Showing posts with label SITTA. Show all posts
Showing posts with label SITTA. Show all posts

8 Jun 2011






Mafisadi CCM wageuka mbogo

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 01 June 2011

SASA ni piga ni kupige ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wanakataa kujiuzulu, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema walipoitwa mbele ya viongozi wakuu wa chama hicho – makamu mwenyekiti Pius Msekwa na katibu mkuu, Wilson Mukama - wanaoitwa na CCM kuwa “watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini,” walishikilia msimamo kuwa hawawezi kujiuzulu kwa kuwa hawana hatia.

Wanaotakiwa kujiuzulu na viongozi wakuu wa CCM ni Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge. Mkutano wa kuwashawishi wajiuzulu, ulifanyika Alhamisi na Ijumaa wiki iliyopita katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo Lumumba, Dar es Salaam.
Taarifa zinasema katika mkutano huo, Msekwa na Mukama waliomba Lowasa ajiuzulu ili kukiokoa chama hicho, lakini yeye alipinga kwa hoja kuwa hana hatia.

MwanaHALISI lilipowasiliana na Msekwa kutaka kufahamu kilichojadiliwa katika mkutano wake na viongozi hao, haraka alisema, “…Umetoa wapi habari hizo?”

Alipoelewa ni vyanzo vya ndani ya chama na serikali, Msekwa alisema, “Hayo ni mambo ya ndani ya chama. Hatuwezi kuyaleta magazetini.”
Lowassa alipoulizwa juu ya kuwapo kwa kikao hicho, alisema ni kweli wamekutana. Hata hivyo, alisema hawezi kueleza walichojadili kwenye vyombo vya habari.

Rostam hakupatikana kueleza upande wake. Hata hivyo, MwanaHALISI limeelezwa na mtoa taarifa wake kuwa mbunge huyo wa Ingunga alitoka kwenye ukumbi wa mkutano akiwa amenuna na kuvurumisha “maneno makali.”

Anasema Rostam alitoka pale akiwa amenuna na kusema yeye hana hatia yoyote na kwa hiyo hastahili kushambuliwa. Amesema yote yanayotokea sasa yanatokana na uadui wa siasa za urais wa mwaka 2005 na ule wa 2015.


Hili linatokea wakati uongozi wa juu wa chama hicho ukishindwa kukabidhi barua ya kuwataka watuhumiwa hao wajiuzulu.
Kuchelewa kwa utekelezaji wa maazimio ya kuwawajibisha Lowassa, Rostam na Chenge kumezaa majungu na umbeya. Hivi sasa taarifa zinasema, Mukama anadaiwa kugoma kuandika barua ya kuwataka watuhumiwa hao kuachia nafasi zao za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) wanazozishikilia.

Baada ya Mukama kugoma kuandika barua hizo kwa hoja kuwa kilichoamuriwa na NEC hakifahamu kwa kuwa alikuwa hajateuliwa, ndipo Nape Nnauye, katibu wa itikadi na uenezi alipoandika barua hizo na kuzipeleka kwa Msekwa.

Naye Msekwa alizipokea barua na kuzirekebisha. Akazirejesha kwa Nape ili azipeleke kwa Mukama kuzisaini. Mukama akagoma. Zikapelekwa kwa mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, ambaye taarifa zinasema, “amezifungia kabatini.”

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya kikao hicho, Lowassa alifika Lumumba saa nne asubuhi. Mazungumzo kati yake, Msekwa na Mukama inakadiriwa yalichukua takribani saa moja.

Katika mazungumzo hayo, Msekwa ananukuliwa akimweleza Lowassa “unatakiwa ujiuzulu nyadhifa zako za uongozi katika chama ili kutekeleza maagizo ya NEC na falsafa ya chama ya kujivua gamba.”

Akijibu hoja hiyo, mtoa taarifa anasema Lowassa alijibu, “Kuhusu Richmond (kampuni feki ya kufua umeme wa dahurula), ukweli unafahamika…Katika hili, mimi sina makosa. Rais anafahamu hilo na kila mmoja anajua hivyo.”

Anasema Lowassa alisema kama kuwajibika kwa makosa yaliyotokana na Richmond tayari amefanya hivyo kwa niaba ya chama chake na serikali pale alipoamua kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri mkuu.
Anasema mbali na kueleza hilo, Lowassa alisikika akisema, “nilikutana na Rais Kikwete. Aliyonieleza si haya.”

Alisema Rais Kikwete alimweleza kuwa hakuna maazimio yoyote ya NEC yaliyomtaka kujiuzulu. Akahoji, “Sasa nimwamini nani, ninyi mnaotaka nijiuzulu au rais aliyesema hakuna azimio kama hilo?”

Habari zinasema mara baada ya Lowassa kuwaeleza viongozi wake msimamo juu ya mazungumzo yake na Kikwete, ndipo Msekwa aliposikika akisema, “Lowassa acha mbio za urais.”

Naye Lowassa hakumkawiza Msekwa. Alijibu, “Lini nimetangaza kugombea urais? Lakini hata kama ninataka kufanya hivyo, ni haramu kugombea nafasi hiyo? Je, kuna mliowaandaa?”

Ni kauli hiyo ya Lowassa, iliyomshutua Msekwa na kusema, “Hapana. Hapana. Hakuna tuliyemuandaa…Haya mambo ya urais yatatuvuruga.”
Akihitimisha hoja zake kabla ya kumalizika kwa mkutano huo, mtoa taarifa anasema Lowassa alikitaka chama chake kuisaidia serikali kutekeleza wajibu wake kwa wananchi, badala ya kufanyia kazi kile alichoita, “majungu ya wanasiasa.”

Naye Chenge taarifa zinasema aliwaambia viongozi aliokutana nao kuwa yeye si fisadi na hafahamu maana ya ufisadi. Akataka kama tuhuma wanazomtuhumu wanaweza kuzithibitisha wamfikishe mahakamani ili aweze kujitetea. Hakuna maelezo ya ziada.

Hata hivyo, watu waliokaribu na kiongozi huyo wanasema, Chenge amejipanga kuhakisha kwamba hang’oki katika kiti chake cha NEC; ikibidi kuondolewa kwa nguvu ametishia kuondoka CCM na kujiunga na upinzani.

Kwa upande wa Rostam Aziz, taarifa zinasema alitakiwa kujiuzulu ujumbe wa NEC kwa tuhuma za kuingiza nchini kampuni feki ya Richmond na baadaye Dowans.

Mtoa taarifa anasema, mara baada ya kuelezwa tuhuma hizo, Rostam alihoji, “Haya ni maamuzi ya NEC?” Naye Msekwa akajibu, “NEC imetaka chama kijivue gamba kuanzia ngazi ya taifa hadi chini kwa kuondoa watu wote wanaotuhumiwa ufisadi.”

Habari zinasema, katika mazungumzo kati ya viongozi hao na Rostam, hakuna mahali popote ambapo Msekwa na Mukama walitaja ushiriki wa mbunge huyo wa Igunga, katika wizi wa fedha za umma kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Kampuni ya Kagoda ni miongoni mwa makampuni 22 yaliyothibitika kuchota mabilioni ya shilingi kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Gazeti hili limeshindwa kufahamu mara moja kilichosababisha Msekwa na wenzake kushindwa kumweleza Rostam ushiriki wake katika Kagoda. Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka minne sasa, CCM imekuwa ikituhumiwa kunufaika na fedha za EPA hasa Sh. 40 bilioni zilizoibwa na Kagoda.

Wakati suala hilo likichukua sura hiyo, taarifa zilizofikia gazeti hili zinasema baadhi ya vigogo wa chama hicho wamepanga kupeleka hoja katika vikao vijavyo vya (CC) na (NEC) kushinikiza kufukuzwa ndani ya chama hicho wanaoitwa, “wasaliti ndani ya chama.”

Wanaopangiwa mkakati wa kufukuzwa ni spika wa zamani wa Bunge, Samwel Sitta na mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe wanaotuhumiwa kuanzisha Chama cha Jamii (CCJ) wakati wakiwa bado wanachama na viongozi wa CCM.

Wengine ni Nape Nnauye, Victor Mwambalaswa na Daniel Porokwa.
Habari kutoka ndani ya CCM zinawanukuu makada mawili; rais mstaafu, na mjumbe mmoja wa NEC wakitaka chama chao kuwafukuza waasisi wa CCJ kwa kukosa uaminifu.

MwanaHALISI limeelezwa na aliyekuwa naibu katibu mkuu wa CCJ, Dickson Ng’hily kwamba Sitta na Mwakyembe waliokuwa waanzilishi wa chama hicho, walimkatiza masomo yake nchini Afrika Kusini ili kusaidia kupatikana usajili wa chama hicho.

Ng’hily ambaye mahojiano yake yatachapishwa kikamilifu katika toleo lijalo amesema, aliyemwingiza yeye CCJ ni Sitta na Dk. Mwakyembe na anasikitishwa na hatua ya viongozi hao kutaka kuficha ukweli.

“Hawa watu ndio waanzilishi hasa wa CCJ. Mimi na Makonda tulipewa jukumu la kutafuta usajili wa chama. Lakini naona wenzangu wameamua kuficha ukweli kwa maslahi binafsi. Hii si sahihi,” ameeleza.

Ng’hily anaonyesha nyaraka za muhtasari wa vikao walivyoshiriki viongozi wakuu wa CHADEMA, John Mnyika, Anthony Komu na Tundu Lissu kuwa ni miongoni mwa watu walioshiriki katika majadiliano ya kuunganisha nguvu kati ya CCJ ya Sitta na CHADEMA.

“Tulikubaliana kama CCJ itakosa usajili, basi mheshimiwa Sitta atagombvea urais kupitia CHADEMA. Lakini kama tutafanikiwa kusajili chama chetu, basi Sitta angegombea urais kupitia CCJ na CHADEMA wangetuunga mkono,” anaeleza Ng’hily.

Kuibuka kwa Ng’hily kuelezea ushiriki wa Sitta na Dk. Mwakyembe katika kuanzisha na kusimamia usajili wa CCJ kumekuja wiki tatu baada ya Fred Mpendazoe kumtaja Nape Nnauye kuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa kwanza wa CCJ.

Mpendazoe aliuambia mkutano mkubwa wa hadhara mjini Njombe kuwa yeye, Sitta na Mwakyembe ndio walianzisha CCJ; bali yeye alitangulia kutoka CCM ili kurahisisha usajili wa chama hicho. Wenzake walikuwa wamfuate baadaye.

CHANZO: Mwanahalisi

5 Mar 2009

SAKATA la ununuzi wa mitambo ya ufuaji umeme wa dharura ya kampuni ya Dowans Tanzania Limited, jana lilimgusa spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta na kuamua kutoa tamko kali la kuitahadharisha serikali dhidi ya azma yake ya kutaka kuinunua mitambo hiyo yenye utata.

Spika Sitta pia ameonya kuwa mkasa wa kampuni tata ya Richmond Development (RDC) LLC uliotikisa kiasi cha kusababisha Edward Lowassa awajibike kwa kujizulu wadhifa wake wa waziri mkuu, lisifufuliwe upya kwa kutumia Dowans, ambayo ilirithishwa mkataba wa miaka miwili wa kufua umeme wa dharura.


Richmond ilishinda zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa njia iliyojaa utata kabla ya matatizo ya usajili wake kuzua maswali mengi na kusababisha Dowans warithishwe mkataba huo mwaka 2006.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Sitta alieleza nafasi ya Bunge katika kuisimamia na kuishauri serikali katika utekelezaji wa majukumu yake, huku akitaka ushauri wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wa kuizuia serikali isinunue mitambo hiyo uheshimiwe.

Sitta pia alisema Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma haikustahili kufuatwa katika kutaka ushauri kuhusu suala hilo kwa kuwa suala hilo lipo kwenye Kamati ya Nishati na Madini na kwamba kama kuna sababu mbadala, wasi ililazimika kuliwasilisha upya kwa kamati hiyo.

"Naitahadharisha serikali juu ya athari zinazoweza kujitokeza iwapo itaamua kuendelea na mchakato wa ununuzi wa mitambo ya Dowans kwa kupuuza ushauri uliotolewa na Kamati ya Nishati na Madini," alisema Spika Sitta.

Alisema: "Isisahaulike kwamba Dowans ni kampuni iliyopatikana kwa kurithishwa mradi na kampuni ya Richmond katika mazingira yenye utata ambao hadi leo ni kitendawili."

Spika Sitta alifafanua kuwa uhalali wa utaratibu wa Richmond kumkabidhi mradi Dowans ulitiliwa mashaka na kamati teule ya Bunge, na kuongeza kuwa Dowans na Richmond ni kama kitu kimoja.

"Dowans na Richmond ni mtu na binamu yake na si vigumu kukubali kuwa bado wao ni wabia hadi sasa: Pamoja na yote mkasa wa Richmond haufai kufufuliwaaa upya kupitia Dowans," alisisitiza Sitta.

Aliongeza kuwa kama kweli Tanesco na serikali inazo Dola 69 milioni za Kimarekani (sawa na Sh90 bilioni za Kitanzania) ambazo ni bei ya mtambo wa Dowans, ingezitumia fedha hizo kama sehemu ya malipo ya kununua mitambo mipya. Alisema Tanesco ingetafuta ushauri kutoka Mamlaka ya Ununuzi Serikalini (PPRA) ili taratibu za dharula zitumike kununua mitambo mipya kukabiliana na "dharula inayotabiriwa".

Sitta alihoji mantiki itakayotumiwa na Tanesco kutaka kununua mitambo ambayo inamilikiwa na kampuni ambayo imeishtaki kwenye Baraza la Usuluhishi ambalo makao yake makuu yako Paris, Ufaransa.

"Gharama za mitambo na gharama za kuikodi haviwezi kuepukwa kuwa ni sehemu ya shauri lililo Paris," anasema Sitta. "NI kwa mantiki ipi kesi baina yao iendelee na hapo hapo mdaiwa (Tanesco) anunue mitambo kutoka kwa mdai (Dowans.

"Tanzania ilikuwa ikilipa Dowans shilingi za Kitanzania milioni 152 kwa siku (Dola 120,000) sawa na Dola 42 milioni kwa mwaka).

"Pamoja na yote, mkasa wa Richmond haufai kufufuliwa upya kupitia Dowans. Tanesco/serikali waelekeze nguvu zao katika njia mbadala za kulipatia taifa umeme wa dharura, badala ya njia hii ya Dowans iliyojaa utata."

Kuhusu mvutano kati ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma na ile ya Nishati na Madini, Spika Sitta amsema si sahihi kwa kamati yoyote ya Bunge isiyo ya sekta husika, kutoa maoni yake hadharani na kuishawishi jamii kwamba Bunge lina ushauri unaopingana kuhusu suala husika.

"Si sahihi kwa Kamati yoyote ya Bunge isiyo ya sekta kutoa maoni yake hadharani na kujenga taswira kwa umma kwamba, Bunge lina ushauri unaokinzana kuhusu suala lililo mbele yake. Kamati nyingine, haina budi kupitisha ushauri na maoni yake kwenye kamati ya kisekta," alisema Sitta.

Zitto Kabwe, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, alikaririwa na vyombo vya habari akieleza msimamo wa kamati yake kuunga mkono Shirika la Umeme (Tanesco), kuinunua mitambo ya Dowans kwa maelezo kuwa hatua itasaidia kulinusuru taifa katika janga kubwa la kukosa umeme na kwamba sheria ya manunuzi si msahafu, hivyo inaweza kubadilishwa.

Lakini Kamati ya Nishati na Madini, ambayo mwenyekiti wake ni William Shelukindo, inapinga hatua hiyo ikieleza kuw ainakiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma, inayokataza serikali kununua vitu ambavyo tayari vimetumika.

Alisema ushauri kwa serikali kuhusu Tanesco kununua au kutonunua mitambo ya Dowans ulikwishatolewa kwa Wizara ya Nishati na Madini na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Desemba 14 mwaka uliopita.

"Huo ndiyo ushauri rasmi na sahihi wa Bunge ninaoutambua. Kwa msingi huo hoja ya kuzikutanisha Kamati hizi mbili (ya Nishati na Madini na ya Hesabu za Mashirika ya Umma) ili kurejea uamuzi au maoni yaliyokwishatolewa na Kamati inayohusika, haina msingi," alisema Sitta.

Alisema mkondo rasmi wa ushauri kwa serikali uliokusudiwa kwenye Ibara ya 63 (2) ya katiba ikisomwa na pamoja na kanuni za Bunge za mwaka 2007 ni kupiti Bunge zima au kamati zake za kisekta kila kamati na sekta yake.

Wakati Spika Sitta akibainisha msimamo wake na wa Bunge, mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba ameunga mkono ununuzi wa mitambo hiyo huku akisema kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa jana inaweza kukwamisha mchakato wa ununuzi wa mitambo hiyo.

Lipumba alisema katika mfumo wa utawala bora wakati kamati za bunge zinazohusika na mambo hayo na bodi za mashirika zipo, rais hapaswi kujiingiza mapema katika mijadala.

“Katika mfumo wa utawala bora ambao una kamati za bunge zinazohusika na sekta ya umeme na manunuzi, kwa rais kujiingiza kunaweza kuwa ni kikwazo cha mchakato mzima wa ununuzi wa mitambo,” alisema Profesa Lipumba.

Alifafanua kuwa, sheria ya manunuzi ya Serikali ina upungufu kwa kuwa inalazimisha ununuzi wa mitambo mipya, jambo ambalo haliwezekani kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania.

“Ununuzi wa mitambo ya kibiashara katika sekta ya biashara huwezi kulazimisha ununuzi wa mitambo mipya hususan katika nchi zinazoendelea kama ya kwetu. Jambo la msingi ni kuangalia uwezo wa mitambo katika kufanya kazi na si kwamba ni mipya au mikongwe,” alifafanua Lipumba na kuongeza:

“Sheria yetu ya manunuzi ni nzuri na inafaa sana kwa kununua vitu vya huduma za serikali, kama magari na vifaa vingine.”

Aliitaka Tanesco kuwa wazi kwa kuwa ni wao waliosema mitambo hiyo hawaitaki hivyo kuamuwa kuvunja mkataba na Dowans iweje leo wanageuka na kusema mitambo hiyo ni mizuri na kuitaka serikali iinunuwe.

“Tanesco walituambia kuwa mitambo hiyo hawaitaki na walivunja mkataba na Dowans, sasa inakuaje leo wanageuka na kusema kwamba mitambo hiyo ni mizuri na inunuliwe kwa ajili ya kuzalishia umeme? Tunahitaji uwazi zaidi kutoka Tanesco,” alihoji Profesa Lipumba.

Naye Stephen Menad ambaye ni mshauri wa masuala ya nishati na mazingira, alisema hakuna kitu kipya kwenye mitambo hiyo ya Dowans hivyo isinunuliwe na badala yake itafutwe mipya ili kuondoa mvutano baina ya wananchi na serikali.

Mussa Hassan, mkazi wa jijini Dar es Salaam ambaye ni mfanyabiashara, alisema ni aibu kwa serikali kula matapishi na kwamba viongozi wasisahau yaliyotokea wakati mitambo ya Richmond ilipokuja na mwisho wake kuwaweka pabaya viongozi waliokuwa serikalini.

Anthony Chambi, ambaye ni mfanyabiashara katikati ya jiji la Dar es Salaam, alisema hataki kusikia kuhusu mitambo hiyo kwa kuwa tayari ilishaiabisha serikali. Alisema anasikia kuna kesi Ufaransa kuhusu mitambo hiyo kitu kinachomshangaza kwa nini serikali inataka kununua mitambo ambayo ina kesi.
CHANZO: Mwananchi
BIG UP,MHESHIMIWA SPIKA.
BINAFSI HADI MUDA HUU SIELEWI HAO WANAOTAKA MITAMBO YA DOWANS INUNULIWE WANA AJENDA GANI!NACHANGANYWA ZAIDI NAPOSIKIA WATU KAMA ZITTO KABWA NA PROFESA LIPUMBA NAO WAKIPIGA DEBE MITAMBO YA DOWANS INUNULIWE.HUU NI UNAFIKI WA MCHANA KWEUPE.WHY?BECAUSE KUNUNUA MITAMBO HIYO NI KUHALALALISHA UJAMBAZI WA DOWANS NA KAKA YAKE RICHMOND.HIVI INAINGIA AKILINI KWELI PALE TAPELI ANAPOKUUZIA MALI FEKI KISHA UKAMKALIA KOONI MPAKA AKAKIRI KUWA KWELI ALICHOKUUZIA NI FEKI,HALAFU UKAISHIA KUONGEZA FEDHA KUNUNUA MALI HIYO FEKI!?
I WOULD ONLY SUPPORT MATUMIZI YA MITAMBO YA DOWANS LAITI INGEKUWA IMETAIFISHWA (NA SIJUI KWANINI HADI MUDA HUU HAIJATAIFISHWA...WE MISS YOU BABA WA TAIFA).ETI AKINA KABWE WANASEMA TUWEKE MBELE UTAIFA KWANZA!UTAIFA KWANZA KWA MANUFAA YA AKINA RICHMOND?HAWA WAMEINGIZWA MKENGE NA VITISHO VYA TANESCO KUWA ETI NCHI IKO HATARINI KUINGIA KIZANI!YALEYALE YA RICHMOND!
WIZI MTUPU!

10 Sept 2008

Pamoja na kuchukua sabbatical leave ya lazima katika uandishi wa makala katika gazeti la Raia Mwema,blogu hii itaendelea kuwaletea kinachojiri kila wiki katika jarida hilo mahiri huko nyumbani.Miongoni mwa habari zilizochukua uzito wa juu katika toleo la wiki hii ni pamoja na kauli ya Spika wa Bunge la Muungano,Samuel Sitta,kwamba amejiandaa vya kutosha kufuatia taarifa kwamba watuhumiwa wa ufisadi wameingiza sumu huko Bongo kwa lengo la kuwadhuru Sitta na Mbunge wa Kyela,Dr Harrison Mwakyembe.Sidhani kama inahitaji kujumlisha mbili na mbili kupata jawaba as to akina nani watakuwa the usual suspects wa unyama wa aina hii.Zaidi BONYEZA HAPA kusoma habari hiyo na nyingine motomoto.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.