Showing posts with label Magufuli. Show all posts
Showing posts with label Magufuli. Show all posts

29 Apr 2020


Shaka imetanda nchini Tanzania kufuatia vifo vya watu 11 mashuhuru ndani ya wiki moja yaliyopita. Muda mfupi kabla ya kuandika chapisho hili, imetangazwa kuwa Mbunge wa Sumve (CCM) Richard Ndassa amefariki.



Kifo hicho ni ni mlolongo wa vifo vya watu maarufu nchini humo ambapo Jumatano iliyopita aliyekuwa Jaji Mkuu, Agustino Ramadhan alifariki.




Kabla ya hapo, Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Ali Haji Pandu alifariki Jumanne siku moja kabla.


Jumapili usiku, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evod Mmanda alifariki,



na siku hiyo hiyo, Mkurugenzi wa zamani wa CTI, Hussein Kamote alifariki pia jijini Dar es Salaam.

Jumanne, Jaji Mstaafu Musa Kwikima alifariki, na siku moja baadaye Afisa mwandamizi wa Idara ya Uhamiaji mkoani Kagera, Pendo Buteghe alifariki.


 Siku hiyo pia ilishuhudia kifo cha wakili maarufu Gaudious Ishengoma.



Watu wengine maarufu waliofariki ni Ben Lowassa - mdogo wake Edward Lowassa, Mbunge wa zamani Abdulkarim Shah na Naibu Meya wa Morogoro Isihaka Sengo.



Kifo cha Ndassa  kinaweza kuhusishwa na tamko la hivi karibuni la Rais John Magufuli kwamba "mvuke unaponya korona," ambapo inaelezwa kuwa chumbani kwa marehemu Ndassa kulikutwa vifaa vya kujifukizia.



Taarifa kutoka kwa wananchi mbalimbali zinaeleza kuwa wamefiwa na ndugu,jamaa na marafiki zao ambao wamezikwa na mamlaka husika lakini hali hiyo haijionyeshi kwenye takwimu za serikali kuhusu idadi vifo.

Leo, baada ya siku kadhaa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza kuwa



Na haya yote yanajiri huku leo ni siku ya 33 tangu Rais Magufuli alipoondoka Dodoma na kwenda kijijini kwake Chato mnamo Machi 28 mwaka huu.

Awali leo, kiongozi mkuu wa Upinzani Bungeni na mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freemani Mbowe, aliongea masuala kadhaa kuhusiana na janga la korona huku akiitaka serikali kuchukua hatua stahili.




Pia jana, kada maarufu wa CCM, Wakili Albert Msando alijitokeza hadharani kueleza kuwa hali nchini Tanzania ni mbaya kuhusiana na ugonjwa wa korona, kauli iliyotafsiriwa kuwa ni uthibitisho wa hali halisi ilivyo japo serikali imekuwa ikificha ukweli huo.



31 Mar 2020


Huenda kuna watakaosema wakati huu ambapo nchi na dunia ipo kwenye kipindi kigumu kutokana na janga la krona, si muda mwafaka wa kutupiana lawama. Lakini vipi kama lawama hizo zinaweza kusaidia kuleta mabadiliko chanya katika jitihada za kukabiliana na janga hilo?

Kuna mfululizo wa matukio yanayoashiria bayana kuwa Rais Magufuli ana mapungufu ya kiuongozi kila wakati Tanzania yetu inapokumbwa na majanga. Tukio kubwa zaidi ni lile la tetemeko la ardhi Kagera ambapo kwanza alipuuza kutembelea wahanga kwa siku kadhaa, na alipoamua kuwatembelea, akaishia "kuwasemea ovyo" kwa kudai si yeye aliyesababisha tetemeko hilo.


Kwanini tukio hili ni kubwa zaidi? Si tu kwa vile liliathiri watu wengi lakini pia kwa sababu Magufuli anatokea eneo hilo. Kwa lugha nyingine, kama anaweza "kuwafanyia hivyo ndugu zake," kwaninia shindwe kwa "watu baki"?

Matukio mengine ambayo yalipuuzwa na Magufuli ni pamoja na maombolezo ya askari wetu waliouawa huko DRC walikokuwa wakishiriki operesheni za kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini humo. Licha ya kuwa Amiri Jeshi Mkuu, hakushiriki kuaga miili ya mashujaa wetu hao.


Janga jingine kwa taifa ambalo Magufuli alilipuuza nivifo vya wanafunzi kadhaa wa shule ya St Lucky huko Arusha

Kadhalika, Magufuli alipuuzia janga jingine lililotokea kanda ya Ziwa ambapo mamia walifariki katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere


Na akapuuzia pia janga la mlipuko wa lori la mafuta uliopolekea vifo kadhaa

Na kama alivyopuuzia janga la vifo vya mashujaa wetu waliouwa huko DRC, Magufuli hakutokea kwenye kuaga miili ya polisi waliouawa huko MKIRU, licha ya kuwa Amiri Jeshi Mkuu

Katika janga hili la korona, mwenendo wake tangu mwanzo umekuwa ni mwendelezo wa dharau zake kwa majanga yanapolikumba taifa letu. Baada ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kutangaza kuwa korona imeingia Tanzania, ilimchukua Magufuli siku 10 hivi kuongea lolote kuhusu janga hilo.

Na alipofungua mdomo wake, akaongea vitu vya ovyo kabisa. Akiwa Kanisani, aliweka kando uanasayansi wake na kudai kuwa "ukimwi unaua, malaria inaua, na ajali pia zinaua," na kusema kuwa "tunatishana sana (kuhusu korona). Haya si maneno ya kuyatarajia kutoka kwa kiongozi mkuu wa nchi ambaye pia ni mfariji mkuu.



Baadaye akahutubia taifa na kuendelea kutoa ujumbe usio na tija.



Baada ya ukimya wa siku kadhaa akaibukia tena huko Dodoma ambapo wakati taifa likiwa kwenye hofu na mashaka ya janga hilo la korona, mkuu huyo wa nchi akaonekana akifanya mzaha kwa kujilaza kwenye mawe.



Na majuzi alionekana akipuuza ushauri wa kitaalamu dhidi ya maambukizi ya korona unaowataka watu kuepuka mikusanyiko.

Na hii ilikuwa baada ya matukio makubwa mawili huko Dodoma yaliyosababisha mkusanyiko - kikao cha baraza la mawaziri na wakuu wa vyombo vya dola, na baadaye kupokea ripoti za TAKUKURU na CAG.
Image

Image

Kwa minajili ya kumbukumbu, mwaka juzi, mwanasiasa nguli wa upinzani Tundu Lissu alihoji kasumba hiyo ya Magufuli kujitenga na majanga ya kitaifa.

Huu sio tu ni mwaka wa tano tangu Magufuli aingie madarakani lakini pia ni mwaka wa uchaguzi mkuu mwingine (kama ataruhusu). Waweza kujiuliza "anapata wapi jeuri hiy ya kupuuzia majanga ya kitaifa miaka yote hii na hata mwaka huu wa uchaguzi?" Jibu ni kwamba anafahamu fika kuwa haitomgharimu chochote. Kwa upande mmoja wapinzani wetu wamekuwa watu wa maneno zaidi kuliko vitendo, ilhali wananchi nao wakiwa bize na ubuyu. Laiti Magufuli angehisi "kuna adhabu inamsubiri" asingefanya dharau hizi. 

Lakini hata kama wapinzani wameshindwa kushikia bango hilo, na wananchi wako bize na ubuyu, ni jukumu letu sie wachache wenye uthubutu wa kukosoa kutochoka kukemea maovu kama haya. Maana sote tukikaa kimyaatadhani tunaafiki kasumba hiyo isiyopendeza.

Nimalizie makala hii kwa ujumbe huu muhimu kuhusu janga la korona.



22 Mar 2020


#Thread: Awali nilipangilia kuwa thread hii iwe maalum kwa ajili ya kueleza jinsi hali ilivyo hapa Uingereza kuhusiana na janga la #Coronavirus kwa matarajio kwamba nanyi huko nyumbani au kwingineko duniani mnaweza kuwa na moja au mawili ya kujifunza. 

Hata hivyo, katika pitapita zangu kabla ya kuandika thread hii nilikutana na makala moja ndefu kuhusu jinsi janga la jorona lilivyoibuka nchini Italia na kwanini nchi hiyo imeathirika vibaya mno, na pia endapo kinachojiri nchini humo ni "template" ya yatayojiri kwingineko. 

Kwahiyo nadhani ni vema nikianza kuongelea kwa kifupi kuhusu makala hiyo, maana ina funzo kwa sie tulioko huku na kwa nyie mliopo huko. 

Kwa kifupi kabisa, moja ya sababu iliyopelekea maambukizi kuwa makubwa na ya kasi nchini Italia ni kusuasua kwa mamlaka kuchukua hatua stahili. 

Kwa mujibu wa makala hiyo, Italia ilikuwa na fursa nzuri ya kujikinga na janga hilo endapo tu kusingekuwepo dhana kwamba "korona ni sawa na mafua tu," (nikamkumbuka MwanaFA na madai yake ya "malaria ni hatari zaidi kuliko korona") na hisia kuwa "korona ni tatizo la China pekee. "

Kilichopaswa kufanywa na mamlaka za taifa hilo ni
(a) "kuyatenga" maeneo yenye maambukizi
(b) kuzuwia movements za watu kitaifa na kuhakikisha sheria kali zinatumika kuhakikisha utekelezaji
(c) mfumo wa mawasiliano usiokanganya kutoka kwa mamlaka husika kwenda kwa wananchi. 

Inaelezwa kuwa katika siku za mwanzo za mlipuko wa janga hilo, Waziri Mkuu wa Italia Conte na viongozi wengine wa ngazi zajuu walijaribu kujenga picha kuwa ugonjwa huo sio tishio kwa nchi hiyo. Walijenga imani feki kuwa mambo ni shwari #tupovizuri

Na hata maambukizi yalipozidi kukua, maelezo yaliyotolewa ni kwamba ongezeko hilo ni matokeo ya "aggressive testing" yaani jitihada kubwa za kupima watu mbalimbali bila hata kujali kama wana dalili za maambukizi. Na kulijitokeza lawama dhidi ya approach hiyo. 

Kama ambavyo sura ngumu Polepole alivyodai majuzi kuwa Tanzania ikifunga mipaka itaathiri sekta ya utalii, awali baadhi ya viongozi wa Italia ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu Conte walikuwa namtazamo kuwa hatua kali dhidi ya korona zingeathiri uchumi wa nchi hiyo. 

Lakini pengine kikubwa zaidi ni kwamba Italia iliangalia kilichokuwa kinatokea China kama "filamu ya sayansi ya kutunga (science fiction movie) ambayo haiwahusi Wataliano."

Kichekesho ni kwamba hali ilipoanza kuwa mbaya nchini Italia, nchi nyingi hasa barani Ulaya na Marekani ziliangalia kinachotokea huko kama "tatizo la Italia tu" kama ambavyo awali Italia ilivyoiangalia korona kuwa ni "tatizo la China tu."

Mtu anayedhaniwa kuwa ndio "msambazaji wa kwanza wa korona" (Patient One) ni mwanaume wa miaka 38 ambaye Februari 18 alikwenda hospitali akiwa na mafua makali lakini hakuna aliyebaini kuwa ni mwathirika wa korona. Na kibaya zaidi, mgonjwa huyo alikataa kulazwa/

Hata hivyo, siku hiyohiyo jamaa huyo alirudi tena hospitalini hapo na kulazwa kwenye wodi ya kawaida (yaani isiyo maalum kwa ajili ya wagonjwa flani). Siku mbili baadaye alizidiwa mno, akapelekwa ICU ambako vipimo vilionyesha ana maambukizi ya korona

Kabla ya kukutwa na korona, mtu huyo alizunguka sehemu mbalimbali ambapo miongoni mwa matukio muhimu ni kuhudhuria pati tatu, alikwenda kucheza futiboli na pia alishirki kwenye jogging na timu ya soka. Yote hayo yalijiri wakati mtu huyo tayari ana maambukizi ya korona

Lakini la kupigia mstari ni kwamba hakuwahi kukutana na mtu yeyote kutoka China wala kutembelea China. 

Maana yake ni kwamba mtu huyo aliambukizwa humohumo Italia, which means kabla yake tayari kulikuwa na mtu/watu wenye maambukizi ya ugonjwa huo. 

Kwa kumalizia kuhusu kilichojiri Italia, moja ya vitu vilivyochangia sana mkanganyiko katika siku za awali ni kitu wanaita "infodemic" yaani kama "pandemic ila inayohusu information."

Kwa hapa Uingereza, hali ni mbaya. Na inatarajiwa kuwa mbaya zaidi. 

Tatizo la hapa ni kama ilivyokuwa Italia, ambapo kulikuwa na kusuasasua kuchukua hatua stahili. Kwa mfano, badala ya "kufunga kila kitu" mapendekezo ya mwanzo yalikuwa kitu kinaitwa "herd immunity."

Herd immunity ni kuacha maambukizi yasambae kisha wingi wa walioambukizwa upelekee kinga ya baadaye dhidi ya wasioambukizwa. 

Matarajio ni kwamba mtu akishaambukizwa virusi vya ugonjwa husika na kupona, anakuwa na kinga ya kuzuwia kuambukizwa tena. 

Lakini wazo hilo la herd immunity lilipingwa vikali hasa baada ya kubainika kuwa lingeweza kupelekea vifo laki mbili unusu au zaidi. 

Kwahiyo serikali ya Waziri Mkuu Boris Johnson ikaja na mkakati wa "watu kujitenga" (social distancing). 

Social distancing inamaanisha hatua kama wafanyakazi kutokwenda makazini na kufanyia kazi kutoka majumbani, sambamba na watu kukwepa kukutana kusiko kwa lazima. 

Kadhalika, mkazo umewekwa kwenye kuongeza kasi ya kupima watu wenye dalili za maambukizi ya korona. 

Sambamba na hilo ni hatua kali dhidi ya mikusanyiko, na kufungashule, sehemu za starehe mabaa, na kupunguza safari za vyombo vya usafiri. Kadhalika, serikali imewekeza vya kutosha kwenye tafiti mbalimbali za kusaka kinga na tiba ya korona. 

Vilevile serikali imechukua jukumu la kulipa asilimia 80 ya mishahara ya waajiriwa ili kuwezesha waajiri kuruhusu wafanyakazi wao wasiende kazini au wafanye kazi kutokea nyumbani. Ikumbukwe pia kuwa hapa watu wasio na kazi hulipwa posho ya kujikimu na ya makazi. 

Inatarajiwa kuwa wiki 12 zijazo zitakuwa ngumu sana kwa nchi hii kwa sababu ndio kipindi ambapo jitihada kubwa zinafanyika kuzuwia maambukizi mapya sambamba na kuzuwia kusambaa kwa maambukizi yaliyopo huku ikitarajiwa kuwa mamilioni ya watu wataweza kujipima wenyewe majumbani. 

Tayari makampuni mbalimbali yamesitisha uzalishaji wa bidhaa zao na kuelekeza nguvu kwenye uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazohitajika katika kipindi hiki cha janga la korona hapa Uingereza. Lakini ni ngumu kubaishiri kuwa hatua hizo zinazochukuliwa muda huu zitafanikiwa kukabili janga hilo.

Kwa upande mmoja, ugonjwa huo ni mpya na upya huo unapelekea ugumu wa kuuelewa vizuri. Kwa mfano hakuna uhakika wa kutosha kuwa mtu akipona hatoambukizwa tena. 

Kuhusu huko nyumbani, kwa kweli mie binafsi nina wasiwasi mkubwa. Kwa upande mmoja, licha ya majigambo ya watawala wetu, sie ni masikini wa kutupa. Hatuna uwezo wa lolote bila kutegemea wafadhili. Kibaya ni kwamba wafadhili wetu nao wapo vitani dhidi ya korona. 

Lakini pengine adui mbaya zaidi kwetu ni kasumbailiyoota mizizi ya kufanya kila jambo kuwa ni la kisiasa. Majuzi mmemsikia sura ngumu Polepole akiufananisha ugonjwa wa korona na wapinzani. Na akajigamba kuwa kama wanavyomudu kupambana na wapinzani basi wataimudu korona pia. 

Wakati ambapo taifa linapaswa kuwa kitu kimoja, hawa wahuni wanaleta mzaha wa siasa. Lakini korona hii si ya kuchezewa maana haibagui kati ya huyu wa chama tawala na huyu mpinzani wala kiongozi na raia wa kawaida. 

Pia tuna tatizo la "infodemic."Pandemic ya information. Kwa upande mmoja ni jitihada za akina Bashite kutumia watu kuhadaa kuwa hali ni shwari, kosa ambalo kama umefuatilia vema thread hii linaigharimu Italia na hata Uingereza na Marekani. 

Lakini pengine baya zaidi ni taarifa ninazopokea kila siku kuwa sehemu kadhaa wananchi wamepigwa marufuku "kuongelea korona," ikiwa ni pamoja na watumishi wa sekta ya afya kutishwa kwamba wakiripoti matukio ya korona kwenye hospitali zao wataadhibiwa. 

Mwisho, tuna Bwana @MagufuliJP ambaye hadi leo sijui siku ya ngapi hajaona umuhimu wa kujitokeza hadharani kuongea na Watanzania. Hizi sio dharau tu bali ni kukosa utu. Lakini hali hiyo imeshazoeleka sasa. Kila linapotokea janga anaingia mitini. 

Hata hivyo, tunashukuru tumefanikiwa kupata uongozi mbadala wa Mheshimiwa @zittokabwe ambaye juzi alihutubia taifa kuhusu janga la korona, hotuba bora kabisa yenye taarifa za kutosha na iliyojaa upendo kwa Watanzania. Icheki hapa (youtu.be/Jc7ZD3PDrXc)

Nimalizie kwa kuwasihi nyote mchukue tahadhari dhidi ya janga hili. Pia ni muhimu kukazania sala/dua. Pia tufahamishane taarifa mbalimbali hususan zinazofichwa kwa minajili ya kisiasa au zozote zile zitakazoisaidia jamii kukabiliana na korona.

Be safe. Jumapili njema

UPDATE: Hatimaye Rais Magufuli amehutubia Taifa japo baadhi ya kauli zake zinaweza kuwa kukwaza jitihada za mapambano dhidi ya #coronavirus. Pichani ni baadhi ya kauli hizo





19 Mar 2020

Ili uielewe vema makala hii ni vema ufanye kulinganisha kinachojiri Tanzania muda huu baada ya kutangazwa kuingia kwa Coronavirus na kinachojiri katika nchi jirani ambazo pia zimekumbwa na janga hilo la kimataifa.

Tuanze na Kenya. Mara baada ya kuthibitika kuwa taifa hilo lina mgonjwa mmoja aliyeambukizwa maradhi hayo, Rais Uhuru Kenyatta aliongea na Wakenya ambapo pamoja na mambo mengine aliwahakikishia kuwa serikali yake ipo nao bega kwa bega katika kipindi hiki kigumu.
Twende Afrika Kusini. Mara baada ya kufahamika kuwa nchi hiyo imekumbwa na Coronavirus, Rais Cecil Ramaphosa aliwapatia Waafrika Kusini taarifa hiyo huku akitanabaisha kuwa hakuna sababu yakuona aibu wala kuficha taarifa hiyo kwa sababu ugonjwa huo umezikumba nchi nyingine pia.
Kwa majirani zetu wa Rwanda, Rais Paul Kagame alikwenda hatua kadhaa mbele kwa kujipanga vilivyo dhidi ya Coronavirus kabla haijaingia nchini humu ambapo licha ya kuweka sehemu za kuosha mikono katika maeneo mbalimbali,
Rais Kagame alimtimua Waziri wake wa Elimu kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu vifaa kwa ajili ya Coronavirus.
Na baada ya nchi hiyo kukumbwa na janga hilo, Rais huyo aliongea na Wanyarwanda na kuwataka wachukue hatua za tahadhari badala ya kuwa na hofu tu.
Na kwa majirani zetu wa DRC, Rais Felix Tshisekedi alihutubia taifa na kueleza mikakati mbalimbali ya serikaliyake katika kupambana na janga hilo la Coronavirus.
Nchini Ethiopia, Waziri Mkuu Ahmed Abiy amekwenda mbali zaidi ya kuwajali Waethiopia wenzie na amefanikiwa kupata sapoti ya mmoja wa matajiri wakubwa duniani Jack Ma, kutoa sapoti kwa mataifa mengine ya Afrika kupambana na janga la Coronavirus.

Na huko Uganda, licha ya nchi hiyo kutokuwa na maambukizi yoyote ya Coronavirus, Rais Yoweri Museveni amehutubia taifa na kutangaza hatua kadhaaza kujikinga dhidi ya janga hilo
Sasa turudi Tanzania kwetu. Mara ya mwisho kwa Rais Magufuli kusikika na kuonekana hadharani ni majuzi ambapo sio tu alidai kuwa Coronavirus haijaingia nchini Tanzania (japo masaa machache baadaye Waziri wake, Ummy Mwalimu alitangaza kuwa in fact tayari Tanzania ina mgonjwa mmoja mwenye maradhi hayo) bali pia hakutangaza hatua zozote za msingi kukabiliana na ujio wa janga hilo. Na kama mzaha vile, alikiri kuwa alikosea kusababisha mkusanyiko wa watu kusikiliza hotuba yake.

Lakini siku hiyohiyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt Abbasi aliongea upuuzi mkubwa dhidi ya Watanzania walioonyesha hofu kuhusu janga la Coronavirus.
Masaa machache baadaye, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akatangaza kuwa Tanzania ina mgonjwa mmoja wa Coronavirus.
Na Waziri Ummy amegeuka simulizi baadaya kupatikana video hii ambapo anatanabaisha kuwa Tanzania haiwezi kukabiliana na Coronavirus.
Tangu tutangaziwe uwepo wa ugonjwa huo hatujamsikia tena Magufuli. Sijui amejificha wapi. Na kama ilivyozoeleka katika nyakati za majanga, "ghafla" Waziri Mkuu Kassim Majaliwa "amekuwa Waziri Mkuu tena"
 ambapo ndio amekuwa "sauti ya serikali" kuhusu hatua mbalimbali dhidi ya janga hilo, ikiwa ni pamoja na hatua ya kufunga shule za awali, msingi na sekondari na vyuo.

Lakini uzeofu unaonyesha kuwa kila inapotokea Tanzania kukumbwa na janga fulani, Magufuli hukwepa dhamana aliyonayo kama "comforter-in-chief," yaani "mfariji mkuu wa taifa." Uthibiisho kuhusu hilo upo kwenye matukio mengi lakini pengine tukio lililoacha kumbukumbu ya muda mrefu kwa Watanzania ni dharau alizowafanyia wahanga wa tetemeko la ardhi huko Kanda ya Ziwa.

Licha ya yeye kuwa mzaliwa wa eneo hilo, alikaa muda mrefu bila kwenda kuwapa pole wahanga wa tetemeko hilo, na alipokwenda "akawasemea ovyo."

Huu si wakati wa kulaumiana lakini pia huu si wakati wa kuzembea. Ni kwa minajili hiyo nimekuwa nikitoa wito kwa viongozi wakuu wa Upinzani, Mheshimiwa  Zitto Kabwe, Mheshimiwa Freeman Mbowe na Mheshimiwa Maalim Seif kutoa ninachokiita "uongozi mbadala wakati huu ambapo Tanzania inakabiliwa na janga kubwa la Coronavirus.
Na endapo Magufuli hatobadilika, kwa maana ya "kuendelea kujificha," basi Watanzania watakuwa na kila sababu ya kutomhitaji tena kwenye uchaguzi mkuu ujao hapo Oktoba mwaka huu

Nimalizie makala hii kwa kukumbushia umuhimu wa kuchukua hatua binafsi dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huu hatari wa Coronavirus. Nimekutengenezea video hii fupi

 Mungu atulinde sote. Amen.

11 Mar 2020


Kusema hukumu nzito dhidi ya viongozi kadhaa wa Chadema iliyotolewa jana kuwa ni ishara mbaya kwa demokrasia nchini Tanzania ni kutoitendea haki hali ya demokrasia katika nchi yetu. Kilichotokea jana hakipaswi kuangaliwa kama tukio pekee bali mwendelezo wa matukio lukuki yaliyojiri tangu Rais Magufuli aingie madarakani takriban miaka mitano iliyopita.


Sidhani kama kuna haja ya kueleza kwanini hukumu hiyo ni ya uonevu uliopindukia kwani takriban kila mtu aliyekuwa anafuatilia mwenendo wa kesi hiyo anaelewa kuhusu hilo. Lakini pia, takriban kila anayefuatilia mwenendo wa Magufuli na demokrasia Tanzania anaelewa hali ikoje kwa sasa.



Kwahiyo, badala ya kutumia muda mwingi kulalamika ni vema kujaribu kutafuta suluhisho japo la muda mfupi kuhusu hali hiyo. Kwa bahati mbaya, uzoefu wangu binafsi kuhusu kuwashauri ndugu zangu wa Chadema haujawahi kuwa mzuri. Kila inapotokea aidha kuwashauri au kuwakosoa, huwa wakali kama pilipili huku wengine wakitumia lugha isiyofaa.



Yayumkinika kuhitimisha kuwa tofauti pekee kati ya Chadema na CCM when it comes to kuwakosoa, ni kwamba CCM ipo madarakani na Chadema wapo upinzani, lakini tabia zao wanapokosolewa ni sawa: hawataki kusikia ushauri wowote tofauti na mtazamo wao hata kama ni fyongo.



Ni muhimu kutambua kuwa unyanyaswaji unaofanywa na Magufuli kwa Chadema hakuanza jana. Tangu kiongozi huyo aingie madarakani hajawahi kuficha chuki yake dhidi ya Chadema. Na anayedhani kuwa kuna siku hali itabadilika, kwamba ghafla chuki hiyo itageuka upendo, basi kichwani hayupo vema.



Ndio maana baadhi yetu tulimshutumu vikali mwenyekiti wa taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, alipomwomba Magufuli kuwe na MARIDHIANO. Lakini kama ilivyo kawaida ya wafuasi wa chama hicho, sio tu walimtetea Mbowe bali pia waliturukia kama mwewe sie tulioona mkakati huo ni fyongo.



It is this simple, huwezi kutaka maridhiano na mtesi wako. It simply doesn't work. Unawezaje kutaka maridhiano na mtu ambaye utawala wake umetawaliwa na matukio mabaya kabisa kuhusiana na wanasiasa na wanachama kadhaa wa Chadema?



Unasakaje maridhiano na Magufuli ilhali siku chache tu baada ya kuingia madarakani Kamanda Mawazo aliuawa kinyama?

Unatakaje maridhiano na Magufuli ambaye muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani aliharamisha shughuli halali kikatiba za vyama vya upinzani ikiwa ni pamoja na Chadema?


Unatakaje maridhiano na Magufuli ambaye alimfunga mbunge Joseph Mbilinyi aka Sugu kwa "kosa feki"?

Image result for sugu afungwa

Unatakaje maridhiano na Magufuli ambaye utawala wake unapaswa kuwaeleza Watanzania alipo kada maarufu na mkosoaji mkubwa wa Magufuli, Ben Saanane?

Image result for bring back ben saanane
Unatakaje maridhiano na Magufuli ambaye utawala wake una damu za Diwani Luena na Katibu Kata Daniel?




Orodha ni ndefu lakini so far response ya Chadema imekuwa ya kusuasua




Na kibaya zaidi, baadhi ya tuonaguswa na madhila yanayowasibu tukijitolea kuwashauri twaishia kutukanwa.



Ni hivi, ili Magufuli alazimike kubadilika, ni lazima kuwa na "incentive" ya kumfanya abadilike. Naamini mmeona jinsi "shinikizo la mabeberu" lilivyomlazimisha amwachie huru mwandishi Eric Kabendera, aitishe mkutano wa kizushi na Maalim Seif, Mbatia na Lipumba, na amemtuma "Profesa aliyeokotwa jalalani" Kabudi aende kuomba suluhu huko Marekani. 



Pia sote ni mashuhuda wa jitihada binafsi za kiongozi mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo kuishinikiza benki ya dunia isitoe mkopo kwa Tanzania zilivyozaa matunda. Chadema kama chama kikuu cha upinzani ilishindwa kuwa mstari wa mbele katika hili.



Na hadi wakati huu hakujawa na mwamko wa kitaifa kwa chama hicho kushinikiza mabadiliko katika mwenendo wa siasa za Tanzania. Na kichekesho ni kwamba ajenda kuu ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ilikuwa MABADILIKO. Je ajenda hiyo ilikufa baada ya Lowassa kushindwa uchaguzi huo na hatimaye kukikimbia chama hicho?



Pengine hadi kufikia hapa, msomaji ambaye ni kada wa Chadema utakuwa umefura kwa hasira ukilaumu kuwa sionyeshi huruma kwa yanayokisibu chama hicho na viongozi wake. Nawaonea huruma sana lakini ni nadra kwa hisia pekee kuleta mabadiliko. Huruma kwa akina Mbowe na wanasiasa wengine wanaoteswa na Magufuli haiwezi kumfanya dikteta huyo abadilike.



Ieleweke kuwa chuki ya Magufuli kwa Chadema inatokana na ukweli kwamba chama hicho ndicho cha pili kwa ukubwa baada ya CCM na kina mtandao mpana wa nchi nzima, na licha ya kuwa chama kikuu cha upinzani, pia ni potential mbadala wa CCM. Kwahiyo, kwa Magufuli ambaye anajua fika kuwa akirogwa tu kutoka madarakani ataishia jela, ni lazima kwake kuibana Chadema kwa nguvu zake zote. Huyu si mtu wa kutaka maridhiano nae hata chembe.



Kwa vile lawama pekee hazijengi, nihitimishe makala hii kwa kuikumbusha tena Chadema kuwa dhamira kuu ya Magufuli ni kuhakikisha chama hicho kinakufa. Najua kuna wanaosema "hawezi kukiua chama hiki" lakini ukweli ni kwamba kifo cha chama cha siasa sio lazima kiwe kama kifo cha binadamu. Endapo dhamira ya Magufuli kuwa katika uchaguzi mkuu ujao Chadema isiambulie jimbo na kata hata moja itatimia, huo ni mwanzo wa kifo cha chama hicho. 



Simaanishi kuwa kitakufa kwa maana ya kutokuwa na mwanachama hata mmoja bali kitabaki "chama kama chama" kama ilivyo CUF ya Lipumba au TLP ya Mrema au NCCR ya Mbatia. Uwepo au kutokuwepo kwa vyama hivyo hakuna maana kwa Watanzania.



Lakini ukiwakumbusha Chadema kwa mifano hai kuwa Magufuli amedhamiria kwa dhati kukiangamiza chama chao, sana sana utaishia kuambulia matusi. 



Nini kifanyike? Kwa bahati mbaya imebaki mezi saba tu kabla ya uchaguzi mkuu ujao hapo Oktoba. Kwa maana hiyo, hakuna muda wa kutosha kwa chama hicho kuanzisha programu kabambe ya kupambana na udikteta wa Magufuli.



However, uchaguzi huo unaweza kutoa fursa ya "kuua ndege wawili kwa jiwe moja," - kutekeleza programu kabambe ya kukomesha udikteta wa Magufuli kama mkakati kabambe wa chama hicho kuingia Ikulu. Kwamba, kama ajenda fyongo ya MABADILIKO (ya Lowassa) ya mwaka 2015, safari hii ajenda iwe kukomesha udikteta wa Magufuli na hatimaye kumng'oa hapo Oktoba.



Lakini ili hilo liwezekane ni muhimu kwa chama hicho kuachana kabisa na mtazamo fyongo miongoni mwa viongozi wengi wa ngazi za juu wa chama hicho na makada mbalimbali kuwa "adui yao mwingine zaidi ya  Magufuli na CCM ni Zitto na ACT-Wazalendo." Kuna wahuni kwenye chama hicho kama "jasusi Yeriko" ambao wamekuwa wakijibidiisha kujenga chuki dhidi ya Zitto na ACT-Wazalendo kwa ujumla pasipo viongozi wa Chadema kukemea upuuzi huo. 



Japo muda ni mchache kabla ya uchaguzi mkuu ujao, lakini ushirikiano wa dhati kati ya Chadema na ACT-Wazalendo - na pengine makundi mengine ya kijamii (rejea wazo la Zitto kuhusu "united front") - pamoja na shinikizo kwa mabeberu ambao fedha zao ndio zinampa jeuri Magufuli, unaweza kabisa kumwondoa madarakani huyo dikteta kwa njia za amani. Uzuri ni kwamba mabeberu wanafuatilia kwa karibu kila kinachojiri Tanzania


Mwisho, japo ninawapa pole viongozi wa Chadema kwa madhila wanayopitia, wanachohitaji zaidi sio huruma yetu bali ujasiri wa kupambana na huyo dikteta kwa kila njia inayowezekana. Na japo sidhauri matumizi ya nguvu katika kudai haki, busara hii ya marehemu Profesa Kighoma Ali Malima bado ina relevance kubwa kwa wanasiasa wa upinzani ikiwa ni pamoja na Chadema.


4 Mar 2020



Kuna njia mbalimbali za kufanya uchambuzi wa kiintelijensia, njia zinazotegemea vigezo mbalimbali, kigezo muhimu zaidi kikiwa tukio husika na/au "key players" (kwenye ushushushu tunawaita "subjects") katika tukio hilo.

Katika kufanya uchambuzi wa kiintelijensia kuhusu tukio la jana ambapo Rais Magufuli alikutana na viongozi wakuu watatu wa upinzani, Maalim Seif Sharif Hamad wa ACT-Wazalendo, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, na Ibrahim Lipumba wa CUF, nitatumia kanuni ijulikanayo kama 'Linchpin,' ambayo ni mwafaka zaidi pale ambapo "ukweli mzima" upo bayana (au "vipande vya ukweli).



Kanuni hii ya Linchpin ilibuniwa na Naibu Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), Douglas MacEachin, na inahusu "matukio ya ghafla/ya kushangaza," ambapo aliitumia kanuni hiyo kueleza tukio la ghafla na Iraki kuivamia Kuwait mwaka 1990. 

Katika kanuni hii, uchambuzi wa kiintelijensia unatathmini tukio/matukio husika kwa kuzingatia "ukweli uliopo/unaofahamika," kitu tofauti kidogo na mbinu nyingine za uchambuzi wa kiintelijensia zinazoanza na hisia au dhana (kama ile ya ACH -Dhana Zinazoshindana -nilioutumia majuzi kuchambua tukio la Membe kufukuzwa uanachama wa CCM)

Kwa vile lengo la makala hii sio kutoa darasa la "mbinu za uchambuzi wa kiintelijensia," bali kutumia kanuni ya Linchpin kueleza "tukio la ghafla," la Jiwe kukutana na Maalim Seif, Mbatia na Lipumba, ni vema nikahamia kwenye uchambuzi husika.

Kwa kutumia kanuni hiyo, kuna "ukweli " (facts) kadhaa ambao ni msingi wa uchambuzi huu. Ukweli mkubwa zaidi ni kitu nilichokiongea wiki iliyopita baada ya mwandishi Erick Kabendera kuachiwa baada ya kuwekwa jela kwa uonevu kwa zaidi ya miezi sita.



Awali nilieleza kuhusu hilo la "Jiwe kukaliwa kooni na mabeberu" katika chapisho langu hili


Kwahiyo ukweli mmoja - na muhimu zaidi - uliopelekea "tukio hilo la ghafla" ni shinikizo la mabeberu. Shinikizo ambalo wiki iliyopita lilipelekea mwandishi Kabendera kuachiwa, na wiki hii limepelekea Jiwe kukutana na viongozi hao watatu wa upinzani.

Nimetanabaisha kuwa huo ni "ukweli muhimu zaidi" kwa sababu kuna ukweli mwingine japo sio wenye uzito sana. 

Uamuzi wa Jiwe kukutana na akina Maalim Seif jana ni sawa na "kuua ndege wawili kwa JIWE moja." Kwa upande mmoja amefanikiwa kutuliza shinikizo la mabeberu ambao wameweka bayana msimamo wao kuwa wanaweza kutochangia bajeti ijayo endapo ukandamizwaji wa demokrasia na haki za binadamu utaendelea. Amewatuliza mabeberu kwa kuwaonyesha kuwa "demokrasia ipo" na ndio maana ameweza kukutana na sio kiongozi mmoja tu wa upinzani bali watatu kwa mkupuo.

Nimesema "ameua ndege wawili kwa jiwe moja." Na "ndege" wa pili ni Membe. Mkutano wake huo na akina Maalim Seif unafikisha salamu muhimu kwa Membe aliyefukuzwa uanachama wa CCM wiki iliyopita, kwamba "hao unaotaka kujiunga nao ndo hawa niko nao hapa Ikulu kwangu."

Kama nilivyoeleza katika uchambuzi kuhusu tukio hilo la Membe kufukuzwa uanachama wa CCM, kuna uwezekano mkubwa wa mwanasiasa huyo kujiunga na ACT-Wazalendo. Na kwa vilekufukuzwa kwake CCM ni matokeo ya uoga wa Jiwe kuhusu upinzani kwenye nafasi ya urais, Membe "kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo" ni worst nightmare kwa Jiwe. 

Naomba nirudie kusisitiza kuwa uoga huo wa Jiwe hauna msingi kwa sababu Membe hana uwezo wa kumwangusha Jiwe kwa sababu nilizowahi kutanabaisha katika makala hii.



Kwahiyo Jiwe akiweza kumzuwia Membe kisaikolojia asiwaamini Wapinzani itakuwa ni nafuu kubwa kwake na uoga wake.

Ukweli mwingine kuhusu mkutano huo kati ya Jiwe na viongozi hao wa upinzani ni "busara ya kisiasa" inayosema "kuwa karibu na marafiki zako, lakini kuwa karibu zaidi na maadui zako."

Ukweli mchungu kuhusu wanasiasa wetu - wa CCM na hao wa upinzani - ni huu: wote wapo katika "tabaka tawala" (ruling class). Hapana, simaanishi kuwa akina Seif, Mbatia na Lipumba ni sehemu ya utawala wa Jiwe bali ukiangalia kwa undani wasifu wa viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, unaweza kubaini kuwa "wote ni wale wale."

Na ukiangalia wasifu wa Maalim Seif, Mbatia na Lipumba hutoshindwa kubaini kuwa ni watu ambao tumekuwa tukiwasikia "miaka nenda miaka rudi" lakini "wakiwa upande wa pili," kwa maana "sio upande wetu" watu wa tabaka la chini. Kwa kuazima neno la mtaani, hawa ni "vigogo."

Ukweli mwingine ni kwamba mkutano huo wa Jiwe na akina Maalim Seif "ndio siasa ilivyo." Kuna kitu kwenye siasa kinaitwa "realpolitik" ambacho kwa tafsiri isiyo rasmi ni "siasa ilivyo kimatendo kuliko kinadharia/kiitikadi." 

Sasa kwenye "siasa halisi" iwe ya kitaifa au ya kimataifa, "hakuna marafiki au maadui wa kudumu bali maslahi tu." Na ndio maana licha ya msimamo wake msimamo wake mkali dhidi ya vikundi vya kigaidi, na kauli maarufu kuwa "we don't negotiate with terrorists," majuzi Marekani ilifikia makubaliano na kundi la kigaidi la Taliban.

Na jana ilifahamika kuwa Rais wa nchi hiyo Donald Trump aliwapigia simu viongozi wa kundi hilo, kitu ambacho kabla ya tukio hilo kilikuwa sio rahisi kukifikiria.



Baada ya kuangalia "ukweli"(facts) huo unaojenga msingi wa uchambuzi huu, kanuni ya Linchpin inawezesha kujenga picha ya matarajio yanayohusiana na tukio/watu husika. Hapa ninamaanisha kuwa hadi kufikia hapa, yawezekana kueleza nini kinaweza kujirihivi karibuni au huko mbeleni.

Moja ni hiyo sintofahamu inayoweza kumkumba Membe baada ya kumuona Maalim Seif akiwa Ikulu na Jiwe. Ikumbukwe tu Lowassa alipoonekana Ikulu bila kutarajiwa "waumini"wake walimtetea na kuamini porojo zake kuwa kaambiwa arudi CCM lakini amegoma. Baadaye ukweli ukadhihirika baada ya Waziri Mkuu huyo wa zamani kurejea CCM.

Simaanishi kuwa Maalim Seif atakubali kurudi CCM. La hasha. Kinachoweza kutokea ni Jiwe kujaribu tena "kuua ndege wawili kwa JIWE moja." Anaweza kumfarakanisha Maalim Seif na Zitto na hapohapo kupunguza tishio kubwa kwake kutoka kwa Zitto kama Zitto, na Zitto akiwa na Maalim Seif.

Ikumbukwe tu kuwa japo Lowassa alikuwa kama 'mungu-mtu' huko Chadema, kitendo chake cha kuonekana Ikulu na Jiwe kiliwafanya hata baadhi ya "waumini" wake waanze kuwa na hofu nae.

Sina uhakika hali ikoje huko ACT-Wazalendo baada ya Maalim Seif kukutana na Jiwe, lakini ni siri ya wazi kuwa Jiwe na Zitto "picha haziivi," na wala sio jambo la kushangaza kuona Zitto hakualikwa kwenye mkutano huo.Na wala  sina hakika kama angekubali mwaliko wa Jiwe.

Kuhusu Mbatia na Lipumba, hakuna haja ya kupoteza muda kuwajadili maana "wapo kama hawapo." 

Moja ya maswali muhimu kuhusu Malim Seif kwenda Ikulu kukutana na Jiwe ni je alipata ridhaa ya Zitto na chama kwa ujumla? Na je tukio hili linaweza kuzua mpasuko huko ACT-Wazalendo? Pengine kukusaidia kuelewa vema "siasa za ACT-Wazalendo," pitia uchambuzi wangu huu nilioufanya mara baada ya Maalim Seif kujiunga ACT-Wazalendo.

Huhitaji kuwa na uelewa mkubwa wa siasa za Tanzania yetu kubaini kuwa mnufaika mkubwa wa mkutano huo kati ya Jiwe na viongozi hao watatu wa upinzani ni Jiwe mwenyewe. 

Hilo lipo wazi. Lisilo wazi ni "yanayoweza kujiri" kutokana na mkutano huo. Je Maalim Seif anaweza kuangaliwa kama "msaliti" kwa kukubali "kukutana na dikteta ambaye majuzi tu akiwa Zanzibar alikuwa anamwaga sumu kwa Dkt Shein kuhusu jinsi ya kumdhibiti Maalim Seif?"

Kwa upande mwingine, kama kweli Jiwe alikuwa na nia njema ya kukutana na viongozi wa upinzani basi pengine wa kwanza kabisa kupewa kipaumbele cha kukutana nae angekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ambaye majuzi tu alimuomba Jiwe kuwe na MARIDHIANO. Lakini ni vema "kuweka akiba ya maneno" kwani haitokuwa jambo la kushangaza tukimuona Mbowe Ikulu kama alivyoongozana na timu yake Mwanza kwenye sherehe za Uhuru Desemba 9 mwaka jana. 

Nihitimishe uchambuzi huu kwa kutahadharisha kuwa intelijensia sio sayansi timilifu (intelligence is not exact science) licha ya uchambuzi huu kuongozwa na kanuni ya Linchpin ambayo ina ufanisi mkubwa penye uwepo wa ukweli kuhusu tukio/mtu husika.


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.