Showing posts with label RELIGION AND POLITICS IN TANZANIA. Show all posts
Showing posts with label RELIGION AND POLITICS IN TANZANIA. Show all posts

22 Jun 2009


Katika MAKALA HII nilionyesha wasiwasi wangu kuhusu hatua ya Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo kutangaza kufutwa kwa misamaha ya kodi kwa taasisi za dini.Katika makala hiyo,nilieleza hivi (najinukuu)

Lakini binafsi natafsiri kuwa hatua hii ina ajenda mbalimbali zilizofichika
ikiwa ni pamoja na kuonyeshana nani mwenye nguvu zaidi: mamlaka za kidunia au za kiroho.Usisahau kauli za hivi karibuni kutoka kwa madhehebu mbalimbali ya Kikristo kwamba mafisadi wameteka nchi....na kuandaa mkakati wa kupata viongozi bora katika uchaguzi mkuu wa 2010.
Toleo la leo la gazeti la Majira lina habari inayothibitisha hypothesis hiyo.Kwa mujibu wa gazeti hilo,kauli zilizoikera Serikali hadi kufikia hatua ya kutoa "kibano" hicho ni pamoja na ile ya Kanisa Katoliki kuanzisha program maalum ya kuelimisha waumini wake kuhusu masuala mbalimbali ya demokrasiapamoja na namna ya kuchagua viongozi bora.

Kwa mujibu wa Majira,kauli nyingine ni ile iliyotolewa na na Jumuiya ya Kikristo Tanzania kwenye Mkutano wake mjini Dodoma ambapo ulitolewa wito kwa waumini wa madhehebu hayo kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu hapo mwakani.




Picha ya gazeti la Majira kwa Hisani ya KENNEDY.

Najiuliza,hivi hapa nimejisifu au nimejipongeza?


4 Nov 2008

KLHN yaweza kuripoti kwa uhakika kabisa kuwa mpango wa kuanzisha uchafuzi wenye mlengo wa kidini na kikabila nchi umeundwa na sasa umefichuliwa. Mpango huo ambao unawahusisha watu mbalimbali wenye majina makubwa umedhihirika kuanzia siku ya Ijumaa iliyopita. Mpango huo ulianza kusukwa wiki chache zilizopita na hatimaye kuanza kutekelezwa siku ya Ijumaa iliyopita. Kwa wanaokumbuka siku ile (ya Ijumaa) kulikuwa na mkutano wa Waislamu kuelezea masuala mbalimbali ya maslahi yao na hasa suala la OIC. Baadhi ya viongozi wa Waislamu toka mikoani walikuwa jijini pia. 

Ilikuwa ni katika nafasi hii timu iliyokuwa imeanza kukusanywa iliweza kuwakutanisha viongozi mbalimbali hao wa Waislamu kwa kuandaa mkakati kamambe ambao kwa madai yao mipango yake inatoka ndani na juu kwenye serikali. Katika kufanya hivyo viongozi kama 9 hivi wa Kiislamu waliweza kupatikana na kukutanishwa katika hoteli ya Regency siku ya Ijumaa. 

Miongoni mwao ni mashehe na viongozi wengine wa kidini; baadhi yao ni pamoja na Shekhe Mazinge, Mwaipopo, Said Liko, Chifu Msokwa, Ustaadh Twaha, Dr. Salehe, Abubakar Bonde, Sheikh Amour Jongo, Rajabu Jazba, na Ustaadh Ramadhani. Waliokuwemo kwenye mkutano huo pia ni pamoja na Albert Marwa (inadaiwa ni mtoto wa kulelewa wa Generali Marwa) pamoja na mtu mmoja aitwaye Mtawa (huyu yasemekana ni mtumishi wa ngazi ya Juu ikulu). Walikuwepo baadhi ya watu wengine ambao wanadaiwa kuwa ni maafisa wa Usalama wa Taifa ambao kutokana na sheria hatuwezi kuwataja majina yao. 

Mpango huo ambao “vijidudu” vya uchunguzi viliweza kuunasa kwa picha na kwa sauti kimsingi una malengo yafuatayo. 

a. Kuwaonesha waislamu kuwa Bw. Reginald Mengi na Freeman Mbowe ndio maadui wakubwa wa maslahi ya Waislamu nchini.
b. Kwamba Mengi na Mbowe wana mkakati wa kuhakikisha kiongozi anayekuja ni kutoka kabila la Wachagga. Katika hili la dhidi ya “Uchagga” wanamkakati walikuwa wana uhakika wa kutobughudhiwa na polisi kwenye mikutano ambayo waliipanga kuifanya hasa wakiamini kuwa IGP Said Mwema yuko upande wao. Hata hivyo mmoja wao aliapa kuwa aliwahi kuambiwa na Dr. Nchimbi kuwa Mwema ni Mchagga (sijui kwa upande wa mama) na hivyo wasitarajie sana.
c. Walioleta mpango huo wamemhusisha kiongozi wa juu serikalini kuwa ndiye aliyewatuma kutekeleza mpango huo hasa kuonesha kuwa vyombo vya IPP vinatumika kueneza Ukristu, kukandamiza Waislamu, na kuinua Wachagga. Hili litaelezwa ili Waislamu waanze kuvisusisa vyombo vya habari vya IPP. 
d. Kuendelea kuwahusisha Mengi na Mbowe katika vifo vya Chacha Wangwe na Gavana Ballali.

Katika kutekeleza mpango huo timu hiyo ilikuwa ijipange na kuandaa bajeti ya kiasi kisichopungua shilingi milioni 100 ambazo zitagawanywa kati yao na kwa wale ambao watakuwa tayari kutekeleza mpango huo. Kiasi ambacho cha awali ambacho kila mmoja alikuwa agawiwe ni kama milioni tatu tatu huko mmoja wa wanamkakati huo akiahidi uwezekano wa kupata fedha zaidi kutoka kwa Bakhresa. Kiasi cha awali kinadaiwa kutolewa na mfanyabiashara Yusuph Manji wa Quality Group.

Siku ya Jumamosi kundi hilo la wanamkakati lilikutana kwenye hoteli ya Golden Tulip kuendelea na mipango yao ambayo ka nzi ka KLHN kalikuwa kanafuatilia kila hatua tena kwa ukaribu kabisa. 

Wakiwa na magari yenye namba za usajili za T267 ABT na T87 ABG wanamkakati wakiongozwa na Mazinge Mwipopo (spelling yaweza isiwe sahihi) na Chifu Msokwa walihamisha kikao chao kingine kutoka Golden Tulip kuelekea Msikiti wa Mtambani ambapo waliamua kubadilisha na kuelekea Msikiti wa kwa Mtoro. Ka nzi kaliweza kunasa habari za kutosha. 

Siku ya Jumapili kikao chao kiliendelea huko Kinondoni mtaa wa Kazina nyumba (censored) ambapo kuanzia saa tisa hadi majira ya Magharibi waliendelea na mipango yao na maazimio yao ikiwemo la kuhakikisha kuwa viongozi watakaoshiriki katika mkakati huo wa kuitisha mikutano mbalimbali mikoani wahakikishe na wao wanapata watu angalau 20 chini yao. 

Kutoka kwenye vikao hivyo iliazimiwa uitishwe mkutano wa waandishi wa habari ili kuweza kufafanua madai yao dhidi ya Mengi na Mbowe na hivyo kuanzisha mchakato huo wa kueneza propaganda hii ya udini na ukabila. Baadhi ya wajumbe walikuwa wameshaondoka siku ya Jumatatu kuelekea mikoani kuanza kazi hiyo na hilo ndilo lililosababisha vyombo vya ITV kurusha hivyo walivyonavyo. 

KLHN imepata nafasi ya kusikiliza masaa ya kutosha ya mazungumzo ya kundi hili na jambo moja ambalo tunaweza kusema kwa uhakika ni kuwa linatia hofu na kuuliza tumefikaje hapa. 

Hata hivyo mpango huo haujaenda vizuri kama ulivyotarajiwa hasa baada ya kutokea mabishano ya kiasi cha fedha huko baadhi ya wajumbe wakiamini kuwa Bw. Albert Marwa amepewa fedha zaidi kuliko alizowapatia wajumbe hao. Wengine wameanza kudai kuwa Bw. Marwa ndiye aliyeinjinia mpango wa wao kunaswa na vyombo vya kielectroniki. 

Jioni ya leo (jumanne) ka nzi ketu kanaruka ruka mikoani kamethibitisha pasipo shaka kuwa baadhi ya simu za wahusika wakuu zimekuwa ‘tapped’ ili kuweza kujua jinsi operesheni hii ilivyoendesha kikamilifu ikihusisha utaalamu na ujasiri wa hali ya juu kuliko uwezo wowote wa TISS kuwanyemelea mafisadi. 

Msimamizi wa Operesheni hii ardhini ambaye alizungumza na KLHN kwa masharti yale yale mliyoyazoea amesema kuwa hawakuwa na mpango wa kuhusisha vyombo vya usalama kwani kwenye suala zima vyombo hivyo baadhi ya wahusika wake wa kuu wamo ndani mpango huu na hivyo njia pekee ilikuwa ni kuwadokeza tu watu kuwa mpango huo upo, unajulikana, na utakapoanza kutekelezwa Watanzania “wasishtuke”. 

Hata hivyo wameahidi kuwa endapo Mwendesha Mashtaka Mkuu ataamua kuunda "Special Tribunal" ya kufuatilia suala hili ili kuona mashtaka yoyote kuletwa au uchunguzi ushirikiano unaweza kutolewa kwa kadiri ya kwamba vyanzo vyote vya habari hii vitabakia kuwa siri na havitalazimishwa kujitaja isipokuwa kuleta ushahidi kama ulivyo (raw evidence). Nje ya hapo amesema kuwa hawana "imani na Polisi wala Usalama wa taifa kwenye suala hili".

KLHN inaendelea kufuatilia kwa karibu mpango huu na kufichua njama yoyote ile ya kifadi yenye lengo la kuleta mgongano wa kidini au kikabila nchini. Baadhi ya habari zitasahihishwa kwa kadiri wingu linavyozidi kusafishika zaidi.


31 Oct 2008

Picha kwa hisani ya BONGOPICHA

WAKATI serikali ikishutumiwa na viongozi wa madhehebu ya Kikristo, juu ya Tanzania kutaka kujiunga na Jumuiya ya nchi za Kiislamu (OIC) na kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amekutana kwa siri na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kujadili masuala hayo.

Kikao hicho cha faragha cha viongozi hao wawili, kilichukua zaidi ya saa moja katika mazungmzo yao yaliyofanyika jana katika ofisi za Jimbo Kuu la Dar es Salaam, kuanzia saa 10:30 jioni hadi saa 11:30.

Membe alikutana na Pengo jana ikiwa ni siku moja baada ya kardinali huyo kurejea nchi akitokea Vatican ambako alikwenda kwa shughuli za kanisa.

Akizungumza na Tanzania Daima, baada ya kumalizika kwa kikao hicho nyeti, Waziri Membe alikiri kuwa na kikao cha faragha na kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki nchini, lakini hakuwa tayari kusema nini walichojadiliana, kwa madai kuwa, hayapaswi kuwekwa hadharani kwa sasa.

“Unajua Kardinali Pengo ni kiongozi wa kiroho wa ngazi ya juu sana, kila tunapokuwa na masuala mazito ya kitaifa, tunapenda kupata ushauri wake pamoja na viongozi wengine wa kiroho ili kuona wanasemaje,” alisema Waziri Membe.

“Mbali na suala la OIC na Mahakama ya Kadhi, tumezungumza mambo mengi ya kitaifa ambayo mimi sipaswi kueleza zaidi kwa undani, kwani unaweza kumuuliza Baba Kardinali mwenyewe kama atataka kukueleza, lakini ni mambo ambayo yanahusiana na maisha ya Watanzania wote,” alisema Waziri Membe.

Kuhusu mjadala unaoendelea juu ya Tanzania kujiunga na OIC na jinsi hali ilivyo kwa sasa nchini, Waziri Membe alisema ni mambo ya kupita na utulivu utarejea hivi karibuni.

“Hali ya amani na utulivu itarudi hivi karibuni, hakuna shida, serikali ina amini na inawahakikishia wananchi kuwa hakuna vurugu kuhusiana na hilo wala suala lingine lolote.

“Watu watulie, wafanye kazi, serikali itakutana na wadau wote na nasema tena, hakuna tatizo kubwa hapa, tutahakikisha suala hili linaisha kwa amani bila kusababisha vurugu zozote,” aliongeza Membe.

Akizungumzia madai yaliyotolewa na Jumuiya ya Maaskofu wa CCT, kumtaka ajiuzulu hivi karibuni, alisema kuwa hilo hataki kuliongelea kwani amechoka, aachwe apumzike kwanza.

Jitihada za kumtafuta Kardinali Pengo, kuzungumzia juu ya kikao hicho cha siri ziligonga mwamba baada ya kuambiwa kuwa, ameingia kwenye kikao kingine na uongozi wa Kanisa la Mt. Joseph na haijulikani kingeisha saa ngapi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita maaskofu wanaounda Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), walielezea kusikitishwa, kushtushwa na kupinga ushawishi unaojengwa na serikali wa kutaka Tanzania iridhie kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC).

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Askofu Peter Kitula ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, alisema hawatakuwa tayari kukubalia kwa vyovyote vile kuona chama fulani cha siasa kikijaribu kutafuta ridhaa ya wapiga kura kwa gharama ya kutishia umoja wa kitaifa na amani ya nchi.

“Hapa ieleweke kuwa ni hatari na kamwe isiruhusiwe njia hii kutumika ili mradi chama fulani kishike dola hata kama ni kwa gharama ya kuvunjika kwa umoja wa kitaifa na amani ya nchi hii! Jambo hili hatutalikubali kwa vyovyote vile kwa chama chochote kitakachokubali mambo haya mawili aidha wakati wa kampeni za uchaguzi au wakati wowote ule,” lilisema tamko hilo la CCT lililoambatanishwa na majina ya maaskofu 64 wa nchi nzima.

Pasipo kufafafanua huku wakisema kwamba CCT, haifungamani na chama chochote cha siasa, maaskofu hao katika tamko lao walisema, iwapo itafikia hatua ya Tanzania kujiunga na OIC na Mahakama ya Kadhi kuridhiwa, basi wao watalazimika kufikiria upya jinsi ya kukishauri chama hicho tawala kwa kuzingatia kile walichokieleza kuwa ni manufaa ya Watanzania.

“Kipekee wakati huu, kutokana na yanayoendelea kujadiliwa bungeni, tunatoa tahadhari kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kutoruhusu kabisa kuendelea kwa mjadala huu kama ambavyo tumekuwa tukiomba mara kwa mara kwa nyakati tofauti zilizopita,” linasema tamko hilo.

Pamoja na hilo, maaskofu hao walimtaka Waziri Membe, kujiuzulu wadhifa wake kutokana na hatua yake ya kujenga ushawishi wenye mwelekeo wa kidini wa kuiingiza nchi katika OIC.

Mbali ya hayo, tamko lilisema kuwa hatua ya Tanzania kujiunga OIC inakwenda kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 19 (2) na Sheria ya Vyama vya Siasa nchini.

Askofu Kitula alisema, wanapinga Tanzania kujiunga na OIC kwa maelezo kuwa, katiba ya jumuiya hiyo imejipambanua wazi kuwa na malengo ya kuendelea na kuulinda Uislamu, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa taifa, lenye watu wa imani nyingine za dini.

Akifafanua askofu huyo alisema, katika Ibara ya 1 (11) ya Katiba ya OIC, kuna kipengele kinachosomeka ‘kusambaza, kuendeleza na kuhifadhi mafundisho ya dini ya Kiislamu….kuendeleza utamaduni wa Kiislamu na kuulinda urithi wake’, maelezo ambayo ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ambayo inahimiza uhiari na uhuru wa mtu binafsi katika masuala yanayohusu kueneza dini au masuala ya imani.

Askofu Kitula ambaye alisoma tamko hilo kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCT, Akofu Donald Mtetemela, aliyesaini tamko hilo, alisema uamuzi wa kujiingiza katika masuala ya namna hiyo ni wa hatari, kwani yanaweza kuleta migogoro kutokana na kuwapo kwa dhana ya udini.

Maaskofu hao walimtaka Waziri Membe kuachana na kauli zake juu ya umuhimu wa kuingia kwenye jumuiya hiyo ya Kiislamu na kuhoji aliyemtuma kufanya hivyo.

CHANZO:Tanzania Daima

29 Oct 2008

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoa wa Dar es Salaam limewaonya maaskofu wa Jumuiya za Kikristo Tanzania (CCT) kutoitisha Serikali katika suala la kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu (OIC) na kuanzisha Mahakama ya Kadhi nchini wakitishia kuwa kitendo hicho ni uhafidhina na ugaidi. 

Tamko hilo limetolewa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Mussa Salum kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mara baada ya kikao cha masheikh na maimamu wa mkoa huo kujadili pamoja na mambo mengine, kauli ya maaskofu hao. 

"Waislamu tunasema suala la Tanzania kujiunga ama kutojiunga ni suala la Serikali ya Tanzania kwa maslahi ya wananchi wote," alisema Sheikh Salum. 

Sheikh Salum aliongeza kuwa suala la Mahakama ya Kadhi ni haki ya Waislamu wa nchini na wala halina mjadala kwa kuwa haliwahusu watu wa dini nyingine na kwamba mifano mingi ipo katika nchi mbalimbali juu ya kuwepo kwa mahakama hizo. 

"Mahakama hizi zilikuwepo tangu ukoloni, hivyo hili siyo suala la kuomba kuanzishwa kwake bali tunaiomba Serikali izirejeshe," alisema. 

Pia masheikh na maimamu hao walihoji uhalali wa kuwepo kwa Balozi wa Vatican hapa nchini kuwa anawakilisha nchi gani na kuliita kuwa suala hilo limegubikwa na udini lakini Waislamu hawakuwa wakihoji. 

"Tunawaonya maaskofu kuacha kuishinikiza Serikali mara kwa mara kuhusu masuala yanayohusu Waislamu na waache kupandikiza chuki kwa waumini wao juu ya suala la OIC na Mahakama ya Kadhi na waumini wa dini ya kiislamu kwa ujumla," alisema. 

Mwishoni mwa wiki iliyopita maaskofu 64 wa makanisa mbalimbali nchini walisaini waraka wa kumpinga Waziri Membe aliyekaririwa awali akiwataka Watanzania kutoogopa kujiunga na OIC kwani ni jumuiya yenye maslahi mazuri ya kiuchumi kwa taifa, akikariri utafiti uliofanywa na Serikali. 

Tayari BAKWATA makao makuu imeshatangaza kuitisha mkutano wa hadhara utakaofanyika kwenye viwanja vya Kidongo Chekundu kesho kueleza msimamo wake kuhusu suala hilo.

CHANZO: Majira

24 Oct 2008


Soma kwa makini stori hizi kisha make your own conclusion

STORI YA KWANZA:
Waziri Membe akana kuubeba msalaba OIC
Na Ramadhan Semtawa
WAZIRI wa Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernad Membe, amekuja juu akisema baadhi ya watu wamekuwa wakimtwisha mzigo kwamba, ameingiza Tanzania katika Jumuiya ya nchi za Kiislam Duniani (OIC), kitu ambacho si kweli.

Kauli hiyo ya Membe ni ya kwanza kuitoa hadharani tangu kuibuka kwa kasi kwa mjadala huo, ambao unaonekana kuigawa nchi katika misingi ya kiitikadi.

Akizungumzia hilo jijini Dar es Salaam jana, Membe alisema si kweli kwamba Tanzania imekwishajiunga na OIC na wala yeye hajasema lazima ijiunge.

Membe akifafanua huku akionekana kuguswa na tuhuma hizo dhidi yake kutokana na kutamka hilo bunge katika hotuba ya bajeti ya wizara yake, alisema uamuzi wa kujiunga au la, uko kwa wananchi.

"Nimekuwa kimya, kuachia na kusikiliza watu waseme, jamani, Tanzania haijajiunga na OIC wala sijasema lazima ijiunge," alisema na kuongeza:

"Uamuzi wa kujiunga au kutojiunga utakuwa chini ya wananchi, wasomi, NGOs na ninyi waandishi wa habari, ndiyo mtakaoamua."

Membe alikuwa akifafanua kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na Iran, ambao unaonekana na baadhi ya watu kama wenye nia ya kuingiza nchi OIC.

Akifafanua zaidi, alisema watu wasiingize vitu visivyokuwa na msingi kwa ajili ya kutunga na kuzungumzia hisia, na kushauri wasome historia kufahamu uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Membe huku akionekana kuchukizwa na fikra mbovu za kupandikiza udini katika nchi, alisema Watanzania ni watu wanaoheshimika duniani kwa umakini wao, ni aibu na haipendezi kujadili udini.

Alisema kama ni kujiunga na OIC ni jambo la kuamua, kwani Uganda ambako kuna Waislam asilimia 10 imeweza kujiunga huku Wakristo wakiwa ni asilimia 66 na wengine wapagani.

"Sasa jamani, msitake kunichinganisha na watu wangu, nawaambieni tena na tena, Tanzania haijajiunga na OIC na haitaweza kujiunga uamuzi huo ni ridhaa ya wananchi," alisisitiza.
CHANZO: Mwananchi

STORI YA PILI KUHUSU SUALA HILOHILO:
Waziri: Tanzania kujiunga OIC ni dhahiri
23 Oct 2008
By Muhibu Said

Tanzania inatarajia kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi za Kiislamu (OIC) wakati wowote katika siku zijazo baada ya serikali kuweka bayana azma hiyo jana.

Azma hiyo ya serikali iliwekwa bayana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Ali Iddi, alipozungumza na Nipashe jana, ikiwa ni wiki chache tangu Waziri wa Wizara hiyo, Bernard Membe, aliambie Bunge kwamba, hakuna madhara yoyote kwa Tanzania kujiunga na jumuiya hiyo.


Balozi Iddi alisema mchakato kwa Tanzania kujiunga na OIC, unatarajiwa kuanza wakati wowote na kwamba, hatua ya mwanzo ya mchakato huo, viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano watakutana na wenzao wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa ajili ya kupata msimamo wa pamoja kuhusu suala hilo.

Naibu Waziri huyo alisema hayo alipoulizwa na Nipashe kama mchakato kwa Tanzania kujiunga na OIC umeshaanza au la tangu Waziri Membe atoe kauli hiyo bungeni, mjini Dodoma, Agosti 22, mwaka huu.

``Bado hatujaanza mchakato. Kuna kikao tunachotaka kwanza kufanya kwa ajili ya kushauriana na wenzetu wa Zanzibar ili tuwe na msimamo mmoja kuhusu hilo. Ilikuwa tuanze sasa, lakini Mheshimiwa Waziri (Membe) hayupo na Bunge linatarajiwa kuanza,`` alisema Balozi Iddi.

Alisema mchakato kwa Tanzania kujiunga na OIC ni mrefu, ambao unatarajiwa pia kulishirikisha Baraza la Mawaziri kufikia maamuzi.

Balozi Iddi alisema hatua nyingine ya mchakato, ambayo serikali inatarajia kuichukua, ni kutoa elimu kwa umma ili kuwaondoa uoga wote walioonyesha hofu iwapo Tanzania itajiunga na jumuiya hiyo.

``Hao wanaopinga, ni waoga tu, hawajaeleweshwa kwani haina maana Tanzania itakuwa nchi ya Kiislamu. Zipo nchi kama vile Uganda zimejiunga na OIC, lakini hazijabadilika kuwa nchi za Kiislamu. Tutawaelewesha wakati ukifika, tunavyo vyombo vya kuelimisha hilo,`` alisema Balozi Iddi.

Agosti 22, mwaka huu Waziri Membe wakati akifunga mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, alisema hakuna madhara yoyote kwa Tanzania kujiunga na IOC.

Waziri Membe alisema serikali mwaka huu, ilifanya kikao na Baraza la Wawakilishi kuhusu suala hilo na kugundua kuwa nchi 21 zimejiunga na jumuiya hiyo.

Alisema kati ya nchi hizo, zimo pia nchi za Wakristo ambazo zimejiunga na hazijapata madhara yoyote.
``Tumeshakusanya takwimu za nje na kuona hakuna madhara yoyote ya kujiunga na IOC, bora tu kufuata taratibu,`` alisisitiza Waziri Membe.

Alisema suala hilo lilileta utata awali kwa sababu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, marehemu Ahmed Hassan Diria, alipeleka ombi la Zanzibar kujiunga kwenye jumuiya hiyo bila kuishirikisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, alisema suala hilo limefanyiwa kazi na serikali na kuona kuwa hakuna madhara kujiunga na IOC.

Siku chache baada ya Waziri Membe kutoa kauli hiyo bungeni, viongozi wa makanisa na baadhi ya wasomi, akiwamo Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Dk. Methodius Kilaini, walipinga vikali kauli hiyo ya serikali.

Wengine waliopinga suala hilo, ni Askofu Stefano Msangi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Pare, Askofu Mkuu wa Kanisa la KKKT Tanzania, Dk. Alex Malasusa, Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengodo Mvungi.

Hata hivyo, Imamu Mkuu wa Msikiti wa Mnyamani, Buguruni, jijini Dar es Salaam, Sheikh Mohammed Iddi, amekuwa akijitokeza kuwapinga maaskofu kuhusu kauli zao za kupinga suala hilo.
CHANZO:Nipashe

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.