Showing posts with label MATHIAS CHIKAWE. Show all posts
Showing posts with label MATHIAS CHIKAWE. Show all posts

30 May 2013

Magufuli amkana Sitta, asema hana ubia naye urais 2015


Siku chache baada ya Waziri wa Afrika Mashariki Samuel Sitta kumhusisha Dk John Magufuli na kundi la urais la mwaka 2015, Waziri huyo wa Ujenzi, ameibuka na kupinga kauli hiyo, akisisitiza hafikirii kuwania nafasi hiyo.
Waziri Sitta alinukuliwa na gazeti hili juzi akieleza kuwa wakati ukifika, yeye na rafiki zake Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, watachagua mmoja wao watakayeona anafaa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015. Alisema hayo juzi kwenye Kongamano la Mawasiliano katika Nyanja za Digitali la wanafunzi wa Idara ya Uhusiano na Masoko, Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT), Mwanza.
Kabla ya hapo alikuwa amewataja rafiki zake hao wakati wa hafla ya kuchangia Kanisa Katoliki, Josephine Bakita, Parokia ya Igoma, Mwanza, Jumapili iliyopita.
Alisema hatagombea tena ubunge mwaka 2015, baada ya kuwa katika ulingo wa siasa kwa miaka 35 na badala yake ataangalia namna nyingine ya kuwatumikia wananchi huku akigusia mchakato wa kuwania urais ambao alieleza anamwachia Mungu.
“Kwa ubunge nimekwishawaeleza inatosha, sitagombea tena kwani miaka 35 inatosha, … lakini hatima yangu ni nini siwezi kujua lakini nina afya nzuri na mmoja wa wanasiasa wakongwe, wenye afya nzuri, mnaona ninavyopendeza... kwa urais namwachia Mungu tutaona,” alisema Sitta.
Kauli ya Magufuli
Akizungumza na gazeti hili nje ya ukumbi wa Bunge jana, Dk Magufuli alisema haelewi msingi wa kauli ya waziri mwenzake huyo, kwani hajui chochote katika mtandao wa urais alioutaja.
Magufuli alisisitiza kusema hana kundi, hakuwahi kuzungumza wala kuhudhuria vikao vya kundi lolote, na kwamba kundi lake ni CCM na Mwenyekiti wake ni Jakaya Kikwete.
“Sina kundi. Sijawahi kuwa na kundi na sitarajii kuwa na kundi lolote. Ninachojua kundi langu ni CCM na kiongozi wake ni mwenyekiti wake, Rais Kikwete,” alisema Dk Magufuli.
Hata hivyo, Dk Magufuli pia alipuuza taarifa kuwa alichangia harambee hiyo akisema, “Si kweli, Mwanza sijatoa hata senti na hata siku ilipofanyika hafla hiyo, nilikuwa Dar es Salaam katika mkutano na makandarasi.” Licha ya kutajwa kuwa miongoni mwa vinara wa urais 2015, Magufuli alieleza kuwa hakuwahi kuzungumza na Sitta suala hilo linalohusu makundi ya urais mwaka 2015.
CHANZO: Mwananchi
WAKATI HAYO YAKITOKEA, JANA PIA ILIKUWA SIKU CHUNGU  KWA SITTA,KAMA INAVYOONYESHA HABARI HII HAPA CHINI
Wassira amvaa Sitta
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, amemtaka waziri wa ushirikiano wa Afrika Mashariki Samwel Sitta, aweke wazi njia anazotumia kupambana na ufisadi nchini ambazo mawaziri wengine wa serikali ya CCM hawawezi kuzitumia.

Wakati Wassira akitaka ufafanuzi huo, Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe kwa upande wake alikataa kuzungumzia mbinu anazotumia Samwel Sitta kwa kile alichoeleza kuwa hawezi kuongelea masuala ya serikali na mtu asiyemjua.

Wassira na Chikawe walitoa kauli hiyo jana wakati gazeti hili lilipotaka maoni yao juu ya kauli ya Sitta iliyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa katika serikali nzima ni mawaziri wanne waliojipambanua kupambana na ufasadi na kutetea wanyonge.

Wassira alisema kwa sasa hawezi kuchangia jambo lolote juu ya kauli hiyo ya Sitta kwa kuwa hajaliona katika vyombo vya habari au kumsikia waziri huyo akisema hadharani.

Alisema kama kauli hiyo imetolewa na Sitta ni vema angefafanua mbinu anazotumia ili wengine waige.
“Mimi siwezi kuzungumzia hayo; mmeyasema nyie pia ingekuwa ni vema kama angeulizwa Sitta mwenyewe na atueleze mbinu zake tuone na wengine wanafanya nini,” alisema Wassira.

Alipoulizwa kama majina yaliyotajwa ni miongoni mwa makundi yanayodaiwa kujipanga ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa ajili ya urais wa 2015; Wassira alisisitiza jambo hilo aulizwe Sitta.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe, alipopigiwa simu kwa ajili ya ufafanuzi wa kauli hiyo, alikataa kuzungumzia jambo lolote kwa madai kuwa alishajeruhiwa kwa kutoa habari kwa njia ya simu.

“Sitaki na sizungumzi mambo ya serikali na mtu nisiyemjua tena katika simu…siku moja alinipigia mtu akasema anatoka Daily News nilipompa habari akaandika anavyojua na ikaniletea matatizo, kwanza kwa sasa niko Arusha,” alisema Chikawe na kukata simu.

Juzi wakati Waziri Sitta, akishiriki harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph katika Parokia ya Igoma jijini Mwanza, aliwataka Watanzania kujihadhari na watu wasio waadilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015.

Alisema watuhumiwa wa kashfa ya ufisadi wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond na Dowans ni hatari na hawastahili kuungwa mkono katika uongozi.

Alisema kutokana na hali hiyo ya ufisadi yeye pamoja na mawaziri wengine watatu wako pamoja katika fikra za kupambana na vitendo vya kifisadi, uonevu na mikataba tata.

Aliwataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, pamoja na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.


7 Jul 2010


Demokrasia katika jamii isiyojali utawala bora ni sawa na kufukia makaratasi ardhini kwa matarajio ya kuota mmea wenye matunda ya noti.Ni mithili ya kualika timu ya Taifa ya Brazil kwa mabilioni ya shilingi kisha mechi husika ituache na bili kubwa pasipo manufaa yoyote.Hebu tafakari.Mwezi Oktoba Watanzania kwa mamilioni yao watapiga kura kumchagua Rais na Wabunge.Japo shughuli hiyo ni ya siku moja tu,maandalizi yake yanagharimu mabilioni ya shilingi.Wenyewe wanasema ndio gharama ya demokrasia.Lakini baada ya uchaguzi,wengi-kama sio wote-wa tutakaowachagua watasahau kabisa kwanini tumewachagua,huku wakiwa bize kutafuta namna ya kufidia gharama walizotumia kuingia madarakani.

Zamani hizo tuliambiwa kuwa demokrasia ni pamoja na uwepo wa vyama vingi vya siasa.Takriban miongo miwili baadaye Watanzania wameshuhudia namna uwepo wa vyamahivyo vingi vya siasa ulivyoshindwa kulikwamua taifa letu kutoka kwenye lindi la umasikini.Sanasana umasikini umekuwa ukizidi kuongezeka huku wanasiasa wetu wakibadili kauli mbiu kila baada ya muhula (kwa mfano kutoka Ari Mpya,Kasi Mpya na Nguvu Mpya kuwa Ari Zaidi,Kasi Zaidi na Nguvu Zaidi).Tumeshuhudia pia mlolongo wa sera,mikakati,mpingo na vitu kama hivyo,from MKUKUTA to MKURABITA to KILIMO KWANZA.Na kwa mawazo mapya hatujambo,shughuli ipo kwenye utekelezaji.

Siku chache zilizopita nilitundika makala kuhusu utata wa kauli za Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe na zile za Makamu Mwenyekiti wa CCM Pius Msekwa kuhusu suala la uanzishwaji Mahakama ya Kadhi.Wakati Waziri Chikawe aliahidi kuwa mahakama hizo zingeanza kazi mwakani,Msekwa alitamka bayana kuwa suala hilo haliwezekani.Hadi leo hakuna ufafanuzi uliotolewa kuhusu suala hilo ila kilicho bayana ni kuwa CCM imeamua kuachana nalo baada ya kuliingiza kwenye manifesto yake ya Uchaguzi mwaka 2005.Kwa vile sie ni mahiri zaidi wa kuhangaika na mambo kwa mtindo wa zimamoto tunasubiri liwake la kuwaka ndipo tuanze kuhangaika namna ya kudhibiti.Taasisi zenye majukumu ya kuwa proactive (yaani kuazuia majanga kabla hayajatokea) ziko busy zaidi na kuhakikisha CCM inarejea madarakani kwa ushindi wa kishindo badala ya kujishughulisha na jukumu lao la msingi la kulinda na kutetea ustawi wa taifa letu.Kwao,siasa (yaani CCM) ndio nchi na ndio kila kitu.

Majuzi umejitokeza utata mwingine wa kauli kati ya mawaziri wawili waandamizi kuhusu suala la uraia wa nchi mbili (dual citizenship).Na kichekesho ni kwamba tofauti na ule mgongano wa kauli kati ya Chikawe na Msekwa,safari hii mgongano wa kauli za mawaziri hao umejiri ndani ya jengo la Bunge katika kikao kinachoendela cha bajeti ya mwaka 2010/11.Awali,Waziri wa Mambo ya Ndani Lawrence Masha alilieleza Bunge Tukufu kuwa serikali imeamua kuwa huu sio wakati mwafaka kwa suala la uraia wa nchi mbili,na kwamba serikali anaangalia uwezekano wa kuanzisha ukaazi wa kudumu (permanent residency).Waziri Masha alieleza kuwa serikali inaandaa hoja kuhusu suala hilo la permanent recidency kwa minajili ya kuileta bungeni ijadiliwe. "Huu sio wakati mwafaka kuruhusu uraia wa nchi mbili,serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha ukaazi wa kudumu badala ya uraia wa nchi mbili", alisema Masha.

Wakati Masha akisema hivyo,Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe alilieleza Bunge hilohilo kuwa serikali imeridhia suala la uraia wa nchi mbili na kwamba Wizara yake iko kwenye mchakato wa kuwasilisha suala hilo kwenye kikao cha Barza la Mawaziri.Pia Membe alieleza kuwa anafanya mawasiliano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ili kupata baraka zao kutokana na suala hilo kuwa la Muungano.Akihitimisha hoja ya bajeti ya wizara hiyo, kwa mwaka wa fedha 2010/2011, Waziri Membe alisema siyo dhambi, Watanzania kutafuta riziki nje ya nchi na ni haki yao kubaki na uraia wa Tanzania.Alisema wakati umefika kwa Watanzania, kupatiwa haki yao ya msingi kwani licha ya kuwa ni manufaa kwao pia ni manufaa kwa nchi kutokana na fursa ya kuongeza pato la taifa.

Kadhalika,inadaiwa kuwa Waziri Membe aliwaeleza Watanzania waliohudhuria mkutano wa Diaspora jijini London hivi karibuni kwamba suala hilo limeshajadiliwa na baraza la mawaziri na linasubiri kuwasilishwa bungeni ili upitishwe au kupingwa na wabunge.Mimi sikuhudhuria Mkutano huo wa Diaspora kwa vile niliamini ungenipotezea muda wangu tu kwa sababu viongozi wetu ni mahiri sana katika kuahidi mambo mazuri kwenye hadhara,na hujifanya wasikivu sana lakini utekelezaji ni zero,sifuri,zilch!

Ni dhahiri kwamba mmoja kati ya mawaziri hawa anadanganya.Wakati sina la kusema kuhusu kauli ya Waziri Masha,kauli za Waziri Membe huko Bungeni na London zinaleta utata unaoweza kuyumkinisha kuwa kuna urongo wa namna flani.Je kauli ipi ni sahihi kati ya hiyo alotoa London kuwa suala hilo limeshajadiliwa na Baraza la Mawaziri na hiyo ya bungeni kuwa suala hilo bado liko wizarani huku likifanyiwa mchakato wa kulipeleka kwenye Baraza la Mawaziri?

Unajua kwanini mmoja wao anadanganya?Sababu ni kadhaa,lakini kwa ufupi,moja,ni kwa vile mdanganyifu huyo anafahamu bayana kuwa wabunge wanaoelezwa suala hilo wapo bize zaidi kufikiri namna watakavyorudi bungeni baada ya uchaguzi (sambamba na kuwazia posho zao nono za vikao vya bunge) kuliko kumkalia kooni waziri aeleze kinagaubaga.Ndio maana mwanzoni mwa makala hii nilibainisha uselessness ya demokrasia yetu.Tunapoteza mabilioni ya shilingi (sambamba na muda wetu kusikiliza porojo za "mkituchagua tufafanya hiki na kile") kuwachagua watu wa kutuwakilisha bungeni lakini wakishafika huko wanakuwa bize zaidi na maslahi yao binafsi.

Pili,anayedanganya kati ya mawaziri hao anafahamu kuwa aliyemteua hatamwajibisha.Kama kuna mtu alimudu kumzuga Rais kwa kuchomekea ishu kadhaa kwenye muswada wa sheria za gharama za uchaguzi na kisha akasalimika,kwanini basi mdanganyifu huyo katika suala hili la uraia mbili awe na hofu?

Tatu,waziri anayedanganya kati ya hao wawili anafahamu udhaifu wa Watanzania katika kudai haki zao za msingi.Kiongozi anaweza kudanganya waziwazi kwenye umati wa watu lakini bado akaishia kupigiwa makofi na vigeregere.Ule wimbo wa "Ndio Mzee" wa Profesa Jay unawakilisha hali halisi ya namna Watanzania wengi wanavyoridhia kuzugwa na wanasiasa wababaishaji.Hebu angalia namna harakati za kuirejesha tena madarakani CCM zinavyopamba moto huko nyumbani.Kwa mgeni,anaweza kudhani labda chama hicho ni kipya na hakihusiki kabisa na kashfa za ufisadi,kubebana,kubomoa uchumi wetu na madudu mengine chungu mbovu yanayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi masikini kabisa duniani licha ya raslimali lukuki iliyojaaliwa kuwa nazo.Binafsi naamini kuwa unyonge huo wa Watanzania umechangiwa sana na siasa za chama kimoja ambapo kiongozi alikuwa mithili ya Mungu-mtu,hakosei,lazima ashangiliwe hata akiongea utumbo,sambamba na suala la kujikomba kwa viongozi kwa matarajio ya kujikwamua kwa namna moja au nyingine.

Na kwa vile vyama vya upinzani vimetuthibitishia kuwa uwezo wao katika kuing'oa CCM madrakani ni kama haupo,basi mazingaombwe kama hayo ya Chikawe na Msekwa,na haya ya sasa kati ya Masha na Membe yataendelea kuwepo kwa muda mrefu sana.Unaweza kuhisi kama nimekata tamaa vile kwa namna ninavyoandika.Hapana,ila safari yetu ni ndefu sana,na tatizo sio urefu tu bali ni kiza kilichotanda kwenye njia yetu ambayo imejaa mashimo kadhaa.Ni sawa na kipofu kumsaka paka mweusi kwenye chumba chenye giza ilhali paka huyo hayumo chumbani humo.

26 Jun 2010

Sijui ni ukosefu wa mawasiliano au uzembe tu,au pengine ni mkakati wa makusudi wa kutoa kauli zinazotofautiana ili baadaye iwe rahisi "kuziruka kimanga",lakini ni dhahiri kuwa mmoja kati ya viongozi hawa anatudanganya.Wakati Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe akirejea ahadi kama ya mwaka 2005 (wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu) kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi,Makamu Mwenyekiti wa CCM Pius Msekwa anasema bayana kuwa suala hilo halipo (labda Waislamu wenyewe walishughulikie "kivyao").Hebu soma kwanza hapa chini

Kwa mujibu wa Gazeti la Tanzania Daima: SERIKALI imesema Mahakama ya Kadhi itaanza katika mwaka wa fedha 2010/11 baada ya jopo la wanazuoni wa Kiislamu wanaoziangalia na kuzihuisha sheria za Kiislamu kukamilisha kazi hiyo.

Jambo hilo lilibainishwa jana bungeni na Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe wakati akisoma hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2010/2011 ambapo ameliomba Bunge limuidhinishie kiasi cha sh bilioni 116.8

Alisema kuwa jopo hilo linaziangalia na kuzihuisha sheria za Kiislamu zinazohusiana na ndoa, mirathi na urithi kwa madhumini ya kuziorodhesha ili zitambuliwe chini ya sheria za dini ya Kiislamu (Islamic Law resstatment act).

Aliongeza kuwa jopo hilo lilianza kazi hiyo baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kukutana na Mufti, Sheikh Mkuu, Issa Bin Shaaban Simba, na kukubaliana kuwa waanzishe mchakato wa Mahakama ya Kadhi.

Lakini Gazeti la Majira linaripoti kwamba:

Katika hatua nyingine, Bw. Msekwa amefafanua sababu za ilani ya CCM mwaka huu kutohusisha kipengele cha uanzishwaji wa Mahakam ya Kadhi kama ilivyokuwa mwaka 2005.

Alisema kuwa ahadi hiyo iliyotolewa 2005 tayari utekelezaji wake umekamilika.

Katika ilani hiyo, kifungu namba 108(b) CCM iliahidi kulipatia ufumbuzi suala la kuanzishwa mahakama ya kadhi Tanzania bara, ambalo limekamilika kwa kukabidhi wenye dini yenyewe wahusike katika uanzishwaji wa mahakama hiyo, kwa kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siyo ya kidini.

"Serikali inaweza kukubali au kukataa, ndiyo maana ya kulipatia ufumbuzi lakini watu wanalitafsiri vibaya kuwa
serikali kupitia kifungu hicho imekubali kuanzishwa kwa mahakama hiyo wakati sivyo," alisema Bw. Msekwa.

Alibanisha kuwa serikali ilifanyia kazi kupitia Tume ya Kurekebisha sheria ambayo ilishauri kwamba haitakuwa sahihi kwa mahakama ya kadhi kuundwa na serikali kwa kuwa ni suala linalohusu taratibu za dini ya kiislamu.

Aliongeza kuwa baada ya serikali kupata ushauri huo ilifanya uamuzi kwamba haitaunda mahakama ya kadhi lakini kwa kuwa suala hilo linahusu taratibu za dini la kiislamu, waislamu wapo huru kuunda mahakama hiyo ndani ya taratibu za dini yao.

17 Dec 2009


Waziri wa Sheria adai Bunge la sasa halina ubavu kwa serikali
Na Leon Bahati
WAZIRI wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe amezidi kutoa kauli tata baada ya kuligeukia Bunge la Jamhuri ya Muungano, akisema halina nguvu ya kuilazimisha serikali kufanya mambo na kwamba kazi yake ni kuishauri.

Hiyo ni kauli ya pili ya waziri huyo katika kipindi kisichopungua wiki moja baada ya kukaririwa Jumatatu akisema kuwa Rais Jakaya Kikwete hana uwezo wa kuwachukulia hatua watuhumiwa wa ufisadi kwa kuwa mfumo wa utawala wa sheria hauruhusu vitendo kama hivyo.

Kauli hizo mbili zinazohusu mamlaka ya kisheria zimetolewa katika kipindi ambacho mjadala mkubwa wa hatua zinazostahili kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa katika kashfa ya utoaji zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond Development (LLC) ukiwa umemgeukia rais.

Pia Chikawe ametoa kauli hiyo wakati Bunge likiishinikiza serikali kutoa taarifa ya utekelezaji wa maazimio yake 23 dhidi ya wahusika kwenye kashfa hiyo kubwa iliyotikisa nchi baada ya Edward Lowassa kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri mkuu kutokana na ushauri uliotolewa na kamati teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza kashfa hiyo....INAENDELEA HAPA

16 Dec 2009


Prof Shivji asema Rais Kikwete ana mamlaka kisheria kuwabana mafisadi
*WENGINE WAMTAKA WAZIRI CHIKAWE AACHE KUKURUPUKA
Na Sadick Mtulya

SIKU moja baada ya Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe kusema Rais Jakaya Kikwete hawezi kutumia mamlaka yake kuwabana mafisadi, baadhi ya wanasheria nchini, akiwamo Profesa Issa Shivji, wamepinga kauli hiyo kwa kusema sio kweli.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana wanasheria hao walisema rais anaweza kuwabana mafisadi kwa kutumia mamlaka yake ndani ya chama na serikali.

Profesa Issa Shivji alisema Rais Kikwete anaweza kupambana na watuhumiwa wa ufisadi kwa kuwavua madaraka walionayo katika chama au serikali.

Gwiji hilo la Sheria na Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, alisema kama watuhumiwa watakuwa watumishi wa serikali au watendaji katika mashirika ya umma, rais anaweza kuwawajibisha kwa kutumia sheria na kanuni za utumishi wa umma.

"Kumwajibisha mtuhumiwa sio iwe kumpeleka mahakamani, unaweza kuchukua hatua za awali ikiwemo kumvua nyadhifa zote. Kama ni mwanasiasa au mtumishi katika serikali na mashirika ya umma, unaweza kumwajibisha kwa mujibu wa sheria za umma," alisema Profesa Shivji.

Alisisitiza Kusema Rais Kikwete hana uwezo wa kuwabana mafisadi sio kweli na Watanzania wanatakiwa kuelewa hivyo kwamba rais anaweza.

Kauli ya Profesa Shivji iliungwa mkono na Profesa Abdallah Safari, aliyetia ngumu akisema sheria za nchi ikiwemo ya utawala, inampa uwezo na mamlaka rais kupambana na vitendo vya ufisadi ndani ya serikali yake na hata katika chama chake.

Rais kukasimu mamlaka yake kwa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ) na kwa DPP haimaanishi kwamba sasa yeye hana uwezo wa kupambana na watu wanaojihusisha na ufisadi. Bado anao, alisema Profesa Safari....INAENDELEA HAPA

Alifafanua kwamba, Rais Kikwete anayewajibika katika kupambana na ufisadi kwa kuwa yeye ndiye anayewajibika moja kwa moja kwa wananchi wa Tanzania.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.