Showing posts with label SNP. Show all posts
Showing posts with label SNP. Show all posts

24 Sept 2014

Scotland's First Minister and leader of the Scottish National Party (SNP) Alex Salmond (C). (Reuters/David Moir)
Chama tawala hapa Uskochi cha Scottish Nationalist Party (SNP) kimekuwa chama cha tatu kwa ukubwa kwa Uingereza nzima baada ya kuvuna wanachama wapya kwa asilimia 66% katika muda wa siku nne tu baada ya kushindwa katika kura ya uhuru wa Uskochi.

Jumla ya wanachama wapya 26,000 wamejiunga na chama hicho tangu Alhamisi iliyopita, na hivyo kutunisha idadi ya wanachama wake hadi kufikia zaidi ya 51,000, takriban maradufu ya idadi ya awali ya wanachama wake.

Takwimu hizo zimeleta mshangao mkubwa kufuatia kambi ya 'Ndiyo' iliyokuwa ikiongozwa na chama hicho tawala kushindwa katika kura ya uhuru kwa asilimia 45 kwa 55, na hatimaye kiongozi wake, Waziri Mkuu wa Uskochi, Alex Slmaond, kutangaz aanaachia ngazi mwezi Novemba mwaka huu.

Takwimu hizo pia zinamaanisha kuwa SNP imefanikiwa kuvuta asilimia 10 ya ya wakazi wa Uingereza nzima, na kuipiga kikipiga kikumbo chama cha Liberal Democrats kwa idadi ya wanachama wenye kadi za uanachama.

Wabunge wa chama hicho waliokutana Hollyrood, katika mji mkuu Edinburgh, walionyesha kuridhishwa na takwimu hizo mpya na mwelekeo wa jumla wa Uskochi kufuatia kura ya aidha Uskochi iwe huru au iendelee kubaki sehemu ya muunganowa Uingereza.

"Devolution (kuipatia Uskochi mamlaka zaidi badala ya uhuru) ililenga kuua utaifa (wa Uskochi)," alisema mbunge mmoja wa SNP. "Kisha matokeo ya kura ya uhuru na kujiuzulu kwa Salmond. Lakini matokeo yamekuwa kinyume kabisa."

Inadaiwa pia kuwa wanachama wapya 3000 wamejiunga chama cha Scottish Greens huku chama kingine cha Scottish Socialist Party kikivuatia wanachama wapya. Vyama vyote hivyo viwili vilikuwa vikisapoti uhuru wa Uskochi.

Jumla mpya ya idadi ya wanachama wa SNP ilikuwa 50000 mnamo saa 6 na dakika 40 jana, kulinganisha na wanachama 25642 Alhamisi iliyopita siku ya upigaji kura ya uhuru.

CHANZO: Imetafsiriwa kutoka vyanzo mbalimbali mtandaoni

1 Jun 2012


Ya Zanzibar si mageni, hata Uskochi yapo
Evarist Chahali
Toleo la 241
30 May 2012


WIKI iliyopita, Waziri wa Kwanza (First Minister, cheo ambacho ni kama Waziri Mkuu) wa Uskochi, Alex Salmond, alizindua kampeni za chama chake cha Scottish Nationalist Party (SNP) kuhamasisha kura ya ‘Hapana’ katika referendum (kura ya maoni ) ya uhuru wa nchi hii inayotarajiwa kufanyika huko mbeleni.
Hoja ya Uskochi kujitenga na Uingereza (kwa maana ya kile kinachoitwa The United Kingdom of Great Britain-England, Uskochi na Wales- and Northern Ireland) imekuwa ikivuma kwa muda mrefu na imepata nguvu zaidi baada ya Salmond na SNP yake kuingia madarakani mwaka 2007.
Kimsingi, sera kuu ya mwanasiasa huyo na chama chake ilikuwa kuhakikisha kuwa hatimaye Uskochi inajitenga kutoka Uingereza.
Walipoingia madarakani tu, SNP walieleza bayana kuwa wana mpango wa kufanyareferendum kusikia maoni ya Waskochi kuhusu wazo hilo la kujitenga.
Hata hivyo, kikwazo ambacho wamekuwa wakikumbana nacho tangu mwanzo ni ukweli kwamba pamoja na tofauti za hapa na pale, ni vigumu kuchora mstari unaoweza kuwatenganisha Waskochi na Waingereza wengine.
Mwingiliano katika takriban kila nyanja ya maisha unawafanya watu hawa kuwa wamoja zaidi kuliko tofauti.
Na wakati naandaa makala hii, Salmond amepata ‘habari mbaya’ kutoka kwa mwendesha kura za maoni (pollster) maarufu hapa Uingereza, Peter Kellner, Rais wa taasisi ya kura za maoni ya YouGov.
Kwa mujibu wa Kellner, kura ya maoni iliyoendeshwa na YouGov Ijumaa iliyopita inaonyesha kuwa wakati ni asilimia 33 tu ya Waskochi wanataka ‘uhuru’ (kujitenga), asilimia 57 wanataka Uskochi iendelee kubaki sehemu ya Uingereza.
Mwendesha kura za maoni huyo amemtahadharisha Salmond kuwa ‘ana mlima mrefu wa kupanda’ kubadili upeo wa wengi wa Waskochi kuhusu nchi yao kujitenga na Uingereza.
Kadhalika, alieleza kuwa kuna ‘vitisho’ kadhaa vinavyoweza kuchangia Waskochi wengi kupinga wazo la kujitenga, na akatoa mfano wa hoja kama wawekezaji kujiondoa Uskochi (kwa kutokuwa na uhakika kama Uskochi itamudu ‘kusimama yenyewe’),  kupoteza ruzuku inayotolewa na Serikali Kuu ya Uingereza (ambayo ni kubwa zaidi ya kodi inayolipwa na Uskochi), matumizi ya sarafu ya pauni ya Kiingereza (British Pound) ambapo kama Uskochi itaamua kutumia sarafu hiyo baada ya kujitenga, Uingereza inaweza kuanzisha hatua za ukalifu (austerity measures) zitakazoathiri uchumi wa Uskochi.
Kadhalika, Salmond ametahadharishwa kwamba hofu nyingine zinazoweza kuwatisha Waskochi kuunga mkono wazo la kujitenga ni pamoja na gharama kubwa za kuendesha nchi kamili (hasa katika kipindi hiki ambapo uchumi wa dunia unayumba) kama vile kumudu kuwa na jeshi kamili, ofisi za ubalozi nchi za nje na gharama za uendeshaji wa taasisi za utumishi wa umma (civil service).
Kimsingi,  katika zoezi lolote lile la kupiga kura, hali ya kutokuwa na uhakika au hofu ya “huko mbele hali itakuwaje” inatosha kuwafanya wapiga kura wengi kuamua kubaki na chama kilichopo au muundo uliopo (iwapo ni referendum ya jambo fulani).
Mbinu hii inatumiwa sana na vyama tawala (ikiwa ni pamoja na CCM) kwenye chaguzi ambapo ujumbe huwa mithili ya ‘zimwi likujualo halikuli likakwisha’ (kwa maana ya chama unachokifahamu ni bora zaidi ya kile kinachoahidi tu pasipo kuwa na mifano hai ya uongozi wa nchi).
Hata hivyo, Salmond na SNP yake wanaendelea na jitihada zao huku wakijipa imani kuwa utajiri mkubwa uliopo Uskochi (kuna mafuta huko Bahari ya Kaskazini) utawezesha kumudu gharama za kuendesha nchi endapo Waskochi wataafiki wazo la kujitenga na Uingereza.
Wakati hayo yakijiri hapa Uskochi, mwishoni mwa wiki huko nyumbani kumekumbwa na habari za kusikitisha ambapo maandamano ya kupinga Muungano huko Zanzibar yaligeuka kuwa machafuko makubwa.
Kama nilivyoeleza katika ujumbe wangu wa Makala za Sauti (Audio Messages, unaoweza kusikia hapa http://goo.gl/r6ngT ), machafuko hayo huko Zanzibar na suala zima la Muungano vinapaswa kuangaliwa kwa mtizamo mpana zaidi.
Binafsi, ninaona kuwa asili ya tatizo la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni waasisi wake, yaani Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume. Hapa naomba nieleweke vizuri.
Wazo la Muungano lilikuwa zuri kwa kuzingatia sababu mbalimbali, kubwa zaidi ikiwa ni ukaribu wa asili za watu wa Bara na wa Visiwani.
Lakini tatizo ambalo pengine lilichangiwa zaidi na mazingira ya kisiasa wakati huo, Nyerere na Karume walidhani kuwa ridhaa yao ilikuwa inawakilisha ridhaa ya Watanganyika na Wazanzibari wote.
Kuna ‘busara’ moja ya Kiingereza inayosema kuwa “jambo zuri si lazima liwe na manufaa. Kwa mfano, wakati kumpa chakula kingi mtu mwenye njaa ni jambo zuri lakini matokeo yake yanaweza kupelekea hata kifo kwenye mtu huyo mwenye njaa kali aliyeishia kupewa chakula kingi.”
Ndiyo, kula chakula kingi ukiwa na njaa kali ni hatari, na ndiyo maana watu wanapofunga au wakiwa hawajala muda mrefu huanza mlo kwa kinywaji cha moto (uji au chai).
Sasa, wazo la Muungano lilikuwa zuri lakini kutosaka ridhaa ya wengi ndiko kumetufikisha hapa tulipo sasa. Kwa muda mrefu kumekuwa na manung’uniko kuhusu Muungano, hususan miongoni mwa Wazanzibari.
Hoja kuu imekuwa ni kwamba wanapunjwa, wanaonewa na wengine wanakwenda mbali zaidi na kudai lengo la Muungano lilikuwa ‘kuimeza Zanzibar.’
Kwa bahati mbaya, siasa za Zanzibar zina tofauti kwa kiasi fulani na za Bara. Kwa Visiwani, dini ina nafasi ya kipekee katika siasa. Kwa hiyo, mara nyingi masuala ya kisiasa yanaweza pia kubeba hisia za kidini, jambo ambalo pasipo uangalifu linaweza kuzua balaa kubwa.
Ninapenda kusisitiza kuwa pamoja na hatari zinazoweza kujitokeza kwa kuchanganya dini na siasa, uzoefu na historia vimeonyesha kuwa laiti busara na maslahi ya jamii yakiwekwa mbele ya hisia binafsi, dini inaweza isiwe na madhara katika siasa.
Huko Marekani, kwa mfano, dini bado ina nafasi ya kipekee. Pengine mfano mzuri zaidi ya namna dini inavyoweza kutoharibu siasa ni Ujerumani ambapo chama cha Kansela Angela Merkel (Christian Democratic Union-CDU) ni cha Kikristo. CDU ndio chama kikubwa zaidi cha siasa katika taifa hilo tajiri.
Kadhalika, chama kinachotawala nchini Uturuki, Justice and Development Party-AKP, ni chama cha Kiislamu. Hata hivyo, chama hicho kimefanikiwa kuifanya Uturuki iendelee kuwa taifa lisiloelemea kwenye siasa zinazoongozwa na dini.
Hata hapa Uingereza, Malkia ambaye ndiye mkuu wa nchi (kiheshima zaidi kuliko kiutendaji) pia ni Mkuu (kiheshima) wa Kanisa la Anglikana, na japo Ukristo ni kama ‘dini ya taifa’ lakini nchi hii inaendeshwa kwa sheria za ‘kidunia’ na si za kidini.
Hata hivyo, tatizo la dini ni ukweli kwamba licha ya kugusa hisia binafsi za muumini, mambo ya kidini hayahitaji uthibitisho wa kisayansi (au kidunia).
Tofauti na dini, siasa ni suala la itikadi zaidi kuliko imani (japo imani kwenye itikadi inaweza kuwafanya wafuasi wa chama kukiona kina umuhimu kama dini). Kadhalika, masuala ya dini yanahusisha ‘maisha ya baadaye baada ya haya ya duniani’ ilhali siasa imejikita zaidi kwenye masuala ya sasa au ya hapahapa duniani.
Balaa linakuja pale muumini wa dini anapoanza kuamini kuwa anapopinga Muungano,  kwa mfano, anafanya kazi ya kiroho na inampendeza Muumba. Ni vigumu sana kumdhibiti mtu wa aina hii kwani hata harakati zake zikihatarisha maisha yake, au akaishia kufa, anaamini kuwa atalipwa na Muumba wake.
Kimsingi machafuko yaliyotokea Zanzibar yamechangiwa zaidi na wanasiasa wetu ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wanachelea kile kinachofahamika kama ‘kuogopa laana ya waasisi wa Muungano pindi Muungano huo ukiwavunjikia mikononi mwao.’
Badala ya kuzishughulikia kero za Muungano na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu, watawala wetu wamekuwa wakijikita zaidi kwenye kujaribu kutuaminisha kuwa wanalishughulikia suala hilo kwa dhati ilhali wanaligusa juu juu tu.
Tumekuwa na Tume ya Kero za Muungano miaka nenda miaka rudi lakini ufanisi wake umekuwa wa kufikirika zaidi kuliko uhalisia.
Tuache unafiki, ‘kelele’ za kudai mabadiliko ya muundo wa Muungano (na hata hizo za kutaka uvunjiliwe mbali) haziwezi kwisha kwa kuzipuuza au kuwa na ‘tume ya milele’ ya kushughulikia kero hizo pasipo kuja na ufumbuzi.
Lakini kingine ni kuwanyamazia mafashisti wanaohubiri chuki dhidi ya wenzao kwa kisingizio cha kero za Muungano. Huko Zanzibar, baadhi ya wanasiasa wamediriki kudai ni Wabara wanaosababisha Wazanzibari kukosa ajira. Lakini huo ni mlolongo tu wa shutuma za aina hiyo, kwani huko nyuma Wabara walishawahi kutuhumiwa kuwa ndio waliopelekea ukimwi Visiwani humo.
Kwa vile hadi wakati huu ninaandaa makala hii bado hali huko Visiwani haijatulia, naomba nihitimishe kwa kutoa pendekezo la umuhimu wa kuwa na kura ya maoni itakayofidia kosa lililofanywa huko nyuma la kusaka ridhaa ya wananchi kuhusu Muungano.
Kama kura hiyo ya maoni itaamua tuwe na serikali tatu, basi hilo liheshimiwe. Kama itaamuliwa Muungano uvunjwe, basi na iwe hivyo (by the way, kuvunjika kwa Muungano hakutomaanisha kufa kwa Tanzania Bara au Zanzibar, kama ambavyo kuvunjika kwa ndoa hakumaanishi kifo kwa mume au mke aliyetalikiana na mwenzie).
Mwisho kabisa, wakati nikiwasihi viongozi wetu kuharakisha kura ya maoni ninayoamini itasaidia kuleta ufumbuzi wa kudumu wa matatizo ya Muungano wetu, ni muhimu kabisa kwa Serikali zote mbili (ya Muungano na ya Zanzibar) kuchukua hatua kali dhidi ya magaidi waliogeuza ‘madai halali kuhusu Muungano’ kuwa sababu ya kuwashambulia Wabara na kuchoma moto makanisa na mali zake.
Wanachofanya wahalifu hawa hakilengi kusaka suluhu ya Muungano bali wanapenda mbegu za uhasama wa kidini kati ya Wakristo na Waislamu.
Mungu Ibariki Tanzania


2 Nov 2007

Ama kweli ni rahisi kupanga sera na kutegemea ifanikiwe lakini ni habari nyingine kwa mpanga sera kuwa sehemu ya utekelezaji huo.Hilo limejihidhirisha katika taarifa kutoka nchini Marekani ambapo maafisa wa mambo ya nje wa nchi hiyo wamefahamishwa kwamba watakuwa wakipelekwa nchini Irak kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.Pamoja na kukumbushwa kwamba wakati wanakubali ajira waliapa kufanya kazi mahala popote watakapopangiwa na mwajiri wao,maofisa hao wameonekana kutoafikiana na pango huo ambapo baadhi yao wamefikia hatua ya kuuita “mpango wa kujipeleka kwenye hukumu ya kifo” hasa kwa vile “ziara” za aina hiyo tayari zimeshagharimu maisha ya maofisa watatu tangu kuanza kwa vita ya Irak.Maofisa wanaokaidi agizo hilo wanakabiliwa na hatari ya kuchukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.Nadhani pamoja na hatari inayoweza kuwakabili maofisa wanaopelekwa huko,nadhani utekelezaji wa agizo hilo utawasaidia kufahamu namna hali halisi ilivyo kwenye uwanja wa mapambano ni ambayo ni ngumu zaidi kuliko urahisi wa kuandaa sera,mikakati na mipango mizuri.



Kwa hapa UK,moja ya masuala ambayo kwa siku kadhaa sasa yametawala duru za habari ni kuhusu “Muungano” wa Uingereza (the United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland). Kumekuwa na mjadala wa muda mrefu kuhusu mambo makuu mawili: kwa upande mmoja ni umuhimu wa Muungano huo (miongoni mwa wale wanaopendelea kuona unadumu milele) na upande mwingine ni hoja kwamba muungano huo unazipunja baadhi ya sehemu zinazounda nchi hii.Katika uchaguzi mkuu uliopita,chama tawala cha Labour kilibwagwa na chama cha SNP (Scottish National Party) kwa upande wa Scotland.Hofu ya awali kwa Labour na “wapenda Muungano” baada ya ushindi wa SNP ilikuwa kwenye ukweli kwamba miongoni mwa malengo ya muda mrefu ya SNP ni kuiona Scotland ikiwa nchi huru inayojiendesha pasipo kuelekezwa na “serikali” ya London.Na katika manifesto yao ya uchaguzi,SNP hawakuogopa kutamka bayana matamanio yao uhuru wa Scotland.Chama hicho kilikuwa kinaelewa bayana kwamba sera hiyo ingeweza kuwapatia ushindi au kushindwa kwenye uchaguzi huo,kwani suala la uhuru wa Scotland ni miongoni mwa mambo yanayowagawa sana watu hawa.Kura mbalimbali za maoni kuhusu suala hilo zimekuwa na matokeo yanayothibitisha mgawanyiko huo,ambapo takriban nusu ya Waskotishi wanadhani uhuru ni wazo zuri huku takriban nusu nyingine wakipinga wazo hilo.Jeuri ya madai ya uhuru inachangiwa na kile Waskotishi wengi wanachokiona kama utajiri katika eneo hili (mafuta) ambao wanadhani unapaswa kuwanufaisha zaidi wao sambamba na kuwa na maamuzi ya namna ya kutumia utajiri huo badala ya kusubiri maelekezo kutoka England.Lakini wapo wanaoonya kwamba Scotland haiwezi kujimudu yenyewe kwa kutegemea tu utajiri wa mafuta,na baadhi ya wachumi wamekwenda mbali zaidi kwa kuonyesha pengo la bajeti litakaloikumba Scotland pindi ikijitoa kwenye Muungano huu.

Mjadala bado unaendelea na ni vigumu kusema bayana iwapo uhuru utapatikana au Muungano utaendelea.Majuzi,kiongozi wa chama pinzani cha Conservatives,David Cameron amewasha tena moto kuhusu suala hilo baada ya kutamka kwamba ana nia ya kusukuma sheria itakayowabana wabunge wa Scotland waliopo kwenye bunge la jumla la Uingereza (yaani linalojumuisha wabunge wa England,Wales,Scotland na Northern Ireland) wasipige kura kwenye masuala yanayoihusu England pekee.Hili ni suala linalujulikana kama “the West Lothian Question” (jina linalotokana na swali lililoulizwa mwaka 1977 na mbunge wa jimbo la Scotland la West Lothian,Tam Dalyell,wakati wa mjadala wa bunge kuhusu kuanzisha serikali-devolved governments-za Scotland na Wales).Swali hilo lilihusu uhalali wa wabunge wa “nchi” hizo mbili kushiriki katika mijadala na maamuzi yanayowahusu watu wa England pekee,ilhali wabunge wa England hawana nafasi kama hiyo kwa vile hawaingii kwenye mabunge ya sehemu hizo.Chama cha Labour kimemshutumu Cameron kwa kile walichokiita sera za kuvunja Muungano lakini kwa vyovyote vile hoja hiyo ni habari njema kwa Alec Salmond (First Minister wa Scotland) na chama chake cha SNP pamoja na wale wote wanaotaka uhuru.

Na kuna mambo yanayoshangaza kuhusu Muungano huu.Kwa mfano,wakati noti zinazotolewa na benki ya England (English Pounds) zinatumika nchi nzima,na zinakubalika mahala popote duniani kama sarafu halali ya nchi hii,noti zinazotolewa na mabenki ya Scotland (ambazo zina thamani sawa na English pounds) zinakataliwa katika baadhi ya maeneo ya England.Nilipokuja huko nyumbani mwaka jana,nilishindwa kabisa kubadilisha Scottish pounds na ilinilazimu nizitume huku ili zibadilishwe kuwa English pounds.Sheria za elimu ya juu na huduma za afya pia zinatofautiana kwa namna flani,ambapo kwa Scotland huduma nyingi zinatolewa bure ilhali kwa England zinaendelea kulipiwa.Scotland pia imekuwa ikilalamikia suala la uhamiaji ambapo sheria zinazotawala ni zile za nchi nzima ilhali mahitaji ya “nguvu-kazi” kutoka nje (kupitia uhamiaji wa wageni) unaathiriwa na sheria “kali” zinazotawala nchi zote zilizopo kwenye Muungano huu. Wakati Scotland imekuwa ikiendesha program kadhaa za kuvutia wageni,ikiwa ni pamoja na kuwashawishi wale walio hapa waifanye “nchi” hii kuwa makazi ya pili (second home) au makazi ya kudumu,kelele za wanasiasa huko England ni kwamba wageni wamezidi na lazima serikali idhibiti zaidi wahamiaji.

Masuala ya muungano ni nyeti na yamekuwa chanzo cha matatizo katika sehemu mbalimbali duniani.Lakini tofauti na wenzetu hawa ambao wanadiriki kutoa mawazo yao hadharani na kukaribisha mijadala kuhusu suala hilo,huko nyumbani kuzungumzia kuhusu Muungano inaelekea kuwa sio wazo la busara sana kwa mwanasiasa anayotaka mafanikio.Kuna kile kinachoitwa “jinamizi la Mwalimu kwa atakayetaka kuvunja Muungano” ambacho kimsingi nakiona ni kama kikwazo kwa wale wote wanaodhani kwamba ni muhimu kuwa na mjadala kuhusu hatima ya Muungano wetu.Tukiendelea kuogopa kuujadili,yayumkinika kusema kwamba tunautengenezea mazingira mazuri ya kuuharibu.Sio siri kwamba wenzetu wa Visiwani wamekuwa wakipiga kelele sana kwamba Muungano unawaumiza,lakini hofu yangu kubwa ni pale wenzao wa Bara nao “watakaposhikilia bango” hoja hiyo ya kuumizwa na mzigo wa Muungano.Na “the West Lothian Question” ya Uingereza “ina-fit” kabisa mazingira yalivyo huko nyumbani ambapo wabunge kutoka Zanzibar wamekuwa wakishiriki (katika bunge la Muungano) katika kujadili na kutoa maamuzi katika baadhi ya mambo ambayo yanayowahusu Wabara pekee ilhali wabunge wa Bara hawana nafasi hiyo kwani hawaingii kwenye Baraza la Wawakilishi huko Zanzibar.

Nafahamu kuwa kuna kitu kama “tume” au “kamati” iliyoundwa kujadili kero za Muungano,lakini japo sijui imefikia hatua gani katika majadiliano yao,yayumkinika kusema kwamba kasi nzima ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu suala hilo sio ya kuridhisha.Pengine katika kuepuka maamuzi yanayotoka juu kwenda chini (yaani kutoka kwa viongozi kwenda kwa wananchi) japo waathirika au wafaidika wakubwa ni hao wa chini,sio wazo baya kufikiria kuitisha kura ya maoni ili kupata mawazo ya wadau wakubwa wa Muungano huo (wananchi).Ashakum si matusi,lakini ni vema Muungano ukavunjika kwa ridhaa kuliko ukadumu kwa manung’uniko,kwani manung’uniko hayo yasipopatiwa tiba yanaweza kabisa kuuvunja Muungano huo pasipo kusubiri ridhaa ya wadau.Kikubwa nilichojifunza katika mjadala wa Muungano wa Uingereza ni namna ambavyo unavyoendeshwa kwa uwazi na upana zaidi kiasi kwamba sauti zote,zinazopinga na kukubali suala hilo,zinasikika waziwazi.Ukiniuliza iwapo Muungano wetu ni muhimu,jibu nitakalokupa hata niwapo usingizini ni “ndio”.Hata hivyo,umuhimu wa Muungano huo hauondoi haja ya kuufanya uwe bora zaidi,wa manufaa kwa pande zote mbili na wenye mazingira yatakayoufanya udumu daima dumu.Tusipoziba ufa leo,kesho tutajenga ukuta.

Mwisho, napenda kutoa pongezi kwa kizazi kipya cha vijana wabunifu. Hivi karibuni, mchora katuni na mtangazaji maarufu Masudi “Kipanya” alizindua duka la nguo za lebo yake ya “KP Wear”. Na msanii wa bongoflava AY nae anaelekea kufuata mkondo huo. Hawa na wengineo wenye mawazo kama hayo wanatumia vizuri umaarufu walionao kwenye jamii na wanastahili sapoti yetu. Wito wangu kwao ni kwamba wanapomiminiwa sifa kwa jitihada zao, wazitumie sifa hizo kuwa chemchem ya kusaka mafanikio zaidi. Pia wanaweza kwenda mbali zaidi kwa kutumia mianya ya biashara ya kimataifa kama vile katika e-Bay ili kuwawezesha Watanzania popote walipo duniani kunufaika na ubunifu wao. Kwa lugha ya mtaani, mie “nawapa tano”.Tanzania ya “masupastaa” wanaovuma kwa ubunifu wao,na sio kwa skendo,inawezekana.

Alamsiki


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.