Showing posts with label TETEMEKO LA ARDHI TANZANIA. Show all posts
Showing posts with label TETEMEKO LA ARDHI TANZANIA. Show all posts

17 Sept 2016

Nianze makala hii kwa kurejea salamu zangu za rambirambi kwa wafiwa na pole kwa majeruhi wa janga la tetemeko la ardhi lililotokea Jumamosi iliyopita huko Bukoba. 

Kadhalika, ningependa kuchukua fursa hii kuwapongeza wote waliojitokeza kuchangia kwa hali na mali kwa wahanga wa tukio hilo. Kipimo cha utu wetu ni katika nyakati ngumu kama hizi.

Pengine kabla ya kuingia kiundani zaidi katika mada ninayotaka kuongelea, nitoe mfano mmoja unaonihusu. Julai 8 mwaka jana, nilifiwa na baba yangu Mzee Philemon Chahali. Japo miaka saba kabla, yaani mwaka 2008, nilimpoteza mama yangu pia, lakini kuondokewa na mtu wa karibu, hususan mzazi, ni moja ya matukio magumu mno kukabiliana nayo maishani. Sikia tu watu wakilia kwa kufiwa na wazazi au ndugu wengine wa karibu, lakini in reality ni kitu kigumu mno 'kudili' nacho.

Sasa, katika mila zetu za Kiafrika, kipimo kikuu cha urafiki ni jinsi wenzetu wanavyoguswa na matukio makubwa maishani mwetu, pengine zaidi kwa yale ya majonzi kuliko ya furaha. Tunatarajia zaidi wenzetu kuwa karibu nasi kwenye misiba pengine kuliko kwenye harusi, birthday party au mahafali.

Wanasema "nikwepe kwenye sherehe yangu lakini usikose kuwepo kwenye msiba unaonihusu." Ni kwamba wakati wa furaha, hatuhitaji mtu wa kutuliwaza. Ni furaha, twafurahi wenyewe hata pale wenzetu wa karibu wasipokuwepo.Lakini kwenye majonzi twahitaji mno watu wa kutuliwaza. 

Kufupisha stori, nilipopatwa na msiba wa baba yangu mwaka jana nilikuwa nina-follow takriban watu 500 kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter. Japo haimaanishi kuwa mtu ambaye sim-'follow back' sio muhimu kwangu (nina-interact zaidi na watu ambao siwa-follow kuliko hao ninaowa-follow), hao takriban 500 niliokuwa ninawa-follow walikuwa na ukaribu wa aina flani nami.

Naam, katika dunia yetu ya sasa ambapo ni vigumu kuchora mstari unaotenganisha maisha yetu mtandaoni na maisha yetu halisi, kum-follow mtu ni sawa na kuanzisha nae urafiki. Na ni kwa mantiki hiyo, tunapowa-follow watu tunakuwa na matarajio flani kutoka kwao kama ilivyo kwa watu tunaofahamiana nao katika maisha yetu halisi nje ya mtandao.

Nifupishe stori, baada ya wiki kama mbili hivi za maombolezo ya kifo cha baba nilirejea mtandaoni, na kitu cha kwanza kilikuwa kupitia lundo la salamu za rambirambi kwa msiba huo. Na kwa hakika zilikuwa nyingi mno. Hata hivyo, baadhi ya watu niliokuwa ninawa-follow "walinikwepa." Na haikunichukua muda kuwa-unfollow kwa kigezo chepesi tu cha "nini thamani ya urafiki wetu kama mmeshindwa japo kunipa pole ya msiba?" Nika-unfollow takriban watu 400 kwa mkupuo.

Kama kum-unfollow mtu kwa vile "kakuangusha" ni jambo la busara au upuuzi, nadhani inategemea zaidi na jinsi mtu anavyothamini mahusiano, yawe ya mtandaoni au katika maisha yetu halisi.  

Lengo la makala hii sio kuelezea kuhusu tukio hilo linalonihusu bali nimelitumia tu kujenga msingi wa mada ninayoizungumzia leo, ambayo ni kile kinachoelezwa kama "ukimya wa Rais Dokta John Magufuli kuhusiana na tetemeko la ardhi huko Bukoba."

Katika makala yangu kwenye toleo la wiki hii la gazeti la Raia Mwema nimeongelea, pamoja na mambo mengine, uamuzi wa Rais Magufuli kuahirisha safari ya kwenda Zambia kuhudhuria kuapishwa kwa Rais Edgar Lungu. Japo niliwakosoa wasaidizi wa Rais kwa kutoa taarifa ya safari hiyo (kabla ya kutoa taarifa nyingine kuwa imeahirishwa na badala yake Rais angewakilishwa na Makamu wake) huku wakielewa bayana kuwa 'Rais angeonekana kituko' laiti angesafiri huku taifa likiwa kwenye maombolezo, nilipongeza uamuzi huo wa kuahirisha safari hiyo kwa mantiki ya kile  Waingereza wanasema 'the end justifies the means,' kwamba haikujalisha kama awali wasaidizi wa Rais 'walilikoroga,' cha muhimu ni kuwa Rais alionyesha kujali wananchi anaotuongoza, kwa kuahirisha safari hiyo.

Hata hivyo, kama ambavyo baada ya matanga ya msiba wa baba mwaka jana nilikerwa na ukimya wa 'baadhi ya watu niliokuwa ninawa-follow Twitter,' ndivyo ambavyo baadhi ya Watanzania wameanza kuguswa na kile wanachotafsiri kama ukimya wa Rais Magufuli kuhusiana na janga la tetemeko la ardhi huko Bukoba. 

Naomba sana nieleweke vizuri katika maelezo haya ya mfano hayamaanishi kwa namna yoyote ile kulinganisha msiba wa baba yangu na janga kubwa la kitaifa lililotokana na tetemeko la ardhi huko Bukoba. Na wala siwalingishi waliokuwa followers wangu huko Twitter na wananchi wanaohoji kuhusu 'ukimya wa Rais Magufuli.' Nimetumia 'case yangu' kwa minajili ya mfano tu.

Katika kumtendea haki Rais Magufuli, ukweli ni kwamba hajakuwa kimya 'kihivyo.' Mara baada ya kupata taarifa ya janga hilo, Rais alitoa salamu zake za rambirambi kama inavyoonekana pichani chini



Lakini binafsi ninawaelewa vema wanaohoji 'ukimya' wa Rais wetu kuhusu janga hilo. Kwamba Dkt Magufuli sio tu ni Rais wetu bali pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, na pengine anatarajiwa kusikika kwa 'maneno ya mdomo' (na sio tamko tu la maandishi) akizungumzia suala hilo. Na pengine wanaohoji 'ukimya' wake walitarajia angekwenda eneo la tukio (hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni 'mwenyeji' wa maeneo yaliyokumbwa na janga hilo). Hata hivyo, binafsi ninaamini kuwa Rais atazuru huko hivi karibuni tu.

Kadhalika, kwa vile Rais ndiye mkuu halisi wa serikali, taasisi yenye jukumu la usalama wa wananchi, basi huenda wanaohoji 'ukimya wake' wanatarajia yeye kuongoza jitihada za serikali kuwapatia confidence wahanga wa tetemeko hilo.

Na vilevile, licha ya ukweli kwamba kuna kundi flani ambalo limejiapiza kumkosoa Dokta Magufuli kwa kila atakalofanya, wanaohoji 'ukimya' wake sio tu wanaruhusiwa na Katiba kufanya hivyo bali pia wanaweza kuwa wanamsaidia Rais wetu ili kuepusha lawama za mapungufu ya kiuongozi wakati wa majanga.

Nihitimishe makala hii kwa kushauri kuwa pengine itakuwa vema iwapo Rais atafanya ziara huko Bukoba mapema zaidi au hata kuongea na taifa kwa njia ya hotuba, sio kwa minajili ya kuwajibu wanaohoji ukimya wake bali kutekeleza kwa ufanisi wajibu wake kama 'baba' wa taifa letu katika nyakati kama hizi.

Naomba pia kutoa angalizo hususan kwa makada wanaoweza kujaribu kupotosha lengo la makala hii kuwa ni kumlaumu Rais (japo sio kosa kikatiba kufanya hivyo) au kumfundisha kazi (pia sio uhaini wala jinai kumshauri Rais). Dokta Magufuli ametuomba mara kadhaa kuwa tumsaidie, na moja ya njia za kumsaidia ni kumfikishia ujumbe kama huu (nimesikia watu wakihoji kuhusu 'ukimya' wake kuhusu tetemeko la Bukoba nami namjulisha kuhusu hilo). Kama tunampenda kweli Rais wetu basi na tusiwe wagumu  kumshauri au hata kumkosoa pale inapostahili.

UPDATE: Apparently, wanaohoji 'ukimya' wa Rais kuhusu tetemeko la ardhi huko Bukoba wamepata 'hoja mpya,' kwamba walitarajia asubuhi hii angeungana na wakazi wa jiji la Dar es Salaam kwenye matembezi ya hiari ya kuchangia wahanga wa tetemeko hilo, lakini badala yake mgeni rasmi amekuwa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi. 

Binafsi nadhani sio vema kulaumu bila kujua sababu. Na ukiniuliza kwanini Rais Magufuli hakushiriki matembezi hayo, jibu langu la haraka haraka laweza kuwa 'sababu za kiusalama.' Hilo ni kwa sie 'tunaoelewa,' lakini si kila mtu anaweza kuelewa hivyo, na hatuwezi kuwalaumu wakohoji.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.