Showing posts with label UNIVERSITY OF DODOMA. Show all posts
Showing posts with label UNIVERSITY OF DODOMA. Show all posts

18 Oct 2008

Wanafunzi 5,300 na wahadhiri wao zaidi ya 100 wa Chuo Kikuu cha Dodoma, wameanza mgomo usio na ukomo wakishinikiza uongozi wa chuo hicho kuwalipa stahili zao mbalimbali.Wanafunzi hao walikuwa wamebeba mabango mbalimbali yenye ujumbe wa kumtaka Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Shabani Mlacha, kujiuzulu kwa madai kuwa ndiye kikwazo. 

Pia walikuwa wakiimba nyimbo za kuhamasisha mshikamano huku wakimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwenda chuoni hapo kuwasikiliza. 

Askari Polisi wakiwa kwenye magari walikuwa pembeni ya wanafunzi hao wakiwa tayari kupambana na wanafunzi hao kama wangefanya fujo hivyo kusababisha uvunjifu wa amani chuoni hapo. 

Hata hivyo, polisi hao walijikuta hawana kazi ya kufanya kwani hakukuwa na hali yoyote ya uvunjifu wa amani na wanafunzi hao walionekana kuwa watulivu wakati wote wa kuimba nyimbo zao. 

Katika mgomo huo ulioanza jana, wanafunzi hao wanalalamikia uhaba wa malazi kwa madai kuwa wanachangia Sh. 500 kila siku, lakini baadhi yao wanalala kwenye nyumba za kulala wageni na wengine wakilazimika kulala kwenye chumba kimoja watu wanne. 

Akizungumzia mgomo huo, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho, Malimi Joramu, alisema sababu nyingine ni uongozi wa chuo hicho kuwatoza wanafunzi Sh. 100,000 kama gharama za matibabu kwa miaka mitatu. 

Alisema malalamiko yao yapo upande wa wanafunzi ambao ni watumishi wa umma ambao hulazimika kuchangia gharama hizo kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, lakini uongozi wa chuo umewataka wote kulipia gharama hizo bila kujali ni mtumishi wa umma au la. 

``Tulishakubaliana na Uongozi wa Chuo mwaka jana kuwa wanafunzi hao wasichangie gharama hizo na wale waliokwisha changia warudishiwe gharama zao, lakini tumeshangaa kwa wanafunzi wa mwaka huu, gharama hizo zimerudishwa tena na wale waliorudishiwa fedha zao, wametakiwa kurudisha gharama hizo,`` alisema Rais huyo. 

Madai mengine alisema ni pamoja na Uongozi wa Chuo kuweka muda mfupi wa usajili wa wanafunzi, ambapo chuo hicho kimetangaza kwamba jana ndiyo mwisho na wale ambao watakuwa hawajajisajiliwa, Chuo hicho hakitawatambua. 

Rais huyo anadai kuwa, muda huo ni mfupi mno ukilinganisha kuwa wanafunzi wengi wanaosoma chuoni hapo wanatoka katika familia maskini na hata walipouomba uongozi wa chuo kuwaongezea muda, ulikataa kufanya hivyo na kushikilia msimamo wake wa kuwafukuza. 

``Tunajiuliza hivi iweje mafisadi wa EPA ambao ni wezi wameongezewa muda wa kulipa fedha walizoiba, sisi ambao ni wanafunzi na tunatoka kwenye familia maskini tunakataliwa kuongezewa muda hata wa mwezi mmoja tu, hii sio haki kabisa,`` alilalamika Joramu. 

Kwa upande wa wahadhiri wa chuo hicho, wao wanadai kutolipwa posho ya kujikimu ya wiki moja ya kuripoti chuoni hapo pamoja na fedha za uhamisho kwa baadhi ya wahadhiri. 

Wengine wamedai hawajalipwa mishahara yao ya mwezi uliopita hali inayowafanya waishi maisha ya kuombaomba, hasa kutokana makali ya maisha kupanda. 

Wahadhiri hao wanaokadiriwa kupita 100, wamegoma kuingia madarasani wakishinikiza kulipwa posho hizo, pamoja na mishahara yao na ikiwa ni vinginevyo, mgomo huo hautakuwa na ukomo. 

Akijibu tuhuma za wanafunzi, Profesa Mlacha alisema gharama za malazi wanazolipia wanafunzi hao, zimepunguzwa kutoka shilingi 700 kwa siku mwaka jana, hadi kufikia Sh. 500 mwaka huu. 

Alisema sababu za kupunguza gharama hizo ni malalamiko ya wanafunzi hao wakidai kuwa ni kubwa na wazazi wao wanashindwa kumudu kulipa. 

``Kutoka na hali halisi ya maisha, tuliwaelewa na tukaamua kushusha hadi kufikia Sh. 500, lakini pamoja na kushusha huko, bado baadhi yao wanaendelea kulalamika kuwa gharama hizo ni kubwa,`` alisema. 

Hata hivyo, Profesa Mlacha alisema chuo hicho kina malazi ya kutosha na kila chumba wanalala wanafunzi wanne kutokana na ukubwa wa vyumba hivyo, kwa kuwa kila mwanafunzi ana kitanda chake. 

Alisema hivi sasa kuna vitanda na magodoro zaidi ya 1,000 ambayo hayajalaliwa na wanafunzi kutokana na wengi wao kuwa hawajaripoti chuoni hapo hadi sasa na kushangazwa na malalamiko ya wanafunzi ambayo aliyaita kuwa ni ya uzushi. 

Kwa upande wa malipo ya matibabu alisema, chuo hicho kilikutana na watendaji wa Mfuko wa Bima ya Afya na kuzungumza nao kuangalia utaratibu wa matibabu ambapo walibaini kuwa, kuna baadhi ya magonjwa ambayo mfuko huo hauyalipii. 

Kuhusu madai ya usajili alisema, hizo ni sheria za chuo kwamba mwanafunzi ambaye hajasajiliwa na chuo, hatambuliki kama ni mwanafunzi. 

``Tangu siku ya kwanza ya mwanafunzi kupata barua ya kuitwa chuoni, anaorodhoshwewa mahitaji yote anayotakiwa kuja nayo, sasa iweje mwanafunzi aje shuleni akiwa hana fedha hata nusu ya gharama hizo, chuo hakitakubali hata kidogo kumsajili mwanafunzi ambaye hajalipa hata nusu ya gharama zinazohitajika,`` alisisitiza. 

Akijibu malalamiko ya wahadhiri, Profesa Mlacha alisema sheria iliyokuwa ikitaka wahadhari hao kulipwa posho hiyo imefutwa, lakini hata hivyo, chuo hicho kimetumia busara ya kuwaombea fedha hizo serikalini na taratibu hizo zilikuwa zinaendelea. 

Hata hivyo, alisema pamoja na kwamba asilimia 80 ya walimu hao hawana sifa za kulipiwa gharama za malazi na chuo, chuo hicho kimejitahidi kuwapatia nyumba ambazo zina kila kitu na kwamba hakuna mhadhiri anayekaa kwenye nyumba za kulala wageni. 

``Wahadhiri hao nao wametufikisha mahali ambapo tunashangaa, mwaka jana tuliwalipa, lakini kutokana na sheria hiyo kufutwa bado tukatumia ubinadamu wa kuwaombea fedha hizo serikalini, lakini wakati suala hilo likishughulikiwa tunashangaa nao wanagoma, chuo hakielewi nia yao ni nini,`` alihoji Prof. Mlacha. 

Aidha, Profesa Mlacha alisema, uchunguzi wa chuo hicho umebaini kuwa, wapo wahadhiri wachache wanaojifanya wanazijua siasa au wanataka kutumia chuo hicho kujifunza siasa. 

``Tumebaini wahadhiri hao ndiyo walioshinikiza mgomo huu, inawezekana wanajifunza siasa ndani ya chuo hiki, lakini tunawaeleza kuwa, hiki sio chuo cha siasa na kama wanataka siasa waende kwenye vyama vya siasa kuonyesha uwezo wao wa kujua siasa,`` alisema Profesa Mlacha. 

Hadi mwandishi wa habari hizi anaondoka eneo la chuo hicho bado wanafunzi hao walikuwa wakiendelea na mgomo wao.

CHANZO: Nipashe

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.