Showing posts with label Nova Kambota. Show all posts
Showing posts with label Nova Kambota. Show all posts

26 Nov 2011


MKUU NIMEFURAHISHWA NA LOWASSA KUANZA KUANIKA UKWELI KUHUSU RICHMOND KWA KWELI NAONA ANAFANYA KILE NILICHOWAHI KUTABIRI KWENYE MAKALA YANGU YA "LOWASSA SEMA NENO MOJA TU" SASA KWA KULIONA HILO NIMEAMUA KUMTUNGIA SHAIRI HILO HAPO CHINI NAOMBA LITUNDIKE KWENYE BLOG YAKO WADAU WALISOME......


Kalamu yangu nashika, shairi nakutungia
Kamanda umeongea, kiwingu umeondoa
Hukutaka kusinzia,makosa kuyarudia
Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

Mwananchi nimesoma, la jana nilinunua
Machoya yakatuama, dukuduku umetoa
Uliyosema Dodoma, Kwakweli yanavutia
Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

Richmond kupasua, mapema uligundua
Kikwete ukamwambia, mkataba kuondoa
Rais akakataa, nini alitegemea?
Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

Nape akashikilia, lile asilolijua
Mikoani kaambaa, uzushi kang’ang’ania
Jinalo kulichafua, wewe ukavumilia
Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

Mapema nilitabiri, falsafa nikapinga
Magamba sikukariri, kuvuana sikuunga
Ukweli niliukiri, mantiki iso kunga
Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

Beti sita nakomea, kalamu naweka chini
Mengi nimeongelea, soma tena kwa makini
Yatazidi kutokea,kusini kaskazini
Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa.

Shairi limetungwa na Nova Kambota Mwanaharakati,
+255717 709618
Tanzania, East Africa
Jumamosi, November 26, 2011


5 Oct 2011



Na Nova Kambota Mwanaharakati,

Mara kwa mara huwa nasema tatizo kubwa la Tanzania yetu ni kupenda kupindisha ukweli, hii imetufanya kuwa watu tusiopenda kufikiri kiasi kwamba tunalambishwa kila linalokuja “tumekuwa madodoki kila uchafu tunasomba”. Naandika hivi kwa nia ya kujenga si kubomoa, naandika hivi kwa mustakabali wa Demokrasia yetu ambayo nathubutu kusema imetikiswa kupita maelezo huko Igunga na tusipokuwa makini Taifa litadondoka siku za usoni.
Kwako Dr Kafumu ambaye umetangazwa kuwa mbunge wa Igunga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), naomba unaposhangilia ushindi wako nikiamini wewe ni msomi na mzoefu katika Nyanja za uongozi wa Taifa hili napenda usome maandishi yaliyo ukutani kisha malizia kwa kuunganisha dots za ushindi wako halafu niambie ikiwa ni kweli unaamini kuwa umeshinda kihalali? Au la niambie kile ambacho kinaitwa “changamoto za uchaguzi Igunga” ni nini kama siyo “mizengwe?”
Kama mchambuzi nisiyeegemea upande wowote nisingependa kutia mwaa mtiririko huu wa hoja zangu kwa hiyo sitaegemea upande wowote bali nitajadili kwa misingi ya hoja ili ikibidi kujibiwa pia nijibiwe kwa misingi ya hoja vivyo hivyo, nataka kuibua hoja zenye mashiko ili zitufikirishe na kutupa majibu ya kisayansi badala ya kumezwa na mawimbi ya watu wenye mkatiko wa mirija ya fikra ambao wamebaki na ushabiki badala ya hoja kiasi kwamba wanatoa majibu ya zamani kwa maswali mapya. Yafuatayo ni mambo manne ambayo yanatia doa ushindi wa Dr Kafumu;
Kwanza Tume Ya Uchaguzi;
Tume ya uchaguzi ya nchi hii haina sifa nzuri na haiwezi kuwa na sifa nzuri mpaka iwe huru, hata I gunga hali ni hivyohivyo tumesikia malalamiko dhidi ya tume hiyo lakini hasa kwa aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa uchaguzi huo ambaye pia ni mteule wa rais na bila shaka kwa kuunganisha mantiki haina shaka kuwa naye ni mwanachama wa CCM au basi anaipenda kimoyomoyo. Uchaguzi wa Igunga ukipimwa kwa mizania hii ya aina ya tume ya uchaguzi tuliyonayo ni vigumu sana kwa mtu mwenye kufikiri kwa mantiki kuridhia matokeo ya uchaguzi huo.
Pili Siasa Uchwara;
Hapa inahitaji moyo mgumu kuyasema lakini kwa vile tangu awali nilishasema kuwa lengo si kufukua makaburi bali kuweka shada la maua juu ya makaburi basi acha niseme hiki ambacho nakiita ni siasa uchwara. Kwanza kabisa jinsi serikali ya CCM ilivyoruhusu kubofywa kwa kile kinachoitwa “kitufe cha udini”, ikumbukwe kuwa hata wakati wa uchaguzi serikali bado ina jukumu la kuilinda katiba na kuhakikisha amani haivurugwi aidha kupitia mirija ya udini wala ukabila, nayasema haya kutokana na baadhi ya viongozi wa dini kuirushia makombora CHADEMA tena wakaenda mbali kwa kutoa wito kwa baadhi ya waumini wa dini Fulani kutompigia kura mgombea wa chamna hiko, lakini cha ajabu hata hiyo hoja ya DC kuvuliwa hijabu imekwama kama gazeti nguli la Mwanahalisi lilivyofunua kuwa Mama Fatuma Kimario uislamu wake una mashaka kutokana na yeye kuwa ni mke halali wa Bw Kimario ambaye ni mkristu wa madhehebu ya Kikatoliki ambapo hata mwanazuoni mashuhuri wa kiislamu nchini Sheikh  Issa Ponda amenukuliwa akisema kuhusu mwanamke au mwanaume wa kiislamu kubadili dini Sheikh Ponda amesema “Hilo ni kosa kubwa sana”.  Lakini cha kusikitisha kuwa wakati haya yote yanatokea CCM walikaa kimya kana kwamba “hawakuliona kosa”, je tukisema kuwa hii ilichangia Wana Igunga kupiga “kura za chuki” dhidi ya CHADEMA tutakuwa tumekosea? Haya ni maswali magumu kuhusu ushindi wa Dr Kafumu.
Jambo la pili ambalo linaangukia kwenye siasa uchwara ni pamoja na vitimbi vya rushwa na vitisho vya “kipuuzi” mfano gazeti la Dira linamtaja mwenyekiti wa mtaa wa Nkokoto huko Igunga Bw Abed Motomoto (CCM) kuwa amekutwa akigawa rushwa “live”kwa wanawake wa mtaa wake kwa lengo la kuwashawishi kumpigia kura mgombea wa CCM (Dr Kafumu), lakini kama hili halitoshi kuna hili la Mh Ismail Aden Rage kupanda na bastola ikining’inia kiunoni halafu tunaambiwa kapewa adhabu ya kulipa laki moja, sasa ladda nitumie fursa hii kumuuliza ndugu yangu Aden Rage kuwa alikuwa anamtisha nani na bastola yake? Au nani kamwambia kuwa ni utamaduni wa kitanzania kuonyeshana vyombo vya moto? Haya ni machache kati ya mengi yanayokinzana na maana ya demokrasia pia kupoteza mantiki nzima ya “uchaguzi huru na wa haki”
Tatu kuchelewesha matokeo;
Hili ni  tatizo linalotia huzuni sana kiasi kwamba nashawishika kuamini kuwa “bado tuna safari ndefu”, nayasema haya kwasababu kwanza idadi ya watu waliojiandikisha ni tofauti sana kwasababu waliopiga kura ni wachache wanaokadiriwa kuwa elfu sitini (60,000) lakini cha ajabu hata kiasi hiki kichache cha kura kimechukua masaa kibao zaidi ya kumi kuhesabu, hiki kama si kiroja ni nini? Au tuamini kuwa kuna lililojificha nyyuma ya pazia hapa?
Nne Matumizi Ya Nguvu;
Nalazimika kuyaandika haya kutokana na tabia inayozidi kukua siku hizi ya polisi kutumia nguvu dhidi ya wananchi , matukio ni mengi lakini hebu tutupie macho kwenye hili sakata la Igunga ambapo nasema kulikuwa na matumizi ya nguvu yasiyo na msingi, mabomu ya machozi ya nini? Watu walitawanywa kwasababu gani? Kwa mamlaka ya nani? Na faida ya nani? Je hii ndiyo demokrasia tunayoitaka? Huu ndiyo tunaouita ushindi halali? Uhalali uko wapi hapa?
Baada ya kuona upungufu huu , sasa tuone nini ambacho Dr Kafumu anaweza kufanya ili kuienzi Demokrasia na kuwapa haki yao Wana Igunga;
1. Awe wa kwanza kulaani matumizi ya nguvu dhidi ya Wana Igunga
2. Awe wa kwanza kuhakikisha Ismail Aden Rage anachukuliwa hatua kali za kimaadili
3.Awe wa kwanza kulaani harakati zozote za wanasiasa kuingiza udini kwenye siasa
4.Awe wa kwanza kuomba radhi kwa niaba ya chama chake kwa kukaa kimya au kushabikia siasa uchwara.
5 Awe wa kwanza ndani ya CCM na Tanzania kukataa ushindi huo na kuitaka Tume kuitisha tena uchaguzi wa jimbo dogo la Igunga , hili lifanywe pasipo kuangalia gharama za zoezi hilo, bali lifanywe ili kuuonyesha Ulimwengu kuwa Dr Kafumu na CCM wameamua kusiamamia misingi ya Demokrasia pasipo kujali gharama za hatua hiyo.
Haya ni mambo ya msingi kwa Dr Kafumu kuyasoma na kuyafanyia kazi, hii itamjengea heshima sio tu ndani ya CCM bali kwa watanzania wote na Ulimwengu mzima. Tafakari! A luta Continua!
  
Nova Kambota Mwanaharakati,
+255717 709618
Wesneday, 5october,2011
Tanzania, East Africa.

2 Sept 2011


Na Nova Kambota,
Namkumbuka mwanamuziki wa kizazi kipya Seleman Msindi maarufu kama Afande sele na kile kibao chake cha “Darubini kali” anapohoji “kama unapenda pepo kwanini uogope kifo?”
Tungo hii kwa namna ya pekee inamgusa waziri mkuu wa Tanzania Mh Mizengo Pinda maarufu kama “mtoto wa mkulima” ndiyo namuuliza Pinda ataonaje pepo pasipo kufa kwanza?
Tangu kuteuliwa kwake mara baada ya Edward Lowassa kujiuzulu, Kwa wale wanaomjua Pinda walishasema kuwa “Pinda atapwaya sana”, sasa ikiwa ni takribani miaka mitatu na nusu tayari mambo hadharani kuwa Pinda “kashindwa kazi”
Kwa wasiomjua Mizengo Pinda tafuteni ukweli mtamjua tu, ni Mizengo Pinda huyu amebaki kuwa mshauri wa Kikwete badala ya waziri mkuu kufikia hatua ya kutamka bungeni kuwa hana mamlaka, ni Pinda huyu asiye na makundi lakini anakubali kumezwa na mitandao na makundi ya CCM na bosi wake Kikwete na sasa nimeanza kusikia watu wakimwita ni “mtoto wa mkulima anayeishi kibilionea”
Hakuna ubishi kuwa hata watetezi wachache wa Pinda waliobaki sasa wamefadhaishwa na udhaifu wake kama sio uwoga wa kupindukia, “jeuri” ya Luhanjo na sakata la Jairo limemwaka njia panda Mizengo Pinda, amebaki kujiumauma na kutapatapa tu, kadhalilishwa lakini hataki kuchukua hatua, katukanwa lakini anachekelea! Huyu ndiye Mizengo Pinda.
Waziri mkuu Pinda akiongelea sakata la Jairo akajiapiza kuwa angekuwa na mamlaka angemfukuza kazi Jairo kwa maana nyingine Pinda amekiri kuwa Jairo anastahili adhabu na serikali haikutaka kumwangusha waziri mkuu “ikamtwanga likizo ya malipo” Bw Jairo lakini ghafla katibu mkuu kiongozi anaibuka na kumdhalilisha waziri mkuu eti Jairo hana kosa arudi kazini, wakati Pinda akisita kuchukua hatua wabunge kwa umoja wao wameamua kumtetea waziri mkuu kwa kudhalilishwa sasa Bunge limeunda kamati.
Hivi katika mduara huu wa “kudhalilishana na kushushiana heshima” ipi nafasi ya Pinda? Yapi maamuzi ya Pinda? Kichekesho ni kuwa Pinda “yupoyupo tu” hajachukua uamuzi na dalili zinaonyesha kuwa kwa mara nyingine tena Pinda amekubali kupiga magoti na kujishusha sehemu aliyotakiwa apigiwe  magoti yeye huyu ndiye Pinda ambaye bilashaka hata “ukimpiga ngumi” yeye wakati wa kukurudishia lazima atavaa gloves ili asikuumize.
Pinda anataka pepo? Anataka watanzania tumkumbuke kuwa ni kiongozi jasiri? Basi hana budi kufa ili aione hiyo pepo! Naam amedhalilishwa sana, ameshushiwa hadhi yake, na sasa ni wakati wayeye kufikiria kujiuzulu.
Haiwezekani Luhanjo na Pinda waendelee kuitumikia serikali moja, hiki kitakuwa ni kiinimacho , ni lazima mmoja wao atoke, na kwa vile wote tunakubaliana Pinda anaitamani pepo, anataka kukumbukwa mioyoni mwa watanzania, lazima aachane na serikali hii ya akina Luhanjo na Jairo, hana budi kumwachia Kikwete ateue waziri mkuu mwingine ambaye atakubali kuvunjiwa heshima, Naam! Pepo haiji hivihivi, ni lazima Pinda afe leo ili aione pepo kesho!

Nova Kambota Mwanaharakati,
+255717 709618
Tanzania, East Africa,
Alhamisi, September 1, 2011.


29 Jul 2011


Na Nova Kambota,

Nasema wazi Anne Makinda hana la kujivunia na pengine hata wanahistoria hawana la kuandika juu ya mwanasiasa huyo ambaye ni dhahiri sasa nyota yake inazidi kufifia kila sekunde.

Yanayoendelea na yatakayoendelea kutoka Bungeni ni ushahidi wa wazi wa udhaifu wa spika Makinda, Job Ndugai, Jenista Mhagama na Simbachamwene ambao kwa nyakati tofauti wameonyesha dhahiri kuwa sasa wameshindwa kazi.

Sitaki kuibua malumbano yasiyo na tija bali nataka niweke wazi kuwa tatizo si wapinzani bali udhaifu wa Makinda na wasaidizi wake.

Ni mwehu gani leo hii hakumbuki mikiki ya Dr Slaa wakati wa spika Sitta? je yalitokea haya tunayoyaona sasa? je nikisema Sitta “KAMFUNIKA” Makinda nitakuwa naongopa? NARUDIA TENA tatizo ni Makinda na wasaidizi wake!

Tangu awali wenye kuona mbali walitoa angalizo kuwa spika aliyechaguliwa kwa kigezo cha jinsia “HAFAI” na leo hii wote tu mashahidi kuwa sasa “MAKINDA ANAWABEBA WALIOMBEBA” amelivuruga Bunge na kweli limevuruga .

Kawafanya wapinzani kuwa na roho ya “KUPAMBANA” dhidi yake na wasaidizi wake na kwa bahati mbaya hana uwezo wa kulitatua hili si yeye wala “wasaidizi wake”

Watanzania hawapaswi kushangaa “eti wabunge wanataka kupigana” nini cha ajabu? au Deo Filikunjombe kutaka “kupigwa makofi?” lipi la ajabu? Lema, Msigwa na Lissu kutolewa nje ya Bunge? nini cha ajabu? pendekezo la wabunge kupimwa akili? haya yote hayana budi kutokea, hebu jaribu kufikiria haya yasipotokea watanzania mtaamini vipi kuwa “HII NI NCHI LEGELEGE?”

Nova Kambota Mwanaharakati,
+255717 709618
[email protected]
www.novakambota.com
Tanzania, East Africa
Ijumaa, Julai 29, 2011.

7 Jul 2011


Na Nova Kambota,

Rais wa awamu ya tatu Mzee Benjamin Mkapa aliwahi kusema kuwa maisha bila vipaumbele ni ujinga mtupu, bilashaka hili halina ubishi kabisa taifa lolote linaloishi bila vipaumbele hugeuka taifa la wahuni, waporaji, mafisadi, wajinga,duni na zaidi huwa taifa legelege na dhaifu.

Wageni mbalimbali kutoka Ulaya, Marekani ,Asia na sehemu nyingine za ulimwengu waliowahi kufika nchini huwa wanashangazwa sana na umasikini wa kutisha unaowaandama wananchi wa taifa hili. Wageni wanatushangaa sana na wataendelea kushangaa kuanzia Mlima Kilimanjaro,Mlima Meru, Udzungwa, Usambara, Ziwa Tanganyika, Victoria, Bahari ya Hindi mbuga nzuri za wanyama kama Mikumi na Ngorongoro lakini pia misitu ya kumwaga tu,mito mingi, mabonde ndiyo usiseme na ardhi yenye rutuba na

ya kutosha lakini bado miaka hamsini baada ya uhuru mamilioni ya watanzania bado ni masikini wa kutupwa.

Kwa mtiririko huu wa mantiki hapa ndiyo inaibuka hoja kuwa watanzania hawafanani na nchi yao hata kidogo kwa maana ni watu mafukara waliozungukwa na utajiri wa kutisha , hakika kuna utofauti mkubwa kati ya watanzania na utajiri wa taifa lao, hata ukifika pale mbuga ya Ngorongoro wanyama wanacheza na kufurahi na ndege wanarukaruka kwa furaha kubwa, nenda kandokando ya bahari ya Hindi uone mawimbi yanavyopanda na kushuka kwa furaha kisha angalia samaki walivyo na furaha kisha sasa rudi katika maisha ya walalahoi wa nchi hii, kweli inahuzunisha kuona wanyama wana furaha kushinda watanzania, inauma sana!

Kuna kisa kimoja cha kuhuzunisha sana ambacho nadhani watoto wetu wanapaswa kufundishwa madarasani. Inaelezwa kuwa mwaka jana 2010 wakati wa uchaguzi mkuu mwangalizi mmoja wa kimataifa kutoka nje alitembelea Tunduru akaona watu wanavyoogelea kwenye umasikini wa kutisha kisha akatupa macho kwa mbali akaona misitu mizuri na mto Ruvuma kisha akahoji kuwa inakuwaje watu hao ni masikini sana? Wananchi hawakuwa na la kujibu baadaye mzungu huyo akasema kuwa “siamini kabisa na hainiingii akilini kuwa CCM huwa inashinda kihalali kwa maana haiwezekani watu masikini kama hawa waichague CCM”

Hivi nani atanishawishi kuwa CCM inashinda kihalali? Hapa uhalali unaozungumzwa sio wa kura tu bali hata wa kuwaacha watu huru, kwa maana haiwezekani watu wanakuwa masikini, wanafanywa wajinga na mifumo mibovu kiasi kwamba hawajui umuhimu wa kura halafu wanajiandikisha watu milioni 19 kupiga kura lakini siku ya kupiga kura wanajitokeza milioni 5 na CCM wanashinda! Kisha uniambie hapo kuna ushindi? Ushindi gani? wakati milioni 14 nzima hawajapiga kura? Idadi hii inaweza kubadili matokeo, kwa maana nyingine yule mwangalizi wa kimataifa yupo sahihi kabisa kuwa watanzania hawaichagui CCM badala yake inajichagua yenyewe na kujipa madaraka, ajabu sana!

Watanzania wanalia kwa mengi, heri wote wangekuwa masikini lakini kuna wenzao “wajanja wachache” wanaishi kama wafalme kwa jasho la watanzania. Cha ajabu katika umasikini huu wa kutisha wa watanzania kuna baadhi ya watanzania wachache wamejigeuza “miungu watu” wamejimilikisha utajiri wote huu wakisaidiana na waporaji mabeberu kutoka Ulaya na Marekani, hawa hawajui njaa ni nini? hawafahamu masikini anafananaje? Wenyewe wanajua kuvaa suti na tai na mwisho wa mwaka wanaenda kwenye maduka makubwa ya nguo huko London na Dubai ili kuwafanyia “shopping” wake zao na watoto wao wapendwa.

Nchi imekuwa ya matabaka kiasi kwamba mpaka taifa linayumba . Leo hii imefika mahali kuna watu wana nguvu za kutisha kwenye nchi mpaka mkurugenzi wa TAKUKURU anakiri kwenye mtandao wa Wikileaks kuwa Tanzania kuna “untouchables” hawagusiki hawa. Katika mazingira haya bado CCM inahubiri usawa, usawa gani? hata mtoto mdogo hawezi kushawishika kuwa kuna hata chembe ya huo usawa kwenye nchi hii, labda kidogo CCM waje na hoja ya kuwa na nchi mbili za kimatabaka kwenye taifa moja ndiyo! Kuna Tanzania ya tabaka la juu na Tanzania ya tabaka la chini.

Huu ndiyo ukweli wa mambo , na matabaka haya mwanzo wake ni kuwa kuna wale walioshikilia utajiri wa taifa na wale waliotengwa na utajiri huo. Cha kusikitisha zaidi serikali inapigia chapuo mpasuko huu wa kitabaka kiasi kwamba imejenga shule za kata maalumu kwa masikini ili wakafeli na kuna mashule ya kimataifa yenye ubora haya ni maalumu kwa ajili ya watoto wao na maswahiba zao. Serikali haijaishia hapo tu sasa hivi Tanzania fedha iko juu ya sheria , nani asiyefahamu ukiwa na fedha nchi hii unaweza kupindisha sheria? Zaidi ya yote kuonyesha kuwa serikali yetu ni legelege ni jinsi inavyozitekeleza hospitali za serikali kiasi kwamba ni kama majengo tu bila dawa na ili kuonyesha kweli ubaguzi ni mfumo rasmi kwenye nchii hii hakuna “mkubwa” anaayekwenda kwenye hospitali za serikali huko ni kwa kapuku na walalahoi, ubaguzi wa kutisha!

Viongozi hawaishii hapo tu kwenye juhudi zao za kuwafukarisha wananchi na kuwaibia mali zao, sasa wameanzisha soko huria la kura na wapiga kura na mnada kila baada ya miaka mitano. Hivi kwanini viongozi wasiwaache huru watanzania? Kwanini wasiwaache wakajichagulia watu wanaowaamini ni viongozi bora? Huu kama sio ujambazi wa haki za masikini ni nini? yaani hao walioko madarakani mwaka jana tu walipambana kununua kura kama sio kwenye ngazi ya chama basi kwenye uchaguzi kamili lakini ndiyo hivyo ukweli ni kuwa wamenunua kura kwa pesa nyingi na sasa wapo madarakani wanashindana kupora mali za wavuja jasho.

Taifa limekosa vipaumbele , limehalalisha rushwa, uporaji na ufisadi, taifa linapepesuka kwa uhuni na tamaa za viongozi , dola imedhoofika sana hata kamanda mkuu Rais Jakaya Kikwete analifahamu hili lakini tatizo “kupe” wamejaa kuanzia huko CCM mpaka serikalini. Kile alichokitabiri Mwalimu Nyerere sasa kinatokea kweli, Mwalimu aliwahi kusema “serikali isiyojali wananchi wake haina uhalali hata kama imepigiwa kura” sitaki kuamini kuwa serikali ya CCM haina uhalali ila nashawishika kuwa haijali wala kuthamini wananchi wake hivyo kwa maana nyingine imeanza kupoteza uhalali wake.

Imefika sehemu sasa watanzania wanapaswa kufanana na utajiri wa nchi yao, viongozi inabidi wafahamu kuwa watanzania hawana sababu ya kuwa masikini kama walivyo sasa. Watanzania lazima wafanywe kujivunia utanzania wao tofauti na hivi sasa ambapo kuna watanzania wanajilaani kwa kuwa watanzania yote kwasababu ya ubabaishaji wa viongozi wao ambao badala ya kuwatumikia wananchi wao wako “busy” kutumikia matumbo yao na familia zao.

Lakini kama kawaida ya viongozi wetu wana tabia ya kuweka pamba masikioni hawataki kusikia bilashaka hata hili watapuuzia lakini nawapa angalizo kuwa watanzania wanafahamu kuwa hawakuumbwa walivyo bali umasikini wao umetengenezwa hivyo ni swala la muda tu lakini siku ikifika uvumilivu utakapowashinda basi watawang’oa wababaishaji wote wanaojineemesha na mali zao tena kwa njia yoyote ile, hizi ni zama za ukweli na uwazi ni wakati sahihi wa kuwa na mgawanyo sawa wa keki ya taifa…..Allutacontinua!

Nova Kambota Mwanaharakati,



+255717 709618

Tanzania, East Africa

07/07/2011, Alhamisi

Naomba kura yako kwenye tuzo za blog Tanzania kwenye category ya best collaboration/group blog, best informative political blog na best political blog kunipigia kura nenda http://www.tanzanianblogawards.com/


 

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.