Showing posts with label MANUMBA. Show all posts
Showing posts with label MANUMBA. Show all posts

19 Jan 2013


IMG-20130119-00371 a18f1
Yuko nje ya nchi kwa matibabu

*Waziri Mkuchika akataa kusema lolote
* Manumba aendelea kupumulia mashine

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Dk. Joseph Hosea, anaumwa na amepelekwa nje ya nchi kwa matitabu.


Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya TAKUKURU, Dk. Hosea, alianza kuugua tangu mwanzoni mwa Desemba mwaka jana na ilipofika Desemba 15 hali ilibadilika.



Hata hivyo, chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya TAKUKURU kilisema hadi sasa haijafahamika ugonjwa unaomsumbua.



“Ni kweli Mkurugenzi anaumwa na kuna taarifa yuko ya nje ya nchi kwa matibabu kati ya Ujerumani au Uingereza.



“Kwa mara ya mwisho nilimuona Mkurugenzi akiwa hayupo sawa kiafya na hata alipokuwa anakuja kazini alikuwa katika muonekano ambao ni wazi anaumwa. Lakini katika wiki hizi sijamuona hapa ofisini,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika kutoka ndani ya TAKUKURU.



MTANZANIA pia ilimtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) George Mkuchika kwa njia ya simu kupata taarifa za kina kuhusu tukio hili lakini alisema hana taarifa yoyote.



“Mhhhh katika hili la ugonjwa wa Dk. Hosea sina taarifa na kama ujuavyo nilikuwa katika msiba wa baba yake Naibu Waziri wa Mifugo, kule Kiteto. Tangu jana nilikuwa n rejea na nimefika Morogoro nimelala hapa na sasa nimeanza safari ya kuelekea Dar es Salaam.



“Kama kuna taarifa yoyote kuhusu hilo kwa sasa siwezi kusema lolote hadi nitakapofika ndugu yangu,” alisema Waziri Mkuchika.



Hata hivyo mmoja wa wafanyakazi wa taasisi hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema Dk. Hoseah yupo nje ya nchi kwa mapumziko ya likizo.



“Ni kweli ofisa uhusiano yupo likizo na pia mkubwa (Dk. Hoseah) naye yupo Marekani ameenda kwa ajili ya mapumziko ya likizo hakuna mtu anayeumwa,” alisema.



MTANZANIA ilimtafuta Msemaji wa TAKUKURU Dorine Kapwani ambaye muda wote simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa hata alipopigiwa kwa simu ya mezani.



Mbali na hatua hiyo hata alipotumiwa ujumbe mfupi kwa simu ya kiganjani ambao ulisomeka; “Dada habari, kuna taarifa Dk. Hosea anaumwa na amepelekwa nje ya nchi kwa matibabu je kuna ukweli gani” hakujibu chochote hadi tunakwenda mitamboni jana usiku.



DCI Manumba apumulia mashine



Naye Elizabeth Mjatta anaripoti kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba sasa anapumua kwa msaada wa mashine baada ya hali yake kuendelea kuwa mbaya tangu alipofikishwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.



DCI Manumba jana alitumia takribani siku nzima kuwa katika chumba cha uchunguzi kwa ajili ya vipimo zaidi, baada ya kutolewa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) kwa ajili ya uangalizi wa karibu wa madaktari na wauguzi.



MTANZANIA ilishuhudia DCI akitolewa katika chumba cha wagonjwa mahututi saa 11:25 akipelekwa katika chumba cha uchunguzi huku akiwa amezungukwa na madaktari na wauguzi huku baadhi yao wakiwa wameshikilia vifaa maalumu ambavyo vilikuwa vikimsaidia kupumua. 



Hata hivyo, baadhi ya madaktari waliokuwa wamemzunguka hawakuweza kuthibitisha iwapo vifaa alivyokuwa amewekewa DCI Manumba vilikuwa ni sehemu ya mashine iliyokuwa ikimsaidia kupumua.



Hali hiyo iliwafanya ndugu na watoto wa kamanda huyo kuwa katika hali ya taharuki ambako baadhi yao walionyesha kushikwa na huzuni huku mmoja wa watoto wake ambaye jina lake halikupatikana akiwa katika hali ya majonzi makubwa.



Hadi MTANZANIA inaondoka katika Hospitali ya Aga khan saa 5:45 jioni mgonjwa huyo bado alikuwa hajatolewa katika chumba cha uchunguzi hali iliyowafanya ndugu kuendelea kusubiri katika eneo la mapokezi ya wagonjwa mahututi.



Alihojiwa na waandishi wa habari kuhusu hali ya mgonjwa, Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali hiyo, Dk. Jaffer Dharsee alisema kwa sasa hawezi kusema lolote hadi vipimo vya uchunguzi vitakapokamilika, huku akiwaahidi waandishi wa habari kuwa atatoa taarifa hiyo leo asubuhi.



“Siwezi kusema kitu kwa sasa kwani bado hali ya DCI inahitaji uchunguzi wa karibu wa madaktari na hadi sasa bado yupo katika chumba cha uchunguzi zaidi hivyo sina cha kusema nasubiri nikamilishe ripoti yote labda kesho ndiyo nitakuwa katika nafasi nzuri ya kusema kitu,” alisema Dk Dharsee.



Hata hivyo katika kipindi chote hicho, hali ya ulinzi ilikuwa imeimarika ambako polisi na askari kanzu walikuwa wamezunguka katika maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo kuhakikisha kunakuwa na ulinzi wa kutosha.



Viongozi



Jana viongozi mbalimbali waliendelea kufika hospitalini hapo kumjulia hali Manumba. Miongoni mwao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima ambaye aliwasili hospitali hapo mchana pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadick.



Viongozi wote hao walipokewa na daktari mkuu wa polisi aliyefahamika kwa jina moja la Dk Makata ambaye aliwapeleka moja kwa moja katika jengo la tatu kilipo chumba cha uchunguzi kwa ajili ya kumjulia hali DCI Manumba.



Dk. Nchimbi baada ya kutoka katika chumba cha mgonjwa hakutaka kuzungumza chochote licha ya kutakiwa kufanya hivyo na waandishi wa habari. “Mnataka niseme nini kwamba mgonjwa hali yake nzuri au mbaya? Mimi si daktari lakini kwa namna nilivyomuona nasema anaendelea vizuri,” alisema Dk. Nchimbi.



DCI Manumba aliugua ghafla na kulazwa katika Hospitali ya Muhimbili na Januari 14 alihamishiwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambapo alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).



Manumba ambaye aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo mwaka 2006 akichukua nafasi ya Adadi Rajabu, haijaelezwa wazi kuwa anasumbuliwa na ugonjwa gani, ingawa taarifa za awali zinasema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la figo.

CHANZO: Mtanzania

3 Jul 2011


DCI Manumba katika kashfa; Adaiwa kumkingia kifua mbunge asikamatwe
Sunday, July 3, 2011, 12:03
Habari, Mtanzania
*Adaiwa kumkingia kifua mbunge asikamatwe

Na Kulwa Karedia

MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, amedaiwa kumkingia kifua Mbunge wa Busega, Dk. Titus Kamani (CCM) asikamatwe.
Uamuzi wa kukamatwa umekuja baada ya mbunge huyo kuhusishwa na njama za kutaka kumuua aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Dk. Raphael Chegeni.

Habari zinadai kuwa, DCI Manumba amekuwa akimkingia kifua mbunge huyo, licha ya Jeshi la Polisi kutangaza azma ya kumkamata kwa nguvu kutokana na ukaidi wa kutotii amri ya jeshi hilo.

Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, DCI Manumba amekuwa akimkingia kifua mbunge huyo kwa kuwa wanatoka wilaya moja ya Magu, mkoani Mwanza.

Taarifa hizo ziliendelea kudai kuwa, tayari Dk. Kamani alikwisha jisalimisha polisi mkoani Mwanza mwishoni mwa wiki kwa mahojiano zaidi.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Manumba alikanusha shutuma hizo na kueleza kuwa tangu mbunge huyo ahusishwe na sakata hilo, hajawahi kumkingia kifua kwa namna yoyote.

“Kwanza nikwambie ukweli, suala hilo ndilo kwanza nalisikia kwako, sielewi kinachoendelea… kama kuna mambo Dk. Kamani amefanya taratibu zote za kisheria zitafuatwa.

“Sijawahi hata siku moja kumkingia kifua, kesi yao naamini inashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi, sasa iweje mimi nijiingize kwenye kitu ambacho sihusiki?” alihoji DCI Manumba.

DCI Manumba alisema yeye hapaswi kuzungumzia kwa undani suala hilo kwa kuwa si msemaji wa polisi na kwamba anayefaa kuhojiwa ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Saimon Sirro.

“Sasa hayo mengine unayosema mimi si msemaji, nakuomba umtafute RPC Sirro yeye ndiye anayeweza kuzungumzia zaidi suala hilo kwa kuwa limetokea kwake,” alisema.

DCI Manumba alikiri kutoka eneo moja na mbunge huyo, ingawa alisema hiyo si sababu ya kumkingia kifua. “Ni kweli huyu ni mbunge wangu na mimi ni mpiga kura wake, lakini hii si sababu ya kufanya nizuie polisi wasifanye kazi yao, hakuna mtu aliye juu ya sheria, hatutoki kijiji kimoja…narudia mimi ni mpiga kura wake, …nawashauri wale wote wanaohusishwa na tukio hili, waendelee na mambo yao, mimi sihusiki hata chembe katika hili,” alisema DCI Manumba.
Alisema upelelezi ndiyo njia pekee itakayomkomboa mbunge huyo kama ana hatia au la.

“Unajua hatufanyi kazi kwa kukurupuka, upelelezi unaoendelea ndiyo njia pekee itakayoamua kama nani ana kesi ya kujibu, tungoje tuone,” alisema.

Mapema wiki hii, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Simon Sirro, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mbunge huyo alijisalimisha na kutoa maelezo yake kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.

Alisema mbunge huyo alifika na kuhojiwa mwishoni mwa wiki na baada ya hapo aliachiwa, huku polisi wakiendelea na upepelezi zaidi kabla ya kumpandisha kizimbani.

Habari zinasema mbunge huyo, alijisalimisha kituo cha polisi Juni 25, mwaka huu na kuhojiwa usiku kabla ya kuondoka kuelekea Dodoma kuendelea na vikao vya Bunge. Akiwa mkoani Shinyanga, gari lake liligonga mtu na kuua papo hapo.

Mei 31, mwaka huu, inaelezwa kuwa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, liliandika barua Ofisi ya Bunge kutaka Dk. Kamani aende Mwanza kwa ajili ya mahojiano dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Barua hiyo yenye namba MZR/CID/SCR/105/2011/4 ilitumwa kwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila ikimtaka Dk. Kamani kwenda kujibu kesi yenye namba ya usajili MW/IR/2607/2011-MR-CC.28/2011.

Dk. Kamani atakuwa mshitakiwa wa tano iwapo atafikishwa mahakamani, baada ya watu wanne ambao ni Dismas Zacharia Ndaki, Erasto Kazimili Kombe, Queen Joseph Bogohe na Ellen Joseph Bogohe, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mwanza.

CHANZO: Mtanzania

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.