Showing posts with label Malkia Elizabeth. Show all posts
Showing posts with label Malkia Elizabeth. Show all posts

6 Jun 2012


Flypast: The Duchess of Cornwall, the Prince of Wales, the Queen, the Duke and Duchess of Cambridge and Prince Harry watch the aerial action

Ndani ya tofauti zao bao Waingereza wamtukuza Malkia Elizabeth wa Pili


Tangu Ijumaa iliyopita, Uingereza imekuwa katika shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya utawala wa Malkia Elizabeth wa Pili. Sherehe hizo za siku tano mfululizo zinaweza kusaidia sana kuonyesha ni jinsi gani kiongozi huyo wa heshima wa taifa hili anavyowaunganisha Waingereza, licha ya tofauti zao za hapa na pale.

Kama nilivyoeleza katika makala yangu ya toleo lililopita, ‘muungano’ unaounda nchi iitwayo The United  Kingdom of Great Britain (England, Uskochi na Wales) and Northern Ireland unakabiliwa na upinzani unaoweza kutishia uhai wake huko mbeleni. Pia nilieleza jinsi ‘chama tawala’ hapa Uskochi, SNP, chini ya uongozi wa Waziri wa Kwanza (mithili ya Waziri Mkuu), Alex Salmond, kilivyoanza mchakato wa kuhamasisha kura ya ‘ndiyo’ kwenye referendum ya kuamua kama Uskochi ijitenge na Uingereza.

Japo sherehe hizo za miaka 60 ya utawala wa Malkia Elizabeth hazijapata msismko mkubwa sana kwa huku Uskochi lakini ukweli unabaki wazi kuwa Malkia huyo anabaki kuwa kiungo muhimu kwa nchi hii. Na pengine sherehe hizo zinaweza kutoa picha nzuri kwa Salmond na chama chake kuhusu ugumu unaowakabili katika azma yako ya kuifanya Uskochi iwe ‘nchi huru.’

Kwa sie wageni katika nchi hii, sherehe hizo na jinsi zilivyoonekana kuwa na umuhimu wa kipekee kwa Waingereza wengi kunatupa fundisho moja la msingi: uwepo wa mtu au itikadi inayolifanya taifa lishikamane.

Kwa huko nyumbani tulibahatika kuwa na Baba wa Taifa, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere ambaye licha ya kuwa muumini mkubwa wa umoja na mshikamano, pia alifanya jitihada kubwa ya kueneza imani hiyo ndani na nje ya Tanzania, hususan kusini mwa Bara la Afrika.

Kwa mujibu wa mila zetu za Kiafrika si vema kumlaumu marehemu. Kwa msingi huo kuna ugumu wa kutosha katika kuzungumzia mapungufu au makosa ya Mwalimu. Lakini kwa vile Mwalimu aliipenda Tanzania, angetamani kuona jitihada zake zikienziwa kwa namna moja au nyingi, basi ninaamini hata angekuwa hai asingechukia kumjadili kwa minajili ya ustawi wa taifa letu.

Moja ya mapungufu machache aliyofanya Baba wa Taifa ilikuwa kutomwandaa mrithi wake wakati wa utawala wake na hata baada ya kung’atuka. Ni vigumu kuwa na sababu sahihi ya kwanini Nyerere hakutaka au hakuona umuhimu wa kuandaa mrithi wake lakini moja ya sababu za kufikirika inaweza kuwa labda hakuona mwanasiasa mwenye sifa stahili za kukabidhiwa jukumu hilo.

Inawezekana pia kuwa labda kwa vile Mwalimu hakupenda ubaguzi wa aina yoyote ile basi huenda ingekuwa vema kutoandaa mrithi bali mwenendo wa kisiasa upewe fursa ya kutoa viongozi wanaostahili.

Kwa bahati mbaya (au makusudi?) mengi ya mazuri aliyofanya Nyerere yalianza kuhujumiwa muda mfupi tu baada ya yeye kuondoka madarakani. Kubwa zaidi lilikuwa kile kinachoitwa Azimio la Zanzibar ambalo inaelezwa kwamba lilisimamiwa na mtangulizi wa Baba wa Taifa, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.

Wakitumia ‘upole’ wa Mwinyi, baadhi ya wanasiasa waliokuwa wakisubiri kwa hamu Nyerere aachie ngazi katika uongozi wa serikali na chama walishinikiza Azimio hilo la siri (hadi sasa sijawahi kuona chapisho rasmi la CCM kuhusu Azimio hilo) na kuua Azimio la Arusha. Kwa lugha nyingine, Azimio hilo lilivunja itikadi ya Ujamaa  iliyowezesha umoja na mshikamano wa Watanzania .

Pengine Nyerere angeweza kupambana na ‘uhuni’ huo lakini nadhani aliamua kutumia busara kutopingana na wana-CCM wenzie hasa ikizingatiwa kuwa kufanya hivyo kungeweza kuzua hisia kwamba ana tamaa ya madaraka na anaingilia kazi za marais waliomtangulia.

Kwa hilo ninaweza kumlaumu tena Mwalimu kwa sababu katika mazingira ya kawaida tu huwezi kumwachia mtu abomoe kitu ulichotumia miongo kadhaa kukijenga. Licha ya hilo, ni wazi kuwa Baba wa Taifa alifahamu kuwa watu aliowaamini kuwa ni wafuasi wake wazuri walikuwa mithili ya mbwa mwitu waliojivika ngozi ya kondoo: wanasiasa waliosimama majukwaani kuhubiri umoja na usawa lakini mioyoni walikuwa wakisubiri fursa ya kujitajirisha kupitia migongo ya Watanzania wenzao masikini.

Nimejaribu kutoa nadharia hapo juu kuhusu sababu ambazo pengine zilimkwaza Nyerere kuandaa mrithi wake. Lakini Azimio la Zanzibar lilipaswa kumtahadharisha kuwa kuondoka kwake madarakani kunaweza kabisa kuipeleka Tanzania kusikostahili. Kwa maana hiyo, kama angetaka-na kwa vile hata baada ya kung’atuka serikalini na kwenye chama aliendelea kuwa na nguvu na mvuto mkubwa-angeweza kufanya jitihada binafsi kuipatia Tanzania kiongozi mwenye sifa ambazo angalau zinakaribiana naye.

Katika stadi zinazohusu hali ya mambo ilivyo sasa huko nyumbani, na zile zinazobashiri hali itakavyokuwa huko mbeleni, kuna mwafaka wa kitaaluma kwamba kukosekana kwa itikadi ya kuwaunganisha Watanzania ni moja ya matishio makubwa kwa umoja na ustawi wa taifa letu.

Itikadi ya Ujamaa sio tu ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kutufanya Watanzania tujione kitu kimoja lakini pia ilimudu kwa kiasi kikubwa kuzuwia nyufa kama za udini na ukabila kuhatarisha umoja wetu.

Sasa tumebaki kama watoto yatima, hatuna mwelekeo unaoeleweka na wengi wa Watanzania wanaogopa kufikiria nchi yetu itakuwaje, kwa mfano, miaka 50 kutoka sasa. Na hatuwezi kuwalaumu wanaoogopa, kwa sababu wakati mwingine inalazimu kuangalia wakati uliopo tu hasa pale ambapo hakuna namna ya kuufanya wakati ujao uwe bora kuliko sasa.

Leo hii ukiwauliza Watanzania wanafikiri mwanasiasa gani ndani ya chama tawala anafaa kumrithi Rais Jakaya Kikwete atakapomaliza muda wake mwaka 2015, uwezekano mkubwa ni kupata jibu hili la kukatisha tamaa, “sioni mwanasiasa yeyote yule anayeweza kutuondoa katika lindi hili la umasikini linalorutubishwa na vitendo vya ufisadi.”

Wananchi wengi wamekata tamaa hasa baada ya kushuhudia nyingi ya ahadi za kutia matumaini zilizotolewa kwenye kila Awamu zikiishia kubaki ahadi tu pasipo kuleta mabadiliko kusudiwa.

Pengine kukata tamaa huko kunaweza kuwa na faida kwa vyama vya upinzani iwapo vitaweza kujitambulisha vya kutosha kwa wananchi na kuwahakikishia kuwa vina jipya zaidi ya CCM.Kwa vile chama hicho tawala ni sababu muhimu ya wananchi wengi kukata tamaa, wapinzani wakionyesha kuwa wanaweza kutekeleza yake yaliyoshindikana kwa CCM basi hakuna sababu ya wao kutochukua hatamu za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.

Ukiangalia vurugu zinazoendelea huko Zanzibar ni rahisi kubaini kuwa ukosefu wa itikadi inayotuunganisha unachangia kutokuwepo kwa hatua mwafaka za kushughulikia na hatimaye kumaliza matatizo ya Muungano na kudhibiti kuchipuka kwa hisia za ubaguzi wa kidini.

Kufanya hali mbaya kuwa mbaya zaidi, ukosefu huo wa itikadi ya kutuunganisha unakuwa tatizo kubwa zaidi unapojumlishwa na kutokuwa na mwanasiasa “anayeweza kusema na akasikilizwa” mithili ya Nyerere: yaani hatuna kitu wala mtu wa kutuunganisha.

Ndio maana wakati Waingereza wanasherehekea miaka 60 ya utawala wa Malkia Elizabeth na jinsi unavyowaunganisha, sie tusio na mtu wala itikadi ya kutuunganisha tunakuwa katika wakati mgumu sana: kutamani tusichokuwa nacho na hapohapo kuvunjwa matumaini kwa vile hakuna dalili za tatizo hilo kupatiwa ufumbuzi (angalau ndani ya chama tawala).

Lakini licha ya ukweli huo wa kuumiza, kuna habari ya kuleta matumaini: uzalendo. Katika mazingira tuliyonayo, Kinachohitajika zaidi si mtu au itikadi (japo ni muhimu) bali kiu kwa kila anayeipenda Tanzania kutimiza wajibu wake kwa maslahi ya nchi yetu. Tukiweza kuweka kando ubinafsi na kuepuka unafiki na tabia isiyopendeza ya kufanya mambo kwa minajili ya kupata fedha au sifa, tunaweza kwa umoja wetu wa kizalendo kuwa sio tu warithi wa Nyerere bali pia umoja wetu huo kuweza kuondoa ombwe linalotokana na ‘kifo’ cha itikadi ya Ujamaa.

Tunaweza kuendelea kumlaumu Nyerere kwa kutotuandalia mrithi wake, na tunaweza kuendelea kuwalaani milele walioua itikadi ya Ujamaa, lakini kwa bahati mbaya lawama na laana haziwezi kubadili chochote. Mkoloni hakutupa uhuru kwa sababu tulimlaumu kwa kututawala pasipo ridhaa yetu, na Nduli Idi Mani hakusalimu amri kwa vile tu tulimlaani kwa kila namna. Kilichomwondoa mkoloni ni jitihada za kizalendo za kudai uhuru wetu na kilichomtimua Amin ni umahiri na ujasiri wa majeshi yetu chini ya uongozi thabiti wa Nyerere.

Kwa kuwa kila Mtanzania mwenye akili timamu anataka tuendelee kuishi kwa amani pasipo kubaguana kwa misingi ya dini au kabila, na hakuna anayetaka kuona Wabara wakiambiwa wahame Zanzibar (na majuzi tumesikia kuna vipeperushi vinavyowataka Wapemba waondoke Unguja), na hakuna anayefurahia umasikini wetu licha ya raslimali lukuki tulizonazo, basi uzalendo ni jukumu la kila Mtanzania. Nia tunayo, sababu tunayo, na njia tunayo (uzalendo), kinachohitajika sasa ni utekelezaji kwa vitendo.

Yes we can!   

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.