Showing posts with label MZEE PHILEMON CHAHALI. Show all posts
Showing posts with label MZEE PHILEMON CHAHALI. Show all posts

8 Jul 2016

Ilikuwa masaa, siku, wiki, miezi na sasa mwaka. Ni vigumu sana kuamini kuwa baba umeondoka moja kwa moja. Kila siku nakumbuka, lakini kuna kitu kingine kinachonikumbusha kila wiki: makala zangu katika gazeti la Raia Mwema. Ulikuwa 'shabiki nambari wani' wa safu yangu katika gazeti hilo, na ulihakikisha unasoma kila toleo la gazeti hilo.

Pamoja na mengi uliyotuachia wanao, moja ninalofanya kila siku ni kusoma na kuandika, vitu viwili ulivyonisisitiza mno tangu nikiwa mtoto mdogo. Na kwa hakika kama ulivyopenda sana kusoma na kuandika, ndivyo ambavyo kwangu vitu hivyo vimekuwa sehemu muhimu ya maisha yangu ya kila siku.

Pia wewe na marehemu mama mlinisisitza mno kuhusu umuhimu wa elimu.Nawashukuru sana mlivyojinyima ili kuhakikisha ninatimiza ndoto zangu za kielimu. Ninasikitika kwamba wakati wewe na mama mlikuwa na kiu sana ya kuniona nahitimu shahada ya uzamifu (PhD), kwa bahati mbaya nyote mmeondoka kabla sijahitimu. Hata hivyo, nime-dedicate thesis yangu kwenye.

Nakushukuru pia wewe na marehemu mama kwa kutuhimiza mno watoto wenu kuhusu upendo, kuthamini utu na kubwa zaidi, kumtanguliza Mungu katika kila tufanyalo. Upendo wako baba ulikufilisi mapema mara baada ya kustaafu mwaka 1981, ambapo mipango yako ya kuwekeza katika kilimo ilizidiwa nguvu na moyo wako wa kuwasaidia ndugu na jamaa pale Ifakara. 

Miaka kadhaa baadae, marupurupu yako ya utumishi wako katika Jumuiya ya Afrika Mashariki nayo yaliishia kwenye kuwasaidia ndugu, jamaa na marafiki. Siku zote ulikuwa unasisitiza kuwa utu ni muhimu ziadi kuliko vitu (including pesa). 

Iliniuma mno kushindwa kuja kukuaga katika safari yako ya mwisho. Lakni nakumbuka sana maeneo yako kuwa "lolote likinitokea, hakikisha kwanza usalama wako..." Wewe baba na marehemu mama siku zote mlikuwa mnahofia kuhusu kazi niliyokuwa naifanya lakini kwa vile mlinipenda mno, mlikuwa mkiniombea kila siku ya Mungu.

Kama kuna kitu kinaniumiza mno ni mapacha Kulwa (Peter) na Doto (Paul). Kwa vile wao walizaliwa wakati umri umeshawapita mkono nyie wazazi wetu, mapacha hawa walikuwa kama wajukuu zenu. Lakini kubwa zaidi, walikuwa ndio marafiki zenu wakubwa. Kila ninapoongea nao najiskia uchungu sana kwa sababu sio tu wamepoteza wazazi lakini pia wapoteza their best friends. Ninaendelea kuwasapoti ili wasielemewe na huu uyatima tulionao.

Kama kuna kitu kimoja nilikuangusha mno ni kutofuata matakwa yako nijiunge na seminari ya Kasita baada ya kuwa mmoja wa wavulana wanne tu waliochaguliwa kujiunga na seminari hiyo. Ulitamani sana niwe padri. Hata hivyo, japo nilikuangusha, angalau mdogo wangu, Sista Maria Solana aliweza kujiunga na utawa, na yeye sasa ndio guide wetu mkuu katika sala.

Pamoja na uchungu nilionao kutokana na kifo chako baba, faraja pekee ni kuwa ninaamini muda huu upo na mkeo mpendwa, mama yetu mpendwa, marehemu Adelina Mapango a.k.a Mama Chahali. Tangu mama afariki, baba ulikuwa ukisononeka mno, kwa vile mama hakuwa mkeo tu bali pia rafiki yako mkuu. Siku zote baada ya kifo cha mama ulijisikia kuwa wewe ndo ulistahili kutangulia kabla yake kwa vile ulikuwa umemzidi umri.

Kipimo cha upendo wako baba ni kipindi kile mama alipopoteza fahamu kuanzia mwishoni mwa Januari 2008 hadi alipofariki Mei 29, 2008. Baba ulikuwa unafunga mfululizo kumwombea mama apate nafuu.Nakumbuka nilipokuja kumuuguza mama tulikushauri upunguze kufunga mfululizo hasa pale sauti yako ilipoanza kukauka na nguvu kupotea kutokana na mwili kukosa lisha na maji. Ulimpenda mno mkeo, na kwa hakika mmetachia fundisho kubwa sana.

Mwaka 2005 niliwarekodi wewe na mama, katika maadhimisho ya miaka 50 ya ndoa yenu. Bado ninayo video ile lakini nashindwa kuiangalia kwa sababu inanitia uchungu sana. Hata hivyo, kila siku ninazingatia yote mliyoniusia katika video hiyo, na ndio mwongozo wa maisha yangu.

Basi baba, nakuombea uendelee kupumzuka kwa amani na marehemu mama na mwanga wa milele uangaziwe na Bwana. Mie ninawakumbuka kwa sala kila siku kabla ya kulala. Sie tulikupenda wewe baba na mama, lakini Baba yenu wa Mbunguni aliwapenda zaidi, akawachukua. Jina lake lihimidiwe milele. AMINA



14 Jul 2015


Nitakuwa siwatendei haki kwa kusema ASANTE au SHUKRANI pekee. Kwa hakika ni vigumu sana kupata neno/ maneno sahihi yenye kuonyesha shukrani za dhati kwa wema mkubwa uliofanyiwa. Labda niseme hivi: nawaombea Mwenyezi Mungu awabariki sana kwa upendo mkubwa na sapoti kubwa kabisa mliyonipatia mie na familia ya Marehemu Mzee Philemon Chahali.

Ninyi sasa ni familia ya Mzee Chahali kwa sababu wengi wenu mlishirikia kumfanyia sala/dua ili apone lakini bahati mbaya akafariki, na mkajitokeza kwa wingi wenu kumlilia kwa salamu zenu za rambirambi lukuki. Sidhani kama kuna upendo mkubwa zaidi ya huo. 

Kitu kimoja nina hakika nacho ni kwamba japo sasa ni marehemu, Mzee Chahali ametuacha akithamini sana upendo wenu usiomithilika. Dua/sala alipokuwa anaumwa na salamu za rambirambi zitoka kwa zaidi ya watu 850 kwa ujumla wenu. Inawezekana idadi ni kubwa zaidi ya hiyo kwa sababu nilishindwa kuhesabu watu wote.

Historia fupi ya marehemu Mzee Chahali ni kama ifuatavyo, Alizaliwa Ifakara tarehe 22/11/1930 na kupata elimu yake katika zama za Ukoloni, kitu kilichomfanya athamini sana elimu kwa sie wanae. Baadaye alifunga ndoa na marehemu mama yetu Adelina Mapngo, ndoa iliyodumu hadi mama alipofariki Mei 2008, ikiwa imedumu kwa miaka 53. Katika uhai wake, baba na mama walijaaliwa kupata watoto tisa, japo mmoja alitangulia mbele ya haki na kwa sasa tumebaki wanane, wanaume sita na wanawake wawili.

Moja ya mafanikio makubwa katika maisha ya marehemu baba ni kuwa mmoja wa mapostamasta wa kwanza wazalendo baada ya uhuru. Kwangu binafsi, moja ya legacies za baba ni kunifanya nipende habari. Kwa kawaida, alipokuwa akitoka kazini alikuja na rundo la magazeti, aliyasoma kisha kutusimulia kilichomo katika magazeti hayo. Vilevile alihakikisha hakosi kusikia taarifa ya habari ya Redio Tanzania zama hizo, na vituo vya redio vya kimataifa kama vile BBC Swahili , Sauti ya Ujerumani na Voice of Amerika kila ilipowezekana. Ile tabia ya kusoma/kusikikia habari kisha kutusimulia hatimaye ilihamia kwangu ambapo kwa hakika ninashindwa kujizuwia kukutana na habari kisha nisiishirikieshe jamii aidha katika blogu hii au kwenye makala za Raia Mwema au kwenye tweet au Facebook.

Baada ya ujio wa televisheni, Mzee alikuwa akitumia muda mwingi kufuatilia habari. Na kila mara nilipompigia simu alikuwa akiniulizia kuhusu habari za kimataifa. Hofu yake kubwa ilikuwa katika maeneo mawili. Kwanza alikuwa anapata wasiwasi sana akiona kwenye TV kuhusu matishio ya ugaidi yanayozikabili nchi za Magharibi ikiwa pamoja na hapa Uingereza ninapoishi. Kingine ilikuwa ni wasiwasi wake kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kutokana na makala zangu magazetini hasa pale nilipoonekana nina msimamo mkali. Baba alipatwa na hofu kubwa aliposikia kwamba kwa wakati flani maisha yangu yalikuwa hatarini kutokana na tishio lililotoka huko nyumbani. Nilijitahidi sana kumpa matumaini lakini kwa hakika alikuwa na hofu kubwa hasa kila nilipokosa kufanya mawasiliano nae japo kwa siku chache.

Miongoni mwa vitu ninavyobaki ninasikitika kwa maana ya 'kumwangusha' marehemu baba ni, kwanza, kutotimiza lengo lake la mie kuwa padre. Nilipomaliza darasa la saba nilichaguliwa kujiunga na seminari ya Kasita huko Morogoro lakini pia nilikuwa nimefaulu kujiunga na sekondari ya serikali. Nikafuata moyo wangu, sikwenda seminari nikajiunga na sekondari ya serikali. Hilo lilimuumiza sana baba, lakini kwa bahatio nzuri alifanikiwa kumshawishi mdogo wangu wa kike na kumwingiza kwenye usista ambao anautumikia hadi leo.

Kingine ni faragha kidogo, ila kwa kifupi, ilinigharimu miaka kadhaa kabla sijamfahamisha nilikuwa ninafanya kazi gani nilipokuwa mtumishi wa umma huko Tanzania. Nilipomjulisha na kumfahamisha kwanini sikumweleza mapema, alinielewa. Lakini hapohapo nikawa nimemwanzishia hofu mpya akidhani kuwa kazi hiyo ilikuwa ya roho mkononi. Na hata aliposikia kuwa 'nimeachana na kazi hiyo,' baba alifanya sala kwenye simu kumshukuru Mungu akinieleza kuwa ilikuwa ikimyima amani rohoni.

Mzee Chahali alifariki tarehe 8/7/15 kutokana na mchanganyiko wa maradhi lakini kubwa likiwa tatizo la moyo. Hata hivyo, baada ya mkewe wa miaka 53- marehemu mama - kufariki mwaka 2008, mzee aliyekuwa na takriban miaka 10 zaidi ya mama, alishindwa kabisa kukabiliana na ukweli kuwa mkewe amemtangulia. Mara kadhaa nilipoongea nae alikuwa akimkumbuka mkewe na kutamani kuwa nae. Kimsingi, marehemu baba na marehemu mama walikuwa zaidi ya mke na mume. Walikuwa marafiki pia hasa kwa vile Mzee Chahali alikuwa mkimya sana na mwenye marafiki wachache. 

Sijui niwaelezeje kuhusu kifo hiki kilivyoniathiri binafsi. Baada ya mama kututoka, mzazi pekee tuliyebakiwa nae alikuwa baba. Sasa tumabaki yatima. Kwa hakika inauma sana.  Lakini yote ni kazi yaMungu.

Mzee Chahali amezikwa kwa heshima zote, ambapo kwa mji wetu wa kidini sana, misa ya mazishi kuendeshwa na Askofu ni heshima kubwa sana, na kwa hakika tunalishukuru sana jimbo la Mahenge kwa kumthamini Mzee wetu kiasi hicho.

Lajkini sijui kama leo hii ningekuwa katika nafasi ya kuandika makala hii bila sapoti yenu kubwa mno. Kila nilipotupa jicho Facebooka au Twitter nilikuta rundo la salamu za kumwombea dua/sala baba alipokuwa mgonjwa, na rundo kubwa zaidi baada ya kuwatangazia taarifa za msiba. Ninawashukuru sana sana sana. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awabariki mno na awazidishie upendo wenu.

Jana nilibandika Makala Maalumu ya Sauti lakini kwa kutambua kuwa si kila mmoja ana muda au access ya kuskiliza audio filela takriban dakika 30 nikaona ni bora niziwasilishe tena salamu hizi za shukrani kwa maandishi.

Ninaomba mniruhusu nisimtaje kila mmoja wenu kwa sababu sio tu mpo wengi sana bali pia ukweli kwamba shukrani za dhati huwa moyoni. Naweza kujibaraguza hapa na sante zangu nyiiingi lakini moyoni nina mawazo mengine. Ila kwa hakika Mungu ndo shahidi wangu. Ninathamini mno mchango wenu wa hali na mali katika kumuuguza baba na kushiriki katika mazishi yake kwa njia ya rambirambi.

ASANTENI SANASANA SANA. SINA MANENO SAHIHI YA KUWAAMBIA LAKINI NINAWAOMBEA BARAKA TELE KUTOKA KWA MWENYEZI MUNGU.

Mwisho, Pumziko la Milele Bwana Mungu ajmjaalie Mzee Chahali, na mwanga wa milele amwangazie apumzike kwa amni, Ameni

ASANTENI SANA

4 Jul 2015

Kwa niaba ya familia ya Mzee Philemon Chahali, ninaomba kuwashukuru nyote mnaoungana nasi kumwombea dua/sala ili apone. Hatuna cha kuwalipa bali kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awabariki kwa upendo wenu. Pia kwa vile hali ya baba bado si ya kuridhisha, tunawaomba tuendelee na dua/sala zaidi. Wanasema 'penye wengi Mungu yupo' basi ni matumaini yetu kuwa ushirikiano huu katika sala/dua utapelekea kupona kwa Mzee Chahali. Again, asanteni sana, na Mungu awabariki sana.

Tangu nipate taarifa za kuumwa kwa baba, nimepunguza kujishughulisha na 'kelele' zangu kuhusu masuala mbalimbali yanayoikabili Tanzania yetu. Sijafanya hivyo kwa maana ya kupuuzia masuala hayo bali kichwa changu kimetawaliwa na suala la afya ya baba yangu kwani ndo mzazi pekee niliyebakiwa naye baada ya kufiwa na mama mwaka 2008.

Hata hivyo, leo nimelazimika kuandika makala hii baada ya kufanya maongezi na jamaa yangu mmoja huko Tanzania ambaye katika nafasi yake kikazi, anafahamu mambo mengi yanayojiri 'nyuma ya pazia.'

Alichoniambia kimenishtua sana. Ni kuhusu kampeni zinazoendelea mtandaoni zinazomhusisha mtoto mdogo anayejiita DOGO JEMBE. Pia kampeni hizo zinatumia hashtag #IkuluSio.

Huyo jamaa yangu, pengine kutokana na majukumu yake kikazi au ufuatiliaji tu, amenionyesha ushahidi unaothibitisha kuwa kampeni hiyo inaendeshwa na mtangaza nia mmoja wa CCM. Kwahiyo tofauti na picha inayojengwa na DOGO JEMBE kuwa yupo upande wa maslahi ya Watanzania, kimsingi mtoto huyo anatumiwa tu na mwanasiasa huyo anayetaka urais. 

Kwa mujibu wa jamaa yangu huyo anayefanya kazi katika taasisi moja 'nyeti' huko nyumbani, kosa la msingi lililofanywa na waandaaji wa kampeni hiyo ni kwenye kitu kinachofahamika kama IP Address ambayo kwa lugha nyepesi ni anwani ya mlolongo wa namba zinazotenganishwa na nukta ambao unaitambua kompyuta katika mtandao. 'Mtaalam' huyo amefanikiwa kubaini kuwa posts za kampeni hiyo zinatoka kwa IP address ya mdogo wa mwania nia fulani. Amenitumia screenshots zenye uthibitisho kuhusu suala hilo.

Amenijulisha pia kuwa taasisi anayoitumikia inafahamu bayana kuhusu 'uhuni' huo, na hii unaisoma hapa kwa mara ya kwanza, usishangae ukikutana na breaking news hii katika vyombo vya habari katika siku chache zijazo. Inaelekea kuna 'wakubwa' hawajapendezwa na mbinu hiyo ya kuwahadaa Watanzania kwa kisingizio cha kumsaka Rais bora.

Kilichomkera, kinachonikera, na ambacho pengine nawe Mtanzania kitakukera ni kitendo cha mwania huyo kuwafanya Watanzania wapumbavu. Kwanini nasema hivyo? Kwanza ni 'kosa' la kumtumia mtoto mdogo kuvuta hisia za watu, kuwaaminisha kuwa lengo ni kupigania maslahi ya taifa kwa kuamsha tafakuri ya nani hasa anatufaa kuwa Rais wetu ajaye, ilhali ukweli ni kwamba kampeni hiyo ina lengo la kumpigia debe mwania nia huyo.

Kumtumia mtoto huyo mdogo kwa minajili ya kisiasa hakuna tofauti na kile kinachoitwa CHILD LABOUR, yaani kuwatumikisha watoto. Sasa hapo tu yatupasa kutambua kuwa child labour ni ukiukwaji wa haki za binadamu, na kwa minajili hiyo, mwania nia anayesaka urais kwa kukumbatia ukiukwaji wa haki za watoto/binadamu HAFAI.

Pili, hadaa, usanii, na uhuni mwingine wa kisiasa ndivyo miongoni mwa vitu vilivyotufikisha hapa. Sasa kama katika hatua hizi za awali tu za kuwania kupitishwa na chama kuwania urais mwanasiasa anaanza kukumbatia vitu kama hivyo, huhitaji kuwa mwenye uelewa mkubwa wa kisiasa kubaini kuwa mwania nia huyo hafai hata ujumbe wa nyumba kumi, achilia mbali urais.

Tatu, japo watoto wana haki ya kikatiba na kidemokrasia kuzungumzia kuhusu hatma ya taifa letu ikiwa ni pamoja na Uchaguzi Mkuu ujao, hiyo sio excuse kwa wamasiasa yeyote yule kutumia haki hiyo ya watoto kwa manufaa yake binafsi. Angekuwa jasiri, angejitokeza mwenyewe hadharani badala ya kujikampenia kwa kutumia child labour.

Kwa mujibu wa jamaa yangu huyo ambaye kwa ninavyomfahamu hana kambi yoyote hasa kwa vile majukumu yake kikazi yanamzuwia kujihusisha na siasa, kuna data nyingine ambazo zinaihusisha moja kwa moja kampeni hiyo na mwania nia huyo.

Japo nipo katika wakati mgumu kutokana na kuzorota kwa afya ya Mzee Chahali lakini afya ya Tanzania yetu ni muhimu pia kama afya ya mzazi wangu, na nimeshindwa kukaa kimya baada ya kuletewa ushahidi kuhusu 'uhuni' huu. 

Amenieleza kuwa kauli ya Dogo Jembe kuwa 'Ikulu sio ya baba yako' ilimlenga Makongoro Nyerere kwa vile yeye ni mtoto wa Nyerere, na kauli kuwa 'Ikulu sio hospitali' illimlenga Lowassa kwa vile mwania nia huyo amedaiwa kuwa afya yake sio nzuri japo haijathibitishwa. 


Lakini pengine hata bila kupata 'ufunuo' huu, ilipaswa tujiulize NANI ANAYEFADHILI KAMPENI HII YA KISASA KABISA?

Kwa mtizamo wa jamaa yangu huyo, kosa jingine la kampeni hiyo ni kwamba imejitengenezea 'ufupi wa maisha' kwa maana kwamba ipo siku Dogo Jembe atalazimika kuwashawishi tena Watanzania kuwa 'mtaka nia flani ana sifa za dogo jembe, na ndio anafaa kuwa Rais,' na hapo all hell will break loose kwa sababu kila mwenye akili timamu atabaini nani alikuwa behind kampeni hiyo.

Anyway, ningetamani kuandika kwa kirefu lakini wito wangu kwa Watanzania wenzangu ni mdogo tu: AKILI ZA KUAMBIWA, CHANGANYA NA ZA KWAKO. Tumeshwahi kuhadaiwa huko nyuma, tumeshaona matokeo ya hadaa hizo, chonde chonde, tusirejee tena makosa hayo. Kama katika kuwania tu kupitishwa na CCM, mwanasiasa yupo radhi kutumia mtoto mdogo kuwahadaa Watanzania, je akifanikiwa kuingia Ikulu itakuwaje? Ni muhimu pia kutambua kuwa mwanasiasa ambaye yupo desperate mno kuingia Ikulu lazima atakuwa na ajenda zake binafsi,

Nimalizie kwa kuwashukuru tena nyote mnaojumuika nasi kumfanyia dua/sala Mzee Chahali, na ninawashukuru sana, na kuwaombea Mungu awabariki sana. 



12 Jul 2011


Ndugu zangu wapendwa,kwa niaba ya familia ya Chahali naomba kuwasilisha shukrani za dhati kwa wote ambao kwa namna moja au nyingine mmeungana nasi kwa maombi kwa baba Mzee Philemon Chahali ambaye hali yake bado ni mahututi kufuatia ajali ya kugongwa na pikipiki huko Ifakara,Alhamisi iliyopita.

Ningetamani sana kutoa shukrani kwa kutaja jina la kila mmoja wenu lakini naomba nitoe shukrani za jumla.Nawashukuru sana bloggers wenzangu ambao licha ya kunisaidia kuweka tangazo la maombi ya sala kwa baba mmekuwa mkinitumia meseji na barua pepe za kunipa moyo pamoja na sala/dua zenu.Katika kuonyesha upendo wa hali ya juu,dada yangu blogger wa hapa UK Rachel Siwa aliweka maombi kwenye misa ya Jumapili iliyopita huko Coventry.Tunakushukuru sana dada Rachel na Mungu akubariki.Bloga mwenzangu Miss Jestina naye amekuwa akitujulia hali ya Mzee mara kadhaa kwa siku,bila kuwasahau wadogo zangu Jackie Lawrence (La Princessa) na Faith Charles Hillary (Candy1World) ,na Mtakatifu Simon Kitururu,bloga Malkiory  Matiya na Nova Kambota

Huko Twitter nimekuwa nikipata sapoti ya kutosha tangu zilipojiri habari za ajali.Dada zangu Maria Sarungi na Lilly  Melody,pamoja na wasanii wetu mahiri kabisa Hamisi Mwinjuma (Mwana FA) na Joseph Haule (Profesa Jay) ni miongoni mwa wana-Twitter wenzangu ambao wamekuwa mstari wa mbele kunifariji.

Kwa bahati mbaya,ukweli mchungu kuhusu maisha ni kwamba mpaka upate tatizo ndio unaweza kufahamu upendo wa watu wanaokuzunguka.Kuna watu nilikuwa sifahamiani nao kabisa lakini baada ya kusikia habari za ajali iliyomkumba baba wamekuwa ni nguzo muhimu kutusapoti.Kwa kweli ninawashukuru sana na Mungu awabariki sana kwa upendo wenu.Ni imani ya familia yetu kuwa sala zenu na zetu zitamsaidia Mzee Chahali sio tu kupata nafuu bali kupona kabisa.

Kwa vile inaniwia vigumu kublog kutokana na tatizo linalonikabili,naomba pia kutumia fursa hii kuwashukuru wasomaji wote wa blogu hii na watu wengineo walionipigia kura katika Tuzo la Blogu za Kitanzania (Tanzanian Blog Awards) ambapo japo sikuibuka mshindi lakini nimepata matokeo ya kupigiwa mstari.Kwa kifupi,blogu hii imeshika nafasi ya pili katika categories za Best Inspiration Blog na Best News Blogs na imeshika nafasi ya tatu katika category ya Best Political Blog.Ukiangalia kwenye hizo categories mbili za mwanzo utagundua kuwa aliyeshika nafasi ya kwanza ni bloga ambaye blogu yake imeshatembelewa na wasomaji zaidi ya milioni 12 wakati blogu hii "inasuasua" na wasomaji 424538 hadi dakika hii.Kwangu hayo ni mafanikio makubwa sana lakini si mafanikio yangu pekee bali ya wadau wote wa blogu hii.Namshukuru kila aliyenipigia kura,na japo hatukuibuka washindi wa jumla,kushiriki kwenye tuzo hizo na kukamata nafasi za juu ni tuzo kubwa sana.

Naomba nimalizie kwa kurejea tena shukrani zangu na za familia yangu kwenue nyote mnaoshirikiana nasi kwenye maombi kwa ajili ya Mzee Philemon Chahali.Ni matumaini yetu kuwa Bwana anasikiliza sala/dua zetu na atamjalia baba uponyaji kwa vile Mungu ni mwema na mwenye upendo.

ASANTENI SANA

7 Jul 2011


Nasikitika kuwafahamisha kuwa baba mzazi Mzee Philemon Chahali amepata ajali mbaya asubuhi hii huko Ifakara.Amegongwa na pikipiki ambazo ndio usafiri mkuu wa huko.Kwa mujibu wa habari nilizonazo hadi muda huu,hali yake ni mbaya,ambapo licha ya kuvnjika mguu pia ameumia kichwani.Kibaya zaidi ni kwamba umri wake ni kwenye miaka ya 80 kwa hiyo mshtuko tu wa ajli unaweza kumwathiri sana.

Basi naomba kutumia fursa hii kuomba sala zenu.Sie Wakristo tunaamini kuwa wanapojumuka wengi kufanya sala basi Mungu naye anakuwepo.Natumaini kwa sala zenu na za familia yetu Mungu atamjalia baba apone na kurejea katika hali yake ya kawaida.

Natanguliza shukrani zangu za dhati.Asanteni 

22 Nov 2009


Happy birthday to the best dad I know,

A father I love and respect,

A dad who fulfills all his duties

To teach, to guide, to protect.

If everyone had such a father,

A really good dad like mine,

The world would be so much better,

It would look like God’s own design.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.