Showing posts with label Modestus Kipilimba. Show all posts
Showing posts with label Modestus Kipilimba. Show all posts

27 Aug 2016

Tarehe 24 mwezi huu, Rais Dokta John Magufuli alimteua Dokta Modestus Kipilimba kuwa Mkurugenzi Mkuu (DGIS) wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Uteuzi huo umefanyika kufuatia kustaafu kwa mkurugenzi aliyemaliza muda wake, Othman Rashid.

Makala hii inajikita katika uchambuzi wa uteuzi huo kwa kuangalia changamoto na fursa zinazomkabili kiongozi huyo mkuu wa taasisi hiyo nyeti kabisa. Kwa mtizamo wangu, kama kuna kitu ambacho kinaweza kuzua maswali kuhusu uteuzi huo basi ni wadhifa wa Director of Risk Management alioshikilia Dokta Kipilimba huko nyuma alipokuwa mtumishi wa Benki Kuu ya Tanzania.

Sote twafahamu jinsi Benki Kuu yetu imekuwa ikiandamwa na matukio mfululizo ya ufisadi, kuanzia EPA hadi Tegeta Escrow. Kwa wadhifa wake katika taasisi hiyo, kuna uwezekano wa bosi huyo mpya wa mashushushu kuonekana ‘sehemu ya mfumo ulioshindwa kudhibiti ufisadi.’ Hata hivyo, utetezi unaweza kuwa huenda yeye alitekeleza majukumu yake vema lakini walio juu yake hawakuchukua hatua stahili.

Kadhalika, huko mtandaoni kuna ‘tuhuma’ kadhaa kuhusu Dokta Kipilimba, lakini itakuwa sio kumtendea haki yeye, blogu hii na mie mwenyewe kujadili tuhuma ambazo hazina ushahidi wowote. Ni muhimu kutambua kuwa Tanzania yetu licha ya kuwa kisiwa cha amani pia ni kisiwa cha majungu, uzandiki, fitna, umbeya na uzushi.

Changamoto kubwa kwa Dokta Kipilimba ni pamoja na kurejesha hadhi na heshima ya Idara ya Usalama wa Taifa. Katika miaka ya hivi karibuni, taasisi hiyo muhimu kabisa imekuwa ikishutumiwa kuwa inachangia ustawi wa ufisadi, ujangili, biashara ya madawa ya kulevya, nk.

Wanaoilaumu taasisi hiyo hawamaanishi kuwa watumishi wake wanahusika katika matukio hayo ya kihalifu as such bali kushindwa kwa Idara hiyo kukabiliana na kushamiri kwa matendo hayo ya kihalifu, ambayo kimsingi ni matishio kwa usalama wa taifa, na kazi kuu ya Idara hiyo ni kukabiliana na matishio kwa usalama wa taifa la Tanzania.

Ninaamini kuwa Dokta Kipilimba anafahamu kanuni muhimu kuhusu ufanisi au mapungufu ya idara ya usalama wa taifa popote pale duniani, kwamba “kushamiri kwa vitendo vinavyotishia usalama wa taifa lolote lile ni kiashiria cha mapungufu ya idara ya usalama wa taifa ya nchi husika, na kudhibitiwa kwa vitendo vinavyotishia usalama wa taifa popote pale duniani ni kiashiria cha uimara wa idara ya usalama wa taifa ya nchi husika.”

Kwahiyo, kwa kuzingatia kanuni hiyo, kushamiri kwa biashara ya madawa ya kulevya, ujangili, rushwa, na ufisadi mwingine ni viashiria vya mapungufu ya Idara yetu ya Usalama wa Taifa.

Changamoto nyingine kwa Dokta Kipilimba ni tuhuma za mara kwa mara dhidi taasisi hiyo muhimu kabisa kuwa katika utendaji kazi wake imegeuka kuwa kama ‘kitengo cha usalama cha chama tawala CCM.’ Idara hiyo imekuwa ikituhumiwa kuwa kwa kiasi kikubwa imeweka kando taaluma ya ushushushu (tradecraft) na kutekeleza majukumu yake kisiasa.

Madhara ya muda mfupi ya kasoro hiyo ni taasisi hiyo kujenga uhasama na vyama vya upinzani na kwa namna flani kupoteza heshima na uhalali wake. Lakini la kuogofya zaidi ni madhara ya muda mrefu, ambapo watu wanaoweza kuwa ni matishio kwa usalama wa taifa letu wanaweza kutumia ‘urafiki’ unaodaiwa kuwepo kati ya Idara ya Usalama wa Taifa na CCM, wakitambua bayana kuwa ‘Idara haina muda na makada wa chama tawala,’ na hatimaye kufanikiwa kutimiza azma zao ovu.

Baadhi ya watumishi wa zamani wa taasisi hiyo walijikuta matatizoni kwa vile tu walitekeleza majukumu yao dhidi ya wanasiasa wa chama tawala, na wakaishia kuonekana kama wahaini.

Changamoto nyingine kwa Dokta Kipilimba ni tuhuma zinazoikabili taasisi hiyo kuhusu mfumo wa ajira ambapo inadaiwa kuwa zimekuwa zikitolewa kwa upendeleo kwa ndugu na jamaa za ‘vigogo.’ Tatizo kubwa hapa ni kwamba utiifu wa ‘ndugu na jamaa hao wa vigogo’ haupo kwa taifa bali kwa vigogo hao waliowaingiza Idarani. Pengine sio vibaya kufikiria ‘utaratibu wa wazi’ katika ‘recruitment’ kama inavyofanywa na wenzetu wa CIA, NSA, MI5, MI6, HGCQ, nk wanaotangaza nafasi za ajira kwenye vyombo vya habari.

Pia kuna tatizo la baadhi ya maafisa usalama wa taifa ‘kujiumbua’ kwa makusudi kwa sababu wanazojua wao wenyewe, kubwa ikiwa kutaka sifa tu, au waogopwe ‘mtaani.’ Hii inaathiri sana ufanisi wa maafisa wa aina hiyo kwani ni vigumu kutekeleza majukumu yao ipasavyo pasi usiri.

Sambamba na hilo ni kasumba ya muda mrefu ambapo baadhi ya maafisa wa Idara hiyo waliopo kwenye vitengo mbalimbali kuwepo huko kwa muda mrefu mno kiasi cha kuathiri utendaji wao. Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na ‘vituo muhimu’ na kwenye ofisi za balozi zetu nje ya nchi. Ikumbukwe kuwa unless afisa ametengeneza deep cover, uwepo wake kwa muda mrefu katika sehemu aliyokuwa ‘penetrated’ au kituo chake cha kazi kwingineko (mfano ubalozini) unaweza kupelekea ‘akaungua’ (burned).

Changamoto nyingine kubwa ni uwepo wa majasusi kibao nchini mwetu, hususan kutoka nchi moja jirani, huku wengi wa majasusi hao wakiwa wameajiriwa katika taasisi za umma na binafsi. Hili ni tishio kubwa kwa usalama wa taifa wa Tanzania yetu.

Kwa upande fursa kwa Dokta Kipilimba, licha ya kuwa ‘mwenyeji’ katika taasisi hiyo muhimu, wasifu wake kitaaluma unamweka katika nafasi nzuri sana kukabiliana na changamoto za karne ya 21 ambayo imetawaliwa zaidi na teknolojia ya kisasa.

Dokta Kipilimba ni msomi aliyebobea kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) na yayumkinika kuamini kuwa anaweza kutumia usomi wake kuibadilisha Idara yetu ya Usalama wa Taifa kwenda na wakati, kufanya kazi kama taasisi ya kishushushu ya karne ya 21, ambayo licha ya kutegemea HUMINT inaweza pia kutumia njia nyingine za kukusanya taarifa za kiusalama kwa kutumia teknolojia (GEOINT, MASINT, SIGINT, CYBINT, FININT na TECHINT kwa ujumla)

Na katika kwenda na teknolojia ya kisasa, basi pengine si vibaya iwapo Idara yetu ikafikiria haja ya uwepo wake kwenye mtandao, kwa kuwa na tovuti yake kamili na pia kufungua akaunti kwenye mitandao ya kijamii, hususan Twitter na Facebook. Hii sio tu inaweza kusaidia kutengeneza "human face" ya intel service bali pia yatoa fursa nzuri katika OSINT.

Fursa nyingine kwa Dokta Kipilimba ni matarajio ya sapoti ya kutosha kutoka kwa Rais Dokta Magufuli ambaye kama alivyoahidi wakati wa kampeni za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka jana, mapambano dhidi ya ufisadi yamepewa kipaumbe cha hali ya juu kabisa. Kama ‘sponsor’ na ‘consumer’ wa taarifa za kila siku usalama, inatarajiwa kuwa Dokta Magufuli atatekeleza ushauri wa Idara katika kukabiliana na matishio mbalimbali ya usalama wa taifa letu.

Dokta Kipilimba ana fursa ya kuleta mageuzi kwa Idara ya Usalama wa Taifa kwa kuangalia uwezekano wa kuwafikia watu walio nje ya taasisi hiyo, hasa pale uwezo wa Idara yetu unapokuwa limited. Nitoe mfano. Katika kupata taarifa mwafaka wa kudumu kuhusu, kwa mfano, mgogoro wa kisiasa huko Zanzibar, Idara inaweza ku-reach out wanazuoni wa historia ya taifa letu walipo ndani na nje ya nchi yetu.

Ikumbukwe kuwa sio rahisi kwa taasisi hiyo kuwa na maafisa au watoa habari katika kila eneo. Wenzetu wa nchi za Magharibi wamekuwa wakikabiliana na hali hiyo kwa kufanya kazi na ‘makandarasi’ (contractors), ambao of course, wamekidhi taratibu kama vile vetting.

Sambamba na hilo ni Idara hiyo kuangalia uwezekano wa kutumia hazina kubwa tu ya maafisa wake wa zamani, hususan wastaafu. Ikumbukwe kuwa wengi wao ni watu wanaowindwa na ‘subjects’ mbalimbali wanaolenga kulihujumu taifa letu.

Nimalizie makala hii kwa kutoa pongezi za dhati kwa Dokta Kipilimba na Naibu wake (DDGIS) Robert Msalika, sambamba na kumtakia mapumziko mema Mkurugenzi mstaafu Othman, na kumkaribisha ‘uraiani.’

MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI IDARA YETU YA USALAMA WA TAIFA




Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.