Showing posts with label U.S. SECRET SERVICE. Show all posts
Showing posts with label U.S. SECRET SERVICE. Show all posts

23 Oct 2014

Makala yangu hii ilichapishwa katika jarifa la RAIA MWEMA Toleo la wiki iliyopita lakini 'nilizembea' kui-post hapa bloguni. Endelea kuisoma:

NIANZE kwa kuelezea matukio mawili, moja linaihusu Marekani na jingine laihusu Israel. 
Tukio la kwanza linahusu kujiuzulu kwa aliyekuwa mkuu wa moja ya idara za usalama za Marekani (zipo nyingi) ambayo ina dhamana ya ulinzi na usalama wa viongozi wakuu wa taifa hilo na familia zao, US Secret Service. 
Mkuu huyo, mwanamama Julia Piersons, alilazimika kujiuzulu baada ya tukio la hivi karibuni la kuhatarisha usalama wa Rais Barack Obama, kutokana na mtu mmoja, Omar Gonzalez, kuruka uzio wa Ikulu ya nchi hiyo akiwa na kisu, kabla hajadhibitiwa na maafisa wa Secret Service. 
Hatimaye tukio hilo lililotawala sana katika vyombo vya habari vya Marekani lilimfanya mwanamama huyo, shushushu mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 30, kuitwa na kuhojiwa na kamati moja ya Bunge la Congress, na mwishowe alitangaza kujiuzulu. 
Licha ya ukweli kwamba mkuu huyo wa mashushushu hakuwa eneo la tukio, dhamira ilimtuma kuwa kama kiongozi wa taasisi yenye dhamana ya ulinzi wa viongozi wakuu wa nchi hiyo, anawajibika kwa uzembe au makosa ya watendaji wake. 
Piersons alikuwa kwenye wadhifa huo kwa takriban miezi 18 tu baada ya mtangulizi wake, Mark Sullivan, kulazimika kujiuzulu baada ya kashfa iliyohusisha baadhi ya maafisa wa Secret Service ‘kufumwa’ wakiwa na makahaba katika ‘msafara wa utangulizi’ (advance party) kabla ya ziara ya Rais Obama nchini Colombia, mwaka juzi. 
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya ushushushu wanamuona Piersons kama mhanga tu wa mapungufu ya kimfumo na kiutendaji yanayoikabili taasisi aliyokuwa akiongoza. 
Wanadai kuwa alikuwa akikabiliwa na jukumu gumu la kuleta mabadiliko ndani ya taasisi hiyo, na wadhifa wake ulikuwa sawa na ‘jukumu lisilowezekana.’ Hata hivyo wanampongeza kwa ‘kubeba mzigo wa lawama’ kwa niaba ya watendaji wake. 
Tukio la pili linahusu filamu ya maelezo (documentary) iitwayo The Gatekeepers, iliyoonyeshwa kwenye kituo cha runinga cha BBC2 mwishoni mwa wiki. 
Filamu hiyo ni ya mahojiano na wakuu sita wa zamani wa Idara ya Usalama wa Ndani wa Israeli, Shin Bet (au 'Shabak' kama inavyojulikana kwa Kiyahudi). 
Filamu hiyo iliyotengenezwa mwaka juzi na kuteuliwa kuwania tuzo za Oscars, imeendelea kuwa na mvuto mkubwa kutokana na ukweli kuwa ni vigumu mno, hasa kwa ‘nchi ya kiusalama’ kama Israeli, kupata fursa ya kufanya mahojiano na wakuu wa taasisi za usalama. 
Katika filamu hiyo inayoelezea kwa undani utendaji kazi wa Shin Bet, idara ya ushushushu yenye ufanisi mkubwa duniani, ikiwa ni pamoja na operesheni mbalimbali za Shin Bet dhidi ya ‘magaidi’ wa Palestina, wakuu hao – Avraham Shalom (1980-1986), Yaakov Peri (1988-1994), Carmi Gillon (1994-1996), Avi Dichter (2000-2005) na Yuval Diskin (2005-2011)- wanatanabahisha jinsi wanasiasa na Wayahudi wenye msimamo mkali walivyo vikwazo kwa jitihada za kutafuta amani ya kudumu katika mgogoro wa muda mrefu wa Israeli na Palestina. 

Kwa ujumla, wote wanahitimisha kuwa licha ya umuhimu kwa serikali ya Israeli na taasisi zake za ulinzi na usalama kutumia nguvu dhidi ya ‘ugaidi wa Wapalestina,’ ukweli mchungu ni kuwa matumizi hayo ya nguvu si tu yanachochea ‘ugaidi’ zaidi bali pia yanakwaza uwezekano wa kupatikana amani ya kudumu. 

Filamu hiyo ilisababisha wakuu hao kushutumiwa na Waisraeli wengi, wakilaumiwa kwa msimamo wao uliotafsiriwa kama kuhalalisha ‘ugaidi’ wa Wapalestina, huku wengine wakiwashutumu kuwa ‘waliongea walichoongea baada ya kustaafu badala ya kubainisha mitizamo yao wakiwa madarakani.’ 
Kwa hakika filamu hiyo (unayoweza kuiangalia hapa http://goo.gl/gY4K6O) si tu inaeleza kwa undani operesheni hatari na za ‘ufanisi wa hali ya juu’ zilizofanywa na Shin Bet chini ya uongozi wa mashushushu hao lakini pia inamsaidia anayeiangalia kufahamu kwa undani mchanganyiko wa siasa na dini na mwingiliano wake katika utendaji kazi wa taasisi za kiusalama za Israeli, na kubwa zaidi ni maelezo ya kina kuhusu mgogoro kati ya nchi hiyo na Palestina. 
Lengo la makala hii si kujadili matukio hayo mawili bali kuyatumia kama ‘darasa la bure’ kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa. Binafsi, nimekuwa moja ya sauti chache kuhusu haja ya mageuzi ya kimfumo na kiutendaji kwa taasisi hiyo muhimu. 
Kwa bahati mbaya – au makusudi- utendaji kazi na ufanisi wa Idara hiyo haukuguswa kwa kiwango kinachohitajika katika kikao cha Bunge la Katiba na hatimaye Katiba pendekezwa. 
Idara hiyo inakabiliwa na matatizo makubwa japo aidha hayafahamiki sana au yanapuuzwa, na huo ndio msingi wa ushauri wangu kuwa kuna haja ya mageuzi ya haraka. 
Tukijifunza katika kujiuzulu kwa mkuu wa Secret Service, twaweza kujiuliza, hivi kwanini hakuna anayewajibishwa licha ya Idara yetu ya Usalama wa Taifa kuboronga mara kwa mara? 
Pengine kuna watakaojiuliza 'imeboronga lini na katika nini?’ Jibu rahisi ni kwamba, kwa mujibu wa ‘kanuni za taaluma ya usalama wa taifa,’ kushamiri kwa vitendo vinavyotishia usalama wa nchi ni dalili ya wazi ya udhaifu wa idara ya usalama wa taifa ya nchi husika. 
Kwa maana hiyo, kushamiri kwa ufisadi, kwa mfano mmoja tu, ni dalili kwamba taasisi hiyo imeshindwa kazi yake. Kadhalika, Idara hiyo kufanya kazi zake kama ‘kitengo cha usalama cha CCM’ si tu kunaipunguzia kuaminika kwake kwa umma bali pia kunaathiri uwezo wake katika kukabiliana na matishio kwa usalama wa Taifa. 
Majuzi, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara hiyo, Jack Zoka, ‘alizawadiwa’ ubalozi wa nchi yetu huko Canada. Sihitaji kuingia kwa undani kuhusu utendaji kazi wa shushushu huyo lakini atakumbukwa sana na vyama vya upinzani, hasa CHADEMA, sambamba na wengi wa waliojitoa mhanga kuwa sauti ya wanyonge, kwa jinsi alivyowadhibiti. Pengine kabla ya kupewa ubalozi baada ya kustaafu utumishi wa umma, ahojiwe kuhusu mchango wake katika ‘ufanisi’ au udhaifu wa Idara hiyo. 


 
Ni mwendelezo wa kasumba inayolikwaza Taifa katika nyanja mbalimbali: mtu anaboronga pale, anahamishiwa kule. Kwanini watendaji wengine wahofie kuboronga katika majukumu yao ilhali wenzao ‘wanazawadiwa’ badala ya kuwajibishwa? 
Somo kutoka kwa wakuu sita wa zamani wa Shin Bet katika filamu ya The Gatekeeper ni kubwa zaidi. Ukiondoa ‘sauti ndogo’ ya Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Idara yetu ya Usalama wa Taifa, Hans Kitine, takriban viongozi wote wastaafu wa Idara hiyo wamekuwa hawana mchango wa maana katika kuiboresha na hata kuisadia isimame katika upande stahili. 
Ni kweli Tanzania si Israeli, lakini wengi wa wastaafu wa taasisi hiyo, kama ilivyo kwenye taasisi nyingine, ni watu wenye ushawishi mkubwa na wanaheshimika vya kutosha, lakini ukimya wao wakati mambo yanakwenda kombo ni doa. 
Mashushushu hao sita wa Israeli walipokubali kushiriki kwenye filamu hiyo walikuwa wanatambua bayana athari zake, kubwa ikiwa ni uwezekano wa kuonekana wasaliti. Lakini ujasiri ni pamoja na kusema yasiyosemeka. 
Na kwa vile, kimsingi, ukiwa shushushu unabaki kuwa shushushu milele, na kwa sababu ni watu wachache katika jamii wenye uelewa kuhusu utendaji kazi wa taasisi za kiusalama, wastaafu au watumishi wa zamani ndio watu pekee wenye fursa ya ‘kuokoa jahazi.’ 
Nihitimishe makala hii kwa kutaja kwa kifupi maeneo yanayohitaji mageuzi (reforms) kuhusiana na Idara yetu ya Usalama wa Taifa. La kwanza ni umuhimu wa uwazi zaidi katika teuzi za viongozi wakuu wa Idara hiyo, hususan Mkurugenzi Mkuu. 
Ni muhimu kutengeneza mazingira yatakayoepusha uwezekano wa Rais ‘kumteua mtu wake au rafiki yake’ kuongoza taasisi hiyo. Madhara ya uswahiba katika uteuzi kuongoza taasisi nyeti kama hiyo ni pamoja na mteuliwa kujiona ana ‘deni la fadhila’ kwa aliyemteua. 
Kuna haja ya, kwa mfano, uteuzi wa viongozi wa juu wa taasisi hiyo kuidhinishwa na Bunge. 
Pili, ni ulazima wa taasisi hiyo kuwajibika kwa umma kupitia taasisi kama Bunge. Hapa ninamaanisha haja ya viongozi wa taasisi hiyo kuitwa katika kamati husika za Bunge, kwa mfano, kuwaeleza Watanzania ‘kwanini ufisadi unazidi kushamiri ilhali taasisi hiyo haipo likizo?’ 
Tatu ni mabadiliko ya kiutendaji ambapo Idara hiyo iwezeshwe kuufanya ushauri wake utekelezwe, badala ya mazingira yaliyopo ambapo kwa kiasi kikubwa suala hilo linabaki kuwa ridhaa ya Rais ambaye ndiye ‘consumer’ wa taarifa za kiusalama anazopatiwa na Idara. 
Hivi inakuwaje pale Idara hiyo inaposhauri kuhusu suala linalohatarisha usalama wa taifa lakini Rais akalipuuza? 
Mwisho, lengo la makala hii ni jema: kuiboresha Idara yetu ya Usalama wa Taifa (ambayo licha ya mapungufu yake lukuki, binafsi nina imani kuwa inaweza ‘kujikwamua’ kama si kukwamuliwa) kwa maslahi na mustakabali wa Taifa. 
Tanzania ni yetu sote na si kwa ajili ya kikundi kidogo kinachojiendeshea mambo kitakavyo.Penye nia pana njia.





16 Jun 2013


Washington- Rais Obama atapokwenda Afrika Kusini mwa Sahara mwezi huu, taasisi zenye jukumu la usalama wake hazifanyi lelemama.

Mamia wa mashushushu wa Kikosi cha Ulinzi wa Rais wa Marekani (US Secret Service) watasambazwa katika maeneo ya usalama huko Senegal, Afrika ya Kusini na Tanzania. Manowari ya Jeshi la Vita la Marekani inayotumika kubeba ndege za kivita au nyambizi, ikiwa na matabibu waliokamilika, itakuwa imeegeshwa pwani kwa ajili ya dharura.

Ndege za kijeshi za kubeba mizigo zitasafirisha magari 56, ikiwa ni pamoja na 'limousines' 14 na magari ya mizigo matatu yote yakiwa na makasha ya vioo visivyopenya risasi vitakavyowekwa katika madirisha ya hoteli atakazofikia Obama na familia yake. Ndege za kivita zitakuwa 'zikizurura' angani kwa zamu, kuwezesha ulinzi wa masaa 24 katika 'anga ya Rais' ili ziweze kuchukua hatua pindi ndege ya adui itakapoingilia kati.

Maandalizi haya mahsusi ya kiusalama-ambayo yataigharimu Serikali ya Marekani makumi ya mailioni ya dola- yapo kwenye nyaraka ya siri iliyopatikana kwa gazeti hili (la Washington Post). Wakati maandalizi hayo yanaendana na mengineyo katika safari nyingine, nyaraka husika inatoa picha ya jitihada za hali ya juu katika kumlinda Amiri Jeshi Mkuu wa wa majeshi ya Marekani anapokuwa ziarani nje ya nchi hiyo.

Safari yoyote ya Rais, kama za wiki hii huko Ireland ya Kaskazini na Ujerumani, zina changamoto na gharama kubwa kilojistiki.Lakini safari hii ya Afrika inakuwa ngumu zaidi kutokana na sababu mbalimbali, na inaweza kuwa yenye gharama zaidi kuliko zote katika utawala wa Obama, kwa mujibu wa watu walio karibu na maandalizi hayo.

Famili ya Obama inatarajiwa kutembelea nchi hizo tatu kuanzia June 26 hadi Julai 3 ambapo maafisa wa Marekani ndio watakaokuwa na jukumu la kuhudumia takriban kila kitu, badala ya kutegemea hudma za polisi, jeshi na hospitali katika nchi wenyeji.

Rais Obama na mkewe pia WALIPANGA KUFANYA ZIARA KWENYE MBUGA ZA WANYAMA ('SAFARI' kwa Kiingereza), ambayo ingehitaji kikosi cha kupambana na mashambulizi dhidi ya Rais kubeba silaha maalum zenye risasi maalum za kumudu kuwaangamiza duma, simba na wanyama wengine hatariu wa mwituni endapo wangekuwa tishio, kwa mujibu wa nyaraka hiyo 

Lakini maafisa walisema Alhamisi kuwa ZIARA HIYO (YA MBUGANI) IMEAHIRISHWA [ NA HII NDIO SABABU ILIYOPELEKEA UZUSHI WA BAADHI YA MABLOGA KUWA ZIARA YA OBAMA KUJA TANZANIA IMEFUTWA] na badala yake imeandaliwa ziara ya kutembelea Kisiwa cha Robben pembezoni mwa pwani ya Cape Town, Afrika Kusini, ambapo Nelson Mandela alifungwa kama mfungwa wa kisiasa.

Gazeti hili lilipowauliza maafisa wa  Ikulu ya Marekani (White House) kuhusu ZIARA YA MBUGANI ('safari') mapema mwezi huu,walisema hawajafikia uamuzi wa mwisho kuhusu suala hilo.Afisa mmoja wa Ikulu hiyo alieleza Alhamisi kuwa kufutwa kwa ziara hiyo ya mbugani hakukuhusiana na udadisi uliofanywa na gazeti hili hapo awali.

"Hatuna nyenzo zisizo na ukomo kufanikisha safari ya Rais, na tumeipa kipaumbele ziara ya Kisiwa cha Robben badala ya ziara ya MASAA MAWILI mbugani nchini Tanzania," alieleza msemaji Josh Earnest. "Kwa bahati mbaya, hatuwezi kufanya mambo yote mawili." [HEBU ANGALIA HAPA JINSI BLOGA HUSIKA ALIVYOCHAPIA SENTENSI HIYO NA HATA JINA LA MSEMAJI HUYO WA IKULU]

Nyaraka za ndani za kiutawala zilizosambazwa mwezi April zilionyesha kuwa familia ya Obama ilipanga kufanya ziara zote mbili- ya mbugani na kisiwani, kwa mujibu wa mtu anayefahamu maandalizi hayo.

Marais wa zamani, Bill Clinton na George W. Bush pia waliwahi kufanya ziara za mataifa mbalimbali ya Afrika, ambazo zilihitaji maandalizi magumu kama haya. Bush alikwenda mwaka 2003 na 2008, akiambatana na mkewe katika safari zote hizo. Mabinti wawili wa Bush pia walisafiri naye katika ziara ya kwanza, ambayo ilijumuisha 'safari' kwenye hifadhi ya wanyama katika mpaka wa Botswana na Afrika Kusini.

"Hata katika nchi zilizoendelea za Ulaya ya Magharibi, kiwango cha huduma kinachohitajika kwa ajili ya ziara ya rais ni cha hali ya juu," alisema Steve Atkiss, ambaye alikuwa mwandaaji wa ziara akiwa msaidizi maalum wa hudma kwa Bush. "Kadri unavykwenda mbali zaidi, katika maendeo yenye maendeleo duni, kwa hakika ni changamoto ya kilojistiki."

Ikulu ya Marekani na Mashushushu wa Secret Service wamekataa kuzungumzia mipango ya kiusalama, na wasiaidizi wa kiutawala wametahadharisha kuwa maandalizi ya safari ya rais hayajahitimishwa.

Safari za nje za Obama zinakuja wakati taasisi za serikali, ikiwa pamoja na Secret Service, zinapambana na kukata matumizi kwa lazima. Walinzi hao wa Rais walilazimika kukata dola milioni 84 katika bajeti yao ya mwaka huu, na mwaka huu Idara hiyo ilifuta ziara za wageni kutembelea Ikulu ya Marekani (kiutalii) ili kuokoa dola 74,000 kwa wiki ambazo ni gharama za watumishi kufanya kazi nje ya muda (overtime).

Taarifa nyingi kuhusu ziara za Rais nje ya nchi hufanywa siri kwa sababu za kiusalama wa taifa, na kuna ufahamu kidogo  tu kwa umma kuhusu gharama za jumla. Ripoti kutoka Ofisi ya Uwajibikaji wa Serikali ilionyesha kuwa ziara ya Clinton barani Afrika mwaka 1998 alipozuru nchi sita iliigharimu Serikali ya Marekani angalau dola miloni 42.7.Kiwango hicho kilitumika zaidi na Jeshi, ambalo lilifanya safari 98 kusafirisha watendaji na magari,na kuandaa maendeo ya dharura za kimatibu katika nchi tano.

Kiwango hicho hakikujumuisha gharama za Secret Service ambazo zinachukuliwa kama siri.

Ziara ya Obama inaweza kugharimu kati ya dola milioni 60 hadi milioni 100 kwa kuzingatia gharama za safari za nyuma barani Afrika. Nyaraka ya Secret Service kuhusu ziara hiyo,ambayo ilionwa na gazeti hii, iliyowasilishwa na mtu anayeguswa na gharama za ziara hiyo, haikuonyesha Idara hiyo itatumia kiasi gani cha fedha.

"Miundombinu inayoambatana na ziara za Rais zipo nje ya uwezo wetu," alisema Ben Rhodes, Naibu Mshauri wa Usalama wa taifa wa Obama katika mawasiliano ya kimkakati. "Mahitaji ya kiusalama hayapangiw na Ikulu, hupangwa na Secret Service."

Maafisa wa zamani na wa sasa wa usalama wa serikali waliohusika na ziara za rais walibainisha kuwa watendaji wa Ikulu nao husaidia katika kuainisha mahitaji hayo, kwani hupanga sehemu za kutembelea na mipaka yake. Secret Service na Jeshi hufuatilia maandalizi hayo ya ziara yaliyowasilishwa kwao kwa kutaja mahitaji ya kiusalama.

Maafisa wa Ikulu ya Marekani wamesema kuwa dhamira ya ziara hiyo imekuwepo kitambo sasa, na itakuwa ya kwanza kwa Obama kama Rais kutembelea Afrika Kusini mwa Sahara licha ya 'kusimama' kwa masaa 22 nhini Ghana kwa msaa 22. Demokrasia changa zilizomo kwenye ratiba ya ziara hiyo ni washirika muhimu wa kiusalama katika eneo hilo, Rhodes alisema.

Obama atafanya mikutano na kila kiongozi wa nchi atakayotembela kwa minajili ya kujenga ushirikiano bora wa kiuchumi katika wakati huu ambapo China inawekeza vya kutosha barani Afrika. Pia atapigia mstari  programu za afya, ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya Ukimwi.

Mke wa Rais, ambaye alitembelea Afrika Kusini na Botswana bila ya mumewe mwaka 2011, atashiriki kwenye baadhi ya amtukio katika ziara hiyo. Hilo pia ni changamoto la kilojistiki kwa vile naye atahitaji maandalizi tofauti ya kiusalama kuhusu walinzi na magari, kwa mujibu wa nyaraka hiyo.

Msemaji wa Secret Service, Ed Donovan, alikataa kuzungumzia maandalizi ya ziara hiyo. "Siku zote huwa tunatoa kiwango stahili cha ulinzi kutengeneza mazingira salama," alisema.

Kwa mujibu wa nyaraka ya Secret Service, Obama atakaa siku moja Dakar, Senegal, siku mbili Johannesburg,Afrika Kusini, na siku moja Dar es Salaam, Tanzania.

KATI YA MAGARI 56 KWA AJILI YA ZIARA HIYO NI 'LIMOUSINES' KWA AJILI YA RAIS NA MKEWE , GARI MAALUM LA MAWASILIANO YA SIMU NA VIDEO, GARI LA KUZUWIA MAWASILANO YA MAWIMBI (FREQUENCIES) YA RADIO KUZUNGUKA GARI LA RAIS, GARI LILILOJITOSHELEZA LA WA WAGONJWA (ambulance) AMBALO LINAMUDU KUKABILIANA NA MAAMBUKIZI YA KIBAIOLOJIA NA KIKEMIKALI NA GARI LA VIFAA VYA MIONZI YA X-RAY

Mashushushu wa Secret Service husafirisha magari kama hayo, pamoja na vioo vya kuzuwia risasi, katika ziara nyingi, ikiwa ni pamoja na zile za ndani ya Marekani, msemaji wa Ikulu alieleza. Lakini kwa vile kuna nchi tatu zinazohusika katika ziara hiyo, kunahitajika seti tatu za maandalizi hayo,kwa sababu hakuna muda wa kutosha wa kuhamisha vifaa, kwa mujibu wa nyaraka hiyo.

Mashushushu 100 wanahitajika kama 'waangalizi' - kumudu maeneo ya kumzunguka Rais- katika kila mji atakaozuru. 66 wanahitajika kumpokea Obama jijini Dar es Salaam. Kabla 'safari' ya Mbuga ya Taifa ya Mikumi haijaahirishwa wiki iliyopita, ziada ya mashushushu 35 ilijumuishwa kwenye maandalizi hayo ili kumlinda Rais, mkewe na mabinti zao wawili, kwa mujibu wa nyaraka hiyo.

Kadhalika, kati ya mashushushu 80 hadi 100 watasafiri na kufanya kazi kwa shifti kwa masaa 24, kwa ajili ya ulinzi wa Obama na familia yake, vikosi vya kupambana na mashambulizi (counterassault teams) na waandaaji wa lojistiki.

Nyaraka hiyo ya maandalizi ya ziara haionyeshi idadi ya mashushushu watakaohusika na ziara hiyo, japo baadhi watafanya kazi katika kituo zaidi ya kimoja.

Maafisa walisema Secret Service haitaki ziara ya Rais pasipo kituo cha hali ya juu cha jirani cha kukabili maradhi. Kitengo cha utabibu cha Ikulu hufanya maamuzi kuhusu hospitali gani Rais awapo ziarani nje ya nchi kinakidhi viwango, kwa kufanya ziara kwenye nchi husika, maafisa walieleza.

Katika nchi zinazoendelea, Jeshi la Majini la Marekani huweka 'hospitali inayoelea' kwenye manowari ya kubeba ndege au nyambizi, jirani.

"Hivi  ndivyo inavyohitajika kuilinda taasisi ya  urais wa Marekani," alisema Atkiss kuhusu mahitaji husika, "pasi kujali nani ni rais."


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.