Showing posts with label POLICING IN TANZANIA. Show all posts
Showing posts with label POLICING IN TANZANIA. Show all posts

10 Jul 2010

Kwa mara ya tatu ndani ya wiki moja askari wa jeshi la polisi amejiua kwa kujipiga risasi.Haya si matukio ya kuyachukulia kimzaha kwani licha ya ukweli kuwa vifo vya askari hao ni pigo na doa kwa jeshi hilo lakini pia inawezekana kesho na keshokutwa,Mungu aepushie mbali,tunaweza kusikia askari amemwagia risasi raia kadhaa wasio na hatia kabla ya kutoa uhai wake mwenyewe.Kuna tatizo ndani ya jeshi hilo lakini kama ilivyo ada kwenye maeneo mengine wahusika wanaendelea kujifanya mbuni kwa kuficha vichwa kwenye shimo huku mwili ukibaki nje.

Nilibahatika kufanya kazi na polisi kwa muda mrefu tu na kwa hakika utawahurumia ukisikia na kuona matatizo wanayokabiliana nayo kimaisha na kiutendaji kazi.Kubwa zaidi ni hali ya maisha yao hususan kwenye suala la makazi.Nenda Kilwa Road,Oysterbay au Temeke na shuhudia mazingira wanayoishi wanadola hao,na utakubaliana nami kuwa si vigumu kwao kukumbwa na shinikizo la kisaikolojia.Hebu tafakari kuhusu askari anayekesha lindoni Masaki,Mikocheni,Upanga,Oysterbay,nk kwa vigogo na kushuhudia watu wanavyokula keki ya taifa wakati mwanadola huyo anaishi maisha ya chini kabisa licha ya mchango wake mkubwa katika usalama wa nchi.Ni dhahiri anaweza kupatwa na mawazo kuwa maisha na kazi aliyonayo havina thamani.

Lakini pia kuna unyanyasaji unaotawala kwenye vyombo vyetu vya dola ambapo viongozi ni miungu watu huku wakipata maslahi manono kupindukia ukilinganisha na wale wanaowaongoza.Na hiyo sio huko polisi tu bali hata katika ofisi nyinginezo-za dola na zisizo za dola-ambapo viongozi hujijengea ukuta mrefu wa kuwatenganisha na wanaowaongoza.Vikao kati ya viongozi na watumishi wa ngazi za chini hutawaliwa na vitisho vinavyokwaza kero na malalamiko ya askari wa ngazi za chini kusikika.

Pasipo kutafuta ufumbuzi wa haraka katika wimbi hili la polisi kujiua kwa risasi basi tuwe tayari kushuhudia balaa.Silaha haziui watu,bali watu hutumia silaha kujiua au kuua wengine.Sasa kama askari wetu tunaowakabidhi silaha wanaweza kujiua kama njia ya ufumbuzi wa matatizo yao binafsi,yayumkinika kubashiri kuwa siku moja wanaweza kabisa kuua watu wengine kabla ya kujiua wao wenyewe.

Tusipoziba ufa tutajenga ukuta.Hebu soma habari kamili katika kiungo kifuatacho

Hebu soma habari kamili kwa kubonyeza KIUNGO HIKI.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.