Showing posts with label MBOWE. Show all posts
Showing posts with label MBOWE. Show all posts

17 Jan 2014

KATIKA hitimisho la makala yangu iliyochapishwa wiki mbili zilizopita, iliyobeba kichwa cha habari ‘Ni mwaka wa siasa za hovyo CCM, CHADEMA, niliahidi kuendeleza utabiri wa mwaka huu 2014, kwa kuangalia anga za kimataifa.
Kwa bahati nzuri, siku nne tu baada ya kuchapishwa makala hiyo, moja ya mambo niliyotabiri - kuendelea kwa mgogoro wa CHADEMA na uwezekano wa migogoro ndani ya vyama vya upinzani kuwa ya hadharani - limetokea.
Ninaomba niweke bayana kuwa masikitiko yangu kuhusu maendeleo mapya katika mgogoro wa CHADEMA ni makubwa zaidi ya furaha yangu kuona nilichotabiri wiki iliyopita kweli kimetokea. Nitakuwa mbinafsi na mnafiki ‘kusherehekea usahihi wa utabiri wangu’ katika jambo lisilopendeza. Laiti ingekuwa ni chaguo langu basi ningetamani mabaya yote niliyotabiri yasitokee, lakini kwa bahati mbaya hali halisi haikwepeki.
Takriban wiki mbili zilizopita, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) Zitto Kabwe alirusha ‘bomu zito’ ambapo alitoa tuhuma kubwa na hatari dhidi ya Mwenyekiti wake taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, na chama hicho kwa ujumla. Pengine ili kuleta ladha halisi ya alichosema Zitto ni vema nikanuu ‘waraka’ mzima kama ifuatavyo:
"Lissu anasema nimepewa magari 2 na Mzee Mkono. Anasema kaambiwa na Mkono. Naamini Mkono alimwambia pia mwaka 2005 alimpa Freeman Aikaeli Mbowe tshs 40m ili Mbowe asifanye kampeni Musoma Vijijini.
“Nadhani alimwambia pia mwaka 2008 (baada ya orodha ya mafisadi kutangazwa 2007) Mkono alimpa Freeman tshs 20m za uchaguzi wa Tarime na Freeman akasema kwenye chama ametoa mkopo na akalipwa. Nadhani alimwambia pia kuwa mwaka 2010 Mkono alimpa Mbowe tshs 200m za kampeni ya Slaa.
“Pia hakusahau kumwambia kuwa Rostam Aziz alimpa Mbowe tshs 100m za kampeni. Lissu anajua kuwa gazeti la Tanzania Daima limeanzishwa na fedha za chama kutoka Conservative Party?
“Nimefanya internship yangu kwa Mkono and Company Advocates kuhusu masuala ya mikataba. Mzee Mkono ni Mzee wangu na alisaini petition ya kumtoa Waziri Mkuu Pinda. Lissu awaambie waliyemtuma wamwambie ukweli wote. Lissu ajue yeye ni kifaranga tu, Mimi namtaka mama wa kifaranga ajitokeze. Aeleze aliingia deal gani na Kinana na Sumaye mwaka 2005 kufuatia deni lake NSSF. Aweke wazi mkataba kati yake na NHC kuhusu nyumba ya umma ilipo Club Bilicanas.
“They must know I am not a push over. Chacha died, I won't. Mtu ambaye hawezi kuheshimu mke wake aliyemzalia watoto hawezi kunyooshea mtu kidole kuhusu maadili."
Zitto alibandika waraka huo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, lakini kwa sababu anazojua yeye pekee, baadaye aliuhariri na kutojumuisha tuhuma hizo. Aidha kwa kutofahamu au makusudi, uhariri uliofanywa na mwanasiasa huyo katika waraka huo haukuzuia kusambaa kwa kasi mtandaoni.
Niliposoma waraka huo nilipatwa na mshtuko mkubwa, nikabaki ninajiuliza iwapo Zitto alikuwa ‘mzima’ wakati anaandika alichoandika.  Japo inawezekana alifanya hivyo kwa kuzingatia kile kinachofahamika mtaani kama ‘umemwaga ugali na mie namwaga mboga...bora tukose wote,” ukweli ni kwamba bandiko hilo lina madhara makubwa, kwa Zitto binafsi na kwa pengine ustawi wa CHADEMA kwa ujumla.
Madhara kwa Zitto ni ya kisheria zaidi. Tayari Mbowe ameonyesha nia ya kumburuza Zitto mahakamani kuthibitisha tuhuma hizo nzito. Bila kujali kuwa tuhuma hizo zina ukweli au la, mtu yeyote mwenye uelewa wa ‘dili za siri’ atafahamu kuwa ni vigumu kuzithibitisha kisheria, yayumkinika kuhisi kuwa Zitto atakuwa na kazi ya ziada katika ‘kesi’ hiyo (iwapo itafunguliwa).
Iwe ni tuhuma za Nimrod Mkono kumpa Mbowe shilingi milioni 260 katika mazingira ambayo si tatanishi tu bali pia kwa namna fulani ni hujuma dhidi ya CHADEMA, au Rostam Aziz kumpatia Mbowe shilingi milioni 100, au ‘dili’ kati ya Mbowe na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, sidhani kama Zitto anaweza kuthibitisha tuhuma hizo iwapo Mbowe atatimiza azma yake ya kufungua kesi. 
Je, inawezekana kuwa kwa kutambua ‘kosa hilo la kisheria’ ndio maana muda mfupi baadaye Zitto alihariri ‘post’ hiyo? Wakati jibu analo Zitto mwenyewe, ukweli unabaki kuwa tuhuma hizo ni nzito mno, na iwapo ni za kweli basi zinapoteza kabisa hadhi ya CHADEMA.
Ikumbukwe kuwa katika waraka uliopelekea Zitto kuvuliwa nyadhifa zake mbalimbali ndani ya CHADEMA, walioandika waraka huo waligusia walichokiita ‘udhaifu wa wanayemtaka’ (wakimaanisha Zitto), na kudai, “Maneno yake mara nyingine hayazingatii anayazungumza katika mazingira gani na hivyo kuwasha masikio ya wanataasisi jambo linalompunguzia kukubalika kwake taratibu.” 
Kadhalika, walieleza kuwa; “Kuna wakati tunayemtaka (Zitto) hujibu kwa taharuki kubwa dhidi ya mashambulizi yanayoelekezwa kwake jambo linalomfanya achukue maamuzi yasiyo sahihi kwa wakati huo. Kwa kifupi kuna wakati tunayemtaka (Zitto) huonekana kufanya maamuzi kwa hisia zaidi badala ya kutulia kwanza na kutafakari kwa kina ikiwa ni pamoja na kutafuta ushauri kwa wenzake kabla ya kujibu.”
Ndugu msomaji, huhitaji kuwa mwanasaikolojia kuhisi kuwa huenda kilichomsukuma Zitto kuandika ‘waraka’ huo kwenye ukurasa wake wa Facebook ni kile Waingereza wanakiita “putting emotions in front of common sense”, yaani kwa tafsiri isiyo rasmi, kuweka mbele jazba badala ya busara.
Kwa kujaribu kuonyesha kuwa Mbowe si mwadilifu (kwa maana ya kupokea misaada kutoka kwa ‘wanasiasa kama Mkono na Rostam waliowahi kutajwa na CHADEMA kuwa ni mafisadi’), linakuja swali la msingi, kwanini Zitto alikalia kimya tuhuma hizo nzito kwa takriban miaka minane hadi sasa baada ya kuvuliwa madaraka? Hivi kuna neno stahili kuelezea hali hiyo zaidi ya unafiki?
Tukiamini tuhuma hizo za Zitto, je naye si sehemu ya ‘uhuni wa CHADEMA’ wa kukemea mafisadi hadharani ilhali pembeni wanapokea misaada ya watu hao hao wanaowatuhumu? Ninasema hivyo kwa sababu Zitto hakuwa katibu wa shina bali Naibu Katibu Mkuu (taifa)  wa chama hicho, na mbunge, na kwa vyovyote vile naye ni mnufaika wa fedha hizo ‘za mafisadi.’
Laiti angekuwa haridhii vitendo hivyo basi aidha angejitoa mhanga na kuweka ukweli hadharani wakati huo (na hiyo ingeweza kuzuia kurejea kwa vitendo kama hivyo) au angeweza kujiuzulu kwa kuona ‘chama chake kinashirikiana na watuhumiwa wa ufisadi. Kwa nini hakufanya hivyo? Jibu jepesi ni hilo nililoandika hapo juu: alikuwa mnufaika wa vitendo hivyo (iwapo kweli vilitokea, maana tayari baadhi ya aliowataja wamekanusha ‘kumpa msaada’ Mbowe).
Binafsi, ninadhani moja ya matatizo yanayomkabili Zitto ni wanaojiita au kujitambulisha kama wafuasi wake. Wengi kati yao ni wenye mapenzi na CCM, na ushabiki wao kwa Zitto ni wa kirafiki (kimaslahi?) zaidi. Ndio, tofauti za kiitikadi hazimaanishi uadui, lakini wengi wetu tunaufahamu msemo ‘nionyeshe marafiki zako na nitakwambia wewe ni nani,’ yaani mara nyingi watu wanaotuzunguka hutoa picha fulani kuhusu sisi wenyewe.
Lakini tatizo jingine kuhusu ‘wafuasi na marafiki hao wa Zitto’ ni kutokuwa washauri wazuri kwake. Ukisoma mengi ya wanayoandika, hususan huko kwenye mitandao ya twitter, utabaini kuwa kimsingi wanachofanya ni ‘kumvimbisha kichwa Zitto’ bila kutoa ushauri unaoweza kusaidia ustawi wa kisiasa wa mwanasiasa huyo kijana.
Na mfano wa hivi karibuni ni baada ya Zitto kubandika waraka huo wenye tuhuma nzito huko Facebook. Wengi wa wafuasi wake walionekana kuchekelea ‘Mbowe alivyoumbuka’ bila kujali athari za kisheria kwa Zitto na ustawi wa CHADEMA kwa ujumla (kwanini wajali ilhali wengi wao ni wanaCCM)?
Kwa wafuasi wa Zitto, mwanasiasa huyo ni majeruhi wa siasa za chuki na mizengwe ndani ya CHADEMA. Lakini kwa wengine, Zitto anaonekana kama mtu anayeendeshwa na ‘ego’ kubwa inayomfanya kujiona yeye ndiye-au zaidi ya- CHADEMA.
Ni vigumu kubashiri hatma ya maisha ya kisiasa ya Zitto lakini kwa hali ilivyo ni vigumu mno kuona mustakabali wake ndani ya chama hicho. Ninakumbuka mwanasafu mmoja wa gazeti hili alimshauri mwanasiasa huyo hivi karibuni kuwa suluhisho la busara kwake kwa sasa ni kutosubiri kuvuliwa uanachama, ajiondoe mwenyewe huko CHADEMA, na kuitaka Mahakama isiingilie kazi ya chama.
Mwisho, bado ninaamini kuwa Zitto ni mwanasiasa mzuri lakini pengine kwa upungufu wa kibinadamu au makusudi, washauri wabovu au sababu nyinginezo, hazingatii umuhimu wa busara hizi tatu katika medani ya siasa: moja, waweke marafiki zako karibu lakini waweke maadui zako karibu zaidi, na pili, hakuna marafiki au maadui wa kudumu katika siasa, na tatu, hakuna mwanasiasa anayeweza kuwa mbadala wa chama (hasa katika mazingira ya siasa zetu ambapo kwa kiasi kikubwa chombo pekee cha uongozi wa kisiasa ni chama cha siasa. Bila chama, mwanasiasa hata awe maarufu kiasi gani anabaki kuwa raia wa kawaida tu).
Katika waraka wake, Zitto aliandika, “They must know I am not a push over. Chacha died, I won't” (lazima wafahamu mie sio mtu wa ‘kupelekeshwa.’ Chacha (Wangwe?) alikufa, mimi sitokufa). Hiki ni kiburi, utoto au? Ni mwanadamu mwenye uhakika wa kutokufa? Nihitimishe kwa kumshauri kwamba labda kweli ana uhakika wa kuishi milele lakini kwa kutanguliza hisia badala ya busara, yayumkinika kubashiri kuwa anaweza kuwa anajiua mwenyewe kisiasa (committing political suicide).



7 Jun 2012

Picha ya kwanza inamuonesha Mwenyekiti Freeman Mbowe akikata utepe wa kufungua Ofisi ya CHADEMA Kijiji cha Mkangaula. Ilikuwa ni baada ya Katibu Mkuu, Dkt. Slaa kutoa hotuba ya ufunguzi na John Mnyika kupandisha bendera ya chama nje ya ofisi hiyo, ikiwa ni ishara ya kupiga hatua katika mapambano ya awamu ya pili.

Picha zingine zinamuonesha Mnyika akitoa 'somo' kwa wanakijiji wa vijiji vya Kata ya Lumesule. Mapema kabla alikaribishwa na kuzungumza na Katibu wa Tawi wa CUF, Bi. Zaituni (pichani). Wananchi walimwelewa vyema. Kadi zikauzwa vizuri. Akaacha uongozi wa muda wa tawi lenye wanachama wa 34. Katika Kijiji hicho cha Lumesule, mwananchi mmoja kwa jina la Yasin Mohamed alihoji ilikuwaje CHADEMA wakaachia Dkt. Slaa ashindwe urais, wakati alichaguliwa kwa kura nyingi na wananchi na wao wanajua alishinda uchaguzi huo wa mwaka 2010.





Picha ZIFUATAZO zinamuonesha John Mnyika akiwa katika vijiji vya Kata za Makukwe na Mkwedu, wilayani Newala. Kwa George Mkuchika ambako alikutana na kiashiria cha wazi kuhusu udhaifu wa Waziri Mkuchika (Mbunge wa Newala) katika kusimamia majukumu yake, baada ya wananchi katika Kijiji cha Tengulengu, Kata ya Mkwedu kumlalamikia kuwa Diwani wa Kata hiyo, Juma Dadi hajawahi kufungua ofisi yake zaidi ya mwaka mmoja sasa. Pamoja na kuwasilisha malalamiko yao kwa barua Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Newala na kwa Mbunge wao, Mkuchika, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Unaweza kuona pia wanawake walivyonogewa na PIPOOOOOOOOOOZ POWER, nao wakaipiga ya nguvu kweli kweli kuonesha umoja na mshikamano katika Falsafa ya Nguvu ya Umma ya CHADEMA, katika kudai uwajibikaji, kupigania haki, uhuru na mabadiliko ya kweli ya mfumo na utawala nchini.

Unaweza pia kumuona Kamanda Alfonsi Mawazo akiendelea kupata uzoefu wa mikikimikiki ya kujenga hoja katika uwanja wa mapambano. Si ofisini.








Picha zifuatazo zinamuonesha John Mnyika akiwa katika vijiji vya Kata za Makukwe na Mkwedu, wilayani Newala. Kwa George Mkuchika ambako alikutana na kiashiria cha wazi kuhusu udhaifu wa Waziri Mkuchika (Mbunge wa Newala) katika kusimamia majukumu yake, baada ya wananchi katika Kijiji cha Tengulengu, Kata ya Mkwedu kumlalamikia kuwa Diwani wa Kata hiyo, Juma Dadi hajawahi kufungua ofisi yake zaidi ya mwaka mmoja sasa. Pamoja na kuwasilisha malalamiko yao kwa barua Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Newala na kwa Mbunge wao, Mkuchika, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Unaweza kuona pia wanawake walivyonogewa na PIPOOOOOOOOOOZ POWER, nao wakaipiga ya nguvu kweli kweli kuonesha umoja na mshikamano katika Falsafa ya Nguvu ya Umma ya CHADEMA, katika kudai uwajibikaji, kupigania haki, uhuru na mabadiliko ya kweli ya mfumo na utawala nchini.

Unaweza pia kumuona Kamanda Alfonsi Mawazo akiendelea kupata uzoefu wa mikikimikiki ya kujenga hoja katika uwanja wa mapambano. Si ofisini.




Pichani chini ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe akihutubia Masasi




Chini,wananchi wakigombea kadi za Chadema




Picha chini,wananchi wakisikiliza hotuba kwa makini








Picha zote zimetumwa na mdau SAJJO

27 May 2012



Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Dk Wilbrod Slaa akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.




 Mwenyekiti wa Taifa Freeman Mbowe Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA  akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


Mbunge wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Singida Magharibi Mheshimiwa Tundu Lissu akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


 Mbunge Wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Ubungo Mheshimiwa John Mnyika akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


Mbunge  wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Mbeya Mjini Mheshimiwa Joseph Mbilinyi aka Mr II(SUGU) akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


 Viongozi wa chadema wakifurahia kadi nyingi za CCM zilizorudishwa leo jioni kwenye mkutano
Deo Munish Katibu mkuu wa BAVICHA akiteta jambo na mmoja aliyehudhuria mkutano wa CHADEMA Wa uzinduzi wa kampeni ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.




  Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe akiwaaga wananchi waliokuwa wamefurika makao makuu ya chama kinondoni walikofika wakitokea jangwani usiku huu
 Mbowe akiwatania wanachama ofini kinondoni baada ya wananchi kuanza kudai chama kimfukuze John Shibuda.Alikuwa akijifanya hasikii wanachosema na hapa anajaribu kuwasikiliza zaidi.hata hivyo Mbowe aliwaondoa wasiwasi na kusisitiza kuwa chama kinao utaratibu wa kushughulika na viongozi wanaokiuka maadili ya chama na kuwaomba wawaamini kama viongozi kuwa wanaouwezo wa kulishughulikia jambo hilo na mengine
 Mh.Mbowe na Mnyika wakiwa wamesimama kwenye gari wakati wa matembezi wakitoka kwenye mkutano
Aliyekua Mbunge wa Arusha Mjini(CHADEMA)Mheshimiwa Godbless Lema akiwa juu ya gari huku akishangiliwa na vijana jioni baada ya mkutano
 Sehemu ya umati uliowasindikiza viongozi wa chadema toka jangwani hadi kinondoni.wamesambaa yapata saa 2 usiku.

PICHA ZOTE NA MAELEZOKWA HISANI YA BLOGU YA MHESHIMIWA HAKI NGOWI

5 Feb 2012

Viongozi wa Chadema jana tarehe 4 Februari 2012 wamekutana na kufanya Mazungumzo na Watanzania wanaoishi Washington DC . Katika msafara huo ambao umeongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Mheshimiwa Freeman Mbowe na Mbunge wa Nyamagana na Waziri kivuli wa Mambo ya nje Mheshimiwa Ezekiel Wenje, wameongelea mambo mbalimbali ikiwemo suala la Mipango ya Maendeleo ya Chama na Mikakati ya kujiandaa na chaguzi zijazo hususani uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Hali kadhalika wakazi hao wa Washington DC wametumia fursa hiyo kumuuliza maswali mbalimbali hususani suala la upatikanaji wa Katiba mpya. Akichangia katika mjadala huo Prof N. Boazi amewakumbusha viongozi hao umuhimu wa kuwa na katiba mpya ambayo itampunguzia madaraka Rais tofauti na sasa inayompa Rais  madaraka  makubwa na kunyima fursa kwa wengine.


Pia wakazi wa Washington DC walimuuliza Mheshimiwa Freeman Mbowe kuhusu suala la mgomo wa madaktari unaoendelea. Akijibu suala hili Mheshimiwa mbowe amesema kuwa alipata nafasi ya kuwasiliana na Viongozi wa mgomo huo lakini walimjibu kwamba hawataki kulifanya suala hilo la Mgomo kuonekana la kisiasa kwa kuwahusisha Chadema.



Mheshimiwa Freeman Mbowe akiwahudubia Watanzania wanaoishi  Washington DC jana jumamosi Feb, 4 2011 Nchini Marekani




 Wakazi wa Washington DC wakimsikiliza Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa makini katika mkutano huo.




Mbunge wa Nyamagana na Waziri kivuli wa Mambo ya nje Mheshimiwa Ezekiel Wenje akiongea katika mkutano huo.


Baada ya Mheshimiwa Freeman Mbowe na  Ezekiel Wenje kuongea,  Watanzania waliohudhuria walipata nafasi ya kuliza masuali, na  moja ya maswali aliyoulizwa Mhe Freeman Mbowe ni ile dhana kuwa CHADEMA ni "chama cha waChagga na matajiri". Hapa chini anafafanua dhana zote hizo na ile aliyosema iliwahi kusambaa kuwa ni "chama cha waKristo"


CHANZO: Swahilivilla. Shukrani pia kwa Mzee wa Changamoto Mubelwa Bandio kwa kunitumia kiungo (link)

6 Jun 2011


Utawala wa Rais Jakaya Kikwete unaendelea na jithada zake za kutaka kuifanya Tanzania isitawalike baada ya jeshi lake la polisi kuendeleza ubabe dhidi ya viongozi wa Chadema.

Katika matukio yanayoweza kuingizwa kwenye vitabu vya historia (chafu),jeshi hilo maarufu zaidi kwa ubabe kuliko uwezo wake kukabiliana na uhalifu limewatia mbaroni Mwenyekiti wa taifa wa Chadema,Freeman Mbowe,na Mbunge maarufu wa chama hicho Zitto Kabwe.Wakati Mbowe,ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Upinzani Bungeni (wadhifa unaomfanya kuwa Waziri Mkuu Kivuli) alikamatwa kwa madai ya kukiuka taratibu za dhamana katika kesi inayomkabili huko Arusha,Zitto alikamatwa kwa madai ya kuzidisha muda wa kuhutubia mkutano wa hadhara.

Tangu Tanzania iridhie uwepo wa mfumo wa vyama vingi vya siasa,mahusiano kati ya vyombo vya dola na vyama hivyo yamekuwa mabaya na ya ounevu kupindukia.Tatizo la wazi ni vyombo hivyo vinavyoendeshwa kwa fedha za walipa kodi pasipo kujali itikadi zao za kisiasa kuendelea kutekeleza majukumu yake kana kwamba ni matawi ya chama tawala.Wakati jeshi la polisi ndilo linaloongoza kwa kuwanyanyasa wapinzani,taasisi nyingine za dola kama Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania pia kwa nyakati mbalimbali zimeonyesha kuweka mbele unazi wa kisiasa na kuipendelea CCM.

Lakini licha ya kushamiri kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani,kuibuka kwa Chadema kama ngome kuu ya upinzani kumekuwa mithili ya pilipili inayowawasha polisi kiasi cha kuwaandama viongozi wa chama hicho kila kukicha.

Ni dhahiri kuwa matendo haya yana baraka za Rais Kikwete kwani laiti angemwamuru rafiki yake Said Mwema,Inspekta Jenerali wa Polisi,kuhakikisha jeshi la polisi sio tu linawapa heshima viongozi wa upinzani bali pia lizingatie haki zao za kibinadamu,ni dhahiri tusingeshuhudia manyanyaso kama hayo waliyopewa Mbowe na Zitto.

Kikwete na jeshi lake la polisi wanapaswa kutambua kuwa kadri wanavyotumia nguvu nyingi kuwadhibiti Chadema ndivyo wanavyozidisha huruma ya Watanzania kwa chama hicho.Mtu yeyote mwenye akili timamu hatoshindwa kubaini kuwa unyanyasaji unaofanywa na jeshi la polisi dhidi ya chama hicho unalenga kukipunguzia nguvu katika jitihada zake za kupambana na ufisadi unaolelewa na serikali ya Kikwete na chama chake cha CCM.

Uzoefu unaonyesha kuwa tunaweza kulilaani jeshi la polisi hata kila sekunde lakini hiyo haitopelekea jeshi hilo lililosheheni mbumbumbu wa sheria za haki za binadamu kubadili utendaji kazi wao wa ovyo ovyo.Tunahitaji kwenda mbali zaidi ya kulaumu na kulaani pekee.

Ni muhimu basi kwa Chadema kuchukua hatua za kisheria dhidi ya jeshi la polisi.Kwa vile mahakama zetu nazo zinaendeshwa kisiasa,basi pengine ni muhimu kujaribu kufungua mashtaka ya aina hiyo katika mahakama za kimataifa.

Tetesi zinadai kuwa tawi la serikali ambalo kikatiba lina jukumu la kutafsiri ya sheria (Mahakama) chini ya uongozi wa Jaji Mkuu Othman Chande linaendesha shughuli zake "kishkaji" na tawi la serikali lenye jukumu la kusimamia sheria,yaani serikali kwa maana ya Executive branch.Tetesi hizo zinapigia mstari hoja kuu mbili.Kwanza,Jaji Mkuu Othman ni kaka wa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa Othman Rashid,ambaye pia ni rafiki wa karibu wa Kikwete,kama alivyo IGP Mwema.Sasa ukiwa na kaka wawili kwenye nafasi nyeti kama hizo,na ambazo kikatiba zinapaswa kufanya kazi zake kwa kuzingatia mgawanyiko wa mamlaka (separation of powers),ni wazi kuwa nchi inaendeshwa kama kampuni ya mtu binafsi.

Kwa upande mwingine,Jaji Mkuu alikuwa miongoni mwa waalikwa kwenye semina elekezi iliyofanyika majuzi jijini Dodoma.Yayumkinika kuhisi kuwa ushiriki wa Jaji Mkuu kwenye semina hiyo kumepelekea Mahakama kumezwa na Serikali (Executive),na si aabu Mahakama ikawa inatekeleza majukumu yake kwa maelekezo ya serikali.Changanya hali hiyo na hizo teuzi za kufahamiana...!!!

All in all,ni lazima ukatili wa jeshi la polisi sio tu ulaaniwe kwa nguvu zote bali pia ukomeshwe kwa hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yake.Na kwa vile mahakama za ndani ndio hivyo tena zishakuwa kama matawi ya CCM,kuna haja ya kutafuta haki kwenye mahakama za kimataifa.

Mwisho,Kikwete na watendaji wake,na jeshi lake onevu la polisi wanaweza kuwatupa ndani viongozi wa vyama vya upinzani kadri watakavyo...kwa muda flani, lakini kamwe hali hiyo haitaendelea milele.Kama ameshindwa dikteta Hosni Mubarak ataweza Kikwete?Tawala dhalimu zinaweza kudhani kuwa ubabe na uonevu ni silaha muhimu za ustawi wake lakini ukweli ni kwamba vitendo hivyo huharakisha uchimbaji kaburi la kuzika tawala za aina hiyo.

Ni muhimu kwa kila mpenda haki na usawa kukemea kwa nguvu zote uhuni huu wenye lengo moja tu: kudhoofisha mapambano yanayoongozwa na Chadema dhidi ya ufisadi unaolelewa na serikali ya Kikwete na CCM yake.Kadhalika,kashkash dhidi ya Chadema inamsaidia Kikwete na CCM yake kupooza mvurugano unaoendelea ndani ya chama hicho ambao umesababishwa na mgongano wa kimaslahi ya kifisadi.

Enough is enough!

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.