Showing posts with label UDINI. Show all posts
Showing posts with label UDINI. Show all posts

26 May 2013



MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameibua suala zito akikihusisha chama chake na “kumnusuru” Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu uliopita.

Tanzania Daima limefahamishwa kuwa Profesa Lipumba alitoboa siri hiyo katika Msikiti wa Idrissa, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, alikokwenda kuswali swala ya Ijumaa, miezi kadhaa iliyopita.

Kwa mujibu wa video ya tukio hilo, ambayo gazeti hili lina nakala yake, Profesa Lipumba alikaribishwa kuzungumza na waumini hao mara baada ya utangulizi uliotolewa na Imamu wa msikiti huo, Sheikh Ali Basaleh, aliyemtaka awaeleze Waislamu hali ya kisiasa nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Huku akisisitiza juu ya umuhimu wa mshikamano wa kiimani, Profesa Lipumba alianza kwa kuzungumzia matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010, na ushindani mkali wa kisiasa uliokuwapo.

Alisema hawaoni matunda ya jitihada walizofanya kumnusuru Rais Kikwete asishindwe, kwani hata chini ya uongozi wake, Waislamu wameendelea kutothaminiwa.

“Ninyi masheikh mnajua vizuri zaidi hali ya kisiasa ilivyokuwa, kwamba ilibidi zifanyike juhudi za makusudi ili kuokoa jahazi. Lakini pamoja na kuliokoa jahazi, hali halisi inaonyesha mpaka sasa hakuna matunda yoyote yaliyopatikana, na tupo katika mtihani mgumu zaidi,” alisema.

Katika hali ambayo inasemekana ushindi wa Rais Kikwete ulipatikana kwa mbinu, huku wengine wakiituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa ilimnusuru mgombea wa CCM, kauli hii ya Profesa Lipumba inadokeza kwamba anajua mkakati zaidi wa kazi ya Tume ya Uchaguzi.

Katika hali isiyo ya kawaida, Profesa Lipumba anaonekana kuhamasisha Waislamu kujipanga akisema “wenzetu wameanza kujipanga” kuelekea 2015.

“Kwahiyo kama Waislamu tunataka kupata haki zetu, kama tunataka kuishi kama raia wa daraja la kwanza katika nchi yetu, lazima tujipange kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015; na sisi tuanze kujipanga kwa sababu wenzetu wameanza kujipanga, vinginevyo tutaendelea kubaki maskini na raia wa daraja la nne katika nchi yetu wenyewe.

“Mwaka 2010 wakati mshindi wa uchaguzi wa rais alipotangazwa, mimi nilikwenda kwenye hafla ya kutangazwa matokeo, na nilikwenda makusudi tu, siyo kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, ila nilikwenda makusudi kwa kujua hali ya kisiasa ilivyokuwa wakati huo.

“Huku nilikutana na Sheikh Basaleh. Nilipokutana naye, alinipongeza; sijui kama yeye anakumbuka, akaniambia ‘umeweka mbele imani yako na umekuwa mwelewa wa mambo.’”

Hata hivyo, licha ya Profesa Lipumba kuwaambia Waislamu wajipange kwa ajili ya uchaguzi mkuu, hakusema wajipange kupitia chama kipi.

Lakini alisisitiza kwamba uchaguzi ujao ni zaidi ya siasa au rais yupi anafaa, bali maslahi, hasa ya rasilimali nyeti zinazopatikana katika ukanda wa Pwani ya Mashariki, eneo ambalo alisema linakaliwa zaidi na watu wenye imani ya Kiislamu.

Katika moja ya kauli zake, Profesa Lipumba alisema kwamba kuna chama kimoja kinataka kuchukua madaraka ya nchi, lakini kinasaidiwa na mataifa ya magharibi, yasiyoenzi wala kuthamini imani ya Kiislamu.

Kwa muda sasa, zimekuwapo tetesi kwamba CCM imekuwa inafanya siasa za udini dhidi ya vyama vya upinzani, hasa inapoona maslahi yake yapo hatarini.

Mwaka 2010 makada kadhaa wa CCM walitumia mitandao ya simu kuchonga (spoofing) ujumbe wa simu ulioshambulia mgombea mmoja wa upinzani, ukimhusisha na imani yake.

Kauli ya Lipumba imethibitisha pia minong’ono iliyokuwapo muda mrefu kuwa baadhi ya kura za Profesa Lipumba zilipotelea kwa Rais Kikwete.

Katika uchaguzi huo, Lipumba alitangazwa kushika namba ya tatu, nyuma ya Rais Kikwete na Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA.

Alipoulizwa kuhusu ziara yake msikitini na kauli aliyotoa, Profesa Lipumba alikiri kwamba alikwenda kuzungumzia hali ya kisiasa nchini. Hata hivyo alisema inawezekana video hiyo imechakachuliwa kwa kuungaunga vipande vya matamshi wanavyovitaka badala ya hotuba nzima.

Hata hivyo, video iliyotazamwa na waandishi wa habari hii, ambayo nakala yake imetunzwa na gazeti hili, haionekani kukatwakatwa.

Katika tukio hilo, Sheikh Baseleh ndiye anayeanza kuzungumza huku akisoma kipande cha gazeti lililomnukuu Waziri wa Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu, akizungumzia mchakato wa katiba, kwamba Tume ya Katiba “haitazingatia maoni ya wachache”, na kwamba mambo ya dini yasiingizwe kwenye katiba.

Katika ufafanuzi wake, Sheikh Basaleh anasema Dk. Nagu alizungumza mambo haya mbele ya waumini wa Kanisa la Chang’ombe kwenye uzinduzi wa kwaya; na kwamba miongoni mwa mambo ambayo yanaitwa ya kidini yasiyotakiwa kuingizwa kwenye katiba ni Mahakama ya Kadhi Mkuu.

Baadaye anamkaribisha Profesa Lipumba, ambaye naye katika hotuba yake, pamoja na mambo mengine, anakosoa msimamo wa serikali kutaka Waislamu waanzishe mahakama yao ya kadhi, akisema mahakama ni chombo cha dola ambacho hakipaswi kuwa nje ya mfumo wa serikali.

Mara baada ya Profesa Lipumba kuhitimisha hotuba yake, Sheikh Basaleh alimkaribisha Sheikh Musa Kundecha, ambaye naye alisisitiza kauli ya Profesa Lipumba kuwataka Waislamu wajipange kwa ajili ya 2015.

Vile vile alifafanua kuwa “wachache” waliozungumzwa na Dk. Nagu ni Waislamu, kwani zilishatoka taarifa katika kituo cha TBC kuwa idadi ya wasiokuwa Waislamu nchini ni asilimia 52.

“Mimi sijaiona hiyo video ila nimeisikia tu kuwa ipo inauzwa mitaani na makanisani, lakini inawezekana waliorekodi wamenichakachua maana imekuwa siku nyingi kidogo tangu niende kuongea pale Msikiti wa Idrissa. Yamewezekana wameungaunga vipande wanavyovitaka ili kunipaka matope mimi na CUF kuwa tuna udini,” alifafanua Profesa Lipumba.

Alipotakiwa akutane na waandishi wa habari hii ili waiangalie kwa pamoja video hiyo ili kujua ukweli kama ni video halisi au ya kuchakachua, Profesa Lipumba alisema waandishi waende kumwona Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma, Abdul Kambaya.

Alipopigiwa simu, Kambaya hakutoa ushirikiano kwa waandishi. Badala yake aliwashambulia kuwa wana ajenda ya siri dhidi ya CUF, akisema wanafuatilia na kuona makosa ya viongozi wa CUF tu na kufumbia macho vitendo vya wanasiasa wengine wanapokwenda makanisani.

“Nyie waandishi wa Tanzania mmezidi, yaani ninyi mnaona matendo ya viongozi wa CUF tu, wengine wakienda makanisani mbona hawafuatiliwi? Mbona hamumfuatilii Lowassa akienda makanisani? Au mbona hamsemi Dk. Slaa akienda kanisani? Sasa Profesa akienda msikitini kuongea na Waislamu wenzake kuna kosa gani? Sasa ninyi andikeni chochote,” alifoka na kukata simu.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro alipotakiwa kuzungumzia video hiyo, alikataa katakata na kuwashauri waandishi wawasiliane na ama Profesa Lipumba mwenyewe au Kambaya.

Itakumbukwa kuwa kumekuwepo tuhuma dhidi ya Rais Kikwete na CCM kuwa mwaka 2010 waliendesha propaganda chafu za udini zenye lengo la kuwagawa Watanzania hususan Wakristo na Waislamu kwa manufaa yao ya kisiasa.

Mwelekeo huo wa kisiasa wa Rais Kikwete na CCM unadaiwa kutokana na hatua ya viongozi wa Kanisa Katoliki nchini kupitia Idara ya Uchungaji kutoa waraka maalumu uliowataka Watanzania kuchagua viongozi waadilifu.

Waraka huo haukuifurahisha CCM, ambayo imekuwa inagubikwa na tuhuma nyingi za ufisadi. Makada na viongozi wa CCM walijaribu kuupinga kwa kuupotosha, wakisema unaingiza mambo ya dini katika siasa.

Kanisa Katoliki lina utaratibu wa muda mrefu wa kutoka nyaraka kuelekeza waamini na wananchi juu ya mambo ya msingi katika jamii.

Katika hali hiyo, Rais Kikwete na CCM wanadaiwa kukimbilia kwa viongozi wa Kiislamu na kuwaomba wawaunge mkono kwa kuwajaza maneno ya uongo, kwamba Wakatoliki walikuwa wamewaagiza waumini wao kupigia kura wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Inadaiwa waliwafitinisha zaidi kwa kuwaeleza kuwa aliyekuwa mgombea kiti cha rais wa CHADEMA katika uchaguzi huo, Dk. Willibrod Slaa ambaye ameshawahi kuwa Padri, alikuwa ametumwa na Kanisa Katoliki ili kuendeleza utawala wa Kikristo nchini.

Propaganda hizo hazikuishia kwa viongozi na waumini wa Kiislamu tu, bali zilielekezwa pia kwa viongozi na wafuasi wa CUF ambao walirubuniwa na kushawishiwa kumpigia kura “Muislamu mwenzao” Rais Kikwete, huku wakiahidiwa kuwa mwaka 2015 Waislamu wa CCM nao watampigia kura mgombea wa CUF kwa hoja kuwa CCM watakuwa wamesimamisha mgombea Mkristo.

Licha ya madai hayo ya udini kuwa wazi kwa muda mrefu, lakini wakati wote Rais Kikwete na CCM wamekuwa wakikanusha tuhuma hizo na kuziita kuwa uongo na uzushi.


CHANZO: Tanzania Daima

20 Nov 2010



Kwa muda mrefu sasa,Rais Jakaya Kikwete amekuwa akitahadharisha kuhusu kuwapo kwa mgawanyiko wa kidini huko nyumbani.Aliongea hayo wakati wa kampeni zake na amerejea tena katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge.

Tuweke kando mjadala wa namna Kikwete na CCM walivyoshinda uchaguzi mkuu uliopita hivi majuzi.Tuijadili hoja yake ya udini.Hivi kama amepata ushindi halali,anaposema kuna mgawanyiko wa udini anamaanisha kura zote alipigiwa na Waislamubwenzake au?Maana kama kweli kuna mgawanyiko wa udini basi ni dhahiri kuwa matokeo ya uchaguzi huo yasingempa ushindi wa zaidi ya asilimia 60 ( tuki-neglect uchakachuaji).

Let's call a spade a spade.Hivi leo Kikwete anathubutu kulalamika kuhusu tatizo lisilokuwepo la udini ilhali yeye na wanamtandao wenzake walimwaga sumu kubwa ya udini mwaka 2005 to an extent "akawaingiza mkenge" Waislam wenzie kwa kuwaahidi Mahakama ya kadhi na kuahidi kushughulikia uanachama wa OIC?

Na hata tukiweka hilo kando,hivi ile kauli ya "CHAGUO LA MUNGU" haikutokana na jitihada za Kikwete na wanamtandao wenzie kuwaghilibu viongozi wa dini hadi wakamtangaza kuwa amechaguliwa na Mungu kuwakomboa Watanzania?Actually,huo haukuwa udini per se bali kufuru kwa Mwenyezi Mungu.Na kwa sie tunaofahamu kuwa Mungu si Athumani,na hapendi kuchezewa,ipo siku atawaadhibu wale wote waliotumia jina lake kwa minajili ya kusaka kura.

Mie nilikuwa Tanzania mwaka from Oktoba 2005 hadi April 2006 kwenye fieldwork yangu.Mungu huyohuyo tuliyeambiwa Kikwete ndio Chaguo lake mwaka 2005 anihukumu iwapo sentensi ifuatayo ni ya uzushi.Miongoni mwa maustaadhi niliowaintavyuu kwenye fieldwork yangu walibainisha waziwazi kuwa waliahidiwa na Kikwete na timu yake kuwa laiti angepata urais angeshughulikia vilio mbalimbali vya Waislam.Kwangu,huo sio udini as such kwa vile kuna matatizo ya msingi yanayowakabili Waislam na ambayo awamu mbalimbali za serikali tangu uhuru zimekwepa kuyashughulikia.Eneo moja la msingi ni elimu.Mwalimu Nyerere alikiri katika hotuba yake ya tarehe 9/12/1962 kwamba " wengi wa waliofanikiwa kupata elimu walifanya hivyo kupitia shule za misheni,na hivyo wengi ni Wakristo.Hapa tena,kwahiyo,tuna mgawanyiko ambao uwepo wake unaweza kuwa tishio kwa umoja wetu".Akaendelea kusema, " marafiki zangu,kila mmoja wetu afanye jitihada za kujenga Tanganyika ambayo hakutakuwa na tofauti na migawanyiko".Japo wakati Nyerere anastaafu mwaka 1985 alidai kuwa amefanikiwa kutimiza azma hiyo,ushahidi wa kitaaluma unapingana na kauli hiyo.

Kwahiyo,binafsi kama Mtanzania ninayependa kuona nchi yetu ikiwa na jamii yenye usawa,naamini kuwa viongozi wetu wana jukumu la kulishughulikia suala hili na kulipatia ufumbuzi.Kumekuwa na unafiki mkubwa katika kushughulikia malalamiko ya msingi ya Waislamu.Lakini kwa vile lengo la makala hii sio kuzungumzia suala hilo,nachoweza kuandika kwa kifupi ni kuwa kwa namna moja ua nyingine awamu zote nne za urais zimezembea kuyapatia ufumbuzi malalamiko ya Waislam huku Awamu ya Nne ikiingia madarakani kwa kujitambulisha waziwazi na kwa siri kuwa sio tu inayatambua matatizo na malalamiko ya Waislam lakini pia imedhamiria kuyatatua.Na katika kuonyesha iko serious,ahadi ya Mahakama ya Kadhi ikaingizwa kwenye manifesto ya uchaguzi ya CCM mwaka 2005.

Waislam wanajua,na sie tusio Waislam pia tunajua,kwamba ahadi hiyo ilikuwa ni danganya toto tu.Miaka mitano baadaye,suala la Mahakama ya Kadhi na kujiunga limeendelea kuwa ngonjera kama ilivyo kwa "maisha bora kwa kila Mtanzania".

Kwahiyo,Kikwete aliingia madarakani kwa kutumia udini lakini sio kwa vile yeye ni Muislam bali alitambua kilio cha Waislam kisha akakitumia kama turufu yake (kwa ahadi kuwa angeshughulikia matatizo yake) kisha baada ya kupata madaraka akajifanya hahusiki na suala hilo (refer kauli ya Kikwete kuwa aliyeanzisha hoja ya Kadhi ni Agustino Mrema-anaedansi nae hapo chini.What a cheap excuse!).Kwa lugha nyepesi,kilichojitokeza ni utapeli kwa kutumia matatizo ya kidini.
Picha kwa hisani MICHUZI

Kikwete analalamika kuhusu udini wakati kwa miaka mitano iliyopita Tanzania imekuwa na Rais na Makamu wa Rais Waislam.Na kwa vile Makamu wa sasa nae ni Muislam,inamaanisha kuwa kwa miaka 10 Tanzania itakuwa imekuwa chini ya Rais na Makamu wa Rais Waislam.Hakuna anayelalamika kwa vile wengi wetu tuna upeo mkubwa zaidi ya wa Kikwete anayetaka kulazimisha kuwa tuna mgawanyiko wa kidini.Ishu ya Rais na Makamu wake kutoka dini moja ni muhimu kwa vile Rais asipokuwepo nchini urais unakaimiwa na Makamu wake.Na likitokea lolote la kutokea,Makamu huyo atakuwa Rais kwa muda.

Sasa huyu Mkwere anapotuambia kuna mgawanyiko wa udini anaashiria kitu gani?Wakristo hawajalalamika muundo wa uongozi wa juu wa CCM ambapo idadi ya Waislam ni kubwa kuliko ya Wakristo (rejea wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM).Kikwete hakuwahi kuekemea jitihada zilizokuwa zikifanywa na magazeti ya Kiislam kujenga picha kuwa Dkt Wilbroad Slaa ni mgombea alietumwa na Kanisa Katoliki.Kikwete hakukemea pale Daily News na Habari Leo,magazeti yanayoendeshwa kwa fedha za walipa kodi,yalifuata mkumbo wa magazeti hayo ya Kiislam kumtambulisha Dkt Slaa kama mgombea aliyetumwa na Kanisa.Hakukemea kwa vile nafsini mwake alikuwa na imani potofu kama hiyo ya wababaishaji hao kuwa Dkt Slaa ana ajenda ya Ukristo.
Tatizo ni kwamba Katiba yetu haitoi fursa ya kumkalia kooni Kikwete.Tatizo jingine ni kukosekana kwa ujasiri huko nyumbani wa kumkalia kooni Kikwete kisheria kwa tuhuma za kuhatarisha usalama wa taifa.Laiti Idara ya Usalama wa Taifa ingekuwa serious basi ni wazi wangemshauri Kikwete aache kuhatarisha usalama wa taifa kwa kauli zake zisizoambatana na uthibitisho kuwa kuna mgawanyiko wa kidini.Au inawezekana wanausalama wetu ndio wanamhadaa Kikwete kuwa kuna mgawanyiko wa udini?


Au inawezekana kuna tatizo kubwa zaidi kuhusu Kikwete,kwamba anaona vitu ambayo sie wengine hatuvioni?Je ni maono ya Sheikh Yahya?Au je kelele hizo za mgawanyiko wa kidini ni maandalizi ya kuihujumu Chadema,au pengine kumuibulia kesi Dkt Slaa kwa kigezo cha kucbochea vurugu za kidini?

Jamani,hata mwezi haujapita na tayari tunashuhudia mazingaombwe tusiyohitaji.Mara TAKUKURU wanamsafisha Chenge.Mara Kikwete anaendeleza ngonjera za mgawanyiko wa udini,mara Kikwete anamchagua Zakia Meghji kuwa mbunge licha ya mwanamama huyo kuhusishwa na suala la EPA ( na taarifa kuwa ana uhusiano wa kifamilia na Kikwete).

Tuspokuwa makini,2010-2015 itashuhudia miujiza ambayo haijawahi kutokea mahala popote duniani katika ulingo wa uongozi na siasa.Sad news is,sie kama wahanga tunaweza tusipate wasaa wa "kushangaa" na kujiuliza "what the hell is going on?"

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.