh 100 bilioni.
Alisema fedha hizo zinapotea wakati wa kusambaza nishati hiyo kutoka kwenye vyanzo vyake hadi kwa watumiaji.
Utouh alieleza kwenye ripoti yake, ambayo gazeti hili lina nakala yake amebaini shirika hilo limepata hasara ya Sh Sh48 bilioni mwaka uliopita kutokana na ununuzi wa umeme kutoka katika kampuni binafsi, ikiwemo IPTL kufuatia mgawo mkubwa uliojitokeza Septemba na Oktoba, mwaka jana.

Ripoti hiyo ya Cag iliyowasilishwa Aprili 6, mwaka huu katika kikao baina ya watendaji wakuu wa Tanesco na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Masharika ya Umma (Poac) kilichofanyika katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam.

Kutokana na hali hiyo, Poac iliiagiza Tanesco kuhakikisha inafanya jitihada za kujinasua katika hali hiyo.



Tanzania Daima: Mitambo jengo jipya la Bunge yakwama


na Kulwa Karedia, Dodoma

SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, jana alilazimika kuahirisha kikao cha Bunge kwa muda wa dakika 45 kutokana na hitilafu ya mitambo ya mawasiliano ndani ya jengo hilo jipya la Bunge.
Spika Sitta alifikia hatua hiyo baada ya kuingia ukumbini, majira ya saa 2.59 na kuanza kusoma dua kama kawaida, ingawa alilazimika kukatisha tena baada ya kipaza sauti chake kutofanya kazi.

Jambo hilo lilisababisha Spika kuendesha dua kwa sauti ya chini huku baadhi ya wabunge wakipigwa na butwaa.

Habarileo: Wagombea watarajiwa wadaiwa kuhonga majeneza 

WATU kadhaa waliotangaza au kuonesha nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ukiwemo ubunge wanadaiwa kutoa rushwa yakiwemo majeneza.

Kisheria kipenga cha kuanza kampeni za kuwania urais, ubunge na udiwani hakijapulizwa na hata kampeni za ndani ya vyama hazijaruhusiwa.

Kampeni hizo haramu zimekuwa zikifanyika hadharani katika mikusanyiko ya watu inayohusu mambo ya kijamii zaidi kuliko siasa na mbaya zaidi imebainika kuwa wagombea hao wamekuwa wakivizia misiba, wakati jamii ikiomboleza kuondokewa na ndugu au jamaa, wao wanafikiria kura za waombolezaji.

Kutokana na hali hiyo ambayo imeonekana kwa wanaotangaza nia za kugombea ubunge kupitia vyama mbalimbali, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imebainisha mwishoni mwa wiki kwamba inafahamu kuwepo kwa vitendo hivyo na imeanza kuwafuatilia wanasiasa hao.

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma wa Takukuru, Mary Mosha alibainisha hayo alipokuwa anatoa mada kwenye semina ya kujadili mbinu sahihi za kuripoti habari za uchaguzi mkuu, inayowashirikisha waandishi waandamizi na wahariri wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo na HabariLeo Jumapili.

Raia Mwema: Utata mpya waibuka 'EPA namba mbili'

Mwandishi Wetu
Aprili 14, 2010
Ni fedha za stimulus package alizozitetea Kikwete bungeni
Gavana BoT aruka kiunzi, amtupia mpira msaidizi wake




SAKATA la matumizi yenye kutia shaka ya fungu la fedha lililopitishwa na Bunge kwa ajili ya kuhami uchumi, maarufu kama stimulus package , sasa limemrudia Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Beno Ndulu, ambaye baada ya baadhi ya kampuni za ununuzi wa pamba kukosa mgawo huo katika mazingira yanayozua maswali zilimtaarifu naye akawajibu kuwa Serikali haina fedha.

Hata hivyo, wakati Gavana akitoa majibu hayo kuwa “Serikali haina fedha” si fedha zote Sh. trilioni 1.7 zilizoidhinishwa na Bunge la Tanzania ndizo zilizotumika katika mpango huo wa kunusuru uchumi uliotikiswa baada ya uchumi wa dunia kuyumba.

Wiki hii Gavana Ndulu amekwepa kuzungumzia suala hilo, akidai kwamba kwa sasa linashughulikiwa na mtu maalumu chini yake anayepaswa kutafutwa kuzungumzia suala hilo.

Raia Mwema ilipozungumza na Profesa Ndulu, ambaye alieleza kuwa yuko mkoani Mwanza kwa ajili ya mkutano, alisema masuala ya ‘‘stimulus package’’ yamekabidhiwa mtu maalumu ndani ya benki hiyo, na kwamba si yeye anayeweza kuyazumngumzia.

“Haya masuala ya stimulus package tumempa mtu maalumu ambaye ni mkuu wa kitengo cha sera na utafiti, mimi siwezi kuyazungumzia,” alijibu Ndulu hata alipotakiwa kujibu yale yanayomhusu moja kwa moja katika sakata hilo pia hakuwa tayari kuzungumzia.

Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kuwa fedha zilizokwishakutumika ni sehemu tu ya Sh trilioni 1.7 zilizopitishwa na Bunge, ambazo ni takriban Sh bilioni 870.8. Fedha hizo Sh bilioni 870.8 kwa mujibu wa taarifa zilizopo ndizo zilizokwishakutolewa na Benki Kuu (BoT), chombo ambacho kimepewa mamlaka ya kutoa fedha hizo.

Kwa mujibu wa utaratibu wa BoT, fedha hizo hutolewa kutoka benki hiyo kwenda katika benki ambazo zilikopesha kampuni zinazostahili kufidiwa, ambazo zimeathiriwa na mtikisiko wa uchumi duniani.
Nipashe: Sungusungu wawavua nguo walimu na kuwachapa viboko



NA ANCETH NYAHORE



14th April 2010

Walimu watatu wa kike na mke mmoja wa mwalimu wa kijiji cha Sakasaka, tarafa ya Kisesa wilayani Meatu, wamevuliwa nguo na kucharazwa viboko na walinzi wa jadi sungusungu wa kijiji hicho kwa madai ya kutohudhuria mkutano uliokuwa umeitishwa na jeshi hilo.

Imedaiwa kuwa walimu hao walishindwa kwenda kwenye mkutano huo kwa sababu ni wajawazito jambo ambalo sungusungu hao walipinga na kuwalazimisha wavue nguo kuthibitisha kama kweli ni wajawazito mbele ya mkutano huo.

Tukio hilo la aina yake na udhalilishaji kijinsia, lilitokea AprilI 7, mwaka huu kati ya saa na 4:00 na 5:00 asubuhi kijijini hapo.Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) wa wilaya ya Meatu, Baraka Owawa, aliiambia Nipashe kuwa walimu hao walikamatwa na sungusungu hao na kuanza kuwapiga, kuwavua nguo kwa madai ya kutohudhuria mkutano.Owawa alisema walimu hao hawakuwa na jinsi yoyote ya kukabiliana na sungusungu hao bali walitii amri hiyo ya askari hao wa jadi kunusuru maisha yao.

Mara baada ya walimu hao kufanyiwa unyama huo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Julius Mtuli, alitoa taarifa kwa uongozi wa juu wilayani hapa ikiwemo polisi na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Meatu na timu maalum kuundwa kwenda kijijini hapo kufuatilia suala hilo.

16 Nov 2009


BUSARA ZINAELEKEA KUSHINDWA KUFANYA KAZI KATIKA TANZANIA YA SASA.BUSARA ZIMEKUWA ZIKITUFUNDISHA KUWA UTU UZIMA DAWA LAKINI TUKIANGALIA JINSI MAMBO YALIVYO SHAGHALA BAGHALA LICHA YA KUWEPO KWA WAZEE-KAMA KINGUNGE NGOMBALE MWIRU-WENYE NGUVU KATIKA ULINGO WA SIASA NI DHAHIRI UTU UZIMA UMESHINDWA KUJIDHIHIRISHA KUWA NI AMANA KATIKA UONGOZI.

PIA KUNA SUALA LA ELIMU.WENGI TUNAAMINI KUWA DALILI ZA KUELIMIKA NI PAMOJA NA KUFANYA YANAYOTARAJIWA NA JAMAA,NA PENGINE KWA NIABA YA JAMII HUSIKA.YAYUMKINIKA KUSEMA KWAMBA KATIKA TANGU NCHI YETU IPATE UHURU HAIJAWAHI KUSHUHUDIA WINGI WA WASOMI KATIKA NYADHIFA MBALIMBALI ZA KISIASA NA KITAALAMU.UNGETARAJI WINGI HUO WA WASOMI UNGEIWEZESHA TANZANIA KUWA KATIKA MAHALA INAPOSTAHILI (YAANI TANZANIA YENYE MAISHA BORA YANAYOENDANA NA UTAJIRI WA RASLIMALI ULIOPO).LAKINI LICHA YA UTITIRI HUO WA WASOMI TUMEZIDI KUSHUHUDIA NCHI IKIGEUZWA SHAMBA LA BIBI HUKU UTAJIRI WETU UKITAFUNWA KANA KWAMBA KUNA MASHINDANO YA KUUMALIZA.

KWA VILE HUKO NYUMA TULIELEZWA KWAMBA ILI TUENDELEE TUNAHITAJI WATU,ARDHI,SIASA SAFI NA UONGOZI BORA,NA KWA VILE ARDHI IPO BWERERE HADI TUNAALIKA WAWEKEZAJI,NA WATU TUPO ZAIDI YA MILIONI 40,BASI NI DHAHIRI KUSUASUA KWA MAENDELEO YETU NI MATOKEO YA SIASA MUFILISI NA VIONGOZI WASIOFAA.

NI KATIKA MINAJILI HIYO NAONA UMUHIMU WA KUHOJI BUSARA ZILIZOMO KATIKA HABARI IFUATAYO



Rais Kikwete Aota kujenga safu ya vijana katika uongozi wa kitaifa
Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete ameahidi kuwa kama akijaliwa kupata kipindi cha pili cha kuliongoza taifa la Tanzania, atafanya jitihada kubwa kuubadilisha uongozi wa Tanzania kuwa uongozi wa vijana.

Rais Kikwete akizungumza juzi, mjini Dar es Salaam na vijana kutoka nchi mbali mbali za Afrika wanaoshiriki katika Mpango wa Kulea Uongozi wa Afrika wa African Leadership Initiative, Rais Kikwete alisema kuwa anauthamini Mpango huo.

Alisema kuwa vijana ndiyo Tanzania ya kesho, na kama Tanzania haikuwekeza vya kutosha katika vijana na maendeleo yao, basi itakuwa haiwekezi katika hali yake ya baadaye.

Aliwaambia vijana hao ambao wanashiriki katika Mpango huo unaodhaminiwa na Askofu Mkuu (mstaafu) wa Kanisa la Anglikan Desmond Tutu wa Afrika Kusini kuwa kwa kadri miaka inavyokwenda ni lazima rika la wazee lipishe lile la vijana....INAENDELEA

CHANZO: Mwananchi

JE WINGI WA VIJANA (NA NENO LENYEWE "KIJANA" NI TETE KATIKA ANGA ZA SIASA ZETU) UTAWEZA KUIFIKISHA TANZANIA INAPOSTAHILI KUWA?JE KIKWAZO CHA MAENDELEO YETU NI WINGI WA WAZEE,UPUNGUFU WA VIJANA AU UKOSEFU WA UZALENDO MIONGONI MWA TULIWAOWAPA DHAMANA YA KUTUONGOZA?

TWENDE MBALI ZAIDI.JE KIJANA KWA MUJIBU WA SIASA ZETU NI MTU WA AINA GANI?MWENYE CHINI YA MIAKA 30,40 AU 50?JE KUNA UHUSIANO WOWOTE KATI YA UJANA NA UONGOZI BORA?JE VIJANA TUOTAKA WASHIKE MADARAKA WATAWEZA KWELI KUTONGOZA WAKATI VIBABU VINATAKA KUFIA MADARAKANI NA HIVYO KUWANYIMA FURSA VIJANA YA KUPATA UZOEFU WA UONGOZI?

NA KWA VILE SIASA ZETU ZIMETAWALIWA NA FEDHA,JE VIJANA TUONATAKA WASHIKE MADARAKA HAWATAKUWA WAMEFADHILIWA NA MAFISADI ILI KUWATUMIKIA?NA VIJANA TUNAOWAZUNGUMZIA NI VIJANA WOTE AU WATOTO WA VIGOGO?

LILILO WAZI,KWA KUZINGATIA UZOEFU WA SIASA ZETU,SI KIGEZO CHA UJANA AU HAIBA KINACHOWEZA KUTUKWAMUA HAPA TULIPO BALI NI DOZI NZITO YA UZALENDO.NA JAPO SIWEZI KUJIPAMBANUA KAMA MCHAMBUZI NILIYOBOBEA KWENYE SIASA,SIJAWAHI KUONA MAHALA PANAPOTHIBITISHA KUWA UJANA NI SAWA NA UZALENDO.

LABDA NI MUHIMU PIA KUFAHAMU KUWA HATUWEZI KUENDELEA KWA KUTOA MAJIBU MEPESI TUNAPOKABILIWA NA MASWALI MAGUMU.NI MUHIMU PIA KUKUMBUKA KWAMBA WENZETU WALIOENDELEA WANAFANYA KILA JITIHADA ZA KUPAMBANA NA UBAGUZI KWA VIGEZO VYA UMRI,JINSIA,RANGI,ASILI AU NAFASI YA MTU KATIKA JAMII.KWA MANTIKI HIYO,TUNAPOTAMANI VIJANA WARITHI WAZEE,HUKU TUKIWA HATUNA UTHIBITISHO KUWA UJANA NI TIBA YA MATATIZO YETU,TUNAWEZA KUKARIBISHA MANUNG'UNIKO KUTOKA KWA MAKUNDI MENGINE KATIKA JAMII HUKU TUKIENDELEA KUPIGA MARK TIME WAKATI TAIFA LETU LINAZIDI KUTAFUNWA KAMA MCHWA NA MAFISADI.

26 Apr 2009


KUNA kila dalili kuwa taifa halielekei pazuri hasa baada ya siku za hivi karibuni kuibuka matukio kadhaa ambayo kwa kiasi kikubwa yameishtua jamii kiasi cha kuhoji taifa linakoelekea.

Matukio ya kiongozi wa nchi kudhalilishwa kwenye mtandao wa kompyuta, malumbano ya wabunge juu ya kuvuja kwa siri za serikali na kuanikwa kwa mishahara yao pamoja na hatua ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, kutaja majina ya watu anaowatuhumu kuwa mafisadi ‘papa’ hadharani.

Kutokea kwa matukio hayo katika kipindi hiki ambacho taifa linaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwakani kumeelezwa ni mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yanaweza kuliyumbisha taifa.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii wanayaona matukio hayo kama ni mapambano ya hatari yanayowahusisha baadhi ya wafanyabiashara na vigogo wa siasa ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kuhakikisha wanafanikisha mikakati ya kuongoza.

Tukio la Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, kuwataja baadhi ya wafanyabiashara na wanasiasa maarufu hapa nchini kuhusika na kashfa za ufisadi limezua mtafaruku miongoni mwa jamii ambapo baadhi ya watu wanaiona hatua hiyo ni mapambano ya hadharani baina ya pande hizo mbili.

Mapambano hayo ambayo katika siku za hivi karibuni yamefikia hatua mbaya kiasi cha kuanza kuhusisha uandishi wa habari usiozingatia maadili ya fani ya habari umeonekana kutumika kwa ajili ya kukashfu na kudhalilisha utu wa baadhi ya walengwa.

Vita ya pande hizo mbili vinaonekana kuanza kushika kasi na kuna habari kuwa baadhi ya wafanyabiashara waliotajwa na Mengi wamejipanga kujibu mashambulizi hayo kwa gharama zozote zile.

Wakati mapambano hayo yakionekana ni ya pande mbili wanasiasa, wafanyabiashara na wananchi mbalimbali wamejikuta ama wanaunga mkono upande mmoja au mwingine hali inayozidisha utete wa vita hivyo.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii wamebainisha kuwa hali hii ya sasa imekuja hasa baada ya ufisadi wa EPA, Meremeta, Richmond na kadhalika ambao ulisababisha baadhi ya viongozi akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowasa kujiuzulu.

Kujiuzulu kwa viongozi hao na kufikishwa mahakamani kwa baadhi ya watuhumiwa walioshiriki katika kashfa hizo na za matumizi mabaya ya madaraka kumechochea vita dhidi ya ufisadi huku baadhi ya wananchi wakitaka pia Rais wa mstaafu, Benjamini Mkapa, naye aondolewe kinga ili aweze kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Hatua ya Mengi kujitokeza hadharani na kutaka majina ya watu anaowatuhumu kwa kashfa za ufisadi na baadhi ya wabunge kuwachachamalia watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi nako kumezidisha joto na hofu ya mapambano hayo.

Wakati mawazo ya watu yakiwa bado katika mzozo huo, limetokea tukio jingine la kusikitisha katika mtandao ambapo kiongozi wa nchi amejikuta akidhalilishwa kwa picha zisizofaa mbele ya jamii.

Tukio hilo kwa kiasi kikubwa linaonyesha ukosefu wa ustaarabu na maadili kwa baadhi ya watu ambao wameamua kutumia vibaya teknolojia ya kisasa hususan upashanaji habari kwa kutumia mtandao.

Jambo hilo kwa kiasi kikubwa limekuwa likihusishwa na mbinu za kuchafuliana majina hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi na kubainishwa kuwa kama hatua za haraka za kuwakamata wanaohusika na mitandao hiyo zisipochukuliwa kuna hatari ya viongozi wengi zaidi kudhalilishwa kupitia mambo mbalimbali.

Moja kati ya tukio la udhalilishaji wa viongozi ni hatua ya kijana mmoja kuamua kumpiga kofi Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, katika sherehe za Maulid zilizofanyika kwenye Ukumbi wa Daimond Jubilee, Dar es salaam.

Sakata jingine ambalo limeonekana kuwagawa zaidi Watanzania na wanasiasa ni kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, kuwa kuanzia sasa wabunge na watendaji wote watakaovujisha siri za serikali watashughulikiwa ipasavyo.

Kauli hiyo ambayo ilionekana kumlenga Mbunge wa Karatu Dk. Wilbrod Slaa (CHADEMA) na baadhi ya wabunge ambao wamekuwa wakitumia nyaraka mbalimbali zinazodaiwa kuwa za siri kuiumbua serikali sasa watakumbana na mikono ya sheria endapo watakutwa na nyaraka hizo.

Kauli hiyo imeonekana kupingwa na wananchi wengi kwa madai kuwa sasa serikali inataka kuwa ya kidikteta hasa kwa kuficha nyaraka za ufisadi uliofanywa au unaofanywa na viongozi waliopo na waliomaliza muda wao madarakani.

Baadhi ya wananchi wamekuwa wakiihusisha kauli hiyo kama ni njama za kuficha uovu ambao umekuwa ukipoteza fedha nyingi za Watanzania kupitia rasilimali mbalimbali.

Mshangao huo wa wananchi uliongezeka zaidi pale baadhi ya wabunge walimshutumu hadharani Dk. Slaa kwa kubainisha vipato wanavyovipata wabunge na kutaka fedha hizo zipunguzwe ili zitumike kwa maendeleo ya wananchi.

Baadhi ya wabunge walimtuhumu Dk. Slaa kwa kutaka kujitafutia umaarufu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu ujao jambo ambalo limepingwa vikali na wananchi wanaoonekana kukubaliana na ushauri wa Dk. Slaa.

Matukio haya kwa kiasi kikubwa kwa namna moja au nyingine yanaonyesha kuliweka taifa katika sehemu mbaya na iwapo kama hatua za kurekebisha baadhi ya mambo hazitachukuliwa kuna kila dalili za kutokea mpasuko mkubwa miongoni mwa jamii.

Naye Rahel Chizoza anaripoti kutoka Dodoma kuwa sakata la wizi wa nyaraka za serikali na kuwekwa hadharani kwa mishahara minono na marupurupu wanayopata wabunge kulikoibuliwa na Mbunge wa Karatu Dk. Wilbrod Slaa (CHADEMA), hivi karibuni limechukua sura mpya baada ya baadhi ya wabunge kuonyesha kumchukia mbunge huyo.

Hali hiyo imejitokeza jana kwenye semina ya maboresho ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma iliyoendeshwa kwa wabunge ambao baadhi yao walionyesha hali ya kumbeza mbunge huyo aliposimama kwa ajili ya kuchangia hoja.

Hali hiyo ilisababisha mwenyekiti wa semina hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje, kuingilia kati na kuwasihi wabunge kupunguza minong’ono.

“Hivi hizi nyaraka zinazodaiwa kuwa ni za siri, kwa nini zinawekwa kwenye makabati ya serikali, naomba Katibu Mkuu aniambie kama ni halali kwa nyaraka za wizi kuwepo katika kabati za serikali,” alihoji Dk. Slaa

CHANZO:Tanzania Daima

6 Apr 2009

MIMI SI MWANASIASA JAPO MALENGO YANGU YA BAADAYE NI KUWA MCHAMBUZI WA SIASA (POLITICAL ANALYST).BINAFSI SIICHUKII CCM ILA NAKERWA NA BAADHI YA KASUMBA ZILIZOOTA MIZIZI NDANI YA CHAMA HICHO KIKONGWE.NA KASUMBA KUU INAYONITATIZA KUHUSIANA NA CHAMA HICHO NI UNAFIKI.

JUZI JUZI TUMESIKIA KAULI ZA MMOJA WA WAKONGWE WA CCM,MZEE JOHN MALECELA,AMBAPO PAMOJA NA MAMBO MENGINE ALIAMUA "KUSIGINA DEMOKRASIA" KWA KUWATAKA BAADHI YA VIONGOZI WA CHAMA HICHO WANAOLUMBANA WAKOME MARA MOJA.>
SWALI LA MSINGI HAPA NI JE KWA KUKOMESHA MALUMBANO HAYO NDIO UFUMBUZI WA "KINACHOLUMBANIWA" UTAKUWA UMEPATIKANA?BUSARA NDOGO TU INAWEZA KUTUELEZA KWAMBA MTOTO ANAPOLIA INAWEZA KUASHIRIA KUWA ANA TATIZO (NJAA,KIU,ANAUMWA,NK).KUMFINYA MTOTO HUYO ANYAMAZE BADALA YA KUCHUNGUZA KINACHOMLIZA HAIWEZI KUWA SOLUTION YA TATIZO.

HUHITAJI KUWA MCHAMBUZI WA SIASA KUBAINI KUWA MALUMBANO YANAOENDELEA NDANI YA CCM NI MKINZANO WA WATETEZI WA UFISADI vs WAPINZANI WA UFISADI,WABINAFSI vs WANAOJUA JUKUMU LAO KWA TANZANIA,WANAFIKI vs WASEMA KWELI,NA MAKUNDI KAMA HAYO.KITU PEKEE KINACHOWEZA KUYAPATANISHA MAKUNDI HAYO NI KWA CCM KUWA WAZI-SI KWA MANENO PEKEE BALI KWA VITENDO-INASIMAMIA UPANDE UPI KATIKA MIKINZANO HIYO.IWAPO CCM IKISEMA INAPINGANA NA UFISADI HALAFU IKACHUKUA HATUA ZINAZOSTAHILI DHIDI YA BAADHI YA VIONGOZI WAKE WANAOTUHUMIWA KWA UFISADINI DHAHIRI BASI MALUMBANO YANAYOENDELEA YATAKOMA.LAKINI TUSITEGEMEE "UKIMYA" KWA HALI ILIVYO SASA AMBAPO,KWA MFANO, MTU KAMA MZEE WA VIJISENTI PAMOJA NA TUHUMA ALIZONAZO ANAENDELEA KUWA MJUMBE WA KAMATI YA MAADILI NDANI YA CHAMA HICHO.

KAULI YA MZEE MALECELA IMEANZA KUPATA SAPOTI KUTOKA KONA MBALIMBALI NDANI YA CHAMA HICHO.JANA,WAKONGWE FLANI WA CCM WAMEITISHA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI AMBAPO PAMOJA NA MAMBO MENGINE WAMEKEMEA MALUMBANO HUKU WAKIONEKANA KUKEMEA BAADHI YA VIONGOZI WA CCM WALIOSHIKILIA BANGO VITA DHIDI YA UFISADI.KWA BUSARA ZA WAZEE HAWA,WANATAKA SUALA HILO LIACHWE MIKONONI MWA CCM.HIVI LAITI CCM INGEKUWA IMEMUDU KUFANYA HIVYO,AKINA MWAKYEMBE,KILANGO NA SELELII (KWA MFANO) WANGEKUWA WANAPIGA KELELE KUHUSU UFISADI?

WANACHOJARIBU KUFANYA WAZEE HAWA (PAMOJA NA MALECELA) NI KUJIAMINISHA KUWA HAKUNA TATIZO NDANI YA CHAMA HICHO,NA KELELE ZINAZOPIGWA NA BAADHI YA VIONGOZI WAKE NI SAWA TU NA UTOVU WA NIDHAMU.YALEYALE YA KUMFINYA MTOTO ANYAMAZE PASIPO KUFANYA JITIHADA ZA KUJUA KINACHOMLIZA.

KUNA WENZETU AMBAO KWA MTIZAMO WAO UKIZUNGUMZIA MABAYA YA CCM BASI UMETENDA KOSA LA JINAI.TATIZO LA WATU WA AINA HII NI KUPUUZA NAFASI YA CCM KATIKA ULINZI WA AMANI NA HATMA YA TAIFA LETU KWA UJUMLA.DHAMANA YA NCHI IKO MIKONONI MWA CHAMA HICHO KWA VILE NDICHO KILICHO MADARAKANI KWA SASA.SOTE TUNAWEZA KUBASHIRI KILICHO MBELE YETU IWAPO TUKIIRUHUSU CCM IENDESHE MAMBO INAVYOTAKA-HATA KAMA INATUPELEKA PABAYA-NA SIE TUENDELEE KUKAA KIMYA!

ANYWAY,HEBU SOMA BUSARA ZA WAZEE WETU HAWA HAPO CHINI:

Wenyeviti wastaafu wa CCM waonya

Wenyeviti wastaafu wa mikoa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamevunja ukimya na kuwataka viongozi wa chama hicho wanaotaka kuyatumia mapambano dhidi ya rushwa kama mtaji wa kisiasa na kujipatia umaarufu, kuacha mara moja. Sambamba na hilo, wazee hao wametaka mapambano dhidi ya rushwa yasiwe kichaka cha kuficha ubovu wa uongozi na kushindwa kuwajibika. Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wastaafu wa chama hicho Dar es Salaam jana, Mwenyekiti mstaafu wa Mkoa wa Dodoma, Pancras Ndejembi alisema mapambano dhidi ya rushwa ni ya CCM na si mwanachama binafsi au kikundi cha wanachama wachache.

“Tunashuhudia baadhi ya viongozi wa CCM kurushiana maneno wenyewe kwa wenyewe kwa kutaka kuonyeshana nani zaidi na nani ni vinara kuliko wengine katika mapambano dhidi ya rushwa, hii si sawa,” alisema Ndejembi aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Tanzania. “Tusingependa kuona mapambano haya yanatumiwa kama njia ya kujipatia umaarufu binafsi, mwenyekiti wetu Rais Kikwete ambaye ndiye jemedari wa mapambano haya humsikii anafanya hivyo na sisi wengine tusifanye hivyo…. kama wewe ni kiongozi na hutekelezi wajibu wako kwa wapiga kura wako wakikuuliza uko wapi, usisingizie kupigwa vita na mafisadi,” walionya.

Ndejembi aliyeambatana na wenyeviti wastaafu Hemed Mkali (Dar es Salaam), Tasil Mgoda (Iringa) na Jumanne Mangara (Pwani), alisema wazee hao wamesikitishwa na malumbano ya hadharani baina ya viongozi wa CCM ambao wengine wa ngazi ya juu ya uongozi ndani ya chama. Alisema tabia inayoonyeshwa na viongozi hao ya kushutumiana, kunyoosheana vidole, kuwekeana visasi, kuonyeshana ubabe na kuwekeana nadhiri ya kupambana baina ya viongozi, kunadhoofisha na kukipunguzia heshima chama hicho.

“Lakini pia kufanya hivyo hadharani, kwa nia ya kutaka kuungwa mkono katika shutuma na visasi hivyo kunajenga chuki, uhasama na migawanyiko katika jamii, viongozi hatupaswi kuwajaza watu chuki na uhasama ndani ya mioyo yao,” alisema Ndejembi kwa niaba ya wenzake na kutaka neno ufisadi lisitumiwe kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwakani. Alisema kumuita mtu fisadi kwenye vyombo vya habari haitoshi katika kushinda mapambano dhidi ya rushwa, bali watu waipigie kelele serikali iimarishe taasisi na vyombo vya kupambana na rushwa kama Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mahakama ambako watuhumiwa wanafikishwa.

Licha ya kuwapo malumbano baina ya viongozi hao wa CCM, wastaafu hao walisema kuhitilafiana ni kitu cha kawaida na kamwe watu wasitarajie chama hicho kitameguka. Wastaafu hao walieleza kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete iwapo atagombea tena urais mwakani na kutaka watu wengine wamuunge mkono, kwa maelezo kuwa anafaa kuongoza nchi. Walitoa sababu za kumuunga mkono kuwa ni kukubalika na anaowaongoza, anawapenda watu wote, mvumilivu, mkereketwa wa maendeleo ya wananchi na hana jazba.

Wazee hao walisema wameamua kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo hayo ili ujumbe uwafikie viongozi, wanachama na mashabiki wa CCM, lakini yote hayo waliyoyaeleza wameshayawasilisha kwenye vikao wanavyoshiriki vya matawi na mashina na wamezungumza na viongozi wa sasa wa chamahicho. Ingawa wastaafu hao hawakuwataja kwa majina viongozi wa CCM waliolumbana hadharani, lakini hivi karibuni Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye ni mwanahisa wa Kampuni ya kuzalisha umeme wa upepo ya East Africa Power Pool, amelumbana na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Dk. Mwakyembe anadai Rostam anatumia vyombo vyake vya habari kumchafua huku Rostam akitaka mbunge huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mwandishi wa habari, kuelezea mgongano wa maslahi wakati alipochaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini. Mbali na wazee hao, pia Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM Tanzania Bara ambaye ni Mbunge wa Mtera, John Malecela alitaka malumbano hayo yakome, kwani hayana faida kwa mwananchi na wahusika watumie vyombo husika vya chama kufikisha malalamiko yao.
CHANZO:
HabariLeo

WITH ALL DUE RESPECT,BAADHI YA HAWA WAZEE NDIO WAMETUFIKISHA HAPA TULIPO KUTOKANA NA ITIKADI HIZIHIZI ZA "KUJENGA UMOJA NA MSHIKAMANO NDANI YA CHAMA" PASIPO KUANGALIA ATHARI ZAKE KWA JAMII KWA UJUMLA (AFTERALL,SIO KILA MTANZANIA NI MWANA-CCM).

HATUJACHELEWA.INAWEZEKANA IWAPO UZALENDO NA MASLAHI YA TAIFA YATAWEKWA MBELE YA (in front of) KUJIPENDEKEZA NA UNAFIKI.

20 Feb 2009




HAYA NDIO MAJIBU YA CCM.CHINI YA MAJIBU HAYO NI HABARI YENYE MATAMSHI YA DR KITINE.


CCM yamjibu Dk. Kitine

na Edward Kinabo

SIKU moja baada yaMkurugenzi mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa nchini, Dk. Hassy Kitine, kudai nchi inaendeshwa kienyeji na kukilalamikia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kuwakumbatia wanachama wake wanaokabiliwa na kesi za ufisadi, chama hicho
kimesema hakiwezi kuwavua nyadhifa hizo, kwa sababu kesi zao bado ni tuhuma tu.

Sambamba na hilo, CCM imesema kauli ya Dk. Kitine kwamba nchi inaendeshwa kienyeji ni maoni yake binafsi, kwani hayana ukweli. Msimamo huo wa CCM ulitolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati, alipozungumza na Tanzania Daima, akijibu shutuma nzito zilizotolewa juzi na Dk. Kitine dhidi ya serikali.

“Sisi tunasema, yeye kama raia ana haki ya kutoa mawazo yake, na hiyo ndiyo demokrasia. Lakini si lazima kila anayetoa mawazo yake yawe sahihi. Mtu anaweza kujiuzulu nafasi yake kupisha uchunguzi ufanyike, hiyo haimaanishi kwamba hilo jambo amelifanya kweli.

“Uchunguzi unapofanyika kuna mambo mawili yanaweza kutokea, la kwanza huyo mtu anaweza kubainika alifanya hicho kitu na la pili anaweza kuonekana hana hatia.

“Hatuwezi kuwavua watu uanachama au nyadhifa zao ndani ya chama kwa sababu hiyo tu. Yeye aliyesema hivyo atutajie ni kiongozi gani wa serikali ambaye pia ni kiongozi wa chama, ameshathibitika kuwa hana maadili halafu kama chama tumeendelea kumwacha. Atuambie…..hakuna,” alisema Chiligati.

Alipoulizwa kwanini CCM isiwafukuze uanachama na kuwavua nyadhifa zao za kichama na ubunge, baadhi ya viongozi wake, ambao tayari serikali ya chama hicho ilisharidhika kwamba walikiuka maadili ya uongozi kwa kutumia vibaya madaraka yao, hata ikaamua kuwafungulia kesi, alisema: “Hatuwezi kuwachukulia hatua kwa sababu kesi zao bado ni tuhuma tu. Wakithibitika kama kweli walifanya hivyo, hatutawaacha,” alisema Chiligati.

Chiligati alipinga madai ya nchi kuongozwa kienyeji na kusisitiza kuwa kauli ya Dk. Kitine, haina ukweli wowote.

Alisema nchi inaongozwa vizuri kwa kufuata utawala wa sheria na mihimili yote ya dola, ikiwemo utawala, Bunge na Mahakama, inafanya kazi zake vizuri. Alibainisha kuwa kielelezo kuwa nchi haiongozwi kienyeji, ni amani na utulivu vilivyopo nchini, kwani kama nchi ingekuwa inaongozwa kienyeji kusingekalika.

“Kwa mfano, hilo alilosema nchi inaongozwa kienyeji, maana yake nini? Nchi kuongozwa kienyeji maana yake hakuna mfumo wa utawala kabisa, hakuna utawala wa sheria. Mahakama hazipo wala Bunge halipo…serikali haipo.

“Kungekuwa na hali hiyo, ingekuwa sawa na kusema nchi inaongozwa kienyeji. Lakini sisi hatujafikia hatua hiyo. Bunge lipo, Mahakama ipo, Serikali ipo. Utawala wa sheria. Nchi haiongozwi kienyeji, ndiyo maana kuna amani na
utulivu,” alisema Chiligati.

Mbali ya CCM kutoa kauli hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliunga mkono kauli ya Dk. Kitine.

“Mzee Kitine ameongea jambo ambalo ninaliongea kila siku kwamba, kuna tatizo kubwa serikalini. Tuhuma za ufisadi zimeshamiri sana, watendaji hawachukui maamuzi, wanasiasa wenye nyadhifa serikalini wamejaza nafasi na hawako tayari kuwajibika. Tunahitaji muafaka wa kitaifa kwenye mambo mengi,” alisema Zitto. Alisema ili mambo yaende vizuri, Tanzania inahitaji kelele za wazee wastaafu kama Dk. Kitine, wasimamie kunena na kushauri na hata kukemea na wananchi wawapigie kura wabunge wengi wa upinzani ili Bunge liwe na meno.

Juzi, Dk. Kitine alisema taifa linakabiliwa na tatizo la uongozi, ambalo halijawahi kutokea katika historia ya nchi. Kada huyo wa siku nyingi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyewahi kuwa mbunge wa Makete, mkoani Iringa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, chini ya uongozi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alisema nchi imekuwa ikiendeshwa kienyeji, kwa sababu ya kuporomoka kwa maadili ya uongozi.

“Hali tuliyofikia si nzuri, tena niseme ni mbaya sana. Kuna kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa maadili ya uongozi. Na hii nawaambia, nchi haijawahi kuwa katika hali mbaya huko nyuma kama ilivyo sasa. Kwa hali tuliyofikia ni ngumu kurekebisha maadili ya uongozi."

“Tatizo kubwa ni viongozi kukosa integrity (uadilifu). Kwanza ni integrity ya viongozi wenyewe, pili ni commitment (wito), tatu ni nationalism (utaifa). Haya ndiyo yalikuwepo wakati wa Mwalimu,” alisema Dk. Kitine. Alisema baadhi viongozi wa serikali wamepoteza sifa kuu tatu za uongozi ambazo ni kuwa na uadilifu, wito na kuweka mbele
utaifa, sifa ambazo alisema ndizo zilikuwa nguzo ya uongozi wakati wa Serikali
ya Awamu ya Kwanza, chini ya Baba wa Taifa, hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Alisema uteuzi mbaya wa viongozi hususan uteuzi wa mawaziri, umechangia
kupatikana kwa viongozi wasio waadilifu, wengi wao wakijihusisha na vitendo vya rushwa

CHANZO: Tanzania Daima



IFUATAYO NI HABARI ILIYOBEBA MATAMSHI YA DR KITINE.

MKURUGENZI Mkuu mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk. Hassy Kitine, amesema taifa linakabiliwa na tatizo kubwa la uongozi, ambalo halijawahi kutokea katika historia ya nchi.

Kitine ambaye aliiongoza idara hiyo nyeti kwa karibu miaka 30 zama za Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili, alisema ukosefu huo wa uongozi umesababisha nchi iongozwe kienyeji.

Kachero huyo namba moja kwa miaka mingi, ambaye alilazimika kujiuzulu wadhifa wa uwaziri wa nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa, mwishoni mwa miaka ya 1990 kutokana na kuhusishwa na kashfa ya mkewe kufuja fedha za umma kiasi cha shilingi milioni 40, alirejea kutoa kilio chake cha miaka mingi cha kuporomoka kwa maadili ya uongozi nchini.

Kitine ambaye aliwahi pia kuwa Mbunge wa Makete kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitoa matamshi hayo mazito katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam jana, alipozungumza na waandishi wa vyombo kadhaa vya habari.

“Hali tuliyofikia si nzuri, tena niseme ni mbaya sana. Kuna kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa maadili ya uongozi.Na hii nawaambia, nchi haijawahi kuwa katika hali mbaya huko nyuma kama ilivyo sasa. Kwa hali tuliyofikia, ni vigumu kurekebisha maadili ya uongozi.

“Tatizo kubwa ni viongozi kukosa integrity (uadilifu). Kwanza ni integrity ya viongozi wenyewe, pili ni commitment (wito), tatu ni nationalism (utaifa). Haya ndiyo yalikuwepo wakati wa Mwalimu,” alisema Dk.Kitine.

Akizungumza kwa kujiamini kama ilivyo kawaida yake, Kitine alisema viongozi wengi wa serikali wamepoteza sifa kuu tatu za uongozi ambazo ni kuwa na uadilifu, wito na kuweka mbele utaifa, sifa ambazo alisema ndizo zilikuwa nguzo ya uongozi wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, chini ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“That was possible (hilo liliwezekana) chini ya Mwalimu. Kama alikuwa akifanya kosa, basi kosa hilo lilikuwa likitokea tu wakati akifanya jambo kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania. "

“Philosophy (falsafa) ya Mwalimu, ilikuwa kwanza Mungu, pili Tanzania, halafu yeye binafsi. Kila kiongozi anayetofautiana na Mwalimu tu hulifikisha taifa hili kubaya, if you differ with him, utaishia kubaya,” alisema Dk. Kitine akionyesha hali ya masikitiko.

Alisema uteuzi mbaya wa viongozi, hususan ule wa mawaziri, umechangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa viongozi wasio
waadilifu, wengi wao wakijihusisha na vitendo vya rushwa. “Haiwezekani viongozi wakateuliwa kwa misingi ya mitandao …sijui, kwa msingi wa politics of division (siasa za makundi) ndani ya chama. Haiwezekani nchi ikaendeshwa kienyeji. Integrity should be number one (uadilifu unapaswa kuwa kitu cha kwanza kuzingatiwa). "

“Mtu anajiuzulu, anafukuzwa uwaziri kwa sababu ya kashfa, kwa sababu ya kukosa maadili, halafu anabakia kuwa mbunge na mjumbe wa kamati kuu ya chama, nini hii? Hii haifai. Waziri akikosa uadilifu anatakiwa aondolewe mara moja nyadhifa nyingine zote alizobakiwa nazo. Nadhani hii itasaidia,” alisema Dk. Kitine pasipo kutaja jina la kiongozi yeyote.

Kitine ambaye wakati wote wa mazungumzo yake alisema alikuwa anataka kujadili masuala muhimu na si watu, alieleza namna asivyo na imani na hatua zinazochukuliwa na serikali katika kukabiliana na tatizo la rushwa kubwa. Kwa mujibu wa kachero, mwanasiasa na mwanazuoni huyo, hatua hizo ambazo zinahusisha baadhi ya watu wenye majina makubwa kufikishwa mahakamani, zimechukuliwa kwa ajili tu ya maandalizi ya uchaguzi ujao.

“Nilikuwa kiongozi wa kwanza kuzungumzia rushwa kubwa miaka 10 iliyopita. Nilisema ndiyo inayovuruga uchumi kuliko hata rushwa ya
nesi, hakimu, polisi,.… hakuna hata mkubwa mmoja aliyekamatwa. Ilinigharimu sana, na mimi nilipata adhabu ya kuzuiliwa kikao kwa miezi miwili, kama huyu nani huyu, Zitto (Kabwe). Wakati huo ilikuwa ndani ya CCM".

“Mimi nadhani hatua hizi zinazochukuliwa hazilengi kukomesha tatizo la rushwa, ni siasa tu za uchaguzi,” alisema Dk. Kitine.

Alipoulizwa nini kifanyike ili kukabiliana na tatizo hilo la uongozi mbaya, pamoja na mambo mengine, alielekeza changamoto zake kwa Idara ya Usalama wa Taifa.

“Usalama wa Taifa should be completely clean (unapaswa kuwa safi kabisa). Idara hii inatakiwa kuwa, juu ya mambo ya rushwa, iwe safi kabisa. Usalama wa Taifa ndiyo unayoteua viongozi, ndiyo inayoshirikiana na rais kwa kumshauri katika kuteua mawaziri. Sasa kama Usalama wa Taifa ukiwa mchafu ndio tunapata viongozi wala
rushwa. Nafikiri vigezo vinavyotumika kuteua viongozi pia vina matatizo,” alisema Dk. Kitine.

Kada huyo wa CCM ambaye kitaaluma ni mchumi na mwanasheria, akizungumzia hali ya uchumi nchini, alisema kwa kiasi kikubwa uchumi umeshikiliwa na wageni kuliko wazawa, na kuelezea kusikitishwa kwake juu ya kuwepo kwa pengo kubwa kati ya matajiri na maskini.

Akitoa mfano alisema, miongoni mwa mambo yanayoonyesha kuparaganyika kwa mambo ni kukithiri kwa idadi ya ombaomba mitaani. “Mwalimu asingeruhusu watu hawa waombeombe barabarani. Kazi za Watanzania ni udereva teksi, daladala, mabasi, kazi ya uboi ndani ya nyumba na kazi ya kufagia barabarani. Hizi ndizo kazi za Watanzania na hawa ndio wenye mali."

“Uchumi huu wa Watanzania si wa kwao. Watanzania ambao ni matajiri hawazidi hata watano. Hakuna sera bora za kusaidia kutumia
maliasili zetu ili zitupe fedha ya kujenga shule, madaraja, hospitali…..”
alisema Dk. Kitine. Akizungumzia utendaji wa kazi wa Bunge katika kusimamia utendaji wa serikali, Kitine alisema kazi inayofanywa na taasisi hiyo hivi sasa ni kubwa kuliko ilivyopata kuwa wakati wowote huko nyuma.

Hata hivyo katika kuusifia utendaji wa kazi wa Bunge, aliupongeza mchango mkubwa na muhimu wa wabunge wa upinzani katika kuiimarisha taasisi hiyo muhimu. “Ni Bunge zuri kuliko lilivyowahi kuwa huko nyuma. Linaonyesha kila dalili za uhuru. Upinzani unafanya kazi nzuri. Bunge liko wazi zaidi na wabunge wanatoa michango mingi yakinifu, yenye manufaa kwa taifa. Likiendelea hivi tutafika mahali pazuri,” alisema
.

CHANZO :Tanzania Daima



WELL SAID!

24 Oct 2008


Pamoja na umasikini,madudu ya kisiasa,ufisadi na mengineyo yanayochukiza kuhusu nchi yetu ya Tanzania,mimi (na pengine wewe mwenzangu) bado tunaipenda nchi yetu.Nina sababu lukuki za kuipenda (au hata kuichukia) Tanzania,lakini ya msingi zaidi ni ukweli kwamba mimi ni Mtanzania,Tanzania ni nchi yangu na kwa vyovyote itakavyokuwa huko mbeleni bado nitabaki kuwa Mtanzania.

Hata hivyo,haitoshi kuwa Mtanzania tu.Haitoshi kuipenda Tanzania pasipo kutafsiri mapenzi hayo kwa vitendo.Kwanini?Kwa sababu pasipo kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa bora,inakuwa mahala salama pa kuishi,na inadumu kama nchi,Utanzania na mapenzi yetu kwa nchi yetu yanaweza yasiwe na faida au kuna mahala tunaweza kufika tunapenda kitu kisichokuwepo.Au kibaya zaidi,tunaweza kufika mahala ambapo ukisema "naipenda Tanzania" unaonekana taahira kama hutoishia kupigwa mawe.

Weka pembeni umasikini,weka pembeni maradhi,ufisadi,na matatizo mengine ya kijamii,kiuchumi au kisiasa.Tatizo kubwa na la hatari zaidi kwa Tanzania ni UZALENDO.Ni tatizo kwa sababu uzalendo unapotea kwa kasi.Ni tatizo kwa sababu nchi iko ilipo sasa kutokana na wachache wasio na uzalendo kwa nchi yetu.Ni tatizo pia kwa vile imefika mahala ambapo baadhi ya wenzetu wameanza kutafsiri uzalendo ni sawa na uhaini.Hawa ni wale ambao kwa vile wana uhakika wa kuamka wakiwa salama,kupata matibabu ya daraja la kwanza,kupata mishahara na posho nono sambamba na usafiri wa bure,pamoja privileges nyingine.Wenzetu hawa wanasahau kwamba wana babu,bibi,baba,mama,kaka,dada,wadogo,ndugu,jamaa na marafiki mtaani ambao wanateseka kutokana na matendo ya wasio wazalendo (mafisadi,nk).

Kwa kulinda maslahi yao binafsi na ya wale waliowaweka kwenye ulaji,wenzetu hawa hawataki kusikia neno lolote linalowahusu watu wa kawaida.Kuzungumzia lolote kuhusu kundi hili la walio wengi inatafsiriwa kuwa ni utovu wa nidhamu,kwenda kinyume na taratibu na pengine uhaini.Wanachosahau ni kwamba Tanzania ikichafuka,hizo raha zinazowalewesha nazo zitapotea.Badala ya kuwanyanyasa wale wanaohangaika kuifanya nchi yetu iwe katika hali nzuri,wanapaswa kuwaenzi na kuwasapoti.

Tanzania ni yetu sote,sio ya kikundi kidogo cha watu wanaotaka kusikia yale wanayopenda wao tu japo nao wanaona kabisa madudu yanayofannywa na majambazi,mafisadi,wazembe,mafuska wa itikadi,nk.Hizi tabia za kupiga makofi ya shangwe hata chifu anaposahau kufunga zipu yake zitatupeleka pabaya.Amani ina tabia tatu kuu: inachukua muda kuipata/kuijenga,inachukua muda mfupi sana kuiharibu/kuipoteza,na inachukua muda mrefu zaidi kuirejesha pindi ikitoweka (na pengine ikishapotea hairejei tena).Tuna kila aina ya mifano inayotuzunguka:Somalia,DRC (Zaire),Sudan,nk.

Tusipofanya sasa tunachopaswa kufanya kuilinda Tanzania kwa nguvu zote na kuwasapoti wazalendo wote wanaotusaidia kufanya hivyo tutaishia kujilaumu huko mbeleni.Na hakuna sehemu mbaya ya tatizo kama inapofikia hatua ya kusema "laiti tunge..."

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.