Showing posts with label TUNDU LISSU. Show all posts
Showing posts with label TUNDU LISSU. Show all posts

27 Oct 2020



Pengine umeshawahi kusikia jina la Profesa Allan Lichtman wa Marekani ambaye ana rekodi ya miaka 30 ya kutabiri kwa usahihi kabisa matokeo ya urais katika nchi hiyo. 



Pengine utabiri uliompatia umaarufu zaidi ni wa mwaka 2016 ambapo takriban kila kura ya maoni ilionyesha kuwa mgombea wa chama cha Democrats, Hillary Clinton, angemshinda mpinzani wake wa chama cha Republican, Donald Trump.

Profesa huyo anatumia vipengele 13 vinavyopatikana kwenye kitabu chake kiitwacho "The Keys To The White House" (funguo za kuingilia Ikulu ya Marekani).

Katika vipengele hivyo 13 ni kauli zenye mrengo wa ushindi kwa mgombea aliyepo madarakani. Kwa muktadha wa Tanzania, vipengele hivi hapa chini vinamhusu Rais John Magufuli wa chama tawala CCM anayechuana vikali na mpinzani wake mkuu, Tundu Lissu wa Chadema.

Endapo majibu ya SI KWELI (FALSE) ni matano au pungufu kwa vipengele hivyo, basi mgombea aliyepo madarakani anatabiriwa kushinda. Lakini endapo majibu ya SI KWELI (FALSE) yatakuwa sita au zaidi, basi mgombea huyo ataanguka kwenye uchaguzi husika.

Naomba nitahadharishe kuwa hii ni mara ya kwanza kwa kanuni hii kutumika kutabiri matokeo ya urais nchini Tanzania. Hata hivyo nimejiridhisha kuwa japo Profesa Lichtman alilenga chaguzi za rais wa Marekani, zaweza pia kutumika kwa muktadha wa Tanzania.

10 Jan 2018

Image result for magufuli lowassa
Jana Januari 9, 2018, wiki moja na siku mbili baada ya kuanza kwa mwaka huu mpya, duru za siasa za Tanzania zilitikiswa na habari kuhusu kiongozi maarufu wa Chadema, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kukutana na Rais John Magufuli kwa “mazungumzo”, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Baada ya “mazungumzo” hayo Lowassa alimmwagia pongezi Magufuli kwa kile alichokiita “kazi nzuri anayoifanya” na kutaja mafanikio katika sera ya elimu bila malipo, ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), na ujenzi wa viwanda na ujenzi wa reli ya “standard gauge”.

Nimepata faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Mheshimiwa Rais, tumezungumza nae na nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na anahitaji kutiwa moyo,” alinukuliwa Lowassa aliyejiunga na Chadema miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 baada ya ndoto zake kuwania urais kwa tiketi ya CCM “kuota mbawa.”


Image result for magufuli lowassa

Mwanasiasa huyo ambaye baada ya kujiunga na Chadema alipitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa vyama vinne vya upinzani – Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD – uliofahamika kama UKAWA, aliendelea kusema kuwa “Moja kubwa ambalo ni la msingi sana ni la kujenga ajira, katika kuanza ujenzi wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hapo anajenga ajira, na kwenye nchi yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira, Stiegler’s Gorge ni kujenga ajira na mingine ya aina hiyo, lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba tunajenga ajira. Jingine ni la elimu, ni muhimu sana, hauwezi kuacha elimu katika mambo yako unayofanya, hili nalo lazima lisemwe vya kutosha, kwa kweli nakushukuru Mheshimiwa Rais, you made my day.

Rais Magufuli kwa upande wake alimpongeza Lowassa kwa kile alichokiita “kutambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali” na kumtaja Lowassa kama mmoja wa viongozi ambaye kwa wakati wake alitoa mchango wake katika nchi.

Magufuli alimmwagia sifa Lowassa akidai kuwa “ni mwanasiasa mzuri kwani hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita ambao naye aligombea kiti cha Urais, hakuwahi kumtukana.”

Mheshimiwa Lowassa ameniomba mara nyingi nikutane nae, na leo nimekutana nae, tumezungumza mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya kwangu. Kwa ujumla Mheshimiwa Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani walifanya mambo mazuri, na mimi napenda kumpongeza Mhe. Lowassa ambaye kama alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi,” alisema Rais Magufuli

Ametaja miradi mbalimbali tunayotekeleza, ametaja mradi wa Stiegler’s Gorge utakaogharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 7, amezungumzia juu ya elimu bure, amezungumzia juu ya maji ambayo kwa bahati nzuri yeye alikuwa Waziri wa Maji na anafahamu sasa tumefikia wapi, amezungumza juu ya umeme tulivyosambaza katika vijiji mbalimbali, elimu bure, huduma za hospitali na mengine” aliongeza Rais Magufuli.

Kwanza, ni muhimu kutambua kuwa kama Mtanzania yeyote yule, Lowassa alikuwa na kila haki ya kukutana na Rais wake. Kadhalika, kama mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani, isingepaswa kuwa jambo la kushangaza kwa viongozi hao wawili kukutana.

Hata hivyo, Lowassa sio tu amekutana na Magufuli, bali pia ammemwamgia sifa. Je ni dhambi kwa kiongozi wa chama cha upinzani kumwagia sifa Rais aliyepo madarakani? Jibu lingepaswa kuwa “si dhambi,” laiti uhusiano kati ya Rais Magufuli, serikali yake na taasisi zake (kama vile jeshi la polisi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa), watendaji wa serikali (hasa mawaziri na manaibu wao, na wakuu wa mikoa na wilaya), pamoja na chama cha Magufuli yaani CCM, na chama anachotoka Lowassa, yaani Chadema, na Upinzani kwa ujumla, ungekuwa mzuri.

Lakini ukweli ni kwamba japo tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, uhusiano kati ya CCM, serikali zake na taasisi zake, na vyama vya upinzani umekuwa “wa kusuasua,” hali katika miaka miwili tu ya utawala wa Magufuli imekuwa mbaya zaidi hususan kutokana na ukweli kwamba hakuna jitihada za kuficha chuki iliyopo dhidi ya Upinzani.

Kama kiongozi wa ngazi za juu kabisa wa Chadema, na pengine mwanasiasa anayeheshimiwa zaidi ya kiongozi mwingine yoyote ndani ya chama hicho, ni wazi Lowassa anafahamu vema msimamo na mtazamo wa chama chake kuhusu Magufuli na utendaji kazi wake, na serikali yake, na chama chake.

Pengine kwa kuweka picha sawia, inaelezwa kwamba hadi wakati huu, zaidi ya wana-Chadema 400 ikiwa ni pamoja na viongozi na wanachama, aidha wapo jela au wana kesi zinazoendelea mahakamani ambazo takriban zote ni matokeo ya chuki za kisiasa zinazofanywa na Magufuli, serikali yake na chama chake.

Kadhalika, katika utawala wa Magufuli, vyama vya upinzani ikiwemo Chadema ambayo Lowassa ni kiongozi wake wa kitaifa vimepigwa marufuku kufanya shughuli zao za kisiasa ikiwa ni pamoja na mikutano na maandamano. Hayo yanatokea wakati CCM ikiwa huru kufanya mikutano na maandamano itakavyo, mara nyingi ikitumia raslimali za umma.

Sambamba na jitihada za Magufuli kubana fursa ya siasa (political space), utawala wa kiongozi huyo umekuwa mstari wa mbele kuvibana vyombo vya habari na kudhibiti uhuru na haki ya wananchi kutoa mawazo yao kama Katiba inavyowaruhusu.

Lakini jingine ambalo Chadema ni mhanga mkubwa, kada maarufu wa chama hicho Ben Saanane “alipotea” Novemba mwaka jana na hadi leo hajapatikana.

Na ni wakati ninaandika makala hii nimebaini kuwa Lowassa hajawahi kuongelea suala la kada huyo (naomba nikosolewe kama nimekosea).
Kubwa zaidi linaloweza kuhalalisha hasira za Chadema kwa utawala wa Magufuli ni tukio la hivi karibuni ambapo Mbunge wake maarufu, ambaye pia alikuwa mpinzani maarufu dhidi ya Magufuli, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kunusurika kuuawa baada ya shambulio la risasi kadhaa huko Dodoma. Kwa sasa Lissu yupo nchini Ubelgiji kwa matibabu, lakini japo Lowassa alimtembelea alipokuwa hospitalini Nairobi, Magufuli hakuwahi kutia mguu kumjulia hali mwanasiasa huyo ambaye pia ni mnadhimu mkuu wa upinzani bungeni na Rais wa Tanganyika Law Society (TLS).

Kwahiyo japo pongezi za Lowassa kwa Magufuli zinaweza kuwa na uzito, mapungufu ya utawala wa rais huyo wa awamu ya tano, hususan kuhusiana na chuki na uonevu dhidi ya vyama vya upinzani, hususan Chadema, yalipaswa “kumzuwia” kada huyo wa zamani wa CCM kumwaga pongezi hizo.

Kibaya zaidi, imebainika kuwa Lowassa alishawahi kumwomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amsaidie kukutana na Magufuli. Hata hivyo, Gambo alipotamka hilo hadharani, Lowassa “aliruka kimanga.”


Hata hivyo, jana Magufuli alitamka bayana kuwa Lowassa aliomba mara kadhaa kukutana naye. Kwahiyo, alichosema Gambo kilikuwa kweli, na Lowassa hakuwa mkweli alipokana kuwa hajaomba kukutana na Magufuli.

Tukio hilo la Lowassa kukutana na Magufuli na kumwagia pongezi limepokelewa kwa hisia tofauti. Wakati kuna kundi dogo la wana-Chadema waliopongeza hatua hiyo, kwa mfano “kada” mmoja wa chama hicho Yericko Nyerere, wengi ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wamepingana waziwazi na Lowassa.

Wakati Yericko aliandika haya


Mbunge maarufu wa Chadema, Godbless Lema alikuwa wa kwanza kueleza bayana kutoafikiana na pongezi za Lowassa kwa Magufuli.


Baadaye, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, naye alieleza kuwa kauli za Lowassa ni zake binafsi na sio msimamo wa chama hicho.

Kadhalika, Mbowe alionekana kumkumbusha Lowassa kuhusu matukio mbalimbali yasiyopendeza katika utawala wa Magufuli

Lakini pengine aliyeeleza kwa kirefu kuhusu suala hilo ni Lissu, ambaye akiwa hospitalini huko Ubelgiji, alitoa waraka huu hapa chini.



Waheshimiwa habari za Tanzania na poleni kwa yote.
Naomba na mimi niseme kwa uchache kuhusu suala hili. Samahani kama 'uchache' wangu utakuwa mrefu kidogo.
Baada ya Mwenyekiti kuzungumzia jambo hili, inaelekea kuwa wazi kwamba Mheshimiwa Lowassa hakumshirikisha Mwenyekiti kabla ya kukubali au kuamua kwenda Ikulu kukutana na Rais Magufuli.
Na juzi tu wakubwa wetu hawa wawili walikuwa pamoja hospitalini kumsalimia Mzee Ngombale Mwiru.
Je, inawezekana Mheshimiwa Lowassa hakuwa anajua tayari kwamba ana appointment Ikulu?
Kama alikuwa anajua, kutokumshirikisha Mwenyekiti wake kuna tafsiri gani hasa?
Katika mazingira ya sasa ya Tanzania ya Magufuli, uamuzi wowote wa kufanya nae mazungumzo, hata kwa nia njema yoyote ile, bila kushauriana au kuwashirikisha viongozi wa juu wa chama, ni uamuzi usio sahihi na mgumu kukubalika.
Vile vile, kauli za aina ambayo tumeisikia leo kutoka kwa Mheshimiwa Lowassa, zina athari kubwa kisiasa.
Sio tu zinachanganya wanachama na wafuasi wetu, lakini pia zinawapa mtaji wa kisiasa maadui zetu.
Kuanzia sasa tutegemee sana kuwasikia maCCM yakishangilia 'busara' za Mheshimiwa Lowassa.
Masuala ya ukiukwaji haki za binadamu, uvunjwaji wa Katiba na mengine mengi sasa yatajibiwa kwa namna moja: Lowassa amemkubali Magufuli nyie wengine mnapiga kelele za nini.
Huu ni mtaji wa bure kwa Magufuli. Ukweli, ambao umesemwa sana humu, ni kwamba amefeli karibu katika kila jambo.
Hata hiyo reli anayosifiwa nayo na Lowassa bado ni ndoto tu: nani ajuaye itajengwa kwa hela za nani???
Za Wachina kama tulivyoambiwa mwanzoni; au za Waturuki kama tulivyoambiwa baadae; au za Afrika Kusini kama alivyosema mwenyewe anaenda kumwomba Zuma???
Kama chama hatujawahi kukataa mazungumzo na Rais au kiongozi mwingine yeyote wa serikali.
Na hatukatai kuzungumza na Magufuli kuhusu matatizo mengi na makubwa yanayoikabili nchi yetu.
Lakini ni muhimu na lazima viongozi wakuu wa chama washirikishane na washauriane kabla ya mazungumzo hayo.
Na baada ya mazungumzo, ni lazima viongozi wakubaliane juu ya kauli za kutoa hadharani kwa umma ili wote tuwe kwenye ukurasa mmoja.
Katika mazingira ya sasa, ambako viongozi na wanachama wetu wanashambuliwa hadharani kwa mapanga na hata kwa risasi, kumsifia Rais ni kumuunga mkono yeye na matendo yake.
Katika mazingira ya kesi nyingi za kutunga dhidi yetu, 'kazi nzuri' inayofanywa na Magufuli ina maana gani hasa, kama sio kuhalalisha ukandamizaji tunaofanyiwa.
Katika mazingira ambapo hata jumuiya ya kimataifa imeanza kuhoji mwenendo wa Rais Magufuli, kutoa kauli kwamba 'anafanya kazi nzuri' ni 'kumtupia taulo' la propaganda litakalomfichia madhambi mengi aliyowafanyia Watanzania katika miaka hii miwili.
Kwa vyovyote vile, kitendo cha Mheshimiwa Lowassa sio cha kunyamaziwa au kuhalalishwa kwa hoja nyepesi nyepesi.
TUNDU LISSU(MB).
Top of Form

Kadhalika, kada maarufu wa kike wa chama hicho, Hilda Newton nae alieleza masikitiko yake kutokana na kauli za Lowassa.



Kama alivyotahadharisha Lissu, ni wazi kwamba CCM watakuwa wamepewa “silaha” mpya katika “kumpamba” Magufuli na “kuwapenda” wapinzani, kwamba “hata Lowassa wenu anamkubali Magufuli.” Na ni rahisi kwa CCM kuonekana wana mantiki katika hoja hiyo, kwa kudai “kama mtu muhimu kabisa kwenye chama chenu (yaani Lowassa) ambaye ndiye aliyekuwa mpinzani mkuu wa Magufuli kwenye uchaguzi mkuu uliopita, anamkubali mkuu huyo wa nchi, ninyi ni akina nani kumpinga?”

Wakati ni wazi kwamba uamuzi wa Lowassa kukutana na Magufuli, na kumwagia pongezi, umezua “sintofahamu” huko Chadema, kuna masuala kadhaa ya muhimu yanayopaswa kuangaliwa kwa makini kwa ajili ya mustakabali wa chama hicho.

Kwanza, ni muhimu kwa viongozi na wanachama wa Chadema kutambua nafasi ya Lowassa katika chama hicho. Wakati baadhi ya wachambuzi wa siasa – mie nikiwa mmoja wao – wanaamini kuwa ujio wa Lowassa katika chama hicho ulikuwa na hasara zaidi kuliko faida, jitihada zilizofanywa na chama hicho kumpigania mwanasiasa huyo zimemjengea hadhi ambayo haipo kwa mwanasiasa mwingine yoyote ndani na nje ya chama hicho.

Ikumbukwe kuwa hadi wakati jina lake lilipokatwa na vikao vya CCM katika mchakato wa kusaka mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho tawala, Lowassa alikuwa ndiye mwanasiasa maarufu kuliko wote Tanzania. Yayumkinika kusema alikuwa mtu wa pili kwa umaarufu baada ya marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Licha ya kulazimika kujiuzulu Uwaziri Mkuu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya Richmond, Lowassa aliendelea kuwa mwanasiasa maarufu na mwenye nguvu kuliko yeyote yule ndani ya CCM, hata zaidi ya Rais na mwenyekiti wa taifa wa chama hicho wakati huo, Jakaya Kikwete.

Na japo kukatwa kwa jina la Lowassa huko CCM kulimpunguzia kidogo umaarufu wake kwa siasa za Tanzania – ilikuwa kama miujiza kuona CCM ilikuwa na ujasiri wa kukata jina la mwanasiasa huyo- alihamia Chadema akiwa na sapoti ya kutosha kiasi japo si kubwa kama ilivyotarajiwa.

Japo kuna “tuliopishana nae mlangoni” – kwa maana yeye alipoingia, sie tukatoka – ujio wake ulipelekea kuwa mwanasiasa maarufu zaidi ya wote wa Upinzani. Na ndio maana haikuwa vigumu kwake kupitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA.

Nimeeleza kuwa baadhi yetu “tulipishana nae mlangoni” kwa sababu mie binafsi nilikuwa naiunga mkono Chadema, si kama mwanachama bali ukweli kwamba kwa muda mrefu nimekuwa nikijihusisha na harakati za mapambano dhidi ya ufisadi, na chama hicho kilijitokeza kuwa championi wa mapambano hayo. Kwahiyo, “naturally” nilijikuita nikikiunga mkono.

Hata hivyo, ujio wa Lowassa katika chama hicho ulinikimbiza. Sababu kuu ni binafsi zaidi, na nisingependa kuongelea hapa, lakini sababu nyingine ni kile nilichotafsiri kama usaliti wa Chadema. Ikumbukwe kuwa tangu mwaka 2006, chama hicho “kilimkalia kooni” Lowassa kumtuhumu kuwa ni fisadi, na ndicho kilichofanya jitihada kubwa zilizopelekea mwanasiasa huyo kujiuzulu Uwaziri Mkuu mwaka 2008.

Sasa bila hata kutumia jitihada kidogo tu za busara, chama kilichomwandama Lowassa kuwa ni fisadi, kwa miaka 9 mfululizo, yaani 2006 hadi 2015, kilionekana kituko kwa baadhi yetu tuliokuwa tukikiamini, kwa sababu, pamoja na mengine, isingewezekana kutumia miezi mitatu (Julai 2015 Lowassa alipojiunga na chama hicho hadi Oktoba wakati wa uchaguzi mkuu) kumsafisha vya kutosha.

Na gharama ya ujio wa Lowassa ilikuwa kubwa. Moja kubwa zaidi ilikuwa lazima kwa Chadema “kuitosa” turufu yake muhimu, ajenda ya vita dhidi ya ufisadi. Ililazimika kufanya hivyo kwa sababu kuzungumzia ufisadi ilhali chama hicho kimemkumbatia mwanasiasa kiliyemwita “baba wa ufisadi” kwa miaka 9 mfululizo ingeonekana kioja.

Kadhalika, kwa kumpokea Lowassa, Chadema ilikuwa haina jinsi ya kukwepa tuhuma kutoka CCM kuwa chama hicho upinzani ni cha kifisadi kwa sababu ya kumkumbatia mwanasiasa ambaye kilikuwa kikimuita fisadi. Jitihada za Chadema kujibu mashambulizi kuwa “kama Lowassa ni fisadi mbona hajachukuliwa hatua,” zilikuwa hazina mashiko.

Lakini jingine lililoipa jeuri CCM ni ukweli kwamba kwa chama hicho, Lowassa alikuwa ni “makapi” sambamba na wanasiasa wengine waliomfuata huko Chadema. Hiyo ilikipa chama hicho tawala “jeuri” ya namna flani. Na waliitumia vema kwenye kampeni, kwamba “hawa jamaa si lolote si chochote. Yani wameshindwa hata kutafuta mgombea wao wenyewe mpaka wakasubiri makapi kutoka kwetu ndo wakapata mgombea urais.” Na pamoja na maneno hayo kuwa machungu, ndo ukweli ulivyokuwa.

Chadema na UKAWA kwa ujumla walikuwa na takriban mwaka mzima wa kujipanga; kuafikiana kuhusu mgombea urais kwa tiketi ya umoja huo, na kumnadi, huku wakitumia “advantage” ya “vita vya wenyewe kwa wenyewe” kati ya zaidi ya makada 40 waliokuwa wakichuana kuteuliwa na CCM.

Badala yake, kumbe tayari kulikuwa na makubaliano ya siri kati ya uongozi wa baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema kwamba wasubiri kutangaza mgombea wao hadi baada ya mchakato wa CCM kupata mgombea wake, ka maana ya “kumhifadhia nafasi Lowassa endapo jina lake litakatwa huko CCM.”

Kabla ya kwenda mbali na makala hii ningependa nishauri Chadema irejee suala hilo la Lowassa kuandaliwa nafasi ya kuwania urais japo wakati huo alikuwa CCM. Hatua stahili zinapaswa kuchuliwa dhidi ya wote waliohusika na mpango huo.

Na ujio wa Lowassa ulipelekea Chadema kumpelekea mmoja wa magwiji wa siasa za upinzani, Dokta Willbrord Slaa. Umahiri wa Dokta Slaa haukuwa tu katika kuchukia ufisadi kwa dhati bali umahiri wake mkubwa katika kujenga hoja kisomi. Kadhalika, alikuwa akiaminiwa na watu mbalimbali muhimu ndani ya serikali, kiasi kwamba baadhi yao walihatarisha ajira zao kwa kumpatia mwanasiasa huyo nyaraka muhimu zilizoiwezesha Chadema kuwa na ushahidi mbalimbali katika vita yake dhidi ya ufisadi.

Na kuonyesha kuwa alikuwa na msimamo imara, Dokta Slaa aliamua kujiweka kando katika uongozi kupinga Lowassa kupewa ugombea urais wa UKAWA. Lakini jambo la kusikitisha mno, kiongozi huyo aliyekifanyia mengi chama hicho alidhalilishwa na kutukanwa kupita kiasi.
Na “akina sie” tulishindwa kustahimili ujio wa Lowassa, na kwa vile kwa baadhi yetu ilikuwa muhimu kumzuwia asiingie Ikulu, na hivyo kulazimika kumpigia kampeni mpinzani wake yaani Magufuli, tulitukanwa kila aina ya matusi. Sijui watu hawa waliojitoa ufahamu wataweka wapi sura zao pindi Lowassa “akirejea nyumbani” CCM.

Wakati anajiweka kando na uongozi wa Chadema, Dokta Slaa alikitahadharisha chama hicho kuwa ili kuleta mabadiliko ya kweli (badala ya hayo “ya kisanii” aliyokuwa akiyanadi Lowassa) chama hicho kinahitaji mkakati makini utakaoongozwa na watu makini. Na kwa hakika, tangu wakati huo, Chadema imekuwa kama kundi la wanaharakati wa kudandia hoja kuliko chama cha siasa chenye ajenda ya kueleweka. Uamuzi wa kuitelekeza ajenda ya vita dhidi ya ufisadi ulipelekea chama hicho kutokuwa na ajenda moja ya maana, huku CCM “wakipora” kiurahisi ajenda ya vita dhidi ya ufisadi.

Je mustakabali wa Chadema ukoje? Japo sio rahisi sana kubashiri kwa uhakika kuhusu hatma ya chama hicho, binafsi – kwa kutumia uzoefu wangu na uelewa wa kutosha wa siasa za Tanzania, sambamba na kuwa na fursa ya kufahamu “yanayojiri nyuma ya pazia” la siasa za nchi yetu – ninadhani kuwa kuna uwezekano mkubwa tu kwa Lowassa kurudi CCM kama sio kuachana kabisa na siasa.

Kwanini Lowassa anaweza kurudi CCM? Kuna sababu kuu mbili. Moja ni dalili za wazi kuwa ndoto zake za urais kupitia chama hicho ni kama zimeyeyuka. Umaarufu wake umegubikwa na kuibuka na kuimarika kwa umaarufu wa Lissu. Ni dhahiri kwamba ikipigwa kura ya maoni kuwa nani kati ya Lowassa na Lissu awe mgombea urais kwa tiketi ya Chadema mwaka 2020, Lissu ataibuka mshindi. Na Lowassa anafahamu kuwa hakuna njia ya mkato kwa yeye “kulazimisha” awe mgombea katika uchaguzi mkuu huo ujao, licha ya ukweli kwamba alishatangaza kuwa atagombea.

Sababu nyingine ni binafsi zaidi. Lowassa ni mmoja wa matajiri wakubwa nchini Tanzania. Kama utajiri huo ulipatikana kihalali au kifisadi, si lengo la makala hii kujiingiza katika mjadala huo. Lililo wazi ni ukweli kwamba licha ya kuwa mwanasiasa, yeye pia ni mfanyabiashara. Na kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, serikali ya Magufuli imefanikiwa kutumia nyenzo yake muhimu dhidi ya wapinzani ambao pia ni wafanyabiashara, KODI.

Inaelezwa pia kwamba mali mbalimbali za mwanasiasa huyo zipo hatarini kutokana na uwepo wake huko Upinzani. Inadaiwa kuwa hata jengo la Tanesco Ubungo ambalo serikali imetangaza kulivunja, linamilikiwa na Lowassa, na tishio la kulivunja lilikuwa kama kufikisha ujumbe kwake.

Katika hili, Lowassa hatoonekana mtu wa ajabu akiamua kurudi CCM ili asibughudhiwe kuhusu biashara na mali zake. Ni nani kati yetu anayeweza kujitoa mhanga kwa ajili tu ya imani yake ya siasa? Si kama hawapo ila ni adimu mnooo! Na kibaya zaidi, hata akiamua kung’ang’ania huko Chadema, hatma yake na ya chama hicho haieleweki kwa sababu hadi muda huu – na hii ni licha ya zuwio la Magufuli dhidi ya vyama vya upinzani kufanya shughuli zao za siasa – chama hicho kikuu cha upinzani “kipo kipo” tu. Hakina ajenda moja ya kueleweka zaidi ya kudandia kila tukio linalojiri.

Iwapo Lowassa ataamua kubaki Chadema, hiyo itakuwa fursa mwafaka kwa chama hicho kumpumzisha. Naamini kuwa wana-Chadema wakiweka kando ushabiki wa kisiasa, wanafahamu fika kuwa mwanasiasa huyo hana nguvu, uwezo wala mvuto wa kukabiliana na siasa hatari zinazoendelea muda huu huko nyumbani.

Kwa upande mwingine, tukio la Lowassa kukutana na Magufuli Ikulu linaweza pia kuhusishwa na tamko la hivi karibuni la Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, ambaye kama Lowassa, alimmwagia sifa Magufuli.

Nimefanya uchambuzi kuhusu kauli za wanasiasa hao wawili hapa, lakini ninachoweza kugusia hapa ni haja ya kutambua kuwa wanasiasa hao bado wanatunzwa na serikali kutokana na nyadhifa walizowahi kushika huko nyuma. Haihitaji uelewa mkubwa kuhusu "siasa za kibabe" kuhisi kwamba huenda "malezi" wanayopewa na serikali yametumika kama "chambo" cha kuwavuta karibu na Magufuli.

Kuhusu matatizo yanayoikabili Chadema muda huu,ukweli ni kwamba ni zaidi ya uwepo wa Lowassa ndani ya chama hicho. Japo huu ni ukweli mchungu usioruhusiwa kabisa kusikika ndani ya chama hicho, licha ya kazi nzuri ya kuifikisha Chadema ilipo leo, mwenyekiti wa taifa Mbowe anapaswa kutoa fursa kwa wana-Chadema wengine kusukuma gurudumu la chama hicho. Na hatua hiyo wala haihusiani na mchango wake mkubwa wa kumleta Lowassa ndani ya chama hicho na “kumpa” ugombea urais wa UKAWA.

Kirefu cha Chadema ni Chama cha DEMOKRASIA na Maendeleo. Sasa ni demokrasia gani hiyo ambayo inaruhusu mwenyekiti mmoja kuwa madarakani milele? What if “uenyekiti wa milele” ni miongoni mwa vikwazo kwa maendeleo ya chama hicho?

Lakini hata kama “muda wa Mbowe kutoka madarakani haujafika,” busara tu inapaswa kumfahamisha kiongozi huyo kuwa ni vema kuzingatia busara za akina Nyerere waliojing’atua wakiwa bado wanahitajika. Sipendi kubashiri hili, lakini laiti Mbowe asipohamasisha mageuzi kwenye medani ya uongozi wa chama hicho, haitokuwa jambo la ajabu akiishia kung’olewa kwa nguvu.

Na kwa bahati mbaya kwake, hili “songombingo” alilolianzisha Lowassa jana linaweza kuwa kama mnyororo mrefu ambao mahala flani yupo Mbowe. Ndiye aliyemkaribisha Lowassa.

Moja ya mapungufu makubwa mno yanayoitafuna Chadema muda huu ni pamoja na kulipuuza kundi muhimu linalokisaidia mno chama hicho, lundo la vijana wanaoshinda na kukesha katika mitandao ya kijamii wakijaribu kukinadi chama hicho angalau kwa kuikemea serikali ya Magufuli au CCM kwa ujumla.

Laiti chama hicho kingekuwa na ajenda ya kueleweka, basi jeshi hili la vijana lingekuwa nyenzo muhimu mno. Ni rahisi kuwalaumu vijana hawa kuwa “kazi yao kubwa ni kudandia hoja tu,” lakini ukweli ni kwamba chama chao hakiwapatii ajenda ya/za kueleweka. Kibaya zaidi, hata pale wanapojaribu kutengeneza ajenda wao wenyewe – kwa mfano jitihada za kumsaka Ben Saanane – hawapati sapoti ya kutosha kutoka uongozi wa juu wa chama hicho.

Ni hivi, wengi wa hawa vijana wanahatarisha maisha yao kwa kuwa tu “upande usiotakiwa” na serikali ya Magufuli. Hawategemei malipo yoyote zaidi ya kuamini kuwa siku moja wanaweza kukiingiza chama chao madarakani. Hakuna jitihada za makusudi za uongozi wa juu wa chama hicho kuwa karibu na kundi hili muhimu.

Ukiwa UVCCM una uhakika wa angalau “kuhongwa na Bashite” au kualikwa kwenye “mnuso” sehemu flani. Lakini ukiwa kijana wa upinzani, “zawadi” kubwa yaweza kuwa kusumbuliwa na vyombo vya dola na kuishi maisha ya wasiwasi. Kwahiyo vijana wa upinzani wana kila sababu ya kuichukia siasa, kwa sababu inahatarisha maisha yao, lakini mapenzi yao katika imani ya chama inawalazimisha kung’ang’ania hivyo hivyo.

Niionye Chadema kuwa katika zama hizi za “ununuzi wa binadamu kama zama za utumwa,” chama hicho kisishangae pindi wengi wa vijana hawa watakapoamua kubwaga manyanga na kukubali “kununuliwa.” Kwanini waendelee kuhatarisha maisha yao ilhali uongozi wa juu wa chama hicho hauna muda nao?

Akina Hilda Newton, Ben Malisa, Bob Wangwe, Ndehani Mwenda, Noel Shao, Gift Nanyaro ni miongoni mwa vijana wanaofanya kazi kubwa kwa ajili ya Chadema, bila ya matarajio ya malipo au fadhila flani, zaidi ya kuhatarisha maisha yao. Kama ilivyo kawaida ya mwanadamu yeyote yule, inaweza kufika mahala mtu akarudi nyuma na kujiuliza, “is it worth it?” Na japo sitarajii kuona makada hao vijana wakiamua kuipa kisogo Chadema, lakini sintoshangaa baadhi yao wakiamua kuipa kisogo siasa, hasa kama tasnia hiyo itaendelea kuwa “yenye manufaa kwa genge flani tu.”

Nihitimishe makala hii kwa kukuhamasisha msomaji kujipatia nakala yako ya kitabu changu kipya cha kielektroniki kinachochambua kwa kina miaka miwili ya utawala wa Magufuli. 




Baadhi ya niliyaoyazungumzia kwenye makala hii yamezungumwa kwa kirefu katika kitabu hicho ambacho hakielemei upande wowote. Kitabu hicho kwa sasa kinasubiri uzinduzi rasmi utakaokiwezesha kununulika kwa “mobile money” kama m-pesa, tigopesa,nk. Nitawataarifu. Ila kwa wasiohitaji kusubiri, waweza kukinunua HAPA

8 Sept 2017



Jana, Septemba 07, 2017, majira ya mchana, zilipatikana taarifa kwamba Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Mbunge wa Singida Mashariki, Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, na Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), amepigwa risasi kadhaa na kujeruhiwa vibaya.

Tukio hilo la kutisha lilitokea jijini Dodoma, wakati Mbunge huyo aliposhuka nyumbani kwake eneo la Area D, inakoelezwa alienda kwa ajili ya kujipatia mlo wa mchana.

Kabla ya kuingia kiundani kwenye makala hii, nitumie fursa hii kutoa salamu za pole kwa Lissu, na kumwombea apone haraka. Salamu za pole pia kwa viongozi, wanachama na wafuasi wa Chadema, chama ambacho Lissu amekuwa akikiwakilisha kwa ufanisi mkubwa.

Pia ni vema nitahadharishe mapema kwamba intelijensia sio sayansi timilifu kwa asilimia 100, kwa kimombo wanasema “intelligence is not an exact science.”

Okey, sasa tuingie mtamboni. Hadi muda huu kuna dhana za msingi tatu ambazo zinatokana na‘mchujo’ wa dhana mbalimbali.

Dhana ya kwanza na ambayo pengine ni maarufu zaidi ya zote ni kwamba jaribio hilo la mauaji ya Lissu lina mkono wa dola. Kwamba sio siri kuwa Lissu amekuwa ‘akiisumbua mno’ serikali, ambapo wafuasi wake wanamwona kama jasiri asiye na uoga wa kusema ukweli, ilhali wapinzani wake wakimwona kama mchochezi.

Yayumkinika kuhitimisha kwamba kama kuna mwanasiasa wa upinzani ambaye amekuwa ‘mwiba mchungu’ kwa serikali ya Rais John Magufuli basi si mwingine bali Lissu.

Na pengine kinachoongeza uzito kwenye dhana hii ni ukweli kwamba Agosti 18 mwaka huu, Lissu aliwaeleza wananchi kwamba anafuatiliwa.

Namnukuu "Naomba kabla sijaanza Mazungumzo yangu nimuombe Mkuu wa idara ya Usalama wa Taifa anaitwa Kipilimba au Inspekta Generali wa Polisi Simon Sirro, wale vijana ambao wamewatuma na kwa wiki tatu mfululizo wananifuata kila nilipo wanaotembea na gari ya Toyota premio namba T460CQV, jana niliwakaba Kanisani St. Peter's.



Kwa upande mwingine serikali ya Magufuli ni kama ilikuwa inatafuta ‘kulaumiwa bure.’ Kwa sababu, Hadi muda huu hakuna sababu moja ya msingi kwa serikali hiyo kuyafanya maisha ya wanasiasa wa upinzani yawe magumu kiasi hiki. Magumu kwa maana ya kuwanyima kila aina ya fursa ya kufanya siasa (political space).

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, zaidi ya viongozi na wafuasi 400 wa Chadema wameshakamatwa tangu Magufuli aingie madarakani. Mtu atayedai kuwa kiongozi huyo ‘anawachukia wapinzani’ hatoonekana mtu wa ajabu japo huenda akatupwa jela.

Katika hotuba zake mbalimbali, Rais Magufuli ameshindwa kuficha hisia zake dhidi ya upinzani na wapinzani. Juni 12 mwaka huu, Rais Magufuli alimweleza Spika Job Ndugai maneno yafuatayo

“Tumia mbinu hiyohiyo ya kuwafanya wasiropokee Bungeni, waropokee nje na kule tutadili nao vizuri kwasababu wanapokua kule ndani wana kinga wanaweza wakatukana chochote, sasa kinga wanayoitumia vibaya bungeni kainyooshe wewe. Wawe wanatoka kule bungeni, ukishamfukuza hata mwezi mzima… atakuja aropokee huku, na mimi nakueleza waache waropokee huku nitadili nao, wala siwatishi lakini hatuwezi kuwa kwenye vita wewe unaanza kugeuka kupiga wale wanaokwenda mbele…. ni nafuu unyamaze ukalale.”

Kwa kuangalia jinsi watendaji wa serikali ngazi za mkoa na wilaya wanavyochuana na polisi kuwanyanyasa wapinzani, hususan wa Chadema, dhana kuwa serikali ina mkono katika jaribio la mauaji ya Lissu ni kama ‘ready-made.’

Hata hivyo, pamoja na ‘dalili zote’ kuashiria uwezekano wa mkono wa serikali katika jaribio la kumuua Lissu, dhana hii inakosa mantiki kiuhalisia. Ni kwamba hakuna tija kwa serikali kumuua Lissu. Sawa, sio siri kuwa uhusiano kati ya serikali na Lissu/ wapinzani sio mzuri, lakini haitokuwa na tija yoyote kwa serikali ya Magufuli kumuua Lissu.

Na hata kama ingekuwa lazima ‘aondoke,’ basi kuna ‘njia mwafaka zaidi’ za mauaji ya watu maarufu (assassination), huku 'kifo cha ajali' ikiwa maarufu na rahisi zaidi.

Halafu kinachotatiza katika tukio la jana, na kinachopunguza zaidi nguvu ya dhana kwamba ‘kuna mkono wa serikali,’ ni jinsi waliofanya shambulio hilo walivyoonekana kama wanahitaji publicity ya kutosha. Kwanini? Jibu lipo kwenye uchambuzi wa dhana ya tatu.

Dhana ya pili ni dhaifu kuliko nyingine mbili. Hii inahusisha mbio za urais mwaka 2020. Kwamba kila siku Lissu amekuwa akijitengenezea mazingira ya mgombea mwafaka wa Chadema/Upinzani katika uchaguzi mkuu ujao, wala halina mjadala. Sio kwamba Lissu amekuwa hodari katika masuala mbalimbali kwa vile anataka urais (hajawahi kutamka nia ya kugombea nafasi hiyo) lakini umahiri wake bungeni na katika masuala ya kisheria na kitaifa kwa ujumla, unamfanya kuwa kipenzi cha takriban kila mfuasi wa Chadema.

Dhana hii dhaifu inasema kuwa jaribio hilo la mauaji ni kazi ya wapinzani wa kisiasa wa Lissu, hususan ndani ya chama chake.

Udhaifu wa dhana hii ni kwamba, kama ambavyo kwenye dhana ya kwanza, hakuna tija katika kumdhuru Lissu hadharani. Kwamba hata kama kungekuwa na lundo la wapinzani wa kisiasa wa Lissu huko kwenye chama chake, kwanini wafanye ‘operesheni’ hiyo waziwazi badala ya kuandaa mkakati wa siri?

Na kama ilivyokuwa kwenye dhana ya kwanza, hata kama wapinzani wa kisiasa wa Lissu ndani ya chama chake wangekuwa wahusika, kwanini basi tukio hilo lifanyike katika mazingira ya ‘kusaka publicity kwa nguvu’?

Hiyo inatuacha na dhana moja, ya tatu, na ya mwisho. Ya mwisho lakini sio haba katika mantiki. Dhana hii inaeleza kwamba jaribio hilo la mauaji limefanywa makusudi na kile wajuzi wa mambo wanaita ‘rogue elements.’  Hizi zilitusumbua sana katika utawala wa Awamu ya Nne wa Rais Jakaya Kikwete. Rogue elements hizi zinajumuisha watumishi halali wa vyombo vya dola wanaofanya shughuli zisizo halali. Nani anawatuma? Hiyo ni habari nyingine.

Kuna kitu kinachofahamika kama ‘Deep state.’ Kila nchi ina tafsiri yake kuhusu ‘deep state’ lakini tafsiri nyepesi kwa mazingira yetu ni ushirika wa watu wenye nguvu katika serikali na jamii – mfano vigogo (hususan wa zamani) wa vyombo vya dola, wafanyabiashara wenye uwezo mkubwa na wanasiasa kutoka upande wowote ule, lakini zaidi chama kilichopo madarakani.

Dhana hii inaliona tukio la kujaribu kumuua Lissu kama njia rahisi ya kuichafua serikali ya Rais Magufuli, ambayo kwa bahati mbaya/makusudi ilishajitengenezea mazingira ya kulaumiwa pindi la kutokea likimtokea mwanasiasa wa upinzani kama Lissu. Rais anaposhindwa kudhibiti ‘chuki zake’ dhidi ya wapinzani, anawapa nafasi nzuri ‘wabaya wake’ kutenda kitu kisha ikawa rahisi tu lawama kuelekezwa kwake.

Ndio maana dhana ya kwanza – kwamba kuna mkono wa serikali ya Magufuli kwenye jaribio la kumuua Lissu – inaonekana kama yenye uzito kwa vile "kuna sababu ready-made.”

Dhana hii inapata uzito kutokana na ukweli kwamba Magufuli amejitengenezea maadui wengi, wenye nguvu, na baadhi yao wakiwa viumbe hatari. Kuna watu waliozowea kuishi maisha ya kifalme ambao sasa wanalazimishwa kuishi maisha ya kawaida. Hawa watu wakipata upenyo wa kumdhuru Magufuli, hawatosita kufanya hivyo.

Lakini kwa vile ni ‘vigumu mno’ (angalau kwa wakati huu) kufanikisha jaribio la kumdhuru kiongozi huyo, njia nyepesi inaweza kuwa katika ‘kuua character yake,’ ambayo bahati nzuri kwa ‘wabaya wake,’ sio nzuri sana.

Kumekuwa na malalamiko kadhaa hasa kutoka upande wa upinzani kumtuhumu Magufuli kuwa ni dikteta. Na ukifuatilia mwenendo wa siasa zetu kwa muda huu, sio siri kwamba kuna chembe chembe za udikteta. Kwahiyo, ni rahisi kwa ‘wabaya wa Magufuli’ kutumia mwanya huo kujenga picha ya “serikali ya dikteta yamuua mpinzani wake mkubwa.”

Na hilo linatuleta kwenye suala la publicity. Kwamba jaribio la mauaji hayo liwe na mwangwi wa kutosha ndani na nje ya Tanzania. Mwangwi huo ni wa makusudi ili uakisi taswira inayojengeka kuwa ‘Magufuli ni dikteta. Na madikteta hunyanyasa wapinzani wao, na ikibidi hata kuwaua.’

Kwahiyo, kama kuna funzo kubwa kwa Magufuli katika tukio hili ni kuepuka mazingira yaliyopo ya uhasama mkubwa dhidi ya upinzani hususan Chadema. Kiongozi huyo anatambua fika kwamba kuna watu wapo radhi kufanya lolote lile kumng’oa, na kwa vile ‘njia za kawaida’ sio rahisi, basi inakuwa ‘anything goes,’ liwalo na liwe.

Na dhana hii ya tatu inaleta uhusiano kati ya tukio la jana la jaribio la kumuua Lissu na lile la hivi karibuni la kuchomwa moto kwa ofisi za kampuni ya uwakili wa IMMA. Kama hili la Lissu, tukio la moto nalo lilifanyika katika mazingira ya kuvutia publicity, yaani kama kulikuwa na jitihada za makusudi za kuushawishi umma kwamba “mnaona huyu dikteta Magufuli anakoelekea? Sasa anachoma hadi ofisi wa ‘wabaya’ wake.”

Nihitimishe uchambuzi huu kwa kueleza bayana masuala mawili matatu. Kwanza, lengo la uchambuzi huu mfupi sio kuingilia kazi za vyombo vya dola vinavyoendelea na uchunguzi kuhusu jaribio la kumuua Lissu. Nimefanya uchambuzi huu kama mtu mwenye uelewa wa masuala ya intelijensia na siasa za Tanzania yetu, ikiwa ni pamoja na “yanayojiri nyuma ya pazia.”

Pili, lengo la uchambuzi huu sio kumshawishi mtu yeyote abadili mtazamo wake kuhusu “nani ana/wanahusika.”

Mwisho, kama nilivyotanabaisha awali, tasnia ya intelijensia sio sayansi kamilifu kwa asilimia 100 (intelligence is not an exact science). Kwa maana hiyo, japo uchambuzi huu ni karibu kabisa na hali halisi, sio rahisi sana kufikia hali halisi yenye uhakika wa asilimia 100.

Nimalizie kwa kumtakia afya njema Bwana Lissu huku nikiamini kuwa malaka husika zitafanya kila jitihada kuwanasa wahusika, sio tu kwa minajili ya serikali kujinasua bali ili Bwana Lissu atendewe haki.

12 Sept 2012

Iliwahi kuripotiwa kuwa Mkurugenzi wa Katiba na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu, aliipinga Tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Dkt Emmanuel Nchimbi kuchunguza mauaji ya mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi.Moja ya sababu alizotoa Lissu ni Tume hiyo kuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Mstaafu Stephen Ihema,ambaye alimtuhumu kuwa na rekodi ya utendaji kazi yenye walakini.

Katika pitapita yangu mtandaoni, nimekutana na habari inayomhusu Jaji Mstaafu Ihema, ambapo alikuwa mjumbe wa Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii, na sasa kamati hiyo imevunjwa kutokana na kulalamikiwa mno kwa vitendo vya rushwa miongoni mwa wajumbe.

Binafsi nimeguswa sana na habari hii hasa kwa vile inahusu tuhuma za rushwa kwa kamati iliyokuwa inamjumuisha Jaji Mstaafu Ihema.Sasa tukiamini kuwa Jaji Ihema ameshindwa jukumu la ujumbe tu kwenye tume hiyo ya ushauri,kwanini tumwamini kwenye uenyekiti wa kamati ya uchunguzi wa kifo cha marehemu Mwangosi?

Wakati ninawapongeza wanahabari waliojitokeza jana kuifahamisha bayana Serikali ya Rais Jakaya Kikwete  kuwa wanalaani vikali mauaji ya mwanahabari mwenzao yaliyofanywa na jeshi la polisi,ningependa kushauri kuwepo upinzani zaidi dhidi ya Tume hii ambayo kuna kila dalili kwamba itaishia kuwa kiini-macho tu.Awali,hofu yangu kuhusu Tume hiyo ilielemea zaidi Watanzania wameshashuhudia utitiri wa tume ambazo mara nyingi ripoti zake zimeishia kufungiwa maandazi na vitafunwa vingine badala ya kuwekwa hadharani//hatua kuchukuliwa.Wengi wetu tunakumbuka kuhusu tume ya milipuko ya mabomu huko Mbagala na Gongo la Mboto.Hadi leo hakuna kilichoelezwa kuhusu ripoti ya tume hiyo...and life goes on.

Je wewe ni mdau wa habari? Unapenda kuona uchunguzi wa kifo cha marehemu Mwangosi unafanywa independently na watu wasio na harufu ya utendaji kazi wenye walakini?Basi ungana na wanahabari kupiga kelele dhidi ya tume hiyo ya kisanii

27 May 2012



Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Dk Wilbrod Slaa akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.




 Mwenyekiti wa Taifa Freeman Mbowe Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA  akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


Mbunge wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Singida Magharibi Mheshimiwa Tundu Lissu akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


 Mbunge Wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Ubungo Mheshimiwa John Mnyika akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


Mbunge  wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Mbeya Mjini Mheshimiwa Joseph Mbilinyi aka Mr II(SUGU) akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


 Viongozi wa chadema wakifurahia kadi nyingi za CCM zilizorudishwa leo jioni kwenye mkutano
Deo Munish Katibu mkuu wa BAVICHA akiteta jambo na mmoja aliyehudhuria mkutano wa CHADEMA Wa uzinduzi wa kampeni ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.




  Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe akiwaaga wananchi waliokuwa wamefurika makao makuu ya chama kinondoni walikofika wakitokea jangwani usiku huu
 Mbowe akiwatania wanachama ofini kinondoni baada ya wananchi kuanza kudai chama kimfukuze John Shibuda.Alikuwa akijifanya hasikii wanachosema na hapa anajaribu kuwasikiliza zaidi.hata hivyo Mbowe aliwaondoa wasiwasi na kusisitiza kuwa chama kinao utaratibu wa kushughulika na viongozi wanaokiuka maadili ya chama na kuwaomba wawaamini kama viongozi kuwa wanaouwezo wa kulishughulikia jambo hilo na mengine
 Mh.Mbowe na Mnyika wakiwa wamesimama kwenye gari wakati wa matembezi wakitoka kwenye mkutano
Aliyekua Mbunge wa Arusha Mjini(CHADEMA)Mheshimiwa Godbless Lema akiwa juu ya gari huku akishangiliwa na vijana jioni baada ya mkutano
 Sehemu ya umati uliowasindikiza viongozi wa chadema toka jangwani hadi kinondoni.wamesambaa yapata saa 2 usiku.

PICHA ZOTE NA MAELEZOKWA HISANI YA BLOGU YA MHESHIMIWA HAKI NGOWI

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.